Yohana 15:18-21 “Iwapo ulimwengu
ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama
mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi
si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo
ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa
kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika
neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina
langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka.”
Utangulizi:
Iwapo ulimwengu ukiwachukia,
mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Yesu alikuwa
akimaanisha ulimwengu utatuchukia kabisa, kwa sababu kwanza ulimwengu
ulimchukia Kristo, Kwa hiyo kila mwanafunzi wa Yesu Kristo hapaswi kuona jambo
hilo kuwa ni jambo geni, Kama ulimwengu ulimchukia Kristo kwa vyovyote vile
hauwezi kuwakubali wafuasi wake.
Mathayo 10:22-25 “Nanyi mtakuwa mkichukiwa
na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho,
ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni
mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata
ajapo Mwana wa Adamu. Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti
bwana wake.Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama
bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si zaidi wale walio
wa nyumbani mwake? ”
Ulimwengu unachukizwa sana na
watu waliomwamini Yesu na kumfuata, kwa sababu sio wa ulimwengu huu, wakati
wanafunzi wa Yesu watatambulikwa kwa upendo wao kwa watu, watu wa ulimwengu huu
watajulikana kwa chuki na wivu dhidi ya watu wa Mungu, wanafunzi wa Yesu sio wa
ulimwengu huu kwa sababu wameitwa kutoka ulimwenguni kuingia katika ufalme wa
mwana wa pendo lake, na kuuacha ufalme wa giza, kwa hiyo tuwapo katika maisha
haya sisi wenyeji wetu uko mbinguni, na kwa sababu hiyo mkuu wa ulimwengu huu
hawezi kuwa na furaha na watu waliookolewa, kwa sababu wao wameuacha ufalme
wake, na hivyo anachukizwa nao, wale walio wa ulimwengu huu wao ndio wenyeji wa
ufalme wa shetani au ufalme wa giza na hivyo hauwezi kuweko urafiki kati ya
nuru na giza, kweli na uongo, na hivyo hakuwezi kuweko kwa Amani na upendo wa
kweli kutoka katika dunia hii inayoongozwa na mfumo wa yule muovu, wala watu wa
Mungu wasitarajie ya kuwa dunia itawatendea haki, kwa sababu mfumo wa ulimwengu
huu unawatema!, Mfumo wa ulimwengu huu uko chini ya Shetani ambaye kimsingi
hana nguvu kama za Bwana wetu Yesu, lakini hata hivyo anatawala mfumo wa uasi
wa dunia na kunyunyizia ushawishi wake duniani.
Yohana 14:30-31 “Mimi sitasema nanyi maneno
mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.
Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru;
ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.”
Tutajifunza somo hili ninyi si wa
ulimwengu huu kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Ufahamu
kuhusu mkuu wa ulimwengu huu.
·
Kuchukiwa
kwa watu wasio wa ulimwengu huu.
·
Jinsi
watu wasio wa ulimwengu huu wanavyopaswa kuishi.
Ufahamu kuhusu mkuu wa ulimwengu huu.
Ni muhimu kufahamu kuwa Shetani
ana majina mengi yanayomtambulisha kama mwenye mamlaka na ulimwengu huu, Katika
maandiko Yesu anamtaja kama mkuu wa ulimwengu huu Katika
Yohana 14:30 “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja
mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.”
Katika biblia ya kiingereza
maneno hayo yanasomeka “I will not speak
with you much longer, for the PRINCE OF THIS WORLD is coming. He has no hold on
me” kwa hiyo shetani anaitwa mkuu wa ulimwengu huu, au kwa jina lingine, mungu
wa dunia hii angalia au mfalme wa
dunia hii, Kwa hiyo kimsingi Shetani ni mtawala wa dunia hii.
2Wakorintho 4:3-4 “Lakini ikiwa injili yetu
imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii
amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake
Kristo aliye sura yake Mungu.”
Unaona katika andiko hili Shetani
anaitwa MUNGU WA DUNIA HII. Aidha katika maandiko mengine Shetani
anaitwa MFALME WA UWEZO WA ANGA “The
Prince of the air” hili unaweza kuliona katika kitabu cha Waefeso
Waefeso 2:1-3 “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;
ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata
mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;
ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu,
tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa
hasira kama na hao wengine.”
Hii ina maana gani? Ni muhimu
kufahamu kuwa katika lugha ya Kiyunani neno Prince of this world, mkuu wa ulimwengu huu, god of this age, mungu wa dunia hii, ruler of the kingdom of air, mkuu wa uweza wa anga huyu kwa kwa
kiyunani anaitwa KOSMOKRATOR kwa kiingereza COSMOCRATOR maana yake RULER OF THE WORLD neno hilo Kosmokrator limetokana na lugha ya asili ya dini za kipagani
hususani Wanostiki na Wamarcion wakimaanisha ni lugha ya kiufundi ya
kumtambulisha Shetani kutokana na kazi zake za uendeshaji wa ulimwenguni kwa hivyo
utaweza kuona jina hilo Kosmokrator
ni mkuu wa anga, au mtawala wa dunia hii au mwenye ushawishi wa akili na tabia
na mwenendo, malengo, matumaini, falsafa, elimu, biashara, mawazo, fikra,
ujasusi, udhibiti, na utaratibu wa kila kitu hapa duniani. Katika ulimwengu wa
watu wasiookolewa ni muhimu ikafahamika wazi kuwa ulimwengu uko chini ya huyu Kosmokrator yaani Shetani. Kwa hiyo
mifumo yote ya uendeshaji wa dunia hii na ushawishi wake uko chini ya mkuu wa
anga anayetenda kazi sasa kwa wana wa kuasi.
Yohana 12:31 “Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu
huu atatupwa nje”. Kwa hiyo Mkuu wa anga anaitwa Kosmokrator wakati ulimwengu na mfumo wake wote unaitwa Kosmos,
Mapambo na vipodozi vyote vinaitwa Kosmetikos, yaani art of beautification kwa hiyo neno Kosmos lilitumika pia kuelezea mfumo wa ulimwengu na ndio maana
nyakati za kanisa la Kwanza mtu aliyeonyesha kuupenda sana ulimwengu
alifikiriwa pia amekuwa adui wa Mungu.
Yakobo 4:4 . “Enyi wazinzi, hamjui ya
kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa
rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.”
Kwa hiyo Maandiko yanapomtaja
shetani kama mkuu wa ulimwengu huu, yanafunua ule ukweli ya kuwa katika
ulimwengu huu wako watu wanaoongozwa na mfumo wake na wanaofuata mfumo wake na
wako chini ya mfumo huo na pia wale waliomwamini Yesu wako katika mfumo
mwingine wanaishi duniani lakini wakiwa wamehamishwa katika ufalme huo wa giza
na kuingizwa katika mfumo wa ufalme wa mwana wa pendo lake yaani Pendo la
Mungu. Hii ina maana gani ina maana ya kuwa watu waliookoka hawako chini ya
utawala wa shetani, kwa hiyo wao sio wa ulimwengu huu
Wakolosai 1:13-14 “Naye alituokoa katika
nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;
ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;”
Kuchukiwa kwa watu wasio wa ulimwengu huu
Kwa sababu mtawala wa ulimwengu
huu yaani shetani amepokonywa mateka yaani watu waliookolewa, wakahamishwa
katika ufalme wa Mungu, Shetani amekuwa adui mkubwa sana wa watu wa Mungu na
anachukizwa nao sana. Yesu akilijua hilo anatuwekea wazi, kuwa nasi tutachukiwa
sana na ulimwengu na hii ni kwa sababu ulimwengu huo huo haukumkubali Bwana
Yesu.
Yohana 15:18-21 “Iwapo ulimwengu
ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.Kama
mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi
si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo
ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa
kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika
neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina
langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka.”
Yesu anaendelea kukazia kuwa
mtumwa si mkubwa kuliko Bwana wake, maana yake hali ile ile ambayo watu
wanamfanyia Bwana wako ni hali ile ile ndiyo watakayo mfanyia mtumwa wake, Hali
anayofanyiwa mwenye nyumba, ndiyo hiyo hiyo watakayofanyiwa wale wa nyumbani
mwake, ikiwa walimsulubisha Bwana wetu Yesu Kristo hali kadhalika wanafunzi wa
Yesu Kristo watasulubiwa na kupata mateso mengi, kwa sababu nao wataishi na
kufanya kazi kama zile zile alizozifanya Yesu Kristo, Yesu ni Nuru ya ulimwengu
hali kadhalika watu wa Mungu ni nuru ulimwenguni, na watu wa dunia hii
wanapenda giza na ndio maana walimsulubisha Yesu Kristo wote wapendao kuishi
kwa hali itokanayo na Kristo Yesu wataudhiwa
2Timotheo 3:10-12 “Bali wewe umeyafuata
mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na
uvumilivu,na upendo, na saburi; tena na adha zangu na mateso, mambo
yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya
adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote.Naam, na wote
wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.”
Kwa hiyo wapenzi msione kuwa ni
ajabu watu waliompokea Yesu, wakikutana na vikwazo vingi, wakikataliwa, wakidharauliwa,
wakichukiwa na dunia, wakifanyiwa fitina, wakizushiwa, wakidhulumiwa,
wakifanyiwa hila, wakihuzunishwa kwa namna mbalimbali, wakibaniwa, wakisalitiwa, wakitafuta kuuawa, Wakristo
watapata mateso na uonevu kwa sababu ya Imani yao, watakutana na vipingamizi
kwa sababu ya mifumo ya kipinzani ya dunia hii,
watatengwa na jamii na familia zao na dini zao, kwa sababu hawakubaliki na mfumo wa ulimwengu
huu, mifumo ya Kosmokrator iko kuanzia ngazi ya ulimwengu, mabara, mataifa,
mikoa, wilaya na kila kijiji, na katika kila eneo nguvu ya ushawishi wa mkuu wa
anga katika eneo hilo atapingana vikali na wakristo wa eneo husika akitumia
aina ya ushawishi wake, katika eneo husika kuwapiga vita wakristo na vita hii
iko katika ulimwengu wa roho.
Waefeso 6:10-13 “Hatimaye, mzidi kuwa
hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu,
mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu
ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili,
juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.Kwa sababu hiyo twaeni
silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha
kuyatimiza yote, kusimama.”
Katika vita hivi na mfumo wa
ulimwengu huu wakristo hawapaswi kuogopa kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu hana
kitu kwa Yesu Kristo na zaidi ya yote neno la Mungu limetuthibitishia wazi ya
kuwa aliye ndani yetu ni mkuu kuliko yeye aliye ulimwenguni.
1Yohana 4:4-6 “Ninyi, watoto wadogo,
mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu
kuliko yeye aliye katika dunia. Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na
dunia huwasikia Sisi twatokana na Mungu. Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye
asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya
upotevu.”
Watu wa Mungu wanapaswa kuwa
hodari Duniani, wanapaswa kuwa na imani, wanapaswa kuwa wapambanaji, wanapaswa
kutumia silaha zote walizopewa kushughulika na wakuu wa anga katika mazingira
yetu na kuharibu nguvu ya ushawishi inayotenda kazi kulingana na mazingira yetu
na kwa kufanya hivyo tutapata upenyo, aidha kila tunapoendelea kuihubiri injili
tunaendelea kumpa shida mkuu wa anga na kumpokonya mateka wake.
Jinsi watu wasio wa ulimwengu huu wanavyopaswa kuishi
1.
Kuishi
kwa kiasi chini ya neema ya Mungu – kila
mtu aliyeokolewa, aliokolewa kwa neema na kwa sababu hiyo hiyo hatuna budi
kuendelea kuishi kwa neema, shetani hatataka mtu aliyeokolewa kwa neema
aendelee kufurahia neema hiyo na kwa vyovyote vile atatupandikizia falsafa za
dunia hii za kututaka tupate kibali kwa Mungu kwa njia ya tendo au matendo fulani,
ni muhimu kukumbuka na kufahamu kuwa dini zote za uongo duniani zina mfumo wa
kukutaka upate kibali kwa Mungu kwa njia ya matendo, Uislamu unakazia matendo
mema, Budha, Hindu, Confucianism, Sikhism,Taoism, Shintoism, Judaism n.k au kuupata wokovu kwa kazi, au kwa matendo
mema, jambo hilo ni kinyume na kweli ya Mungu kwa sababu wokovu, na uzima wa
milele ni zawadi kutoka kwa Mungu, ni kipawa ni karama ambayo kamwe haitokani
na nafsi zetu wala matendo yetu bali
neema ya Mungu, tunaokolewa kwa neema na tunaendelea kuishi kwa neema tukimpendeza
na kusaidiwa na Roho wake Mtakatifu kumpendeza Mungu kwa neema yake.
Waefeso 2:8-9 “Kwa
maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi
zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”
2.
Kuishi
kwa Imani isiyotikisika - watu wa
Mungu watapitia dhiki na mateso mengi lakini mateso yao au yetu isiwe sababu ya
kuyumba wala kuogopa mateso, watakatifu waliotutangulia waliishi kwa Imani
isiyotetereka hata wakati wa majaribu Makubwa walichagua kupata mateso pamoja
na watu wa Mungu badala ya kujifurahisha kwa anasa huku wakiikana Imani, Badala
yake walikaza kumwangalia Mungu kwa matokeo.
Waebrania 11:24-27 “Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti
Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko
kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake
Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo
malipo. Kwa imani akatoka Misri, asiogope ghadhabu ya mfalme; maana
alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana.”
3.
Kuishi
kwa uvumilivu na ustahimilivu - Hakuna jambo linauma kama kuteseka ili hali
hujakosea kitu, hata hivyo maandiko yanatutaka kutokuogopa na kutokufadhaika na
badala yake kuendelea kustahimili tukivumilia mateso na shida huku tukiiga
mfano wa wenzetu ambao walidhihakiwa, walipigwa mijeledi, walifungwa kwa
minyororo, walitiwa gerezani, walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno lakini
kwaajili ya Imani katika Mungu na upendo wao kwa Kristo walikubali hata kuuawa
kuliko kumkana Bwana.
1Petro 3:14 “Lakini
mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala
msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu.”
Waebrania 11:35-38 “Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa
vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine
walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;
walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga;
walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa
wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa
nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika
mapango na katika mashimo ya nchi.”
4.
Kutokuifuta
namna ya dunia hii – Nyakati za
kanisa la Kwanza wanafunzi wa Bwana walijitolea kuishi maisha ya uadilifu na
kujitofautisha sana na mifumo ya ulimwengu huu, neno namna ya dunia hii maana
yake ni kushi chini ya kiwango, au chini
ya uadilifu neno linalotumika hapo standard
of this world au Pattern of this
world kwa kiyunani suschēmatizo yaani Fashion au design au
model, au alike kwa hiyo lazima watu wa
Mungu wajitofautishe na watu wa dunia hii katika mtindo wao wa maisha, neno la
Mungu linaagiza hivyo na neema ya Mungu itatusaidia kutufundisha namna ya kuishi zaidi ya kiwango cha
dunia hii nje ya muundo
Warumi 12:2 “Wala
msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate
kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”
Tito 11:11-12 “Maana
neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa
ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika
ulimwengu huu wa sasa;”
5.
Kuonyesha
upendo uzidio – Pamoja na changamoto ambazo ulimwengu utatuletea kutokana
na mfumo wake watu wa Mungu ambao wao sio wa ulimwengu huu wanapaswa kuendelea
kuonyesha upendo mkubwa kwa wengine hususani wale wanaotuchukia na kufikiriwa
kuwa ni adui zetu, kuwapenda maadui au kuwaombea wale wanaotuchukia na kuishi
kwa kuonyesha upendo uzidio na hii sio hali ya kawaida kwa ulimwengu huu kwa
kufanya hivyo tutawavuta wale watu wa ulimwengu huu kuona na kujua ya kuwa kuna
kitu cha ziada katika Kristo.
Mathayo 5:43-46 “Mmesikia
kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi
nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa
Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema,
huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi
mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? ”
Matendo 7:58-60 “wakamtoa
nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa
kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba,
akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu,
Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa
akiona vema kwa kuuawa kwake.”
6.
Kuvaa
silaha zote za Mungu - watu wasio wa ulimwengu huu wako vitani, na hivyo
maandiko yanaagiza kuwa wavae silaha zote za Mungu kama inavyoelezwa katika
kitabu cha Waefeso
Waefeso 6:11-18 “Vaeni
silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana
kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka,
juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa
roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku
ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga
kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari
tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa
hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni
chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na
maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu
katika kuwaombea watakatifu wote;”
Hiyo inaashiria
kuwa tunapaswa kuwa tayari katika hali ya kiroho kukabiliana na utendaji wa
mkuu wa anga na nguvu zake za ushawishi na uovu duniani, ili kujilinda katika
vita tuliyonayo kiroho, Kila mkristo kwa kuwa anajua ya kuwa yuko katikati ya
adui anapaswa kuwa na msimamo thabiti katika Imani na kupambana kwa ujasiri kwa
neema ya Mungu kuweza kuzishinda hila zote za adui zinazozuia ukuaji wa ufalme
wa Mungu kwa njia ya injili. Wewe mwenyewe pia ukiyalinda maisha yako kwa kuwa
uko vitani, uongezewe neema!
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni