1Samuel 16:1-3 “Bwana akamwambia Samweli,
Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze
pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana
nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli
akipata habari, ataniua. Basi Bwana akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme,
Nimekuja ili kumtolea Bwana dhabihu. Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami
nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako.”
Utangulizi:
Kaka zangu dada zangu Leo
tutachukua muda kiasi kutafakari ujumbe wa Muhimu wenye kichwa “Utamlilia Sauli Hata lini?” Kama
tulivyosoma katika kifungu cha msingi, ujumbe huu una maana kubwa na zaidi sana
leo unatufundisha umuhimu wa kusahau mambo yaliyopita ambayo kimsingi yanaweza
kuwa kikwazo cha kutupeleka katika mambo mapya au hatua nyingine ambayo Mungu
ametuandalia. Wote tutakuwa tunakumbuka kuwa Mungu alimfunulia Samuel Nabii
kuhusu Mfalme Mpya wa Israel na kumuagiza akampake mafuta.
1Samuel 9:15-17 “Basi Bwana alikuwa
amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema, Kesho, wakati
kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe
mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya
Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao
kimenifikilia.Hata Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, Huyu ndiye
niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu.”
Pamoja na kuwa ni kweli Sauli
alikuwa ni chaguo la Mungu, Na Samuel alimtia mafuta Lakini ulifika wakati
ambapo Mungu alikuwa na mpango mwingine, na hivyo alimkataa Sauli na kumtaka
nabii Samuel ampake mafuta Mfalme mwingine mwenye nguvu zaidi na mwenye
kuupendeza moyo wake na aliye mwema kuliko Sauli, Mfalme huyo alikuwako
Bethelehemu katika nyumba ya Yese. Kukataliwa kwa Sauli kuliwekwa wazi mapema
kwa neno la kinabii ona;-
1Samuel 15:26-28 “Samweli akasema, Sitarudi
pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, Bwana naye amekukataa wewe,
usiwe mfalme wa Israeli. Naye Samweli alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika
upindo wa vazi lake, nalo likararuka. Basi Samweli akamwambia, Leo Bwana
amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema kuliko
wewe”
Hata hivyo Samuel kama nabii
inaonekana aliendelea Kumuombea neema Saul kwa majuma kadhaa, alimpenda,
alitamani aendelee kuwa naye, ilikuwa ni tabia ya Samuel kuwaombea wana wa
Israel na mfalme pia kwa mujibu wa maandiko Samuel kuacha kuwaombea Israel kwake
ilikua ni kama kufanya dhambi
1Samuel 12:23 “Walakini mimi, hasha!
Nisimtende Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha
katika njia iliyo njema, na kunyoka”
Kwa hiyo huenda Samuel aliendelea
kumuombea Sauli kwa Mungu, na hakuacha alisikitika
moyoni kumpoteza kijana yule mzuri aliyemtia mafuta yeye mwenyewe shujaa, mtu
mrefu Mzuri kutoka kabila la Benjamin lakini Mungu aliyakataa maombi ya Samuel
kwa sababu alikuwa amekusudia kuwapa Israel Shujaa, kijana mzuri zaidi,
anayeupendeza Moyo wa Mungu mtu aliye mwema na atakayekuwa bara kubwa kwa
Israel, Hivyo Mungu alimkemea Samuel na kumuuliza utaendelea kumlilia Sauli
mpaka lini ikiwa mimi nimemkataa, inawezekana ikawa ni stori nzuri sana na
imenyooka haiitaji tafasiri yoyote, lakini leo hii katika kisa hiki, Mungu
anataka kusema nasi kuhusu swala la kuachilia Mambo ya kale ili aweze kutuingiza katika mambo mapya,
hupaswi kukaa chini na kuyalilia mambo yaliyopia hata kama ni mazuri kiasi gani
kwani kuyalilia hayo kunatufanya tusipige hatua katika kuuendea ukurasa mpya ambao
Mungu anataka uufungue, ili tukue na kuelekea katika kiwango kingine, Tutajifuza
somo hili Utamlilia Sauli Hata lini kwa kuzingatia vipengele vitatu
vifuatavyo:-
·
Umuhimu wa kusahau yaliyopia.
·
Umuhimu wa kutambua mapenzi ya Mungu.
·
Utamlilia Sauli hata lini?.
Umuhimu wa kusahau yaliyopita.
1Samuel 16:1 “Bwana akamwambia Samweli,
Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze
pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana
nimejipatia mfalme katika wanawe.”
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu
anapokuwa na mpango mpya katika maisha yetu, anapenda tuelewe na kusonga mbele
na kuyasahau yaliyopita, siku zote kuendelea kulia lia kwaajili ya mambo ya
zamani kunaweza kutuzuia kuona yale mapya ambayo Mungu ametuwekea mbele yetu,
na siku zote mbele ni kuzuri zaidi, kwa hiyo ni lazima tuukubali kusahau
yaliyopita, ni vigumu sana wakati mwingine kusahau yaliyo nyuma na wakati
mwingine inaonekana kama ni jambo lisilowezekana lakini historia ya nyuma
inaweza kuwa kikwazo kikubwa cha mpango na mapenzi ya Mungu kwaajili yetu na
kwa sababu hiyo ni lazima tuyachuchumilie yaliyo mbele na kukubali kusahau yote
yaliyopita.
Wafilipi 3:13-14 “Ndugu, sijidhanii nafsi
yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo
nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya
thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”
Paulo mtume aliyepitia dhiki na
mateso mengi sana Hakubali hata kidogo kukaa katika hayo lakini wakati wote
alikuwa akijitahidi kuwaza mbele, Ni mapenzi ya Mungu kwetu kusahau mambo yaliyopita hususani yale ambayo
yametuletea maumivu makubwa katika maisha yetu, au makosa amkubwa ambayo tumewahi kuyafanya
huko nyuma, Mungu mwenye rehema na neema wakati wote hutupa nafasi ya pili, na
ya tatu na ya nne na ya tano na ya sita na ya saba na ya nane na kadhalika yeye
anatutaka wakati wote tusilie kwaajili ya yaliyopita na badaa yake tusonge mbele
bila kujali kile ulichokipitia, iweni talaka, au uonevu, au umepoteza kazi, au
umeingia katika changamoto zozote nzito, au umekosea sana, au umefiwa au
ulifeli vyovyote vile Mungu anatutaka tusonge mbele na kuacha kumlilia Sauli
kwa sababu ana mpango mpya nawe, Mwana riadha wakati wote anapaswa kuangalia
mbele, na kuendelea na mbio, kwani kuangalia nyuma kunaweza kuwa kikwazo, kwa
msingi huo usipoteze muda na maswala yaliyopita yawe mazuri au mabaya wewe
angalia mbele, Mungu anayekuwazia mema na mpango mpya!
Isaya 43:18-19 “Msiyakumbuke mambo ya
kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa
litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji
nyikani.”
Ilikuwa ngumu kwa Samuel kuacha
kumlilia Sauli, kwa kuwa alikuwa Mfalme Mzuri na alipewa na Mungu, Lakini sasa
Mungu ana mpango mpya ulio bora zaidi, kwa hiyo, yuko Daudi mwana wa Yese
kwaajili yako hivyo sahahu utawala na ufalme uliopita chukua chupa yako umtie
mafuta yule ambaye Mungu atakuelekeza
Umuhimu wa kutambua mapenzi ya Mungu
Mungu alikuwa na mpango mpya
kwaajili ya Israel Kama alivyo na mpango mpya kwaajili yako, Mungu alikuwa
amechagua mmoja wa wana wa Yese na alikuwa yuko tayari kumpaka mafuta Ili
atawale baada ya Sauli na ulikuwa ni wajibu wa Samuel kwenda Bethelemu na Chupa
yake ya mafuta na kumtia mafuta yule
ambaye Mungu alikuwa amemkusudia, hapa ulikuweko mtihani wa kuyajua mapenzi ya
Mungu na ulikuwepo mpango unaohitaji subira, wakati huo ni lazima tuaachane na
mambo tuliyoyazoea kwa sababu Mungu ana mpango mpya, sauti zinaweza kuwa nyingi
sana wakati tunauendea mpango mpya wa Mungu na tunaweza kufikiri kuwa ni huu au
ule lakini hatimaye Mungu atakufunulia
mpango wake kamili ambao huo Yesu yumo ndani yake, The best is yet to come !
1Samuel 16:6-11 “Ikawa walipokuja,
alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake. Lakini
Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa
maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana
wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo. Ndipo Yese akamwita
Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, Bwana hakumchagua huyu.
Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, wala Bwana hakumchagua huyu. Yese
akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, Bwana
hakuwachagua hawa. Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa?
Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli
akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja
huku.”
Kujua mapenzi ya Mungu kwaajili
ya mpango mpya sio kazi nyepesi, ilimsumbua Samuel ilimsumbua Yese, hawakujua
mfalme mpya ni nani, na kwakuwa hakuwepo pale walihitaji subira, tunahitaji subira
kuyajua mapenzi ya Mungu, Katika maisha yetu tunaweza kukutana na changamoto
kama hizi, wakati huu tunapaswa kuongeza uwezo wa kuisikia sauti ya Mungu, na
kuwa na moyo wa Subira, ili kuachana na mazoea na kuyajua mapenzi yake kwa hiyo
kuna umuhimu wa kuyatambua mapenzi ya Mungu, kuna mambo matatu tu tunaweza
kuyafanya wakati huu
1. Kujaza pembe Mafuta – hii inahusiana na
kufanya maandalizi ya kiroho kwa hiyo ni muhimu kwetu kujitoa kwa Roho
Mtakatifu, kwa kuomba na kujitakasa na kutubu, tendo hili litatuweka karibu na
Roho Mtakatifu na kutusaidia kuijua
sauti yake na zaidi ya yote inatusaidia
kuyatii mapenzi yake na kuyajua
1Samuel 16:4-5 “.Samweli akafanya
hayo aliyosema Bwana, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki,
wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akasema, Naam, kwa
amani; nimekuja kumtolea Bwana dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye
dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu”
Matendo 13:1-3 “Na
huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni
Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa
ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia
Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa
kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao
juu yao, wakawaacha waende zao.”
2.
Kutii
maagizo ya Mungu – Samuel alitii maagizo ya Mungu na kukubalia kumsahau
Sauli na akaenda kwa Yese ili kumtia mafuta Daudi, Tunapaswa kuyatii maagizo ya
Mungu na kusonga mbele bila kuchelewa, ni muhimu kufahamu kuwa mambo ya zamani
yanakamata sana na yanataka kuturudisha nyuma, Lakini Mungu ameruhusu tusonge
mbele kwa hiyo hatuna budi kwenda pale Mungu anaposema twende “Samuel akafanya
hayo aliyoyasema Bwana, akaenda Bethelehemu” kule Bwana atakakosema
wende nenda na yale maagizo ambayo Bwana amekuagiza kuyafanya yafanye kwa
kutumia Hekima chini ya neema yake.
3.
Ruhusu
Mpango mpya wa Mungu - Samuel na
Yese walikubali mapenzi ya Mungu, alipokuja yeye aliyesubiriwa na asiyetazamiwa
Samuel alimtia mafuta kwani Bwana alisema naye huyu ndiye, kwa hiyo
walilazimika kumsahau Sauli na kumkubali Daudi, Mambo ya zamani ambayo hayana
nafasi tena katika maisha yetu na ambayo hayako katiika mpango wa Mungu ni
lazima tuyafukuzilie mbali, ili lile jipya ambalo Mungu amekusudia kulifanya
liweze kuchukua nafasi.
1Samuel 16:12-13 “Basi
akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na
umbo lake lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana
huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya
ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi
Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”
Utamlilia Sauli hata lini?
Utamlilia Sauli hata lini? Ni
swali ambalo Mungu alimuuliza Samuel na ni swali ambalo linatuita katika
kutafakari maisha yetu, Je kuna jambo bado unalishikilia? bado una shikilia
mambo ya zamani ambayo Mungu anataka tuyaache na kuyasahau? Je unajiandaa kwa
mambo mapya? Tunapotulia katika maombi
hatuna budi kuendelea kumuomba Mungu atuongoze na kutuandaa na kutuweka tayari
ili tukubali kuyatii mapenzi yake, na kupokea kile kipya ambacho Mungu
amekikusudia katika maisha yetu na Mungu
ni mwema atakutendea mema usilie!
Kuacha mambo ya zamani kunahitaji
ujasiri, na Imani, Samuel alihitaji ujasiri na kukubali mabadiliko kwa Imani,
kwa sababu Mungu alimthibitishia kuwa ana mpango bora zaidi kwaajili ya Israel
Mpango wenye manufaa sio kwaajili ya Israel tu bali kwa ulimwengu mzima, Mungu alikuwa
amemkusudia mwana wa Daudi kuja kukaa katika kiti cha Enzi milele na huyo ni
Yesu Kristo, uwepo wa Mungu uko mbele, Mungu alikuwa amekwisha kumuacha Sauli
na sasa Roho Mbaya ilikuwa inamkalia, Mahali ambapo uwepo wa Mungu umeondoka,
Shetani na mapepo huchukua nafsi
1Samuel 16:14-15. “Basi, roho ya Bwana
ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa Bwana ikamsumbua. Nao
watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu
inakusumbua.”
Mungu alikwisha ondoa uwepo wake
kwa Sauli na kuruhusu mashetani kumkalia, Mungu anapotushauri jambo ni vema
kwenda nalo, kwa kuwa huko ndiko uwepo wake unakokwenda hatupaswi kujivunia
Sauli tena kwani sasa ni nyumba ya mapepo na uwepo wa Mungu umehama, uwepo wa
Mungu sasa ulikuwa uko juu ya Daudi kwa nguvu!
1Samuel 16:13 “Ndipo Samweli akaitwaa pembe
yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia
Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”
Acha kulilia ya nyuma Songa mbele
Mungu anampango mwema zaidi msahau Sauli, Mungu anaye Daudi wako je utaendelea
kumlilia Sauli hata lini ikiwa mimi nimemkataa? Uwepo wa Mungu uko mbele!,
Usilie kwaajili ya kazi uliyofukuzwa, usilie kwaajili ya nyumba uliyohama,
usilie kwaajili ya mchumba ambaye ameondoka, usilie kwaajili ya mke
aliyekuacha, usilie kwaajili ya mume aliyekuacha, usilie kwaajili ya bosi
aliyekuacha Mungu anao mpango mwingine kwaajili yako, usilie kwaajili ya
uhamisho uliohamishiwa kuna kusudi kubwa na jipya kwaajili ya Mungu. Na
Kwaajili yako na familia yako na watu wako!
1Wafalme 9:5 “ndipo nitakapokifanya imara
kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba
yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni