Andiko
Kuu: Danieli 9:1-2 “Katika mwaka wa kwanza wa
Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya
milki ya Wakaldayo; katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii,
kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia
Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.”
Utangulizi
Ni
muhimu kufahamu kuwa moja ya njia kubwa ya kijiongezea ufahamu na kukua katika
Hekima maarifa na hali ya kiroho ni Pamoja na kuwa na tabia ya kujisomea
vitabu, Neno la Mungu linahimiza Wakristo kuwa na bidii ya kusoma vitabu, hasa
vile vinavyoweka wazi mapenzi ya Mungu na maarifa muhimu kwa maisha yetu.
Danieli aligundua wakati wa ukombozi wa Israeli kwa kusoma vitabu, kwa kuvisoma
vitabu alipata ufahamu, jambo linaloonyesha kuwa kusoma kunafungua macho ya
kiroho kiakili na kiufahamu na kutufanya tujue wakati na mapenzi ya Mungu. Sio
hivyo tu Walimu na wahudumu wa neno la Mungu wanapaswa kuwa na bidii katika
kusoma ili wawe na ujuzi wa mambo mengi na ni ukweli ulio wazi kuwa ujuzi
mwingi umewekwa katika Makala mbali mbali duniani, kwa hiyo kusoma vitabu ni
mapenzi ya Mungu na maandiko yanahimiza kuwa na tabia hiyo:-
1Timotheo
4:13-16 “Hata nitakapokuja, ufanye bidii KATIKA KUSOMA na kuonya na
kufundisha. Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa
unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee. Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili
kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote. Jitunze nafsi yako, na mafundisho
yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na
wale wakusikiao pia”
Unaweza kuona Paulo mtume alimtia moyo
Muhubiri wa injili, mtenda kazi pamoja naye na mwangalizi wa makanisa nyakati
za kanisa la kwanza, Timotheo kwamba afanye bidii katika kusoma na kuonya na
kufundisha, Kwa hiyo utakubaliana nami ya kuwa kusoma ni sehemu muhimu ya
maisha ya mtumishi wa Mungu ni sehemu muhimu ya huduma. Tutajifunza somo hili
muhimu lenye kichwa Kwa kuvisoma vitabu Kwa kuzingatia vipengele vitatu
vifuatavyo:-
- Kwa
kuvisoma vitabu
- Mifano ya
watu walionufaika kwa kuvisoma vitabu.
- Ufanye
bidii katika kusoma.
Kwa kuvisoma vitabu
Tumeona katika utangulizi wa ujumbe
huu ya kuwa Daniel aligundua wakati muhimu wa Ukombozi wa Taifa lake na kuchukua
hatua ya kumuomba Mungu na kumkumbusha juu ya swala Hilo, hii inatufungua akili
ya kuwa yako mambo ambayo ni ya kiroho kabisa na ya kimwili na kitaifa ambayo
yanaweza kuwa bayana kwetu kupitia kusoma, Daniel alikuwa Nabii na Kuna mambo
ambayo aliweza kumuomba Mungu ili afunuliwe, lakini maswala mengine aliyapata
Kwa kusoma vitabu tena vya manabii kama Yeremia aliyekuwa Nabii kabla ya yeye
na aliyekuwa kama yeye tu
Danieli 9:1-2 “Katika mwaka wa kwanza
wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya
milki ya Wakaldayo; katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii,
kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia
Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.”
Kumbe basi Kwa kusoma vitabu tunaweza
kupata mambo mengi ya muhimu, Kwa ufupi Kuna faida kubwa nyingi mno zitokanazo
na kusoma vitabu hapa nitataja baadhi Lakini kabla ya kutaja nitaelezea kwa
kifupi vitabu ni nini hasa?:-
Kitabu au vitabu ni mkusanyiko wa
maneno yaliyowekwa pamoja kwa kusudi la kufunga au kuainisha au kutaarifu
ujumbe Fulani, au fundisho Fulani au maelekezo Fulani, ambayo yamekusudiwa
kuwafikia watu kwa muda Fulani au maisha yote, kitabu kinaweza kusomwa au
kuandikwa, inaweza kuwa ni kazi Fulani ambayo Mungu anataka iwekwe kwa kusudi
Fulani
Yohana 1:11 “Nalikuwa katika Roho,
siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu,
ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa
saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na
Laodikia.”
Kitabu kinaweza kuwa maandhishi
yanayoanzia ukurasa mmoja na zaidi ambayo yamefungwa katika kifuniko kimoja, au
mgawanyo mkubwa sana wa vifungu, utenzi, kweli, jumbe, sheria, taratibu, maonyo
au maelekezo. Zamani sana vitabu viliandikwa katika magombo ya ngozi na kwa
sababu hiyo pia viliitwa chuo
Luka 4:16-17 “Akaenda Nazareti, hapo
alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi
yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo,
akatafuta mahali palipoandikwa,”
Pia viliandikwa katika mawe, na
vilianza kujulikana kama vitabu kwenye karne nne baada ya Kristo 400 AD na Karatasi zilikuja kugunduliwa kwenye karne
ya 15 hivi kwa sababu hiyo hata Biblia
maana yake imetokana na neno la asili la kiyunani Biblos ambalo maana yake ni
mkusanyiko wa vitabu au maktaba yaani Library, na katika biblia kujna mkusanyiko
wa vitabi 66 yaani 39 katika agano la kale na 27 katika agano jipya, Biblia ni
Library au maktaba ya neno la Mungu, nan je yako viko vitabu vingine, hata somo
hili na jumbe ninazohubiri kwa njia ya maandishi ni vitabu
Ndani ya vitabu kuna maarifa, kukuza
ufahamu, kujenga uadilifu, kutia moyo, kuburudisha na kukuandaa kwaajili ya
ubunifu, katika ulimwengu wa sasa vitabu vinaweza kuwa katika mtindo wa nakala
laini zinazopatikana katika mtindo wa kidigitali maandiko yanapotutia moyo
kujisomea ni pamoja na makala hizo. Baadhi ya faida zipatikanazo katika vitabu baadhi
ni kama ifuatavyo:-
- Ufahamu wa Mapenzi ya Mungu
Danieli alipata maarifa kuhusu miaka 70 ya utumwa kwa wana wa
Israel huko Babeli na kutambua kuwa wakati huo ulikuwa umetimia na hivyo
akaanza kufunga na kuomba ili Mungu amfunulie nini cha kufanya, aliweza kuyajua
mapenzi hayo ya Mungu kwake na taifa lake kwa kusoma unabii wa Yeremia yaani
kwa kusoma vitabu vya manabii waliomtangulia
Yeremia 25:8-12 “Basi Bwana wa majeshi asema hivi, Kwa kuwa
hamkuyasikiliza maneno yangu, angalieni, nitapeleka watu na kuzitwaa jamaa zote
za upande wa kaskazini, asema Bwana, nami nitatuma ujumbe kwa Nebukadreza,
mfalme wa Babeli, mtumishi wangu, nami nitawaleta juu ya nchi hii, na juu yao
wakaao ndani yake, na juu ya mataifa haya yote yaliyopo pande zote; nami
nitawaangamiza kabisa, na kuwafanya kitu cha kushangaza, na kitu cha kuzomewa,
na ukiwa wa daima. Tena, nitawaondolea sauti ya kicheko, na sauti ya furaha,
sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na nuru
ya mishumaa. Na nchi hii yote pia itakuwa ukiwa, na kitu cha kushangaza; nayo
mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini. Na itakuwa miaka hiyo
sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na taifa lile, asema Bwana,
kwa sababu ya uovu wao, nayo nchi ya Wakaldayo pia; nami nitaifanya kuwa ukiwa
wa milele.”
Hii inafundisha kuwa wakati mwingine ili kuyajua mapenzi ya
Mungu na kujua mpango wa Mungu kunahitaji kusoma na kutafakari maandiko na
vitabu vyenye hekima ya kiroho. Au vitabu vya watu wengine wenye roho wa Mungu
kama sisi waliofunuliwa maswala kadhaa na kuamua au kusukumwa wayaweke maswala
hayo katika vitabu, kusoma huku kunatuletea ufahamu wa maswala ya kiungu, Yesu
alikuwa na ufahamu wa Tabia ya Daniel nay eye mwenyewe alikuwa anaufahamu
unabii wa Daniel na hata alipokuwa akifundisha maswala kadhaa kuhusu Daniel
alikazia kwa maneno asomaye na afahamu, kwa sababu alijua kuwa ndani ya kusoma
kuna maarifa, kuna ujuzi na kuna ufahamu utapata ufahamu mwingine wa kiroho
kupitia kusoma.
Mathayo 24:14-15 “Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu
wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja. Basi
hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli,
limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu),”
Kumbe tunaweza kupata fahamu na maarifa ya kiroho kutoka
katika vitabu, ni wazi kuwa Daniel alisoma kitabu cha nabii Yeremia, lakini
vile vile sio jambo la kushangaza kwamba Yesu naye alisoma kitabu cha unabii wa
Daniel na kunukuu kama unavyoweza kuona hapo kwa hiyo kwa kuvisoma vitabu
tunaweza kupata maarifa na ufahamu na kutyajua mapenzi ya Mungu katika maisha
yetu
2.
Kuongezea
maarifa na ukuaji wa kiroho.
Kusoma vitabu yaani Biblia na vitavu vya kiroho kunakuongezea
maarifa na ukuaji binafsi wa kiroho na kukupa mwanga, mwongozo, na ufahamu wa kina
na uelewa mpana wa maswala ya kiroho, falsafa, Hekima na utendaji wa kitheolojia
(Practical Theology), usomaji huu utakuongeza
nguvu za kiroho, ufahamu kuhudu mapenzi ya Mungu na kutimiza kusudi la kuwako
kwako duniani, sio hivyo tu utajengwa, utatiwa moyo na kupanua ufahamu wako
ambao kimsingi utakufanya uwe tofauti na wahudumu wengine wa injili
2Timotheo 3:14-17 “Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na
kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa
tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata
upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya
Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa
kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili,
amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”
Mithali 4:5-8 “Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala
usiyakatae maneno ya kinywa changu. Usimwache, naye atakuhifadhi; Umpende, naye
atakulinda. Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote
jipatie ufahamu. Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia.”
Unaona maandiko yanatukumbusha hapa kuhusu umuhimu wa hekima
na maarifa ambayo yatakulinda, yatakuongoza, yatakuadabisha, yatakuhifadhi, na
yatakukuza
3.
Kukuza
Uwezo wa Kufundisha na Kuhubiri.
Kuwa Mwalimu wa neno la Mungu na Mwalimu katika fani
nyinginezo, kunahitaji umahiri, kunahitaji taaluma na mbinu maalumu, Yesu Kristo alikuwa Mwalimu kweli kweli na Paulo Mtume pia alikuwa Mwalimu kweli
kweli na Nabii Musa pia alikuwa Mwalimu kweli kweli, ili uweze kuwa Mwalimu
mzuri mwenye uwezo mkubwa wa kufundisha na kuhubiri ni lazima USOME, sio lazima
tu mfumo maalumu wa kielimu, Lakini pia mfumo binafsi wa kielumu ambao kimsingi
ni pamoja na kujitia nidhambu ya kusoma vitabu, ili kupata ujuzi wa maswala
mbalimbali, Mwalumu mzuri anaweza kusoma mpaka vitabu vingine vilivyoandikwa n
ahata watu wa Imani potofu, sababu kubwa ni ili kujua yaliyomo kwa makudusi ya
kuweka sawa kweli za kimungu, huwezi kufundisha kitu ambacho huna. Kwa hiyo ni
lazima ujuzi wa neno la Mungu ukae kwa wingi ndani yako ili uweze kuwa na kitu
cha kuwafunza wengine na ili ufanikiwe
katika hilo njia pekee na rahisi ni kwa kuvisoma vitabu, kuna sifa kubwa tano
tu za Mwalimu mwema ambazo Yesu Kristo Mwalimu kuu alikuwa nazo Mwalimu mwema
ni lazima awapende watu wake, Mwalimu mwema ni lazima awajue watu wake, Mwalimu
mwema ni lazima alijue somo lake, Mwalimu mwema ni lazima ajue jinsi ya
kufundisha na Mwalimu mwema ni lazima aishi kile anacho kifundisha, sasa ili
uweze kuwa Mwalimu mwema ni aidha uwe mtu uliyechukua muda mrefu sana kujifunza
na unayeeendelea kujifunza lakini ni laaimza kuvisoma vitabu iwe ni sehemu ya
maisha yako ya kila siku ya kujitoa nay a kinidhamu
Matendo
7:22 “Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri,
akawa hodari wa maneno na matendo.”
Luka 1:46-47 “Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi
katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia
walistaajabia fahamu zake na majibu yake.”
Matendo 22:3 “Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa
Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa
sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi
nyote mlivyo leo hivi;”
1Timotheo 4:13 “Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya
na kufundisha.”
Wote tunaowasoma katika maandiko waliokuwa watumishi wa Mungu
na kurumiwa na Mungu kipekee walikuwa watu waliokuwa na bidi katika kujifunza
na kusoma, Mwalimu hawezi kuwa na kitu cha kuwapa watu kama yeye mwenyewe hana
vitu vilivyozidi, uwezo wetu wa kuhubiri na kufundisha na kuyapanda maarifa
unaweza kuwa bora zaidi siku hadi siku kama tu endapo tutatia bidi katika
kusoma vitabu na kwa kuvisoma vitabu tutakuwa na ujuzi wa mambo ambayo
tunatamani katika huduma zetu kuwafundisha na kuwahubiri wengine, kila Mtumishi
wa Mungu licha ya maswala mengine anapaswa kuwa na maisha yaliyojaa kusoma ili
awe na ujuzi sahihi katika yote atakayokuwa anayazungumza kwa watu wenye uelewa
na ufahamu na elimu tofauti tofauti.
4.
Kukuza
uwezo wa kufanya uchambuzi wa kina
Kwa kuvisoma vitabu utaongeza uwezo wako wa kufanya uchambuzi
wa kina, utakuwa na uwezo wa kuweka mambo bayana na kwa ufasaha, ukiwa na uwezo
wa kutambua mawazo mbalimbali ya watu na kuwa kama mtu uliyeandaliwa ukiwa na
majibu mbali mbali yenye ufumbuzi wa watu kwa jamii, wako watu katika maandiko
ambao walikuwa hodari, lakini uhodari wao ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na
uwezo wa kujifunza na kusoma uliokuwa nyuma yao ambapo Roho Mtakatifu
aliwawezesha kuwa na taarifa za kina na za kutosha kiasi cha kuweza kuvutia
jamii zao za wakati ule
Matendo 6:8-10 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya
maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi
lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale
wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza
kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.”
Matendo 18:24-26 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa
Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko.
Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa
ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua
ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila
na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi
zaidi.”
Matendo 17:11 “Mara hao ndugu
wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia
katika sinagogi la Wayahudi. Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa
Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo,
wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.”
Watu wote hao walikuwa na uwezo mkubwa sana wa kufanya
uchambuzi wa kimaandiko, uwezo mkubwa wa kujieleza na kuelezea kwa sababu
walikuwa watu wenye hekima, walikuwa nawatu wa elimu na walikuwa watu waungwana
hawa ni watu waliokuwa wakiitafuta kweli na kuwa na kiu ya kutaka kuwajulisha
wengine kile walichokuwa wamemeza nguvu kubwa ya msukumo na utendaji mkubwa wa Roho
wa Mungu ndani yao haukuwa tupu tu ulichangiwa na maarifa waliyokuwa wameyabeba
na ni namna gani waliweza kuwa na uwezo huo ni kwa kuvisma vitabu
5.
Kusoma
ni amri
Mungu aliwaamuru watu kusoma wakati huo kitabu pekee cha
kusoma kilikuwa ni Torati tu na haikuwezekana kupatikana kwa kila mtu hivyo
watu walijifunza na kusomewa na kuisikiliza
tu lakini leo hii Mungu ameamuru watumishi wengi wa Mungu kuandika
wanaandika masomo mbalimbali, wanaandika vitabu, wanapewa jumbe na kutoa muda
wao kuandika sana kwa hiyo leo hii tunaweza kujiongeza kuwa tuisome Biblia
ambalo ni neno la Mungu, tuende katika vyoa vya biblia na kujifunza kutoka kwa
walimu walioidhinishwa lakini vile vile tusiache kusoma vitabu vya kiroho na vipeperushi
mbali mbali na maandiko mbalimbali ya kiroho ambayo kimsingi yanaandikwa kwa
lengo na kusudi la kuujenga mwili wa Kristo, katika maandiko watu wengi sana
waliamuriwa na Mungu kusoma kwaajili ya mafanikio ya huduma zao na maisha yao
Kumbukumbu 31:9-13 “Musa akaiandika torati hii, akawapa makuhani, wana wa
Lawi, waliolichukua sanduku la agano la Bwana, na wazee wote wa Israeli. Musa,
akawaamuru, akasema, Mwisho wa kila mwaka wa saba, wakati wa maachilio, wakati
ulioamriwa wa sikukuu ya vibanda, Israeli wote wafikapo ili kuonekana mbele za
Bwana, Mungu wako, mahali pale atakapopachagua, uisome torati hii mbele ya
Israeli wote masikioni mwao. Wakusanye watu, wanaume na wanawake na watoto, na
mgeni wako aliyemo malangoni mwako wapate kusikia na kujifunza, na kumcha
Bwana, Mungu wenu, na kuangalia kutenda maneno yote ya torati hii; na watoto wao
wasiojua, wapate kusikia na kujifunza kumcha Bwana, Mungu wenu, siku zote
mtakazokaa katika nchi mnayoivukia Yordani ili kuimiliki.”
Yoshua 1:6-9 “Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe
utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa.
Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote
aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa
kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke
kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia
kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo
utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi
niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa
kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”
1Wafalme 2:1-4 “Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia
Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari,
ujionyeshe kuwa mwanamume; uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika
njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake,
sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila
ufanyalo, na kila utazamako, ili Bwana afanye imara neno lake alilonena kwa
habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele
zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa
mtu katika kiti cha enzi cha Israeli.”
Mifano ya watu walionufaika kwa kuvisoma
vitabu
Tumeona
katika kipengele kilichotangulia umuhimu wa kuvisoma vitabu, licha ya kuwa na
faida kadhaa nyingi ikiwepo pamoja na kupunguza stresses yaani mkandamizo wa
mawazo, kuongeza ufanisi katika ujuzi wa lugha na kungezea misamiati na kukupa
ujasiri na kukutia moyo vitabu pia vinaonekana kuwanufaisha watu mbali mbali
katika maeneno mbalimbali duniani, lakini katika maandiko nitatoa hapa mifano
michache sana ya watu walionufaika kwa usomaji, ambao kimsingi usomaji ulikuwa
na manufaa katika maisha yao ya kimwili na kiroho
Yesu Kristo - kwa mfano maisha yake na
maneno yake na matendo yake yote yalikuwa yametanguliwa kuandikwa kwa hiyo yeye
alikuja duniani akiwa anajua wapi pa kukanyaga kwa sababu aliandikiwa yeye
mambo yote
Zaburi 40:6-8 “Dhabihu
na matoleo hukupendezwa nazo, Masikio yangu umeyazibua, Kafara na sadaka za
dhambi hukuzitaka. Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la chuo
nimeandikiwa,) Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.”
Waebrania 10:5-7 “Kwa
hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili
uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo;
Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa)
Niyafanye mapenzi yako, Mungu.”
Vifungu
hivyo vya maandiko ni vya muhimu sana katika maisha ya Bwana wetu Yesu na kwetu
wenyewe, Mungu alikuwa ameshachoshwa na matumizi ya wanyama na dhabihu za
sadaka za kutekeketezwa na hivyo
alikuwa ameandaa mpango ya kuwa mtu mmoja wa kipekee aliyeandikiwa mapenzi ya
Mungu ataishi kwa utii kwa kila lililoandikwa katika neno la Mungu na kuwa
atayatoa maisha yake kama sadaka kwaajili ya wengi na hivyo kutimiza mpango au mapenzi yote ya
Mungu, Yesu aliyatimiza yote na kila alilolofanya lilikuwa limeandikwa katika
maandiko hakufanya jambo Fulani kwa mapenzi yake na nadhani ili aweze kuatimiza
yote haya aliyasoma kwa umakini na kuyatendea kazi akitimiza yote kwa kufa
kwake msalabani
Wewe
na mimi kama tunataka kunufaika na kuyajua mapenzi ya Mungu nay ale ambayo
Mungu ametuandikia tuyafanye hatuna budi kujisomea Biblia ambayo kmsingi ni
Library/ Maktaba ya vitabu na kuchungulia yake tuliyoandikiwa ili tuyafanya na
kuyatimiza, kwa hiyo Yesu alifaidika na kila alichokuwa ameandikiwa kukifanya
kwa sababu viliwekwa katika gombo la chuo alisoma na kuishi kile alichokisoma
Luka 4:16-21 “Akaenda
Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama
ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya,
akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu,
Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha
huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo,
akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi
wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni
mwenu.”
Unaona
je unafahamu kuwa mambo mengi ambayo tunapaswa kuyatimiza duniani tumeandikiwa?
Lakini unawezaje kuyatimiza mapenzi hayo ya Mungu bila kuyasoma basi kila
tuliloandikiwa na kuagizwa liko katika neno la Mungu na maandishi ya kiroho
yaliyoandikwa na watu kwa kusudi la kukutoa katika hatua moja na kukupeleka
katika hatua nyingine unaweza kufaidika vipi katika maisha yako ni kwa kuvisoma
vitabu
Daniel – Aliweza kugudua kuwa wakati wa
ukombozi wa wayahudi umetimia sawasawa na alivyotabiri nabii Yeremia, Daniel
aliweza kuyajua mapenzi ya Mungu kwa klizazi chake n ahata kutujuza mapenzi ya
Mungu ya wakati ujao kwa kusoma vitabu lakini pia kwa kuandika, kwa kusoma
vitabu aligundua wakati wa kukaa utumwani Babeli umetimia na hivyo aliingia
katika maombi ya kitaifa na kutubu kwaajili ya taifa lake akimdai Mungu haki ya
watu wake
Daniel 9:3-19 “Katika
mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa
kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo; katika mwaka wa kwanza wa kumiliki
kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo
neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani,
miaka sabini. Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na
dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. Nikamwomba Bwana,
Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha,
ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya
dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo
yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa
jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote
wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe, lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi
leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio
karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa
yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na
wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni
kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu
wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha
watumishi wake, manabii. Naam, Israeli wote wameihalifu sheria yako, kwa
kugeuka upande, wasiisikilize sauti yako; basi kwa hiyo laana imemwagwa juu
yetu, na uapo ule ulioandikwa katika sheria ya Musa, mtumishi wa Mungu; kwa
sababu tumemtenda dhambi. Naye ameyathibitisha maneno yake, aliyoyanena juu
yetu, na juu ya waamuzi wetu waliotuamua, kwa kumletea mambo maovu makuu; maana
chini ya mbingu zote halikutendeka jambo kama hili, lilivyotendeka juu ya
Yerusalemu. Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Musa, mabaya haya yote
yametupata lakini hata hivyo hatukumwomba Bwana, Mungu wetu, atupe fadhili
zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake. Basi Bwana
ameyavizia mabaya hayo, akatuletea; maana Bwana, Mungu wetu ni mwenye haki
katika kazi zake zote azitendazo; na sisi hatukuitii sauti yake. Na sasa, Ee
Bwana Mungu wetu, uliyewatoa watu wako hawa katika nchi ya Misri kwa mkono
hodari, ukajipatia sifa, kama ilivyo leo; tumefanya dhambi, tumetenda maovu. Ee
Bwana sawasawa na haki yako yote, nakusihi, hasira yako na ghadhabu yako
zigeuzwe na kuuacha mji wako Yerusalemu, mlima wako mtakatifu; maana kwa sababu
ya dhambi zetu, na maovu ya baba zetu, Yerusalemu na watu wako wamepata
kulaumiwa na watu wote wanaotuzunguka. Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize
maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu
pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana. Ee Mungu wangu, tega sikio lako,
ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina
lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu
ya rehema zako nyingi. Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana,
usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu
mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako. Basi hapo nilipokuwa nikisema, na
kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu Israeli, na kuomba
dua yangu mbele za Bwana, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu
wangu; naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona
katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu
ya jioni. Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danieli, nimetokea sasa, ili
nikupe akili upate kufahamu.”
Kutoka
katika hatua ya kuvisoma vitabu Daniel anaonekana kugundua kuwa walifanya
dhambi, walifanya makosa, hawakuwasikiliza manabii, alitubu aliomba alitambua
kuwa yaliyowapata yameandikwa katika torati ya Musa, na pia yalitolewa kama
maonyo na kina Yeremia, na kutokea hapo alijibiwa maombi yake na malaika
Gabriel na kufunuliwa mambo muhimu sana yanaoihusu Israel na wakati wa Masihi n
ahata sisi leo, Daniel aliwezaje kuwa nabii mzuri kiasi kile ni kwa sababu
alinufaika katika kusoma vitabu, vitabu vya manabii waliomtangulia
Towashi wa kushi – Alikuwa ni mtu wa
Kushi yaani Ethiopia alikuwa mkazi wa Afrika lakini alikuwa mtu Mcha Mungu
aliyemheshimu Mungu wa wayahudi kule Israel alikuwa akipanda siku za sikukuu
kwaajili ya kuabudu na inaonekana wazi licha ya cheo chake kikubwa alikuwa
anapenda kusoma, hata hivyo hakuwa amefahamu kwa ufasaha yale aliyokuwa
anayasoma, lakini Mungu kwa Rehema zake alimtuma mwinjilisti Philipo kumwendea
na kumfahamisha na alipoelewa maandiko maisha yake ya kiroho yalibadilika sana
Matendo 8: 26-39 “Malaika
wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata
njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa. Naye
akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini
ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa
amekwenda Yerusalemu kuabudu, akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo
cha nabii Isaya. Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili,
ukashikamane nalo. Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii
Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma? Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu
asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye. Na fungu la
Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo,
Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo
yeye naye hafunui kinywa chake. Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa.
Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika
nchi. Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno
haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine? Filipo
akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari
njema za Yesu. Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule
towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe? Filipo
akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya
kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.] Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka
wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha, walipopanda
kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena;
basi alikwenda zake akifurahi.”
Kwa
hiyo kumbe unaweza kukubaliana nami pamoja na maandiko ya kwamba kuna faida
kubwa sana zinazoweza kupatikana kwa mambo yaliyoandikwa, kwa hiyo maandiko
yanatutia moyo kusoma, yanatutia moyo kizitafuta kweli na kweli nyingine
zimeandikwa wazi na kuwekwa katika maandishi na watumishi wa Mungu mbalimbali
nikiwemo mimi, ili kukufundisha na kukufunulia mapenzi ya Mungu na uweze
kunufaika na kuenedna na kuishi kwa hayo, kwa kupitia kusoma vitabu Mungu
anaweza kuanzia hapo na kukupeleka katika viwango vingine, Miaka mingi nyuma
Mungu alisema na mimi na kuniambia na kuniamuru kuandika alisema na mimi katika
njozi ya usiku na katika njozi hiyo alinilisha kalamu mdomoni mwangu na tangu
wakati huo sisikii Amani kukaa kimya bila kuandika, ninatumia muda mwingi
kuandika, na vocha nyingi kurusha masomo yangu bure katika mitandao ya kijamii,
siweki namba zangu kuomba mchango wa kitu chochote, siuzi masomo yangu, sizuii
mtu kujisomea na kuyahubiri kwa sababu sio ya kwangu, Mungu alinipa kwaajili ya
kanisa lake, sipendelei mtu yeyete ninapoandika wala dhehebu lolote mimi
nimeamriwa niseme tu kile Mungu anataka nikiseme na ameniamuru kuyaweka yote
katika maandishi lakini ni nani atakayefaidika ni yule atakayeondoa uvivu na
kusoma, na kwa kuvisoma vitabu na maandishi haya utajengeka na kunufaika kroho!
Sio wewe tu na kanisa lako unalolihudumia, utanufaika kama walivyonufaika watu
wengine, maarifa mengi sana yamefichwa katika vitabu hivyo hakikisha unajisomea
ukiyapenda mafunsiho yangu chukua namba zangu yaombe omba somo lolote katika
whatsapp nitakurushia bure kwa sababu neno la Mungu limesema mmepewa bure toeni
bure
Ufanye bidii katika kusoma
Neno la Mungu linatutia moyo kuwa
tusome, kusoma sio jambo lenye kufurahisha sana, kama ilivyo kuandika pia, ili
usome au kuandika ni lazima uutoe sadaka Muda wako, ujifungie na utafute
utulivu, ukae muda mrefu sana, na suome sana na kupitia maandiko mengi sana na
chunguzi nyingi sana jambo hili bila bidi, unaweza kujikuta unaingia uvivu wa
kusoma na kuandika pia, kwa hiyo neno la Mungu linatutaka tuwe na bidi katika
kusoma Ezra alikuwa Mwalimu wa neno la Mungu, na Mungu alimtumia kuleta uamshi
mkubwa sana kupitia mafundisho yake lakini kabla ya kutumiwa na Mungu Ezra
alitia bidi katika kusoma na kufundisha
Ezra 7:6-10 “huyo Ezra akakwea kutoka
Babeli; naye alikuwa mwandishi mwepesi katika sheria ya Musa, aliyokuwa ameitoa
Bwana, Mungu wa Israeli; naye mfalme akamjalia matakwa yake yote, kama mkono wa
Bwana, Mungu wake, ulivyokuwa pamoja naye. Nao wakakwea baadhi ya wana wa
Israeli, na wa makuhani, na wa Walawi, na waimbaji, na mabawabu, na Wanethini,
ili kwenda Yerusalemu, katika mwaka wa saba wa mfalme Artashasta. Naye Ezra
akafika Yerusalemu mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa huyo mfalme. Maana
alianza kukwea kutoka Babeli siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, naye akafika
Yerusalemu siku ya kwanza ya mwezi wa tano, kama mkono mwema wa Mungu wake
ulivyokuwa pamoja naye. Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake
kuitafuta sheria ya Bwana, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika
Israeli.”
Ezra alikuwa mwandishi yaani Mwalimu
na ndiye mwanzilishi wa kundi la waandishi, yaani walimu wa Torati, maneni
aliuelekeza moyo kuitafuta sheria ya bwana na kuitenda na kufundisha maagizo na
hukumu katika Israel ni ushahidi wa moyo wake kuwa alijikita katika kusoma na
kuyaishi yale aliyojifunza ili afundishe , jambo la namna hii linahitaji
kujitia na linahitaji bidi alikuwa na bidii jambo hili ni sawa tu na Paulo
mtume alivyomuagiza Timotheo kuwa anwe na bidi katika kusoma na kufundisha 1Timotheo 4:13 “Hata
nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha.”
Wote
tutakuwa tunakumbuka na kufahamu kuwa Paulo mtume ndiye mtume aliyeandika
vitabu vingi sana na kufanya kazi kubwa kuliko mitume wote lakini ni ukweli
ulio wazi kuwa mtume huyu msomo licha ya kupata elimu mbali mbali na mafuno
makubwa ya aina mbalimbali maisha yake yote mpaka uzee wake hakuacha kuwa na
tabia ya kusoma vitabu
2Timotheo 4:9-13 “Jitahidi
kuja kwangu upesi. Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa,
akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda
Dalmatia. Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja
nawe, maana anifaa kwa utumishi. Lakini Tikiko nalimpeleka Efeso. Lile joho
nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu, hasa vile vya
ngozi.”
Paulo
mtume alikuwa gerezani, alimwandikia Timotheo waraka wa kumtia moyo, akimhimiza
pia kumtembelea upesi hata hivyo aliagizia joho lake bila kusahau vitabu vyake
hasa vile vya ngozi, yaani maana yake alitaka maktaba yake iwe karibu naye
maisha yake yalijawa na kusoma vitabu kila wakati kama unataka kuwa wa kiroho
kama Paulo mtume basi usiache pia kusoma vitabu na maandishi mbali mbali ili
kujiimarisha katika maisha yako ya kiroho na huduma, kiufupi tu nilitakiwa
nikuambie soma vitabu basi , Paulo alikuwa na mafunuo mengi sana aliandika
nyaraka nyingi sana lakini alikuwa akisoma sana vitabu ndugu uwe na bidi katika
kusoma vitabu
Uvivu
wako sio wako ni kuwa shetani hataki usome vitabu, hataki uwe na maarifa kwa
sababu mengi ya maarifa hayo watu wa Mungu na waliotembea na Mungu wameanika
siri hizo katika vitabu shetani anajua utamwambia imeandikwa kwa hiyo atakuzuia
uwe mvizu usijisomee ili usiwe na maarifa na hatimaye uweze kuishiwa, sasa kama
wewe kuhani huongezi maarifa, hujisomei vipi kuhusu watu wako?
Hosea 4:6-9 “Watu
wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi
nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi; kwa kuwa umeisahau sheria ya
Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.Kadiri walivyozidishwa, kwa
kadiri iyo hiyo walinitenda dhambi; nami nitageuza utukufu wao kuwa aibu.
Hujilisha dhambi ya watu wangu, hujifurahisha moyo kwa uovu wao.Hata itakuwa,
kama walivyo watu, ndivyo atakavyokuwa kuhani; nami nitawaadhibu kwa ajili ya
njia zao, na kuwalipa kwa matendo yao.”
Kusoma
vitabu kutakusaidia kuongeza ufahamu, kujilinda na mapokeo ya wanadamu,
kujilinda na taratibu za kidini, kuleta uamsho, kujijenga kiroho kuepuka ujinga
wa kiroho na kadhalika lakini pia kuepuka mitego ya adui
Mafanikio
yoyote ya kimwili na kiroho yanategemea na ustawi wako katika maarifa, Wakristo
wanapaswa kuelewa kuwa wanatakiwa wawe na bidi katika kujisomea na kuyachunguza
maandiko na pamoja na Biblia kusoma vitabu vingine vya kiroho ili wafunguliwe
nataka nikuhakikishie kuwa kama umsomaji wa vitabu unaweza kuwa na maarifa
makubwa sana kuliko hata wale viongozi wa kiroho ambao wako busy na masala ya
maongozi wakihangaika huko na huko kwenye vikao na mikutano na maswala ya
kikatiba na kuacha kuwa na Muda wa kujisomea ikiwa Paulo Mtume aliyekuwa
gerezani aliagizia vitabu mimi ni nani nisiwe na Muda wa kujsomea kila nipatapo
nafasi soma vitabu
HITIMISHO
Kama
Danieli alivyosoma vitabu na kupata maarifa kuhusu mpango wa Mungu, vivyo hivyo
Wakristo wanapaswa kuwa na tabia ya kusoma vitabu vya kiroho. Kusoma kunasaidia
kujua mapenzi ya Mungu, kukua kiroho, na kuwa tayari kwa kazi ya Bwana.Je,
unajipa muda wa kusoma vitabu vyenye maarifa ya kiroho? Kama hufanyi hivyo anza
sasa katika jina la Yesu kristo na utakuja kunishukuru baadae
Na Mchungaji Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni