MIthali 31:1-3 “Maneno ya mfalme Lemueli;
mausia aliyofundishwa na mama yake. Ni nini, mwanangu? Tena ni nini, mwana wa
tumbo langu? Tena, ni nini mwana wa nadhiri zangu? Usiwape wanawake nguvu zako;
Wala moyo wako usiwape wale wawaharibuo wafalme.”
Utangulizi:
Kitabu cha Mithali ni kitabu
kinachotufunza maswala ya muhimu katika maisha na maadili na maonyo ya kila
siku pamoja na kutupa hekima jinsi na namna inavyotupasa kuenenda, Moja ya
maswala ya msingi tunayojifuza leo ni pamoja na wosia aliopewa Mfalme Lemuel
kutoka kwa mama yake ambayo alimfunza ili kutusaidia sisi tuliofikiwa na miisho
ya zamani hizi.
Mithali 31:2-3 “Ni nini, mwanangu? Tena ni
nini, mwana wa tumbo langu? Tena, ni nini mwana wa nadhiri zangu? Usiwape wanawake
nguvu zako; Wala moyo wako usiwape wale wawaharibuo wafalme”
Mama anaonekana kusisitiza sana
kuonyesha namna anavyohitaji umakini wa
jambo ambalo anataka kulileta kwa mwanae ambalo pia analileta kwetu, ambalo
kimsingi ingawa lilikuwepo katika siku za zamani sana na leo linaendelea
kushika kasi kwa namna mbalimbali, tutajifunza somo hili USIWAPE WANAWAKE NGUVU
ZAKO kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
Ø Maonyo
kutoka kwa mama.
Ø Usiwape
wanawake nguvu zako
Ø Mambo
yawapasayo wanaume kufanya!
Maonyo kutoka kwa mama.
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
mtazamo wa kale wa mashariki ya kati jukumu kubwa la malezi na makuzi mazima ya
mtoto awe wa kiume au wa kike na hata misingi ya imani yake ilisadikiwa kuwa
ilitoka kwa mama, Kama mtoto angeonyesha hekima na ubora baba yake angejivunia
sana na kama mtoto akionyesha tabia mbaya waliangalia sana kuwa mama yake
alikuwa ni mtu wa namna gani ona Mithali
10:1 “Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali
mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye.” Kwa msingi huo utaweza kuona
hata nyakati za utawala wa wafalme wale waliokuwa waovu au waliofanya mema mama
zao walitajwa na ubini wao kuonyesha kuwa chanzo cha tatizo au mafanikio ya
mfalme husika imechangiwa na aina ya mama aliyekuwa naye ona kwa mfano
2Nyakati 29:1-2 “Hezekia alikuwa na umri wa
miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka
ishirini na kenda; na jina la mamaye aliitwa Abiya binti Zekaria. Akafanya
yaliyo ya adili machoni pa Bwana, sawasawa na yote aliyoyafanya Daudi babaye.”
Unaona kama mfalme alifanya
vizuri maana yake kulikuwa na mama mzuri mwenye tabia nzuri mwenye busara na
hekima na mcha Mungu anayetoka katika familia iliyofunzwa vizuri, kadhalika pia
wamama walitajwa kulingana na aina ya mfalme kama mfalme huyo alikuwa mwovu
utaweza kuona na aina ya mama anatajwa na anakotokea ona kwa mfano
1Wafalme 15:1-3 “Mwaka wa kumi na nane wa
mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, Abiya alianza kutawala juu ya Yuda. Miaka
mitatu akatawala huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Maaka, binti
Absalomu. Akaziendea dhambi zote za babaye, alizozifanya kabla yake; wala moyo
wake haukuwa mkamilifu na Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi babaye.”
Ni kwaajili ya mambo kama haya
Mungu aliwaelekeza Israel kuhakikisha kuwa wanaoza watoto wao kwa watu sahihi
wenye tabia njema ili mioyo yao isikenguke kutoka kwa Bwana ona
Kumbukumbu 7:1-4 “Bwana, Mungu wako,
atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang'oa mataifa mengi watoke
mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi,
na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe; wakati Bwana, Mungu
wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe
kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao; binti yako
usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake. Kwa kuwa
atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo
itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi.”
Kwa msingi huo kwa mujibu wa
maandiko Mwanamke ana nafasi kubwa sana ya kuambukiza maswala ya kiimani na
uadilifu kwa watoto kuliko tunavyoweza kufikiri ukweli huu unathibitishwa pia
katika maisha ya Timotheo ambaye baba yake alikuwa myunani na mama yake myahudi
na bibi yake alikuwa myahudi pia na imani ilitembea kwa wanawake hao mpaka kwa
kijana wao Timotheo ona kile Paulo mtume anakithibitisha hapa
2Timotheo 1:5 “nikiikumbuka imani uliyo
nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika
mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo.”
Unaona Paulo mtume mkuu wa
wajenzi pia alikuwa na imani kuwa imani njema iliyokuwa kwa bibi yake Timotheo,
ilikaa wazi pia ndani ya mama yake Eunike na alikuwa na imani kuwa Timotheo
ameirithi, ni ukweli ulio wazi kuwa uadilifu, imani, tabia na mwenendo wetu unaathiriwa kwa
kiwango kikubwa na wazazi wetu wa kike kifupi imani inakaa kwa mwanamke.
Ni katika hali kama hiyo Mfalme
Lemuel anakumbuka sana mausia aliyopewa na mama yake, yalikuwa ni maelekezo
Muhimu sana ambayo mama yake aliyazungumza kwa msisitizo akimtaka kijana wake
ayashike ili aweze kufanikiwa katika maisha yake na katika ufalme wake, Mama
yake alikuwa anajua mioyo ya
wanawake wa ulimwengu huu na alikuwa na ujuzi kuwa watu wengi sana hususani
wanaume wamepotezewa Muda, na kupotezewa heshima zao na kuharibikiwa katika
uchumi na mafanikio yao kupitia wanawake, ona tena maonyo hayo muhimu
MIthali 31:1-3 “Maneno ya mfalme Lemueli;
mausia aliyofundishwa na mama yake. Ni nini, mwanangu? Tena ni nini, mwana wa
tumbo langu? Tena, ni nini mwana wa nadhiri zangu? Usiwape wanawake nguvu zako;
Wala moyo wako usiwape wale wawaharibuo wafalme.”
Usiwape wanawake nguvu zako!
Katika maelekezo hayo muhimu
ambayo Lamuel alipewa na Mama yake na ameshirikisha jamii hapa ili wote tuweze
kujifunza ni hatari kuhusu wanawake! USIWAPE
WANAWAKE NGUVU ZAKO hili ni moja ya
maonyo ya msingi sana ambayo tunataka kujifunza na sisi leo, kila kijana wa
kiume anapaswa kulitilia hilo maanani, jambo hili la kuwapa wanawake nguvu zako
pia linaendana na linalofuata
WAWAHARIBUO WAFALME, kuwapa wanawake nguvu zako na kuwapa wanawake moyo
wako kunaleta anguko la mfalme! Kunaangusha, kuonaondoa heshima, kunaharibu
mwelekeo wa maisha kunasambaratisha ustawi wa kiuchumi wa mtu, Nafsi yako
ikitekwa na uzuri wa wanawake hatima ya kijana wa kiume inakuja kuwa yenye
majuto makubwa baadaye jambo hili limeonywa mara kadhaa katika maandiko ona
Mithali 5:1-10 “Mwanangu, sikiliza hekima
yangu; Tega sikio lako, mzisikie akili zangu; Upate kuilinda busara, Na midomo
yako iyahifadhi maarifa. Maana midomo ya malaya hudondoza asali, Na kinywa
chake ni laini kuliko mafuta; Lakini mwisho wake ni mchungu kuliko pakanga; Ni
mkali kama upanga wa makali kuwili. Miguu yake inatelemkia mauti; Hatua zake
zinashikamana na kuzimu; Hata asiweze kuiona njia sawa ya uzima; Njia zake ni
za kutanga-tanga wala hana habari. Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Wala
msiache maneno ya kinywa changu. Itenge njia yako mbali naye, Wala usiukaribie mlango
wa nyumba yake. Usije ukawapa wengine heshima yako, Na wakorofi miaka yako;
Wageni wasije wakashiba nguvu zako; Kazi zako zikawa ndani ya nyumba ya mgeni;”
Unaweza kuona maonyo ya Mfalme Sulemani
yanaenda sambamba na Maonyo ya mama yake Lemuel wote wanaonya Hasara zinazoweza
kupatikana kwa Mwanaume kujihusisha na wanawake hususani katika maswala mazima
ya kufanya ngono, kufanya zinaa au umalaya au kuwanda wanda katika maisha yetu
na uzuri wa wanawake au kutaka kuwaonja wanawake wa aina zote wanaojitokeza
katika maisha yetu jambo hili lina madhara kadhaa ambao wenye hekima
wameyaainisha hapo, usiwape wanawake nguvu zako!
Nini maana ya KUWAPA WANAWAKE NGUVU ZAKO neno nguvu
linalotumika hapo katika kiebrania ni CHAYIL
ambalo kimsingi linazungumzia UWEZO,
yaani uwezo wako wote kama vile Jeshi au kila kitu ulicho nacho ambacho
kinakujenga wewe kuwa wewe, Mfano, HESHIMA,
FEDHA, MALI, WATOTO, KAZI, AU NJIA ZAKO ZOTE ZA UCHUMI, MAISHA YAKO, AU MUDA, Kwa hiyo neno CHAYIL ni mjumuisho wa maswala kadhaa
muhimu kama kazi, heshima, cheo, muda nguvu na uwekezaji wako wote. Kwa mujibu wa wenye hekima hapo ni kuwa
unapojitoa katika maisha ya kuwapenda wanawake na umalaya utafutilia mbali kila ambacho umesumbuka
kukijenga kwa miaka kadhaa ya maisha yako neno WAHARIBUO katika Kiebrania
ni DEREK ambalo maana yake ni kufutuilia mbali, wanaume wengi hutumia nguvu zao na na muda wao kujijenga kitaaluma, kiuchumi,
kiroho na kadhalika lakini moja ya changamoto kubwa sana kibinadamu inayowapata
wanaume ni kuwa wanapokuwa na mafanikio makubwa na kuwa maarufu na kuwa na
nguvu kubwa kiuchumi, na hata kimwili na kujipatia umaarufu basi adui mkubwa
sana wa mafanikio yao au anguko lao kubwa sana linalowakabili ni WANAWAKE, kila mwanamke anavutiwa sana
na mwanaume aliyejijenga, Mwenye fedha, mwenye six Park, aliye ha umaarufu,
mwenye uchumi mzuri, mwenye tabia nzuri, mwenye nyumba, gari na mafanikio
mbalimbali katika maisha, Mama wa Lemuel alikuwa na ufahamu huo na akamuonya
mwanaye kuwa asitoe moyo wake kwa hawa wanaoangusha wafalme sikiliza; wafalme
hapa sio lazima wawe watu walioko kwenye mamlaka za kiserikali au rais na
kadhalika Ufalme hapa unazungumzia kufikia kiwango Fulani cha utukufu ni kiwango
Fulani cha mafanikio, kilele Fulani cha mafanikio na heshima unapokifikia hicho
wewe ni mfalme na unaweza kuharibikiwa kama moyo wako hautajali kujilinda na
wanawake, na kumbuka vilevile Mama wa Lamuel Hakusema Mwanamke bali amesema
wanawake maana yake ile hali ya kupenda kumiliki au kutembea na wanawake wengi
baada ya mafanikio, kitabu hicho hicho kumbuka kuwa kina imani kuwa mtu
muadilifu anaweza kutafuta mke mmoja tu na akatulia naye Mithali 31:10 “Mke mwema, ni nani awezaye
kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani.” Kwa hiyo
tatizo sio mke tatizo ni wanawake hawa wanaleta uharibifu na neno la Mungu
linathibitisha hayo kama tutakavyoona mbeleni:-
-
Kiuchumi
– Maandiko yanatufundisha kuwa tangu siku za zamani limekuwa ni jambo la
kawaida kuwa kunapokuwa na mahusiano ya kimapenzi kati ya mwanamke na Mwanaume
fedha au mali huusika katika kuwapa wanawake, wanaume wameumbiwa kutoa na
wanawake wamaumbiwa kupokea, hivyo linaweza kuwa jambo la kawaida wanawake
kutaka malipo katika mahusiano,
Mwanzo 38:14-18 “Basi akavua nguo za ujane wake, akajivika
utaji, akajifunika uso, akakaa mlangoni pa Enaimu, karibu na njia ya kuendea
Timna. Maana aliona ya kwamba Shela amekuwa mtu mzima, wala hakuozwa awe mkewe.
Yuda alipomwona alimdhania kuwa ni kahaba, maana amejifunika uso. Akamgeukia kando ya njia, akasema, Niruhusu
niingie kwako. Maana hakujua ya kuwa ni mkwewe. Akamwuliza, Utanipa nini,
ukiingia kwangu? Akasema, Nitakuletea mwana-mbuzi wa kundini. Naye akamwuliza,
Je! Utanipa rehani hata utakapomleta? Akasema, Nikupe rehani gani? Akamjibu,
Pete yako ya muhuri, na kamba yake, na fimbo yako iliyo mkononi mwako. Basi
akampa, akaingia kwake, naye akapata mimba.”
Ni kifungu cha
zamani sana japo kinaweza kuwa na mafunzo mengine mengi tofauti lakini moja ya
kitu tunajifunza hapo ni kuwa tangu zamani wanawake walipenda kupokea kitu
kutoka kwa wanaume na wanaume walihonga, mwanamke aliuliza utanipa nini
ukiingia kwangu? Na mwanaume alisema nitakupa mwanambuzi, katika nyakati za leo
wanawawake wameharibika zaidi, hali ya kutaka kuhongwa imepanuka katika kiwango
ambacho leo kinaitwa kuchunwa, wanaume wamepewa majina ya mabuzi na wanawake ni
wachunaji, kuna utapeli mwingi na mkao mkubwa wa wanawake kuhitaji fedha kama
malipo ya ngono, lakini sio kwa malipo ya ngono tu ila watawekeza mioyo yao katika
kuwaelemea wanaume kwa sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni ugumu wa maisha
lakini vilevile na kwa moyo wa ubinafsi hata kama hawauzi mapenzi au kufanya
biashara ya mapenzi, lakini vyovyote vile hali hii inachangia katika
kudhooficha uchumi wa mwanaume, wanawake wa leo ambao wengi wao wana mikopo
wanayotakiwa kurejesha mawazo yao makubwa yamekuwa katika fedha zaidi kuliko
kwenye penzi lenyewe kuwaendekeza Malaya kutakueletea anguko la kiuchumi, na
kufilisi uwezo wako, katika maeneo mbalimbali likiwemo hili la uchumi.
-
Nguvu –
Huu ni uwezo wa kimwili na Kiroho, kisaikolojia wanawake wanavutiwa sana na
Mwanaume mwenye nguvu, hili sio jambo la ajabu kiasili, kwani hata wanyama
katika ulimwengu wao majike huwa hayavutiwi na mwanaume mnyonge, kama mwanaume
atakuwa hana nguvu anapoteza heshima kwa mwanamke, lakini hata hivyo
kujihusisha katika ngono kulikokithiri kwa wanawake wa aina mbalimbali pia
hupelekea kupoteza nguvu za kimiwli, na kiroho na nguvu za uzazi au hata nguvu
za kiume
Zaburi 127:3-5 “Tazama,
wana ndio urithi wa Bwana, Uzao wa tumbo ni thawabu. Kama mishale mkononi mwa
shujaa, Ndivyo walivyo wana wa ujanani. Heri mtu yule Aliyelijaza podo Lake
hivyo. Naam, hawataona aibu Wanaposema na adui langoni”
Maandiko
yanazungumzia umuhimu wa watoto, Nguvu ya familia yoyote ni watoto wake tabia
ya kujaribu kujifurahisha na kila mwanamke inaweza kuathiri uzao wako au
unaweza kupoteza mbegu zako na watoto wako wakawa wa mtu mwingine, wako watu
wengi leo wamezaa hovyo hovyo na wamezaa
mpaka na wake za watu na ni ngumu kwenda kudai watoto katika familia isiyokuwa
yako, watoto wanajenga jamii ni thawabu kutoka kwa Mungu lazima wazaliwe katika
utaratibu na mpangilio maalumu ili uzao wako usipotee kama mishale mkononi mwa
shujaa ndivyo walivyo watoto wa ujanani, Heri mtu yule aliyelijaza podo lake,
yaani heri mtu mwenye mishale mingi, kuwa na watoto wengi lilikuwa moja ya
jambo lenye heshima kubwa sana nyakati za Biblia. Lakini sio watoto
waliotawanyika ni watoto wanaolelewa katika boma moja (Podo) ni chombo maalumu
cha kuhifadhia mishale ambayo unaweza kuitumia wakati wa mapambano, shujaa
hawezi kutumia mshale ambao hauko kwenye podo lake!, Uzaaji wa watoto hovyo
hovyo pia unaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuharibu uchumi na
uadilifu wa kitabia unaoukusudia uwe kwa watoto wako!
Aidha pia nguvu
zako za kiume zinaweza kuharibiwa kupitia tabia ya kulala hovyo na wanawake,
asili ya nguvu zako za kiuchumi, kimwili na kiroho pia inaweza kuharibiwa kama
hutakuwa na tahadhari na wanawake hasa unapokuwa na mahusiano ya kingono na wao.
Waamuzi 16:13-18 “Delila
akamwambia Samsoni, Hata sasa umenidhihaki, umeniambia maneno ya uongo; niambie
sasa, waweza kufungwa kwa kitu gani? Akamwambia, Ukivifuma hivi vishungi saba
vya nywele za kichwa changu katika mtande wa nguo. Basi akazifunga kwa msumari,
akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Naye akaamka usingizini, akaung'oa ule
msumari, na ule mtande. Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na
moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia
asili ya nguvu zako nyingi. Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila
siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa. Ndipo alipomwambia yote
yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu
kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu;
nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama
wanadamu wenzangu. Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni
mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii
tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti
wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao.”
-
Heshima –
Daudi alikuwa ni Mfalme aliyeheshimika sana mbele za Mungu na wanadamu kwa
ujumla ndiye mtu anayetajwa katika maandiko kuwa aliupendeza moyo wa Mungu,
jambo hili lilimpa heshima kubwa sana lakini aliposhiriki ngono na mke wa Mtu
alipoteza mamlaka yake na heshima, jambo hili lilimletea aibu kubwa sana ona
2Samuel 11:4 “Basi
Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye;
(maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani
kwake”.
Unaona kitendo
hiki hata Nathan nabii alimweleza wazi kuwa kwa jambo hili umewapa adui za
Bwana nafasi kubwa ya kukufuru ona
2Samuel 12:14 “Lakini,
kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za Bwana nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto
atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa.”
Nguvu na heshima
aliyokuwa anapewa Daudi iliingia shidani kupitia zinaa alijivunjia heshima japo
alitubu na aliendelea kuuelekeza moyo wake kwa Mungu, Lakini aliitia daosari
karatasimyake ya kuwa mfalme muadilifu
Mwanaye Sulemani
vilevile anajieleza mwenyewe kuwa wanawake ndio sababu ya anguko lake kubwa na
anaeleza wazi kuwa anguko lake lilisababishwa na upenzi wake mkubwa kwa
wanawake na kutokusikiliza mausia ya mama yake Lemuel anayejitaja hapa ni mwandishi wa kitabu hiki Jina Lemuel kwa Kiibrania maana yake ni “ALIYEJITOA KWA MUNGU” au “KWAAJILI YA MUNGU” FOR GOD
OR DEVOTED TO GOD jina hilo halijulikani
katika orodha nya wafalme wa Yuda na Israel ni huenda ni jina ambalo Sulemani
aliitwa na mama yake Bathsheba au ni jina analoamua kulitumia katika utunzi wa
stori hii au shairi hili kwa ni ni
anatumia jina hili nadhani anatumia jina la fumbo kwa kusudi tu la
kutuletea somo husika katika Israel, kwa msingi huo mwandihi wa Mithali hizi ni
Suleimani na hapa anaonyesha hekima yake aliyiojifunza kutoka kwa mama yake
mwenye hekima na uadilifu kwa hiyo hakujawahi kuwa na historia ya kuwepo mfalme
aliyeitwa Lemuel, na hivyo tunaamini Lemuel ni Suleimani nanamamam yake ni
Bathsheba. Sasa Pamoja na heshima kubwa sana aliyokuwa nayo na hekima aliyopewa
na Mungu Sulemani aliharibikiwa kwa kutokufuata maonyo na mafundisho ya mama yake
na hapa anataka kutumia uzoefu alioupata kutufunza sis nasi tusiharibikiwe!.
1Wafalme 4:4-6. “Maana
ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu
mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa
Daudi baba yake. Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni
na Milkomu, chukizo la Waamoni. Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa
Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake.”
Anguko hili la
Sulemani la kufikia hatua ya kuabudu miungi mingine ndilo kwa namna Fulani
limechangiwa na moyo wake wa kuwapenda wanawake wengi ona
1Wafalme 4:1-3 “Mfalme
Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake
wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, na wa
mataifa Bwana aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie
kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani
akaambatana nao kwa kuwapenda. Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na
masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo.”
Akiwa katika
hali hii ya majuto baadaye ndio anatuasa kama Lemuel akionya kuwa tusikilize
hekima sio lazima sana Mwalimu awe mama Lakini katika mafunzo ya Hekima wakati
wowote chanzo cha mafunzo kinaitwa mama, kama mtu alikuwa na hekima kubwa sana
na mali nyingi na muda na mafanikio mengi sana akapata hata anguko la kuabudu
miungu ni sawa na kupoteza muda wake na kuharibikiwa katika kila kitu, Suleimani
alikuwa na akili moyoni mwake hangeweza kuzungumza habari za baba yake na mama
yake Bathsheba kama sisi tunavyoweza kuzungumza lakini akilini alikuwa na ujuzi
kujihusu kuhusu na kupitia uzoefu alioupata ni uwazi kuwa Sheria ya Mungu pia
ilikuwa imewaonya wafalme kutokujitwalia wake wengi Kumbukumbu 17: 17 “Wala asijizidishie wake,
ili moyo wake usikengeuke; wala asifanye fedha zake na dhahabu kuwa nyingi mno.”
Lakini yeye hakusikiliza wala kujali jambo lililopelekea kuleta madhara
makubwa katika maisha yake!
-
Nguvu za
kiroho – Kupenda wanawake licha ya kuharibu nguvu za uchumi, heshima na
mali pia wanawake wanaharibu hali ya Msimamo wa kiroho, Kupenda wanawake
husababisha kuwapenda wao zaidi kuliko kumpenda Mungu, Ni swala lililowazi kuwa
Baba Yetu Adamu angeweza kutokukubaliana na Mwanamke katika kula lile tunda na
angeweza kutoa ripoti kwa Mungu kwa kile kilichotokea na pia kuwa na toba au
kuomba msamaha kwa tukio lile hii inawezekana ya kuwa ilichangiwa kwa kiwango
kikubwa na upendo wake kwa mkewe na Mungu akimsomea hukumu anaanza kwa kusema
Kwakuwa umeisikiliza sauti ya mkeo …. Ona
Mwanzo 3:17-19 “Akamwambia
Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao
nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu
utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia,
nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata
utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe,
nawe mavumbini utarudi.”
Muda usingeweza
kutosha kurejea hali ya Mwamuzi maarufu Samsoni, na Mfalme maarufu Daudi na mtu
mwenye hekima Sulemani, hasa Sulemani tunaona kuwa aligeuzwa moyo kuabudu
Miungu mingine, hapa tunajifunza kuwa ukiacha shetani na ushawishi mwingine wa
Dunia wanawake wana nafasi kubwa sana ya kugeuza mwelekeo wa Moyo wa Mwanaume,
Mambo yawapasayo
wanaume kufanya!
Luka 10:27. “Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako
wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na
jirani yako kama nafsi yako.”
Ni muhimu kufahamu kuwa wanaume wanawajibika katika kila
hali itakayotokea katika maisha yao, wanaume wanatakiwa kutumia nguvu zao,
akili zao, fedha zao na hisia zao zote ambazo Mungu amewapa kuhakikisha kuwa
wanalinda usalama wao na baraka ambazo Mungu amezikusudia kwao, Kama wanaume wanampenda
Mungu basi nivema akili zao, na moyo wao na roho zao zikaelekezwa kwa Mungu na
kulitiii neno lake.
Moja ya adhabu iliyotangazwa na Mungu katika bustani ya Edeni
kama mgogoro kati ya mwanamke na mwanaume ni pamoja na ugomvi dhidi ya nguvu,
yaaani mamlaka na utawala ona Mwanzo
3:16 “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia
uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa
kwa mumeo, naye atakutawala.”
Kimsingi sehemu muhimu ambayo nataka kila mtu msomaji wangu
na wasikilizaji wangu waweze kunielewa ni eneo ambalo maandiko yanasema TAMAA YAKO ITAKUWA KWA MUME NAYE ATAKUTAWALA,
katika maandiko ya kiibrania neno NENO tamaa linatajwa kama neno TESHUQAH Katika kiibrania kwa
kiingereza ni STRETCHING OUT AFTER ambalo maana yake ni kujaribu kujitutumua
dhidi ya na Mungu anapotangaza mgogoro
huu anaoshesha na matokeo ni kutawaliwa neno naye ATAKUTAWALA – linasomeka kama
MASHAL ambalo hapa linatumika kama kuzidiwa, kutawaliwa, au kuwa na nguvu
juu yako, kwa tafasiri nzuri maana yake ni kuwa wanawake watakuwa na tamaa ya
kutaka kuwatawala wanaume lakini hatimaye watatawaliwa unaweza kuona
Kwa hiyo kinachotokea ni kuwa mwanaume anapojitoa katika
mapenzi, kwa haraka sana Mwanamke atajinyoosha kwenye utawala, atatawala hisia
zako, mwili wako, tama yako, uchumi wako, roho yako na kuiteka nafsi yako na
usipoweza kujinasua katika hilo maana yake
UMEWAPA WANAWAKE NGUVU ZAKO na uwezo
wako wa kutawala mambo mengine unakuwa umeishia hapo, akiweka msingi wa
maongozi katika kanisa Paulo mtume katika nafsi yake analiweka hili wazi kuwa
kama kiongozi hawezi kuitawala nyumba yake hataweza kufaa kuwa mtawala katika
kanisa ona 1Timotheo 3:4-5 “mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha
watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe,
atalitunzaje Kanisa la Mungu?)”
Kwa msingi huo ili mwanaume ajikwamue ni lazima ajui
kujitawala na kutawala na akiweza hicho hatawekwa chini ya uweza wa kitu
chochote,aidha kabla ya kujiingiza katika mahusiano mwanaume anatakiwa kupiga
hesabu kama mtu aendaye vitani ajue kuwa anajiingiza katika gharama kubwa sana Luka 14:31 “Au
kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza
na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule
anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?”
Kila mwanaume ana nguvu ya kutubu na kufanya mabadiliko
katika maisha yake, kama mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana katika kazi zetu,
na kutupa kupuuzia maswala ya msingi kama Familia na ibada kwa Mungu wetu
tunazo nguvu za kutengeneza mambio ya nyumba zetu na kuwa watulivu, wote
tunauwezo wa kushinda, wanaume wote kwa namna moja ama nyingine tuna udhaifu
wote ukiacha Yesu Kristo, lakini iko nguvu katika maamuzi ambazo tunaweza
kufanya, tunaweza kutubu, neno toba katiika kiyunani ni Mtanoia ambalo maana
yake ni kugeuka kuna nguvu ya kufanya maamuzi ya kugeuka na kuacha njia zetu
mbaya na tukajikuta tunafanikiwa badala ya kuzitumia nguvu zetu na kupotea
tunaweza kuzitumia nguvu zetu katika kumtii Mungu
Na Rev. Innocent
Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi
mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni