Jumanne, 30 Desemba 2025

Tengeneza mambo ya nyumba yako!

 


2Wafalme 20:1-3 “Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana akasema, Nakusihi, Bwana, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.”


Utangulizi:

Moja ya wafalme na watawala wa ufalme wa Yuda aliyekuwa mwaminifu sana ni pamoja na Hezekia, Ni mfalme aliyemcha Mungu na kufanya mapinduzi makubwa ya uamsho ikiwa ni pamoja na kurejesha ibada ya Mungu wa kweli katika Hekalu lililokuwako Yerusalem na kukomesha kabisa ibada za kipagani, taarifa zake zinapatikana katika kitabu cha Wafalme wa pili, Nyakati wa pili na kitabu cha nabii Isaya, ambako kote anasifiwa kama mtawala mcha Mungu, ambaye alimtegemea Mungu hata wakati wa vita mbalimbali, Yeye alikuwa ni wa uzao wa Daudi na anayefikiriwa kama moja ya viongozi wacha Mungu sana, hata hivyo habari yake maarufu zaidi ni pamoja na habari zake za kuugua sana na akiwa katika kuugua huko akapokea onyo kali kupitia nabii Isaya kuwa atengeneze mambo ya nyumba yake kwani atakufa  na wala hatapona, jambo lilopelekea yeye kumlilia Mungu na kuomba kwa machozi.

Isaya 38:1-3 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.”

Mara kadhaa tumehubiri sana kuhusu kisa hiki na kuonyesha nguvu za maombi na hasa maombi ya kulia sana na machozi na tumehubiri vile vile kuhusu swala zima la Hezekia kuongezwa miaka 15, lakini ni vigumu sana kuwasikia wahubiri wakieleza ni kwa nini mfalme huyu mwaminifu alitakiwa atengeneze mambo ya nyumba yake? Na ni kwa nini alipewa karipio kali kuwa hatapona bali atakufa? Tena akiwa anaumwa! Na kwanini Mungu alikuwa ameahirisha mpango wake na kumuongezea miaka? Ni changamoto gani ilikuweko nyuma ya karipio hili ambalo kimsingi linaweza kuwa ndio sababu ya mkasa huu mzima! Leo Roho Mtakatifu anatuwekea wazi, kuhusiana na swala hilo. Tutajifunza somo hili tengeneza mambo ya nyumba yako kwa kuligawa katika vipengele vikuu vitatu muhimu vifuatavyo:-

 

·         Tengeneza mambo ya nyumba yako.

·         Sababu za kutengeneza mambo ya nyumba yako.

·         Jinsi ya kutengeneza mambo ya nyumba yako.


Tengeneza mambo ya nyumba yako.

Isaya 38:1 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.”

Hezekia aliyekuwa mfalme mwaminifu katika utawala wa Yuda, ambaye alisababisha mabadiliko makubwa sana ya kiimani na kuleta uamsho mkubwa sana, alitakasa Hekalu, na kuharibu madhabahu za kipagani na ibada za sanamu, na kurejesha ibada sahihi za Mungu aliye hai, na sikukuu za Pasaka tofauti na Ahazi baba yake, Hezekia alikuwa mtu wa imani na maombi, mtu aliyemtegemea sana Mungu kiasi ambacho aliwahi kushinda vita kwa kupiganiwa na Malaika baada ya kuitisha mfungo na Mungu akaingilia kati dhidi ya majeshi ya Waashuru chini ya Senakeribu.

2Nyakati 32:20-22 “Na kwa ajili ya hayo Hezekia mfalme, na Isaya nabii, mwana wa Amozi, wakaomba, wakalia hata mbinguni. Naye Bwana akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga. Ndivyo Bwana alivyomwokoa Hezekia, na wenyeji wa Yerusalemu, na mkono wa Senakeribu, mfalme wa Ashuru, na mikononi mwa wote, akawaongoza pande zote.”

Hezekia pia alijenga mradi wa maji maarufu kama mfereji wa Hezekia (Hezekiah’s tunnel) unaopitisha maji chini kwa chini katika mji wa Yerusalem wa zamani kama njia ya kujikinga na maadui endapo atazingirwa pande zote mfereji huo maarufu wa maji uko hata siku za leo, Anatambuliwa kama moja ya wafalme maarufu sana na mfano mzuri wa kuigwa akionyesha imani kwa Mungu na maombi na anatajwa katika ukoo wa masihi katika agano jipya kwenye kitabu cha Mathayo kama moja ya mababu waliomleta Yesu Kristo ulimwenguni kwa uzao wa Daudi. Ona:-

Mathayo 1:6-9 “Yese akamzaa mfalme Daudi. Daudi akamzaa Sulemani kwa yule mke wa Uria; Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa; Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia; Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia;

Hata pamoja na sifa hizi njema tunaona ghafla baadae alianza kuugua jipu baya sana na akiwa katika maradhi haya mabaya na katika hali ya kuugua na kuumwa, Isaya nabii anatumwa na Mungu kwenda kumpa ujumbe ya kwamba atakufa na wala hatapona na hivyo atengeneze mambo ya nyumba yake, kwa nini mfalme huyu mwadilifu anatamkiwa maneno makali hivi ya kutisha tena akiwa katika wakati wa kuumwa? Na kwa nini onyo alilopewa na nabii linaonekana kuwa ni onyo kali sana na kisha katika namna ya kushangaza baada ya kuomba kwake linaahirishwa kwa haraka baada ya maombi na anaongezewa miaka 15? Nini kilipelekea Hezekia apewe onyo hili kali Tengeneza mambo ya nyumba yako maana utakufa wala hutapona, tunajifunza nini kwenye hili?

Isaya 38:1 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.”

Sababu za kutengeneza mambo ya nyumba yako.

Mungu alimtuma nabii Isaya kumuonya Mfalme Hezekia na kumtaka atengeneze mambo ya nyumba yake, kwa ujumla sababu za kwanini onyo hili lilikuwa kali kiasi hiki haliko wazi sana katika Biblia Lakini unaweza kupata picha ya wazi kwamba Hezekia alikuwa na kiburi na ubinafsi uliopitiliza ambao ungeweza kuzuia mapenzi ya Mungu, alikuwa ni mtu aliyejihesabia haki kupita kawaida na hakuwa mtu mwenye kuamini haki ya wengine, Mfalme Hezekia alinyooshwa katika ugonjwa mzito na angekufa kweli, lakini Mungu hawezi kujipinga mwenyewe hivyo alimuongeza miaka 15 kwa sababu maalumu na za msingi sana ambazo tutaziangalia hapa:-

1.       Hezekia alikuwa ni mfalme ambaye hakuwa ameoa wala hakuwa anataka kuoa kwa mujibu wa maelezo ya tamaduni za kiyahudi Hezekia alikuwa anaogopa kuwa akioa na kuzaa mtoto anaweza kuzaa watoto wasio na haki na wasiomcha Mungu kama alivyo yeye na hivyo wangeweza kumuudhi Mungu, hivyo alijiamini mwenyewe na kujihesabia haki, akidhani kuwa wengine hawataweza kuwa kama yeye, kwa hiyo aliamini ni afadhali asioe kuliko kuoa na kuzaa watoto watakaomkosea Mungu, Mungu alichukizwa sana na mawazo ya Hezekia kwa sababu kama angelikufa bila kuzaa watoto, utawala wa Yuda ungekosa mfalme wa nasaba ya Daudi jambo ambalo lingevunja ahadi ya  mpango wa Mungu kwa utawala wa kudumu kwa uzao wa Daudi;-

 

2Samuel 7:12-16 “Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu; lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.”

 

Mwanzo 49:8-10 “Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia.Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemwamsha? Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.”

 

2.       Hezekia  alikuwa ni mfalme asiyetazama mbali; hata wakati anaumwa kwa muda mrefu bado alikuwa hafikirii lolote kuhusu uongozi ujao, alikuwa amejaa ubinafsi akijifikiri yeye mwenyewe, Mungu alimchungulia wakati anaumwa ikaonekana kuwa anafikiria kumaliza vizuri na Mungu lakini hakuwaza kamwe kuandaa kiongozi mwingine kwaajili ya kuendeleza uongozi ujao baada yake, wala hakuwaza kuwa watu wake wataongozwaje, alikuwa mfalme mwema na wa kiroho lakini mbinafsi, Mrithi alitakiwa kuandaliwa aone shughuli za kifalme na kujifunza maswala ya utawala hata kabla ya kifo chake lakini yeye hakuliangalia hilo, Neno tengeneza mambo ya nyumba yako katika lugha ya kiebrania ni “tsâvâh” ambalo maana yake kwa kiingereza ni appoint, au command au charge, set officially, arrange, determine, give orders, give instruction, show direction, chagua, Amuru, weka mtu mbadala, tangaza, andaa mrithi wako, amua, weka utaratibu, toa maelekezo, onyesha muelekeo lilikuwa ni agizo ambalo lingemfanya Hezekia akili zake zimrudie na afikiri kwa kina, nani anaweza kumrithi katika kiti cha ufalme baada yake,Kama yeye atakufa nini kitafuata, Sababu zake hazikuwa za msingi kwa Mungu, woga wake na hofu yake haikuwa na maana kwa Mungu, swala la uzao wake watakuaje watamcha Mungu au la, halikuwa linamuhusu  huwezi kuingilia na kuamua mambo ya Mungu ndani ya mtu mwingine ni kazi ya Mungu kujua nani atakuwa mwema au itakuwaje, ni wajibu wa Mungu kujua kuwa ajaye atafaa watu wake ama itakuwaje sio wewe, Kwa hiyo Hezekia alitakiwa kuoa na kuzaa na kumuandaa mfalme ajaye ili baada yake kazi ya Mungu iendelee, na uzao wa Daudi uendelee, yeye hakufanya hivyo, Musa aliandaa mtu ambaye angeshika madaraka baada yake  na Daudi aliandaa utaratibu wa mfalme ajaye na hata majukumu yake watu walijua baada ya Daudi nini kitafuata, Mungu alimuagiza hata Eliya kumuandaa Elisha kuwa nabii baada yake na alumuandaa hivyo mapema, kumbe viongozi huandaliwa:-

 

Hesabu 27: 18-23 “Bwana akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako; kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao. Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii. Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za Bwana; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia. Musa akafanya kama Bwana alivyomwamuru; akamtwaa Yoshua, akamweka mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote;kisha akaweka mikono yake juu yake, akampa mausia, kama Bwana alivyosema kwa mkono wa Musa.”

 

1Nyakati 28:1-9 “Kisha Daudi akawakusanya huko Yerusalemu wakuu wote wa Israeli, wakuu wa kabila, na maakida wa vikosi wenye kumtumikia mfalme kwa zamu, na maakida wa maelfu, na maakida wa mamia, na wenye kutawala juu ya mali na milki za mfalme, na za wanawe, pamoja na matowashi, na mashujaa, naam, waume mashujaa wote. Ndipo Daudi mfalme akasimama kwa miguu yake, akasema, Nisikilizeni, ndugu zangu, na watu wangu; Mimi nalikuwa na nia ya kuijenga nyumba ya kustarehe kwa ajili ya sanduku la agano la Bwana, na kiti cha kuwekea miguu yake cha Mungu wetu; hata nalikuwa nimeweka tayari kwa kujenga. Lakini Mungu akaniambia, Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umekuwa mtu wa vita, nawe umemwaga damu. Walakini Bwana, Mungu wa Israeli, alinichagua katika nyumba yote ya babangu kuwa mfalme juu ya Israeli milele, kwa kuwa amemchagua Yuda awe mkuu; na katika nyumba ya Yuda, alichagua nyumba ya babangu, na miongoni mwa wana wa babangu, aliniridhia mimi ili kunitawaza niwe mfalme juu ya Israeli wote; tena katika wana wangu wote (kwani Bwana amenipa wana wengi), amemchagua Sulemani mwanangu ili aketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wa Bwana, juu ya Israeli. Akaniambia, Sulemani, mwanao, ndiye atakayeijenga nyumba yangu na nyua zangu; kwa kuwa nimemchagua awe mwanangu, nami nitakuwa babaye. Na ufalme wake nitauweka imara milele, akijitia kwa bidii kuzitenda amri zangu na hukumu zangu, kama hivi leo. Basi sasa, machoni pa Israeli wote, hilo kusanyiko la Bwana, na masikioni pa Mungu wetu, angalieni na kuzitafuta amri zote za Bwana, Mungu wenu, ili mpate kuimiliki nchi hii njema, na kuwarithisha wana wenu baada yenu hata milele. Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa Bwana hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele.”

 

1Wafalme 19:15-17 “Bwana akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako.Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua.”

 

3.       Hezekia alikuwa anaamuriwa kuweka utaratibu, alikuwa ni kiongozi mzuri sana na mwema lakini alikuwa haandai utaratibu, angeacha mambo hayana hata muelekeo baada ya kifo chake, je hujawahi kuona viongozi wanaanzisha taasisi kisha wakifa wao nazo zinakufa? Watu wanaobaki wanakuwa hawajui hata la kufanya wote wanamtegemea yeye tu, Mungu ni Mungu wa utaratibu, Hezekia alikuwa hafiriki lolote kuhusu utaratibu utakuwaje baada yake wakati wenzake waliomtangulia walikuwa ni watu walioweka utaratibu yeye hata mke wa kuoa alikuwa anaogopa kuwa hatapata mke mcha Mungu na hivyo hatakuwa na watoto wazuri wala haonyeshi mrithi wake ni nani na nini kifanyike baada yake, kwa kufanya hivi ni kama alikuwa anazuia mpango wa Mungu wa baadaye, kila kiongozi kuanzia ngazi ya kifamilia anapaswa kukumbuka kuwa sisi ni wapitaji duniani, na baada ya kuongoza kwetu basi lazima aweko kiongozi mwingine na taratibu za baadae

 

Yehoshafati aliweka utaratibu mzuri sana wa kiserikali na kimaamuzi kabla ya kifo chake, Hezekia yeye alikaa kimya tu, anaugua na haweki mipango mingine vizuri, yalikuwa ni mawazo mabaya hakuwa kiongozi mbaya alimcha Mungu lakini hakuwa akifikiri zaidi ya mambo katika jicho la kiungu, hakuwaza kazi ya Mungu baada yake itakuwaje, kiongozi ambaye angemrithi angekosa hata pa kuanzia hajui aanzie wapi, hii ilikuwa changamoto yake ona mfano wa Yehoshafati yeye aliweka taratibu nzuri za kimaongozi na kiserikali ona!

 

2Nyakati 19:4-11 “Na Yehoshafati akakaa Yerusalemu; akatoka tena kwenda kati ya watu toka Beer-sheba mpaka milima ya Efraimu, akawarudisha kwa Bwana, Mungu wa baba zao. Akasimamisha makadhi katika nchi, katikati ya miji yote yenye maboma ya Yuda, mji kwa mji; akawaambia hao makadhi, Angalieni myafanyayo; kwa kuwa hammfanyii mwanadamu hukumu, ila Bwana; naye yupo pamoja nanyi katika neno la hukumu. Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu; angalieni mkaifanye; kwa maana kwa Bwana, Mungu wetu, hapana uovu, wala kujali nafsi za watu, wala kupokea zawadi.Tena katika Yerusalemu Yehoshafati akasimamisha wa Walawi na makuhani, na wakuu wa mbari za mababa wa Israeli wawe kwa hukumu ya Bwana, na kwa mateto. Nao wakarudi Yerusalemu. Akawaagiza, akasema, Ndivyo mtakavyotenda kwa hofu ya Bwana, kwa uaminifu, na kwa moyo kamili. Na kila mara watakapowajia na teto ndugu zenu wakaao mijini mwao, kati ya damu na damu, kati ya torati na amri, sheria na hukumu, mtawaonya, wasiingie hatiani mbele za Bwana, mkajiliwa na ghadhabu ninyi na ndugu zenu; fanyeni haya wala hamtakuwa na hatia.Tena angalieni, Amaria, kuhani mkuu, yu juu yenu kwa maneno yote ya Bwana; naye Zebadia, mwana wa Ishmaeli, jemadari wa nyumba ya Yuda, kwa maneno yote ya mfalme; Walawi nao watakuwa wasimamizi mbele yenu. Jitieni nguvu, mtende, naye Bwana awe pamoja nao walio wema.”

Hata hivyo jambo jema ni kuwa baada ya maonyo Hezekia aliutafuta uso wa Mungu, aligeukia ukutani na kutafuta uso wa Mungu, aliomba na kulia sana alijutia tabia yake na ubinafsi wake aliokuwa nao, alimkumbusha Mungu jinsi alivyotembea kwa uaminifu alilia na kujutia kosa lake na Mungu alimrehemu haraka na kumuongezea Muda wa kufanya maandalizi, ni katika muda huu wa nyongeza ndipo alipooa na ndani ya miaka mitatu alizaliwa Manase

Isaya 38:2-6 “Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la Bwana likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.”

Jinsi ya kutengeneza mambo ya nyumba yako

Kuna mambo kadhaa ya kujifunza kutoka kwa maisha ya Hezekia na mkasa huu, waalimu wa Kiyahudi wanaelezea ya kuwa Hezekia alioa haraka sana baada ya kuponywa na alimuoa mwanamke ambaye alikuwa ni binti wa nabii Isaya baada ya kukemewa na kuponywa, Nabii Isaya alimuelekeza jinsi ya kutengeneza mambo ya nyumba yake alitakiwa kuoa haraka hata bila kujali kuwa wazao wake watakuwa wema au wabaya, hakutakiwa kuogopa mambo yajayo wala kuharibu yanayobaki,alitakiwa kuweka utaratibu na kuandaa mrithi wa kifalme kwaajili ya Daudi mtumishi wa Mungu ili ahadi ya Mungu itimie, Mfalme Hezekia alimuoa “Hefsiba” ambaye alikuwa ni binti wa nabii Isaya  na miaka mitatu baada ya kuponywa kwake walifanikiwa kumpata mtoto aliyeitwa Manase, huyu akawa mfalme mpya hata hivyo akawa muovu sana kuliko wafalme wote katika Yuda, aliwahi kumtoa mwane sadaka ya kuteketezwa,akajihusha na waganga na wachawi na ibada za sanamu na kuabudu malaika na machukizo ya kila aina

Isaya 62:4-5 “Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula; kwa kuwa Bwana anakufurahia, na nchi yako itaolewa.Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.”

2Wafalme 21:1-6 “Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na mitano katika Yerusalemu, na jina la mamaye aliitwa Hefziba. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli. Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopaharibu Hezekia baba yake; akamjengea Baali madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia. Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya Bwana, napo ndipo alipopanena Bwana, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu. Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika behewa mbili za nyumba ya Bwana. Akampitisha mwanawe motoni, akatazama bao, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa Bwana, hata kumkasirisha.”

Mambo ya kujifunza:-  

1.       Hakuna mtu mwenye uhakika na kesho, kesho iko mikononi mwa Mungu tu, Hezekia ingawa alikuwa mwema lakini bado alikumbushwa kuwa kuna kifo na akapokea taarifa hizo bila kutarajia, kwa kawaida huwa tunajisahau kama wanadamu tunadhani tutaendelea kuwepo siku zote, uzima huu unatupa kiburi, pumzi hii inatufanya tufikiri ubovu ni wa wengine na kifo ni cha wengine, tunajifikiri sisi tu, hatufurahii kuandaa wengine, hatufikirii uhai wa taasisi wakati ujao, maisha ya mwanadamu ni kama mvuke tu, na kama ua la kondeni, usisahau kuwa kuna kifo, hata Musa alikumbushwa na Mungu akamuandaa Yoshua, Eliya alimuandaa Elisha, Paulo Mtume alimuanda Timotheo na wengine, wewe na mimi tunataka tukizimika wengine waone giza tu hicho ni kiburi na sio mpango wa Mungu.

 

Ayubu 14:1-2 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe

 

2.       Kutengeneza mambo ya nyumba yako sio agizo kwa Hezekia tu, ni agizo la kila mtu, iandae familia yako, andaa waandae kwaajili ya mambo yajayo, andaa mahusiano mazuri na watu, andaa  kwa kuondoa madeni ya kimwili na kiroho hakikisha yanalipwa, kumbuka kuweka maagizo, kumbuka kuna maisha baada ya kazi, kuna maisha baada ya kustaafu, kuna kutafuta kwa bidii kuwa na amani na watu wote, wewe na mimi hatutakuwepo milele tuache ubinafsi, Ondoa kinyongo chako moyoni, usijiweke katika nafasi ya Mungu, acha kuhukumu wengine na kudhani kuwa uko wewe peke yako Mungu anao watu wengi sana na anaweza kuwatumia, lakini ni wajibu wetu kuwaandaa na wengine waweze kutimiza hivyo Majukumu ya mbeleni.

 

Kutokujiayarisha kwa maswala ya Mungu kunaitwa upumbavu katika maandiko, lakini tukihesabu siku zetu fupi za kuweko duniani na tukazitumie vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa tayari tunaitwa wenye hekima na akili

 

Zaburi 90:10-12 “Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara.Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako? Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.”

 

Luka 12:15-21 “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.” 

 

3.       Fanya mambo yao yote kwa uaminifu, Hezekia alikuwa mwaminifu na uaminifu wake ulikuja kumkomboa baadaye, Mungu alimuongezea umri kwa sababu alikuwa mwaminifu na alikubali mapenzi ya Mungu baada ya kuponywa jipu lake sugu, kumbuka wakati wowote unaweza kufa, hata kama wewe u mwema usisubiri tangazo la kifo ndipo uanze kujiandaa, je umeandaa watoto wako wa kiroho, umeandaa viongozi wajao, ndoa yako iko vizuri, watoto wako wamefundishwa njia za Bwana, je umesamehe waliokukosea, je una Amani na watu wote, je kwa Mungu uhusiano wako uko salama, Geuka ukutani leo ujifanyie tathimini wewe na Mungu wako kama mambo yako yako sawa sawa au la kama kuna kwa kutengeneza tubu, tengeneza mambo ya nyumba yako

 

2Petro 3:9 “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.”

 

4.        Unyenyekevu ni nyenzo ya thamani kubwa, - Kuugua kwa Hezekia kulimkumbusha swala zima la unyenyekevu, alipopewa taarifa za kutokupona alionyesha ya kuwa anamtegemea Mungu, alijinyenyekeza kwa Mungu wake, ni mfalme lakini aliamini katika maombi, alitubu na hakujihesabia haki, alipopona na kuongezwa maiaka 15 aliitumia vema kukamilisha kazi iliyosalia mbele yake kwa uaminifu, Hezekia alijifunza wazi kuwa iko sauti ya Mungu wakati tunapougua, lazima tujifunze na kujua kuwa Mungu anataka jambo gani lifanyike wakati wa kuugua kwetu na Hezekia aliyajua mapenzi ya Mungu na alijua dhambi zake akatubu

 

Isaya 38:17-20 “Tazama; nalikuwa na uchungu mwingi kwa ajili ya amani yangu; Lakini kwa kunipenda umeniokoa na shimo la uharibifu; Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako. Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; Wale washukao shimoni hawawezi kuitarajia kweli yako. Aliye hai, naam, aliye hai, ndiye atakayekusifu, kama mimi leo; Baba atawajulisha watoto kweli yako.Bwana yu tayari kunipa wokovu. Basi, kwa vinubi tutaziimba nyimbo zangu, Siku zote za maisha yetu nyumbani mwa Bwana.”

Na. Rev, Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: