Jumatano, 5 Februari 2025

Wewe ndiye mtu yule !


1Wakorintho 1: 26-29 “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu



Utangulizi

Ni muhimu kufahamu kuwa Katika maisha, watu wengi sana hujiona kuwa hawana maana kwa sababu ya hali zao, historia yao, au upungufu wao na udhaifu walionao. Wengine hujidharau kwa sababu hawana elimu kubwa, hadhi ya kijamii, au uwezo wa pekee au vipawa. Lakini Biblia inafundisha kwamba Mungu hachagui watu kwa vigezo vya wanadamu bali kwa kusudi lake mwenyewe. Tena bila kujali Hali zao, Leo tunajifunza jinsi Mungu anavyoyachagua mambo manyonge, yaliyodharauliwa, na yasiyo na sifa za dunia kwa ajili ya utukufu wake. Na kwaajili yake yeye mwenyewe.

Tutajifunza somo hili WEWE NDIYE MTU YULE  kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


Uchaguzi wa Mungu

• Mifano ya watu waliochaguliwa na Mungu

• Wewe ndiye mtu yule


Uchaguzi wa Mungu. 

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu katika Hekima yake anaweza kuamua Kwa kuwa ana Haki ya kuamua kumchagua na kumtumia mtu yeyote yule bila kujali kama mtu huyo anakidhi au kutosha vigezo vya kawaida vya kibinadamu, uchaguzi wa Mungu ni wa tofauti na Wa kibinadamu Kwa sababu Mungu huangalia Moyo.


1Samuel 16:7 “Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo


Warumi 9:11-15 “kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye), aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo. Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia. Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha! Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye


Tabia hii ya Mungu inathibitisha kuwa Mungu hutumia watu wasiotegemewa na jamii waliokataliwa, wanyonge na hata waoga na wasiojiamini wakati mwingine ili kuonyesha utukufu wake. Hivyo, mtu yeyote anayejiona hafai hana sababu ya kujidharau, bali anaweza kumtumaini Mungu ili amtumie kwa utukufu wake.


Mifano ya watu waliochaguliwa na Mungu 


Wengi wa watu waliochaguliwa na Mungu au kutumiwa na Mungu walikuwa ni watu wenye changamoto za kukosekana kwa vigezo vya kibinadamu vya kukidhi haja na mahitaji ya nafasi ambazo Mungu alikuwa amewaitia ili wamtumikie, na wakati mwingine hata wao wenyewe walijiweka katika mzani na kujipima na kijibaini kuwa hawatoshi katika vigezo na masharti au viwango sawa na majukumu waliyokuwa wamepewa.


1. Musa  - Aliogopa sana kumkabili Farao ambaye Kwa nyakati zile alikuwa ni mtawala wa Dunia ya wakati huo tena dikteta katili mwenye jeshi lisilo na mpinzani, Pamoja na kujifikiria kuhusu uwezo wake wa kunena Kwa sababu ya kigugumizi Musa alimshauri Mungu kuchagua mtu mwingine.


- Ni jambo la kushangaza kuwa Mungu hakuponya kinywa Chake Wala kigugumizi ingawa angetaka angemponya lakini alimuhakikishia kuwa atakuwa Pamoja naye.


- Kutoka 3:10-11 “Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri. Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri?


- Kutoka 4:10-12 “Musa akamwambia Bwana Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito. Bwana akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, Bwana? Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena.”


2. Gideoni - Alihofia kuwa yeye ni masikini na anatokea katika kabila ndogo, pia alikuwa mtu mwenye hofu na woga, ni ukweli ulio wazi kuwa mwenyewe alijiona kuwa sio kitu, Lakini Bwana alimtumia na kumchagua kuwa mwamuzi wa Israel


- Waamuzi 6:14-15 “Bwana akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu.”


- Mungu alimuhakikiashia kuwa atakuwa Pamoja naye na kuwa atawapiga Wamidiani kama mtu mmoja


- Waamuzi 6:16 “Bwana akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja

- Hata Pamoja na kuhakikishiwa Hilo ni ukweli ulio wazi kuwa Gideoni bado alibaki kuwa mwoga udhaifu wake unaweza kulinganishwa na njozi uliyootwa na kambi ya adui zake ambao waliota ndoto na kutafasiriana, kuwa Gideoni ni kama mkate wa shairi (Ngano) ambao ulisambaratisha hema za wamidiani, mfano huu wa ndoto unaonyesha jinsi ambavyo Mungu anatumia kitu dhaifu sana katika kufanikisha kazi yake kwaajili ya utukufu wake


- Waamuzi 7:9-15 Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako. Lakini, ukiogopa kushuka, shuka pamoja na Pura mtumishi wako kambini; nawe utasikia wanayoyasema, na baada ya haya mikono yako itatiwa nguvu; ushuke kambini. Ndipo akashuka pamoja na Pura mtumishi wake hata kufikilia mwisho wa watu wenye silaha waliokuwa kambini. Nao Wamidiani na Waamaleki na, hao wana wa mashariki walikuwa wametua bondeni, mfano wa nzige kwa wingi; na ngamia zao walikuwa hawana hesabu; mfano wa mchanga wa ufuoni, kwa wingi. Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, naliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika hata hema moja, ukaipiga hata ikaanguka, nao ukaipindua, hata ikalala chini. Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake. Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana Bwana amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu


3. Sauli - Alikuwa Anatafuta Punda wa baba yake, lakini kumbe Mungu alikuwa amemwambia Samuel kuwa atamleta mtu ambaye atakuwa mfalme wa Israel na kuwa Samuel alipaswa kumpaka mafuta Kwa kuwa Mungu Amekusudia awe mfalme.


- 1Samuel 9: 1-6 “Basi, kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu. Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote. Na punda za Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kishi akamwambia Sauli mwanawe, Haya basi, twaa mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, uende ukawatafute punda hao. Naye akapita kati ya nchi ya milima milima ya Efraimu, akapita na kati ya nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona; kisha wakapita kati ya nchi ya Shaalimu, wala huko hawakuwako; wakapita kati ya nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwapata. Hata walipofika nchi ya Sufu, Sauli akamwambia yule mtumishi aliyefuatana naye, Haya, na turudi, baba yangu asije akaacha kufikiri habari za punda akatufikiri sisi. Naye akamwambia, Tazama, katika mji huu mna mtu wa Mungu, naye ni mtu mwenye kuheshimiwa; yote asemayo hutukia kweli kweli; basi, twende huko; labda yeye aweza kutuambia habari ya safari yetu tunayoiendea.”


- Unaona hapo tunapata habari ya Sauli aliyekuwa anatafuta punda waliopotea wa baba yake. Alikuwa mtu wa kawaida kutoka kabila la Benyamini, ambalo lilikuwa dogo kati ya makabila ya Israeli.


Inaonekana Mungu anasababisha mkasa huu wa kupotea Kwa Punda lakini yeye anaandaa mpango wa kumleta mtu yule Kwa Samuel ili kupakwa mafuta, mwendo wa siku tatu Porini bila kupiga mswaki, au kuoga unaweza kusababisha wewe uliyeagizwa kumpaka mafuta mfalme kufikiri kuwa Mungu amechagua mtu mchafu lakini hii ilikuwa njia ya Mungu kutimiza kusudi lake, hivyo Samueli alimpaka mafuta, Je Sauli alijiona mwenye kutosha ? La hasha ! 


- 1 Samweli 9:21 – Sauli alimwambia Samweli: “Je! Mimi si Mbenyamini, wa kabila ndogo katika Israeli? Na jamaa yangu si ndogo katika kabila la Benyamini? Mbona basi unanena nami maneno kama haya?


- Alikuwa hajui kuwa Mungu alikuwa amempangia kuwa mfalme wa Israeli.


- 1 Samweli 10:1 “Samueli alimpaka mafuta na kumwambia: “Bwana amekutia mafuta uwe mkuu juu ya watu wake Israeli.”


- Hii inatufundisha kuwa hata pale mtu anapokuwa anashughulika na mambo ya kawaida, Mungu anaweza kuwa na mpango mkubwa juu yake. Hata pale mtu anapojifikiri kuwa yeye sio mwenye kutosha au kufaa Mungu husema kuwa wewe ndiye mtu yule!


4. Daudi - Alikuwa ni mtoto aliyekataliwa na kudharauliwa na jamii na hata baba yake na ndugu zake, haiwezekani Yese kuwaita watoto Saba wanaume katika sherehe muhimu ya kuweka wakfu mfalme ajaye, Kisha mtoto huyu akaachwa Porini! Ni dhahiri kuwa hakuhesabika kuwa ni mwenye kufaa, vyanzo vya kale vinaelezea kuwa Daudi alihesabika kama mwana haramu katika nyumba ya baba yake, kuwekwa kwake kuchunga kondoo katika mazingira ya Dubu na Simba ilikuwa yamkini ikiwezekana afie huko, ni Samuel ndiye aliyekujua kuondoa utata wa mashaka kuhusu Daudi kuwa mwana wa Yese Kwa kuuliza kama Yuko mtoto mwingine na hata hivyo yeye akawa ndiye mtu yule ambaye Mungu amekusudia ona:-


- 1Samuel 16: 8-12 “Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, Bwana hakumchagua huyu. Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, wala Bwana hakumchagua huyu. Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, Bwana hakuwachagua hawa. Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye.”


5. Petro - Alikuwa mtu mwenye hofu, lakini pia mwenye kujiaminisha kupita kawaida, pia alikuwa mtu mwenye kukata tamaa, Yeye aliwahi kumkana Yesu mara tatu, lakini pia kabla ya kukutana na Yesu alijihisi kuwa yeye ni mtu mwenye dhambi, Yesu alimtia moyo kuwa asiogope kwani yeye angemfanya kuwa mvuvi wa watu, baadae Mungu alimtumia Kwa viwango vya juu na kuwa mojawapo ya watu ambao ni nguzo ya Kanisa


- Luka 5:3-10 “Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni. Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana. ‘Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata; na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.”


- Luka 22:33-34 “Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui.”


- Luka 22:56-60 “Ndipo mjakazi mmoja akamwona ameketi mwangani, akamkazia macho akasema, Na huyu alikuwa pamoja naye. Akakana, akisema, Ee mwanamke, simjui. Baadaye kitambo mtu mwingine alimwona akasema, Wewe nawe u mmoja wao. Petro akasema, Ee mtu, si mimi. Halafu, yapata saa moja, mtu mwingine alikaza kusema, Hakika na huyu alikuwa pamoja naye, kwa kuwa yeye pia ni Mgalilaya. Petro akasema, Ee mtu, sijui usemalo. Na papo hapo alipokuwa katika kusema, jogoo aliwika.”


- Matendo 4:13 “Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu


Wewe ndiye mtu yule! 


Penginepo wewe ni mtu unayejihukumu na kujidharau na kujifikiria kuwa wewe sio kitu na kuwa Labda huna vigezo, na Kwa sababu ya vipimo vyako na mitazamo kadhaa ya kibinadamu unaweza kujifikiria kuwa Labda hufai mbele za Mungu lakini neno hili limekujia maalumu kwako ili kukujulisha ya kuwa hupaswi kujidharau wewe ndiye mtu yule ambaye Mungu amekusudia kukutumia bila kujali hali yako, Historia yako, kabila yako na changamoto zozote unazozipotia.

Hupaswi kujidharau, Mungu aliyekujua na kukuandaa tangu tumboni anakujua vema na Kwa vigezo vyake wewe ndiye mtu yule ambaye Mungu anataka kukutumia Kwa vigezo vyake na sio vyako au vya wanadamu, usikubali wakati wowote kuwekwa katika vigezo vya kibinadamu na badala yake kumbuka kuwa ni Kristo ndiye aliyekufa kwaajili yako na wewe ndiye mtu yule ambaye Mungu amekusudia kumtumia!


Yeremia 1:4-7 “Neno la Bwana lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru.”


Mungu anakujua vizuri sana anakujua vema, hujazaliwa Kwa bahati mbaya, Mungu anapokuwa na wewe wewe hubaki tena kuwa mtu wa kawaida, nyenyekea katika neema yake na Roho wake Mtakatifu atakubeba, hakuna jambo lolote katika mapenzi ya Mungu ambalo tunaweza kulifanya Kwa uwezo wetu au nguvu zetu hapana


Yohana 15:5 “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.”


Zekaria 4:6 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.”


Acha kujidharau, acha kujiona duni fanya kazi na wajibu ule ambao Mungu ameukusudia kwako, yeye aliyekuita anakujua vizuri na anajua Hali unayoipitia, na changamoto ulizo nazo yeye ndiye utoshelevu wetu pale inapoonekana kuwa hatutoshelezi.


2Wakorintho 3:5-6 “Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu. Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha.”

Uongezewe neema! 


Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!