Ufunuo 2:3-5 “tena ulikuwa na subira na
kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako,
ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka;
ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako,
nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”
Utangulizi:
Nyakati hizi tulizo nazo ni
nyakati za mwisho, maandiko yanasema mwisho wa mambo yote umekaribia 1Petro 4:7 “Lakini
mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala.”
Katika nyakati hizi za mwisho nabiii nyingi zinazozungumziwa kama dalili za
mwisho wa dunia zimekaribia, Na ndio maana Petro anatukumbusha kuendelea
kukesha yaani kudumu katika maombi, kuwa macho na kuongeza umakini. Moja ya
unabii mkubwa unaoonyesha kuwa tuko katika wakati wa mwisho Yesu alisema licha
ya kuongezeka kwa maasi lakini tunaelezwa kuwa Upendo wa wengi utapoa
Mathayo 24:10-12 “Ndipo wengi
watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. Na manabii wengi wa uongo
watatokea, na kudanganya wengi. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa
wengi utapoa.”
Upendo wa wengi kupoa pia ina
maana ya kwamba kutokana na kuongezeka kwa maasi na uwepo wa manabii wengi wa
uongo watu wengi watapoteza upendo wa kweli kwa Mungu na wanadamu, au tunaweza
kusema upendo kwa Mungu na kwa kanisa lake, na matokeo yake ni kuwa katika
nyakati hizi za mwisho ambazo shetani ataongeza kasi ya utendaji wake kazi, moja
ya njia kubwa sana atakayo itumia ni kuhakikisha ya kuwa ile hamu na shauku ya
kumuabudu Mungu na hata kumtumikia Mungu, kasi hiyo itapoa, na hapo ndipo
tunaposema kuwa kanisa limepoa, au kanisa limelala au kanisa limekufa na
linahitaji uamsho!
Kwa msingi huo basi katika somo
hili lenye jina Uamsho: Upendo wa Kwanza tutachukua muda kujifunza na
kutafakari kwa makini na kwa undani sana maswala yahusuyo uamsho na namna ya
kuleta uamsho katika makanisa yetu; Bwana ampe neema kila mmoja wetu kufuatilia
somo hili kwa umakini katika jina la Yesu Kristo Amen!, Tutajifunza somo hili
kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya
Uamsho
·
Namna ya
kujua kama unahitaji uamsho
·
Jinsi ya
kurejesha uamsho
Maana ya Uamsho:
Kimsingi sio rahisi kupata neno
uamsho moja kwa moja kutoka kwenye Biblia, lakini tunaweza kuliona neno uamsho
katika namna isiyokuwa ya moja kwa moja kama tunavyoweza kuona katika mstari
wetu wa Msingi ona
Ufunuo 2:3-5 “tena ulikuwa na subira na
kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini nina neno juu yako,
ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka;
ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako,
nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”
Neno uamsho kibiblia linaweza
kabisa kufananishwa na neno kuurudia upendo wa Kwanza, kama tunavyoweza kuona
wito wa Bwana Yesu katika waraka wake kwa kanisa la Efeso kupitia Yohana katika
kitabu cha ufunuo, Yesu aliliona Kanisa la Efeso kama Kanisa lililokuwa na
uvumulivu, yaani subira, kwa ajili ya jina lake tena anawaona ya kuwa
hawakuzimia moyo, lakini aliwaona pia kuwa upendo waliokuwa nao kwanza umepoa
na ndio maana anawalaumu kuwa wameuacha upendo wa Kwanza, na kuwataka kufanya
matendo yale ya kwanza, vinginevyo watapata adhabu! Wasipogeuka na kutubu,
kihistoria kanisa la Efeso lilianza na wanafunzi 12 tu ambao kimsingi walikuwa
hawajajazwa Roho Mtakatifu, na Paulo mtume alipofika hapo watu hao waliombewa
na kumpokea Roho Mtakatifu, mahali hapo Mungu alimtumia Paulo mtume kwa miujiza
mikubwa isiyohesabika, tena miujiza inayoitwa ya kupita kawaida, watu
waliokolewa kwa wingi katika mji huu na watu waliotumia mambo ya uchawi na
uganga walichoma vitabu vyao kukawa na uamsho mkubwa sana jina la Yesu
likatukuzwa
Matendo 19:1-7 “Ikawa, Apolo alipokuwa
Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana
na wanafunzi kadha wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu
mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia.
Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana.
Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini
yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina
la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu
akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri. Na jumla yao walipata
wanaume kumi na wawili.”
Matendo 19:11-12 “Mungu akafanya kwa mikono
ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo
zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.”
Matendo 19:17-20 “Habari hii ikajulikana na
Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la
Bwana Yesu likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama,
wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya
uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya
hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo
ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.”
Unapoyaangalia maandiko hayo
yanakuonyesha wazi kuwa Kanisa la Efeso lilikuwa ni moja ya Kanisa lenye nguvu
kubwa sana, watu walijazwa Roho Mtakatifu, miujiza ya kupita kawaida
ilitendeka, hofu ya Mungu iliushika mji mzima neno la Mungu lilipata nguvu,
Kanisa la Efeso lilianzishwa katika mwaka wa 52-54 AD Baada ya Kristo, Lakini unaweza kuona kuwa wakati Yesu
anawaandikia waraka katika mwaka wa 95-100
AD ni muda wa miaka kama 40 hivi au 41 Kanisa lilikuwa tayari limepoteza
hali yake ya kwanza, yaani limeuacha upendo wa kwanza na Yesu analiita kutubu,
kanisa lilikuwa limepoa, kanisa lilikuwa limelala kanisa lilikuwa linahitaji
uamsho! Je Kanisa lenu lina miaka mingapi sasa? Kama nyakati za kanisa la
kwanza miaka 40 tu watu walikuwa wameanza kupoa je kanisa lenu linahitaji miaka
mingapi sasa ili mjue ya kuwa limepoa? Baki na jibu lako moyoni! Je ni vibaya kuliamsha? je huoni ya kuwa
mnahitaji uamsho? Uamsho ni nini Hasa?
-
Neno uamsho
kwa kiingereza linatumika neno REVIVAL
ambalo tafasiri yake kwa kiingereza ni Restoration to life, consciousness,
vigor, strength au awakening in the
church or community of interest and care for matters relating to Personal
religion
-
Kwa hiyo Uamsho kurejesha kwenye uhai, kufufua,
dhamiri, au kuamsha nia ya mtu asiyejitambua ajitambue, au kurejesha nguvu
zilizopungua au kupotea
-
Uamsho ni kufufua Habakuki 3:2 “Ee Bwana, nimesikia habari
zako, nami naogopa; Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka; Katikati ya
miaka tangaza habari yake; Katika ghadhabu kumbuka rehema.” Neno la
kiingereza linalotumika kuhusu Fufua ni neno REVIVE katika kiebrania neno hilo linasomeka kama CHAYAH ( חיק ) ambalo maana yeke ni REPAIR
sawa na neno UKARABATI katika Kiswahili au kuhuhisha
-
Yesu anatumia neno kurejesha upendo wa kwanza,
hii maana yake ni nini hasa?
Wengi wetu tulipompokea Yesu kwa
mara ya kwanza, tulijawa na furaha kubwa sana, tulijisikia huru, tulijiona
wepesi ni kama Yesu ameondoa mizigo Fulani iliyokuwa inatuelemea, tulijawa na
upendo mkubwa sana kwa Mungu na tulihisi kuwa tuko karibu sana na Yesu! Mioyo
yetu ilijawa na kiu na hamu na shauku,
ya kutaka kumtumikia Mungu, tulisoma neno la Mungu kwa nguvu na mioyo yetu
yote, tulihudhuria ibada bila kukosa huku tukitoa kipaumbele kwa ibada kuliko
kitu kingine, tulikuwa waombaji, tulihudhuria mikesha, tulishuhudia habari
njema na kuwaleta wengi kwa Yesu, tulikuwa na mijadala ya kidini na ndugu na
jamaa zetu, hatukuweza kutulia, tulijawa
na wivu kwa ajili ya Mungu, tulifuatilia watoto wachanga kiroho, tulitembelea
magerezani, mahospitalini, wagonjwa, yatima na wajane, tulijali mambo ya Mungu,
tulitoa bila kusukumwa, hata ndoto na maono yetu yalikuwa ya kimbingu, maisha na mwenendo wetu haukuwa na mashaka
watu walikuwa na kiu na hamu na shauku ya kuwa kama Yesu Kristo!, Nyimbo zetu
zilikuwa nataka kuwa kama Yesu moyo wangu, nataka kuwa kama Yesu maisha
yangu! Hali hii ndio inaitwa upendo wa
Kwanza, ni kama Uchumba au ndoa inavyokuwa mwanzoni, kila mmoja anavyojitoa kwa
mpenzi wake hali hiyo ndiyo inaitwa upendo wa Kwanza! Kila mmoja wetu alikuwa
nayo, na makanisa yetu mengi yalikuwa hivyo, Pepo walikuwa wakiwatoka watu
wenyewe wakati wa kusifu, au hata kwa kuwepo tu kanisani, kabla hata ya kukemea
kwa nguvu udhihirisho wa Mungu ulikuwa ni kitu cha wazi wazi! huo ndio, watu
walikuwa na kiu ya kutenda haki, hakukuwa na majivuno, hakukuwa na kiburi,
hakukuwa na ukaidi, utii ulikuwa wa hali ya juu, hakukuwa na upendeleo
makanisani, hakukuwa na ukabila, hakukuwa na ugomvi wala mafarakano, hakukuwa
na kupindishwa kwa haki, wala dhuluma, wala wivu, wala kubaniana, wala hakukuwa
na urasimu, Mungu alikuwa akisema wazi wazi na watu wake hata kwa unabii,
karama za Roho Mtakatifu zilidhihirika!
Je mambo hayo yapo? Wakati huo hakukutumika sana mafuta wala visaidizi
vya kiroho, hatukujua chumvi, wala maji ya Baraka (sisemi kwamba kutumia vifaa vya kiroho ni vibaya) lakini visaidizi
vya kiroho hutumiwa na watu ambao Imani imeshuka sana yaani wenye Imani ya
kawaida kwaajili ya kuinua Imani zao, Wakati wa uamsho mkubwa sisi tulilijua
jina la Yesu tu! Huo ndio uamsho! Jina
la Yesu lilikuwa ni utoshelevu mkubwa kwa kutamka tu wakati wa uamsho watu walifanya maamuzi
magumu,Watu waliacha kazi Redioni, ili tu wasipige miziki isiyompendeza Mungu,
watu walifunga baa zao, watu waliacha kuuza sigara huo ndio ulikuwa uamsho! Watu waliuza nyumba zao na mali zao kwaajili
ya injili, Watu walikuwa wakiokolewa na wokovu ulikuwa una vita kali sana
katika ngazi za familia na jamii, watu walikuwa na msimamo mkali hiyo ndio
ilikuwa hali ya uamsho, watu walijitenga na dunia wala hawakufuatisha namna ya
dunia hii katika usemi, menendo Imani na ufasi, haki ilitendeka kila mahali
watumishi walizaa watumishi, watu walikuwa kiroho kwa haraka, kazi ya Mungu
ilisonga mbele na Mungu alidhihirika wazi wazi kati ya watu wake!
Ni Muhimu kufahamu kuwa Kanisa
linapokuwa na nguvu kubwa namna hii, maana yake ufalme wa Shetani unapata taabu
sana, na shetani hawezi kukubali kirahisi ashambuliwe na watu wake kuchukuliwa
mateka kwenda upande wa ufalme wa Mungu,
na ndio maana mara baada ya mtu kuokolewa yeye anaanza kuwa na mipango mikakati
ya kuhakikisha kuwa anawarejesha nyuma au katika ufalme wake wale wote ambao
wametekwa kwenda upande wa ufalme wa Mungu, shetani anajua wazi kuwa ni kazi
ngumu kuwarejesha mateka wake katika mikono ya Mungu
Yohana 10:27-29 “Kondoo wangu waisikia
sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala
hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba
yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya
katika mkono wa Baba yangu.”
Kwa hiyo mbinu kubwa anayoitumia
shetani ni kuhakikisha kuwa watu wa Mungu wanapoa, wanakinai, wanachoka,
wanapoteza tumaini, wanakosa upendo, shauku na hamu ya kumpenda Yesu, Shetani
hatakurudisha nyuma kwenye dini yako ya zamani, lakini anakufanya usiwe na
madhara katika ufalme wake huku ukiwa katika ufalme wa Mungu, atahakikisha kuwa unabaki kama Mtumishi au
Mkristo asiye tishio katika ufalme wa ibilisi, hutaomba tena, hutakuwa mshabiki
wa mikesha, huoni umuhimu wa kuhudhuria ibada husikilizi nyimbo za injili tena
na huna madhara kwa wasiookoka wala kwa shetani mwenyewe huko ndiko kuuacha
upendo wako wa kwanza ndio kupoa! Atakuacha shetani uwe vuguvugu, atakuacha
ufungiwe nira na wasiamini, atakuacha uwe na urafiki na giza, atakuacha uipende
dunia, haijalishi uko katika kanisa gani wala haijalishi kuwa uko na mtumishi
wa kiwango gani cha kiroho utapoa tu
2Timotheo 4: 9-10 “Jitahidi kuja kwangu
upesi. Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda
Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia.”
Kwa msingi huo ni muhimu kila mtu
na kila kanisa kujihoji na kujiuliza kama wako salama au la? Na ni vigumu sana
kwa kanisa au mkristo aliyepoa kukubali kuwa amepoa au amekufa kiroho, lakini
swala la msingi la kujiuliza ni je bado tunampenda Yesu kwa kiwango kile kile?,
je tunatafuta ufalme wa Mungu kwanza na haki yake? Je tuna upendo wa kweli na
ushirika wa kweli kwa na ndugu zetu katika Bwana? Je tunashuhudia matunda ya
Roho katika maisha ya wakristo na watumishi wa Mungu leo? je ziko nguvu za
Mungu katika maisha yetu na kanisa letu?, Leo hii imefikia hatua hata wachwi
wanaabudu katika makanisa ya kiroho, watu wa Mungu pia wanarogwa! Niliwahi
kumsikia Mchungaji mmoja akilalamika kuwa wachawi wanakopera sadaka katika Kanisa
Lake! Mpaka aliposimama na kukemea kwa midomo yake kuwa waache tabia hizo ndio
sadaka zikaongezeka! Sikumjibu lolote nilikuwa na mke wangu hakua aliyesema
kitu pale lakini tulipofika nyumbani tulianza kujiuliza, kama Askofu yule
angeliruambia sadaka zinaibiwa angalau akili yangu ingeweza kuwa na Amani,
kwamba wako wezi ambao hawana hofu ya Mungu wameingia makanisani, lakini hebu
fikiria wachawi wanakopera sadaka katika kanisa la kiroho? Ni jambo la
kusikitisha sana, ni lazima kanisa lirejee, lirudi mahali pake mahali ambapo
limejengwa na malango ya kuzimu hayataliweza! Na msingi huo ni Yesu Kristo
Mwana wa Mungu aliye hai!, Je hali ya kanisa lenu wewe na hali yakow ewe mwenyewe
na hali ya wenzako na zamani zile ikoje? Yako makanisa ukiokoka leo na ukawa wa
moto sana wenzako waliokutangulia utasikia kaka ana moto sana dada ana moto
sana aaa ni uchanga tu atapoa sasa hivi Je umewahi kusikia hali kama hiyo?
Marko 12:30 “nawe mpende Bwana Mungu wako
kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu
zako zote.”
Mathayo 6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme
wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”
1Yohana 1:7 “bali tukienenda nuruni, kama
yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana
wake, yatusafisha dhambi yote.”
1Yohana 4:20-21 “Mtu akisema, Nampenda
Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake
ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa
na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.”
Wagalatia 5:22-23 “Lakini tunda la Roho ni
upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi;
juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”
Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha
kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika
Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”
Kama maswali yote tuliyojiuliza
hapo juu yanatoa jibu hapana au kuna upungufu basi ukweli ni kuwa tunahitaji
uamsho! au kwa lugha nyingine ni kuwa tumepoa au kanisa lisilo na hayo au lenye
mapoungufu kuhusu hayo limepoa limekuwa la baridi na sio la moto tena moto
umezimika au moto umefifia kwa hiyo tunahitaji uamsho!
Namna ya kujua kama unahitaji uamsho;
Ni vigumu watu, mtu au kanisa
lolote lile kukubali kuwa limelala, au limepoa na linahitaji uamsho lakini ni
rahisi kujijua kama tuna uamsho au la kwa kujiuliza maswali kadhaa Muhimu, maandiko
hayakatazi kujitathimini, na kujijaribu wenyewe ili kujua kama tumekuwa katika
Imani au lahasha
2Wakorintho 13:5 “Jijaribuni wenyewe kwamba
mmekuwa katika imani; jithibitisheni wenyewe. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu
Kristo yu ndani yenu? Isipokuwa mmekataliwa.”
Tunawezaje kujua kama tuko vema
au la Maswali kadhaa yajayo yatasaidia kujitambua tuko hai kiasi gani au tuko
hoi kiasi gani
1. Je
tunampenda Mungu kuliko Kazi zetu, familia zetu, biashara zetu, anasa zetu na
mambo yetu? Mathayo 6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme
wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. ”
2. Kumnung’unikia
Mungu na watumishi wake katika kila hali unayokutana nayo katika maisha 1Wakorintho 10:10 “Wala
msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu.”
3. Tunapenda
sifa za wanadamu? Tunapenda kusifiwa kwa kila tendo jema?, tunapenda kutukuzwa
sisi kuliko Kristo? Yohana 12:42-43 “Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini;
lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi. Kwa
maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.”
4. Kuwa
na uchungu, kukosa uvumilivu kwa wengine, kukosoa wengine, kuwa mkali sana
ukikosolewa, wivu kwa wengine na kutokutaka mafanikio ya wengine, kukomoa
wengine na kufurahia tunapoona wanaharibikiwa? Waebrania
12:14-15 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu
wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;
mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije
likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”
5.
Kukwaza wengine, kupenda mabishano, kujiona
uko sawa wakati wote, mkali sana kwa wengine, kujisikia vibaya wengine
wakifanikiwa, kuogopa watu watasemaje, kufurahia watu wengine wanapokwama, au
kuanguka, kukosa kabisa matunda ya roho na kujaa matunda ya mwili,
kutokusemeshana, dhuluma, majungu, hila, fitina, uzushi, husuda yaani ni
matunda ya mwili tupu, Wagalatia 5:19-21
“Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya,
uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira,
fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo,
katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu
watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.”
6.
Kukosa uaminifu, kutokuwa mkweli, kusema
uongo, kuficha maovu, kujitahidi kujipa raha ili hali huna raha, wala Amani,
kuishi maisha ya kinafiki, kuwa na sura mbilimbili, Mathayo 23:27-28 “Ole wenu, waandishi na
Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo
kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu
wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali
ndani mmejaa unafiki na maasi.”
7.
Kusumbuliwa na mawazo, mgandamizo wa mawazo,
kukata tamaa na kuacha kumtumaini Mungu
Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani
kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na
kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”
8.
Kuwa wakavu kiroho, kuwa wa kawaida sana, kutokushuhudia,
kutokufanya uinjilisti, kuwa dhaifu kiroho, kuwa vugu vugu, kurudi nyuma Ufunuo 2:4-5 “Lakini
nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni
wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya
hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”
Ufunuo 3:15-16“Nayajua
matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa
baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto,
nitakutapika utoke katika kinywa changu.”
9.
Kuanza kuifuatisha namna ya dunia hii,
kuupenda ulimwengu, kuanza kufikiri, kusema na kutenda kama watu wa ulimwengu
huu tu Warumi 12:1-2 “Basi, ndugu
zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo
hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala
msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate
kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”
10.
Kuacha kuomba, kuacha kushuhuhudia, kuacha
kuhubiri injili, kuacha kuhudhuria ibada, kuacha kujali waliorudi nyuma, kuacha
kusoma neno, kupuuzia karama za roho, kutweza unabii, kuwasumbua wenye vipawa
badala ya kuwalea, kuacha kufundisha neno la Mungu, kuhubiri mafanikio ya
mwilini zaidi kuliko maswala ya rohoni, na mkazo wa matumizi ya vifaa vya
kiroho zaidi kuliko jina la Yesu, kukatisha tamaa watu wenye bidi katika bwana,
kuwabania watumishi wa Mungu wenye vipawa, kumzimisha Roho Mtakatifu 1Wathesalonike 5:19 “Msimzimishe Roho”
11.
Kurudi kwa magonjwa mbalimbali makubwa
ambayo zamani yalikuwa yakiwasumbua watu wa dunia hii Kutoka 23:25-27 “Nanyi mtamtumikia BWANA,
Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea
ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika
nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza. Nitatuma utisho wangu utangulie
mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya
hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao.”
12.
Endapo utaanza kuona uovu na uharibifu Habakuki 1:2-4 “Ee
Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu,
ila hutaki kuokoa. Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana
uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea. Kwa
sababu hiyo sheria imelegea, wala hukumu haipatikani; kwa maana watu wabaya
huwazunguka wenye haki; kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka.”
Endapo kila
mmoja na kila kanisa litajifanyia tathimini na kujichunguza kuona mapungufu
yetu ukilinganisha na jinsi tulivyoanza wakati tunakutana na Yesu na tukibaini
kuwa kuna mapungufu, basi mara moja tunaweza kufahamu kuwa tunahitaji uamsho
bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa na ufahamu na kuanza kuutafuta uamsho
katika maisha yetu katika jina la Yesu Kristo.
Jinsi ya kurejesha uamsho
Uamsho ni kurejesha upendo, ule
upendo wetu wa kwanza tuliokuwa nao kwa Yesu Kristo, ni kurejea katika kila jambo ambalo
tuliliacha na ambalo limeagizwa katika neno la Mungu, ni kurejesha afya ya
kiroho ambayo imepungua katika maisha yetu na katika kanisa, na jambo la kwanza
ambalo tunaweza kuanza nalo ni toba, na kuomba rehema za Mungu, ujumbe wa toba hauna uhusiano na watu walioko
nje, watu ambao hawajaokolewa ujumbe wao ni habari njema ya kuwa Yesu Kristo
anaokoa, na hivyo wanapaswa kumuamini na kukubali kazi yake aliyoifanya
msalabani kwaajili ya ulimwengu mzima, ujumbe wa toba ni ujumbe kwa kanisa ni ujumbe kwa watu wa Mungu, wanaoambiwa
watubu ni makanisa ni watu ambao walimjua Mungu na kisha wakaingia kwenye njia
mbaya kwa hiyo unatolewa wito kwao kumrudia Bwana na Mungu takapoona mioyo yetu iko tayari yeye
ndiye anayeleta uamsho, bidi na jitihada za kibinadamu kamwe haziwezi kuleta
uamsho!
Mathayo 26:40-43 “Akawajia wale wanafunzi,
akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata
saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini
mwili ni dhaifu.Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa
haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. Akaja
tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito.”
Wakati wote wanafunzi walipokuwa
wamelala ni Yesu ndiye aliyewaamsha, umasho hauwezi kuletwa na mwanadamu
mwenyewe, yako maandalizi ya kawaida ya kufanya lakini mwenye kuamsha hiyo nia
na hiyo hari ni Mungu mwenyewe kumbuka yale maombi ya nabii Habakuki. Habakuki 3:2 “Ee
Bwana, nimesikia habari zako, nami naogopa; Ee Bwana, fufua kazi yako katikati
ya miaka; Katikati ya miaka tangaza habari yake; Katika ghadhabu kumbuka rehema.”
Hata hivyo kama wanadamu tuna wajibu wa kufanya sehemu yetu na haya ndio
tunayoweza kuyafanya!
Toba:
Ufunuo 2: 4-6 “Lakini nina neno juu yako,
ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka;
ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako,
nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu. Lakini unalo neno
hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia”
Ufunuo 2:14-16 “Lakini ninayo maneno
machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye
aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu
vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini. Vivyo hivyo wewe nawe unao watu
wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile. Basi tubu; na usipotubu, naja
kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.”
2Nyakati 7:14 “ikiwa watu wangu, walioitwa
kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha
njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na
kuiponya nchi yao.”
Marekebisho:
Toba haiwezi kuwa kamili bila
kufanya marekebisho, au matengenezo, hatuna budi kuhakikisha kuwa tunaweka sawa
pale ambapo tuliharibu, mfano kama ulidhulumu watu umetubu na watu hao wapo
uerejeshe kile ulichodhulumu, uliazima vitabu Library (maktaba ya shule) na
hujavirudisha rejesha, una mume ambaye si wako, au mke ambaye si wako mwachie
aende kwa mmewe au mkewe, swala la toba
na malipizo katika makanisa mengi linachukuliwa poa, lakini ni fundisho halali
na liko, umemkosea mtu usijikaushe tu nenda kaombe msamaha, Kumbuka jinsi Yakobo alivyotafuta Amani kwa bidi
kwa kaka yake Esau!, hakikisha hauna mtu moyoni mwako samehe, sahau achilia.
Mathayo 5:23-24 “Basi ukileta sadaka yako
madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache
sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha
urudi uitoe sadaka yako.”
Luka 19:8-9 “Zakayo akasimama, akamwambia
Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa
nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.Yesu akamwambia, Leo
wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.”
Ezra 10:1-3 “Basi hapo Ezra alipokuwa
akiomba na kuungama, akilia, na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya
Mungu, wakamkusanyikia katika Israeli wote kusanyiko kubwa sana la wanaume, na
wanawake, na watoto; maana watu hao walikuwa wakilia sana. Hata Shekania, mwana
wa Yehieli, mmoja wa wana wa Elamu, akajibu, akamwambia Ezra, Sisi tumemkosa
Mungu wetu, nasi tumeoa wanawake wageni wa watu wa nchi hizi; lakini kungaliko
tumaini kwa Israeli katika jambo hili. Haya basi! Na tufanye agano na Mungu
wetu, kuachana na wake zetu, na wale waliozaliwa nao, tukilifuata shauri la
bwana wangu, na shauri la hao wanaoitetemekea amri ya Mungu wetu; mambo haya na
yatendeke kwa kuifuata torati.”
Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na
amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana
asipokuwa nao;”
Maombi:
Maombi ni funguo muhimu sana
katika kutafuta uamsho wa katika kanisa, unaposoma vitabu vingi sana
vuinavyozungumzia uamsho huwezi kuona kuna mwandishi amewahi kuacha kuzungumzia
maombi kuwa ni moja wapo ya nyenzo muhimu sana katika kuleta uamsho, ndio njia
ya Imani, unyenyekevu, na yenye kuchochea mabadiliko, Mungu anatutegemea
tumuombe ili aweze kuleta Baraka zake kwetu kwa mtu mmoja mmoja na kanisa zima
kwa ujumla, maombi hayo ndiyo yanayohusisha toba, na kutafuta rehema, na kutimiza kiu yetu ya
kukleta uamsho, tunaweza kumuomba Mungu aokoe wengine, kuombea umisheni na
uinjilisti, kuhitaji uwepo wa Mungu, karama na vipawa, nguvu za Roho Mtakatifu
na mpenyo wa kiroho maombi maombi maombi
Matendo 1:12-14 “Kisha wakarudi kwenda
Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu,
wapata mwendo wa sabato. Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa
wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo
na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo.Hawa wote
walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu
mama yake Yesu, na ndugu zake.”
Kufunga:
Kufunga ni njia ya kujitia
nidhamu ya kiroho kwa kusudi la kujiungamanisha na Mungu, kumlingana Mungu,
kuutafuta uso wake kwa bidii ili kwamba Mungu aweze kuingilia kati na kuleta
badiliko tunalolikusudia, Kufunga kunaongezea nia yetu ya kuonyesha kuwa
tunamtafuta Mungu kwa bidi hii ni kwa sababu kufunga huambatana na kuomba,
kuomba kunajumuisha unyenyekevu, tafakari, na kutafuta mpenyo wa kirohoni
nyenzo muhimu, yasiyowezekana katika hali ya kawaida yanaweza kusawazishwa kwa
maombi ya kufunga, kufunga kufunga. Kufunga kulitumika kama njia ya kuonyesha
kujidhabihu kama ibada ya kuutafuta uso wa Mungu lakini pia kwaajili au ikama
njia ya kumrudia Bwana
Yoeli 2:12-14 “Lakini hata sasa, asema
Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa
kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu
wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira,
ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. N'nani ajuaye kwamba hatarudi na
kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya
kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu? ”
Matendo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika
kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni
aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa
mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na
kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile
niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao,
wakawaacha waende zao.”
Unyenyekevu: watu wengi sana
hawafahamu siri ya kuinuliwa na Mungu, Mungu anapendezwa sana na watu
wanyenyekevu, anakaa yeye na watu wanyenyekevu na waliotubu, moja ya sababu ya
watu wengi kuachwa na Mungu ni kwa sababu ya kiburi na majivuno, siku hizi hata
makanisa ya kipentekoste wachungaji wanaitwa Baba! Na watu wanaona ni jambo la
kawaida tu wala hawalikemei, Mungu hakai na watu wenye kiburi, watu
wanaojifikiri kuwa bora zaidi kuliko wengine, na hata kujikinai wakiwadharau
wengine kama tunataka uwepo wa Mungu na kukubaliwa na Mungu hatuna budi kuweka
mbali kiburi na majivuno, na wakati wote tukiri ya kuwa tunahitaji neema ya
Mungu
Isaya 66:2 “Maana mkono wangu ndio
uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu
huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka,
atetemekaye asikiapo neno langu.”
1Petro 5:5-6 “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini
wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu
Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi
nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake”
Yakobo 4:5-6 “Lakini hutujalia sisi neema
iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema
wanyenyekevu.”
Luka 18:10-14 “Watu wawili walipanda kwenda
hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama
akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu
wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi
nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule
mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni,
bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia,
huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana
kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”
2Nyakati 7:14 “ikiwa watu wangu, walioitwa
kwa jina langu, WATAJINYENYEKESHA, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha
njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na
kuiponya nchi yao.”
Neno la Mungu:
Neno la Mungu ndio kiini kikuu
cha uamsho, lenyewe ndilo ambalo hutumika kama nyenzo ya uamsho na mabadiliko,
linakazia ukweli na kutuelezea kile kilichopungua kwetu na njia ya kufanya,
wakati wa uamsho Kuhubiri na kufundisha huwa ni nyenzo muhimu ya wakati wote
inayotumika kusema na mioyo yetu, lenyewe linafunua dhambi zetu, linatuonyesha
njia na kutupa tumaini na namna ya kumtafuta Mungu na kudumisha uhusiano na yeye,
Ezra alipata uamsho, kwa sababu alirudisha moyo wake kwenye mkazo au msingi wa
uamsho huo ambao ndio neno la Mungu. Mitume nyakati za kanisa la kwanza
walihakikisha kuwa wanabaki katika kulihudumia neno, hii ni kwa sababu walikuwa
na ufahamu wa umuhimu wa kutunza uamsho na uwepo wa Mungu kwa kudumu katika
neno
Ezra 7: 10 “Kwa maana huyo Ezra alikuwa
ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Bwana, na kuitenda, na kufundisha
maagizo na hukumu katika Israeli.”
Matendo 6:3-4 “Basi ndugu, chagueni watu
saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima,
ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia
lile Neno.”
Utii kwa Roho Mtakatifu:
Roho Mtakatifu pekee ni Bwana wa
uamsho, yeye nndiye anayeweza kuichochea mioyo yetu, na kutupa nguvu za kuwa
mashahidi wa Mungu, kwa ujumla tunaweza kusema ya kuwa Uamshio ni kazi ya Roho
Mtakatifu, kwa hiyo hata kama wanadamu watautaka uamsho na kuvaa majoho ya
kutaka kuuuketa kamwe bila Roho Mtakatifu kuhusika hakuwezi kuweko kwa uamsho,
Uamsho wa kweli unakuja tu mara anaposhuka Roho Mtakatifu, bila Roho wa Mungu
kutenda kazi ya kuvumisha upepo mifupa mikavu isingeliweza kuwa hai
Ezekiel 37:1-14 “Mkono wa Bwana ulikuwa juu
yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya
bonde; nalo limejaa mifupa; akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama,
palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana. Akaniambia,
Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua
wewe. Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa
mikavu, lisikieni neno la Bwana. Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya;
Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi. Nami nitatia mishipa juu yenu,
nami nitaleta nyama iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani
yenu, nanyi mtaishi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. Basi nikatoa unabii
kama nilivyoamriwa; hata nilipokuwa nikitoa unabii, palikuwa na mshindo mkuu;
na tazama, tetemeko la nchi, na ile mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa
mwenziwe. Nikatazama, kumbe! Kulikuwa na mishipa juu yake, nyama ikatokea juu
yake, ngozi ikaifunika juu yake; lakini haikuwamo pumzi ndani yake. Ndipo akaniambia, Tabiri, utabirie upepo,
mwanadamu, ukauambie upepo, Bwana MUNGU asema hivi; Njoo, kutoka pande za pepo
nne, Ee pumzi, ukawapuzie hawa waliouawa, wapate kuishi. Basi nikatabiri kama
alivyoniamuru; pumzi ikawaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi
kubwa mno. Kisha akaniambia, Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli;
tazama, wao husema, Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea;
tumekatiliwa mbali kabisa.Basi tabiri, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi;
Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu,
enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli.Nanyi mtajua ya
kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika
makaburi yenu, enyi watu wangu. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi
mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana,
nimesema hayo, na kuyatimiza, asema Bwana.”
Luka 24:49 “Na tazama, nawaletea juu yenu
ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”
Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha
kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika
Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”
Zekaria 12:10 “Nami nitawamwagia watu wa
nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao
watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu
amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile
mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.”
Roho Mtakatifu anaweza kuanza na
mtu mmoja au wawili tu na akaweka mzigo wa maombi ndani yao na kupitia wao
wengine wakaambukizwa, kumbuka kuwa hatuwezi hata kuomba au kufunga bila msaada
wa Mungu, ni kazi ya Mungu Roho Mtakatifu, kuamsha roho zetu, kwa hiyo unaweza
kuanza peke yako, usitegemee kuwepo kwa uamsho wa ujumla, tegemea kuanza wewe,
Roho Mtakatifu hutoa nguvu ya kuomba, huleta mvuto wa toba, nguvu ya kuhubiri
na kuokolewa kwa wengi na Mungu kuwatumia wengi, kwa ujumla tunaweza kusema
Roho Mtakatifu ndiye wa Muhimu zaidi kwa kazi ya uamsho: Na bado uamsho ni
neema ya Mungu mwenyewe kwa kanisa lake na watu wake,sisi tuna sehemu ndogo
sana ya kufanya lakini yeye ndiye mshika dau, na ndiye mwenye kuamsha nia na
neema ndani yetu, aamshe nia ndani yetu kuombea viongozi wa kanisa wasichoke,
kuombea mikutani ya injili, kuamsha nia ya kusifu na kuabudu, kuamsha ibada
zenye nguvu, kuamsha karama na vipawa
vya Roho Mtakatifu, kuamsha nia ya vikundi vya maombi, kuamsha nia ya kusoma
neno, kuamsha Imani, kuamsha kiu na hamu na shauku ya kutafuta na kudumisha
uhusiano na Mungu, na kuhakikisha kuwa upendo unatawala katika kanisa la Mungu.
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
0718990796.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni