Mwanzo 47:7-9 “Yusufu akamleta Yakobo
babaye ndani akamweka mbele ya Farao. Yakobo akambariki Farao. Farao akamwuliza
Yakobo, Je! Siku za miaka ya maisha yako ni ngapi? Yakobo akamjibu Farao, Siku
za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu
zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya
baba zangu katika siku za kusafiri kwao.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa maisha
yetu hapa duniani yanafananishwa na safari, siku zetu za kuishi ni chache na
tena zimejaa taabu sana, Maisha yetu yamejaa mabadiliko mengi sana na
changamoto nyingi sana za kimwili na kiroho, kwa ujumla maisha yetu duniani ni
ya kitambo kifupi sana ingawaje yana kusudi kubwa la Mungu na maana kubwa sana
ya kiroho, Na ndio maana Yakobo alielewa wazi kuwa maisha yake duniani ni kama
safari, anapita katika hii dunia kama mgeni na mpitaji tu, Yakobo alikuwa na
ufahamu kuwa dunia hii sio nyumbani kwetu na kwamba hata kama ataishi maisha
merefu kiasi gani bado miaka hiyo itakuwa ni miaka ya kusafiri kwake tu. Hivi
ndivyo maandiko yanavyotukumbusha hata leo ili tuishi vizuri tukiwa na uhusiano
mzuri na Amani kwa Mungu na wanadamu wote!
1 Petro 2:11-12 “Wapenzi, nawasihi kama
wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Mwe na
mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya,
wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.”
Miaka ya kusafiri ni usemi (Metaphor) unaokazia kuwa maisha ni
safari ya mchakato wenye kutupa uzoefu, mafunzo, kukua, kuelewa, kukomaa,
kuongeza ufahamu na maarifa na kukutana na mambo chanya na mambo hasi,
kutuchonga, kuuelewa ulimwengu na zaidi sana kuelewa kusudi la kuwepo kwetu,
kwa utukufu wa Mungu Baba, hata hivyo maisha ni ya kitambo/yaani ni ya muda
mfupi, sana na kwa sababu hiyo tunatiwa moyo kukabiliana na changamoto zote na
kuzihesabu kuwa ni nafasi ya kipekee ya kutuandaa kwaajili ya maisha yajayo,
Maisha ni safari kwa sababu hapa duniani sio mwisho na hatujafika na badala
yake tunapita tu. Leo tutachukua muda basi kutafakari somo hili muhimu kwetu “Siku za miaka ya kusafiri kwangu” kwa
kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Siku za
miaka ya kusafiri kwangu.
·
Siku za
miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu.
·
Wakristo
kama wasafiri
Siku za miaka ya kusafiri kwangu
Mwanzo 47:7-9 “Yusufu akamleta Yakobo
babaye ndani akamweka mbele ya Farao. Yakobo akambariki Farao. Farao akamwuliza
Yakobo, Je! Siku za miaka ya maisha yako ni ngapi? Yakobo akamjibu Farao, Siku
za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu
zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya
baba zangu katika siku za kusafiri kwao.”
Ni muhimu kujifunza na kutafakari
jinsi ambavyo Yakobo anayachukulia maisha kama safari, Maisha ni safari kweli
ya kimwili na kiroho, Safari hii inakabiliwa na maswala mengi chanya na hasi
lakini zaidi sana nyakati muhimu za kufanya maamuzi ambayo yataamua hatima yetu
ya baadaye, ndani ya maisha tutapimwa imani, utii, na changamoto za kimaisha zitakazolazimisha
maisha yetu yawe na mabadiliko kadhaa na kuzaa uvumilivu utakaotusaidia kuwa na
uwepo wa Mungu na ukomavu.
Yakobo anaonyesha kuwa sio yeye
tu alikuwa katika safari ya maisha lakini hata baba zake yaani Ibrahimu na
Isaka nao walikuwa katika kusafiri kwao, hivyo Ibrahimu, na Isaka na Yakobo
waliishi duniani kama wasafiri na wapitaji duniani, hawakuwa na makazi ya
kudumu, waliishi kwa Imani, walijitambua kuwa hapa duniani wao ni wapitaji tu.
Waebrania 11:13-16 “Hawa wote wakafa katika
imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia,
na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi. Maana hao wasemao
maneno kama hayo waonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. Na kama
wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurejea. Lakini sasa
waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa
Mungu wao; maana amewatengenezea mji.”
Yakobo anahesabu miaka ya kukaa
duniani kama miaka ya safari tu, Yeye na wazazi wake waliishi hivyo, hii ni kwa
sababu hawakuishi katika nyumba za kudumu kama tunavyoishi leo, maisha yao
yalikuwa ya kutanga tanga na kuhama hama (Nomads),
kwa hiyo hawakuwa na makazi ya kudumu, waliishi duniani kama wapitaji
wakiashiria ukweli halisi wa maisha ya kuwa maisha ni safari, na imejaa
mabadiliko ya iana mbalimbali kimwili na kiroho, wakipitia changamoto nyingi na
majaribu mengi, pamoja na baraka za Mungu, lakini maisha ya kawaida ya kibinadamu
yana changamoto nyingi wao walikuwa ni mfano tu wa kutukumbusha sisi tunaoishi
leo kwamba tuko safarini, na kuwa duniani tunapita tu, tuko hapa katika hali ya
ugeni tu na dunia sio nyumbani kwetu kwa kudumu, maisha ya mwanadamu ni ya muda
tu, ujumbe wake Yakobo na majibu yake kwa Farao yalikuwa ni
mauhubiri tosha kumjulisha Farao kuwa wanadamu wote hapa dunia ni
wanasafiri akiwepo yeye aliyekuwa na madaraka makubwa duniani kwa wakati ule,
Yakobo alitaka hili lifike akilini kwa mtu huyu mkubwa kumkumbusha kuwa Pamoja
na mamlaka yake kubwa na nguvu alizo nazo anapaswa kukumbuka kuwa siku za miaka
yetu ni siku za miaka ya kusafiri kwetu tu na hakuna cha kudumu duniani!
Waebrania 11:8-9.“Kwa imani Ibrahimu
alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka
asijue aendako. Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika
nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja
naye wa ahadi ile ile.”
Kila mwanadamu mwenye akili
timamu anapaswa kukumbuka kuwa maisha haya ni “temporally” ni ya muda tu tunapita kwa kasi sana na kwa sababu hiyo
hatuna budi kuishi kwa Amani na wenzetu na kuwafanyia watu mambo mema,
tusiwafanyie watu ubaya, wala tusiwawekee watu kinyongo, na kujilimbikizia mali
na madaraka kana kwamba sisi ni watawala wa kifalme, watu wengi hujisahau
katika hili, Yakobo alikuwa amebarikiwa sana lakini hakusahau kuwa yeye ni
msafiri, tuishi na watu vizuri, isifikie wakati watu wakafurahia kufa kwetu au
kuugua kwetu, badala yake watuombolezee, siku hizi linaanza kuwa jambo la
kawaida watu kufurahia kifo cha watu wengine kana kwamba wao hawatakufa, lakini
sababu kubwa ni kuwa watu hao waliishi bila ya kujali wengine, au waliumiza
wengine kwaajili ya ubinafsi na mafanikio yao, na wengine, walijisahau kuwa wao
wanapita tu, kila kitu duniani ni cha muda tu na maisha kwa ujumla yana masomo
mengi ya kutufunza! Na la muhimu sisi ni wasafiri na tuko duniani kwa muda!,
acha kinyongo, acha kuhukumu wengine, acha ubinafsi, acha kinyongo, tafuta kwa
bidi Amani na wote
Siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu.
Yakobo wakati anashuka Misri na
kuonana na Farao wakati huu alikuwa na miaka 130 na mpaka anafariki alikuwa na umri wa miaka 147 tu, kwa msingi huo aliishi Misri
kwa muda wa miaka kama 17 hivi, Yakobo anaziona siku hizi kuwa
ni chache sana, Ibrahimu aliishi miaka 175,
wakati Isaka aliishi miaka 180. Kwa
hiyo Yakobo anayaona maisha yake kuwa mafupi na yaliyojaa taabu sana kuliko
maisha ya baba zake, na pia ingawa hakuwa anajua ataishi umri gani lakini
alijitabiria kuwa siku zake ni chache na zilizojaa taabu sana kuliko siku za
baba zake, yaani Isaka na Ibrahimu, Yakobo alipanda milima na mabonde
akipambana na maisha yaliyojaa ugumu wa maswala mbalimbali kama:
1.
Migogoro
ya kifamilia – Yakobo alilazimika kukimbia nyumbani siku za maisha ya ujana
wake na kuishi mbali na baba na mama kwaajili ya kumkimbia kaka yake, Esau,
hayakuwa maisha ya kawaida, tabia yake ya hila na kuutumia upole wa kaka yake
kwa faida zake mwenyewe uliweza kuongeza ugumu wa maisha na kumfanya kuwa mbali
na wapendwa wake wa karibu uko uwezekano kuwa Yakobo Hakuonana na Rebeka tena
mpaka kifo kwajili ya tukio hili.
Mwanzo 27:41-45 “Esau
akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema
moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu
yangu Yakobo. Rebeka akaarifiwa maneno ya Esau, mwanawe mkubwa. Akapeleka mtu
kumwita Yakobo, mwanawe mdogo, akamwambia, Tazama, katika habari zako Esau,
ndugu yako, anajifariji moyo wake, maana anakusudia kukuua. Na sasa, mwanangu,
sikia sauti yangu, uondoke, ukimbilie kwa Labani, ndugu yangu huko Harani; ukae
kwake siku chache, hata ghadhabu ya ndugu yako igeuke; hata ikuondokee ghadhabu
ya ndugu yako, akasahau uliyomtenda. Ndipo nitakapopeleka watu kukuchukua
kutoka huko. Kwa nini nifiwe nanyi nyote wawili siku moja?”
2.
Dhuluma
na ukatili kutoka kwa mjomba – Yakobo alipokuwa akifanya kazi kwa mjomba
wake, ni ukweli usiopingika kuwa Yakobo alikuwa na mjomba aliyejaa hila zaidi
kuliko yeye, aliishi na mjomba katili, alimdanganya katika maswala ya ndoa na
kuishia kumtumikisha, lakini alibadili-badili maswala ya mkataba wa mshahara
wake zaidi ya mara kumi, siku chache zilizokadiriwa na kudhaniwa na Rebeka,
zikawa ni miaka mingi ya kitumwa uko uwezekano kuwa alikaa ugenini kwa mjomba
wake kwa miaka 20 akidhulumiwa tu
Mwanzo 29:18-27 “Yakobo
akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti
yako mdogo. Labani akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa
kwangu. Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama
siku chache tu kwa vile alivyompenda. Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu,
maana siku zangu zimetimia; niingie kwake. Labani akakusanya watu wote wa
mahali pale, akafanya karamu. Ikawa wakati wa jioni akamtwaa Lea, binti yake,
akamletea Yakobo, naye akaingia kwake. Labani akampa Lea mjakazi wake Zilpa,
awe mjakazi wake. Ikawa, kulipokuwa asubuhi, kumbe! Ni Lea. Akamwambia Labani,
Nini hii uliyonitenda? Sikukutumikia kwa Raheli? Mbona umenidanganya? Labani
akasema, Havitendeki hivi kwetu, kumtoa mdogo kabla ya mkubwa; timiza siku zake
saba, nasi tutakupa huyu naye kwa utumishi utakaonitumikia, miaka saba mingine.”
Mwanzo 31:1-9 “Basi
Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote
ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote. Yakobo akaona
uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi. BWANA akamwambia Yakobo, Urudi mpaka nchi ya
baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe. Yakobo akatuma watu,
akawaita Raheli na Lea waje nyikani kwenye wanyama wake. Akawaambia, Naona uso
wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama jana na juzi. Lakini Mungu wa baba
yangu amekuwa pamoja nami. Nanyi mmejua ya kwamba kwa nguvu zangu zote
nimemtumikia baba yenu. Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu
mara kumi; lakini Mungu hakumwacha kunidhuru. Aliposema, Walio na madoadoa
watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na
milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia. Hivi
Mungu akamnyang'anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi.”
3.
Mateso
katika familia yake – Yakobo alikutana na changamoto kutoka katika familia
yake mwenyewe, watoto wake waliokuwa wakichukiana wao kwa wao, walimuuza ndugu
yao Yusufu kijana wake mpendwa na kumdanganya kuwa amefariki, Yakobo
aliomboleza sana akijua kuwa mwanae atakuwa amefariki, hii ilizidisha shida na
huzuni kubwa katika maisha yake, nadhani walifanya msiba na kuzika nguo lakini
kumbe alikuwa amedanganywa tena!
Mwanzo 37:31-35 “Wakaitwaa
kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu.
Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii;
basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo
kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo
akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi.
Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa
kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba
yake akamlilia.”
4.
Njaa
iliyosababisha safari Misri – Pamoja na mapito kadhaa wa kadhaa ilimlazimu
kusafiri na kuiacha nchi ya ahadi akiwa na umri mkubwa 130, anakumbwa na njaa inayowalazimisha kushuka Misri kwaajili ya
chakula na wito wa mwanaye Yusufu, Ingawa Abrahamu na Isaka walikutana na
changamoto mbalimbali katika maisha, Yakobo anahisi maisha yake yalikuwa magumu
zaidi kuliko wao kwa sababu ya wingi wa
mateso na maumivu na migogoro ya kifamilia aliyoipitia, Hata hivyo katika hali
isiyokuwa ya kawaida Mungu alimtia moyo kushuka Misri na aliambiwa na Mungu
kuwa atakuwa pamoja naye, atafia huko mikononi mwa Yusufu
Mwanzo 46:2-4 “Mungu
akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema,
Mimi hapa. Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka
Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka
Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya
macho yako.”
Wakristo kama wasafiri
Kimsingi yako maswala mengi ya
kujifunza kutoka kwa Yakobo na mtazamo wake wa maisha kama safari
1.
Tunajifunza
kuwa maisha yetu ni ya muda – Haijalishi utaishi duniani kwa muda gani
lakini vyovyote iwavyo maisha ni ya muda mfupi sana na maandiko yako wazi
kuhusiana na jambo hili, na kuonyesha ufupi wa maisha ikionyesha mifano ya
maua, mvuke, majani, usingizi na kadhalika
Zaburi 90:5-6 “Wawagharikisha,
huwa kama usingizi, Asubuhi huwa kama majani yameayo. Asubuhi yachipuka na
kumea, Jioni yakatika na kukauka.”
Yakobo 4:13-15 “Haya
basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo
mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui
yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa
kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na
kufanya hivi au hivi.”
2.
Tunajifunza
kumtegemea Mungu na neno lake – Wakati wote wa mahangaiko yake Yakobo
pamoja na safari zake alizokuwa akizunguka duniani Mungu alimtokea mara kwa
mara na kumuonyesha dhahiri kuwa atakuwa pamoja naye, wakati mwingine katika
maisha yako utahangaika huku na huko na unaweza ukafikiri kuwa labda Mungu hako
pamoja nawe lakini nataka nikudhihirishie kuwa yuko pamoja nawe, haijalishi
ulikoenda ni utumwani au unakutana na shida gani kama Mungu alivyomuongoza
Yakobo atakuongoza na wewe pia katika safari yako ya maisha, changamoto za
maisha na ugumu wake ni jambo la kawaida.
Mwanzo 28:10-15 “Yakobo
akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulani akakaa huko usiku
kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale
akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na
tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena,
tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, BWANA
amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na
Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako
utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki,
na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia
watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami
nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia
hayo niliyokuambia.”
Mwanzo 46:2-4 “Mungu
akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema,
Mimi hapa. Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka
Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka
Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya
macho yako.”
Zaburi 119:105 “Neno
lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.”
3.
Tunajifunza
kujitayarisha kwa Mungu – Kwa kuwa maisha ni ya muda tu maana yake pamoja
na kupanga na kuweka maono na mikakati ya kibinadamu, kamwe tusiache kujitayarisha
kwa Mungu, maandiko yanamuita mtun anayejiwekea mikakati ya kidunia na kuacha
kujitayarisha kwa Mungu kama mtu mpumbavu, kwa sababu hiyo Mungu atupe moyo wa
hekima ili tujue itupasavyo kuhesabu siku zetu.
Luka 12:16-21 “Akawaambia
mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza
kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno
yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa
zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia,
Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi;
pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe,
usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya
nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”
4.
Tunajifunza
kuwa tayari kukabiliana na magumu – Kuwa mtu wa Mungu kamwe hakukufanyi
wewe usikutane na magumu hapa duniani, Yakobo alikuwa mtu wa Mungu na Mungu alimbariki
sana lakini hata hivyo maisha yake au miaka ya kusafiri kwake duniani ilijaa taabu
kuliko ya siku za baba zake kama anavyosema, hii inatufundisha na kutuimarisha
kuwa, kuwa mtu wa Mungu hakutazuia wewe kukutana na magumu, lakini pamoja na
hayo tusiache kumcha Mungu na kuwa na uhusiano naye, Yakobo alikutana na
changamoto nyingi lakini aliendelea kuwa na uhusiano na Mungu na kuwa mvumilivu
na mwenye subira na Mungu akawa pamoja naye.
Waebrania 13:5-6 “Msiwe
na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye
mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata
twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda
nini?”
5.
Tunajifunza
kuishi kwa viwango – Wasafiri na wapitaji hawaishi kwa viwango vya ugenini
na badala yake huishi kwa viwango vya nchi zao, sisi wenyeji wetu uko mbinguni
na kwasababu hiyo kamwe hatupaswi kuishi sawa na watu wa dunia hii, wala kufungwa
na mambo ya dunia hii, badala yake tuishi sawa na viwango vya kule tunakokwenda.
Warumi 12:1-2 “Basi,
ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu
iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala
msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate
kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”
Mathayo 6:19-21 “Msijiwekee
hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali
jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi
hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo
wako.”
Hitimisho
Maisha ya Yakobo yanatufundisha kuwa safari ya maisha yetu
duniani inaweza kugubikwa na changamoto nyingi sana lakini hata hivyo, Bado
Mungu atakuwa pamoja nasi, kwa msingi huo sisi kama wakristo hatupaswi
kujisahau na badala yake tuendelee
kutumaini na kuwa na imani, uvumilivu, saburi na kuwa tayari kuongozwa na Mungu
na neno lake ili kufikia malengo ya kuwa pamoja naye mbinguni, na hata kama maisha
yatajaa taabu kama yale ya Yakobo, Neno la Mungu lina ahidi kuwa Mungu atakuwa
pamoja nasi atatushika mkono na kututia nguvu hadi mwisho wa safari yetu, Siku za
miaka ya kusafiri kwetu ni chache nazo imejaa taabu. Ilikuwa ushuhuda kwa Farao
pia
Ayubu 14:1-2 “Mwanadamu aliyezaliwa na
mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama
vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe.”
Isaya 41:8-10 “Nawe, Israeli, mtumishi
wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Ibrahimu, rafiki yangu; wewe
niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia,
Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa; usiogope, kwa maana mimi ni
pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Muungu wako; nitakutia nguvu, naam,
nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni