Jumatano, 27 Novemba 2024

Mafundisho kuhusu Shetani!


Ezekiel 28:13-15 “Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako.

 


Utangulizi

 

Leo tutachukua Muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusu Shetani, inawezekana kuwa ni mara nyingi sana umewahi kusikia kuhusu shetani na huenda anatajwa sana na kila mwanadamu na katika mahubiri anatajwa mara nyingi kila kona ya dunia, lakini uko uwezekano kuwa hujawahi kupata mafundisho ya kutosha kuhusu shetani, Leo Roho Mtakatifu anatutaka tuchukue muda kidogo kujifunza na kujikumbusha kuhusu shetani pamoja na kazi zake zote anazozifanya na kuhakikisha kuwa wakati wote tunamuelewa vema na kujifunza mikakati yake na mbinu zake anazozitumia ili asipate kustushinda kwa kukosa kuzijua fikra zake.

 

2Wakorintho 2:10-11 “Lakini kama mkimsamehe mtu neno lo lote, nami nimemsamehe; kwa maana mimi nami, ikiwa nimemsamehe mtu neno lo lote, nimemsamehe kwa ajili yenu mbele za Kristo, Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.”

 

Kujifunza na kumfahamu shetani, asili yake, kwanini yuko na hatima yake pamoja na utendaji wake wote ni swala la muhimu sana kwa kila Mkristo, kwa sababu shetani licha ya kuwa adui wa Mungu ni adui mkubwa wa wanadamu na adui hatari zaidi kwa watu waliookoka, kwa hiyo utambuzi kuhusu shetani ni agenda Muhimu itakayotusaidia kumtambua adui yetu na namna tunavyoweza kumshinda, kwa msingi huo basi tutajifunza somo hili Muhimu Mafundisho kuhusu shetani kwa kuzingatia vipengele vinne vifuatavyo:-

 

·         Asili ya Shetani.

·         Mafundisho kuhusu shetani.

·         Uwezo na utendaji wa shetani.

·         Hatima ya shetani.

 


Asili ya Shetani

 

Ni muhimu kufahamu kuwa shetani kwa asili anajulikana kama malaika aliyeasi dhidi ya Mungu na kupoteza heshima yake kutoka mbinguni, na kulaaniwa pamoja na malaika wengine waovu, Imani kubwa tatu zilizoko duniani, ambazo asili yake ni Abraham zinamtambua shetani kama mshitaki na adui mkubwa wa wanadamu aliyepoteza heshima yake kutoka mbinguni, na kuwa yeye ni sababu kubwa ya mwanadamu wa kwanza kufukuzwa kutoka katika uwepo wa Mungu yaani Bustani ya Edeni. Maandiko hayajawahi kutuambia kuwa sio malaika, kwa hiyo anatambulika kuwa ni malaika na moja ya malaika wakubwa sana ambao kimsingi, wako karibu na kiti cha enzi cha Mungu, kuondolewa kwake katika mpango huo na kuhukumiwa kwake kumempa hasira kubwa sana na kumfanya awe mpinzani wa mipango yote ya Mungu na uumbaji wa Mungu akiwepo Mwanadamu. Jina lake aliitwa Lucifer yaani mwenye kuangaza au mfano wa nyota ya alfajiri, na hili ndio jina lake. Kutokana na kuanguka kwake shetani Lucifer aliitwa Ibilisi kwa sababu ya kiburi chake na majivuno na mwenendo wake wa moyoni wa kutaka kujiinua kuliko Mungu.

 

1Timotheo 3:6-7 “Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi.”

 

Kwa msingi huo endapo shetani ni ana asili ya malika ni wazi kuwa yeye ni kiumbe aliyeumbwa na Mungu wakati fulani pamoja na malaika wengine kwa amri ya neno lake Mungu ona

 

Zaburi 148:2-5 “Msifuni, enyi malaika wake wote; Msifuni, majeshi yake yote. Msifuni, jua na mwezi; Msifuni, nyota zote zenye mwanga. Msifuni, enyi mbingu za mbingu, Nanyi maji mlioko juu ya mbingu. Na vilisifu jina la Bwana, Kwa maana aliamuru, vikaumbwa.”

 

Kwa msingi huo tunapata ufahamu ya kuwa malaika pamoja na Lucifer waliumbwa kwa amri ya Mungu, kwa sababu hiyo malaika wote wema au malaika wateule na malaika wote waovu yaani mashetani hawastahili kuabudiwa kwa kuwa wao ni viumbe tu, hawana tofauti na sisi katika mtazamo  wa kuwa Mungu aliwaumba kwa kusudi na kuwa sehemu mojawapo ya utumishi wao ni pamoja na kujihusisha na wanadamu na kuwahudumia hii ni kwa malaika wateule na wale walioasi, wako karibu nasi kwa kusudi la kuharibu makusudi yote ya Mungu na mpango wa Mungu kwa wanadamu wote. Tofauti na sisi viumbe hawa ni wa kiroho na hawafi, hawana uwezo kuoa, kuolewa.

 

Luka 20:36 Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa;lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo.”

 

Wakati shetani na mashetani wakiwa ni maadui wakubwa wa wanadamu, malaika wateule wao hufanya kazi kwa karibu na wanadamu na kuwahudumia wale watakaourithi wokovu

 

Waebrania 1:13-14 “Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wo wote, Uketi mkono wangu wa kuume Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako? Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?

 

Kama wote tunakubaliana na msimamo wa kimaandiko ya kwamba shetani aliumbwa kama mojawapo ya malaika ni Muhimu tukafahamu basi sifa kadhaa za malaika ambazo kimsingi hata shetani na majeshi yake wanazo.

 

·         Malaika ni roho ambao kimsingi waliumbwa wawepo milele, kwa sababu hiyo malaika hawafi, wataendelea kuwepo milele na milele, Maandiko yanatufundisha hivyo kuwa hawakuweko toka milele ni viumbe waliumbwa na Mungu wakati fulani lakini waliumbwa wawepo milele, kwa hiyo malaika wote wema au wabaya wanaendelea kuwepo milele, na ndio maana wako watu wanajiuliza kwa nini Mungu hamuui shetani? Jibu lake ni kuwa Mungu aliwakusudia malaika wawepo milele kwa hiyo wanaendelea kuwepo siku zote mpaka pale Mungu atakapomuhukumu shetani katika wakati ambao ameutenga yeye mwenyewe, kwa sababu Yesu anatutaarifu ya kuwa uko moto wa milele ambao Mungu ameuandaa kwaajili ya shetani na malaika zake. 

 

Luka 20:36 Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa;lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo.”

 

Mathayo 25:41 “Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;”

 

·         Malaika wana nguvu kimsingi malaika wana nguvu lakini hawana nguvu zote, yaani wana uwezo Fulani, kama jinsi ambavyo wanadamu wana uwezo Fulani na nguvu Fulani, lakini nguvu zao hazizidi za Mungu mwenye enzi na Nguvu zote Katika 2Wathesalonike 1:7 tunataarifiwa kuwa Yesu Kristo atarudi kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake neno uweza au malaika wa uweza wake kwa kiingereza linasomeka with his MIGHTY angels, ambalo kwa kiyunani ni DUNAMIS – ambalo maana yake ni ability, power, strength sawa na neno Uweza, Nguvu na mamlaka kwa hiyo utaweza kuona ya kuwa viumbe hao wana nguvu, ukilinganisha na wanadamu malaika ni askari ni majemadari ni wanajeshi na wanatajwa kuwa na ukuu, uwezo na nguvu na wenye uwezo wa kupigana au kupiga ni Hodari kwa kiingereza “Angels that excel in strength”  wana weledi mkubwa kivita ni majenerali. Malaika mmoja tu kwa mfano aliweza kupiga watu zaidi ya laki moja na themanini na tao elfu 185,000 ambao walikuwa askari wa majeshi ya waashuru

 

2Wafalme 19:35 “Ikawa usiku uo huo malaika wa Bwana alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia na themanini na tano elfu. Na watu walipoondoka asubuhi na mapema, kumbe! Hao walikuwa maiti wote pia.”  

 

2Wathesalonike 1:6-9 “Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi; na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake;

 

2Petro 2:11 “Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana.”

 

Zaburi 103:20 “Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake.”

 

Daniel 10:12-17 “Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi. Sasa nimekuja kukufahamisha mambo yatakayowapata watu wako katika siku za mwisho; maana maono hayo ni ya siku nyingi bado. Na alipokwisha kusema nami maneno hayo, nikauelekeza uso wangu chini, nikawa bubu. Na kumbe, mmoja mfano wa wanadamu akanigusa midomo yangu; ndipo nikafumbua kinywa changu, nikanena, nikamwambia yeye aliyesimama karibu nami, Ee Bwana wangu, kwa sababu ya maono haya huzuni zangu zimenipata tena; hata sikusaziwa nguvu. Maana, mtumishi wa Bwana wangu huyu atawezaje kusema na Bwana wangu huyu? Kwa maana kwangu mimi, mara hazikusalia nguvu ndani yangu, wala pumzi haikusalia ndani yangu.”

 

·         Malaika wana akili na hekima – 2Samuel 14:20b “…; na bwana wangu anayo akili, kama akili ya malaika wa Mungu, hata ajue mambo yote ya duniani.”       

 

Malaika wana akili na hekina na wanajua mambo na mafumbo kadhaa kwa kina na kwa ukamilifu wake kwa hiyo tunapojifunza kuhusu shetani ni lazima ukumbuke ya kuwa naye anazo sifa hizi, zote kama walivyo na malaika wengine kwa hiyo kamwe usifikiri unaposhughulika na shetani unashughulika na kitu tu cha kawaida hapana unashughulika na malaika mwenye uwezo mkubwa, akili nguvu na maarifa na ni rahisi kwake kukudanganya na kukuingiza mtegoni na kukupoteza na hata na hayuko hovyo katika utendaji wake, ana mpangilio mzuri wa kiserikali kisera, kiuchumi, na kiutendaji, huyu ndiye Lucifer ambaye leo tunachukua muda kujifunza habari zake.

 

·         Malaika wana utaratibu wa kiserikali – Kule mbinguni Bwana pia huitwa Bwana wa Majeshi, na uko ufalme mbinguni na iko serikali mbinguni na uko utaratibu mbinguni, katika mpangilio kama huo mfano malaika Mikael ambaye hujulikana kama malaika mkuu yeye pia ni mkuu wa anga la nchi ya Israel, maana yake anashughulika pia na ulinzi wa wayahudi

 

Daniel 10:13 “Akaniambia, Ee Danieli, mtu upendwaye sana, yafahamu maneno nikuambiayo, ukasimame kiwima-wima; maana kwako nimetumwa sasa. Na aliponiambia neno hili, nalisimama nikitetemeka. Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi.”

 

Daniel 10:20-21 “Ndipo akasema, Je! Unajua sababu hata nikakujia? Na sasa nitarudi ili nipigane na mkuu wa Uajemi; nami nitakapotoka huku, tazama, mkuu wa Uyunani atakuja.Lakini nitakuambia yaliyoandikwa katika maandiko ya kweli; wala hapana anisaidiaye juu ya hao ila huyo Mikaeli, mkuu wenu.”                

 

Waefeso 6:10-12 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.”

 

Maandiko yanatufahamisha kuwa mkao wa kishetani hauko hovyo, kuna mpangilio wa maswala mbali mbali ya kiutawala yaani Dola, neno falme, mamlaka, wakuu wa giza, na majeshi katika biblia ya kiyunani yanatajwa kama archē, - Chief (Magistrate power principality, principle rule) kuna utawala wa kimahakama, kuna jaji mkuu, waendesha mashitaka na mahakimu, kisha exousia – wenye mamlaka, kisha Kosmokratōr – watawala kwa kila nchi, mkoa, wilaya, taifa na mahali, Kratos – Dominion might Wakuu wa Dola au Himaya (empires)Mabara, au tawala kubwa zaidi ya nchi, Pneumatikos – viongozi wa kidini au kiimani, na epouranios – majeshi ya pepo wengi wabaya ambao ni ponēria wenye kuendesha ukatili na uovu au ubaya na kupanga utendekaji wa dhambi, kwa hiyo utendaji wa kimamlaka wa kishetani uko katika taratibu za kiserikali na kimamlaka na unatenda kazi katika mtiririko maalumu

 

Mafundisho kuhusu shetani.

 

Ni muhimu kufahamu kuwa Mafundisho kuhusu shetani na asili yake yanaonekana kuwa kama dhana flani hivi hasa kwa sababu ya matumizi ya maandiko yanayoonyesha asili ya Shetani, kuwataja wafalme halisi wa Babeli, na Tiro, jambo ambalo katika muktadha wa kibiblia ni kweli kabisa kuwa maandiko hayo yanaonekana kuwataja wafalme wanadamu wa Babeli na Tiro mfano

 

Isaya 14:12-15 “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu. Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo.”

 

Ezekiel 28:13-19 “Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama. Kwa wingi wa maovu yako, katika uovu wa uchuuzi wako, umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao. Wote wakujuao kati ya kabila za watu watakustaajabia; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele.”

 

Isaya 14:12-15 ni kifungu ambacho kimsingi kweli kinamzungumzia Mfalme wa Babeli, lakini katika uhalisia kifungu hiki kinatumiwa kwa kina katika lugha ya kinabii kwa undani kumuelezea shetani, kwa sababu ile roho ya kutaka kuabudiwa baada ya kuinuliwa na Mungu, na kuumbwa vema na Mungu na kufanikishwa na Mungu sasa roho hiyo haitaki tena kujinyenyekeza kwa Mungu na badala yake inataka ibada ielekezwe kwake maana yake ile tamaa na shauku aliyokuwa nayo mfalme kuwa atakiinua kiti chake juu kuliko Mungu na atakuwa kama Mungu Nabii anaiona sio tu kuwa ni roho iliyokuwa imemuathiri mfalme lakini ni ukweli kuwa mfalme alikuwa amepagawa na roho ambayo ni sawasawa na ile ile iliyomuathiri shetani kutukuka kwake mfalme huyu kulimfanya awe anajiona anang’aa kama nyota ya alfajiri (Lucifer) Je ni kweli kuwa katika Babeli mfalme alifikia ngazi ya kutaka kuabudiwa kama Mungu? Jibu ni ndio Je mfalme huyu aliyekuwa mtawala wa dunia nzima hakutumia kuinuliwa kwake kuwapotosha watu wote wa dunia waache kumuabudu Mungu aliye hai na badala yake waabudu miungu yake na sanamu yake aliyoisimamisha? Jibu ni ndio na ni kitu gani shetani huwa anakifanya hapa duniani?  je filimbi na ngoma na zumari na machezo zilikuwa zinaelekezwa wapi? Kwa Mungu aliye hai au kwa mungu wa Nebukadreza na sanamu yake?

 

Daniel 3:1-14 “Nebukadreza, mfalme, alifanya sanamu ya dhahabu, ambayo urefu wake ulikuwa ni dhiraa sitini, na upana wake dhiraa sita; akaisimamisha katika uwanda wa Dura, katika wilaya ya Babeli. Ndipo Nebukadreza akatuma watu kuwakusanya maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, ili wahudhurie wakati wa kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadneza aliyoisimamisha. Ndipo maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, wakakusanyika ili kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha; wakasimama mbele ya ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha. Ndipo mpiga mbiu akapiga kelele akisema, Enyi watu wa kabila zote, na taifa, na lugha, mmeamriwa hivi, wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, lazima kuanguka na kuiabudu sanamu ya dhahabu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha. Na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa saa iyo hiyo katika tanuru ya moto uwakao. Basi wakati huo, watu wa kabila zote walipoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, watu wote na mataifa na lugha wakaanguka, wakaiabudu ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha. Basi baadhi ya Wakaldayo wakakaribia, wakaleta mashitaka juu ya Wayahudi. Wakajibu, wakamwambia mfalme Nebukadreza, Ee mfalme, uishi milele. Wewe, Ee mfalme, ulitoa amri ya kwamba kila mtu atakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, ni lazima aanguke na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu; na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa katika tanuru ya moto uwakao. Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme. Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha?

 

Ezekiel 28:13-19  kifungu hiki hali kadhalika kinaelekezwa na nabii moja kwa moja kwa mfalme wa Tiro katika frikra nyembamba, Lakini katika fikra pana anazungumziwa Kerubi malaika wa ngazi ya juu sana aliyeumbwa kwa uhodari na ubora akiwa na hekima kubwa na uzuri lakini aliharibiwa kwa kiburi ambacho kimsingi ndicho kilichopelekea anguko lake ufafanuzi huu pia kama ulivyo ule wa Nyota ya Alfajiri katika Isaya na huuwa Kerubi mwenye kutiwa mafuta moja kwa moja katika fikra pana unamzungumzia shetani ambaye ndiye kimsingi aliwapagaa wafalme hawa kutaka kuabudiwa kama Mungu, kwa hiyo katika mtazamo mwembaba wanazungumzwa wafalme wa Tiro, na Babeli, Lakini katika mtazamo mpana anazungumzwa shetani na utendaji wake ambao uliwaathiri wanadamu hawa wafalme

 

Ezekiel 28:2 “Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari; lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu.”

 

Wakati ni kweli vifungu hivyo vinawazungumzia wafalme wanadamu waliotawala Babeli na Tiro, Lakini ni ukweli ulio wazi kuwa dhambi zao na kuzama kwao katika haribiko la kiroho uliruhusu wao kwenda ndani zaidi na manabii wanawaona katika ulimwengu wa roho wakifanya dhambi sawa tu na ile aliyoifanya shetani, waliangukia katika mtego wa ibilisi, walijawa na kiburi, sawa tu na kile alichokuwa nacho shetani, walijiona ni nyota ya alifajiri na walijiona ni makerubi, kwa hiyo kwa jicho la kinabii Mungu anawaona wafalme hao kuwa wamefikia kiwango cha juu cha dhambi sawa na ile aliyoifanya shetani na ndio maana kwa miaka mingi vifungu hivi vimekuwa vikitafasiriwa na wanatheolojia wa kiyahudi na Kikrsto ya kuwa vinamzungumzia shetani hasa kwa sababu manabii waliweza kuona mambo yaliyopo, yaliyopita na yajayo, kwa hiyo wakati manabii wakitangulia kuwaonya wafalme hao wanazungumza pia katika wakati uliopita wakitafakari au kuunganisha maonyo yao na kile alichokuwa amekifanya na kikampata Lucifer mwenyewe kwa hiyo vifungu hivi ndio vinavyokubalika kutupa historia iliyojificha kuhusu anguko la Shetani na sababu zake.  

 

Mungu hatakuja kuvumilia hata siku moja mtawala mwanadamu, kujitukuza na kujiinua kama Mungu au kutaka kuwaongoza watu na kuwapotosha wamuache Mungu aliye hao hayo kimsingi yanaweza kufanywa na Shetani na mara kadhaa amezitumia serikali au wafalme wakubwa na wenye nguvu duniani kuwalazimisha watu kufanya maovu, na hii ndio kazi ya shetani, endapo mfalme mwanadamu atafanya kama hayo atashushwa hata kuzimu mara moja 

 

Ufunuo 13:13-15 “Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu.Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya mbele ya huyo mnyama, akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi.Akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama, hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe.”

 

Matendo 12:21-24 “Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho. Neno la Bwana likazidi na kuenea.”

 

Ushawishi huu wa wafalme na watawala na wenye mamlaka na wanadamu kuwa na dhana ya kujifikiri kuwa wao ni Mungu, kwa asili inatoka kwa shetani, kwa hiyo maonyo kwa wafalme wa Babeli na Tiro wanayoonywa kuwa yatawapata manabii walitumia kuwa hukumu ile itakayowapata itakuwa sawa tu na ile iliyompata aliyewashawishi wanadamu kutaka kuwa kama Mungu tangu mwanzo ambaye kimsingi ni shetani, wapi wanadamu wanatoa au kupokea ushawishi huu wa kutamani kuwa kama Mungu? Ni kwa mwanzilishi wa uovu huo ambaye ni shetani!

 

Mwanzo 3:1-5   Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

 

Kwa hiyo unaweza kumuona shetani katika picha ya kiburi na ubora kuwapitia viongozi wa dunia wasio mcha Mungu na namna na jinsi wanavyojiinua kinyume na Mungu, tumekwisha kujifunza sifa za malaika ambazo kimsingi shetani pia anazo, lakini ni vema pia tukaangalia na kumchambua shetani ni nani na alivyo na hali yake kibinafsi namna ilivyo ni kiumbe wa namna gani hasa?

 

1.       Jina lake: Katika maandiko jina analopewa mtu au kiumbe huwa linafunua na kuelezea uhalisia wa jinsi na namna mtu huyo alivyo, hii ni hali ya kawaida ukitaka kumjua Mungu, Bwana Yesu na Roho Mtakatifu utaweza kujua kupitia majina anayopewa katika maandiko, hali kadhalika tunapojifunza somo kuhusu Lucifer au shetani leo tutapitia pia majina yake ili tuweze kupata picha na kujihoji ni kwanini shetani ameitwa namna hiyo:

 

a.       Shetani - Jina shetani kwa kiibrania ώâtân kiingereza Adversary – “the arch enemy of good” katika Kiswahili ni shetani yaani adui wa mema neno hili limetumika mara 19 katika Biblia ya kiingereza ya KJV kazi yake ni kuharibu kila mpango mwema ambao Mungu ameukusudia katika jamii ya wanadamu, ukiacha ya kuwa aliwaharibu wanadamu, lakini pia alikuwa anataka kuharibu mpango wa Mungu wa ukombozi kupitia mwanamke kwa kutaka kuua uzao wa mwanamke ili kumuua masihi na kuacha hai wa kwake

 

Mwanzo 3:14-15. “BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.”

 

1Yohana 3:11-12 “Maana, hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi; si kama Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya, na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.”

 

Shetani ni mpinzani na adui wa kila mpango mwema wa Mungu uliokusudiwa katika maandiko, anapambana katika ulimwengu wa roho akiratibu kila kitu kinachoonekana katika ulimwengu wa mwili, alikusudia kuwaharibu wanadamu wote wakaao juu ya uso wa nchi, alikusudia kuwaharibu, wana wa Israel kwa kuwatumikisha huko Misri kupitia Farao, alikusudia kumuangamiza Yakobo kupitia Esau, hata leo anachukizwa na uwepo wa taifa la Israel na anatumia mataifa adui, kutamani au kutaka kuifuta Israel ili kuharibu Historia ya Mungu na mpango wake wa baadaye wa utawala wa Masihi, na anachukizwa na kanisa na anatumia kila mbinu kutaka kuliangamiza, na kama yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomuudhi yule aliyezaliwa kwa roho ndivyo ilivyo hata sasa.

 

Wagalatia 4:29 “Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa.”

 

Shetani amekuwa akishambulia kila kilicho cha Mungu na kutaka kukiangamiza kabisa, analishambulia kanisa kupitia njia ya mateso na njia ya mafundisho ya uongo, ana watu wake kama jinsi ambavyo Mungu ana watu wake, wako wanaofanya kazi upande wake akiwatumia kama Mungu anavyotumia watu wake wanaofanya kazi upande wake, kwa bahati mbaya watu wengi hawajui kuwa shetani ana watu wake duniani, wanafikiri kuwa kila mtu ni mwema na hawachukui tahadhari kwa sababu hawajui!

 

1Timotheo 4:1 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;”

Mathayo 13:38-39 “lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika.”

Ufunuo 2:10 “Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.”

b.      Ibilisi – Shetani anaitwa ibilisi au yule joka la zamani, jina ibilisi  kwa kiingereza Devil kwa Kiyunani  “diabolos” ambalo kiingereza tafasiri yake ni false accuser, au slanderer kwa Kiswahili ni Mshitaki kwa hiyo jina ibilisi linatumika sana akiwa anafanya kazi ya kuwashitaji wateule wa Mungu, kila mtu wa Mungu shetani humtafuta kwa udi na uvumba apate jambo la kumshitaki, Shetani humshitaki Mungu kwetu na kutushitaki sisi kwa Mungu, kama u mwema atafanya kila aliwezalo kuhakisha kuwa anakuchafua anawaaminisha watu kuwa wewe hufai, atakushambulia kutoka ndani na nje kuhakikisha kuwa unaonekana hufai hasa kama una kitu cha Mungu ndani yako, shetani atakushitaki au atasimama kama mwendesha mashitaka kuhakikisha hukubaliki kwa Mungu na kwa wanadamu, ili kupingana na kitu cha kiungu kilichomo ndani yako au kumshawishi Mungu aachane na mpango wake juu yako.

 

Mwanzo 3:2-5Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”    

 

Ufunuo 12:9-10 “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.”

       

Ayubu 1:8-11 “Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.”

       

Zekaria 3:1-2 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye.Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni?

 

1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”

 

c.       Mharabu au mharibifu – Shetani anaitwa Mharabu, kwa kiyunani ni “Apollyon” apolioni na kwa kiebrania ni “Abaddon” abadoni hii inadhihirisha hasira kubwa sana aliyonayo na chuki dhidi ya Muumba na kazi yake, na mipango yote ya Mungu yeye anabainishwa kama muharibifu naye amejiweka kwa kazi hiyo

 

Ufunuo 9:9-11 “Nao walikuwa na dirii kifuani kama dirii za chuma. Na sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya magari, ya farasi wengi waendao kasi vitani. Nao wana mikia kama ya nge, na miiba; na nguvu yao ya kuwadhuru wanadamu miezi mitano ilikuwa katika mikia yao. Na juu yao wanaye mfalme, naye ni malaika wa kuzimu, jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani analo jina lake Apolioni.”

 

Yohana 10:10-11 “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.”

 

d.      Nyoka au Joka – Shetani anaitwa nyoka hivyo katika maandiko kama nembo ya kumbukumbu ya yale aliyoyafanya zamani yaani kwa wivu wake na uharibifu wake kuleta anguko kwa mwanadamu kwa kujibadilisha au kujivika umbo la nyoka, lakini pia kama neno ya werevu na hila au ujanja wake alionao

 

Ufunuo 12:9-10 “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.”

 

Mwanzo 3:1-5 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

 

e.      Mjaribu – Shetani anaitwa mjaribu,  kwa sababu ndiye chanzo cha majaribu yote yenye ushawishi wa kuwafanya watu watende maovu kwa Mungu kwa mtindo wa kuwaonea, ni kazi yake kuwajaribu watu na kuwatia katika udhaifu na kuwashawishi wamkosee Mungu, majaribio anayoyatoa shetani ni kuhakikisha anakuoenea ili kuangalia uwe mwaminifu au usiwe mwaminifu kwa Mungu, hakuna mwanadamu wa ngazi yoyote ile ambaye shatani ataacha kumjaribu, shetani anatumia ushawishi, mvuto, uchochezi, na wakati wote anakudanganya kuwa unaweza kufanya dhambi bila kupata madhara ilihali dhambi ina madhara makubwa sana katika maisha ya mwanadamu, Mjaribu kwa kiingereza Tempter kwa kiyunani “Peirazō” sawa na neno “scrutinizer” – a person who examines something with great care or investigator who observes carefully hii maana yake ni nini shetani ni mjaribu ambaye anatumia akili sana ni mwangalifu katika jambo analolifanya ni mjanja mno kama mwindaji anavyotega mtego wa kukamata ndege au paa kwa hiyo unahitaji kuwa na hekima sana kujichomoa kutoka katika mitego ya adui,

 

Mathayo 4:1-3 “Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi. Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa. Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.”

 

Mithali 6:4-5 “Usiache macho yako kupata usingizi, Wala kope za macho yako kusinzia.Ujiponye kama paa na mkono wa mwindaji, Na kama ndege katika mkono wa mtega mitego.”

 

f.        Mdanganyifu – Ni muhimu pia kufahamu kuwa shetani anaitwa mdanganyifu kwa sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na maneno na matendo na mafundisho yake  kama inavyofundishwa katika maandiko, uongo ndio moja ya silaha yake kubwa sana anayoitumia akitumia akili, hila na ujanja mkubwa sana katika kuhakikisha anafanikisha kazi yake hiyo.

 

§  Alimdanganya Hawa – Mwanzo 3:1-5 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa,kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”

 

§  Hupotosha ukweli -  Shetani ni mtaalamu wa kupotosha ukweli na kuufanya uonekane uongo na uwongo uonekane kama kweli, shetani ana mafundisho yake ambayo huyatumia kuliharibu kanisa kwa kutumia mafundisho ya uongo na roho zidanganyazo

 

1Timotheo 4:1-5 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.”

 

§  Hujaribu kuficha ukweli kuhusu Mungu – Shetani siku zote atajaribu kuuficha upendo na rehema na fadhili za Mungu kwa wanadamu, siku zote atawafanya wanadamu waamini ya kuwa Mungu ni mkali, mwenye kuhukumu na hajali kuhusu maisha ya wanadamu, ndio maana watu wengi nyakati za agano la kale kila walipopatwa na mabaya walidhani Mungu ndiye anayesababisha hayo, hii ni kwa sababu shetani hujaribu kumshitaki Mungu kwetu ili yamkini sisi nasi tuweze kujenga chuki kwa Mungu na kumuona Mungu kama asiyetenda haki asiyejali na katili kwa watu wake aliowaumba yeye mwenyewe.

 

Ruthu 1:19-21 “Hivyo hao wakaendelea wote wawili hata walipofika Bethlehemu. Na ikawa walipofika Bethlehemu, mji wote ulitaharuki kwa habari zao. Nao wanawake wakasema, Je! Huyu ni Naomi?Akawaambia, Msiniite Naomi niiteni Mara,kwa sababu Mwenyezi Mungu amenitenda mambo machungu sana,Mimi nalitoka hali nimejaa, naye Bwana amenirudisha sina kitu, kwani kuniita Naomi, ikiwa Bwana ameshuhudia juu yangu, na Mwenyezi Mungu amenitesa?

 

Mwanzo 16:1-2 “Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri.Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai.”

 

1Samuel 1:1-6 “Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea Bwana wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa Bwana, walikuwako huko.Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, waume kwa wake, sehemu zao; lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo. Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo.”

 

Ayubu 1:16 “Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.”

 

§  Hujaribu kututenganisha na Mungu – Lengo lingine la shetani ni kuhakikisha anatumia kila aina ya mbinu anayoweza kututenganisha na Mungu, anatumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mashaka, hofu, kukata tamaa, dhambi, na tamaa ili kufanikisha tuwe mbali na Mungu, Shetani anajua wazi kuwa usalama wetu uko kwa Mungu na kuwa akifanikiwa kututenga na uwepo wa Mungu anaweza kusababisha madhara makubwa kwa wanadamu.

 

1Nyakati 21:1-3 “Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Israeli.Basi Daudi akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni kawahesabu Israeli toka Beer-sheba mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao. Naye Yoabu akasema, Bwana na awaongeze watu wake mara mia hesabu yao ilivyo; lakini, bwana wangu mfalme, si wote watumishi wa bwana wangu? Mbona basi bwana wangu analitaka neno hili? Mbona awe sababu ya hatia kwa Israeli?

 

§  Hujaribu kuwafanya watu waamini uongo – anatoa matumaini hewa na kupotosha ukweli kuhusu Maisha, furaha na mafanikio, anatufanya tuamini ya kuwa tunaweza kuwa na furaha katika vitu vya dunia badala ya uhusiano na Mungu.

 

2Wakorintho 11:14-15 “Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.”

 

2Wakorintho 11:3-4 “Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo. Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye!                    

 

g.       Mkuu wa ulimwengu huu, Mungu wa dunia hii – Shetani anaitwa hivgio Mungu wa dunia hii katika maana ya kuwa kwa sasa ni mtawala wa dunia hii, lakini Mungu ambaye ni mtawala wa yote amemuwekea mipaka, hakuna anachoweza kukifanya bila Mungu kuruhusu au kunyamaza kimya, ni kama tu vile alipozungumza na Mungu kuhusu Ayubu kuna mipaka Mungu alimuwekea shetani.

 

2Wakorintho 4:3-4 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”

 

Yohana 12:31 “Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.”

 

Waefeso 2:1-2 “Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;”

 

1Yohana 5:19 “Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu.”      

 

Tangu baada ya anguko la mwanadamu ambaye ndiye aliyepewa na Mungu kuutawala ulimwengu huu na vyote viujazavyo, Shetani aliweza kuwa na nguvu ya kimamlaka ya kutawala ulimwengu na kuingiza mawazo, elimu, falsafa, na utaratibu mzima wa kuhakikisha kuwa anaitawala dunia kwa kutumia uwongo bila wanadamu kuelewa akitumia hila na ujanja wa hali ya juu kuhakikisha kuwa wanadamu hawaijui njia ya Mungu kwa usahihi, kwa hiyo usidhani wala kufikiri kuwa kila kitu duniani hata kinachoonekana kuwa kina ukweli ni kweli, shetani anatumia malengo na mitazamo na wakati mwingine mitazamo ya wengi, biashara na kuweka mifumo ambayo kamwe haitaruhusu watu kujali kitu kuhusu Mungu.

 

Shetani sio mtawala wa ulimwengu mzima kwa ukamilifu wake, Mungu ndiye anayetawala lakini yeye kama mkuu wa anga ameachiliwa na Mungu kufanya kazi chini ya mipaka Fulani, wakati ikisubiriwa siku ya hukumu yake kamili kwa hiyo ana mamlaka katika ulimwengu lakini chini ya udhibiti wa Mungu.

 

Ayubu 1:7-12 “Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako. Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana.”

 

Aidha ni muhimu kufahamu kuwa shetani ana utaratibu, wa kiserikali wenye kila kitu na mengi akiwa ameyaigiza kutoka mbinguni kwa Mungu, isipokuwa tu anauweka utaratibu wake utende kazi kijanja sana kwa kusudi la kuwanasa na kuwashika wanadamu ili yamkini waweze kupotea na kwenda naye wakati wa hukumu katika lile ziwa liwakalo moto aliloandaliwa yeye.

 

 

Uwezo na utendaji wa shetani

 

Baada ya kuwa tumejifunza mafundisho kuhusu shetani sasa ni muhimu kwetu kuangalia uwezo na utendaji wa shetani yaani sifa zake na utendaji wake, tunaweza kumuelewa vizuri zaidi kwa kuangalia uwezo wa utendaji wake, lengo kubwa sio kumtukuza lakini lengo kubwa ni kuelewa kuwa Msaada wetu ni katika bwana na Mungu ndiye anayetusaidia tunapokuwa tunamshinda adui shetani ni lazima tuelewe kuwa ni kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

 

1.       Shetani ana akili – Watu wengi sana wanafikiri kuwa shetani ni kiumbe kisicho na akili na kinachokurupuka tu lakini maandiko yanamuelezea shetani kuwa ana akili “He has intelligence” intelligence maana yake kwa kiingereza the ability to acquire and apply knowledge and skills yaani ni ana uwezo wa kuelewa na kutumia akili zake au maarifa yake kwa usahihi na ustadi mkubwa

 

2Wakorintho 2:11 “Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.”

 

Maandiko yanamuonyesha shetani kuwa ana FIKRA neno fikra katika lugha ya kiyunani linatumika neno noēma ambalo maana yake ni the intellect disposition yaani ni mwenye weledi katika kutumia akili, elimu na mbinu nyingine kwa uangalifu mkubwa na kwa bidii, pia ana mbinu, Stategic plans (Mpango mkakati) kwa msingi huo kama ni mikakati vita shetani angependa sana kutumia vita laini sana ya kukuzidi fikra na kukunasa hata bila wewe kujielewa, kwa hiyo ili kumshinda shetani watu wa Mungu hawana budi kujiandaa na kujipanga kwa sababu sasa unajua ni aina gani ya adui ambaye unakwenda kukabiliana naye, wakati wote tunapaswa kujifunza kuwa hodari kwa sababu tunayekwenda kupambana naye ni Hodari na mjuzi wa vita

 

Waefeso 6:10-11. “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.”

 

Matumizi ya akili kubwa ni moja ya silaha yake kubwa sana anayoitumia bila kujali wewe ni wa rohoni kwa kiwango gani, anauwezo wa kuisoma akili yako na kukuharibu na kukuharibia hata kabla hujafikiri, vita zake nyingi sana hutumia akili na uongo au hila na kwa hila anaweza kukusababishia madhara Shetani anatajwa tangu mwanzo kuwa alikuwa mwerevu, kuliko hayawani wote walioumbwa na Mungu

 

Mwanzo 3:1 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?

 

Neno hilo mwerevu katika lugha ya kiibrania ni ârûm ambalo kwa kiingereza ni cunning, au subtil, au prudent au crafty yaani ni mjanja, mwerevu, mwenye kutumia busara, na msanii mkubwa, kama umewahi kuwachunguza wachawi, waganga, wanamazingaombwe na matapeli, majambazi, makahaba, na kama umewahi kutapeliwa utaelewa akili kubwa walizonazo au wanazozitumia waganga utaweza kuona kuna ujanja mwingi, lugha nzuri, na akili kubwa sana wanayoitumia kuiongoza akili yako mpaka wakutapeli au uweze kuamini, kwa hiyo utapeli ni moja ya kazi kubwa na mbinu kubwa sana anayoitumia shetani ndio maana anaitwa muongo na baba wa uongo yaani mwanzilishi wa uongo wote.

 

Ufunuo12:9 “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani,audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.”

 

Shetani anaweza kujua atamalizana nawe vipi hata baada ya miaka kumi ijayo, anaweza kushughulika na wewe katika mtindo ambao hautakuja ugundue kuwa uko vitani, na mbinu hizi hizi wanazo watumishi wake wote anaowapagaa kutekeleza mpango wake huu, kumshinda shetani lazima uwe na akili sana ujue fikra zake. Na akili hizo na maarifa hayo utayapata kwa kusoma neno la Mungu na kuelewa kwa msaada wa Roho Mtakatifu, Shetani haogopi dini yako, haogopi unashika vipi maandiko, haogopi wewe uko katika ngazi ya ukuhani mkuu, haogopi umaalumu wako na hatakuja kwako katika njia utakayogundua kuwa amekuja. Atajaribu kwa kiwango kikubwa kuharibu, kubomoa, kuchelewesha, kuzuia, na kusimamisha huduma yako na ukristo wako kama unataka kukataa jiulize wale mafarisayo washika dini waligeukaje kuwa wana wa Ibilisi? Ilihali walikuwa washika dini? Jiulize hawa wana wa Ibrahimu, hawa washika maandiko, hawa washika dini, ni lini na ilikuwaje wakawa wana wa ibilisi? Na je hawakumuua Yesu? Je hawakupingana na kweli ya Mungu? Je hawakumsingizia Yesu uongo mbele ya Pilato? Je hawakumuwekea vikao vya majungu na kutafuta namna watakavyomuangamiza? au wadhani Yesu alikuwa anasema uongo kuwa wao wamekuwa wa ibilisi? Na wanatekeleza mapenzi ya baba yao ibilisi? Shetani anatumia akili ona

 

Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo

 

2.        Shetani analijua neno – Wakati anamkabili Yesu Kristo alipokuwa katika mlima wa majaribu, tena akiwa amefunga siku 40 usiku na mchana yaani Yesu akiwa kiroho kweli kweli akiwa amejaa Roho Mtakatifu na unajua Yesu alikuwa amejaa neno la Mungu pia na alikua anajua kulitumia kwa usahihi, Shetani alicheza na maandiko pia alipokuwa akimjaribu bwana Yesu

 

Mathayo 4:5-7 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.”

 

Unaona wakati akimjaribu Yesu Shetani alinukuu andiko kama lilivyo, je unadhani alikuwa na biblia mkononi? Je unadhani alikuwa na simu, au tablet au computer bila shaka alinukuu kutoka kichwani, hii maana yake ni nini Shetani amejaa neno la Mungu, sijui wewe umejaa neno kwa kiasi gani lakini elewa ya kuwa shetani analijua neno na ameweka katika kichwa tu we hauogopi? Huoni kuwa ni jambo la kutisha kama huna bidii katika kujifunza neno la Mungu, yeye amelishika na ni kwa sababu gani? Ni ili aweze kulitumia wakati wowote na mda wowote autakao, anayajua maeneo yote ya udhaifu wako, anayajua maeneo yote yenye udhaifu katika ndoa yako, anayajua maeneo yote ya dhambi zako anakumbuka kila kitu kiovu ambacho umewahi kukifanya na anauwezo wa kumkumbusha Mungu yale uliyoyafanya wakati wa kukushitaki, anajua wakati gani una nguvu na wakati gani umechoka, alimjia Yesu wakati anasikia njaa, kwa hiyo anakujua ni wakati gani utampinga na ni wakati gani utamlegezea na atapata ushindi, katika kumjaribu Yesu sio kuwa aliishia pale maandiko yanasema alimuacha kwa muda, hii maana yake alimjia tena na tena mara nyingine, shetani atakucheki mara kwa mara taratibu tu wala hana haraka na wewe.

 

Luka 4:13 “Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.”

 

3.       Shetani ana maarifa -     ni muhimu kuelewa ya kuwa shetani anajua na ana maarifa ni mwelewa neno maarifa katika kiebrania linatumika neno “yādha” na “da’ath” ambalo katika kiyunani ni “oīda”  na “ginōskō” yaani “knows” and “to know fully”  kwa hiyo shetani sio kuwa ana maoni au mawazo anajua na anauelewa mpana sana ana maarifa, anajenga hoja, ana uwezo wa kufikiri, anachunguza na kuelewa kwa hiyo anamjua kila mtu duniani, anajua Baraka zako, anajua nguvu yako na anajua apige wapi ili akuharibu kiimani, ana namna ya maarifa anajua afanye nini kwako na asirudie tena na awe amekupata!

 

Ufunuo 12:12 “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”

 

Ayubu 1:8-11 “Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.”

 

Ayubu 2:3-6 “Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake, ujapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize pasipokuwa na sababu. Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake. Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako.Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake

 

Unaweza kuona shetani alikuwa anamjua Ayubu, alikuwa amemsoma na kujua kila kitu alichokuwa nacho, anajua aguse wapi na kutokee nini unaona, anajua wewe ukinyimwa tendo la ndoa, nini kitatokea, anajua wewe ukiwa na cheo nini kitatokea, anajua wewe ukiwa masikini nini kitatokea, anajua wewe ukiwa mgonjwa utaenda kwa mganga, anajua wewe ukitegeshewa hela utaiba, anajua wewe mumeo akiwa dhaifu utazini, anajua mumeo akiwa mzinzi utakimbia ndoa, anajua hasira yako, anajua wivu wako, anajua tamaa yako na anajua taratibu namna na jinsi anavyoweza kukuleta katika dhambi, anajua namna na jinsi anavyoweza kukufanya dhaifu kwa nini kwa sababu anajua na ana maarifa ya wewe ni nani, na afanye nini aguse kipi ili kuyababaisha maisha yako, kwa hiyo haogopi maombi yako, wala ujuzi wako kuhusu neno na anajua namna ya kukunasa katika dhambi na wala humpi shida anaweza kukupa hata kiburi tu ukajiona wewe ndio wewe kama mafarisayo kumbe wameshakuwa watoto wa ibilisi siku nyingi bila kufanya dhambi.               

 

4.       Shetani ana mapenzi yake -  kama jinsi ambavyo Mungu ana mapenzi yake na wakati mwingine tunaomba kuwa mapenzi yake yatimizwe hapa duniani kama huko mbinguni, ni muhimu kufahamu kuwa shetani naye ana mapenzi yake na huenda akataka yatimizwe hapa Duniani, na yatimizwe wakati mwingine hata na watu wa Mungu aliowanasa katika mtego wake.

 

2Timotheo 2:24-26 “Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli; wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.”        

 

Isaya 14:12-14 “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu.”

 

Kwa hiyo unaweza kuona na kugundua mapenzi ya ibilisi, kuinua kiti chake kuliko cha Mungu, kuketi juu ya mlima wa mkutano, kupaa juu kuliko Mungu na kufanana na aliyejuu, kwa hiyo yuko tayari kuharibu lolote linalompa Mungu utukufu, yuko tayari, kuharibu mpango wa Mungu juu yako na yangu, chochote ambacho Mungu amekijenga ndani yetu mpango wake ni kukuharibu na kufutilia mbali programu zote za kiungu zilizoko ndani yako na kuweka zake, na hali kadhalika mpango wowote wa ibada ya kweli unaomwelekea Mungu.

 

5.       Shetani hana sura mbaya -  Ni muhimu kuwa na ufahamu katika hali ya kawaida tu hakuna mahali tunaelezwa ya kuwa shetani ni mweye sura mbaya, au ana mapembe kama tunavyoweza kuona katika michoro mbalimbali, ni kweli alikataliwa na ni kweli alifukuzwa katika uwepo wa Mungu na matendo yake ni mabaya lakini hata hivyo hii haimaanishi kuwa ana sura mbaya liko swali liliwahi kuulizwa ni kwanini watu humuonyesha shetani au kumchora shetani akiwa na sura mbaya sana na likajibiwa hivi kwa lugha ya kiingereza “Because it’s human nature to venerate beauty, and denigrate ugliness. If we were to portray the Devil as beautiful, then people might feel more inclined to venerate the Devil. Sadly, in endorsing the denigration of ugliness the church has led us astray away from the calling of Christ.” Tafasiri isiyo rasmi tafasiri yangu “kwa sababu ni asili ya mwanadamu kuheshimu uzuri na kudhalilisha ubaya. Ikiwa tungemuonyesha ibilisi kuwa mrembo basi huenda watu kuwa na muelekeo wa kumuabudu ibilisi na kumkubali, lakini cha kusikitisha ni kwamba  katika kuunga mkono na kudharaulika kwa ubaya kanisa limepotiosha ukweli kuhusu shetani mbali na wito wa Kristo” kwa majibu haya tunakubaliana ya kuwa ubaya wa sura ya shetani umetiwa chumvi jambo ambalo kikristo haliko sahihi.

 

6.       Shetani ana matakwa – Shetani ana matakwa kwaajili yetu anatamani kututumia, anatamani kutushinda, ana tamani kutuharibu, anatamani kutudanganya, anatamani kutuua, anatamani kutukomesha, anatamani kututoa nje ya mstari wa Mungu, anaweza kutuzuia tusimtumikie Mungu katika njia inayoonekana kuwa inakubalika, tamu, au njia sahihi, njia ya kistaarabu sana na ya kawaida au yenye sababu zinazokubalika, anaweza kuzuia na anaweza kuchelewesha, anaweza kupinga na anaweza kushambulia kwa matakwa yake

 

Luka 22:31 “Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.”

 

1Petro 5:8-9 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.”

 

Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo

 

7.       Shetani ana kiburi – Shetani ana kiburi, hii ndio dhambi yake ya kwanza na kubwa iliyosababisha akafukuzwa mbinguni, shetani anaposhindwa kukupata katika maeneo mengine yote sindano muhimu atakayoitumia ili unajisikie ni kiburi, kwa kuwa Shetani alikataliwa kwa sababu ya kiburi, njia ya kukubalika kwa Mungu ni unyenyekevu, kama njia ya kushusha ni kiburi basi njia ya kupandishwa juu ni unyenyekevu

 

Ezekiel 28:17 “Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.”

 

Wafilipi 2:5-9 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;”

 

Shetani anatamani tuwe kama yeye, tuwe na kiburi, wakati wowote kama kuna jambo ambalo sisi wakristo tunapaswa kujihami nalo ni pamoja na kiburi, kiburi kinaweza kuharibu kila kitu tulicho nacho ikiwa ni pamoja na utumishi wetu. Na ndio maana maandiko yanatuonya kuwa makini tusijivune na kuanguka katika hukumu ya ibilisi yaani kukataliwa.

 

1Timotheo 3:6 “Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.”

               

8.       Shetani ana hasira –  Tofauti na utendaji wa kiungu ambao unasukumwa na upendo katika kumuokoa mwanadamu, shetani anasukumwa na uchungu, hasira kali sana au hasira kubwa sana, hasira iko moyoni mwake, ana ghadhabu kubwa sana nah ii ndiyo inayomsukuma kwa uchungu mkubwa kushambulia watu.

 

Ufunuo 12:12 “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”

 

Neno Hasira au ghadhabu nyingi katika kiingereza great wrath, kwenye biblia ya kiyunani neno linalotumika hapo ni “thumos” ambalo tafasiri yake ni “fierceness”, yaani forceful and aggressive maana yake anasukumwa na uchungu mwingi sana kwa hiyo hata kama humuoni shetani akitumia nguvu fahamu tu moyoni mwake ana uchungu na wewe na mimi, anachukizwa na sisi sana, Hasira hii anayo siku zote uchungu huu anao siku zote kwa hiyo shetani hafanyi jambo kwa kukuhurumia ataendelea hivyo mpaka mwisho, kwa msingi huo kwa kadiri tunavyoendelea kutembea na Mungu na kumtumikia yeye anachukizwa sana na ana uchungu mno na wewe na mimi na kila kitu tulicho nacho. Jambo kubwa la kumshukuru Mungu ni kuwa tunalindwa na nguvu za Mungu. Kumbuka kila anachokifanya shetani anafanya akisukumwa na chuki na hasira na uchungu, tushukuru tunalindwa na nguvu za Mungu na malaika zake wapo.

 

9.       Shetani ni mwenye nguvu -  angetamani sana atujaze kwa nguvu zake ili tuyatende mapenzi yake, na anatoa nguvu Fulani kwa watu wake katika kuhakikisha kuwa wanayatimiza mapenzi yake sawa tu na namna Mungu anavyotujaza Roho wake Matakatifu tuwe mashahidi wake yeye anaweza kushusha aina Fulani ya ushawishi au nguvu kwa mtu au chochote ili kutimiza mapenzi yake anawapa nguvu ya uponyaji waganga, anawapa nguvu ya kudhuru wachawi, anawapa ushawishi matapeli, anawapa ujanja, mbinu na mvuto makahaba na kadhalika anaweza kutoa uwezo mwingi kwa watumishi wake ili kutekeleza matakwa yake duniani.

 

Ufunuo 13:1-4 “Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru. Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi. Nikaona kimoja cha vichwa vyake kana kwamba kimetiwa jeraha la mauti, na pigo lake la mauti likapona. Dunia yote ikamstaajabia mnyama yule. Wakamsujudu yule joka kwa sababu alimpa huyo mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule mnyama, wakisema, Ni nani afananaye na mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye?

 

10.   Shetani ni Nafsi – Shetani ni nafsi iliyo hai na halisi, (Person) maandiko yanavyomuelezea hayaelezei kama dhana au nguvu fulani, yanamuelezea kama “MTU” hapa namaanisha nafsi iliyo hai na halisi kwa hiyo maandiko yanampa nafsi na ni nafsi kweli sio nguvu hasi hii ni kwa sababu ziko dhana za falsafa fulani duniani ambao huamini kuwa ziko nguvu mbili zinazoongoza ulimwengu yaani nguvu hasi na nguvu chanya, au nguvu njema na nguvu mbaya kama wanavyoamini wabudha (yin yan) nguvu chanya au njema ikiwa ni Mungu na nguvu hasi na mbaya ikiwa ni Shetani, maandiko hayakubaliani na dhana hiyo na badala yake yanatuthibitishia kuwa ni nafsi na kama nafsi ina sifa zifuatazo kujidhihirisha

 

a.       Anazungumza – Ayubu 1:6-12 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako. Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana.”

 

Kama shetani anaweza kuzungumza ni wazi kuwa pia hutoa maagizo kwa watumishi wake ana uwezo wa kuwasiliana, kuamuru, kuagiza na kutekeleza maswala kadhaa katika maisha ya ulimwengu wa roho na kupitia maajenti wake duniani

 

b.      Anaweza kumjia mtuMathayo 4:3-11 “Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate. Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.”

 

Shetani kama nasfi inaweza kumjilia mtu au kumtokea mtu, na kufanya mazungumzo hii inadhihirika wakati huu ambapo shetani alimtokea Yesu na Yesu alizungumza naye kihalisia na kuchukuliana naye kwa uangalifu mkubwa sana na hekima kubwa kwa hiyo tunajifunza ya kuwa shetani sio nguvu pinzani bali ni mpinzani wa Mungu na wanadamu au watu wa Mungu na ya kuwa ikiwa Yesu alimchukulia kwa tahadhari kubwa sana sisi nasi hatuna budi kumchukulia kwa tahadhari kubwa zaidi

 

c.       Anaelezewa kama Nafsi – Waandishi wa neno la Mungu karibu wote hawajawahi kumuelezea shetani kama nguvu hasi bali wanamuelezea kama nafsi kiumbe halisi na matamko yake yako hivyo hivyo

 

Zekaria 3:1-2 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni?        

 

Yakobo 4:6-7 “Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.”

 

Ufunuo 20:1-7 “Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache. Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu. Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu. Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu. Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake;”

 

d.      Anatajwa kuwa ana moyo na ni mzuri sana kwa kuumbwa -  Maandiko hayajawahi kumuelezea shetani kama kiumbe kibaya, japokuwa alimuasi Mungu, ana kiburi, ni muasi lakini Luciferi hajaharibiwa kuwa na sura mbaya na mapembe au kuwa mweusi na kama vile watu wanavyomchora, shetani alikuwa mzuri sana na ni uzuri wake pia uliochangia kiburi chake na anguko lake, ni hekima yake iliyochangia majivuno yake na tamaa yake maandiko yanamtaja kuwa ana moyo japo ni kiumbe cha kiroho lakini kinapewa utu, kama Mungu anavyopewa utu, Nimemwona Daudi mwana wa Yesu mtu aupendezaye moyo wangu, basi shetani ana moyo

 

Isaya 14:13 “Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini.”

 

Ezekiel 28:17 “Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.”

 

Ezekiel 28:11-17 “Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.”

 

Shetani amefukuzwa kutoka mbinguni kama kitu najisi, lakini hajaharibiwa sura, wala nguvu wala hali ya kuwa na uwezo kama kerubi, na tunaona katika maandiko Mungu akizungumza na ibilisi au shetani bila chuki, na Yesu pia alizungumza na shetani bila chuki wala jazba wala hasira, sisemi kwamba watu wasimchukie shetani lakini kazi yetu kubwa ni kumuelewa na kumjua na kuomba neema ya Mungu na kujitegemeza kwake kwa sababu adui yetu sio wa kawaida ni mwenye nguvu nasi tunahitaji nguvu za Mungu, ulinzi wake na msaada wake na Mungu atatusaidia kwa sababu yeye anamuelewa na kumjua shetani kwa kina na mapana na marefu kuliko sisi.

 

11.    Shetani ana nia – Ukiacha mpango wake wa kutaka kuabudiwa na kutaka kuwa kama Mungu, kazi yake kubwa na nia yake kubwa ni kuiba, kuchinja na kuharibu, wakati nia ya Kristo ikiwa ni kutupa uzima wa milele

 

Yohana 10:10 “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.”   

 

Kwa nini shetani ana nia ya kuiba, kuchinja na kuharibu? Hii ni kwa sababu ana chuki kubwa sana na uumbaji wa Mungu, anachukizwa sisi kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kwa hiyo hana urafiki na wanadamu, anachukizwa na ukweli ya kuwa tutakuwa na utukufu wa Mungu milele, wakati yeye aliupoteza, ana wivu ana uchungu, ana wivu na furaha ya mielele tutakayokuwa nayo, kumbuka kama alivyokokota theluthi ya malaika anataka pia kukokota wanadamu wapatikane watakaokwenda naye kwenye ziwa la moto, anachukizwa na sisi kwa sababu maelfu Rabbi mmoja wa zamani sana aliwahi kusema “kwa wivu wa shetani kifo kiliingia ulimwenguni na wale wamfuatao wako pamoja naye” mwisho wa kunukuu.

 

12.   Shetani ana uwanda mpana wa utendaji – Shetani ana uwanda mpana sana katika utendaji wake wa kazi, na ndio maana kanisa linapaswa kuwa macho, yeye hafanyi kazi tu miongoni mwa watu waovu lakini ana daraja la juu sana katika utendaji wake kama malaika wa Nuru, kwa kusudi la kushughulikia watu wa kanisani yeye pamoja na watumishi wake.

 

2Wakorintho 11:13-14 “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.”

 

Shetani pia ana mafundisho ambayo yako wazi na yanajulikana kama mafundisho ya mashetani, lengo lake kuu ni kuchakachua na kupoteza kabisa waamini na watumishi wa Mungu, anajihusisha na ibada za uongo, watumishi wa uongo na mafundisho yake.

 

1Timotheo 4:1 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;”

 

Ufunuo 2:9-10 “Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani. Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.”

 

Shetani pia anaonekana kuingia katika makusanyiko ya kiimani wakati malaika wanapokusanyika

 

Ayubu 1:6-7 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao.Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.”

 

Shetani anajua nguvu ya kanisa na mafundisho ya kweli na kusanyiko la ibada na maombi na anajua kuwa akifanikiwa kuharibu kanisa ambalo ndilo chumvi ya ulimwengu basi kila kitu kitazolewa kwa urahisi kuelekea upande wake na kuwa mawindo yake.                 

 

13.   Shetani ana mipaka - Pamoja na kutambua uweza na utendaji wa shetani na kukubali kuwa ana akili na mjanja ni muhimu kufahamu kuwa shetani ni kiumbe na ana mipaka kila mtu anayemuamini Bwana Yesu anahesabika kuwa amemshinda shetani, Shetani hana kitu kwa Yesu mwenye nguvu zote, shetani hatawagusa wamwaminio Mungu mpaka kwa ruhusa ya Mungu mwenyewe ama kwa mwamini kufungua mlango wa kushughulikiwa kwa kukushitaki n ahata pamoja na hayo Yesu atasimama kututetea.

 

Yohana 14:30 “Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.”

 

1Yohana 4:4-6 “Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia, Sisi twatokana na Mungu. Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli, na roho ya upotevu.”

 

Yakobo 4:7-8 “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.”

 

Aidha shetani hana uwezo wa kusoma mawazo yetu, Maandiko hayajawaho kuonyesha ya kuwa Shetani ana uwezo wa kusoma mawazo yetu, Lakini badala yake ni Mungu pekee ndiye anayeweza kujua kile kinachoendelea katika moyo wa mwanadamu

 

1Wafalme 8:39 “basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukasamehe, ukatende, ukampe kila mtu kwa kadiri ya njia zake; wewe ujuaye moyo wake; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu wote);”

 

Kwa hiyo ni Mungu peke yake ndiye aijuaye mioyo ya wanadamu, Shetani hayuko mahali kote na huwategemea malaika zake kukamilisha baadhi ya kazi zake, shetani hajui mambo yote ni kiumbe na sio Mungu kwa hiyo ana mipaka katika utendaji wake, japo kuwa shetani anaweza kukuingizia mawazo mabaya na kuotea na kusoma kile anachohisi anaweza kukitumia kwa faida zake, ili kuweza kumshinda ni kumtii Mungu na kumpiga , kutumia neno la Mungu na kukataa mawazo yoyote unayohisia na kujua kuwa yako kinyume na mapenzi ya Mungu        

14.   Shetani ni adui wa injili – Pamoja na kazi zingine anazozifanya shetani usisahau hili, shetani ni adui wa injili ni adui mkubwa sana wa injili, hataki injili iwafikie watu na hataki mafundisho sahihi yawafikie watu anapambana kwa kila jinsi kuhakikisha kuwa anaiharibu injili, anatumia mawazo mbadala, mafundisho potofu lakini pia anapofusha fikra za watu wa ulimwengu huu ili isiwazukie nuru ya injili

 

2Wakorintho 4:3-4 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.”

 

1Wathesalonike 2:18 “Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia.”       

 

Mathayo 13:19 “Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia.”

 

15.   Shetani anaweza kumtumia mtu – Ndio uko uwezekano wa shetani kumtumia mtu katika kushauri au kufanya jambo ambalo liko kinyume na mapenzi ya Mungu, uko wakati Fulani ambapo Yesu alimkemea Petro kwa kutokuwaza mapenzi ya Mungu na kufikiri kibinadamu, Yesu alipofunua mpango wa Mungu kuhusu kufa kwake msalabani kwa ukombozi wa mwanadamu Petro alimpinga Yesu na moja kwa moja Yesu alimkemea, Kimsingi Petro hakuwa shetani lakini alitoa wazo ambalo kimsingi lilikuwa wazo la shetani la kumtaka Kristo asitimize mapenzi ya Mungu, aidha katika mkakati wa kuhakikisha Yesu anakamatwa na kusulubiwa kwa usaliti mkubwa tunaambiwa kuwa shetani alimuingia Yuda ili kutekeleza mpango huo.

 

Mathayo 16:21-23 “Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

 

Luka 22:2-4 “Na wakuu wa makuhani na waandishi walikuwa wakitafuta njia ya kumwua; maana walikuwa wakiwaogopa watu. Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara. Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao.”               

 

Hatima ya shetani

 

Hakuna marefu yasiyo na mwisho au ncha, Maandiko yanaonyesha kuwa shetani ana mwisho, na Mungu aliutangaza mwisho huo mapema mara baada ya kuingilia na kujaribu kuharibu kusudi la Mungu kwa wanadamu

Mwanzo 3:14-15 “BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.”              

Unabii huu unaonyesha ya kuwa Yesu Kristo uzao wa mwanamke utamponda kichwa Shetani anayewakilishwa na nyoka hapo.

Amefukuzwa kutoka mbinguni Ufunuo 12:9Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.”

Wakati wa utawala wa Yesu Kristo wa millenum miaka 1000 shetani atafungwa kwa muda huo na baada ya muda huo atatupwa katika ziwa la Moto milele na milele.

Ufunuo 20:2-3 “Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache.”  

Ufunuo 20:9-10 “Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala. Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima

Maoni 4 :

Wilbert alisema ...

Mch kamote. Mungu akubariki sana. Ninapopata nafasi ya kusoma na kutafakari jumbe zako kwa kweli huwa najifunza mengi . Asante sana.

Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima alisema ...

Asante sana Mtu wa Mungu, endelea kuombea huduma hii ili Roho Mtakatifu aendelee kutufunulia mapenzi yake, nasi tuko tayari kiyaweka wazi Kwa jamii

Bila jina alisema ...

Ubarikiwe na Mungu

Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima alisema ...

Amen