Jumapili, 7 Desemba 2025

Nafsi yangu inakuonea kiu kama Ayala!


Zaburi 42:1-4 “Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji. Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu. Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai, Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu? Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako. Nayakumbuka hayo nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu, Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano, Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu, Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu.”




Utangulizi:

Kila mwanadamu aliyeumbwa na Mungu katika roho yake ameumbiwa kiu, njaa, hamu na shauku ya kutaka kuwa na uhusiano na Mungu, kimsingi mwanadamu aliumbwa ili awe na ushirika au uhusiano na Mungu, ushirika huo au uhusiano huo unafananishwa na kiu ya maji aliyonayo Ayala, hii ni kiu ya uhitaji wa uwepo wa Mungu, kiu ya kutaka kumsikia Mungu, kiu ya kutaka kumuabudu, kiu ya kutaka kumtumikia Mungu katika viwango vyenye kuleta utoshelevu, kiu ya kutaka kuongozwa na yeye na kumuona Mungu akitembea katika utukufu wake, Kama kuna jambo linaumiza moyo wa mtu aliyezoea kuwa na ushirika na Mungu ni pamoja na kutokuhisi ule uwepo wake, Musa alikuwa na kiu na shauku ya kutaka uwepo wa Mungu uwe pamoja naye kiasi kwamba alimwambia Mungu uso wako usipokwenda pamoja nasi usituchukue kutoka hapa, hii ilikuwa ni shauku ya kuhitaji uwepo wa Mungu kama jambo la lazima, aliona bila uwepo wa Mungu yeye na wana wa Israel hawawezi lolote.

Kutoka 33:13-15 “Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.”

Mwandishi wa zaburi hii ya “42” ambaye kitaalamu ni wana wa Kora waliitumia zaburi hii ambayo iko katika kundi la zaburi za Kuomboleza, yaani za mwandishi anaomboleza kwamba hawezi tena kwenda Hekaluni nyakati za sikukuu mbalimbali, kutokana na mazingira kumtenga asikaribie uwepo wa Mungu, Mwandishi anatumia hapo mfano wa Ayala (Kulungu) kuonyesha jinsi ambayo nasfi yao ilivyo na shauku na kiu ya kutaka maji, Nao wana wa Kora wana kiu ya kuona uwepo wa Mungu, yaani wana kiu na shauku ya uwepo wa Mungu. Lakini wako katika mazingira magumu ambapo kuabudu kwao sio kwa furaha na uhuru kama vile kwenda Hekaluni, kiu hii ya kuutafuta uwepo wa Mungu hekaluni mwake inatupa fursa ya kuitafakari zaburi hii chini ya kichwa Nafsi yangu inakuonea kiu kama Ayala! Na tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Kwa nini kiu kama Ayala?.

·         Nafsi yangu inakuonea kiu kama Ayala.

·         Umuhimu wa kuwa na kiu kama Ayala.

 

Kwa nini kiu kama Ayala?

Zaburi 42:1-2 “Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji. Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu. Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai, lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu?

Mwandishi yaani wana wa Kora wakiimba kwa niaba ya Daudi, wanaonyesha kiu kubwa sana ya kutamani kwenda nyumbani mwa Bwana ili kujihudhurisha mbele za Mungu, akitaka kuielezea kiu yake na hamu na shauku ya kutaka kuutafuta uwepo wa Mungu mwandishi anatumia mfano wa Ayala atamanivyo maji ya mto sawa na kiu yake ya kumtafuta Mungu, Mwandihi hakuchagua mfano huu kwa bahati tu lakini bila shaka alikuwa na ujuzi mkubwa kuhusu mnyama huyu Ayala au (Kulungu) Katika lugha ya Kiebrania mnyama huyu anaitwa ‘ayรขl sawa na neno Ayala la Kiswahili na Deer la kiingereza jina lingine la Kiswahili ni Kulungu, au paa, ingawa paa wako wa aina nyingi sana!

Ayala au Paa ni mnyama anayejulikana  sana kuwa ni rahisi sana kushambuliwa na wanyama wakali, na kwa sababu hiyo kwaajili ya kujilinda wao huishi katika maeneo ya milimani hasa katika mbuga za wanyama jangwani au nyikani na pia wana uwezo wa kukimbia kwa umbali mrefu kwa kasi, kutokana na uwezo wake wa kukimbia kwa kasi kati ya 35-40 mph huku akiruka ruka uwezo wake wa kuruka ruka ni kati ya 8-10 futi sana yeye hutumia nguvu ambazo zinapoteza maji mwilini mwake kwa haraka, kwa hiyo hujikuta akisumbuliwa sana na kiu, na kwa sababu hiyo hawezi kutulia ni lazima atafute maji bila kuacha,Mwili wa Ayala umeumbwa kwa maji kwa asilimia 65% kwa hivyo hata kama kuna chakula cha kutosha Maji yana umuhimu mkubwa sana kwake vinginevyo hataweza kuwa na nguvu za kukimbia maadui zake, lakini pia hawezi kuishi muda mrefu bila maji kwa hiyo uhai wake unategemeana sana na kunywa maji, sio hivyo tu maisha yake juani na jangwani na kwenye joto huchangia kuifanya kiu yake kuwa kali kuliko wanyama wa kawaida, kwa hiyo hawezi kuishi bila maji, maji kwake ni hitaji lisilozuilika, maji kwake ni uhai, maji kwake ni ya lazima, maji kwake ni swala la dharula kwa hiyo wana wa Kora wanatumia mfano wa Ayala kuonyesha kuwa wao nao uwepo wa Mungu una umuhimu mkubwa sana sawa tu na Ayala anavyohitaji maji ya mito kwa kunywa!

Zaburi 63:1-3 “Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu, Nizione nguvu zako na utukufu wako. Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai; Midomo yangu itakusifu.”

Nafsi yangu inakuonea kiu kama Ayala.

Kwa nini Mwandishi alikuwa na kiu hii inayofananishwa na kiu ya Ayala? Mwandishi anaonekana kuwa alikuwa katika kipindi cha shida na taabu, alikuwa amefukuzwa mbali na nyumba ya Bwana, kwa hiyo hakuwa na Muda wa kujiudhurisha mbele za Mungu na badala yake alikuwa akikimbia kutoka nyika moja kwenda nyika nyingine, alikuwa katika mashambulizi makali, hali ngumu na kipindi cha giza la kiroho, kwa hiyo alihisi maisha yake yako hatarini na uwepo wa Mungu pekee ndio ulinzi wake na hata ingawa alimtegema Mungu adui zake waliohoji yuko wapi Mungu wake, mwandishi alikuwa akitoa machozi usiku na mchana na machozi yakawa kama chakula chake!

Zaburi 42:3-6 “Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako. Nayakumbuka hayo nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu, Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano, Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu, Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu. Nafsi yangu, kwa nini kuinama, Na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; Kwa maana nitakuja kumsifu, Aliye afya ya uso wangu, Na Mungu wangu. Nafsi yangu imeinama ndani yangu, kwa hiyo nitakukumbuka, Toka nchi ya Yordani, na Mahermoni, na toka kilima cha Mizari.”

Unaona anakumbuka alivyokuwa akiongoza watu kwenda nyumbani mwa Bwana kwa furaha, lakini siku hizo zimetoweka, yuko mbali na uwepo wa Mungu anakaukiwa kwa hiyo kiu yake kwa Mungu iliongezeka kwa sababu ya mazingira magumu aliyokuwa anayapitia, sasa hafurahii uwepo wa Mungu kama zamani kwa sababu yuko mbali, yuko mbali na madhabahu ya Bwana, na Hekaluni, anaukosa uwepo wa Mungu na uwepo wa Mungu unaibuka kuwa kiu yake kubwa, Yeye kimsingi hakuwa analenga Baraka au uhitaji mwingine lakini yeye alikuwa na hamu au kiu ya ushirika na Mungu yeye mwenyewe, kiu ya aina hii ni kiu yenye Baraka kubwa sana kama watu watakuwa nayo

Mathayo 5:6  Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.” Mwandishi alikuwa na kiu ya kusikia kutoka kwa Mungu, kiu ya neno la Mungu, alikuwa na kiu ya kutaka kuabudu na kufurahia uwepo wake na ukaribu wake na Mungu, Kumkosa Mungu kwake ilikuwa ni sawa na kuwa katika nyika au katika nchi ya ukame, uhai wake ulikuwa unahitaji sana vitu hivi, alikuwa anatambua kuwa ushirika kati yake na Mungu ndio chanzo cha Baraka nyinginezo zote, alitambua kuwa ulinzi wake na usalama wake unategemeana sana na ukaribu wake na Mungu, Maneno ya Mwandishi wa zaburi hii ni ya muhimu na ya msingi kwa kila mwanadamu duniani, Unaishije bila kuabudu, unaishishe bila maombi, unaishije? Unategemea nini na usalama wako ni nini Maisha yetu bila uwepo wa Mungu ni kujihatarisha ni lazima tuwe na kiu na hamu na shauku ya mambo ya Mungu wetu, ziko nyakati katika maisha tunaweza kukosa kabisa nafasi ya kuufurahia uwepo wa Mungu, Ayala bila kunywa maji hata kama kuna chakula uwezo wake wa kuishi unapungua sana na uwezo wake wa kujihami unapungua mno na mauti inakuwa karibu, uhai wake unategemea sana maji na sisi nasi uhai wetu unamtegemea sana Mungu, mwandishi wa zaburi alimtegemea sana Mungu sisi nasi hatuna budi kumtegemea sana Mungu na kuona ya kuwa bila yeye sisi hatuwezi kuishi, Ayala hukimbia anakokimbia lakini lazima atafute vijito vya maji ili maisha yaweze kuendelea, wewe na mimi tunawezaje kuishi bila Mungu na bila kuwa na uhusiano naye? Ni lazima kuwa na kiu kwa maswala ya Mungu, kiu ya kuabudu, kiu ya kujazwa na Roho wake Mtakatifu, na kiu ya kumuabudu

Amosi 8:11-12 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana.Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione.”       

Umuhimu wa kuwa na kiu kama Ayala.

Tunaona mwandishi akiomboleza kwa sabahu alikuwa katika kipindi ha mateso na majaribu, na alikuwa na uhakika kuwa Mungu ndiye msaada wake mkubwa, kwa hiyo kiu yake sio ya maji na chakula, ni kiu ya uwepo wa Mungu kama zamani, ni kiu yanafasi ya kumuabudu Mungu, inaonekana mwandishi aliwahi kuwa Hekaluni na aliwahi pia kuongoza ibada, au kuongoza watu kuelekea ibadani lakini sasa anakosa jambo hili muhimu, na anateseka, jambo hili linaibua kiu ya kumuhitaji Mungu kwa wingi zaidi, Uhai wetu wa kiroho unategemea sana na uhusiano wetu wa amani na Mungu, kila mwanadamu anahitaji hili, ni kiu hii ya ndani ya kuhitaji ushirika na Mungu ndiyo inayotufanya tuwe na uwezo wa kumtafuta Mungu, kiu hii husababishwa na Roho wa Mungu ndani

Yeremia 29:11-13 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.”

Ayala anategemea sana Maji pia sio kwaajili ya kunyumbulika kwa misuli yake lakini maji pia humfanya akue na kuongezeka hatua kwa hatua, kiu ya uwepo wa Mungu hutusaidia katika ukuaji wetu wa kiroho, Mtu aliyeokoka karibuni anaitwa mtoto mchanga wa kiroho, kama mtu atakosa kiu ya neno la Mungu, na kiu ya ibada, na kiu ya kuutafuta uwepo wa Mungu ni dhahiri kuwa ukuaji wake wa kiroho utaathiriwa anaweza kudumaa au kuwa na miaka mingi katika wokovu lakini akiwa amebaki vile vile tu, kama kiu hii itaondoka kwa kweli tunaweza kusema kuwa uhai nwako wa kiroho umeondoka! Kifo cha kiroho kimetokea, Kama uzima wa kiroho uko ndani yako tamaa au kiu ya kumtafuta Mungu itakuweko ndani yako nah ii ndio dalili ya uhai wako wa kiroho.

1 Petro 2:2 “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;”

Waebrania 5:11-14 “Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia. Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu.Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.”

Moja ya changamoto kubwa inayolikabili Kanisa katika nyakati za leo, sio tu kukosa uamsho pekee lakini pia kanisa limejawa na wakristo na hata watumishi waliodumaa kiroho, wako vile vile miaka yote matendo ya mwilini yanaonekana wazi wazi, mafarakano na fitina zinazonekana wazi wazi na hii ni dalili ya kuwa watu wamedumaa kiroho au wamebaki katika hali ya uchanga ni kiu ya neno la Mungu na uwepo wake pekee utakaotusaidia kukua kiroho siku hadi siku na kuondoka mwilini ona:-

1Wakorintho 3:1-3 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi,kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?

Ni kiu ya aina kama ile ya Ayala ambayo kimsingi pia inaleta uamsho na uwepo wa Roho Mtakatifu unapohisi kukaukiwa kiroho basi unayo kiu hii na Mungu ametoa wito kumpa maji ya uzima kila mwenye kiu

Isaya 44:1-3 “Lakini sikia sasa, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na Israeli, niliyekuchagua; Bwana, aliyekufanya, na kukuumba toka tumboni, yeye atakayekusaidia, asema hivi; Usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na wewe, Yeshuruni, niliyekuchagua. Kwa maana nitamimina maji juu yake aliye na kiu, na vijito vya maji juu ya mahali pakavu; nitamwaga roho yangu juu ya wazao wako, na baraka yangu juu yao utakaowazaa;”              

Yohana 7:37-38 “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.”     

Huduma za kiroho zinatolewa kwa watu wenye kiu, kama mtu akipoteza kiu amepoteza uhai wa kiroho, Roho Mtakatifu anatolewa kwa watu wenye kiu, kama huna kiu huwezi kupokea mito ya maji hai inayoahidiwa na Neno la Mungu, Mungu anamtarajia kila mwanadamu awe na kiu hii, sio wakati wa mapito na shida tu lakini kila siku kama tunavyohitaji maji katika maisha yetu tunamuhitaji na Mungu pia, Mtu wa rohoni aliye hai ni yule mwenye kiu, kiu yake inamlazimisha kufika katika ibada za mafundisho katikati ya wiki, na siku za ibada kuu kila jumapili, na kumtafuta Mungu sisi wenyewe binafsi,tukiwa na kiu hii Mungu hutujalia neema na utoshelevu wa kiroho, Ayala huyatafuta maji kwa gharama yoyote hata kama yako mbali anajua uhai wake umeungamanishwa na maji, sisi nasi tunapaswa kumtafuta Mungu kwa bidii kama Ayala ayatafutavyo maji ya mto, Mwandishi ameonyesha wazi kuwa kama Ayala asivyoweza kustahimili maisha bila maji, sisi nasi hatuwezi kustahimili maisha bila uwepo wa Mungu, ni kiu yetu ndiyo inatayotupeleka katika vyanzo ma maji ya uzima na kutupa wakati wa kuburudishwa na Roho Mtakatifu jambo litakalofungua baraka kubwa za kiroho katika maisha yetu ya kila siku na kuchochea ukuaji wa kiroho na ukomavu wake!

“Nafsi yangu yakutamani, Nafsi yangu yaona kiu, Kama Ayala atafutavyo maji ya mto, Bwana nafsi yangu yakutamani, Nijaze Roho Mtakatifu, niweke karibu na wewe, Kama Ayala atafutavyo maji ya mto Bwana nafsi yangu yakutamani”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Jumapili, 30 Novemba 2025

Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale!


Maombolezo 5:19-21. “Wewe, Bwana, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi. Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.”


Utangulizi:

Je? umewahi kufikiri kuwa siku kadhaa au miaka kadhaa huko nyuma ilikuwa bora katika maisha yako kuliko ilivyo sasa? Siku ambazo furaha yako ilikuwa timilifu, siku ambazo afya yako ilikuwa njema, siku ambazo uhusiano wako na Mungu ulikuwa mzuri sana, siku ambazo ulikuwa mwombaji sana, siku ambazo ulikuwa hukosi mikesha, huachi kufunga, siku ambazo hata upitie taabu gani hukuona shida, siku ambazo ni kama zilikuwa siku za ushindi wako, siku ambazo familia ziliishi kijamaa, tuliwatembelea Babu na Bibi zetu vijijini, tulikutana na ndugu wengi, ulikuwa na marafiki wengi, watu walikaa pamoja kwa umoja na upendo ulikuwa ni kama umefikia kilele cha hali ya juu cha furaha ya maisha, unazikumbuka siku zile na unatamani kama zingerudia tena upya! Hali kama hii ndiyo iliyomkuta nabii Yeremia alikumbuka siku za utukufu mkubwa wa Mungu katika Uyahudi, wakati Hekalu la Yerusalem lililojengwa na Suleimani bado halijatiwa moto na kubomolewa zilikuwa siku njema, lakini Mungu alikuwa ameziondoa na sasa anaona uharibifu na mambo hayako kama siku zile, anaona ni kama Mungu amewaacha na kuwasahau kwa muda mrefu na kwa siku nyingi sana.

Maombolezo 5:19-21. “Wewe, Bwana, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi. Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.”

Hali hii ni hali ya kuhuzunisha sana ni hali yenye mchanganyiko wa majonzi na kukata tamaa ni wakati ambapo maisha ya mwanadamu yanakuwa yamezidiwa na kumbukumbu ya mambo mabaya yaliyotokea na yanayoendelea katika wakati ulioko, huku ukikumbuka siku zile za utukufu ambazo sasa unatamani ungezirudisha siku nyuma, uweze kuzifurahia na kupata Amani, Kisaikolojia hili tukio linaitwa “Nostalgia”.  Nostalgia is a state of being sick emotional for the past period or homesick, university days etc. Hali ya kuumwa kihisia kwaajili ya kukumbuka mambo mazuri ya zamani au kukumbuka nyumbani au siku zako za chuoni na kadhalika, Yeremia sasa anaumwa ugonjwa huu na anamuomba Mungu kwamba asikawie anamuomba Mungu awageuze nao watageuka na azifanye mpya siku zao kama siku za zamani!, ilikuwa ni sauti ya kuomboleza iliyojaa uchungu hasa baada ya Hekalu la Yerusalem kutiwa moto na kubomolewa na mfalme wa Babeli mwaka 586 KK Yeye alikuwa ameshuhudia siku nzuri za utukufu wa Hekalu hilo na siku mbaya za uharibifu mkubwa Hekalu likiwa limebomolewa, watu wamechukuliwa kwenda uhamishoni, taifa limepoteza fahari yake, na Mungu anaonekana kuwa kimya kwa hiyo moyo wake umejaa ombi lenye huzuni, toba na matumaini. Wewe je unapitia hali ya namna gani hapo ulipo? Familia yako je? Umri wako je? Ndoa yako Je? Hali yako ya kiuchumi, hali yako ya kiroho? Uhusiano wako je? Kanisa lako je kuna uamsho? Watu wanampenda Mungu kama zamani? Uzuri wako? kazini kwako je zipi siku bora katika maisha yako? Leo tutachukua muda kujifunza kwa undani somo hili muhimu lenye kichwa Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale! Na tutajifunza somo hili litakalo kurejeshea matumaini kwa kuzingatia vipengele vitatu muhimu vufuatavyo;-

·         Kilio cha kukumbuka siku za kale

·         Sababu za kukumbuka siku za kale  

·         Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale!

Kilio cha kukumbuka siku za kale

Maombolezo 5:19-21. “Wewe, Bwana, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi. Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.”

Kimsingi kifungu hiki yalikuwa ni maombolezo au kilio ya Nabii Yeremia ambaye alikuwa akiomboleza baada ya mashambulizi mazito na hali mbaya ambayo watu wake na yeye mwenyewe walikuwa wameishuhudia, uharibifu mkubwa uliofanywa na majeshi ya Wakaldayo chini ya utawala wa Nebukadreza mfalme wa Babeli, Yeremia alikuwa anaona uchungu na sasa anaomboleza juu ya mateso ya taifa huku akiona kana kwamba Mungu amewasahau na kuwaacha kwa hiyo Yeremia alikuwa akimlilia Mungu na kumtaka awarejeze katika hali yao waliyokuwa nayo mwanzo.

Kisaikolojia hisia hizi zinaitwa “Nostalgic feelings” yaani hii ni tabia ya mwanadamu kukumbuka siku nzuri za utukufu za zamani zilizokuwa za furaha kwaajili ya kufidia hali ngumu anayokutana nayo katika wakati ulioko, akili haitaki kuona mambo mabaya inataka mambo mazuri, akili haitaki nyakati ngumu inataka amani raha na utulivu tu kwa hiyo kwa mfano umri unapokuwa unaenda mtu anaanza kukumbuka enzi za ujana wake, anakumbuka siku za zamani shuleni, chuoni na kadhalika, katika mahusiano anaanza kukumbuka siku nzuri ambazo alikuwa na soko, anapendwa na kila mtu, unapokuwa mpweke unakumbuka zamani familia zilipokuwa zinakaa pamoja na kula na pamoja na sikukuu tulizokuwa tunaenda kwa Babu na Bibi na kujumuika pamoja, unapokuwa na afya mbaya unakumbuka siku zako ulizokuwa na uzima ukiwa na nguvu, ulipokuwa na uwezo wa kula nyama na mahindi ya kuchoma na sasa meno hayana uwezo huo tena, unakumbuka siku za kale mlivyokuwa mkihubiri injili, unakumbuka wahubiri wakubwa wa zamani, miujiza mikubwa iliyokuwa ikifanyika, unakumbuka nyakati ambazo ulikuwa maarufu, na wakati wa mafanikio, unakumbuka nyimbo za zamani, wachezaji wazuri wa timu yako uliyoipenda ilipokuwa ikitwaa ubingwa, unakumbuka vipindi maalumu ambavyo sasa ni kama vimepita na haviwezi kurudi tena, unakumbuka kipindi chako kiitwacho “the golden age” hii ni hali ya kawaida wakati mwanadamu anapopitia magumu, Israel walikumbuka chakula walichokuwa wanakula Misri japo walikuwa utumwani na waliteswa

Hesabu 11:4-6 “Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N'nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu.”

Hali kama hii inamkuta nabii Yeremia anakumbuka jinsi Wayahudi walivyokuwa na amani katika taifa lao, walivyokuwa wakipanda kwenda Hekaluni, anakumbuka Mungu alivyokuwa mtetezi wao na jinsi Mungu aliyokuwa akisema nao na kuwapa wafalme na mahitaji yao, sasa kila kitu kimebakia historia mambo yameharibika, watu wamechukuliwa uhamishoni Babeli, Taifa limepoteza matumaini hakuna uhai tena, watu wako utumwani Mungu yuko kimya amegeuza uso wake Yeremia anamlilia Mungu anamuomba kwa unyenyekevu, anamuuliza mbona umetuacha, umetuacha muda mwingi, yaani unakawia, utugeuze kwako nasi tutageuka, lakini zaidi ya yote zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.

Yeremia 5:20-21 “Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.”

Sababu za kukumbuka siku za kale.

Maombolezo 5:19-21. “Wewe, Bwana, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi. Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi? Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.”

Kwa nini Yeremia anakumbuka siku za kale? Kwa nini wewe na mimi tunazikumbuka siku zile? Siku za kale ulikuwa ni wakati wa utukufu, ulikuwa ni wakati watu wamejitoa kwa uaminifu, ulikuwa wakati wa uhusiano mzuri na Mungu, ulikuwa ni wakati watu waliabudu na kutembea na uwepo wa Mungu na miujiza mingi ilifanyika, ulikuwa ni wakati wa uhusiano mzuri, urafiki mwema wakati wa kuoneana shauku, wakati ambapo kila unaloliomba linajibiwa ulikuwa ni wakati wa Baraka, akitokea adui watu walijaa Roho Mtakatifu na maadui walikimbizwa, taifa lilikuwa na heshima, watu walikuja kutafuta Hekima na kumuabudu Mungu wa Yakobo, watu walivyotoa sadaka kwa unyoofu wa moyo, katika mahusiano watu walipendana, sasa nyakati hizo haziko tena, majumba yamekuwa magofu, upako haupo, miujiza imepotea, watu hawana mikesha tena, hekalu limechomwa moto Yeremia analia anaomboleza anamwambia Mungu zifanye upya siku zetu kama siku za kale, msikilizaji wangu na msomaji wangu wewe u hali gani sasa? Uko wapi, familia yako iko wapi, ndoa yako iko wapi, malezi yako yako wapi, furaha yako iko wapi, utukufu wako uko wapi, u hali gani, kanisa lako li hali gani na wewe mwenyewe hali yako ya kiroho ikoje?  Je unaugua kama Yeremia? Asante Mungu kwaajili ya nabii Yeremia alimfahamu Mungu alijua ya kuwa Mungu anauwezo wa kuzifanya upya ziku zetu na kuzirejeza zikawa kama siku za kale, leo ni siku yako ambayo Bwana atazifanya upya siku zako Mungu wetu anauwezo wa kurejesha, neno la Mungu linatueleza hivyo ana uwezo wa kututia nguvu

Zaburi 103:1-5 “Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema, Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai;”

Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale!

Mungu anawezaje kuzifanya upya siku zetu kama siku za kale? Yeremia alikuwa amegundua siri mojawapo muhimu katika dua yake ambayo inatufunulia maswala muhimu sana yanayoweza kutuasaidia na sisi katika Maisha yetu ili tusiweze kumezwa na huzuni kutokana na hali unayoipitia!

Maombolezo 5:21 “Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.”

Katika lugha ya Kiebrania kifungu hiki muhimu kinasomeka hivi “Hashivenoo ADONAI elecha venashuvah, chadash yamenu ke’kedem” Kwa kiingereza maneno hayo yanasomeka hivi “turn us back Adonai and we will come back, renew our days, as they were in the past”

Hashivenoo (shuv)  - Uturudishe nyuma, utugeuze, uturejeshe, tugeuze, tubadilishe, ni neno linalotumika katika lugha ya Kiebrania mara nyingi likimaanisha kutubu, kubadilika moyo, kutoka dhambini, kumrudia Mungu, Yeremia hasemi tunageuka anasema utugeuze, akimaanisha Mungu ndiye chanzo cha toba ya kweli, hii inamaanisha toba ya kweli sio matokeo ya hisia zetu  na matakwa yetu wanadamu tu bali ni neema ya Mungu inayoufanya moyo wa mwanadamu ulainike na kumgeukia Mungu na kuamua kufuata njia za Mungu, kwa hiyo Yeremia anajua ya kuwa siku njema kama za zamani haziwezi kurejea hivi hivi bila ya msaada wa Mungu, ni lazima Mungu atuamshe tena na kuwasha upya moto ndani yetu utakaotusaidia kurudi kwake na sio maamuzi ya kibinadamu.

Warumi 9:15-16 “Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.”

Venashuvah – Tutageuka, tutaitikia, tutakubali, yaani tutakubali mabadiliko tutatii, Yeremia anatambua kuwa ili siku njema ziweze kurejeshwa ni lazima Mungu mwenyewe awashe moto wa mawasiliano na kugeuza mioyo yetu na kuturehemu na sisi nasi tuitikie kwa kutii kwa hiyo hapa tunajifunza kwamba uamsho ni ushirikiano kati ya Mungu na Mwanadamu, Mungu anapoanza kwa rehema zake sisi ni wajibu wetu kuitikia kwa toba na utii kwa uaminifu na moto ule utawaka.

Chadash (Chadesh) – Kufanywa upya kurejesha, kuhuhisha kujenga hari mpya, neno Chadash linatokana na neno Chodesh ambalo maana yake ni mwezi mpya mwenzi mchanga, mwezi unaochomoza kwa upya kutoka gizani, Yeremia anamsihi Mungu aanzishe jambo jipya katika mioyo yetu alete uhai katika mambo yote yalitopotea atupe mwanzo mpya arejeshe hali ya kiroho, kiuchumi na kimaisha aturejeshee furaha, atupe nuru hii pia ni kazi ya Mungu ndani yetu kutuhuisha

Zaburi 51:10-12 “Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu Usinitenge na uso wako, Wala roho yako Mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi.”

Maombi ya Yeremia yalikuwa yamejaa ujuzi na hekima ya kuwa ni Mungu mwenyewe peke yake na mwitikio wetu kwa rehema zake unaoweza kusababisha mabadiliko na kurejeswa kwa siku zetu kama siku za kale, Kama watu wa Mungu wanataka kurejeshewa siku za furaha na amani basi ni lazima tumsihi Mungu kama Yeremia alivyoomba kwamba Mungu aturejeshe na sisi tukubali kurejea tukatae kupoa kiroho, tukatae ubaridi katika uhusiano wetu na Mungu ambaye ndiye chanzo cha Baraka, tumsihi Mungu afufue mambo yote yaliyokufa ndani yetu, aiponye mioyo iliyovunjika atupe uwezo wa kusamehe, atupe nguvu ya kuomba, atupe kuliheshimu neno lake, atupe ile hali ya kumuhofu, atupe kuihubiri injili ya kweli na Mungu ataturudishia siku zetu zilizopotea hii haimaanishi kuwa ataturudisha tulikotoka au kwenye miaka ile ya zamani, lakini maana yake zitakuja nyakati za kuburudishwa ambazo roho zetu zitafurahi tena na tutasahu maumivu yetu, Mungu yuko tayari kuzifanya upya siku zetu yuko tayari kuziburudisha siku zetu na kuyafutilia mbali machozi yetu yote badala ya kukumbuka mambo ya zamani yeye ameahidi kufanya mambo mapya katika maisha yetu.

Matendo 3:19-21 “Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani; ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu.”

Isaya 43:18-19    “Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima 



Jumapili, 23 Novemba 2025

Je mama aweza kumsahau mtoto anayenyonya?

 

Isaya 49:14-16 “Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau.  Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.”




Utangulizi:

Upendo wa Mungu kwa watu wake ni mkubwa sana na wa kudumu, hata kuliko upendo wa mama anayenyonyesha, Mungu anajenga hoja kwa watu wake ambao walikuwa utumwani huko Babeli na walikuwa wanadhani ya kuwa kwa vile wanapita katika hali ngumu sana na wameonewa na adui zao kwa kiwango cha kusikitisha sana waliona kama Mungu amewaacha na pia kama vile amewasahau, akijibu hoja zao Mungu anaanza kwa kujibu manung’uniko yao kwa kuuliza swali Je mama aweza kumsahau mtoto anayenyonya? Asimuhurumie mwana watumbo lake? Kisha anasema hawa wanaweza, Lakini Mimi sitakusahau wewe! Mungu anatuonyesha kuwa yeye ana upendo na huruma ya kweli isiyotikisika kama ilivyo ya mama anyonyeshaye yeye ni zaidi! Yeye akionyesha jinsi wewe ulivyo wa muhimu kwake anasema amekuchora katika vitanga vya mikono yake.

Isaya 49:16-19 “Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.Watoto wako wafanya haraka, hao wakuharibuo, nao waliokufanya ukiwa, watatoka kwako.  Inua macho yako, ukatazame pande zote; hao wote wanajikusanya na kukujia. Kama niishivyo, asema Bwana, hakika utajivika na hao wote, kama kwa uzuri, nawe utajifungia hao, kama bibi arusi. Maana katika habari za mahali pako palipokuwa ukiwa, pasipokaliwa na watu, na nchi yako iliyoharibika hakika sasa utakuwa mwembamba usiwatoshe wenyeji wako, nao waliokumeza watakuwa mbali.”

Mungu anajizungumzia mwenyewe kuwa ni Mungu mwenye kujali, anajielezea kuwa huruma zake kwa watu wake sio za kawaida, upendo wake kwa watu wake hauwezi kufananishwa na lolote, yeye ana huruma na upendo na ni mwenye kujali kuliko mama anayenyonyesha, yaani kama mama anavyomuhurumia mwana wa tumbo lake, yeye ni zaidi, hakuna unachoweza kulinganisha naye namna anavyojali na kujihusisha na maisha ya watu wake, hakuna unachoweza kulinganisha nacho duniani, wote tunafahamu jinsi wakina mama wanavyowajali watoto wachanga lakini maelezo ya Mungu yanaonyesha kuwa kujali kwao huko hakuwezi kamwe kufananishwa na kujali kwa Mungu

Neno ameniacha katika lugha ya Kiebrania linasomeka kamaรขzab” kwa kiingereza fosake ambalo limetumiwa mara 129 na katika Kiyunani limetumika neno “aniฤ“mi” kwa kiingereza leave au abandoned  ambalo maana zake “turn away from entirely” sawa na neno kutelekeza katika Kiswahili au kuacha bila msaada au kukuacha kabisa katika ufafanuzi wa kutelekeza maana yake ni unyanyasaji wa kumuacha mtu anayehitaji msaada wako bila malezi au kumpa mahitaji yanayohitajika kwa kutokumjali, Mwanadamu anaweza kutelekeza na kuacha hata kitoto kichanga kinachonyonya lakini Mungu hawezi kukuacha wewe! Tutajifunza somo hili Je mama aweza kumsahau mtoto anayenyonya kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Yehova ameniacha, Bwana amenisahau.

·         Je mama aweza kumsahau mtoto anayenyonya.

·         Mimi sitakusahau wewe.


Yehova ameniacha, Bwana amenisahau

Isaya 49:14 “Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau.” Kulikuwa na manung’uniko miongoni mwa watu wa Mungu kutokana na hali ngumu walizokuwa wanazipitia wakaona ni kama Mungu amewaacha, na ni kama Mungu hawajali, Sayuni inawakilisha watu wa Mungu hapo, Sayuni ni mji wa Yerusalem na hapo unasimama kama uwakilishi wa watu wa Mungu, Mungu ameahidi mara nyingi katika neno lake ya kuwa atawasaidia watu wake na kuwaokoa, lakini wao walipokuwa wakiyatazama mazingira ya nje na hisia zao za ndani waliona kama wametelekezwa kama wameachwa, watu wa Mungu walichukuliwa utumwani na mfalme katili, mnyama sana, ambaye aliitiisha Dunia kwa hofu, akiiongoza dunia kwa mkono wa chuma yaani dikteta, alikuwa na nafsi ngumu sana katili mno, aliipiga Yerusalem yaani Sayuni, akaliharibu hekalu lao na kulitia moto, mji wote uliharibiwa, alikuwa tajiri sana kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufanya biashara, alikuwa na nguvu kiasi cha kusahau kuwa kuna Mungu na kutaka hata kuabudiwa yeye, aliwaonea watu wa Mungu na kuwafanyia unyama, Wayahudi walipelekwa utumwani kilomita 1448 sawa na miles 900 kwa miguu moja kwa moja bila kupumzika wala kupewa nafasi ya kuomba au kusali njiani, waliishi maisha ya huzuni Babeli na walilia sana walipokumbuka Sayuni nyumbani kwao.

Zaburi 137:1-4 “Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?

Kutokana na changamoto lukuki walizokuwa wamekutana nazo, waliona kuwa ni Dhahiri kuwa Mungu amewaacha na sio tu kuwa amewaacha lakini pia ni kama amewasahau, Mungu alikuwa amewaahidi kuwa atawaletea mwokozi, lakini hawakuona matumaini yoyote na badala yake hali yao ilizidi kuwa mbaya, Ndivyo wote tunavyofikiri kila wakati  na kujiona wakati hali inapokuwa mbaya, tunadhani ya kuwa maombi yetu hayasikiwi, hakuna mguso, hakuna uponyaji, hakuna nuru ni giza kila mahali, nasfi inasagika sagika tunanung’unika, tunalia tunadhani na kufikiri kuwa Mungu ametuacha, hivi ndivyo walivyokuwa wakifikiri Wayahudi wakati walipokuwa katika hali ngumu utumwani.

Je mama aweza kumsahau mtoto anayenyonya.

Kabla Mungu hajajibu hoja yao, aliwataka kwanza wafikiri kuhusu mfano wa mama anayenyonyesha, Mungu aliutumia mfano huu kwa sababu ulikuwa ni mfano uliokaribu na unaoleweka vema na wanadamu wote wenye akili timamu, mfano wa mama anayenyonyesha unajenga uzito mkubwa wa kisaokolojia, kihisia, na kiroho, kwa sababu

1.       Mama anayenyonyesha ana ukaribu wa hali ya juu sana na mwanaye – Ni vigumu sana Mama kuwa mbali na mtoto anayenyonya, na ndio maana utaweza kuona sio rahisi kumuacha hata kama mama ana safari mtoto anayenyonya yuko karibu sana na moyo wa mama yake na akili ya mama yake kwa hiyo kuna uhusiano wa karibu mno, mama anayenyonyesha akimtelekeza mtoto katika hali ya kawaida, kama hatafikiriwa kuwa ni katili basi huenda akafikiriwa kuwa hana akili, uhusiano wa mama na mtoto anyonyaye ni uhusiano wa asili uliokomaa na usioweza kutenganishwa katika mazingira yoyote kwa hiyo Mungu anatuthibitishia kuwa yeye anawahurumia watoto wake kuliko mama anayenyonyesha.

 

Zaburi 103:13-14 “Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.”

 

2.        Mama anayenyonyesha anaijua hali ya mtoto kwa ukaribu zaidi – Mama anayenyonyesha anaijua hali ya mtoto kwa ukaribu zaidi kuliko watu wengine nyumbani, anaweza kujua kama ana joto, njaa na hali nyingine yoyote anayoipitia, Mungu anaonyesha kupitia mfano wa mama anyonyeshaye ya kuwa yeye anatujua vema zaidi kuliko mtu awaye yote anatujua kukaa kwetu, kuamka kwetu na mawazo yetu na maneno yetu hata kabla hatujayasema na zaidi ya yote hata nywele zetu za kichwani yeye Mungu peke yake anajua idadi yake

 

Zaburi 139:1-4 “Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana.”  

 

Luka 12:6-7 “Je! Mashomoro watano hawauzwi kwa senti mbili? Wala hasahauliwi hata mmojawapo mbele za Mungu. Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi, bora ninyi kuliko mashomoro wengi.”

 

3.       Mama anayenyonyesha ni mwangalizi na mlinzi wa mtoto – Kitendo cha kunyonyesha humfanya mama awe mwangalizi wa karibu na wa muda wote wa mtoto na mlinzi, kwa hiyo mfano wa mama anayejali  unatufundisha ya kuwa Mungu ni mlinzi na mwangalizi wa karibu anayetuangalia usiku na mchana na hatuwezi kupotea katika macho yake, Mama mlezi hata wakati wa usiku halali wala hasinzii kwaajili ya kuhakikisha usalama wa mtoto

 

Zaburi 121:3-8 “Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye; Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli. Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume. Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku. Bwana atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.”

 

Isaya 46:3-4 “Nisikilizeni, enyi wa nyumba ya Yakobo, ninyi mlio mabaki ya nyumba ya Israeli, mliochukuliwa nami tangu tumboni, mlioinuliwa tangu mimbani; na hata uzee wenu mimi ndiye, na hata wakati wenu wa mvi nitawachukueni; nimefanya, nami nitachukua; naam, nitachukua na kuokoa.”

 

4.       Mama anayenyonyesha hawezi kusahau mtoto wake – haijawahi kutokea mama anayenyonyesha akasahau kuwa ana mtoto wake anayemtegemea yeye, Mungu anaonyesha kwa mfano huu kuwa hawezi kutusahau kamwe, na kulithibitisha hilo anasema wazi kuwa amatuchora katika vitanga vya mikono yake, wakati ambapo baba yako na mama yako wanaweza kukuacha yeye bwana anakupokea na kamwe hawezi kukuacha

 

Isaya 49:15-16    Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.”

 

Zaburi 27:9-10 “Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali Bwana atanikaribisha kwake.”

Kwa hiyo neno la Mungu linatuthibitishia kuwa ziko nyakati ambapo hata mama wa kawaida wa kibinadamu anaweza kumsahau mtoto anayenyonya, Lakini sivyo kwa Mungu, ninakumbuka kuna wakati ambapo, kulitokea ajali ya jahazi kwenye bahari huko Pemba kuja Pangani, wakati wa ajali hiyo maji yalianza kuingia kwenye jahazi, na matokeo yake baadhi ya kina mama kwa hofu ya kifo waliwatupa watoto wao baharini, upendo huu wa asili wa akina mama kuna wakati unagoma lakini upendo na huruma ya Mungu wetu haina wakati wa kugoma, Je mama aweza kumsahau mtoto wake anayenyonya? Huyo anaweza lakini sio Mungu wetu tunayemtegemea na kumuabudu.


Mimi sitakusahau wewe.

Isaya 49:14-16 “Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, Bwana amenisahau.  Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.”

Wakati jamii ilipokuwa inapitia changamoto za aina mbalimbali wao walidhani na kufikiri ya kuwa Mungu amewaacha na kuwasahau, Hata hivyo tunaona Mungu nanatumia mfano huo wenye mguso wa kupita kawaida kujijengea hoja madhubuti ili wanadamu waweze kufahamu jinsi Mungu wetu anavyojali, mama anapokuwa amemsahau mtoto kwa kawaida kibinadamu linakuwa ni jambo lenye kushangaza sana  wao wana upendo wa asili unaoumiza, Mungu anaonyesha kuwa yeye anaumia zaidi kuliko mwandamu wa kawaida na anaonyesha ya kuwa upendo wa mama unaweza kuharibika lakini sio wake, kwa hiyo hakuna makosa yanatokea katika maisha yako ukadhani Mungu amekosea au haoni, kila mwanadamu anapopita katika changamoto mbalimbli za maisha hufikiri kuwa Mungu amemuacha, Yesu pale Msalabani alilia Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha lakini Mungu alikuwa na mpango wa kumfufua mwanae na kumpaisha juu Mbinguni na kuweka adui zake wote chini ya miguu yake, yeye anathibitisha ya kuwa hata kama upendo wa mama unaweza kufikia ukingoni wake hauwezi, Mungu anakujua, Mungu anakufikiria, Mungu anakujali, Mungu anakulinda, Mungu anakulisha, Mungu anakutunza,  Mungu anatupenda kupita upendo wa kibinadamu na upendo wake ni wa milele kwa hiyo haupaswi kuogopa unayoyapitia

Yeremia 31:3 “Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu.”

Ziko nyakati katika maisha yetu unaweza kufikri kuwa umeachwa na Mungu, leo nataka tujikumbushe kuwa mawazo hayo ni batili, na hasi na sivyo ilivyo kwa Mungu wetu kutokana na maneno yake ya uzima, Kila mtu anaweza kukuacha lakini sio Mungu wetu ahadi zake ni ndio na kweli na kamwe hawezi kukusahau wewe, Yeye ni mwaminifu kama alivyoahidi atatenda.

“Je mama aweza kumsahau mtoto anayenyonya? Huyo aweza, lakini Mungu hatakusahau wewe”

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumapili, 16 Novemba 2025

Msigombane njiani!


Mwanzo 45:21-24 “Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani. Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili. Na babaye akampelekea kama hivi, punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula kwa babaye njiani. Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani.




Utangulizi:

Mojawapo ya agizo la msingi na la muhimu sana lililotolewa na Yusufu kwa ndugu zake ni pamoja na agizo hili, la “Msigombane njiani”, Agizo hili lilikuwa ni la muhimu na lenye kujenga umoja na amani ya kitaifa na kifamilia, hasa baada ya mafarakano, toba na msamaha na mapatano baada ya wana wa Israel kumuuza ndugu yao Yusufu utumwani ambako kwa neema ya Mungu alipata madaraka makubwa na akajitambulisha kwao, Yusufu anatoa maagizo haya ili kuilinda jamii yake wasiwe na mafarakano katika wakati wa mpito, kuelekea kwenye kuishi pamoja kwa furaha na amani kupitia mwaliko wake kwa familia nzima waje kuishi katika inchi ya Misri, wana wa Israel wangeliweza kuanza kushutumiana na kulaumiana kwaajili ya mambo yaliyopita wakati Yusufu amekwisha kutoa msamaha, maneno ya Yusufu kwao yanasimama kama onyo lenye kuweka msingi wa kuepusha migogoro njiani.

Neno la Mungu linaonya vikali kwamba katika vitu ambavyo ni chukizo kubwa kwa Mungu ni pamoja na kupanda mbegu ya fitina kati ya ndugu, yaani kugombanisha watu, Yusufu hakutaka kutoa ruhusa kwa ndugu zake ambao kimsingi aliwapima na kujua kuwa wamebadilika sana mioyoni mwao kwa hiyo asingelitoa nafasi ya wao kufarakana na kuumizana kwa sababu ya fitina na ugomvi kama wa mwanzo uliowafarakanisha wao na yeye kwa ndugu zake.

Mithali 6:16-19 “Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia;Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.”

Yusufu alikuwa amefahamu mpango wa Mungu, kwamba watu wanaweza kufarakana na kufitiniana lakini Mungu akawa amekusudia jambo jema katika fitina hizo na kutimiza mpango wake, kwa sababu hiyo sasa ulikuwa ni wakati wa kuhakikisha kuwa familia inakuwa na umoja, na inalinda mpango wa Mungu wa kuwa na amani, na kwa sababu hiyo agizo lake sio adhabu, bali ni somo la kiroho kwa jamii yake, taifa lake na ndugu zake kwamba wasigombane tena kwa sababu Mungu amekwisha kutimiza mpango wake kwao! Tutajifunza somo hili Msigombane njiani kwa kuzingatia vipengele muhimu vitatu vifuatavyo:-

·         Maana ya kugombana njiani

·         Msigombane njiani

·         Athari za kugombana njiani


Maana ya kugombana njiani

Mwanzo 45:21-24 “Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani. Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili. Na babaye akampelekea kama hivi, punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula kwa babaye njiani. Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani.

Moja ya jambo ambalo linavuruga sana umoja wa kifamilia, kitaifa na kijamii ni pamoja na ugomvi, kugombana kuna athari kubwa sana yaani athari hasi katika maisha ya mtu mmoja mmoja, wanandoa, jamii na taifa, watu wanaogombana wanaharibiana na kuleteana athari kubwa sana kimaisha, kihisia na mahusiano na kuacha majeraha ya uchungu, hasira, kisasi, chuki na mgawanyiko, kwa ujumla ninaweza kusema hakuna sumu mbaya katika mahusiano kama ugomvi, watu wanapoanza kugombana, kuchukiana na kuchochea hasira na migawanyiko, mwelekeo wake unakuwa ni kutengeneza matatizo makubwa zaidi yanayoharibu maisha hususani ya wale wanaohusika katika ugomvi huo, akilijua hili Yusufu katika hekima yake na akili yake aliwaonya ndugu zake kuwa wasigombane njiani!, kama kuna jambo huwa linasikitisha sana katika jamii ni kuishi katika jamii inayogombana!

Kugombana njiani hasa maana yake ni nini? Katika lugha ya asili ya Kiebrania neno kugombana linasomeka kama neno “ragaz” au “tirgำ™zแฟก” kwa Kiyunani “orgizethe”, au “orgฤ“” maana zake kwa kiingereza ni  fall not out”, “quarrel”, “argue”, “become troubled”, “disagree in words”, kwa Kiswahili tunaweza kusema “Msikosoane”, au “msikoseane”, “Msigombane” au “msibishane”, Msisumbuane”, au msileteane taabu, msisumbuane kwa meneno, au msikose kufikia muafaka,  na neno njia kwa kiyunani ni “hodล” ambalo maana yake ni safari ya maisha, kwa hiyo sio tu njia ya kawaida lakini katika maisha, kwa msingi huo neno la Mungu linamtaka kila mmoja katika jamii, wanandoa, kanisa, ndugu, jamaa, marafiki na taifa lolote kwamba wasigombane njiani, yaani wasiwe na mafarakano katika safari ya maisha, watu waache kuwa na uchungu, waache hasira, wasiwe watu wasiofikia muafaka, kimsingi mafarakano yoyote humzimisha Roho Mtakatifu na kuondoa maarifa, hekima na busara katika mioyo ya watu.

Yusufu alikuwa na ufahamu kuwa mambo mabaya yanaweza kutokea pale watu, ndugu, wanandoa au jamii na taifa kwa ujumla wakiruhusu magomvi, wanafungua ufunguo wa shina la uchungu, kupoteza umoja, kuruhusu mafarakano, migawanyiko na hata mauaji lakini sio hivyo tu watu wanaogombana wanafanya upumbavu na kumuhuzunisha Roho Mtakatifu, na kuthibitisha kuwa wao bado hawana ukomavu wa kiroho, kiakili na kifikra na wanaharibu uhusiano wao na Mungu na kutengeneza kizuizi kwa maombi na baraka za Mungu zilizokusudiwa katika maisha yao. Ugomvi huwaweka watu katika vifungo vya kiroho na kuweka ukwazo wa wao kufunguliwa na kuwahuru

Mithali 20:3 “Mtu kujitenga na ugomvi ni heshima kwake; Bali kila mpumbavu ataka kugombana”.

Mathayo 5:22-26.“Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.”

Msigombane njiani.

Mwanzo 45:24 “Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani.”  Kimsingi Yusufu alitoa agizo Msigombane njiani akiwa na uzoefu wa kutosha na mpana sana wa kutaka kuilinda jamii yake, kama kila Taifa, Kanisa, wanandoa  na jamii wanataka kujilinda ana aibu na kujilinda na kumpa shetani nafasi hawana budi kujilinda na mafarakakano, na ugomvi usio na tija, mtu mmoja Mwalimu wa zamani sana wa chuo cha Biblia Dodoma (AGBC) kwa sasa (CBC) Mwalimu Ndosi mwaka 2000 alisema hivi nanukuu “Watu wanapopendana huwa hatuulizi kwanini wamependana na wala hatuwaingilii, lakini watu wanapogombana tunaingilia na kuuliza ni kwanini wanagombana” mwisho wa kunukuu, Mwalimu Ndosi alikuwa anamaanisha kuwa watu wanapopendana huwa hakuna kelele kwa hiyo hakuna mtu anayesikia na kujua kuwa nini kinaendelea lakini watu wanapogombana kunakuwa na makelele na hivyo watu wengine huja kuingilia na kuuliza kwa nini mnagombana, ugomvi huleta aibu, na kumfanya kila mtu hata majirani kujiuliza kwanini hawa wanagombana, mnapopendana hakuna vikao, mnapogombana vikao vinaanza, mnapopendana mnafukuza maadui mnapogombana maadui wenu huanza kupata mwanya wa kuwaingilia na kuwavuruga zaidi hii ni kuanzia ngazi ya familia hadi ngazi ya kitaifa, hususani katika nyakati za leo ambako kuna uwazi mkubwa wa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii hamuwezi kujificha, Kaini na Habili walipoanza kuwa na mzozo kwa sababu ya wivu wa Kaini kwa nduguye, Mungu aliingilia kati na kuanza kuuliza, lakini walipoishi kwa umoja, amani na upendo hata Mungu hakuuliza maswali, kwani hali ilikuwa shwari.

Mwanzo 4:3-11 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua. BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;”

Kaini hakutenda haki, hakufanya vizuri, lakini Habili alitenda haki na alifanya vizuri, waliishi kwa utulivu lakini walipoanza kugombana Mungu alisikia ugomvi wao, Mungu aliingilia kati na Mungu alielekeza njia ya kufanya, Mungu amekusudia kumpa kibali kila mmoja, na amekusudi kumbariki kila mmoja jambo la msingi ni kila mtu kusimama katika wajibu wake na kutenda haki,  UKITENDA VEMA HUTAPATA KIBALI? agizo la kutokugombana njiani lilikuwa linamtaka kila mmoja kutokuwa sababu ya ugomvi na sababu ya malumbano katika jamii, kama viko vyama vya siasa vyama hivyo vina wajibu wa kuwatumikia wananchi na kuwatendea haki na kuwaletea maendeleo, tuko katika safari ya kuelekea kwenye kilele cha maendeleo na hakuna sababu ya kugombana njiani, kama mtu anahisi kupoteza kibali, njia sahihi ni kufanya vizuri na kutokugombana, kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu kwa maslahi mapana ya jamii na sio kwa manufaa ya watu wachache na ubinafsi, Yusufu aliwaasa ndugu zake kutokugombana sio kwa maslahi yao tu bali na masalahi ya familia nzima, alitaka kumlinda na Yakobo Baba yake, alifahamu kuwa ugomvi wa ndugu hawa njiani pia ungemuathiri Baba yao, ambaye alikuwa amedanganywa kuwa Yusufu amekufa na wakachukua kanzu yake na kuichana chana na kuitia damu na kumwambia Baba yao kuwa Yusufu amekufa!, Ugomvi wao ungemuhuzunisha mzee kule nyumbani na hasa kama sasa angejua ukweli kuwa sasa Yusufu yuko hai!.

Mwanzo 37:31-34 “Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi.”

Yusufu alikuwa anajua kuwa ugomvi wa kifamilia, kitaifa na kijamii unawahuzunisha sana wazee, alifahamu kuwa mgogoro wao unaweza kuwafikia wazazi na kuwafanya walie na kuhuzunika, wazee wetu ambao wametulea kwa shida na taabu mpaka tumekua wametuoza, wametusomesha na kuhakikisha ya kuwa tuna maisha haya tuliyo nayo wamestaafu na kutulia nyumbani, wamelitumikia taifa hili na kulipigania, wamepambana tangu kuipatia uhuru nchi yetu hatuwezi kuwalipa upumbavu, hatuwezi kuwapelekea maiti wala kanzu zilizojaa damu, mgogoro wa Kaini na Habili ulimuhuzunisha Adamu, migogoro yetu na ugomvi unahuzunisha watu wasio na hatia na kuwafanya wahuzunike na kujisikia vibaya, Mzozo na ugomvi ni aibu kubwa sana kwa familia, jamii na taifa msigombane njiani.

Wazee wetu wanahitaji habari njema, wanahitaji mavazi, chakula utulivu, Amani na kula mema ya nchi waliyoyataabikia na hawahitaji tena kusikia magomvi, wanahitaji kucheza na wajuu zao na sio kupelekewa kanzu zilizojaa damu, wala kupelekewa kazi ya kutatua migogoro ya ndoa zenu, wala kusikia habari mbaya wanahitaji habari njema iliyokamilika, mioyo yao ichangamke, Yakobo alipopokea habari njema roho yake ilifufuka ndani yake

Mwanzo 45:21-24 “Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani. Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili. Na babaye akampelekea kama hivi, punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula kwa babaye njiani. Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani.

Mwanzo 45:26-28 “Wakampasha habari, wakisema, Yusufu angali hai; naye ndiye mtawala katika nchi yote ya Misri. Moyo wake ukazimia, kwa sababu hakuwasadiki. Wakamwambia maneno yote ya Yusufu, aliyowaambia; na alipoona magari aliyoyapeleka Yusufu, ili kumchukua, roho ya Yakobo baba yao ikafufuka.Israeli akasema, Yatosha! Yusufu mwanangu angali hai; nitakwenda, nionane naye kabla sijafa.”

Israel/Yakobo alipopewa habari njema roho yake ikafufuka alisema neno moja tu YATOSHA hakutaka kusikia habari nyingine alijawa na furaha, aliona na magari aliyoletewa na mwanae; Je ugomvi wetu una manufaa gani kwa jamii, unamanufaa gani kwa watoto wetu, una manufaa gani kwa wanawake una manufaa gani hata kwetu wenyewe, ROHO YAKE IKAFUFUKA katika Kiebrania linatumika neno “Chรขyรขh” kwa kiingereza “recovered” au “repaired” Yakobo alipokea uponyaji wa roho yake kwa sababu alipokea habari njema na akasema “Yatosha” ameridhishwa na habari njema na taarifa njema hiki ndio familia inataka kusikia, hiki ndicho jamii inataka kusikia, hiki ndio taifa na watu wa Mungu yaani kanisa tunataka kusikia, habari za ugomvi na mafarakano katika jamii huongeza migandamizo ya mawazo, hurudisha watu nyuma, huleta majeraha na vidonda vya moyo na kuufisha moyo tuache kugombana!

Yusufu aliweka katazo lenye kuleta Baraka na kujenga umoja wa kijamii,kifamilia na kitaifa ambao kimsingi unaruhusu uwepo wa Mungu na kusababisha baraka kubwa sana, safari ya kutoka Misri mpaka Kanaani kwa kutembea pamoja na punda na ngamia ingeweza kuchukua kati ya siku 10 -14 muda huu kama usingelikuwa na onyo kama hili la msigombane njiani wangefika wakiwa wamevurugana vya kutosha lakini pia ilikuwa aibu kwa wageni waliombatana nao kwa magari maalumu yaliyokuwa yanaenda kumpelekea Yakobo zawadi na kumchukua kuja Misri

Zaburi 133:1-3 “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake. Kama umande wa Hermoni ushukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko Bwana alikoamuru baraka, Naam, uzima hata milele.”          

Athari za kugombana njiani.

Neno la Mungu linatupa uwanja mpana wa kuelewa kuwa ugomvi una athari hasi, na zenye kuharibu, mahusiano ya kijamii na maisha ya kiroho, watu wanaoanzisha magomvi wanafananishwa na watu au mtu anayetoboa mtumbwi ukiwa kwenye maji, na mafuriko yanaweza kuuzamisha na safari ikakwama.

Mithali 17:12-14 “Afadhali mtu akutwe na dubu aliyenyang'anywa watoto wake, Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake. Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake. Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji; Basi acheni ugomvi kabla haujafurika.”

Kwa hiyo tunajifunza kwamba kuna madhara au athari kubwa sana ya kimwili na kiroho na hata kisaikolojia inayosababishwa na ugomvi, na huenda Yusufu mwana wa Yakobo alikuwa na ufahamu huo na alitaka kuilinda na kuitunza familia yake kiroho na kimwili ili wawe na uhusiano mzuri na Mungu na pia wawe na uhusiano mzuri wao kwa wao hapa ziko athari kadhaa zitokanazo na kugombana njiani:-

ร˜  Kutokugombana njiani kunatujengea uhusiano mwema na Mungu, wakati migogoro na ugomvi unaweza kuharibu mawasiliano yetu na Mungu na kuzuia maombi na ibada, kutokugombana kuna athari chanya kwani kunatujengea uhusiano mwema na Mungu.  Wanandoa wanaogombana sio tu kuwa wanaiweka ndoa yao rehani, lakini pia wajue ibada zao, maombi yao na dua zao haziwezi kukubalika kwa Mungu kama kuna mtu hujamalizana naye, hujapatana naye na kuweka mambo vizuri, ibada yako na sadaka yako hazikubaliwi

 

1Petro 3:7-9 “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe. Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka.”

 

Mathayo 523-24 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.”

 

ร˜  Ugomvi ni dalili ya kutokukomaa kiroho na kifikra – Paulo mtume anawaona watu wenye mafarakano kama watu waliokosa ukomavu, watu walio wachanga na wenye kuonyesha udunia kama ni Wakristo basi wanaitwa Wakristo wa mwilini. Lakini jamii yoyote ile isiyokuwa na ukomavu na subira hishia katika ugomvi

 

1Wakorintho 3:1-3 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi,kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?

 

ร˜  Ugomvi humuuzunisha Roho Mtakatifu – watu wa Mungu wanapojihusisha na ugomvi, hasira, ghadhabu, uchungu, kelele na matukano ambayo kimsingi ni matunda au matokeo ya ugomvi humuuzunisha Roho Mtakatifu na kuanza kumfifisha katika kanisa la Mungu na jamii na taifa.

 

Waefeso 4:29-31 “Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;”

               

ร˜  Ugomvi unaweza kuwakosesha watu ufalme wa Mungu – Ugomvi ni moja ya matunda ya mwili au kazi za mwili, na wote wanaohusika na ugomvi kamwe hawawezi kuurithi ufalme wa Mungu.

 

Wagalatia 5:19-21 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.”

 

ร˜  Ugomvi ni hekima ya Shetani – Ugomvi ni chanzo na sababu ya dhambi nyingine, Shetani katika hekima yake anajua namna na jinsi ya kuondoa Amani miongoni mwa wanajamii na taifa kwa sababu hiyo ugomvi ni hekima ya shetani anajua kabisa katika magomvi atazalisha kiburi, mafarakano na kusababisha uharibifu mkubwa utakaozaa dhambi nyingine ikiwezekana hata mauaji, sio hivyo tu ataondoa Amani  kwa mfano hata wanandoa hawawezi kufurahia ndoa kama ugomvi unakuwa ni moja ya mtindo wa maisha kwa hiyo upendo huathiriwa, Yakobo anaonyesha kuwa hii ni hekima ya kishetani kwani yeye ndiye sababu ya machafuko!

 

Yakobo 3:15-17 “Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki.”

Hitimisho:

Neno la Mungu linatuagiza kwamba tutafute kwa bidii kuwa na amani na watu wote, nyakati za Biblia wazee wetu walihakikisha kuwa wanatafuta Amani kwa bidii, kwa kuwa tuko duniani hitilafu zinaweza kutokea lakini hitimisho lililobora kwa watu wa Mungu na watu wenye busara ni kuhakikisha kuwa wanazika tofauti zao na kuitafuta Amani kwa bidii na huo ndio moyo wa kiungu ambao wazee wetu wa imani walikuwa nao.

Warumi 12:18-20 “Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake.”                

Waebrania 12:14-15 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”            

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.