Jumatatu, 25 Desemba 2023

Hata ulipowadia utimilifu wa wakati !


Wagalatia 4:4-5 “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.”

 


 

Utangulizi:

Leo ni sikukuu ya Christmas, wakristo wote Nchini wanaungana na wakristo wengine duniani kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulikotokeza zaidi ya miaka 2000 iliyopita huko Bathelehemu, Israel. Katika wakati huu ni muhimu kujikumbusha kuwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo hakukutokea kwa bahati mbaya kwani Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulitokea kwa wakati mkamilifu, katika mpango wa Mungu, watu wengi wanaweza wasielewe umuhimu wa Yesu kuzaliwa kwa wakati,  na ikawa kwao kama watu ambao walikuwa na shughuli nyingine wakati Yesu anazaliwa wasijue kuwa mwokozi amekuja kwaajili yao, Kuzaliwa kwa  Yesu Kristo huu ulikuwa ni mpango kamili wa Mungu, na ulitekelezwa ulipowadia utimilifu wa wakati, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Hata ulipowadia utimilifu wa wakati!

·         Kukombolewa kwa waliokuwa chini ya sheria

·         Kupokea hali ya kuwa wana

 

 Hata ulipowadia utimilifu wa wakati.

Wagalatia 4:4-5 “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.”

Neno Utimilifu wa wakati katika Biblia ya kiyunani linasomeka kama “Pleroma - Chronos”. Pleroma ikiwa na maana ya Kujaa kabisa, au kukamilika completion or Filled, na Chronos ni Time  kwa hiyo utimilifu wa wakati kwa kiingereza Fullness of the time  yaani ni kama mtu aliyekuwa anakijaza chombo kwa muda maalumu, kisha kikajaa, au muda uliokusudiwa kwa kitu Fulani kutimia, kwa hiyo Kiswahili kilichotumika hapo ni sahihi na chepesi zaidi ya mafafanuzi sawa tu utimilifu wa wakati, Kwa hiyo Kuzaliwa kwa Yesu Kristo hakukutokea tu kwa bahati mbaya, bali kulitoka kwa wakati mtimilifu ambao Mungu alikuwa ameukusudia katika mpango wake!.

Huu ulikuwa ni wakati utawala wa kiyunani ulikuwa umeisha na umeacha athari ya Lugha ya Kiyunani (Greek) na tamaduni kadhaa za kiyunani (Hellenistic culture), Lugha hii kwa wakati huo ilikuwa ni lugha ya kisomi na iliyotumiwa na wasomi wengi wa nyakati zile jambo lilolopelekea Maandiko kutafasiriwa na hata kuandikwa katika kiyunani kwani ulimwengu wa wakati huo ulikuwa ni ulimwengu wa kisomi sana na athari zake zilikuwa zimeachwa na Wayunani.

Warumi walikuwa sasa ndio wanaotawala ulimwengu wa wakati huo na walikuwa ni watu waliohakikisha Amani inakuwepo kila mahali duniani, na pia waliunganisha ulimwengu wa wakati ule kwa mifumo ya bara bara zilizorahishisha mawasiliano na ulinzi mkali uliohakikisha Amani inatawala kila mahali duniani, utaratibu na ustawi mkubwa sana wa kijamii (Pax Romana)

Wayahudi walikuwa na matazamio Makali ya kutimizwa kwa unabii hususani wa Daniel kuhusu majuma sabini,  na walikuwa tayari wamejiandaa kumpokea Masihi, wakielewa wazi kuwa wakati wowote masihi atazaliwa, ili awakomboe na kuleta faraja na kuondoa uchovu wa kukandamizwa na utumwa wa kigeni na utumwa wa sheria

Pia ulikuwa wakati ambapo watu wamechoshwa na kufilisika sana kiroho, wamefilisika kidini na kiimani, na walikuwa wameshindwa kabisa kuishi sawa na sharia ya Musa ambayo kwa wakati huu ilikuwa inaonekana kuwa ina viwango ambavyo wanadamu wa kawaida hawaviwezi, dhambi ilikuwa imewaelemea na wanyama wa kutekeketzwa kwaajili ya dhambi lilianza kuonekana kama jambo lisilowezekana tena

Ni katika wakati huu Ndipo Yesu anazaliwa, anazaliwa katika wakati ambapo watu walikuwa wamefilisika kiimani, kidini na kiuadilifu, uadui kati ya mwanadamu na Mungu ulikuwa umeongezeka sana, kwa hiyo kuja kwa Yesu na kuzaliwa kwake kwa wakati hasa wakati ambapo wanadamu wamechoka, ilikuwa ni kuleta auheni na unafuu mkubwa, kuleta neema na kutangaza rehema ulikuwa ni wakati sahihi kwa wanadamu kutangaziwa wokovu ambao wameusubiri kwa muda wakati wa kukombolewa kutoka katika laana zinazotokana na wanadamu kushindwa kuzitii sheria za Mungu, kuelekea wazi katika adhabu ambazo kwa ukweli hakuna mtu angeweza kulipa  na ndio katika wakati huu sasa Mungu anamleta Yesu Kristo kwaajili ya ukombozi.

Sio hivyo tu Paulo mtume anazungumzia wakati ambapo mtoto wa kifalme ambaye alikuwa chini ya usimamizi anapoanza kuhesabika kama mtoto wa kifalme ambaye ameiva na yuko tayari kwa utawala na kuanza kujitegemea kutoka chini ya mwangalizi, kama ukiangalia vizuri kwa kina katika kitabu cha Wagalatia Paulo anazungumza yafuatayo:-

Wagalatia 4:1-5 “Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote; bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba. Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia. Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.”

Paulo anachokizungumza hapo, ni utaratibu uliokuwa unafuatwa katika nyumba za kifalme, ambapo mtoto wa kifalme anapokuwa mdogo anakuwa chini ya uangalizi wa mtu maalumu anayeitwa kwa kiyunani “EPITROPOS”  yaani kwa kiingereza  Domestic Manager or guardian yaani Mwangalizi maalumu wa watoto wa kifalme nyumbani, ambaye kazi yake ni kutoa maelekezo na kufundisha mtoto wa kifalme namna anavyotakiwa kuishi kama mfalme maelekezo anayoyatoa yanaitwa “PEDAGOGY”  yaani mafundisho na melekezo maalumu, kwa hiyo watoto wote wa kifalme huwa chini ya watu hao wakipokea maelekezo na mafundisho, wakielekezwa na kuamuliwa nini cha kufanya, wapi waende wapi wasiende, wakati mwingine hufudishwa hata vita au kupelekwa jeshini na kushiriki vita na wakati huu wanakuwa kama watumwa tu, mpaka  unapofikia wakati uliokusudiwa na mfalme  wawe wamefuzu Mfalme huwapangia majukumu ya kiutawala au kuwapa majimbo ya kurithi kiutawala ili watawale pamoja naye

Kwa msingi huo basi tunapozungumza kuhusu utimilifu wa wakati, ambao Paulo mtume anauzungumza ni wakati ambapo Mungu alikusudia sasa wa kuwaweka watu huru kutoka katika vifungo mbalimbali pamoja na kifungo cha sharia ya Musa (Torati), na kuwakomboa wanadamu ambao walikuwa wanateswa na mateso ya aina mbalimbali na laana zinazotokana na kuivunja torati sasa anazaliwa Kristo kwa wakati kwa kusuda la kutukomboa kutoka katika hali ya utumwa.

Wagalatia 3:11-14 “Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo.Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.”

Kwa hiyo utimilifu wa wakati unaozungumzwa hapo, kimsingi ni wakati wa kuwapa wote waliomuamini Yesu mamlaka kamili, ya kuondoka kuwa chini ya sheria na kuwa wafanya sheria hii ni Baraka kubwa sana kuliko zote, wakati Israel alipokuwa akiwabariki watoto wake na kutoa unabii ya kuwa masihi yaani mtawala atatokea katika kabila la Yuda, kabila hii ilibarikiwa pia kuwa haitakosa mfanya sheria katika miguu yake

Mwanzo 49:8-10 “Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia. Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemwamsha? Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.”

Ni aina hii ya mamlaka, kutumikiwa, kuwa na uweza dhidi ya adui zetu, kutumainiwa, kutokukosa mawindo, kuogopwa, kuwa na mamlaka, kuwa wafanya sheria, hii inakuja kwa kila mtu anayemuamini Bwana Yesu na huu ni wakati wa furaha sana kwani kristo amekuja kutuondoa katika hali ya unyonge na kutuleta katika wakati wa kutawala na kumiliki na kuwashinda maadui zetu, hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu anamtangazia kila mmoja wetu kuwa umewadia utimilifu wa wakati sasa, ni wakati wa ushindi, ni wakati wa kutawala, ni wakati wa kumiliki, ni wakati wa kuweka huru, ni wakati wa kufurahia uhuru kutoka utumwani ni wakati wa kuondoka katika uonevu ni wakati wa Amani na utulivu ni wakati wa ustawi, ni wakati wamkunena kwa lugha mpya, ni wakati wa kutembea na uungu ndani yetu, wakati wa kupakwa mafuta, wakati wa kuzungumza kwa mamlaka ya kifalme, wakati wa ushindi, wakati wa upenyo, wakati wa kutoboa, wakati wa kuyataja yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuufurahia wakati mtimilifu uliokusudiwa kwa Baraka zake katika jina la Yesu Kristo Amen!  

Kukombolewa kwa waliokuwa chini ya sharia.

Katika utimilifu huo wa wakati Paulo mtume anaeleza kuwa moja ya sababu ya ujio wa Yesu Kristo ni kuwakomboa wanadamu katika laana ya torati, yaani wale waliokuwa chini ya sheria, hapa inamaanisha sharia ya Musa ambayo ki msingi inapatikana katika vitabu vitano vya Musa, ambayo ina maelekezo yote ya namna ya kumuabudu Mungu na kumtumikia jambo ambalo kwa ujumla halikuwa rahisi, kuivunja torati kuliambatana na tangazo la laana kubwa na nyingi sana  nzito na za kusikitisha mno angalia :-

Kumbukumbu la torati 28:15-56 “Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata. Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani. Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia. Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo, Bwana atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo. Bwana atakuambatanisha na tauni, hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo kwa kuimiliki. Bwana atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa hari ya moto, na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie. Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma. Bwana atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga; itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie. Bwana atakufanya upigwe mbele ya adui zako; utawatokea juu yao kwa njia moja, lakini utakimbia mbele yao kwa njia saba; nawe utatupwa huko na huko katika falme zote za duniani. Na mzoga wako utakuwa chakula cha ndege wote wa angani, na wanyama wote wa duniani, pasiwe na mtu wa kuwafukuza. Bwana atakupiga kwa majipu ya Misri, na kwa bawasiri, na kwa pele, na kwa kujikuna, ambayo hupati kupoa. Bwana atakupiga kwa wazimu, na kwa upofu, na kwa bumbuazi la moyoni; utakwenda kwa kupapasa-papasa mchana, kama apapasavyo kipofu gizani, wala hufanikiwi katika njia zako; nawe sikuzote utaonewa na kutekwa nyara, wala hapatakuwa na mtu wa kukuokoa. Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake.Ng'ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, usile nyama yake; utanyang'anywa punda wako mbele ya uso wako kwa jeuri, usirudishiwe; kondoo zako watapewa adui zako, usipate mtu wa kukuokoa. Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako. Matunda ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na kupondwa chini daima; hata uwe mwenye wazimu kwa yaonwayo na macho yako, utakayoyaona. Bwana atakupiga magoti na miguu kwa jipu lililo zito, usilopata kupozwa, tokea wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa. Bwana atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe. Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza Bwana. Mbegu nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila. Utapanda mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani italiwa na mabuu. Utakuwa na mizeituni katika mipaka yako yote usijipake mafuta yake; kwa kuwa mzeituni wako utapukutika. Utazaa wana na binti, lakini hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani. Miti yako yote, na mazao ya nchi yako, nzige watakuwa nayo.Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini.Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia.Na laana hizi zote zitakujilia juu yako, zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake alizokuagiza; nazo zitakuwa juu yako kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako milele; kwa kuwa hukumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote; kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta Bwana juu yako, kwa njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza. Bwana atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai; taifa usiloufahamu ulimi wake; taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana; naye atakula uzao wa ng'ombe wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa; wala hatakuachia nafaka, wala divai, wala mafuta, wala maongeo ya ng'ombe wako, wala wana-kondoo wako, hata atakapokwisha kukuangamiza. Naye atakuhusuru katika malango yako yote, hata kuta zako ndefu, zenye maboma, ulizokuwa ukiziamini, zishuke, katika nchi yako yote kila upande; naye atakuhusuru katika malango yako yote kila upande, katika nchi yako yote aliyokupa Bwana, Mungu wako. Nawe utakula uzao wa tumbo lako mwenyewe, nyama ya wana wako na binti zako aliokupa Bwana, Mungu wako; katika mazingirwa na katika mkazo utakaokazwa na adui zako. Mtu mume kati yenu aliye mwororo na laini sana, jicho lake litakuwa ovu juu ya nduguye, na juu ya mke wa kifuani mwake, na juu ya masalio ya wanawe waliosalia naye; hata asitake wao mmojawapo apewe katika nyama ya wanawe atakaowala, kwa kuwa hana kitu kilichomsalia kwake; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako yote. Mwanamke kati yenu aliye mwororo na laini, ambaye hangehatirisha kuweka wayo wa mguu wake nchi kwa umalidadi na ulaini, jicho lake huyu litakuwa ovu juu ya mume wa kifuani mwake, na juu ya mwanawe, na juu ya binti yake,”

Kutii maagizo yote na amri zote za Mungu kwa wanadamu halikuwa jambo rahisi, ilikuwa ni dhambi na ilileta laana hii isingeliwezekana kwa wayahudi na hata wasio wayahudi, lilikuwa ni agizo gumu sana ambalo kila wakati lingekufanya ujione mwenye dhambi, unayestahili hukumu na hasira ya Mungu na kifo tu Petro mwenyewe alisema wazi kuwa sharia ya Musa lilikuwa ni kongwa ambalo sisi wala baba zetu tusingeliweza kulimudu angalia

Matendo 15:7-11 “Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini. Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia, akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi; wala hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani. Basi sasa mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua. Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao.”

Unaona ni jambo la kushangaza ya kuwa walimu kutoka uyahudi walisambaa ameneo mbalimbali na kuwafundisha wakristo kuishika sharia ya Musa jambo ambalo lingewarudisha nyuma utumwani mahali ambako Kristo alikuwa amekwisha kuwatoa na hivyo kuishika sharia ya Musa tena kungeleta laana, kwa msingi huo Yesu alizaliwa kwa wakati ili pia aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika laana ya Torati ujio wa Yesu Kristo duniani ulikuwa ni kwa utimilifu wa wakati wakati wa kuwakomboa wanadamu kutoka katika kongwa zito la Sheria hii ina maana gani? Neno ukombozi linalotumiwa na Paulo katika Wagalatia  kwa kiyunani ni EXAGORAZO ambalo lina maana ya kununua, kwamba kama mtu ni mtumwa wa mtu na yuko chini ya sharia na unataka kumkomboa kutoka katika sharia za mtu huyo unamnunulia uhuru wake  na anakuwa huru mbali na sharia na adhabu za mtu huyo kwa hiyo yeye aliyenunuliwa na kuwekwa huru katika utumwa wa sharia maana yake hapaswi tena kuwa chini ya sharia na kanuni  za Musa ambazo wana wa Israel walilazimika kuzishika, sio hivyo tu hata laana za sharia hazituhusu, kwa namna yoyote ile tusingeweza sisi kuishika sharia yote ya Musa kwa uwezo wetu wenyewe na ndio maana Kristo alikuja kuitii kwa niaba yetu na kutulipia deni huko ndio kuikamilisha torati na manabii.

Mathayo 5:17 “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.”

Warumi 8:33-39 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

Yesu amekwishakufanya kila kitu kwa niaba yetu, hatuwezi tena kuwa chini ya sharia ya kitumwa wala hatuwezi kuadhibiwa na Mungu kwa kushindwa kuishi sawa na sharia, wala hatuhitaji tena kuua au kuchinja wanyama kwaajili ya dhambi zetu na laana zetu kwani Kristo amemaliza kila kitu hii sasa ina maana gani tunaweza kufanya lolote tulipendalo hapana iko sharia ya kifalme tumeondolewa katika utumwa sharia ambayo ilikuwa Mwalimu, wa watoto wa mfalme, sasa tumekuwa wafalme wafanya sharia na iko sharia ya kifalme ambayo kwayo inatuongoza ni ipi hiyo hii hapa

Yakobo 2:8 “Lakini mkiitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa, Mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda vema.”

Kwa hiyo kukombolewa katika laana ya torati maana yake ni kuwekwa huru katika kushika na kufuata sharia na kanuni ambazo zingeleta hasira ya Mungu juu yetu, kwa hiyo Yesu aliyahukumu hayo pale Msalabani na sasa sisi tunaweza kuishi kwa njia iliyo rahisi kumpenda Mungu na kuwapenda wanadamu wenzetu jambo ambalo litatupelekea kufikiri pale tunapotaka kuwafanyia dhambi wengine

Mathayo 7:12 “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii.”

Kupokea hali ya kuwa wana.

Paulo anaeleza manufaa mengine ya Yesu kuja katika utimilifu wa wakati, kwamba tunapokea hali ya kuwa wana au watoto wa Mungu, hapa anamanisha kwa wale wanaompokea

Yohana 1:12 -13 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.”

Ni mtoto yule yule aliyekuwa chini ya Mwangalizi sasa anapatiwa nafasi ya kutawala pamoja na baba yake, neno linalotumika katika maandiko kupokea kuwa mwana ni Adoption ambalo maana yake ni KUMRITHI au KUMUASILI, ni kitendo cha mtu hususani mtoto kupewa haki kwa baba mwingine  na kuhesabiwa kuwa amestahili kuwa mwanae wa kudumu aitwe kwa jina lake na kuwa na haki zote sawa na watoto wa baba husika jambo hili linathibitishwa kwa kuvunjiliwa mbali kwa hofu ya kuona Mungu kama Mtawala na kumuhisi Mungu kuwa ni baba na ndani yetu tunapewa uhakika wa kumuita Mungu baba yetu kupitia muunganiko wa kazi za Roho Mtakatifu, Baada ya kutununua na kutuweka huru mbali na sharia anatufanya kuwa watoto wake na sio watumwa tena

Wagalatia 4:6-7 “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.”

Warumi 8:15 -16 “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;”

Ujio wa Yesu Kristo duniani kwa wakati mtimilifu ulikusudiwa na Mungu kutukomboa kutoka katika hali ya utumwa na kutupandisha kwa heshima katika ulimwengu wa roho ili awe baba yetu na tuweze kutawala pamoja naye, hatupaswi kuogopa tena, tunapaswa kuwa na ujasiri, dhambi sio tatizo tena, adhabu ya Mungu na hukumu zake hazina nguvu tena sharia ya kifalme ndiyo dira yetu hakuna kitu cha kututenga na upendo wa kristo, tunapoadhimisha siku kuu hii ya Christmas hatuna budi kufahamu kuwa Bwana wetu Yesu amekuja kuyapandisha juu maisha yetu amekuja kutupa thamani, amekuja kutubadilisha kutoka chombo cha hasira za Mungu na kuwa chombo cha upendo wa Mungu, sisi sasa tuna mamlaka kamili  sisi ni kama yeye ni wafanya sharia tunayoyatamka yanakuwa, kwanini kwa sababu sasa tunakuwa kama yeye alivyo  maana tu watoto wake na tamko la mfalme ni sharia ona  

1Yoahan 4:16-18 “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake. Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; KWA KUWA, KAMA YEYE ALIVYO, NDIVYO TULIVYO NA SISI ULIMWENGUNI humu. Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo.”              

Hapa hapa ulimwenguni sisi sio wa kawaida tena, maisha yetu yamebadilishwa kupitia kuja kwa Yesu Kristo kwa utimilifu wa wakati, kila mmoja anaweza kuutumia wakati huu kumkubali Yesu na kumkaribisha ili awe Bwana na mwokozi wa maisha yake, sisi tuliompokea tuliutumia wakati vizuri wewe nawe hujachelewa leo unaposikia ujumbe huu na unaposoma ujumbe huu anza kuchangamka ukijua kuwa Mungu anatupenda na ulipowadia utimilifu wa wakati alimtuma Kristo atukomboe, Kuna watu hapa leo ni wakati wao wa kuponywa, kuna watu ni wakati wao wa kutoka kwenye madeni, kuna watu ni wakati wao wa kupokea heshima, kuna watu ni wakati wao wa kuolewa, kuna watu ni wakati wao wa kutolewa katika vifungo vya utumwa, kuna watu ni wakati wao wa kuponywa, kuna watu ni wakati wao wa ukombozi, Kuna watu ni wakati wao wa kutoka katika adhabu, kuna watu ni wakati wao wa kufunguliwa, kuna watu ni wakati wao wa kupandishwa cheo, kuna watu ni wakati wao wa kuinuliwa, kuna watu ni wakati wao wa ushindi, kuna watu ni wakati wao wa kuongezeka, kuna watu ni wakati wao wakuzaa sana, kuna watu ni wakati wao wa kutoka katika magereza za aina mbalimbali, kuna watu ni wakati wao wa kuacha kudharaulika, kuna watu ni wakati wao wa kufurahia maisha, kuna watu ni wakati wao wa kukomesha udhalilishaji, kuna watu ni wakati wao wa kupata mpenyo, kuna watu ni wakati wao wa kuvikwa vazi jipya, kuna watu wakati wao mtimilifu umewadia wa kufurahia Baraka za Mungu wewe sio mtumwa tena, hofu imetupwa mbali, wewe ni mwana wa Mungu haleluyaaaaaaa!, leo nafanya sharia mpya kwa kukutangazia kuwa wakati wako mtimilifu umewadia Yesu Kristo yuko hapa leo kukuhudumia haleluyaaaaa!, wewe sio wa chini tena wewe ni wajuu, wewe sio wa kuonewa tena, wewe sio wa kupokea maagizo, wewe ni wa kutoa maagizo, Kuzaliwa kwa Yesu ulipowadia utimilifu wa wakati kumemuinua mwanadamu na kumleta katika heshima ile kubwa ambayo malaika wanaichungulia leo ni siku ya kusimikwa kwako kuwa mfalme na kutoka kifungoni, kutoka gerezani, kutoka kwenye migandamizo na kuwa mtawala na lolote utakalolitamka kwa jina la Yesu Kristo litageuka kuwa Baraka na kutimia na lolote watakalokutamkia la kukutakia laana litawarudia juu yao Hakuna mtu alimtukana mfalme akaishi, Happy Christimas !

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima. !







Hakuna maoni: