Mathayo 2:1-12 “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya
Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika
Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana
tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.”
Utangulizi:
Moja
ya stori zenye mvuto mkubwa sana katika Biblia ni pamoja na stori ya ujio wa
watu wenye hekima kutoka mashariki ya mbali waliokuja kutoka Mashariki ya mbali
wakiongozwa na nyota mpaka Bethelehemu alikozaliwa Masihi, kwaajili ya
kumuabudu, Stori hii Mathayo ameipa uzito mkubwa sana na maneno yao yenye mvuto
mkubwa zaidi ni haya:- Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana
tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. Utamu wa
maneno yao na matendo yao unanifanya leo nitulie na kutafakari pamoja nawe
jambo kubwa ambalo Mungu amelifanya kupitia wenye hekima hao maarufu kama
mamajusi kwa Kiswahili cha zamani, (kwa
sasa wenye hekima- Wise man); Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na
mapana na marefu kuhusiana na swala hili:-
Ufahamu kuhusu
Mamajusi.
Mojawapo
ya tukio maarufu na la kusisimua sana wakati inapokaribia sikukuu ya Krismasi
ni pamoja na safari ya ujio wa Mamajusi kutoka mashariki, Kimsingi neno
mamajusi kwa kiingereza “Magi” linatokana
na neno la kiyunani MAGOS ambalo ni
sawa na neno Magician ambao zamani
walijumuishwa katika kundi la watu wenye hekima, wachawi na wanajimu waliokuwa
na sayansi ya kutoa suluhu kunapotokea changamoto katika falme za Babeli angalia kwa mfano katika kitabu cha Daniel
Daniel 2:1-3 “Hata katika mwaka wa pili wa kumiliki kwake Nebukadreza,
Nebukadreza aliota ndoto; na roho yake ikafadhaika, usingizi wake ukamwacha.
Ndipo mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na wasihiri, na
Wakaldayo, wapate kumweleza mfalme ndoto zake. Basi wakaingia, wakasimama mbele
ya mfalme. Mfalme akawaambia, Nimeota ndoto, na roho yangu imefadhaika hata
niijue tafsiri yake.”
Daniel 5:4-9. “Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha,
na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe. Saa iyo hiyo vikatokea vidole
vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya
mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule
mkono ulioandika. Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha;
viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana. Mfalme akalia kwa
sauti kubwa, akaamuru waletwe wachawi, na Wakaldayo na wanajimu. Mfalme
akanena, akawaambia wenye hekima wa Babeli, mtu awaye yote atakayesoma maandiko
haya, na kunionyesha tafsiri yake, atavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na
kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atakuwa mtu wa tatu katika
ufalme. Basi wakaingia wenye hekima wote wa mfalme; lakini hawakuweza kuyasoma
yale maandiko, wala kumjulisha mfalme tafsiri yake. Ndipo mfalme Belshaza
akahangaika sana, uso wake ukambadilika, na wakuu wake wakaona fadhaa.”
Kwa
hiyo ilikuwa kawaida ya wafalme wa zamani walipopata changamoto za aina
mbalimbali katika falme zao kuwaita wenye hekima (Wiseman) ili waweze kutatua changamoto mbalimbali walizokuwa
wanakutana nazo hawa ndio waliitwa MAGI
au Mamajusi au wenye hekima, kwa kusudi la kutatua changamoto zao
Tukio
linalofanana na hayo hapo juu lilitokea mapema zaidi ya miaka 1000 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu, wakati
wana wa Israel walipokuwa wakitokea Misri na kuwapiga wafalme wa waamori,
mfalme wa Moabu aliogopa sana na hivyo alimuita mchawi aliyeitwa Balaam ili aje
kuwaroga au kuwalaani Israel wasiweze kumdhuru
Hesabu 22:1-6 “Kisha wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi
tambarare za Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu ya Yeriko. Na Balaki mwana
wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli wamewatendea Waamori. Moabu
akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu akafadhaika kwa sababu
ya wana wa Israeli. Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu
litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya
mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile. Basi
akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka
nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka
Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi. Basi,
njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi.
Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa
maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.”
Hata
hivyo katika namna ya kushangaza Nabii huyu badala ya kuwalaani Israel yeye
aliwabariki sawa na jinsi Mungu alivyomuamuru, Ujumbe wa Mungu kwa Balaki
kupitia Balaamu ulikuwa na maonyo makubwa sana badala ya kulaani aliamuriwa
kuibariki Israel na kutoa unabii kuwa atakuja mfalme mwenye nguvu sana na
Mfalme huyo atawahukumu maadui wa Israel mfalme huyo mkuu ilionekana nyota yake
alisema namwona lakini si sasa Namtazama lakini si karibu Nyota itatokea Katika
Israel:-
Hesabu 24:15-19 “Akatunga mithali yake akasema, Balaamu mwana wa Beori
asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema, Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu,
Na kuyajua maarifa yake Aliye Juu. Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka
kifudifudi, amefumbuliwa macho, Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si
karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli;
Nayo itazipiga-piga pembe za Moabu, Na kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia. Na
Edomu itakuwa milki Seiri pia itakuwa milki, waliokuwa adui zake; Israeli
watakapotenda kwa ushujaa. Mwenye kutawala atakuja toka Yakobo, Atawaangamiza
watakaobaki mjini.”
Unabii
huo kimsingi ulikuwa unamuhusu Daudi katika mawazo finyu na unamuhusu Yesu
Kristo katika mawazo mapana, (in a
narrow sense, Daivid, in a broad Sense Jesus) Huenda unabii huu ulihifadhiwa na wanajimu wa
ukaldayo, ama ulisomwa nao katika vitabu vya kale, ama walisoma kitabu cha
Daniel na kuwa na ufahamu wa Muda kamili wa kuja kwa mfalme huyu mkuu sana wa
wayahudi
Daniel 9:24-25 “Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu
ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya
upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele, na kutia muhuri maono
na unabii, na kumtia mafuta yeye aliye mtakatifu. Basi ujue na kufahamu, ya
kuwa tangu kuwekwa amri ya kutengeneza na kuujenga upya Yerusalemu hata zamani
zake MASIHI ALIYE MKUU; kutakuwa na majuma saba; na katika majuma sitini na
mawili utajengwa tena pamoja na njia kuu zake na handaki, naam, katika nyakati
za taabu.”
Na
au mara katika sayansi yao ya unajimu walipoiona nyota ambao kwa kusema kweli walikuwa na uelewa wa
moja kwa moja kuwa kiongozi huyo ni Mfalme mkuu wa ulimwengu mzima na anayepaswa
kuabudiwa,
Katika
kundi la wenye Hekima kulikuwa na wanajimu ambao nao walikuwa wakifanya kazi
katika jumba la kifalme kazi yao kubwa ni kuwa waliamini katika mwendo wa nyota
na walikuwa na uwezo wa kutambua kila jambo muhimu linalotokea duniani kupitia
nyota, kwa hiyo ilikuwa ni kazi yao kutoa taarifa kwa mfalme endapo kuna jambo
lolote Muhimu limetokea Duniani, waliamini kuwa mwenendo wa nyota unaashiria
tukio Fulani duniani kwa hiyo ilikuwa ni kazi yao kuzisoma na kuzichunguza
angani wakati wa usiku ili kutambua jambo muhimu linalotokea duniani na wakisha
kugundua walimpa taarifa mfalme kuhusu taarifa walizozibaini.
Katika
tukio hili wenye hekima hawa waliongozwa na nyota hii ambayo ilikuwa
ikimwakilisha masihi ni kwaajili ya hayo sasa unaweza kuona Mathayo analichukua
tukio la ujio wa mamajusi kama mojawapo ya tukio la kimuujiza linalomuonyesha
Yesu kuwa ni Mfalme wa wayahudi na ni mfalme wa ulimwengu na kuwa amekuja
kwaajili ya watu wote,
Mathayo 2:1-2 “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za
mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema,
Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake
mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.”
Mamajusi
walikuwa na utambuzi kupitia nyota waliyoiona kuwa ilikuwa inaashiria kwamba
amezaliwa Mfalme na kiongozi mkuu sana swa na unabii wa Kiyahudi, baadaye Nyota
hiyo iliwaongoza mpaka Bethelehemu mahali ambapo kweli walimkuta Mtoto huyo
ambaye ni Bwana wetu Yesu Kristo, walijawa na furaha kubwa sana na walimuabudu
na kutoa sadaka yao
Mathayo 2:8-12. “Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize
sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende
nimsujudie. Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile
nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, hata ikaenda ikasimama juu ya mahali
alipokuwapo mtoto. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno.
Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka
wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na
uvumba na manemane. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie
Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.”
Kinyume
na furaha waliyokuwanayo mamajusi Mfalme Herode yeye hakuwa na furaha, badala
yake aliwaita mamajusi na kutaka kujua muda sahihi tangu walipoiona ile nyota
akidai kwamba ili na yeye aweze kwenda kumshujudia, hata hivyo akiwa na nia ovu
na mpango wa siri wa kumuua mtoto Yesu
Mathayo 2:3-8 “Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na
Yerusalemu pia pamoja naye. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa
watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika
Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, Nawe
Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa
kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli. Kisha Herode
akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu
ilipoonekana ile nyota. Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize
sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende
nimsujudie”
Ashukuriwe
Mungu kwa sababu alifahamu nia ya Herode na hivyo Mungu alisema na mamajusi na
kuwaonya kutokurudi Yerusalem na kumpa taarifa mfalme kwani alikuwa na nia ovu,
Mathayo 2:1-13 “Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie
Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine. Na hao walipokwisha kwenda zao,
tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka,
umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa
maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize.”
Tukio
hili linatufundisha ya kuwa Mungu ni mwenye nguvu kubwa sana na ndiye
anayeutawala ulimwengu na vyote vilivyomo, yeye hufanya kazi katika mazingitra
yoyote kutokezesha kile ambacho yeye anakitaka, anaweza kufanya chochote kwa
kawaida au kwa njia ya muujiza, anaweza kuingilia kati lolote kwa yoyote kwa
jinsi yoyote, Mungu yuko nyuma ya kila tukio linalotokea Duniani, Hakuna sababu
ya kulaumu chochote wala kujisumbua kwa lolote linalotutokea Duniani wala
hatupaswi kumuhoji Mungu kwanini hili linatokea, Mungu anajua kila kitu ana
nguvu ya kutumia mazingira na ana nguvu ya kuwatumia watu wote, anauwezo wa
kuzungumza hata na wanajimu, na wachawi na waganga na wenye hekima na hakuna
mtu wa kukutikisa wala kubadilisha makusudi na mpango wa Mungu katika maisha
yako na yangu!
Herode
ambaye ni adui mkubwa wa Yesu Kristo aliweza kutambua kuwa Yesu ni nani na
alimuogopa, alifahamu kuwa Yesu ndiye mtawala wa ulimwengu na ni mfalme mwenye
nguvu na kuwa kila kitu katika maisha yake kinatakiwa kubadilika na hivyo
alikusudia kumuua.
Dunia
haiwezi kuvumilia kujua na kuona nyota yako iking’ara, hawawezi kufurahia
mafanikio yako, unapoona unapigwa vita kubwa maana yake umebeba kusudi kubwa,
vita kubwa kazi kubwa, mtu mkubwa majaribu makubwa, mtu mgumu majaribu magumu
lakini yote katika yote Mungu anachukua utawala anamiliki kila jambo, Mungu
ndiye mratibu wa kila jambo kwenye maisha yetu na hivyo hatupaswi kuogopa, kama
alivyo mtetea mwanaye atatutetea na sisi, kama alivyomficha mwanae kule Misri
atakuficha na wewe hata watakapoangamia wote wanaoitafuta roho yako,
unapokaribia kuiadhimisha siku njema ya Christmas na kuadhimisha kuzaliwa kwake
kumbuka yeye ni mtetezi wetu aliye hai na atakwenda kukutetea ni wakati wa
nyota yako kung’aa na hakuna wa kukuzuia uwe na wakati mzuri na mkesha mzuri wa
kuadhimisha kuzaliwa kwa Kirsto katika jina la Yesu Kristo ameen!
Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana
tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima
moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa
kiburi chake.”
Rev. Innocent
Samuel Kamote
Mkuu wa Wajenzi
mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni