Jumatano, 19 Februari 2025

Msidanganyike!

 


Wagalatia 6:7-8 “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.”



Utangulizi:

Mojawapo ya maonyo yanayotolewa na neno la Mungu upande wa agano la kale na agano jipya ni pamoja na kuionya jamii kuhusu kudanganyika, katika ulimwengu huu tulio nao chanzo cha kila uovu duniani kilisababishwa na udanganyifu uliofanywa na shetani kwa Mwanamke, na kupitia udanganyifu dhambi ikaingia ulimwenguni na tangu wakati huo udanganyifu umekuwa ni moja ya silaha kubwa sana ya shetani kuwaingiza wanadamu katika mtego wa mateso na changamoto nyingi.

1Timotheo 2:13-14 “Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.”

Ni kwaajili hiyo maandiko yana maonyo mengi sana ambayo yanayotuonya kuhusu uwezekano wa kuingizwa kwenye udanganyifu, leo basi tutachukua muda kujifunza maeneo kadhaa ambayo kwa hayo maandiko yametuonya kwamba tuwe makini kwa sababu uko uwezekano wa kudanganyika katika hayo, na kwa sababu hiyo tutaweza kuchukua tahadhari katika maisha yetu ya kiroho, na kimwili, tutajifunza somo hili Msidanyanyike kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Maana ya neno Msidanganyike.

·         Jinsi mwanadamu anavyoweza kudanganyika.

·         Jinsi ya kufanya ili kuepuka udanganyifu.


Maana ya neno Msidanganyike.

Ni muhimu kufahamu kuwa mojawapo ya sababu kubwa ya Bwana wetu Yesu Kristo kuweka wengine katika kanisa kuwa Mitume, Manabii, Wainjilisti, Wachungaji na Waalimu ni ili waujenge mwili wa Kristo, hata kazi ya huduma itendeke, hata sote tukue na kufikia katika cheo cha kimo cha utumilifu wa Kristo, lakini zaidi pia wakristo wasiwe tena wachanga na kuchukuliwa na kila aina ya upepo wa elimu kwa kufuata njia za udanganyifu, hii maana yake ni kuwa kanisa tusiposimama vizuri uwezekano wa watu kudanganywa upo, uwezekano wa watu kufuata mafundisho ya uongo upo ona

Waefeso 4:11-14 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu”.

Udanganyifu hasa ni nini? Neno udanganyifu katika agano la kale linasomeka kwa lugha ya kiebrania kama “nāshā  na linasomeka hivyo katika agano jipya kwa kiyunani kama neno “planáōambayo kwa kiingereza maana yake hufafanuliwa kwa neno Deceivableness ambalo maana yake ni kudanganyika au kukengeushwa “to be lead astray” au neno la kiebrania “pāthāh”  kudanganywa kwa kuvutiwa “to be entice” au “to be tempted by attract”, kujaribiwa kwa ushawishi, kwa hiyo shetani na watumishi wake yaani manabii wa uongo, na walimu wa uongo, na mitume wa uwongo, hawatakuja katika namna ambayo wewe utashituka kuwa huu ni uwongo, lakini watakuja katika namna ya kushawishi, kwa kusudi la kuleta ukengeufu, shetani hatakuja katika namna ya kutisha kwanza hatishi, kwa sababu yeye aliumbwa kama malaika, haji kwa vitisho, lakini atakuja kama malaika wa nuru,  na akitumia njia ya ushawishi.

2Wakorintho 11:13-15 “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo. Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.”

Mwanzo 3:4-6 “Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.”

Kwa hiyo kila mtu mwenye nia ya kumtafuta Mungu kwa dhati anapaswa kuchukua tahadhari, kuhusiana na uwezekano wa kudanganywa, kunakoratibiwa na shetani na watumishi wake, hii maana yake ni nini wako mitume wa kweli, manabii wa kweli, wainjilishi wa kweli na wachungaji na walimu wa kweli, na hata washirika wa kweli, lakini pia wako watumishi wa uwongo wakiwakilisha au wakitumia majina hayo hayo, na wote sisi ni walengwa wa kudanganywa, unaweza kudanganywa hata na mtumishi mwenzako, lakini pia unaweza kudanganywa hata na washirika wa uwongo, kwa hiyo onyo la kuchukua tahadhari tusidanganyike linatuhusu wote.           

Jinsi mwanadamu anavyoweza kudanganyika

Yako mambo kadhaa wa kadhaa ambayo kimsingi tusipoyatilia maanani tunaweza kujikuta kuwa tumedanganyika, Maandiko yameorodhesha maswala kadhaa ambayo kama tutayazingatia tunaweza kuwa salama na kama tusipoyazingatia tunaweza kujikuta kuwa tumeingia matatani na kudanyanyika, kumbuka udanganyifu ambao shetani anaukusudia licha ya kuwalenga wanadamu wote lakini kusudi kubwa hasa ni kuwalenga wale waliookolewa ili wote kwa ujumla waweze kupotea, sasa tunawezaje kudanganyika hapa neno la Mungu linaelezea namna mwanadamu anavyoweza kudanganyika:-

·         Tukisema kwamba hatuna dhambi – Moja ya njia hatari sana anayoitumia shetani hasa kwa watu tuliookoka ni kutuingizia mawazo ya kijinga ya kujifikiri kuwa hatuna dhambi au tumekuwa wakamilifu, huku ni kudanganyika, haijalishi tunajitahidi kwa kiasi gani hatuwezi kamwe kufikia ngazi ya kujitangaza kuwa tumekamilika na hatuna dhambi, Mungu ni Mtakatifu sana na kamwe kwa utakatifu wake hakuna mwanadamu anayeweza kufikia viwango anavyovihitaji, kila wakati unapomsogelea Mungu utaweza kuhisi mapungufu yako na kwa sababu hiyo hakuna mwanadamu anayeweza kukiri kuwa yeye ni mkamilifu na amemaliza ukamilifu wetu na kuhesabiwa kwetu haki mbele za Mungu kunatokana na ukamilifu wa Yesu Kristo na sio sisi wenyewe, wala juhudi zetu hazina mchango wowote, furaha yetu ya wokovu tunaweza kusema ni kwa sababu tumesamehewa dhambi zetu na kuhesabiwa haki bure kwa Imani na kwa kuzaliwa mara ya pili na kwa kutakaswa kwa damu yake Yesu, kwa hiyo kusema kuwa hatuna dhambi ni kujidanganya

 

1Yohana 1: 8-10 “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.”

 

Isaya 65:5 “watu wasemao, Simama peke yako, usinikaribie mimi, kwa maana mimi ni mtakatifu kuliko wewe; watu hao ni moshi puani mwangu, moto uwakao mchana kutwa.”

 

Tabia ya kutokunyenyekea na kujihesabia haki inamuudhi sana Mungu, kimsingi neno la Mungu halitutii moyo kutenda dhambi hata kidogo, lakini Mkristo wa kweli ni yule ambaye ataendelea kujitakasa kila siku, na kuendelea kumuomba Mungu msamaha, kila iitwapo leo, na kuendelea mbele kwa kuishi maisha matakatifu bila ya kujikweza kwa Mungu na kujifikiri kuwa tumekamilika, Mitume walikuwa wanyenyekevu sana hawakuwahi kujikweza na kujiweka katika kundi la watu waliokamilika badala yake walionyesha kuwa wanaendelea kupambana, Kristo Yesu katika mafundisho yake alionya wazi tabia ya kujifikiri kuwa umefika na kufikiri ya kuwa tunafaa na wakati mwingine ukijilinganisha na wengine na kujijengea tabia ya kiburi ya kujidhania kuwa wewe umekamilika haya yakijengeka ndani yetu ni rahisi kukataliwa.

 

Yakobo 3:2 “Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.”

 

Wafilipi 3:12-14 “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”

 

Luka 18:10-14 “Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”

 

Luka 6:41-42. “Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.”

 

Mungu ndiye anayetuhesabia haki, ni yeye ndiye aliyetufia, na ni yeye ndiye aliyetuokoa na kutusafisha na kutuhesabia haki na ni yeye ndiye anayetuombea na ameketi mkono wa kuume wa Mungu, kwa hiyo kila mtu aliyeokolewa anapaswa kuwa mnyenyekevu, na kuacha kujivunia neema ya Mungu, badala yake kuipokea kwa shukurani na unyenyekevu, na kuendelea kujitakasa kila iitwapo leo huku tukiacha kabisa tabia ya kuwanyooshea wengine vidole, na kujihesabia haki. Endapo tutajipima wenyewe na kujifikiri kuwa tunafaa tutakuwa tumedanganyika.

 

·         Tukijifikiri kuwa tuna hekima ya dunia – Hekima ya dunia hii maana yake ni Elimu za fani mbalimbali hapa duniani, kuwa na elimu sio jambo baya kwa sababu maandiko yanatia moyo swala zima la kusoma, lakini tukiwa na kiburi kwa sababu ya elimu ya dunia hii, na kupuuzia maswala ya Mungu eti kwa sababu tumesoma maandiko yanatuambia huko ni kudanganyika, awaye yote ambaye hataki kuongozwa na neno la Mungu ni mpuuzi bila kujali kuwa ana elimu kiasi gani, Neno la Mungu linasema kuwa Mungu ameifanya hekima ya dunia hii kuwa ni upuuzi, kwa hiyo kujivunia elimu ni kujidanganya, Elimu ni nyenzo ya kuturahisishia kazi na sio nyenzo ya kutujengea kiburi dhidi ya Mungu na watu wengine.

 

1Wakorintho 3:18-20 “Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima. Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao.Na tena, Bwana anayafahamu mawazo ya wenye hekima ya kwamba ni ya ubatili.”

 

·         Kama tukiongozwa na Mapokeo ya wanadamu – mapokeo ya wanadamu ni utaratibu wa fulani wa kijamii katika imani, ni muundo wa desturi zilizorithiwa katika kundi fulani au dhehebu fulani na kuingizwa katika imani huku yakiwa sio msingi uliojengeka katika neno la Mungu, mapokeo haya yamekuwa sababu ya kudanganyika kwa watu wengi sana  baadhi ya mapokeo haya ni kama vile ubatizo kwa watu wasioamini kama watoto wachanga, kuomba kwa kutumia Rozali, kuabudu kwa kuhusisha sanamu, pamoja na kuandama mwezi na kuutiisha mwili kwa ukali, kutawadha  na kadhalika watu wanaofuata mapokeo hayo wamedanganyika

 

Wakolosai 2:4-8 “Nasema neno hili, mtu asije akawadanganya kwa maneno ya kuwashawishi. Maana nijapokuwa sipo kwa mwili, lakini nipo pamoja nanyi kwa roho, nikifurahi na kuuona utaratibu wenu na uthabiti wa imani yenu katika Kristo. Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.”

 

Mathayo 15:7-9 “Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.”

 

·         Kufikiri kuwa unaweza kuurithi ufalme wa Mungu huku unaendelea na maisha ya dhambi – mtu awaye yote anayedhani ya kuwa anaweza kuurithi ufalme wa Mungu huku akiwa anaendelea na maisha ya dhambi mtu wa namna huyo amedanganyika, mtu aliyeokoka ni lazima aishi mbali na dhambi, lazima uache kuvuta bangi, kula madawa ya kulevywa, kujihusisha na maswala ya utoaji wa mimba, kuuza baa, kutoa huduma za guest house za kufanyia ngozo, kuuza pombe, kujihusisha na duluma, kuishi maisha ya uasherati, kuabudu sanamu, kuzini, kujihusisha na  ufiraji, ulawiti, ulevi, tamaa mbaya, ushoga, usagaji, kutukana, wizi na utapeli, uchafu, mapenzi ya jinsia moja, uchawi, ushirikina, uadui, ugomvi, wivu wenye uchungu, fitina, majungu, mafarakano, uzushi, husuda, ulafi, picha za ngono na maswala yote yanayofanana na hayo kama wakristo watayatenda hayo neno la Mungu liko wazi watakuwa wamedanganyika na hawataweza kuurithi ufalme wa Mungu

 

1Wakorintho 6:9-10 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi.”

 

Wagalatia 5:19-21 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.”

 

·         Tukiwa wasikiaji wa neno na sio watendaji – Kusikia neno la Mungu sio kitu kibaya kila mtu anapaswa kuwa msikivu kwa neno la Mungu lakini hiyo pekee haitoshi, ni lazima tulitii neno la Mungu, kutii ndio kulifanyia kazi, ndio kuwa watendaji wa neno, Mungu hakutuokoa kwaajili ya kusikia, Mungu ametuokoa kwa sababu tumeamini, na kama tumeamini basi kila mwamini wa kweli ni yule anayelitendea kazi neno la Mungu na kulitendea kazi kunahusisha kutii

 

Yakobo 1:22-25 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.”

 

Katika ufalme wa Mungu utendaji una tmanani kubwa sana kuliko maneno na Muitikio, kimsingi kutendea kazi neno la Mungu ni hekima na kutokulitendea kazi neno la Mungu ni upumbavu, Bwana ampe neema kila mmoja wetu asidanganyike kwa kutokulitendea kazi neno

 

Mathayo 21:28-31 “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu. Akajibu akasema, Naenda, Bwana; asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu, akaenda. Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu.”

 

Mathayo 7:24-27 “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”

 

·         Kujifikiri kuwa kitu – kujifikiri kuwa kitu mbele za Mungu ni kujidanganya, Neno kujifikiri kuwa kitu  katika lugha ya kiyunani linatumika neno “tis” kwa kiingereza linatumika neno “enclitic” kwa kiyunani “enklitikos” au “enkilinesthai” kwa lugha nyepesi “to lean on”  au “to rely on” hii ni tabia ya kufikiri kuwa mambo hayawezi kwenda bila mtu huyo kuwepo, ni kujifikiri kuwa wewe ni maalumu sana na kuwa wewe ni wa kutegemewa, usipokuwepo wewe mambo hayaendi, huku ndio kujiona kuwa kitu, hii  nitabia ya kiburi cha uzima, na kiburi cha kibinadamu, mtu moja alisema hakuna mtu anayeweza kujifikiri kuwa yeye ni wa muhimu sana na kama unafikiri kuwa wewe ni wa muhimu sana kufa na utaona mambo yote yataenda, yataenda bila msaada wako, mkeo au mumeo ataishi, watoto wako wataishi, wazazi wako maisha yataendelea lakini zaidi ya yote kazi ya Mungu itaendela bila kujali wewe ni wa muhimu kiasi gani, kujiona kuwa kitu ni dhambi na ni kiburi, dumia imewahi kuwa na watu mashuhuri sana na wamepita na mambo yanaenda hata bila wao, wewe na mimi sio wa kujiona kuwa kitu na kufikiri kuwa bila wewe na mimi mambo hayatakwenda yataenda na utakachoambulia ni kupewa neno RIP tu ukizikwa tu habari yako inaishia hapo n ahata waliokuwa wakikulilia hawalii tena.

 

Wagalatia 6:2-3 “Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo. Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake.”

 

·         Kupuuzia dalili za siku za mwisho – Maandiko hayajatuelezea siku ya kurudi kwa Yesu Kristo, lakini yametupa dalili za siku za mwisho na kurudi kwake Bwana wetu Yesu Kristo, kupuuzia dalili tulizopewa na kuhusu kurudi kwa Bwana Yesu na Matukio ya mwisho wa dunia ni kudanganyika, wako watu wanapuuzia swala zima la kurudi kwa bwana wetu Yesu huku wakilichukulia swala hili kama mzaha, Kristo Yesu alionya kuwa ni lazima tuchukue tahadhari kwa kadiri tuonavyo dalili zile zikiwa zinakaribia, maandiko yanaonyesha kutakuwa na udanganyifu wa aina nyingi sana kuhusiana na nyakati za mwisho na ujio wa Bwana Yesu.

 

Luka 21:7-8 “Wakamwuliza wakisema, Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini ishara ya kuwa mambo hayo ya karibu kutukia? Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao.”          

               

2Wathesalonike 2:3-4 “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu; yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.”

 

·         Kupuuzia swala la marafiki wabaya – Marafiki wabaya wanaweza kuchangia swala zima la kudanganyika kiimani, Paulo mtume aliwaonya wakorintho kutokuwa na marafiki wabaya “Bad company” biblia ya Kiswahili imetumia neno mazungumzo mabaya, hawa walikuwa ni waalimu wa uwongo, watu waliokuwa wanafundisha kuwa hakuna ufufuo wa wafu, jambo ambalo lingepelekea kuondoa tumaini la muhimu duniani na kuwafanya watu waishi vile wanavyotaka, au kwa anasa kwa sababu ya kutckuwa na matumaini, kimsingi maandiko yanatuonya kutokuwa na ufungamanifu wa ndani sana na watu ambao wanaonekana kuwa na imani potofu au iliyo kinyume na yetu au ile misingi uliyojifunza, kwani kwa kuruhusu hayo tunaweza kudanganyika na kupokea ukengeufu, udanganyifu.

 

1Wakorintho 15:32-34 “Ikiwa, kwa jinsi ya kibinadamu, nalipigana na hayawani wakali kule Efeso, nina faida gani? Wasipofufuliwa wafu, na tule, na tunywe, maana kesho tutakufa. Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe.”

 

2Wakorintho 6:14-18 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,”

 

·         Kuzungumza maneno yasiyo na maana ya uasi – Uasi ni sumu inayoenea kwa haraka sana, neno la Mungu linatuelekeza kuwa kufuata maneno ya kuasi  yasiyo na maana ni kudanganyika, maandiko yanatutaka wakati wote tuzungumze maneno yenye kujenga na wala sio ya kubomoa, wala hatupaswi kufuata mkumbo wa wale wanaoasi ili tuweze kuwa salama, kuchochea kwa gharama yoyote ile maneno ya uasi kunatuweka katika nafasi ya kudanganyika na kuruhusu hasira ya Mungu kuja juu yetu

 

Waefeso 5:6-11 “Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi. Basi msishirikiane nao. Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo Bwana. Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee;”

 

Mathayo 12:34-37 “Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”

 

·         Kujivunia Dini au dhehebu kuliko utakatifu – Maandiko yanaonyesha wazi kuwa kujivunia dini kuliko maisha matakatifu ni aina nyingine ya udanganyifu, nyakati za leo watu husifia dini zao na madhehebu yao na wameacha kabisa kumuinua Kristo kwa maneno yao na kwa matendo yao, Nyakati za kanisa la kwanza watu walijivunia dini, huku Yatima na wajane wakiishi katika wakati mgumu, hakukuwa na watu wa kuwatunza, na hali ya kipato ilikuwa mbaya na dini zilikuwepo, badala ya watu kuonyesha upendo kivitendo kwa kushughulika na kujali masikini na wenye mahitaji ya kijamii, wao walijikita katika kutangaza dini zao na madhehebu yao huku wakijisifia kuwa ni madhehebu bora, Yakobo aliwafundisha kurudi katika upendo wa kweli kujali, jamii yenye uhitaji na kuishi maisha safi yasiyo na taka na kutokuifuata dunia hii, kama tutajisifia kuwa tuna madehebu mazuri na dini nzuri, huku kanisa letu likiwa limejaa ubinafsi na kutokujali, na huku watu wake hawana upendo yaani hawajali hayo yote yatakuwa ni kazi bure na ni kujidanganya

 

Yakobo 1:26-27 Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai. Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.”

 

1Wakorintho 13:1-7 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.”

               

·         Kuufuta moyo kuliko neno la Mungu – aina nyingine ya kudanyanyika ni ile tabia ya kuutii moyo kuliko neno la Mungu, wako watu duniani ambao huujali sana moyo kuliko kanuni na taratibu za kutusaidia zilizoko katika neno la Mungu, wanasema upe moyo kitu unapenda, huku ni kuufuata mwili na ni kutaka kufa, maandiko yanaonya kuwa kuufuata moyo ni kufuata kifo kwa sababu moyo una ugonjwa wa kuua, Kwa hiyo ukitii kila kitu ambacho moyo unakuongoza unajikuta umeingia pabaya na kwa kweli utakuwa umedanganyika, moyo ni chombo cha tamaa ambacho mara nyingi huwaongoza watu wa dunia hii na sio wana wa Mungu hatuna budi kumuomba Mungu aweke sheria zake katika mioyo yetu tusiifuate tamaa na kudanganyika kwa sababu tamaa hukaa moyoni

 

Yeremia 17:9-10 “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.”

 

Tito 3:3-5Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana. Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu;”       

 

Yakobo 1:13-15 “Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu. Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.”

 

Jambo kubwa na la msingi ni kuujaza moyo wetu kwa neno la Mungu ili lituongoze lenyewe ndani ya moyo wetu badala ya kuufuata moyo, bila neno la Mungu moyo utatuendesha sawa na kawaida ya ulimwengu huu, Mwandishi wa Zaburi anaonyesha jinsi alivyoliweka neno la Mungu moyoni mwake na kumuomba Mungu asiongozwe na moyo kusudi kubwa ni ili asimtende Mungu dhambi.

 

Zaburi 119:9-11 “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako. Kwa moyo wangu wote nimekutafuta, Usiniache nipotee mbali na maagizo yako. Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.”

                 

·         Kupenda kutiwa moyo kuliko kukemewa na Bwana – Ni muhimu kufahamu kuwa ni rahisi sana kudanganyika pale watu wanapotutia moyo zaidi kuliko kutukemea, mojawapo ya kazi za kinabii ni pamoja na kutia moyo na kukemea, Neno la Mungu limeweka wazi kuwa Mwana yule anayependwa na baba yake hukemewa, na ikiwa hakuna kukemewa basi unakuwa mwana wa haramu

 

Waebrania 12:5-8 “tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali.”

 

Nyakati za biblia kama ilivyo nyakati za leo watu wengi wakiwemo wafalme hawakuwa wanafurahia sana kukemewa, na badala yake wengi walipenda kutiwa moyo na kuambiwa kila wakati Amani, Amani Amani, jambo hili lilimuudhi sana Mungu na hivyo Mungu aliwaachia manabii wa uwongo wawadanganye, hawa ni manabii ambao kimsingi Mungu hakuwatuma lakini walijikinai wakijua mioyo ya watu inataka nini na wakafanya kama watakavyo na kuwatabiria mema, tu kumbe pepo wa uongo walikuwa wamechukua nafasi ya kuwadanganya

 

Yeremia 29:8-9 “Maana Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Manabii walio kati yenu, na wabashiri wenu, wasiwadanganye ninyi, wala msisikilize ndoto zenu, mnazootesha. Kwa maana kwa jina langu hutabiri maneno ya uongo kwenu; mimi sikuwatuma, asema Bwana.”

 

Yeremia 23:25-28 “Nimesikia waliyoyasema manabii wanaotabiri uongo kwa jina langu, wakisema, Nimeota ndoto; nimeota ndoto. Je! Mambo hayo yatakuwa katika mioyo ya manabii wanaotabiri uongo hata lini, manabii hao wenye udanganyifu katika mioyo yao wenyewe? Wanaodhania ya kuwa watawasahaulisha watu wangu jina langu kwa ndoto zao, wanazomhadithia kila mtu jirani yake, kama vile baba zao walivyolisahau jina langu, kwa ajili ya Baali. Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana.”

 

1Wafalme 22:2-23 “Ikawa, mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme Wa Yuda akamshukia mfalme wa Israeli. Mfalme wa Israeli akawaambia watumishi wake, Je! Hamjui ya kuwa Ramoth-Gileadi ni yetu? Nasi tumenyamaza tusiitwae mkononi mwa mfalme wa Shamu? Akamwambia Yehoshafati, Je! Utakwenda nami tupigane na Ramoth-gileadi? Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Mimi ni kama wewe, na watu wangu ni kama watu wako na farasi zangu ni kama farasi zako.Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la Bwana. Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya pamoja manabii, kama watu mia nne. Akawaambia Je! Niende juu ya Ramoth-Gileadi kuupiga vita, au ninyamaze? Wakasema Kwea; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme. Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii wa Bwana tena, ili tumwulize yeye? Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza Bwana kwa yeye, yaani Mikaya mwana wa Imla; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema, ila mabaya. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi. Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida, akamwambia, mlete hima Mikaya mwana wa Imla. Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wakikaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika sakafu langoni pa Samaria; na manabii wote wakafanya unabii mbele yao. Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, Bwana asema hivi, Kwa hizo utawasukuma Washami, hata waharibike. Na manabii wote wakasema hivyo kwa unabii, wakisema, Kwea Ramoth-Gileadi, ukafanikiwe; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme. Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia sasa, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja husema mema kwa mfalme; neno lako na liwe, nakusihi, kama neno la mmojawapo wao, ukaseme mema. Mikaya akasema, Kama Bwana aishivyo, neno lile Bwana aniambialo, ndilo nitakalolinena. Na alipokuja kwa mfalme, mfalme alimwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-Gileadi kupiga vita, au tunyamaze? Akamwambia, Kwea, ufanikiwe; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme. Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la Bwana? Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji. Bwana akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya? Mikaya akasema, Sikia basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto. Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo. Basi angalia, Bwana ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako.”

 

Unaona Mungu ni baba yetu mwenye upendo, sio kila wakati atatutia moyo tu, kuna wakati atatukemea na kutukaripia ili kutuchonga tuweze kukamilika kwaajili ya utukufu wake, kwa hiyo kila mtu aliyeokolewa anapaswa kukubali makemeo, makemeo hutupeleka katika ngazi nyingine, na hutusaidia kujiangalia na kujiona kama tuko sawa na kama hatuko sawa ni lazima tukubali kutubu, ikiwa hatutakuwa tunapenda kukemewa Mungu ataruhusu manabii wa uongo watudanganye na kwa sababu hiyo ni rahisi kujikuta tumepotea kumbuka wakati wote lililotukuka kwa wanadamu ni chukizo kwa Mungu, tusidanganyike na kusifiwa na wanadamu wakati wote na badala yake tukubali pia na kukosolewa badala ya kujaa sifa tu.

 

Luka 6:26 “Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo.Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi.”

 

Luka 16:15 “Akawaambia, Ninyi ndinyi mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu; kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu.”

 

·         Kuamini kuwa miujiza ilikoma – iko dhana ya baadhi ya jamii za kikristo ambao hawaamini kuwepo kwa miujiza na uponyaji, na wanaamini katika kukoma kwa karama za rohoni baada ya mitume na maandiko wanayoyatumia ni

 

1Wakorintho 13:8-13 “Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.”

 

Kuwa na imani ya namna hiyo kwa tafasiri hii mbaya ya kimaandiko ni kudanganyika hakuna mahali popote pale katika maandiko ambapo inathibitishwa kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kuwa miujiza, ishara na uponyaji ulikoma wakati wa mitume, Mungu hajaacha kuwatendea mema watu wake na kama wako wanaoamini hivyo basi wamepotoka

 

Yakobo 1: 16-17Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike. Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.”

 

Dhana ya kwamba ishara na miujiza na karama za utendaji wa Roho Mtakatifu kukoma havijawahi kuthibitishwa kokote katika maandiko, Neno la Mungu linaonyesha wazi kuwa miujiza, uponyaji na karama za Rohoni ni utendaji wa Mungu na ni sehemu ya kazi ya Mungu kupitia kanisa lake hata leo, maandiko yanaonyesha kuwepo kwa ishara na miujiza na karama za Roho Mtakatifu kwanza ikiwa ni pamoja na ahadi ya Yesu Kristo mwenyewe

 

Yohana 14:12 “Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.”

 

Kukanusha kuwa hakuna ishara na miujiza na karama za Roho Mtakatifu ni sawa tu na kukanusha au kukataa kazi za Roho Mtakatifu, karama hizi ni zawadi zinazotolewa na Roho Mtakatifu kwa kanisa, naelewa kuwa zinatenda kazi kwa kadiri ya viwango vya Imani, lakini haimaanishi kuwa hakuna uponyaji huu wa kiungu.  

 

1Wakorintho 12:4-11 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.”

 

Maandiko aidha yanaonyesha ushahidi kuwa sio mitume peke yao waliofanya miujiza na kwa sababu hiyo awaye yote ambaye anadai kuwa karama zilikoma mara baada ya mitume hana uwezo wa kutosha kuwa Mwalimu wa neno la Mungu, maandiko yana ushahidi wa kutosha kuwa waamini wengine wasiokuwa mitume walitumiwa na Mungu kwa karama mbali mbali kama ilivyokuwa kwa kanisa la korintho na mengineyo

 

Matendo 6:8 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.”

 

Matendo 8:5-7 “Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa.”

 

Hao wanaotajwa katika maandiko hapo juu hawakuwa mitume, lakini walitumiwa kwa viwango vikubwa Mungu Roho Mtakatifu akifanya kazi pamoja nao bila kubagua kiviwango, wale wanaoamini katika kifungu kile cha 1Wakorintho 13:8-13

 

1Wakorintho 13:8-13 “Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.”

 

Kifungu hiki hakizungumzii hata kidogo kukoma kwa karama katika wakati huu wa sasa, Paulo anachozungumzia hapa ni kuwa karama zitakoma wakati wa utimilifu wa wakati  na huu ni ule  wakati Yesu Kristo atakaporudi na wakati wa ufalme wa mbinguni na sio kwa wakati wa mitume wala wakati wa sasa

 

Aidha katika kanisa leo ziko shuhuda mbalimbali nyingi sana za kazi za uponyaji na ishara na miujiza inayoshuhudia kuendelea kuwepo kwa Kazi za Roho Mtakatifu, shuhuda hizi haziwezi kupuuzwa kwa sababu nyingi zinatoka kwa watu waaminifu nikiwemo mimi mwenyewe ambaye nimeombea watu na kuona wakiponywa, Ishara na miujiza ni sehemu muhimu sana inayorahisisha kazi ya injili na kwa sababu hiyo Paulo mtume aliwasihi wakorintho kutamani sana karama za rohoni,  hivyo kuamini kuwa miujiza ilikoma ni imani ya kijinga na ya kipuuzi inayotaka kupuuzia utendaji wa Roho Mtakatifu na kulifanya kanisa kuwa taasisi ya kawaida kama ya kimwili tu isiyo na madhihirisho ya nguvu za Mungu.

 

1Wakorintho 14:1 “Ufuateni upendo, na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu.”

 

·         Kutokupuuzia kanuni ya kupanda na kuvuna – Iko kanuni ambayo inatisha sana ni kanuni ya kupanda na kuvuna wahindi wanaiita Karma, kwamba ni tambia ya kujirudia rudia kwa matendo unayotenda, iwapo unatenda mema kuna namna utakuja kuyavuna kwa wakati wake, lakini vile vile ukitenda yasiyopasa uko uwezekano wa kuyavuna pia, maandiko yanatuonya kutokudanganyika katika hilo, yaani kufikiri hutavuna kile unachokipanda kwa hiyo ukipanda katika mwili utavuna uharibifu na ukipanda katika roho utavuna uzima milele.

 

Wgalatia 6:9-10 “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.”

 

Wagalatia 6:7-8 “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.”

 

Kama hutaki kujiumiza moyo wako basi ni muhimu sana ukaizingatia kanuni hii, hii ni kanuni ya ulimwengu wa roho, Mungu hulipa kisasi na kisasi ni juu yake kwa msingi huo ni muhimu sana kujiepusha kuwafanyia watu mambo yale ambayo wewe hungependa kufanyiwa vinginevyo uwezekano wa kanuni hii kutenda kazi unaweza kuwa mkubwa

 

Mathayo 7:12 “Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii.”

 

Jinsi ya kufanya ili kuepuka udanganyifu.

Maandiko yanatupa tahadhari kwamba tuwe waangalifu ili tusije tukadanganyika kwa msingi huo yale yaliyoelezwa katika kipengele cha pili na mengineyo ambayo sijayaorodhesha lakini Roho wa Mungu yu aweza kukufunulia katika maandiko basi yazingatiwe ili tusiingie katika udanganyifu.

Waebrania 3:12-19 “Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai.Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho; hapo inenwapo, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha. Maana ni akina nani waliokasirisha, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa? Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa? Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale walioasi? Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.”

Luka 21:8 “Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao.”                             

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima

Hakuna maoni: