Jumatano, 4 Desemba 2024

Mzabibu mwema, umegeukaje kuwa mzabibu mwitu?


Yeremia 2:19-21 “Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha Bwana, Mungu wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema Bwana, Bwana wa majeshi. Kwa maana tangu zamani wewe umeivunja nira yako, na kuvipasua vifungo vyako; ukasema, Mimi sitatumika; kwa maana juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, umejiinamisha, ukafanya mambo ya ukahaba. Nami nalikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu?

 



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu wetu ni Mungu ambaye anatarajia matunda mema kutoka katika maisha yetu, kila mtu aliyeokolewa katika lugha ya mficho ya kimaandiko anatajwa kama mti hususani mzabibu, na Mungu anaturatajia kama mche mzuri wa mzabibu kumzalia yeye matunda yaliyo mema, Haipendezi kama mtu anaweza kusema ya kuwa ameokolewa na kisha matunda yanayotokana na toba yake yasionekane, Haiwezekani kuwa Mkristo aendelee katika wokovu na kukomaa kiroho kisha matunda ya ukomavu wake yasionekane, Mungu alikuchagua wewe na mimi kama mbegu au mche ulio mwema wa Mzabibu na kutufanyia kila linalowezekana kwaajili ya wokovu wetu ili tuweze kumzalia yeye matunda, na kwa sababu hiyo kama hatutamzalia yeye matunda tutajiweka katika hatari ya kukatwa, na kutupwa motoni kama maandiko yasemavyo:-

Luka 3:7-9 “Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto. Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”

Yohana 15:1-8 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.”

 

·         Kupandwa kwa mzabibu mwema.

·         Mzabibu mwema, umegeukaje kuwa mzabibu mwitu?

·         Jinsi ya kuwa mzabibu mwema!

 

Kupandwa kwa mzabibu mwema

Yeremia 2:19-21 “Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha Bwana, Mungu wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema Bwana, Bwana wa majeshi.Kwa maana tangu zamani wewe umeivunja nira yako, na kuvipasua vifungo vyako; ukasema, Mimi sitatumika; kwa maana juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, umejiinamisha, ukafanya mambo ya ukahaba. Nami nalikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu?”

Nabii Yeremia anatoa ujumbe wenye nguvu na wa Muhimu sana kwa watu wa Mungu, Katika wakati huu Mungu alikuwa anazungumza na wana wa Israel utawala wa Yuda kwa kinywa cha nabii Yeremia kuonyesha masikitiko yake na kuumizwa kwake moyo, yeye kama mkulima au mwenye bustani aliyepanda mzabibu mwema, mkulima huyu anaonyesha wazi kuwa alizingatia masharti na vigezo vyote vya kupanda mbegu iliyo njema, kama wote tunavyofahamu kuwa katika uchaguzi wa mbegu ni muhimu na lazima kwa mkulima kuchagua mbegu au mche ulio bora zaidi kwaajili ya matokeo bora zaidi, Neno la Mungu linaonyesha ya kuwa Mungu alipowachagua Israel kutoka Misri alikuwa amechagua mbegu njema ya uzao wa Ibrahimu, watu ambao walimcha Mungu na kumtii, Mungu alikuwa amewandaa wana wa Israel kwa mkono wenye nguvu ili wamtegemee yeye, Mungu aliwapa sheria na utaratibu na kuwafunza uadilifu kupitia viongozi bora kama Musa na Haruni na wengine na hatimaye kuwaleta katika nchi ya mkanaani, kuchaguliwa kwao na Mungu wakati wote kumefananishwa na mkulima anayezingatia vigezo na masharti katika kuipata mbegu iliyo bora, hakukuwa na kitu chenye upungufu ambacho mkulima huyu hakukizingatia kuanzia na matayarisho ya ardhi, upandaji umwagiliaji, palizi na hata uondoaji wa matawi yasiyo sahihi ili mmea huu uweze kustawi ipaswavyo na kutoa matunda, mazuri na yenye ubora uliokusudiwa!.

Isaya 5:1-4 “Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu katika habari za shamba lake la mizabibu. Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, Kilimani penye kuzaa sana; Akafanya handaki kulizunguka pande zote, Akatoa mawe yake, Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri, Akajenga mnara katikati yake, Akachimba shinikizo ndani yake; Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, Nao ukazaa zabibu-mwitu. Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu. Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu?       

Zaburi 80:7-11 “Ee Mungu wa majeshi, uturudishe, Uangazishe uso wako nasi tutaokoka. Ulileta mzabibu kutoka Misri, Ukawafukuza mataifa ukaupanda.Ulitengeneza nafasi mbele yake, Nao ukatia mizizi sana ukaijaza nchi. Milima ilifunikwa kwa uvuli wake, Matawi yake ni kama mierezi ya Mungu.Nao uliyaeneza matawi yake hata baharini, Na vichipukizi vyake hata kunako Mto.”

Mungu alikuwa amewapanda Israel katika nchi ya mkanaani kwa mfano wa mzabibu, yeye ndiye aliyewatoa katika inchi ya Misri na kuwapanda katika nchi ya mkanaani, huenda Mungu alitumia mfano wa mzabibu kwa sababu Mzabibu ulifikiriwa kuwa ni mti wa Baraka, na mmea huu ulimea katika inchi ya Kanaani kwa miaka mingi sana na kwa karne nyingi sana, kwa hiyo lilikuwa jambo jema na la Baraka kwa Mungu kuwaweka watu wake katika inchi hii, zabibu pia zilikuwa ishara ya Amani na utulivu, Mungu alipowapanda Israel katika Kanaani ilikusudiwa wawe wema na baraka kwa ulimwengu mzima.

Kutoka 15:13-17 “Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa, Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu. Kabila za watu wamesikia, wanatetemeka, Wakaao Ufilisti utungu umewashika. Ndipo majumbe wa Edomu wakashangaa, Watu wa Moabu wenye nguvu tetemeko limewapata, Watu wote wakaao Kanaani wameyeyuka. Hofu na woga umewaangukia; Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe; Hata watakapovuka watu wako, Ee BWANA, Hata watakapovuka watu wako uliowanunua. Utawaingiza, na KUWAPANDA katika mlima wa urithi wako, Mahali pale ulipojifanyia, Ee BWANA, ili upakae, Pale patakatifu ulipopaweka imara, BWANA, kwa mikono yako.”

Mungu aliwakusudia Israel na Yuda wawe watu wake watakaokuwa nuru kwa mataifa yote na kuifunua neema ya Mungu ya ukombozi wa mwanadamu duniani pamoja na mfano wa haki na hukumu, na upendo wake kwa ulimwengu mzima, hili halikuwa jambo dogo, ilikuwa ni neema kubwa na upendeleo usio na kifani miongoni mwa mataifa ya dunia

Isaya 49:5-6 “Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.”

Kuzaliwa kwa zabibu mwitu.

Katika namna yenye kushangaza sana pamoja na ukweli kuwa Mungu anasema alichagua mbegu au mche mwema na kuzingatia vigezo vyote vizuri vya kilimo cha mzabibu, Israel ambao ndio mzabibu wenyewe ulizaa zabibu mwitu, wao walimuacha Mungu na kugeukia ibada za sanamu, waliiacha sheria ya Mungu na kuanza kuabudu miungu, ni ukweli ulio wazi kuwa tunapotenda mema kwa Mungu haiwi jambo la kushangaza kwa sababu tuliumbwa tutende mambo mema, lakini tunapotenda maovu Mungu hushangazwa sana kwa sababu alipotuumba kila kitu kilikuwa chema, lakini watu kwa hiyari yao na utashi walichagua kutokumtii Mungu na kusababisha madhara duniani. Swali kubwa analouliza Mungu ni kuwa imekuaje mzabibu mwema uliohudumiwa kwa vigezo na masharti yote ya mkulima stadi nini kimetokea mzazbibu huo ukazaa zabibu mwitu?

Katika lugha ya kitaalamu mmea uliochaguliwa vizuri, na kuoteshwa katika kitalu kama mbegu iliyo njema kisha ikaoteshwa kwa kuzingatia vigezo vyote kisha ukazaa zabibu mwitu tendo hilo linaitwa “degeneration” kwa kiyunani “ekfylismόs” ni tukio la kutokea kitu kisichotarajiwa na kisichokuwa cha kawaida katika mmea mfano, kunyauka kwa majani, kubadilika rangi ya majani, mizizi kubadilika, kudumaa au kuzorota kwa mmea au kuzaa matunda duni na madogo sana, au kupoteza ubora, tendo hili husababishwa na maambukizi ya virusi kutoka katika ardhi, Katika mfumo wa uzazi wa mwanadamu ni mfano wa Mungu kuweka kizazi kizuri ndani ya tumbo la mwanamke na kisha badala ya tumbo hilo kushika mimba na kuzaa watoto wazuri linatengeneza aina fulani za uvimbe mkubwa ambao ni lazima uondolewe kwa upasuaji na wakati mwingine kulazimika kuondoa na kizazi ili uvimbe huo usijirudie tena, katika hali kama hiyo mzabibu unapopata maambukizi kama hayo wenyewe huondolewa na kuharibiwa ili kuzuia aina hiyo ya ugonjwa kuenea “degeneration” inaweza kusababishwa na aina fulani ya virusi, ambavyo vinauzorotesha mmea halisi na kusababisha matokeo duni, kudumaa, na hata kuzaliwa kwa zabibu zisizo na afya, Katika ulimwengu wa roho kirusi hicho kinaweza kuwa ni utendaji wa shetani na udanganyifu wa mioyo ya wanadamu na kiburi pamoja na tamaa za dunia, Maandiko yanaonyesha kuwa mpanzi anaweza kabisa kupanda mbegu njema lakini adui akapanda magugu.

Mathayo 13:37-43 “Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie.”

Tukio hilo la mzabibu kuharibika na kutokuzaa matunda yaliyokusudiwa licha ya Mkulima kujitahidi kuchagua mbegu njema na kuipanda katika udongo mzuri ndio tukio la Israel na Yuda na ndio linalowakuta watu wa Mungu ambao katika siku za leo, Leo Mungu anazungumza na kanisa lake anazungumza na watu waliokoka leo hii watu wengi waliookoka wameharibika bila kujua na mioyo yao imekuwa kinyume na Mungu aliye hai jambo ambalo linamshangaza sana Mungu,  watu wamelelewa vizuri kiroho, waliokolewa kwa neema, wamejazwa na Roho wake Mtakatifu, wamepata mafundisho yote ya wokovu, lakini unashangaa watu wana roho mbaya, wana hasira, wana kiburi, wamejaa majivuno, wanataka kuabudiwa, wachoyo, wakaidi, wanakomeshana, wanaumizana, wanasemana vibaya, wanasengenyana, wachawi wameingia makanisani, watu wanauana, watu wanaharibiana, watu wanafanyiana mabaya, hakuna matunda ya roho, hila na ubaya, ubinafsi na uchoyo,kuna uchafum kuna uasherati, kuna wivu, kuna mafarakano, kuna ubabe, kuna uzushi, kuna husuda, kuna ulafi, anasa, na kupenda fedha kuliko Mungu, kuna mafundisho potofu na uongo, hayo ndio matunda yaliyozaliwa na watu ambao Mungu alitegemea watakuwa na kiasi, wema, wenye furaha, Amani, wenye fadhili, waaminifu, waliojaa upendo, siku hizi kama unataka kuyaona mambo yaliyokinyume na hayo njoo katika makanisa yetu ya kiroho, utashangaa kushuhudia roho ya nubaya ikitawala hata waamini hawana furaha na makanisa yao, chumba za siku hizi hazina uaminifu, Mungu anashangazwa na mbegu hii njema aliyoipanda!. Swali kuu mzabibu mwema umegeukaje kuwa mzabibu mwitu?

Ezekiel 17:2-8 “Mwanadamu, tega kitendawili, ukawaambie nyumba ya Israeli mithali; useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tai mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya marefu katika mabawa, mwenye kujaa manyoya, yaliyo ya rangi mbalimbali, alifika Lebanoni, akakitwaa kilele cha mwerezi; akakikata kitawi kilicho juu katika vitawi vyake, akakichukua mpaka nchi ya biashara, akakiweka katika mji wa wachuuzi. Akatwaa tena mbegu katika mbegu za nchi hiyo, akaipanda katika udongo uzaao sana, akaiweka kando ya maji mengi; aliipandikiza kama mti ukuao karibu na mto. Ikakua, ikawa mzabibu wenye kuenea sana, wa kimo kifupi, ambao matawi yake yalimgeukia, na mizizi yake ilikuwa chini yake; basi ukawa mzabibu, ukatoa matawi, ukachipuza vichipuko. Kulikuwa na tai mwingine mkubwa, mwenye mabawa makubwa na manyoya mengi; na tazama, mzabibu huo ukapinda mizizi yake imwelekee yeye, ukachipuza matawi yake yamwelekee yeye, toka matuta yake ulipopandwa; ili yeye apate kuunywesha. Ulikuwa umepandwa katika udongo mwema, kando ya maji mengi, upate kutoa matawi, na kuzaa matunda, uwe mzabibu mzuri..”

Wanadamu wote wamekuwa sawa na mzabibu huu ambao Mungu anausikitikia, ya kuwa alifanya kila kitu kuwa chema lakini uhusiano wa wanadamu na Mungu umezorota, ndoa yako ilikuwa njema lakini imezorota, uchumba wako ulikuwa mwema na mlikuwa mnawasiliana vizuri lakini siku za karibuni uhusiano huo umezorota, ulikuwa unapenda sana ibada lakini siku za karibuni uhusiano wako na Mungu umezorota, ulikuwa muombaji sana lakini siku za karibuni hali ya mzabibu huu umezorota, ulikuwa mtoaji na mkarimu na mwenye upendo mkubwa lakini siku za karibuni umezorota, ulikuwa na biashara inayoenda vizuri, uchumi uliokuwa unastawi, mahusiano yaliyokuwa yanastawi, ulikuwa mchapa kazi, mshuhudiaji mzuri, na mfuatiliaji wa watoto wachanga wa kiroho, ulikuwa unampenda Mungu wakati huo ulikuwa mche mwema lakini sasa mzabibu umezorota, moyo wa ubinafsi, choyo, chuki na wivu, ugomvi, ukatili ni matunda ambayo Mungu anashangazwa kwa kuwa alitarajia matunda mema lakini umezaa zabibu mwitu! Na mizizi yako imeelekea kwingine! Hii maana yake ni nini badala ya kuzaa matunda mema watu wamezaa matunda mabaya mizizi imeenda kujiunga na chanzo kingine cha udongo usio sahihi ona:-

Wagalatia 5:19-23 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”

Maandiko yanaonyesha kuwa ni mzabibu mmoja tu ndio umekuwa mzabibu wa kweli na mzabibu huu ni Yesu Kristo, lakini mizabibu mingine yote imezorota na ina mapungufu mbalimbali na kwa kweli sio mizabibu halisi au ya kweli wote tumekuwa mizabibu mwitu, Yesu Peke yake ndiye wa Mzabibu wa kweli, na ili tuweze kuwa mzabibu wa kweli wenye kuzaa matunda hatuna budi kupandikizwa katika Kristo Yesu, na kuendelea kukaa ndani yake kama tawi, hapo ndipo tunapoweza kuzaa matunda mazuri, na tutaendelea kusafishwa, lakini nje ya Yesu, mbingu utazisikia kwa hadithi tu, uwezo wa kuzaa vema hautakuwepo, na uwezekano wa tawi hilo kuondolewa ni mkubwa sana.

Yohana 15:1-2 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.”

Jinsi ya kuwa mzabibu mwema!

1.       Tunaweza kumsihi Mungu atupe neema ya kuwa mbali na kiburi, wana wa Israel waliharibiwa na kiburi, walishika dini na sheria za Musa pamoja na mapokeo ya baba zao, wakagoma kabisa kumpa Mungu nafasi ya kushughulika na maisha yao, wakati wote walijifikiria kuwa wako sahihi, hata nyakati za leo wako watu kwa sababu ya kiburi cha kidini, hawana muda wa kujichunguza wanadhani wako sahihi na Mungu, Shetani alikuwa pia mzabibu mwema wakati fulani, lakini moyoni mwake alijaa kiburi na majivuno, alitaka kujiinua kuliko Mungu, aliwaambukiza dhambi yake wanadamu,  wayahudi na bila kujijua wakawa watoto wa shetani, Hebu jaribu kuwaza kuwa wayahudi hawa wenye kuishika sheria ya Musa kwa kiwango hiki ni lini waligeuka na kutokuwa watoto wa Mungu hata Yesu anawaambia ninyi ni wa baba yenu ibilisi? Walikuwa mzabibu mwema lakini hawakujua kuwa wamegeuka kuwa mzabibu mwitu na kwa sababu ya ukaidi wao, wao ndio walikuja kumshulubisha Bwana Yesu na kumsaliti na kumkabidhi mikononi mwa waovu ili asulubiwe!

 

Yohana 8:42-45 “Yesu akawaambia, Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma.Mbona hamyafahamu hayo niyasemayo? Ni kwa sababu ninyi hamwezi kulisikia neno langu.Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.Nami, kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki.”

 

Jiulize ni kwanini Yohana alikuja na ubatizo wa toba kwa wayahudi?  Je unadhani watu hawa walikuwa wanahitaji toba? Je walikuwa hawashiki imani? Je walikuwa hawafungi? Je walikuwa hawaepuki dhambi? Nini kiliwaponza wana wa Ibrahimu mche mzuri wakawa wana wa nyoka? Nadhani kanisa tunahitaji kujiangalia vizuri na kwa umakini mkubwa, kama tulizaliwa tukiwa wana wa Mungu inawezekanaje tena tukawa wa uzazo wanyoka?, shetani ni mjanja sana hatatumia zinaa, wala ulevi kutuangusha atatumia kiburi, atatumia majivuno atatumia njia ya kujibebesha utukufu wa Mungu na tukajikuta tumekataliwa kistaarabu.

 

Luka 3:7-9 “Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto. Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.”              

 

2.       Tunaweza kurudi kwa Yesu ambaye ndiye mzabibu wa kweli na kuwa tawi linalostawi ndani yake na ambaye tukikaa ndani yake tutazaa sana matunda na kusafishwa zaidi ili tuzidi kuzaa!

 

Yohana 15:4-6 “Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea.”

 

Endapo tutaacha kiburi na unafiki na kutubu na kukaa ndani ya Yesu Kristo yeye yuko tayari kutupokea na kutusamehe kabisa na kurejesha uhusiano wetu na yeye na tunaweza kumzalia matunda, watu wenye kiburi wakati wote hujifikiria kuwa watakatifu na kuwa hawana dhambi ya kutubia, sio hivyo tu wakati wote wao hunyooshea kidole watu wengine na kukuza makosa ya wengine badala ya kujikagua wewe mwenyewe, kumbuka kila mmoja atalichukua furushi lake mwenyewe!, Matunda unayozaa ndio yanayotambulisha kuwa ani alikuwa mti mbaya na nani alikuwa mti mwema na vile utakavyozaa matunda, matunda hayo ndio yatafunua asili yako hatuwezi kuigiza, mbele za Mungu matunda yatasema

 

1Yohana 1:8-10 “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.”

 

Luka 6:41-45 “Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako. Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri;   kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu. Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.”

 

3.       Lazima tukubali kuwa wanyenyekevu -  Neema ya Mungu haikai na watu wenye kiburi, neema ya Mungu inakaa na watu wanyenyekevu, uwepo wa Mungu unakaa na watu wanyenyekevu, toba wakati wote inaenda na unyenyekevu, bila unyenyekevu na moyo uliopondeka hatuwezi kufaidi uwepo wa Mungu

 

Isaya 66:2 “Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.”

 

1Petro 5:5-6 “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;”

Hitimisho:

Ujumbe wa Yeremia ni ujumbe wa nyakati zote Mungu analionya taifa la Israel, analionya kanisa na kila mmoja wetu, wote tunahitaji toba, wote tunapaswa kuitikia wito wa Mungu na kukubali kuwa Mungu anaumia anapoona tunaacha kuzaa matunda yaliyokusudiwa na kuzaa zabibu mwitu, Mungu anatuvumilia sana vinginevyo tungekuwa tumeshakatwa, Bwana amempa neema kila mmoja wetu kuwa na uwezo wa kuzaa matunda mema yanayokusudiwa katika Ukristo wetu, Mungu alipokuchagua wewe na mimi alituamini, alijua ya kuwa tutamzalia bwana matunda na tutaongoza wengi katika mema na kuwa nuru na Baraka kubwa kwa ulimwengu, mambo yanapokuwa tofauti maana yake ni kuwa Mzabibu mwema umegeuka kuwa mzabibu mwitu, Upewe neema wewe na mimi tusiwe mzabibu mwitu katika jina la Yesu Kristo, wakati huu tunapoelekea kuumaliza mwaka kila mmoja anapaswa kujifanyia tathimini na kuongea na Mungu na kujenga hoja ni kwa nini asikatwe?  Na kama hutaki kukatwa basi tuzae matunda

Luka 13:6-9 “Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: