Ufunuo 12:9-11 “Yule joka akatupwa, yule
mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu
wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia
sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu
wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu
zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda
kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha
yao hata kufa.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya
Silaha yenye nguvu kubwa sana kuliko zote duniani katika ulimwengu wa roho ni
pamoja na damu ya Yesu. Bila damu ya Yesu hata Imani yetu isingeweza kuendelea
kuwepo duniani, Damu ya Yesu Kristo inawakilisha kila kitu ambacho Yesu Kristo
alikifanya pale msalabani, Kuhesabiwa haki, ukombozi, upatanisho, Msamaha,
utakaso,Uhuru kutoka katika adhabu na hasira ya Mungu, na agano, Yote haya ni
marupurupu yanayopatikana katika damu ya Yesu, kwa msingi huo basi, kuwa na
ufahamu kuhusu utendaji wa Damu ya Yesu ni muhimu sana kwetu kama wakristo,
kwaajili ya kuelewa haki zetu zipatikanazo kwa Damu ya Yesu ili tuweze kuwa na
ushindi siku zote za maisha yetu. Tutajifunza somo hili Wakamshinda kwa damu ya
Mwana-Kondoo kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Kazi ya damu katika nyakati za agano la kale.
·
Kazi ya Damu ya Yesu katika nyakati za agano
jipya.
·
Wakamshinda kwa damu ya Mwanakondoo.
Kazi ya damu katika nyakati za agano la kale.
Ni muhimu kufahamu, kwamba ili
tuweze kuelewa vema Kazi ya Damu ya Yesu Kristo, uweza wake na nguvu zake ni
muhimu kwetu kuchukua muda kidogo, kujifunza matumizi ya damu jinsi yalivyokuwa
nyakati za agano la kale, ili tuweze kujua utendaji huo namna unavyokuwa sasa
katika agano jipya, Nyakati za agano la kale Damu zilizotumika zilikuwa damu za
wanyama na kazi ya damu ilikuwa ni moja ya ishara muhimu sana ya msingi sana
katika ibada za agano la kale kwa sababu zifuatazo:-
1.
Ilikuwa
sehemu muhimu ya dhabihu ya upatanisho – Damu ilikuwa ni kiini muhimu cha
ibada za dhabihu ambayo iliagizwa katika torati ya Musa. Dhabihu/Kafara za
wanyama zilikuwa zinatolewa na damu ya wanyama hao zilikuwa zinanyunyizwa
katika madhabahu kama njia ya upatanisho kwaajili ya dhambi.
Mambo ya walawi 17:10-12 “Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni
mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja
uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa
kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya
madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu
ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli,
Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati
yenu asile damu.”
Damu ilikuwa ni
nyenzo muhimu ya kufanya upatanisho, yaani kwa kuwa mwanadamu anapotenda dhambi
mara moja dhambi huharibu uhusiano wao na Mungu na kudai kifo, kwanini kifo kwa
sababu Mungu alikuwa amemuonya mwanadamu wa kwanza kuwa siku atakapofanya dhambi
hakika atakufa, kwa hiyo Damu kama uhai inamwagika kwa niaba ya mwanadamu na
kugeuka kuwa sadaka ya kumpatanisha mwanadamu na Mungu, Kwa hiyo Damu hufanya
kazi ya upatanisho. nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili
kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; Nafsi za wanadamu
hupatanishwa na Mungu kwa njia ya Damu, uadui wetu na Mungu unapoozwa au
kufunikwa kwa sababu ya Damu.
Upatanisho ni
nini? neno upatanisho katika Biblia ya kiingereza limetumika neno atonement karibu mara 71 katika lugha
ya kiebrania neno atonement linasomeka kama neno Kậphar ambalo hutamkwa Kaw-far sawa na neno la Kiswahili
KAFARA ambalo maana yake ni kuwaleta
pamoja watu waliokuwa maadui au waliotengana kwa kuwapatanishan, kwa hiyo neno
atonement “at- one- ment” is reparation,
au reconciliation ambalo maana yake ni bringng together into harmony of those
who heve been separated or enemies, kwa hiyo damu ina nguvu ya kuvunja uadui uiotokana na dhambi zetu kati yetu sisi
wanadamu na Mungu na kumpa Mungu nafuu, uhalali, kibali, cha kukubali
kutuachilia, na kuwa rafiki yetu.
2.
Alama
muhimu ya agano – Damu katika agano la kale vilevile ilitumika kama alama
ya agano kati ya watu na Mungu, Damu iliponyunyizwa juu ya watu iliwafanya
wanadamu, kupata kibali kwa Mungu na kuzuia hasira za Mungu zisiwake juu ya
watu wake, Damu iliwafanya watu hao kuwa mali ya Mungu, na kuwa na urafiki wa
kudumu na Mungu!
Kutoka 24:7-11 “Kisha
akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote
aliyoyanena BWANA tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu,
akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja
nanyi katika maneno haya yote. Ndipo akakwea juu, Musa, na Haruni, na Nadabu,
na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli; wakamwona Mungu wa
Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti
samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake. Naye hakuweka mkono wake juu
ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa.”
Agano ni nini?
Neno agano katika biblia ya kiingereza linatumika neno Covenant ambalo limetumiwa katika biblia mara 264 katika lugha ya
kiibrania neno Covenant linatumika neno Beriyth
ambalo maana yake ni muungano wa ushirikiano wa kirafiki au kisiasa confederation au alliance – the permanent
union yaani muungano wa kudumu mfano
nchi zipatazo 50 au zaidi za America zilikubaliana kuwa kitu kimoja na kupatikana
United States of America, kwa hiyo Damu husababisha watu na Mungu kuwa na
serikali moja, jeshi moja, na ushirikiano wa kudumu wa kirafiki na kisiasa na
Mungu
3.
Alama
ya utakaso na wakfu – Damu katika agano la kale ilitumika kama alama ya
utakaso na kuweka wakfu kwa Bwana, Mfano makuhani wale waliochaguliwa kwa kazi
ya utumishi walitakaswa na kuwekwa wakfu ili watumikie Mungu kwa damu ya
wanyama angalia:-
Kutoka 29:20-21 “Kisha
utamchinja kondoo, na kuitwaa damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la
Haruni la upande wa kuume, na katika ncha za masikio ya kuume ya wanawe, na
katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vikuu vya
miguu yao ya kuume, na kuinyunyiza hiyo damu katika madhabahu kuizunguka
kando-kando. Kisha twaa katika hiyo damu iliyo juu ya madhabahu, na katika hayo
mafuta ya kutiwa, na kumnyunyizia Haruni, juu ya mavazi yake, na wanawe, na
mavazi yao pia, pamoja naye; naye atatakaswa, na mavazi yake, na wanawe, na
mavazi ya wanawe, pamoja naye.”
Sio hivyo tu
Damu ilitumika kama nyenzo katika ibada kama njia ya kusafisha na kutakasa kwa
kutumia damu. Na pasipo kumwagika Damu hakuna ondoleo la Dhambi.
Waebrania 9:19-22 “Maana
kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyoamuru
sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na
hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote, akisema, Hii ni damu ya
agano mliloamriwa na Mungu. Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada
alivinyunyizia damu vivyo hivyo. Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa
kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.”
Kutakaswa au
kuwekwa wakfu ni kitendo cha kutengwa na Mungu kwaajili ya Mungu na kufanywa
mtakatifu jambo ambalo pia linafanywa na Damu ya Yesu
Waebrania 13:11-12 “Maana wanyama wale ambao damu yao huletwa ndani ya patakatifu na
kuhani mkuu kwa ajili ya dhambi, viwiliwili vyao huteketezwa nje ya kambi. Kwa
ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya
lango.”
4.
Alama
ya Pasaka – Ukombozi mzima wa wana wa Israel kutokuuawa kwa wazaliwa wao wa
Kwanza na kuruhusiwa kutoka utumwani, na kumtiisha Farao kulikuwa ni matokeo ya
kazi ya Damu ya ukombozi ambayo mwanakondoo wa Pasaka alichinjwa na damu yake
ikanyunyizwa katika miimo ya milango, na kwa tendo hilo na utii wake wana wa
Israel waliokolewa kutoka pigo la mwisho, walipata ulinzi na waliokolewa kutoka
utumwani na kutembea kwa ujeuri kurudi katika inchi yao.
Kutoka 12:3-13 “Semeni
na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu
atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu
wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye
na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa
kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya
hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa
mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku
ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli
watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo
miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula
nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena
pamoja na mboga zenye uchungu. Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali
imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani. Wala msisaze kitu chake cho chote hata
asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto. Tena mtamla
hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu
mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya BWANA. Maana nitapita
kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika
nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu
yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile
nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate
pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri.”
Neno Pasaka katika lugha kiingereza
linatumika neno Passover sawa na
neno la kiibrania Pesach na kiswahili Pasaka neno hilo katika tafasiri ya
kiingereza linaweza kutamkwa “passed
over” maana yake Skipping au Passing
over yaani Mungu alikuwa napita katika inchi ya Misri kuhukumu kwa kuua
wazaliwa wa kwanza wa kila mlango usiokuwa na alama ya Damu, lakini kila mlango
uliokuwa na akama ya damu aliiruka au kupita juu yake bila kuhukumu, kwa sababu
damu ilifanya tukio liitwalo Propitiation
yaani kuacha kukasirikia au kuhukumu kwa hoyo damu husababisha tuache
kukasirikiwa na Mungu.
5.
Alama
ya uzima na mauti – Damu katika agano la kale ilitumiwa na Mungu kama alama
ya uzima na mauti, Damu ilitumika kuyatakasa maisha ya mwanadamu, na ndio maana
Mungu aliwakataza wana wa Israel na wanadamu wote mpaka leo kutokuitumia damu
kama chakula kwa sababu inawakilisha uhai, Damu ilikuwa ikitolewa kama mbadala
wa dhambi yaani uhai unatolewa ili mwingine apate uzima asiuawe.
Walawi 17:10-14 “Kisha
mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati
yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo
alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa kuwa uhai wa mwili u
katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya
upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa
sababu ya nafsi. Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni
mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu. Mtu
ye yote aliye wa wana wa Israeli, au wa hao wageni wakaao kati yenu, ambaye
amemshika mnyama, au ndege ambaye huliwa, katika kuwinda kwake; atamwaga damu
yake, na kuifunika mchanga. Kwa maana kuliko huo uhai wa mnyama, hiyo damu yake
ni moja na uhai wake; kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya
mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake;
atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali.”
Kwa hiyo unaweza
kuona kuwa nyakati za agano la kale Damu ilikuwa ni alama au ishara muhimu
kwaajili ya upatanisho, agano, utakaso, maisha na uhai, na ilitumika kumpa
mwanadamu haki zake zote kutoka kwa Mungu ambazo alizipoteza kwa sababu ya
kuweko kwa dhambi, damu ilisimama mahali palipobomoka kuwapatanisha wanadamu
kwa Mungu na lakini hata hivyo ilikuwa ni alama au ishara inayoonekana na ambayo
ilisimama kama kivuli cha damu halisi na safi na kamilifu itakayokamilisha
maswala hayo yote katika agano jipya.
Kazi ya Damu ya Yesu katika nyakati za agano jipya
1.
Damu ya Yesu inatupa Ondoleo la dhambi
- Damu aliyoimwaga Bwana Yesu kupitia mateso yake pale msalabani inafanya kazi
ya kufuta, kuondoa, kumaliza kabisa, kulipa kabisa Deni la dhambi, Damu ya Yesu
inazifutilia mbali dhambi zote ambazo tumewahi kuzifanya jana, leo na hata
milele.
Mathayo 26:27-28 “Akakitwaa
kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii
ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.”
Ufunuo 1:5-6 “tena
zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa
waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu
katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba
yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.”
1Yohana 1:7 “bali
tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi,
na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.”
Neno Ondoleo la dhambi linalotumika katika Mathayo 26:28 katika biblia ya kiingereza linasomeka kama
neno for remission of sins yaani
katika kiyunani ni Aphesis ambalo
maana yake ni Msamaha wa dhambi, au kufutiwa deni kwa kiingereza the cancellation of debt, charge or penalty
yaani kufutiwa deni, au kufutiwa kesi au kuondolewa adhabu, Kwa hiyo Mtu
anapomwamini Bwana Yesu kwa kazi yake aliyoifanya pale msalabani dhambi zako
zote zinasamehewa na anahesabika hana cha kulipa, hawezi kuadhibiwa tena hakuna
tena hukumu ya adhabu juu yake Warumi 8:1 “Sasa,
basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu.”
Neno ondoleo la
dhambi katika kiyunani linasomeka kama Aphesis
– ambalo linaweza kutafasiriwa kwa maneno ya kiingereza kama Pardon, Deliverence, Forgiveness,
Liberty and Remission, Lakini neno Remission
linatumika kimahakama zaidi na neno Liberty
linatumika kiutawala Neno lililotumika katika maandiko ni neno Remission ambalo limetumika zaidi ya
mara tisa neno hili la kimahakama linahusiana na kumuachilia mfungwa mwenye
hatia kwamba awe huru mbele ya sheria bila kubadili asili ya mashitaka yake Remission is to reduce without changing
the nature of the sentence where by the prisoner is released with or without
condition and in the eyes of the law he/she will be free man or woman, Na neno
Liberty – is a state of civil or political freedom – ni Hali ya kuwa huru
kiraia au kisiasa, ni kama vile Rais anapoamua kuwaachia watu huru wakati
wa sikukuu za muungano au uhuru, kuna wafungwa ambao wanaachiliwa huru kwa
matamko ya kisiasa, Kwa hiyo Damu ina mtindo huo wa kumtangaza au kumfanya mtu
awe huru mbele za Mungu kwa mujibu wa sheria au kiutawala na kuhesabika kuwa
raia wa kawaida bila kutumikia adhabu iliyokusudiwa au bila kulipa kodi.
Damu ya Yesu pia inaosha – neno kuosha
katika kiyunani ni “Louō” ambalo maana yake ni kufua au kuogesha
ni tendo la kumsafisha mwanadamu katika ukamilifu wake kwa jinsi ya mwili,
nafsi na roho, kwa hiyo damu ya Yesu inawasafisha wale wanaomuamini, kuna
maneno mawili yanayotumika kuhusu kuosha kuna neno kuosha “Louō”
na “Katharizō” washed and Cleanses ambalo maana yake kutakasa au kufanya
safi.(Purify)
2.
Damu ya Bwana
Yesu pia inasababisha watu wahesabiwe haki - kuhesabiwa haki ni lugha ya kimahakama
yenye maana ya kutokuonekana na hatia, ingawa sisi tulikuwa wenye hatia halisi
lakini Mungu kwa amri ya kimahakama anakutangaza kuwa na haki kana kwamba
hujawahi kukosea kwa sababu ya kumuamini Mwana wake kwa kazi aliyoifanya pale
msalabani Justification – kwa kiyunani “Dikaioō” yaani kutangazwa kutokuwa na
hatia you are innocent , free justify
ni lugha ya kimahakama ya kukutangaza kuwa huna hatia.
Warumi 5:1-2 “Basi
tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa
njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani
kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la
utukufu wa Mungu.”
Warumi 5:8-9 “Bali
Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa
ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha
kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye.”
Wagalatia 3:10-14 “Kwa
maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana
imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika
kitabu cha torati, ayafanye. Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki
mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na
torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. Kristo
alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu;
maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka
ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho
kwa njia ya imani.”
Tito 3:5-7 “si kwa
sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa
kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia
kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa
neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini
letu.”
3.
Damu ya
Yesu pia inatupa ukombozi - Neno ukombozi katika maandiko ya kiingereza ni
Redemption neno hili katika lugha ya
kibiblia Neno hilo Redemption kwenye kiyunani linatumika neno “Apolutrōsis” ambalo maana yake kwa
kiingereza ni Ransom in full ambalo
tafasiri yake a sum of money demanded or paid for release of a captive, lugha hii inaweza kutumika katika
mazingira ya mfano, watekaji nyara wanamteka mtu na kumuweka kizuizini, kisha
wanadai kiwango fulani cha gharama kilipwe ili mateka huyo aweze kuwa huru,
lugha hiyo ya kulipia deni ili mtu huyo mfungwa au aliyetekwa aweze kuachiwa
huru ndio lugha ya ukombozi inayotajwa katika maandiko, kwa hiyo adui hana
uwezo wa kukumiliki tena kwa sababu madai yake yamelipwa yote kwa ukamilifu
hawezi tena kukuweka kizuizini na hana madai tena, Kwa hiyo Damu ya Yesu pia
hufanya kazi ya kutukomboa yaani kututoa kifungoni, au kutuweka huru bila madai
yoyote kutoka kwa aliyekuwa anatuzuia yaani shetani.
Waefeso 1:6-8 “Na
usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.Katika
yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na
wingi wa neema yake. Naye alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi;”
Wakolosai 1:14 “Naye
alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa
Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa
dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.”
1Petro 1:18-19 “Nanyi
mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu;
mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa
damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya
Kristo.”
Wagalatia 5:1 “Katika
ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena
chini ya kongwa la utumwa.”
Kwa hiyo
tunaweza kuona kuwa Damu ya Yesu inafanya kazi ya ukombozi, ambao unajumuisha
kusamehewa dhambi, urejesho kutoka katika nguvu za kitu chochote kile ambacho
kilikuwa na haki ya kukushikilia, zikiwemo nguvu za giza, unapomjia Yesu nguvu
hizo hazina mamlaka ya kukushika kwa sababu zozote zile, hauko tena chini ya
utumwa, au ufungwa au mateka ya adui kwa kuwa sasa wewe ni mali ya Yesu.
4.
Damu ya
Yesu inatuhuhisha tena na kutuweka karibu na Mungu - Kabla ya kumuamini Yesu kila mkristo na asiye
mkristo ambaye hajaokolewa anahesabika kuwa alikuwa mbali na alikuwa ni adui wa
Mungu, hatungeweza kuwa karibu na Mungu na kupata msaada kwake kwa sababu
dhambi humweka mtu mbali na Mungu, lakini baada ya kazi aliyoifanya Yesu pale
Msalabani sisi tuliokuwa mbali sasa tunaletwa karibu na Mungu kwa damu ya Yesu
Waefeso 2:11-13 “Kwa
ajili ya hayo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi, mlio watu wa Mataifa kwa jinsi
ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale wanaoitwa Waliotahiriwa, yaani, tohara
ya mwilini iliyofanyika kwa mikono; kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo,
mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa
hamna tumaini, hamna Mungu duniani. Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi
mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.”
Wakolosai 1:21-22 “Na
ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa
matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa; katika mwili wa nyama yake, kwa kufa
kwake, ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama;”
5.
Damu ya
Yesu inatupa kibali na ujasiri wa kupaingia patakatifu pa patakatifu – wote
tutakuwa tunakumbuka ya kwamba Hekalu lilikuwa na maeneo makuu matatu, yaani
uwa wa nje, kisha uwa wa ndani na ndani kabisa, uwa wa nje ni mahali ambapo watu
walifika na kufanyiwa ibada za upatanisho za kila siku, na uwa wa ndani ni
mahali ambapo makuhani waliingia kwa zamu kwaajili ya kufukiza uvumba kila
siku, na uwa wa ndani kabisa mahali palipoitwa patakatifu pa patakatifu kuhani
mkuu aliingia mara moja tu kwa mwaka na kuweka damu katika madhabahu ya Mungu
ambacho ni kiti cha rehema kwaajili ya kuwaombea watu, eneo hili kuhani mkuu
aliingia baada ya kuwa amejitakasa kwa siku saba, palikuwa ni mahali ambapo
palikaa uwepo wa Mungu nyakati za agano la kale, hapa palitengwa kwa pazia maalumu
lenye unene wa inchi sita sawa na unene wa tofali, lakini siku Yesu anakufa
msalabani kwa kuimwaga damu yake Pazia hili lilipasuka vipande viwili na watu
wakapaona mahali patakatifu ambapo ilikuwa sio rahisi kupaona, pazia hili
liliwakilisha mwili wa Kristo uliosulubiwa na damu yake imetupa rehema na neema
ya kuweza kumfikia Mungu moja kwa moja bila kizuizi wala bila kuhitaji mtu wa
kuingia kwa niaba yako kwa kuwa wewe nawe umefanyika kuhani kwa nafsi yako.
Mathayo 27:51-54 “Na
tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi
ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya
watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka
kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao
waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo
yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu”
Waebrania 10:19-21 “Basi,
ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile
aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na
kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu; ”
Waebrania 4:14-16 “Basi,
iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na
tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana
nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi
katika mambo yote, bila kufanya dhambi.Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa
ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”
Maandiko
yanapotualika kukaribia kwa ujasiri katika kiti cha Rehema au patakatifu maana
yake tunaalikwa kumkaribia au kuukaribia uwepo wa Mungu pasipo hofu sisi
wenyewe mahali ambapo tutapokea msamaha na rehema na upendo wa Mungu, hii ni
kwa sababu zamani kabla ya Yesu kufa Msalabani hakuna mtu aliruhusiwa
kuukaribia uwepo wa Mungu pasipo kuhani au kuitwa na Mungu mwenyewe na
ukikaribia ilikuwa ni kifo, kwa hiyo katika nyakati za agano jipya baada ya
kifo cha Bwana Yesu sasa tunaweza kwenda kwa uwazi, kwa uhuru, pasipo hofu,
wala pasipo kuhani au mpatanishi, bila woga, bila kuhukumiwa na kukabiliana na
Mungu sisi wenyewe na kujielezea kwake bila mtu kuingilia kati na kumwaga mizigo
yetu, mashaka yetu, fadhaa zetu na hatutauawa kwa sababu ya rehema zake na
upendo wake mkubwa kwetu atatusaidia, kwa sababu ya rehema zake atatupokea bila
kujali ukubwa wa makosa yetu, hatuhitaji kuigiza kuwa sisi ni wakamilifu, hatuhitaji
kujitafutia haki kwa sababu hatuwezi kuwa na haki yetu wenyewe, Sadaka pekee na
kibali pakee kinachotupa ujasiri huo ni Kazi ya Yesu iliyofanyika pale
Msalabani. Yaani Damu yale aliyoimwaga, na kwa njia ya Imani damu hii iakupa
ruhusa, kibali au tiketi ya kumfikia Mungu
6.
Damu ya
Bwana Yesu inatupa Amani na Mungu – Damu ya Yesu Kristo inatupa Amani
ya kweli, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama hujasamehewa dhambi, huwezi kuwa
na Amani ya kweli kama uko chini ya ufalme wa giza, huwezi kuwa na Amani ya
kweli kama una uadui na Mungu, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama huna ujasiri
wa kupaingia patakatifu, huwezi kuwa na Amani ya kweli kama u mfungwa na mateka
katika utawala wa ibilisi hivyo tunapomuamini Bwana Yesu, ambaye aliteseka kwa
niaba yetu tunapata Amani ya kweli.
Waebrania
9:12-14 “wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali
kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata
ukombozi wa milele. Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya
ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili;
basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi
yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo
mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?”
Isaya 53:3-5 “Alidharauliwa
na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu
ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.
Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania
ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa
yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na
kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”
Wakamshinda kwa damu
ya Mwana-Kondoo!
Ufunuo 12:9-11 “Yule joka akatupwa, yule
mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu
wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia
sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu
wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu
zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda
kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha
yao hata kufa.”
Katika kifungu hiki cha maandiko
tunapewa taarifa ya mfumo wa vita kubwa iliyoko katika ulimwengu wa roho na
namna ya kuishinda vita hiyo, hii ni vita kati ya nuru na giza ni vita kati ya
nguvu za uovu na wema wa Mungu, Kifungu kinafunua siri kubwa ya ushindi wa watu
wa Mungu, kushinda kwa damu ya mwana kondoo kunajumuisha maswala yote muhimu
ambayo tumeyapata kupitia damu hiyo ambayo yalikuwa yanampa nafasi shetani
kutumia mfumo wa kimahakama na kibunge kutushinda kama mshitaki au mwendesha
mashitaka na kwa sababu hiyo anapoteza haki na uwezo wa kutushitaki kwa sababu
Damu ya Yesu Kristo imemaliza kila hati yake ya mashitaka anayotaka kuitumia
ili tuharibiwe;-
Zakaria 3:1-4 “Kisha akanionyesha Yoshua,
kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono
wake wa kuume ili kushindana naye. Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee
Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si
kinga kilichotolewa motoni? Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye
alikuwa akisimama mbele ya malaika. Naye huyo akajibu, akawaambia wale
waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha
akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya
thamani nyingi.”
Nyakati za agano la kale Shetani
aliendelea kufanya kazi zake za kushitaki wateule wa Mungu hata sasa bado
anaifanya kazi hiyo na ndio maana anaitwa mshitaki wetu
1Petro5:8-10. “Mwe na kiasi na kukesha; kwa
kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta
mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa
mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. Na Mungu wa neema
yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha
kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na
kuwatia nguvu.”
Kwa hiyo shetani alipata haki ya
kuwashitaki watu wa Mungu kwa sababu kulikuwako hakuna damu ya Yesu,
alimshitaki kuhani mkuu Yoshua kwa sababu kweli alikuwa mchafu na Bwana
alimkemea, lakini sasa katika agano jipya damu ya Yesu inafanya kazi ya
kumkemea ibilisi kwa niaba yetu kama tutaitumia kwa Imani kwa hiyo andiko la
msingi linaonyesha kutupwa kwa Mshitaki huyu na sababu kubwa ya kutupwa kwake
na ushindi mkubwa kupatikana ni Damu ya mwanakondoo na neno la ushuhuda.
a.
Ametupwa
chini Mshitaki wa Ndugu zetu – Ibilisi hufanya kazi katika ulimwengu wa roho
kwa mfumo wa kimashitaka na kwa kweli tuna haki ya kushitakiwa kutokana na
ukweli ya kuwa tuna dhambi, lakini mashitaka ya shetani hupoteza haki kwa
sababu damu ya Yesu iliyopatikana kwa
kazi iliyofanyika msalabani inafanya
kitu cha tofauti
i.
Inatunenea
mema – Waebrania 12:22-24 “Bali ninyi mmeufikilia
mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya
malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa
mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki
waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo
mema kuliko ile ya Habili.”
Damu ya Yesu inauwezo wa kuzungumza maneno mema mazuri
kwaajili yetu kuliko mashitaka ya adui, kupitia ushindi wake pale Msalabani,
Yesu amechukua ushindi dhidi ya nguvu za giza, Kwa hiyo Kazi ya damu hii ni
kutunenea mema na kwa sababu hiyo huwezi kuhesabiwa kuwa na hatia, au u mtumwa
ama vyovyote vile huwezi kuangamizwa kwa sababu ya damu ya Yesu, kwa hiyo neno
hilo ni mjumuisho wa ushindi tulio nao kupitia damu ya Yesu ambayo kwayo
inatupa neema juu ya neema, sio hivyo tu Damu ya Yesu inamkemea shetani asiwe
na nguvu ya kutushitaki wala kufanya uonevu wa namna yoyote katika nafsi mwili
na roho zetu.
Wakolosai
2:13-15 “Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya
makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye,
akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya
kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena,
akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa
mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”
Warumi 8:33-39
“Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu
ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye
aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa
kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa
Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?
Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa,
Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote
tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha
kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye
mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu,
wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo
wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Ni hatari sana kumshitaki au kumuhukumu mtu
anayemuamini Yesu kwa sababu anahesabiwa haki na Mungu, Andiko katika Warumi
8:33 katika kiingereza NIV mstari huo unasomeka
“Who will bring any charge against those whom God hase
chosen? It is God who justifies.”
Maana yake ni nani atakaye wahesabia kuwa wana hatia
watu ambao Mungu amewachagua “Charge
against” (KATA) kiyunani. Na swala hili jibu lake Mungu ndiye mwenye
kuwahesabia haki Justifies anouced
Innocent (DIKAIOŌ) kiyunani. yaani wale waliotangazwa na hakimu kuwa
hawana hatia INNOCENT maandiko
yanaonyesha kuwa kupitia kazi aliyoifanya Yesu pale Msalabani kwa kumwaga damu
yake (Kristo Yesu Ndiye aliyekufa) alafu
yeye ndiye kuhani mkuu anayefanya upatanisho kwaajili yetu (Tena ndiye anayetuombea) kwa hiyo awaye yote ambaye anatuhesabia
hatia au kutuhukumu kuwa hatufai ili hali Yesu amefanya kazi ya ukombozi na
anatuombea huyu anaunganishwa na ibilisi katika kushindwa
Alaaniwe mtu awaye yote anayekuhesabia kuna na dhambi
wakati Yesu amekufia msalabani na kumwaga damu yake nasema alaaniwe,
aharibikiwe mtu awaye yote anayeongea maovu yako ili hali Mungu amekutangaza
kuwa huna hatia, Bwana na amkemee kila mtu anayeipuuzia kazi ya damu ya Yesu
iliyofanyika kwaajili yetu pale msalabani na kujidhani kuwa yeye ndiye yuko
sawa, Ni damu ya Yesu inayotupa kiburi cha kuuliza ni nani atakayetushitaki? Ni damu ya Yesu ndiyo iliyotuleta katika neema
hii, kwa hiyo mtu yeyote anayehubiri kinyume na kazi ya damu Amelaaniwa.
Wagalatia 1:6-9
“Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye
aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala
si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya
Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili
yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia
kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote
isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.”
ii.
Na
kwa neno la ushuhuda – Ushuhuda huu unaotolewa na waamini ni ushuhuda gani?
Ushuhuda wetu ni kuhusu kazi iliyofanywa na damu ya Yesu katika maisha yetu, tunapozungumza
habari za ukombozi mkubwa unaosababishwa au uliosababishwa na Damu ya Yesu
katika maisha yetu, tunaposhuhudia habari za ukombozi huu tunaendelea kueneza
habari mbaya katika ufalme wa ibilisi kwa jinsi Damu hii inavyoleta neema na
wepesi wa kila mwanadamu kukubali njia hii sahihi ya ukombozi iliyowekwa na
Mungu Msalabani, na ushuhuda huo unatia hasara kubwa sana kwa upande wa shetani
na kumletea kushindwa, kumbuka wakamshinda kwa Damu ya mwana kondoo na kwa neno
la ushuhuda. (Injili).
1Wakorintho
1:17-18 “Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali
niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije
ukabatilika. Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu
sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.”
Warumi 1:16-17
“Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza
wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani
pia. Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani;
kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.”
iii.
Damu
ya Yesu ni silaha – Damu ya Yesu inasimama kama silaha kubwa ya kivita ya
hatari sana katika ulimwengu wa roho, inatumika kama ulinzi kwaajili yetu na silaha ya kumshinda shetani, anakosa
nguvu kabisa tunapoikumbuka kazi aliyoifanya Yesu Pale msalabani, Damu hii ni
ngao, damu hii inatulinda dhidi ya mashambulizi yote ya ibilisi, tunapokumbuka
tu na kujua umuhimu wake na kazi yake ambayo imefanyika kila kitu katika
ulimwengu wa roho hasa wa giza unaachia, kama liko giza haliwezi kusimama kwa
kazi ya Msalaba, kila kikwazo chochote duniani ambacho kinatokana na
mashambulizi ya ibilisi kinasambaratiswa kupitia Damu ya Yesu, tunachotakiwa ni
kuitumainia Damu ya Yesu kwa Imani na kuendelea kuzungumzia utamu wa ushindi
tunaoupata kupitia Damu ya Yesu, Nisikilize kazi yote ya msalabani na tangazo
la Yesu Kristo kuwa imekwisha inakamilishwa katika Damu, ile iliyomwagika
msalabani kwaajili yetu. Damu hii ni kitambulisho ya kuwa tuna uhuru,
tumekombolewa, mfame ametangaza kuwa tuko huru, tuna ushirika wa kudumu na
Mungu, hatudaiwi kodi, ni wageni tulioruhusiwa kufanya kazi zetu kwa kibali cha
mfaome hapa duniani, tuna muungano wa kisera, kisiasa na ushirika na Mungu,
tuna kibali, hatuna hatia, hatuna mashitaka, tumewekewa alama ya kutokuuawa,
tuna utambulisho wa uhuru kwa sababu tumemuamini Mungu na tumeikubali kazi yake
ya ukombozi.
Yoshua 2:18-19 “Angalia, tutakapoingia katika nchi hii, funga kamba hii
nyekundu katika dirisha hili ulilotutelemshia; nawe uwakusanye kwako nyumbani
mwako, baba yako, na mama yako, na ndugu zako, na watu wote wa nyumba ya baba
yako. Itakuwa mtu awaye yote atakayetoka katika mlango wa nyumba yako kwenda
njiani, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, na sisi tutakuwa hatuna
hatia; na mtu atakayekuwa ndani ya nyumba yako damu yake itakuwa juu ya vichwa
vyetu, mkono wa mtu ukimpata.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni