Zaburi 35:9-10 “Na nafsi yangu itamfurahia
Bwana, Na kuushangilia wokovu wake.Mifupa yangu yote itasema, Bwana, ni nani
aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam,
maskini na mhitaji na mtu amtekaye.”
Utangulizi:
Kwa kawaida katika ulimwengu huu
limekuwa ni jambo la kawaida katika mazingira Fulani, wenye nguvu kuwaonea wale
wasio na nguvu, au Matajiri, kuwaonea masikini, au mtu aliye hodari kumuonea
aliye mnyonge, Hali hii inaweza kuwa imekutokea wewe au familia yako katika
mazingira Fulani. Familia nyingi za kiafrika bado ziko katika kipindi cha
mpito, kutoka katika hali duni kuelekea katika hali njema kwa hiyo watu wengi
sana wamewahi kukutana na uonevu wa namna nyingi, kutoka kwa wenye nguvu, wenye
mamlaka, au watu Fulani kulingana na nyadhifa zao, wanaweza kwa namna mmoja ama
nyingine kuwa wamekutana na aina Fulani ya uonevu Daudi alikuwa mmoja ya watu
waliokutana na hali kama hiyo na kupata maumivu nafsini mwake, Hali hii inamkuta
mtu anapokuwa Katika namna au nafasi ambayo hakuna wa kuingilia kati isipokuwa
Mungu mwenyewe.
Katika Zaburi ya 35 Daudi
anajaribu kumuomba Mungu sasa ili Mungu aweze kuinglia kati kwa haraka na
kumtoa katika mazingira magumu aliyokuwa anakabiliana nayo ambayo yalikuwa
hayana mtetezi. Na anamuahidi Mungu kuwa endapo atamletea msaada basi yeye ata
mfurahia Bwana na kuushangilia wokovu wake!
Zaburi 35:9 “Na nafsi yangu itamfurahia
Bwana, Na kuushangilia wokovu wake.” Kwa sababu hii sisi nasi leo
tutachukua muda mfupi kujifunza na kutafakari kifungu hiki muhimu kwa
kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
·
Bwana ni
nani aliye kama wewe
·
Umponyaye
masikini na mtu aliye hodari!
Bwana ni nani aliye kama wewe!
Zaburi 35:10b “Mifupa yangu yote itasema,
Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda
yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.”
Daudi akitumia lugha ya
kimashairi hapa anaanza kwa kuahidi kuwa atamtukuza Mungu, endapo BWANA
ataingilia kati mahitaji yake na maombi yake na kwa kweli yalikuwa ni maombi ya
mtu mwenye uchungu mwingi yanayodhihirisha kuwa alikuwa amechoshwa na hali
inayomkabili, Mifupa yangu yote itasema
Bwana ni nani aliye kama wewe, Ni Muhimu kufahamu kuwa Waebrania walitumia neno
Mifupa kumaanisha nafsi au mtu wa ndani, wao walikuwa wakifikiri kuwa mtu wa
ndani kabisa anawakilishwa na mifupa, kwa hiyo hata mtu alipokuwa akimaanisha
mtu wake wa karibu au wa ndani sana au
ndugu alitumia neno Mifupa
Mwanzo 2:23 “Adamu akasema, Sasa huyu ni
mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke,
kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.”
Zaburi 6:2-4 “Bwana, unifadhili, maana
ninanyauka; Bwana, uniponye, mifupa yangu imefadhaika. Na nafsi yangu
imefadhaika sana; Na Wewe, Bwana, hata lini? Bwana urudi, uniopoe nafsi yangu,
Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.”
Kwa hiyo Daudi alikuwa
akimaanisha nafsi yake imeumizwa na kama Bwana ataingilia kati dhidi ya adui
zake ambao kimsingi walikuwa na nguvu au mamlaka au wenye kutisha kuliko yeye
au wenye uwezo kuliko yeye au wenye uchumi mzuri kuliko yeye, au wenye nguvu,
au uwezo wa kumchukua mateka, na kumuokoa Basi nafsi yake yaani kwa kibrania
mifupa yake ingempa Mungu utukufu na kumshukuru sana na atasema Bwana ni nani
aliye kama wewe! Mifupa katika lugha ya kiibrania wanatumia neno ETSEM ambalo linazungumzia mtu wa ndani
Selfsame yaani nafsi neno hili limejitiokeza katika maandiko mara 126 katika
mistari karibu 108.
Usemi huu Bwana ni nani aliye kama wewe ulikuwa ukionekana mara kwa mara
katika mashairi ya kiibrania likitumika kama swali la kimashairi kuhoji kuwa
ni nani mwenye nguvu au anayeweza kuwa na kiburi na jeuri kiasi cha
kujilinganisha au kusimama kinyume na Mungu aliye hai anapoamua kuingilia kati
mambo yake, wakati Farao alipokuwa na nguvu za kijeshi kuliko taifa lolote
duniani na kuamua kusimama kwa ujeuri kinyume na wana wa Israel na hata
walipookolewa aliamua kuwafuata ili awarejeshi utumwani, Israel baada ya udhihirisho
mkubwa wa Mungu na ukombozi ulio hodari wa Bwana wa majeshi waliimba na kusema
Bwana ni nani aliye kama wewe!
Kutoka 15:10-12 “Ulivuma kwa upepo wako,
bahari ikawafunikiza; Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu. Ee BWANA,
katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika
utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu? Ulinyosha mkono
wako wa kuume, Nchi ikawameza”
Israel Walimshangilia Bwana na
kumuimbia kwa furaha huku wakihoji ee Bwana katika miungu Ni nani aliye kama
wewe huu ulikuwa ni usemi wa kawaida katika Israel wenye kuonyesha ya kuwa
Hakuna wa kulinganishwa na Mungu mwenye nguvu wa Israel
Zaburi 89:7-9 “Mungu huogopwa sana barazani
pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka. Bwana, Mungu wa
majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako
unakuzunguka. Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari. Mawimbi yake yainukapo
wayatuliza Wewe.”
Zaburi 71:17-19 “Ee Mungu, umenifundisha
tokea ujana wangu; Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo. Na hata nikiwa
ni mzee mwenye mvi, Ee Mungu, usiniache. Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki
nguvu zako, Na kila atakayekuja uweza wako. Na haki yako, Ee Mungu, Imefika juu
sana. Wewe uliyefanya mambo makuu; Ee Mungu, ni nani aliye kama Wewe? ”
Zaburi 113: 4-5. “Bwana ni mkuu juu ya
mataifa yote, Na utukufu wake ni juu ya mbingu. Ni nani aliye mfano wa Bwana,
Mungu wetu aketiye juu;”
Bwana ni nani aliye kama wewe ni
usemi unaoonyesha Mungu ni mwenye nguvu na hakuna mfano wake,ana uwezo kuliko
kitu chochote, ana nguvu kuliko nguvu za wachawi na waganga na washirikina, ana
nguvu kuliko jeshi lolote duniani, ana mamlaka kuliko mtu yeyote duniani, ana
uweza, ulio juu kuliko mungu yeyote duniani, ana utajiri kuliko yeyote duniani
na ndiye mkombozi na mtetezi wa wanadamu hasa kwa sababu yeye hapendi uonevu,
kwa hiyo wakati tunajiona duni na tumeachwa tukiwa hatuna mtetezi, tumeachwa
tupate kudhalilika, tuko katika hali ya unyonge hatuna budi kujiandaa kwa
shuhuda, Daudi alikuwa anajiandaa kwa shuhuda alipokuwa anaomba kwamba Mungu
akingilia kati na kumsaidia alisema nafsi yangu itakushukuru, atashuhudia jinsi
Mungu alivyo mtenda miujiza mikubwa na mwokozi na mtetezi na kimbilio la
wanyonge, na hivyo fadhili za Bwana zina
nguvu kuliko majeshi yoyote, mamlaka yoyote na wapanda farasi wake!
Zaburi 33:16-18. “Hapana mfalme aokokaye
kwa wingi wa uwezo, Wala shujaa haokoki kwa wingi wa nguvu. Farasi hafai kitu
kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake. Tazama, jicho la Bwana
li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake.”
Kwa hiyo haijalishi ukubwa wa
changamoto zinazokukabili, haijalishi nguvu ya yule unayepambana nawe kama
ilivyokuwa kwa Daudi liitie jina la Bwana na Mungu atajifunua kwako kutoka
katika pembe ya kile unachokabiliana nacho ukijua wazi ya kuwa hakuna aliye
kama yeye naye atatenda mambo makuu,
Nani aliye kama Bwana?
Umponyaye masikini na mtu aliye hodari!
Zaburi 35:10b “Mifupa yangu yote itasema,
Bwana, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda
yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.”
Neno Umponyaye hapa linaweza pia kutumika sambamba ba
Uokoaye, Kwamba mtu wa Mungu anaweza kupitia katika hali ngumu na mateso na
usumbufu wa mwili, nasfi na roho lakini hatimaye Bwana anaweza kukuokoa nayo
yote, na anaweza kukuponya nayo
yote, Maandiko yanaonyesha wakati wote
tunapokabilia na mambo magumu ya kuumiza nafsi zetu, iwe ni magonjwa, iwe ni
migogoro ya ndoa, migogoro ya malezi, migogoro ya kazini, migogoro ya maisha,
kesi mahakamani, kukosa ada za shule, umasikini, mateso magonjwa ya aina
mbalimbali, njaa, madeni, uonevu wa mirathi, uonevu wa mipaka ya shamba,
kusalitiwa, kuogombana, vita baridi na kurushiana maneno huku na kule nataka nikuhakikishie ya kuwa tukimlilia
Bwana kwa mapenzi yake akaamua kutujibu atatutoa katika hali zote
zinazotukabili.
Zaburi 34: “Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na
waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana
humponya nayo yote.”
Hakuna changamoto ambayo Bwana
hawezi kuitatua yeye anayaweza yote yeye ni mponyaji wa nafsi zetu na ni
mwokozi wa kila janga linalotukabili
hata kama tunaweza kupita katika hali ngumu kwa sababu ya kuweko Duniani
na kuweko kwa shetani, ni Muhimu kufahamu kuwa tutaokolewa katika hayo yote
yanayotukabili labda kama Mungu sio Muaminifu kwa neno lake! Jambo ambalo
haliwezekani kwa sababu uaminifu wake unadumu kizazi hata kizazi
2Timotheo 3:10-11 “Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu,
na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu, na upendo, na saburi; tena na adha
zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika
Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo
yote.”
Jambo kubwa la msingi ni
kumtumainia Bwana na kumuweka yeye mbele naye atafanya kitu, yeye ni mwenye
nguvu, na uwezo wa kutukinga na kila
kilicho hodari duniani anao kwa msingi huo wakati wote tunapopita katika wakati
mgumu tukimtumainia yeye tutasimama tena, “Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye,
Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye.” Masikini katika luga ya
kiebrania hapo linatumika neno ANIY ambalo
maana yake ni mtu awaye yote ambaye yuko katika hali ya kudhikika, kuanzia
kwenye akili mpaka katika mazingira ya kawaida, mtu mnyonge, mwenye uhitaji,
masikini, aliyeonelewa, mtumwa, aliyechukuliwa mateka, mtu wa hadhi ya chini,
mgonjwa anayeonewa na kitu chenye nguvu kiasi cha kumuumiza Hali zote hizo
bwana hawezi kukubali hata kidogo, yeye huingilia kati na kuokoa na kuponya.
Jambo kubwa la ziada ni kumtumaini yeye kama
asemavyo;
Mithali 3:5-6. “Mtumaini Bwana kwa moyo
wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri
yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni