1Timotheo 6:6-10 “Walakini utauwa pamoja na
kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi
kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini
hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi
zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na
uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo
wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu
mengi.”
Utangulizi
Bila shaka umewahi kushuhudia
katika maisha haya kama mwanadamu kuwa unaweza kuwa na hamu au shauku ya kupata
kitu fulani na ukapambana mpaka ukakipata na baada ya kuwa umekipata ukaanza
kujuta moyoni, Hali hii inaweza ikatokea mara baada ya kufanya maamuzi kadhaa
katika maisha yetu kisha baada ya maamuzi hayo unasikia hisia za majuto,
unajiona kama umefanya maamuzi duni, ya kijinga na kipumbavu au kama umefanya
makosa ya kiufundi umekosea malengo, au hujafanya maamuzi sahihi, wakati
mwingine maamuzi ya aina hiyo yanaweza kuleta uchungu na hisia hasi na kuathiri
afya na maendeleo ya mtu, kimwili, kiroho na kisaikolojia, ingawa kujuta pia
kunaweza kujenga hisia chanya na kumfanya mtu kufanya maamuzi mazuri baadaye,
maa na yake ni nini?, si kila kitu tunachikitaka na kufanikiwa kukipata duniani
kinaweza kutuletea furaha, viko vitu vingine tunaweza tukavitamani sana lakini
baada ya kuvipata vinaweza kuwa chanzo cha maumivu makubwa na huzuni na majuto,
vitu hivyo inaweza kuwa mali, fedha, vyeo, mahusiano na kadhalika ambavyo
tumevipigania kuvipata kwa shauku/tamaa lakini baadaye vinatuletea maumivu.
Yakobo 4:3 “Vita vyatoka wapi, na mapigano
yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika
viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi
kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata
mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. Enyi
wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila
atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.”
Watu wengi sana duniani
wametamani sana kupata mali, vyeo, na hata mahusiano Fulani kwa tamaa zao,
lakini baadaye walijuta na kulia machozi, ni muhimu sana kupata lolote
tunalolitamani katika mapenzi ya Mungu na sio kwa tamaa ya kibinadamu, sio kila
kitu tunachokitaka duniani kinaweza kutupa raha, na furaha, vingine vinaweza
kutuletea maumivu, uchungu na majuto, mengi, wengi wamejilaumu wenyewe,
kujikosoa na kujisikia vibaya au kukata tamaa kwa sababu ya hali hii “Getting and regretting” yaani kupata
na kujuta kisaikolojia tendo hili linaitwa
“Cognitive dissonance” ambalo ni tendo la kukosa raha, baada ya mambo kwenda
kinyume na ulivyoamini!
Leo kwa msingi huo tutachukua
muda kujifunza somo hili Kupata na
kujuta kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-
·
Maana ya
kupata na kujuta
·
Kupata na
kujuta.
·
Jinsi ya
kupata katika mpango wa Mungu
Maana ya kupata na kujuta
Kupata na kujuta ni tendo la
kupata huzuni, kukata tamaa, kupata masononeko katika akili yanayokuja baada ya
kupata jambo fulani ambalo ulitarajia kuwa litakupa furaha lakini ukajutia kuwa
haikuwa kama ulivyokuwa unafikiri, na ukatamani kama ungelifanya vinginevyo,
hii ni mojawapo ya sehemu ya kawaida katika maisha ambayo imewakumba watu
wengi, aidha baada ya kupata nafasi fulani nzuri na kushindwa kuitumia au
kupata nafasi fulani wakaitumia lakini isilete furaha au matarajio
uliyoyafikiri, tendo hilo kisaokolojia linaitwa Cognitive dissonance – Psychological conflict resulting from
incongruous beliefs and attitudes held simultaneously, kwa Kiswahili
tunaweza kusema Majuto ni Matokeo ya mgogoro wa kisaikolojia unaotokana na kutokuenda
sawa kwa kile ulichikiamini au kukitarajia sawa na mtazamo ulioufikiria, Kwa Kiebrania
linatumika neno “Nâcham” naw- kham kimatamshi, kwa kiingereza to sigh – physical and emotional response to strong feeling like
grief, regret, repent Kwa mfano Mungu alipomuumba mwanadamu, aliatarajia
wanadamu wataishi kwa shukurani na utii kwa Mungu, lakini badala yake wanadamu wakaanza kuishi tofauti na kile
Mungu alichokuwa amekitarajia kwa hiyo Mungu alijuta, aidha Mungu alijuta pia
alipomtawaza Sauli akijua kuwa atatii yote anayomwagiza, lakini Sauli alirudi
nyuma asifuate aliyoagizwa na Mungu
Mwanzo 6: 1-6 “Ikawa wanadamu walipoanza
kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona
hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.
BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye
ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini. Nao Wanefili
walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia
kwa binti za binadamu, wakazaa nao wana; hao ndiyo waliokuwa watu hodari
zamani, watu wenye sifa. BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa
duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. BWANA
akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.”
1Samuel 15:10-11 “Ndipo neno la Bwana
likamjia Samweli, kusema, Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana
amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika,
akamlilia Bwana usiku kucha.”
Katika maandiko yote hayo lugha
ya kiebrania inayotumika ni “Nâcham” ikimaanisha kuwa Mungu
alijuta baada ya kuwa alifanya jambo kwa nia njema lakini baadaye hakupata
matokeo kama yale aliyokuwa ameyaamini au kuyategemea au kuyatarajia huu ni
mfano sasa wa kupata na kujuta, Katika maisha, kupata na kujuta kumewatokea
watu wengi sana na kunaendelea kuwatokea, Bwana ampe neema kila mmoja wetu
asitembee katika maisha ya majuto na badala yake aweze kufurahia maisha, Mungu
akupe akili hizo na ufahamu huo, isitokee ukaja kujuta katika maisha yako Ameeeeen
Kupata na kujuta.
Kila mwanadamu anapaswa kuwa
makini sana katika maeneo yote ya maamuzi katika maisha yake kwani kanuni
inayotumika hapo ndiyo ambayo inaweza kutuletea furaha au majuto, endapo
maamuzi yetu yatafanyika yakiwa yanaongozwa na tamaa na misukumo ya kibinadamu
bila kuzingatia ua kufikiri sana katika upana wake kwa njia za kiungu na
kutimiza mapenzi ya Mungu tunaweza kujikuta tunaingia katika kundi la watu
wanaojuta katika maisha yao, Neno llinatuasa:-
Mithali 3:5-7 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako
wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye,
Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana,
ukajiepushe na uovu.”
Maandiko yanaonyesha kuwa wako
watu wengi sana ambao walitazama kitu kwa mitazamo yao na kukitamani lakini
bila kuzingatia mapenzi ya Mungu na wakapata lakini walijuta sana baadaye
-
Hawa –
Mwanzo 3:6-7 “Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti
wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi
alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. Wakafumbuliwa
macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini,
wakajifanyia nguo.”
Adamu na Hawa
walijutia sana katika maisha yao na vizazi vyao swala zima la kutokumtii Mungu
na kufuata mapenzi yao kwa kula mti waliokatazwa na Mungu, wao waliutamani ule
mti na katika fikira zao walifikiri wanaweza kupata furaha wakala kwa tamaa ya
kufanana na Mungu, na kwa masikitiko makubwa wakagundua kuwa wameingia matatizoni
na wamekuwa uchi kabisa, uamuzi wao uliwapa kujuta siku zote za maisha yao
kupata na kujuta
-
Lutu – alifanya uamuzi wa kuchagua kuishi katika
bonde la Sodoma ambalo kwa macho ya kawaida liloonekana kuwa kama bonde la
Mungu, ardhi ilikuwa nzuri yenye kuvutia na akaamua kuishi huko nadhani pia
alioa huko, alipata lakini alitoka na majuto kwani alipoteza kila kitu
alichokuwa nacho na hata mkewe pia na kujikuta akiishi katika pango akiwa
masikini na asiyekuwa na kitu, na kuishia katika uvunjifu mkubwa wa kimaadili
uliochagiwa bintize.
Mwanzo 13:10-13 “Lutu
akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina
maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA,
kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari. Basi Lutu akajichagulia Bonde lote
la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao.
Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde;
akajongeza hema yake mpaka Sodoma.Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye
kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA.”
Mwanzo 19:26-30 “Lakini
mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi. Ibrahimu akatoka
asubuhi kwenda mahali aliposimama mbele za BWANA, naye akatazama upande wa
Sodoma na Gomora na nchi yote ya hilo Bonde, akaona, na tazama, moshi wa nchi
ukapanda, kama moshi wa tanuru. Ikawa Mungu alipoiharibu miji ya Bondeni, Mungu
akamkumbuka Ibrahimu, akamtoa Lutu katika maangamizi alipoiangamiza miji hiyo
aliyokaa Lutu.Lutu akapanda kutoka Soari akakaa mlimani, na binti zake wawili
pamoja naye, kwa sababu aliogopa kukaa katika Soari. Akakaa katika pango, yeye
na binti zake wawili.”
-
Amnoni
mwana wa Daudi alimpenda sana Tamari binti ya baba yake alimpenda sana
mpaka akawa anakonda na kuumwa, alimtamani sana alimpenda mno ndio maandiko
yanavyotueleza mpaka akapanga mikakati ya kumpata kwa hila, hata hivyo baada ya
kumpata tu neno la Mungu linasema alimchukia machukio makuu sana kuliko yale
mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza jambo hili lilimfanya apate lakini ajute
2Samuel 13:11-19 “Naye
alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo
ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze
nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami
nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli.
Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini
yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye,
akamtenza nguvu, akalala naye. Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa
kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda
kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako. Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa
mabaya haya ya kunitoa ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa
kumsikiliza. Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa
mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake. Naye alikuwa amevaa kanzu
ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo
mtumishi wake akamleta nje, akafunga mlango nyuma yake. Naye Tamari akatia
majivu kichwani mwake, akairarua hiyo kanzu ndefu yake aliyoivaa, akaweka mkono
kichwani akaenda zake huku akilia kwa sauti.”
-
Yuda
Iskariote – alitamani sana fedha, alifahamu au kudhani ya kuwa anaweza
kumsaliti Yesu Kwa vipande 30 vya fedha, akidhani kuwa labda Yesu angeliponyoka
katika mikono ya adui zake, hakufikiri kwa kina zaidi ya tamaa zake lakini
baadaye alijutia sana umauzi wake alizitupa fedha hizo na kwenda kujinyonga,
kupata fedha sio kubaya lakini kutafuta fedha nje ya mapenzi ya Mungu au kufanya
mambo kwa tamaa ni jambo baya sana linaloweza kutuletea majuto, Kwa hiyo Yusa
alifanikuwa kupata fedha kwa kumsaliti yetu Lakini alijutia
Mathayo 26:14-16 “Wakati
huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa
makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia
vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate
kumsaliti.”
Mathayo 27:1-5 “Na
ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu
ya Yesu, wapate kumwua; wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato
aliyekuwa liwali. Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha
kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande
thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.
Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe. Akavitupa
vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga.”
Kusudi la Mungu ni kumtunza
mwanadamu na maumivu mengi, kumlinda mwanadamu dhidi ya tamaa, kumkumbusha
mwanadamu ya kuwa anapaswa sana kumtegemea Mungu katika maamuzi yake yote na
njia zake zote, wanadamu wengi sana waliookoka na wale wasiookoka wamejikuta
katika madhara makubwa kwa sababu ya kuongozwa na tamaa na matakwa yao wenyewe,
ni vema kila unapofika wakati wa kufanya maamuzi watu wakawa wanautafuta uso wa
Mungu kwa bidii ili kuyapata mapenzi ya Mungu badala ya kuzifuata njia zetu
wenyewe ambazo baadaye zinaweza kutuletea majuto, Neno la Mungu linayo maelekezo
ya kutosha ya namna ya kupata yale tuyatakayo katika mapenzi ya Mungu na ikiwa
hivyo katika maisha yetu tutaepuka kwa kiwango kikubwa kujuta.
Mithali 14:12-14 “Iko njia ionekanayo kuwa
sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti. Hata wakati wa
kucheka moyo huwa na huzuni; Na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo. Ageukaye
moyoni hushiba njia zake mwenyewe; Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake.”
Jinsi ya kupata katika mpango wa Mungu
Maisha yamejaa majuto mengi sana
wako watu wanajuta kwa sababu mbalimbali katika maisha walipata lakini
wanajuta, ukifanya utafiti, wako watu wamechoka mno mioyo yao imejaa simamzi na
uchungu kwa sababu walipata au walifanya jitihada za kupata lakini wanajuta kwa
namna moja ama nyingine, yale waliyoyapigania ili wapate yalileta majuto badala
ya furaha, yale yaliowapotezea muda mwingi sana wakawekeza huko yakawalipa
mabaya wasiotarajia, sasa wanajuta, wako wanaojuta kwa sababu, Walipopata kazi,
walifanya kazi kwa bidii na kwa kujituma sana lakini hawakutoa muda wa kutosha
kwa familia zao, marafiki zao na ndugu na jamaa, wakati wote walikuwa bize na
kazi zao lakini walipojikuta wako vitandani na wanakaribia kufa walijuta kwa
sababu kazi walizipata na fedha
walizipata lakini walijikuta wanafanya kazi sana na kutumia masaa mengi
makazini na wakakosa wakati muhimu wa kuwa na familia zao, nahata kuwaweka sawa
watoto wao, wanakuja kubaini watoto wamepotoka, wamekuwa bila upendo wa baba na
mama,
Wako waliokataa wachumba zao kwa
sababu walichelewa kuwaoa kwa sababu ya umasikini, nitamsubiria mpaka lini, mtu
akaamua kuolewa na kijana aliyejitokeza kwa sababu ana kazi nzuri na gari
nzuri, na pesa bila kujiuliza alivipataje lakini baada ya maisha kuendelea
maisha yalitoa majibu tofauti, walipoteza upendo wa dhati kwa sababu ya vitu
vinavyoonekana kwa muda sasa wanajuta
Wako watu ambao hawakuishi maisha
yao halisi, na badala yake waliishi maisha ya kuigiza, wakitaka kuwafurahisha wengine
walifurahia kusifiwa na kutambuliwa na watu, hawakuchagua ndoto zao walichagua
ndoto za wazazi wao, hawakuchagua waume au wake waliowapenda wakachagua wale
waliopendekezwa kwao na wachungaji, mabosi wao na vinginevyo, hawakuchagua kazi
zao na fani zao walichagua kile dunia inakitaka kwaajili yao na wakawekeza muda
wao huko na sasa wanajuta
Wako watu ambao wanajuta kwa
sababu hawakuwa na muda wa kutunza afya zao, waliishi maisha ya hovyo, mabaya,
hawakuwa na muda wa kutengeneza na watu, waliharibu mahusiano, na watu, familia
zao na kupuuzia mapatano, na sasa wanajuta, wako waliopuuzia muda wa kulala, muda wa kufanya mazoezi,
walikunywa misoda na mavitu ya Super-market na sasa wanagundua kuwa wameharibu
kila kitu wana huzuni kwa sababu hawakufanya mazoezi, wana huzuni kwa sababu
hawakuzingatia lishe bora, wana huzuni, kwa sababu hawakufanya mapatano, wana
huzuni kwa sababu hawakuwa wanalala usingizi wa kutosha afya zimeharibika na
sasa wanajuta, wako hata waliokuwa wakifunga kwa kusudi la kuutafuta uso wa
Bwana lakini walifunga hovyo hovyo bila kuzingatia kanuni za afya na sasa wana
madonda ya tumbo, na hawawezi kufunga tena na wanajuta
Wako watu ambao wanajuta kwa
sababu hawakuwekeza, hawakuweka akiba za kutosha hawakufikiri mambo ya baadaye
sasa ni masikini, hawana fedha, hawakuwekeza mashamba wala mifugo hawakujali
tabia zao zitawaletea matunda gani ya baadaye na sasa wanajuta, hawakupanga
wanazaa watoto wangapi na kwa kiasi gani, wao kila kilichotokea kiliwatokea
kama bahati tu, wako wanaojuta kwa usaliti, kupigania vyeo wakavipata lakini
baadaye wakajuta hata kwanini walipigania vyeo hivyo, kutaka umaarufu, kuoa au
kuolewa na watu wasio sahihi na kadhalika na sasa wao wako Jehanamu ya moto wa
ndoa zao wakati wengine wako Paradiso umepata lakini unajuta!, wako
waliozalishwa wakiwa nyumbani, waliona raha kujirusha lakini sasa wanajuta, wako
ambao wameolewa na kuachika, wako waliotoa talaka na wanajuta, wako waliodai
talaka na sasa wanajuta hii ndio hali
halisi ya Dunia pale tunapofanya mambo na kuchagua mambo kwa kuyapa uthamani wa
kwetu wenyewe machoni petu wenyewe na kufanya mambo ambayo yanaweza
kutufurahisha kwa muda mfupi badala ya kuwaza yatakayotufurahisha kwa muda
mrefu, chaguzi za namna hiyo ni chaguzi za kiesharati kwa mujibu wa maelekezo ya
kimaandiko, mwesharati ni mtu anayewaza kumaliza haja zake za muda mfupi tu na
ikamgharimu maisha yake, badala ya kufikiri mbele hii ilikuwa changamoto ya
Esau ambaye alijuta sana baadaye baada ya kuuza urithi wake kwa sikumoja.
Waebrania 12:16-17 “Asiwepo mwasherati wala
asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa
ajili ya chakula kimoja. Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi Baraka,
alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi.”
Wewe hapo ulipo ulitamani nini na
ukakitafuta na kukipigania kwa nguvu zako zote na ukakipata lakini sasa unajuta
moyoni, wako watu wengi wenye majuto ya kila aina hapa duniani na wewe sio wa
kwanza sisi kama wanadamu tunaweza kufanya maamuzi ambayo baadae yanaweza
kutuletea majuto makubwa sana katika mioyo yetu! Tufanyeje tujiue, turudi nyuma
hapana tunashauriwa cha kufanya Na maandiko
Ufanyeje sasa ili usishi kwa majuto?
Mungu wakati mwingine anatutaka
tuwe na subira, subira hupita njia ndefu na ngumu sana na ndio maana watu wengi
hawaipendi njia hii, ni njia ngumu lakini inaweza kutuletea matokeo mazuri ya
kiungu na kuiungwana unajua Mungu hufanya mambo kwa wakati, lakini mwanadamu
hutaka matokeo ya haraka na ni vigumu kwetu kuvumilia na kusubiri wakati wa
Mungu, kwa haraka zetu.
Muhubiri 3:11 “Kila kitu amekifanya kizuri
kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi
mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata
mwisho.”
Mungu anatutaka tutangulize faida
za kiroho kabla ya zile faida za mwilini, wengi wanaopitia njia za majuto ni
wale ambao tunafikiri kwa jinsi ya mwili, kwa kuangalia vinavyoonekana na
kupuuzia vile visivyoonekana ambayo kwa asili ni vya milele na hutupa furaha ya
kudumu, ni lazima tuutafute kwanza ufalme wa Mungu na haki yake na mengine yote
tutazidishiwa
Luka 12:16-21 “Akawaambia mithali, akisema,
Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake,
akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema,
Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo
nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu,
una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule,
unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo
wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo
alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”
Nadhani kila unapofikia wakati wowote
katika maisha mahali ambapo tunataka kufanya uamuzi basi ni vema sana
tukatafuta sana mapenzi ya Mungu na uongozi wa Mungu neno linasema usizitegemee
akili zako mwenyewe bali katika njia zako zote mtegemee Mungu
Warumi 8:13-16 “kwa maana kama tukiishi kwa
kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa
Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa
Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho
ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe
hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;”
Mithali 3:5-7 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako
wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye,
Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana,
ukajiepushe na uovu.”
Linda dhamiri yako wakati wote
unapotaka jambo - unataka hicho unachokitaka kwa sababu gani? Mungu huangalia
nia ya moyo na kuhukumu kulingana na nia ya moyo, kama kuna kitu unakihitaji
lakini kwa tamaa unaweza usipewe au unaweza ukapewa lakini kikakutokea puani
Hesabu 11:18-20 “Kisha uwaambie watu hawa,
Jitakaseni nafsi zenu kabla ya kesho, nanyi mtakula nyama; kwa maana mmelia
masikioni mwa Bwana, mkisema, Ni nani atakayetupa nyama, tule? Maana huko Misri
tulikuwa na uheri. Basi kwa sababu hiyo Bwana atawapa nyama, nanyi
mtakula.Hamtakula siku moja, wala siku mbili, wala siku tano, wala siku kumi,
wala siku ishirini; lakini mtakula muda wa mwezi mzima, hata hapo nyama hiyo
itakapotoka katika mianzi ya pua zenu, nanyi mtaikinai, kwa sababu mmemkataa
Bwana aliye kati yenu, na kulia mbele zake, mkisema, Tulitoka Misri kwa maana
gani?”
Hata kama tumemkosea Mungu na
ikaleta majuto katika maisha yetu, ni Muhimu kwetu tukamrudia Mungu huyo huyo,
kwa toba, kukiri, na kuutafuta uso wake tena, Upendo wa Mungu na rehema zake
hauna mipaka, tukinyenyekea kwake atatupokea tena kama ilivyokuwa kwa mwana
mpotevu, kupoteza kwetu sio mwisho wa maisha, kwani Baba wa rehema anayi nafasi
nyingine, ttutafute uwepo wake naye atatutia nguvu na kuturejesha tena
Luka 15:17-20 “Alipozingatia moyoni mwake,
alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na
mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na
kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana
wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye.
Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio
akamwangukia shingoni, akambusu sana.”
Hitimisho:
Mpango wa kamili wa Mungu ni kila
mmoja wetu kuyafurahia maisha, Mungu kama Baba aliye mwema anatufikiria mema na
yuko kwaajili yetu, lakini pia yule muovu yuko, hata hivyo pamoja na kuweko kwa
yule muovu, na majaribu mbalimbali mpango wa Mungu ni kuhakikisha ya kuwa
anatubariki na kutupa mambo ya kudumu ambayo kimsingi hatachanganya nayo na
huzuni wala majuto. Baraka za kweli kutoka kwa Mungu ni zile zinazokuja kwetu
na hazituletei majuto, ukipata katika mpango wa Mungu bila ya hila, utaufurahia
uwepo wa Mungu maisha yako yote, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa na
Baraka za Mungu zisizo changamana na huzuni wala majuto. Amen
Mithali 10:22 “Baraka ya Bwana hutajirisha,
Wala hachanganyi huzuni nayo.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni