Mathayo 27:45-50 “Basi tangu saa sita
palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza
sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu,
Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao
waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao
akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi,
akamnywesha. Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa.
Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.”
Utangulizi:
Moja ya matukio muhimu tunayoweza
kuyazingatia katika msimu wa kukumbuka Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, Kifo
chake na kufufuka kwake ni Pamoja na Saa ile aliyokata roho, yaani saa tisa,
Karibu kila mwandishi wa Injili anaonyesha tukio hili la kipekee la Yesu kukata
roho saa tisa, licha ya kuwepo kwa giza kubwa na la kipekee kuanzia saa sita mpaka
saa tisa na kisha saa tisa Ndipo Yesu alikata roho. Tunaweza kuona, tukio hilo
likirudiwa tena na tena katika injili nyingine:-
Marko 15:33-34 “Na ilipokuwa saa sita,
palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa. Na saa tisa Yesu akapaza
sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu,
Mungu wangu, mbona umeniacha?”
Luka 23:44-46. “Hapo ilikuwa yapata saa
sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake;
pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee
Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu”
Tukio la Yesu Kristo kufa saa
tisa jioni lina umuhimu mkubwa sana kwa mujibu wa injili na ndio maana
limeelezwa na injili zote tatu, tunaelezwa kuwa katika muda huo tofauti na
kawaida kulikuwa na giza tangu saa sita hata saa tisa, na saa tisa Yesu alipaza
Sauti ya kilio Mungu wangu Mungu wangu Mbona umeniacha, na kisha Yesu alifikia
hatua ya kutimiza kusudi lote la ukombozi wa mwanadamu kwa kujitoa dhabihu yeye
mwenyewe, kwa ukombozi wa Mwanadamu. Lakini labda swali muhimu linaweza kubakia
pale pale kwa nini saa tisa? hilo linatupa nafasi ya kutafakari somo hili hata
saa tisa kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu yafuatayo:-
·
Saa tisa
katika masimulizi ya kale ya tamaduni za kiyahudi
·
Saa tisa
kwa mujibu wa maandiko
·
Hata saa
tisa!
Saa tisa katika masimulizi ya kale ya tamaduni za kiyahudi
Kwa mujibu wa masimulizi ya Kale
Wayahudi waliamini kuwa Mungu alikuwa na tabia ya kumtembelea Adamu katika
Bustani ya Edeni, Saa ya jua kupunga, Kwa kiingereza “In the cool of the day” Ruach/yom
Mwanzo 3:8-9 “Kisha wakasikia sauti ya
BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe
wakajificha kati ya miti ya bustani, BWANA Mungu asiwaone. BWANA Mungu akamwita
Adamu, akamwambia, Uko wapi? ”
Kwa mujibu wa masimulizi ya
kiyahudi Muda au wakati wa jua kupunga katika unaitwa YOM ambalo kwa tafasiri wakati wa
jioni ambapo wayahudi walikuwa wanaamini ni mida ya saa tisa, Kwa mujibu
wa masimulizi ya kiyahudi Muda huu kwa kawaida Mbingu huwa zinafunguka, na
Mungu huwa ana kuwa na shauku ya kuimarisha uhusiano wake na wanadamu, hili ni
moja ya jambo la kwanza na muhimu ambalo tunalipata katika Masimulizi ya
kiyahudi na ndio maana moja ya saa za maombi katika jumuiya ya kiyahudi ni
pamoja na kuomba saa tisa. Meno mawili ya kiebrania yanatumika kuelezea Saa ya
jua kupunga in the cool of the day ambalo ni Ruach na Yom yakiwa na
maana wakati wa utembeleo wa Roho wa Mungu.
Aidha kweli nyingine ya
Masimulizi ya kale ya kiyahudi inasema ni katika muda huu, Mungu alimpa Adamu
usingizi Mzito na kuchukua sehemu ya ubavu wake na kumuumba Mwanamke.
Mwanzo 2:21-23 “BWANA Mungu akamletea Adamu
usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama
mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu BWANA Mungu akaufanya
mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa
yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa
katika mwanamume.”
Usingizi mzito katika lugha
ya kiibrania wanatumia neno TARDEMA
ambalo maana yake ni hali inayosababishwa na Mungu mwenyewe kwaajili ya
kumletea mwanadamu ufunuo muhimu, au kufanya jambo la Muhimu kwa mwanadamu
Masimulizi mengine ni kuwa saa
tisa ni muda ambao wayahudi walikuwa wanautumia kwa maombi, kuna vipindi
vikubwa vitatu vya maombi katika tamaduni za kiyahudi. Hata manabii na
waandishi wa zaburi wana nukuu kadhaa katika maandiko, zinazoashiria kuwa
wayahudi walikuwa na vipindi vitatu vya maombi na ambavyo wameendelea kuwa
navyo hata siku za leo angalia
Zaburi 55:16-17 “Nami nitamwita Mungu, Na
Bwana ataniokoa; Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua, Naye
ataisikia sauti yangu.”
Daniel 6:10-11 “Hata Danieli, alipojua ya
kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na
madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;)
akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake,
kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.Basi watu hao wakakusanyika pamoja,
wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake”
Vipindi hivyo vitatu vya ibada za
maombi, ambavyo Wayahudi wanaendelea navyo mpaka leo kwa lugha ya asili ya
Kiibrania vinaitwa SHACHARIT, MINCHA NA
MAARIV ambavyo tunavichambua kama ifuatavyo:-
1. Shacharit: - huu ni muda wa maombi ya
alfajiri ambapo Wayahudi husali baada ya kupambazuka kwa jua, Maombi haya
hufikiriwa kuwa ni maombi ya muhimu sana ambayo wayahudi huamini kuwa wanapokea
Baraka kubwa sana, maombi au sala ya alfajiri huambatana na Kusifu, kusoma
maandiko hususani Torati. Na hii inasadikiwa kufanyika kati ya muda wa asubuhi
mpaka saa tatu na hasa kilele chake ni saa tatu.
2. Mincha: - huu ni Muda wa maombi ya
jioni (afternoon) Maombi haya ndiyo ambayo hufanywa saa tisa, ni maombi mafupi
sana, ukilinganisha na Maombi ya alfajiri yaani Sacharit, maombi haya ya saa tisa hujumuisha kuomba, kusoma zaburi
na kunyamaza kimyaa (Amidah) kusimama kimyaa, nah ii inasadikiwa kufanyika kati
ya saa sita mpaka saa tisa na kilele chake hasa kilikuwa saa tisa
3. Maariv au Arvit: Maariv pia huitwa Maarib au Magharibi kwa Kiswahili,
Maombi haya yanafanyika baada ya jua kuzama ni kwaajili ya kuukaribisha usiku
na kuuaga mchana, maombi haya hujumuisha Baraka, na ukiri wa SHEMA ukiri wa shema ni ukiri
unaopatikana katika Kumbukumbu la torati 6:4-5 nimenukuu hapa:-
Kumbukumbu 6:4-5 “Sikiza,
Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu
wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.”
Shema ndio kiini
kikuu cha Imani ya kiyahudi, Maombi haya ya Maariv au magharibi kilele chake ni
jioni saa kumi na mbili wakati wa kuzama kwa jua.
Kwa hiyo kwa mujibu wa tamaduni
za kiyahudi, na dini ya kiyahudi, yanashikiliwa na wayahudi katika maisha yao
yote na siku zote, Kwa hiyo kuna saa tatu, kuna saa tisa na kuna saa kumi na
mbili, Kwa hiyo Saa tisa ni moja ya saa
nyeti katika tamaduni na dini ya kiyahudi. Wayahudi wengi waliamini kuwa muda
huu ni muda mwema sana Saa tisa Muda wa dhabihu ya jioni Mungu husikia kwa
haraka sana na hujibu kwa haraka sana, na ni saa ya miujiza mikubwa.
Zaburi 141:1-2 “Ee Bwana, nimekuita, unijie
hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo. Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba,
Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.”
Saa tisa kwa mujibu wa maandiko:
Nadhani sasa unaweza kupata picha
ya umuhimu was aa tisa, ya kwamba ni saa yenye neema ya ajabu, ni saa yenye
faida kubwa sana, kila mtu aliyeokolewa ana neema kubwa na amepewa neema ya
kuzijua siri za ufalme wa Mungu, lakini kufunuliwa kwa nguvu za ufalme wa Mungu
kunategemeana sana na ujuzi wa kanuni, kama vile ambavyo ziko hesabu huwezi
kuzifanya bila kujua kanuni, au huwezi kupata majibu bila kujua kanuni, ufunuo
kuhusu kanuni unatofautiana kati ya Mtu na mtu, Kadiri unavyozijua kanuni hizo
ndio unajiweka katika nafasi kubwa sana ya mafanikio na siri za ufalme wa Mungu
na kufaidika kiroho, kwa hiyo maombi ya saa tisa ni ufunuo wa Muhimu sana kwako
leo, lakini ili uweze kuwa na ufahamu sasa tufuatane nani katika maandiko
kuweza kuona saa hii kwa mujibu wa maandiko:-
-
Ulikuwa
ni Muda ambao Bwana alimtembelea Ibrahimu na kuwa na ushirika naye pamoja
na Sarah Na kumuahidi kupata mtoto Mwanzo
18:1-2 “BWANA akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni
ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari.
Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye
alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi,
akasema, BWANA wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa
mimi mtumwa wako.” Neno Mchana wakati wa Hari katika kiibrania
linatumika tena neno YOM ambalo lina
maana ya jioni mida ya saa tisa
-
Ulikuwa
ni Muda ambao makuhani waliagizwa kutoa dhabihu ya jioni Kutoka 29:38-42 “Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi;
wana-kondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku daima. Mwana-kondoo mmoja
utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni; tena, pamoja na
mwana-kondoo mmoja utatoa vibaba vitatu vya unga mzuri uliochanganyika na
mafuta yenye kupondwa, kiasi cha kibaba na robo kibaba; na divai kiasi cha
kibaba na robo kibaba, iwe sadaka ya kinywaji. Na huyo mwana-kondoo wa pili
utamchinja wakati wa jioni, nawe utamfanyia vivyo kama ile sadaka ya unga ya
asubuhi, na kama ile sadaka yake ya kinywaji, iwe harufu nzuri, ni dhabihu ya
kusongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto. Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele
katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya BWANA;
hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo.”
-
Ulikuwa
ni Muda wa kuchoma au kufukiza uvumba wakati wa dhabihu ya jioni Kutoka 30:7-8 “Na Haruni atafukiza uvumba wa manukato juu yake; KILA
SIKU ASUBUHI atakapozitengeneza zile taa, ataufukiza. Na Haruni atakapoziwasha
zile taa WAKATI WA JIONI, ATAUFUKIZA, UWE UVUMBA WA DAIMA mbele za BWANA katika
vizazi vyenu vyote.”
2Nyakati 13:11 “nao
humtolea Bwana kila asubuhi, na kila jioni, sadaka za kuteketezwa na fukizo la
manukato; mikate ya wonyesho pia huiweka kwa taratibu yake juu ya meza
takatifu, na kinara cha dhahabu chenye taa zake, kuwaka kila jioni; kwa maana
sisi twayalinda malinzi ya Bwana, Mungu wetu; bali ninyi mmemwacha.”
Luka 1:8-14 “Basi
ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za
Mungu, kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika
hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba. Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali
nje saa ya kufukiza uvumba. Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa
kuume wa madhabahu ya kufukizia. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu
ikamwingia. Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako
imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita
Yohana.Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa
kwake.”
-
Ulikuwa
ni Muda ambao Eliya alimuomba Mungu dhidi ya manabii wa baali katika mlima
Karmel na Mungu akamjibu kwa moto kutoka mbinguni 1Wafalme 18:36-39 “Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii
akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli,
na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni
mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee
Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya
kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza
sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji
yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi;
wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.”
-
Ulikuwa
ni Muda huu ambao Ezra aliomba Maombi ya toba na maombezi yaliyoleta uamsho
mkubwa sana miongoni mwa jamii ya Wayahudi waliokuwa wamerudi nyuma Ezra 9:4-8
“Ndipo wakanikusanyikia watu wote walioyatetemekea
maneno ya Mungu wa Israeli, kwa sababu ya lile kosa la watu wa uhamisho; nami
nikaketi kwa mshangao hata wakati wa sadaka ya jioni. Na wakati wa sadaka ya
jioni nikainuka baada ya kunyenyekea kwangu, nguo yangu na joho yangu
zimeraruliwa, nikaanguka magotini nikakunjua mikono yangu mbele za Bwana, Mungu
wangu; nikasema, Ee Mungu wangu, nimetahayari, naona haya kuinua uso wangu
mbele zako, Mungu wangu; kwa maana maovu yetu ni mengi, hata yamefika juu ya
vichwa vyetu, na hatia yetu imeongezeka na kufika mbinguni. Tangu siku za baba zetu
tumekuwa na hatia kupita kiasi hata leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na
wafalme wetu, na makuhani wetu, tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi,
tumepigwa kwa upanga, tumechukuliwa mateka, tumenyang'anywa mali zetu, tumetiwa
haya nyuso zetu, kama hivi leo. Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na Bwana,
Mungu wetu, hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake
patakatifu. Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika
kufungwa kwetu.”
-
Ulikuwa
ni Muda ambao Daniel nabii aliletewa majibu ya maombi yake kupitia malaika
Gabriel Daniel 9:20-22 “Basi hapo nilipokuwa
nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu
Israeli, na kuomba dua yangu mbele za Bwana, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima
mtakatifu wa Mungu wangu; naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule,
Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa
panapo wakati wa dhabihu ya jioni. Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee
Danieli, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu.”
-
Ulikuwa
ni Muda ambao Yesu Kristo alikuwa ameimaliza kazi yote Pazia la hekalu
lilipasuka na Yesu akakata roho kwa kuikabidhi roho yake mikononi mwa Baba Luka
23:44-46. “Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa
giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu
likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi
mwako naiweka roho yangu”
-
Ulikuwa
ni Muda ambao Petro na Yohana walikuwa wakihudhuria maombi katika hekalu na Kiwete
akaponywa na ukawa ndio muujiza wa kwanza katika kanisa la kwanza ulioambatana
na uamsho mkubwa na kuokolewa kwa watu wengi zaidi Matendo 3:1-7 “Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda
hekaluni, saa ya kusali, saa tisa. Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni
mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa
hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu
huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro,
akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia,
akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala
dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa
Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na
vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.”
-
Ulikuwa
ni Muda ambao Kornelio Mmataifa
aliyekuwa anaomba na kutoa sana sadaka alipata utembeleo wa malaika akiagizwa
na Mungu, kumuita Petro aje kumueleza habari za Kristo Matendo 10:1-6 “Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa
kikosi kilichoitwa Kiitalia, mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake
yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima. Akaona
katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na
kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana?
Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za
Mungu. Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye ni
mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake
iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda.”
Hata saa tisa!
Luka 23:44-46. “Hapo ilikuwa yapata saa
sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake;
pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee
Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu”
Nadhani sasa unaweza kuona
umuhimu wa saa tisa, kimsingi ilikuwa ni Muda wa kutoa dhabihu ya jioni kwa
wayahudi, ilikuwa ni saa ya kinabii, ulikuwa ni muda ambao wayahudi walipiga
tarumbeta ya wito wa kwenda hekaluni kusali, Na Yesu yeye ndiye Dhabihu Halisi
ya jioni, Alitumia Muda huo huo kukamilisha kazi yake ya ukombozi, Kristo alikuwa
amekamilisha mpango wa Mungu wa
kurudisha ushirika na wanadamu, ulikuwa ni muda ambao Msimamizi wa Mateso
askari yule alimpiga Yesu Mkuki wa ubavuni ili kuthibitisha kama amekwisha
kufa, ubavu ule ulitoa maji na damu, ambayo kimsingi ina thamani kubwa sana
katika upatanisho wa watu kwa Mungu, Yesu alipewa Mkewe kutoka katika ubavu
wake, (ni Kanisa) limezaliwa kutoka katoka moyo wa upendo wa Kristo, tunaona
miujiza mingi, muda huo, tunaona watu wakijibiwa maombi muda huo, tunaona ni
Muda ambao wayahudi hawakuomba sana walitumia muda mfupi tu, kwanini kwa sababu
Mungu ni Mungu aliye karibu anapatikana na zaidi sana ulikuwa ni muda ambao
wengi walitembelewa na malaika, kama muda wa usingizi kwa Adamu muda huo watu
wengi waliofanya kazi kutwa nzima wanaweza kusinzia kidogo, ni Muda wa muujiza,
ni muda wa rehema ni muda wa neema ya Mungu.
-
Mafunuo makubwa kuhusu Mungu yalishushwa saa
tisa.
-
Utembeleo mkubwa wa malaika ulifanyika saa tisa.
-
Kupasuka kwa Pazia la Hekalu na watu wakaona
patakatifu ilifanyika saa tisa.
-
Ulikuwa ni muda ambao wayahudi walitoa dhabihu
ya pili ya mwanakondoo kwaajili ya upatanisho wa dhambi zao, na sasa tukio hilo
la kinabii linakamilishwa na Bwana wetu Yesu
-
Dhabihu ya ukombozi wa mwanadamu ilikamilika saa
tisa
-
Yesu alitundikwa Msalabani muda wa kutoa dhabihu
ya asubuhi na alikufa muda wa kutoa dhabihu ya jioni
-
Ulikuwa muda wa Kujibiwa maombi kwa Eliya na
Mungu alijibu kwa Moto.
-
Ulikuwa ni Muda wa Kujibiwa maombi Daniel kwa
kutumiwa malaika
-
Ulikuwa ni Muda wa kutembelewa Abrahamu na
wageni watatu
-
Ulikuwa Muda wa kufukiza uvumba katika madhabahu
ya kufukiza uvumba wakati wa dhabihu ya jioni
-
Ulikuwa ni muda ambao malaika wa Bwana alimtokea
Zekaria na kupewa ahadi ya kuzaliwa Yohana
-
Ulikuwa ni Muda wa kusali kwa Petro na Yohana na
Muujiza mkubwa kwa kiwete wa miaka 40
-
Ulikuwa ni muda wa utembeleo kwa Kornelio kuona
maono ya malaika
-
Miujiza mikubwa ya kubadilika kwa maisha ya watu
ilitokea muda huo
-
Ulikuwa ni muda unaowakilisha saa ya kukubaliwa
kwa maombi, Maandiko yanaonyesha hakuna mtu aliwahi kukataliwa kujibiwa maombi
yake katika muda huo, japo Mungu anatusikia kila wakati.
-
Jambo kubwa la msingi na la Muhimu kuliko yote
saa tisa ndio saa ya ukombozi wetu, kwani Yesu alikufa saa tisa na pazia la
Hekalu lilipasuka kumpa kila mmoja nafasi ya kuweza kumfikia Mungu moja kwa
moja kupitia sadaka iliyotolewa Msalabani na mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo.
Saa tisa ilifanya kazi katika
agano la kale na katika agano jipya, siwezi kukufundisha kuwa ufanye kitu saa
tisa au uabudu saa tisa au uombe saa tisa,
lakini nataka kusema hivi, kila mtu anayeamini katika mateso, kufa na
kufufuka kwa Bwana wetu Yesu na kuokolewa hapaswi kuwa gizani kuwa anapaswa
kufanya nini muda huo na uzuri wake hauchukui muda mrefu, hivyo hata kama uko kazini,
fanya kitu kidogo kwaajili ya Uhusiano wako na Mungu, Nyenyekea utaona miujiza
mikubwa na utajua kwanini Yesu alikufa muda huo kifo kibaya sana kwaajili yetu,
utajua kwanini pazia la hekalu lilipasuka, na patakatifu pakaonekana hii maana
yake nini ni muda ambao unaweza kukikaribia kiti cha neema na kujipatia Rehema
kutoka kwake aliyekuumba na nataka nikushuhudie ya kuwa utamuheshimu milele kwa
sababu Bwana takupa neema ya kukusaidia wakati wa mahitaji yako, Kwa kweli saa
tisa ni saa ambayo unaweza kuamuru muujiza wako, saa tisa ni kama saa ambayo
Mungu yuko tayari kuamka na kufanya kitu kwaajili ya mwanadamu, ni saa ambayo
tunaweza kusema Mzee hufungua ofisi yake ili asikilize watu wake, Hebu itumie
saa hiii kwaajili ya kuamuru Baraka zako. neno hili ni kweli ni nani awezaye
kulifahamu?
Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye
kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana
maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika
mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo
yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili
tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni