Jumatano, 12 Februari 2025

Mkijijenga juu ya Imani yenu!


Yuda 1:20-21 “Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu, jilindeni katika upendo wa Mungu, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo, hata mpate uzima wa milele.



Utangulizi:

Mojawapo ya changamoto kubwa tuliyonayo katika nyakati za leo ni pamoja na kuwa na wakristo dhaifu sana, na walio legelege mniwie radhi kwa lugha hii niliyoitumia, ukilinganisha na wakristo wa miaka ya nyuma, Lakini sababu mojawapo kubwa ambayo imepelekea wakristo wa nyakati za leo kuwa dhaifu licha ya kuwa kuna teknolojia kubwa na upatikananaji rahisi wa mafundisho ya neno la Mungu katika mitandao, na hata kuwepo kwa vitabu vikubwa vya mawazo na michango mbalimbali ya kibiblia ambavyo zamani vilikuwa ghali sana kuvipata, lakini siku hizi unaweza kuvipakua kutoka kwenye mitandao ya kijamii hata bure mfano hata kupitia “www.pdfdrive.com” Pamoja na hayo bado kuna upungufu mkubwa wa wakristo wa nyakati za leo kushindwa kuwa na uwezo wa kujijenga kiimani na kuwa imara kiasi cha kuweza kuitetea imani, kujijenga kiimani hakutofautiani sana na kujijenga kiafya kwa kufanya mazoezi ili uwe na afya nzuri, kujiweka vizuri, kuhakikisha unakuwa na nguvu na kuwa fiti au kuwa imara kimwili, sasa katika hali kama hiyo hiyo kujijenga katika imani kuna maana ya kufanya mazoezi na kujiandaa ili uweze kuwa vizuri na hata kukabiliana na mazingira yoyote yale ya mashambulizi ya kiroho na kiimani na zaidi ya yote kuweza kuwa na uwezo wa kupambanua mafundisho yasiyo sahihi, na yaliyo sahihi na hata kuweza kuwasaidia wengine. 

1Wakorintho 9:25-27 “Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika. Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.”

Paulo mtume anayafananisha maisha ya kiroho na maisha ya wanamichezo ambao wakati wote mazoezi ni sehemu ya maisha yao, wanamichezo huchukua mazoezi ya aina mbalimbali kwaajili ya kujenga afya ya miili yao na kwaajili ya kukabiliana na ushindani wa aina mbalimbali wanaoweza kukutana nao katika mashindano ya aina mbalimbali, mtu anapokuwa hana nidhamu ya mazoezi uwezo wake wa kustahimili na kushindana hupungua na kuwa rahisi kushindwa, vivyo hivyo katika maisha ya kiroho, na ndio maana Paulo mtume anasema naye anashiriki zoezi anashiriki kujitia nidhamu ili asiishie kuwahubiri wengine kisha yeye akawa mtu wa kukataliwa. Mazoezi ya kiroho yanaweza kuhusisha, kuabudu, kuomba, kusoma neno la Mungu, kufunga, kutoa, kustahimili majaribu, kuishindania Imani, kusoma vitabu vya kiroho, kuijua misingi ya imani yako na kuisimamia, na kukua katika hekima na busara.

Katika kifungu cha msingi, ambacho ndio moyo wa somo letu leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kile anachokizungumza Yuda ili sisi nasi tuweze kujijenga juu ya imani yetu jambo ambalo litatusaidia kukuwa kiroho na kiufahamu na kuweza kuishindania Imani. Moja ya dalili zinazonyesha kuwa watu wengi hawajajengeka kiufahamu ni pamoja na kuchukuliwa huku na kule na kila wimbi la mafundisho na mlipuko wa kimakanisa ua kimahubiri na au wafanya maombezi na kadhalika.

Waefeso 4:11-14 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.”

Unapoliangalia kanisa la Mungu katika nyakati za leo utaweza kuona kwa uwazi kuwa watu wana upungufu mkubwa sana wa uwezo wa kuisimamia na kuitetea Imani, kwa sababu kwanza ni kama hawajui hata wanachokiamini na badala yake wamekuwa washabiki wa makundi mbalimbali ya milipuko ya kiinjili, watu wana ukuaji hafifu wa kiroho na ni kama wanakosa misimamo na sababu kubwa ni kutokujijenga kiroho na kuacha kujijenga kiimani, kwa hiyo kila wanachoambiwa na watu wajanja wajanja wanatii bila kuuliza uliza wala kuhoji ni kama watu wanapokea imani na mafundisho kwa njia ya hisia zaidi kuliko kwa njia ya kutumia akili na nadhani wanafikiri labda kutumia akili ni dhambi, sio dhambi kutumia akili katika kujifunza neno la Mungu na kuhoji juu ya maswala ya kiimani, na kimaandiko, tunapoteza uungwana wa kujifunza kwa sababu imani yetu imejengwa katika kupokea zaidi bila kuhoji, kutii zaidi bila kufanya uchunguzi, Imani ni kama chakula huwezi kuokota tu na kukipeleka kwa wengine wale bila kujua usalama na ubora wa chakula hicho, kila mtumishi duniani mafundisho yake yanapaswa kupimwa, na kufanyiwa uchunguzi na utafiti ili kubaini kuwa anachokisema ndivyo kilivyo? Bila kujali umaarufu na ukubwa wa mtu

Matendo 17:10-12 “Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi.Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini, na wanawake wa Kiyunani wenye cheo, na wanaume si wachache.”

Watu waungwana ni wale wanayoyachunguza maandiko na kuyapima ili kujithibitishia kama mafundisho hayo ni sahihi au la, na sio swala la kwa sababu andiko limesomwa tu, hata shetani anayajua maandiko na anaweza kuyatumia kwa hiyo ni wajibu wetu sisi kama walaji kupima kama fundisho hilo lina ubora au la. Sasa basi ili tuweze kujijenga kiimani Yuda anazungumza maswala muhimu manne ambayo tunaweza kuyatumia kujijenga katika imani, maswala hayo yanapatikana katika kifungu hiki ambacho tutachukua muda kukitafakari na kukifanyia uchambuzi wetu wa kina katika siku ya leo.

Yuda 1:20-21 “Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu, jilindeni katika upendo wa Mungu, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo, hata mpate uzima wa milele.”

Mkijijenga juu ya Imani yenu - Neno mjijenga juu ya Imani yenu katika Biblia ya kiingereza NIV linasomeka “build yourselves up” au kwa kiingereza changu “by building yourselves up” Neno hilo kujijenga katika kiyunani linasomeka kama “epoikodomeĊ” maana yake kwa kiingereza “to buil up or to build upon” mkijijenga juu ya misingi au msingi wa Imani yenu, au kujenga juu ya msingi ambao umekwishakuwekwa yaani kujijenga juu ya imani ambayo ni takatifu sana ambayo imejengwa juu ya Kristo na mitume na manabii


Waefeso 2:20-21 “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana.”


Kwa sababu hiyo yaani kila mtu aliyeokolewa anapaswa kujijenga katika misingi ya imani anapaswa kujua kuwa anaamini nini na anapaswa kuielewa hiyo misingi ya imani yake, Imani ya kweli imejengwa katika ufunuo ulioletwa kwetu na Yesu Kristo na mitume na manabii kwa hiyo wakristo wakiwa na uelewa juu ya misingi iliyowekwa na Kristo na mitume na  manabii ambayo kimsingi inapatikana katika neno la Mungu na inakazia utakatifu wataweza kuwa na misimamo thabiti kujua wanachokiamini na kukitetea kwa sababu kitakuwa kimewekwa wazi kwao kupitia mafundisho ya neno la Mungu, Yuda alikuwa anaandika waraka wake wakati ambapo kanisa lilikuwa na uvamizi wa mafundisho potofu, walimu wa uongo walikuwa wakilishambulia kanisa kwa mafundisho yasiyo sahihi na hivyo alikuwa akiwataka wakristo waishindanie Imani, na wafikie ngazi ya kuwa na uwezo wa kijisimamia na kuishindania imani 


Yuda 1:3-4 “Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo.” 


Kwa kawaida huwezi kuwaambia watu waishindanie imani kama imani yenyewe hawaijui kwa sababu hiyo kila mkristo anapaswa kuacha uvivu na kukubali kujifunza neno la Mungu kwa kulisoma, kuandika notes na kwa kuuliza maswali, wakristo hawapaswi kuwa wajinga kiasi ambacho hata ukiambiwa kuna kadi za kusamehewa dhambi unanunua, kuna sabuni za upako unaogea tu, ukiambiwa ugali wa upako unajilia tu, hauna hata msingi wa kimaandiko wa kuhoji kuwa agizo la namna hii limeandikwa wapi, katika biblia?  upungufu mkubwa tulio nao leo ni kuwa na wakristo wa hovyo samahani pia kwa neno hilo hii ni kwa sababu ya kukosa watu wanaojitoa katika neno la Mungu na kujifunza imani yao kwa kina na mapana na marefu, Nyakati za Kanisa la kwanza watu walikaa katika fundisho la Mitume na walijifunza neno la Mungu kwa umakini na wakajijengea uwezo wa kuitetea imani, kwa sababu walilijua neno, walilijua kusudi la Mungu na walijua jinsi ya kulitumia neno la Mungu kwa halali na kukuwa kiroho hata kuwa walimu wa wengine. 


Matendo 2:42 “ Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.


Matendo 20:27-28 “Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu. Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.”


2Timotheo2:15 “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.” 


Martin Luther alipokuwa akiishindania imani ilipokuwa imechakachuliwa na wakatoliki aliweka misimamo mikuu mitano ya maswala ya msingi ambayo mtu anayeiamini Biblia na anayemuamini Mungu wa kweli anapaswa kujiuliza kama imani ya mtu huyo haikuzingatia maswali haya muhimu matano tayari alihisi kuna changamoto ya kiimani


Sola scripura (Scripture alone) – Msingi wa Imani hiyo utokane na uwiano wa maandiko na sio mapokeo ya wanadamu.

Solus Christus (Christ alone) – kiini cha ujumbe na njia ya kuhesabiwa haki itokane na kile ambacho Kristo amekikamilisha pale Msalabani, na kwa njia yake na fundisho lake

Sola fide (Faith alone) – kuwa wokovu unapatikana kwa Imani kupitia kazi iliyofanywa na Yesu msalabani sawa na inavyoelekezwa katika maandiko

Sola gratia (Grace alone) – kila tunachokipokea kutoka kwa Mungu kwa njia ya wokovu mwanzo mpaka mwisho kinatokana na neema ya Mungu

Soli deo Gloria (Glory to God alone) – Lolote tunalolipokea na kulifurahia katika wokovu wetu ni kwaajili ya utukufu wa Mungu na sio vinginevyo.


Ni kama Luther aliweka Rula rahisi kwa mwamini wa kawaida kujihoji na kujiuliza kile anachokiamini je ni cha kibiblia? Kimo katika maandiko kwa uwiano wake?, Imani hii ina mtu anatafuta jina au anamuinua Kristo? Imani yake na maelekezo yake ya kiimani yanatokana na neno la Kristo na yanaelekeza huko? Je tunayoyapokea ni kwa neema? Na je Mungu anatukuzwa, kwa wataalamu wa uchambuzi wa neno la Mungu viko vipimo vingi zaidi ya hivi vya kupima mafundisho ya kweli na iko misingi mingi zaidi ya hii lakini hayo ni maswali Muhimu ambayo Mkristo wa kawaida anaweza kujiuliza, Leo hii inasikitisha sana kuona kuwa wakristo hawafundishwi neno la Mungu katika kiwango cha kutosha, na hawajifunzi ipaswavyo, na hawajui hata kusudi la kuweko kwao wala kusudi la Mungu, na wala hawajui kulitumia neno la Mungu kwa halali, tuna wakristo ambao wanaruka huku na huko wakiwa hawajui hata wanalolitafuta, wako wengine wana miaka mingi lakini hawajui lolote wala hata kanisani hawaandiki notisi za kile kinachohubiriwa na kinachofundishwa, mimi ninapoandika neno la Mungu mara baada ya Roho Mtakatifu  kunipa ujumbe kwa kawaida huwa natumia masaa yasiyopungua nane mpaka siku mbili au tatu kuandaa ujumbe, na wakati mwingine wasomaji wangu wameniambia somo zuri lakini ni refuuuuuu, mimi siandiki kwaajili ya watu wavivu, naandika kwaajili ya watu wanaojua ambao Mungu atakuja kuwatumia kuzisoma jumbe zangu na kuzitumia kuujenga mwili wa Kristo na sio lazima somo liishe siku hiyo hiyo, sio hivyo tu kama wewe unaona unatumia vocha nyingi kwa kusoma tu mimi natumia gharama kubwa na muda mwingi kusoma, kutafakari, kuomba kumsikiliza Mungu, kujitenga, kuhariri na kuyarusha kwenye mitandao ili ikufikie, wewe ambaye unaweza kutumia nusu saa tu kujisomea, au unaweza kukopi na kuhamishia kwenye simu yako ukajisomea baadae, wakristo wavivu sio sehemu ya wanafunzi wangu. Mimi wakati ninaokoka pale Mwenge Full Gospel Bible Fellowship ibada ilikuwa inaanza saa mbili asubuhi na inaisha saa mbili usiku wale wanaokumbuka kati  ya 1995-1996 tulipokuwa na ujenzi wakati huo uko ukumbi namba moja tu, hatukuwa tunakula chakula, wala kunywa chai, mchungaji wetu wakati huo @Zachary Kakobe alikuwa akifundisha kwa kutumia maandiko mengi sana, kumsubiri tu mpaka atokee madhabahuni ilikuwa inahitaji uvumilivu, yeye ametusaidia kuwa imara sio kama wakristo wa kidigitali ambao kila saa wanaangalia saa, wanarushiwa maandiko kwenye screens sisi andiko likikupita unakwenda kujitafutia, Mazoezi yale yalitusaidia sana kujijenga kiimani, sisemi kuwa watu wawe na ibada ndefu na zisizoajli muda kwa sababu Mungu ni Mungu wa utaratibu, lakini nasema hatukuona shida wakati uole Mchungaji wetu kutumia muda mwingi na mrefu sana kutuzamisha katika neno la Mungu,  na kumbuka wakati huo Mchungaji wetu alikuwa anasemwa vibaya kila mahali, ukijitambulisha kuwa unasali kwa Kakobe kila anayekusikia anafikiri wewe ni pepo, ulikuwa ni wakati mgumu sana lakini ulitufanya imara sana. Paulo mtume kuna nyakati alikuwa anafululiza kuhubiri na kutoa maagizo mpaka kuna mtu alisinzia akaanguka ghorofani, akafa akafufuliwa na mahubiri yakaendelea  ona ni ukweli unaothibitisha kuwa wakristo wa nyakati za kanisa la kwanza walikaa katika neno kwa muda mrefu sana na hawakusema kuwa amekosa hekima ona:- 


Matendo 20:7-11 “Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane. Palikuwa na taa nyingi katika orofa ile tulipokuwa tumekusanyika. Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka orofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa. Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake. Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hata alfajiri, ndipo akaenda zake.”


Mkristo kaaa katika neno, jifunze neno la Mungu, jadilianeni neno la Mungu, hoji kila kitu usichokielewa, Biblia sasa iko wazi kwa kila mtu, nyenzo za kutusaidia kutafasiri maandiko ziko kila mahali, maarifa yameongezeka, usikubali kuwa miongoni mwa watu wanaoweza kubebeka hovyo hovyo, Maswala ya Mungu yasiwe maswala ya kufanyiwa majaribio, lazima tuyapime maandiko, tuipime miujiza, na tuwapime watumishi wa Mungu wa ngazi yoyote ile hata kama wanashusha moto kutoka mbinguni, mtu aliyejijenga kiimani ataweza kupambanua kwa mujibu wa misingi ya Imani aliyolelewa na iliyo sawa na maandiko.


Kuomba katika Roho - Kuomba katika Roho Mtakatifu ni mojawapo ya njia muhimu sana inayosaidia sisi kuwa imara kiroho na kujijenga wenyewe. Kuomba “Katika” neno hili Katika kwa kiingereza “in” kwa kiyunani ni “en” tafasiri yake kwa kingereza ni “instrumentality” maana yake kwa kingereza “the quality or state of being instrumental” huku ni kuomba kwa ubora na uwepo wa Roho Mtakatifu, kuomba kwa roho, kuomba kupitia Roho Mtakatifu, kuomba tukitumiwa au kwa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu, Wakristo wengi sana wanapenda kuwa mashujaa wa maombi na wengi sana wanajiumiza kwa sababu wanatumia nguvu zao katika kuomba, wanashindana na neno la Mungu ambalo limesema hatujui kuomba kama itupasavyo kuomba kwa sababu hiyo ni lazima tumtegemee Roho Mtakatifu atusaidie katika maombi yetu kila wakati yawe marefu au mafupi, lakini maombi hayo yataenda zaidi ya maneno yetu ya kawaida, na hisia zetu za kawaida na yatakuwa ya ndani sana yenye mzigo na kuugua kwa hivyo  hayatakuwa ya kujilazimisha bali yatakuwa yanabebwa na Roho wa Mungu  kwa hiyo ni lazima uwe naye  na umuhishishe yeye na wakati mwingine utumie muda mrefu kunena. Kabla ya maombi yoyote yale mimi moyoni huwa namwambia Roho Mtakatifu nisaidie kuomba kwa sababu mimi mwenyewe siwezi, na matokeo ya maombi wakati wote yamekuwa yenye ubora.


Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa


Waefeso 6:18 “kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”


Roho Mtakatifu ndiye anayetuumbia hisia za kutaka kuwa na mawasiliano na baba yetu wa Mbinguni, na ni kuomba katika Roho ndiko kunakomuimarisha mkristo kwa kujijenga na zaidi ya yote kuomba katika Roho kunayafanya maombi kuwa rahisi sana kuliko uwezo wetu na zaidi ya hayo ni moja ya silaha za kiroho zinazoainishwa katika neno la Mungu yaani kusali katika Roho, je unamtegemea Roho wa Mungu katika maombi yako? Au unatumia nguvu zako? Je unajijenga kwa kuomba katika Roho? Unanena kwa lugha?


1Wakorintho 14:2-4 “Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake. Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo. Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa.”


Kujilinda katika upendo wa Mungu – hii ina maana gani? Ni muhimu kufahamu kuwa kukaa katika upendo wa Mungu kuna maana pana na rahisi sana katika mtazamo wa agano la kale mwanadamu ndiye aliyekuwa na wajibu mkubwa wa kutumia nguvu, akili na moyo wetu wote katika kumpenda Mungu na kumtii, lakini katika agano jipya tunaelezwa kuwa ni Mungu ndiye aliyetupenda ona:-


Kumbukumbu 6:4-5 “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.”


Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”


Katika agano jipya ni Mungu ndiye aliyetupenda, na Bwana Yesu alitupenda upeo kwa hiyo wajibu wetu mkubwa ni kuitikia upendo huo wa Mungu kwa kukaa ndani yake na kushika yale yote ambayo Bwana Yesu ametuamuru, kwa hiyo mwitikio wetu sio kutumia nguvu na akili mwitikio wetu ni kukubali kwa moyo kukaa katika pendo lake tunampenda kwa sababu alitupenda kwanza, tunampenda kwa sababu ametusamehe, ametuokoa, ametubariki, ametupa uzima, ametulinda, ametupa neema kwa hiyo tunaonyesha mwitikio kwa upendo wake kwa kuendelea kukaa katika upendo wake huo kwa kuzishika amri zake na wala sio nzito ni kwa hiyari na kuitikia  na ni kwa kupenda tu, yaani kumpenda Mungu na wenzetu.


Yohana 15:9-10 “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu.Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.”


1Yohana 4:9-11 “Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye.Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu. Wapenzi ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana.”

 

Neno kukaa katika Pendo la Mungu kwa kiyunani kukaa linatumika neno “MenĊ” neno hili kwa kiingereza ni abide (mara 61), remain (mara 16), dwell (mara 15), continue (mara 11), tarry (mara 9), endure (mara 3), misc (mara 5) kwa jumla limetumika katika maandiko mara 127 maana yake Kukaa, kubaki, kuishi, kuendelea, kawia, vumilia, jistawishe, maneno hayo yanamaanisha kuendelea kuweko katika fungamano na upendo wa Yesu hadi mwisho, ni kama vile wanandoa wanapooana wakapendana au mume akampenda mke akamuoa, ili ndoa hiyo idumu mke anapaswa kuendelea kuwepo kwa mumewe, na shughuli zote katika nyumba na mahusiano zinapaswa kuendelea, kwa hiyo mke huyo huheshimiwa kwa sababu anajulikana ni mke wa mtu Fulani kwa sababu maisha yao ya uhusiano yanaendelea kwa hiyo endelea kudumu katika uhusiano wako na Mungu na endelea kufanya mambo yote yale yanayodumisha uhusiano wako na Yesu Kristo hivyo tu, kama ulivyo ulinzi wa mke wa mtu, utajilinda kaatika Imani kwa kuendelea kushikamana na Yesu.

 

Kwa kungojea Rehema – Watu waliookoka wengi wetu tuna tabia ya kujihakikishia kuwa tunaingia mbinguni! Sio vibaya kujigamba namna hiyo lakini ni lazima tuwe wanyenyekevu sana tunapaswa kujikumbusha kuwa Yesu atarudi kama hakimu wa mwisho, yeye ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kuamua nani aende mbinguni na nani abaki, Hakuna mtu anaweza kumuamulia, na wale wanaojifikiri kuwa wanastahili wanaweza kujikuta wakikataliwa. Hakuna mwanadamu hata mmoja anaweza kuwa na kigezo za kujifikiri kuwa anafaa kuingia mbinguni, isipokuwa hatuna budi kusubiri au kungojea kwa Rehema kwa kiyunani neno Rehema ni “eleos”  ambalo maana yake ni “compassion” ambalo kwa Kiswahili ni huruma, kwa hiyo wakristo ni lazima tuwe na unyenyekevu kwani mbinguni hatujiingizi tu, wala huwezi kuwa na kipimo sahihi cha kufikiri kuwa wewe ndio utaingia vigezo vyote vya msingi anavyo mwenye harusi, anavyo aliyetoa mwaliko anavyo hakimu mkuu Yesu Kristo, maandiko yanaonya kuwa kuna watu wengi ambao watafanya mambo ya muhimu kwa jina la Yesu na watajifikiria kuwa wana vigezo vya kuingia mbinguni lakini watakataliwa, tuache kiburi bila rehema za Mungu hakuna mtu hata mmoja anayeweza kutoboa na kudhani ya kuwa ataingia mbinguni hata kama utakuwa na bidii, Yesu mwenyewe ndiye anayewajua atakaowakaribisha kwake tuache unafiki, tuache kiburi, tuache kujihesabia haki, tuache kuhukumu wengine kana kwamba sisi tumekwisha kufika, kuingia mbinguni ni kwa kungojea rehema, huyu anayezungumza hapa ni mdogo wake Yesu wamenyonya ziwa moja anasema “HUKU MKINGOJEA REHEMA YA BWANA WETU YESU KRISTO, HATA MPATE UZIMA WA MILELE” kumbe uzima wa milele ni kwa rehema tu na hivyo wakristo wanapaswa kusubiria kwa unyenyekevu  kimsingi neno kungojea kwa rehema katika maandiko ya kiyunani linasomeka hivi “Prosdechomai eleos”  tafasiri yake ni “to intercourse hospitality credence” ambalo tafasiri yake “kusubiria uthibitisho wa kitabibu” yaani wakristo wanapaswa kumsubiria Yesu kama mgonjwa anayesubiri wito wa daktari au kama mgonjwa anayesubiria majibu ya vipimo vya afya yake subira ya namna hiyo hainaga kiburi, ni subira yenye unyenyekevu ndani yake mgonjwa husubiria huruma za daktari akuthibitishie kuwa uko sawa au hauko sawa, sasa kama wewe unajifikiri au unakiburi na unajidhania kuwa wewe hivyo ulivyo Yesu atakuingiza tu mbinguni bila rehema zake subiria kwa kiburi majibu yako yanakuja, sisemi hivi kukutisha bali nataka utambue kuwa sisi wanadamu tulivyo hatupaswi kujivunia wokovu na kujifikiri kuwa tunaweza kusimama kwa nguvu zetu, kama tumeokolewa kwa neema tutaingia mbinguni kwa neema na sio kwa kujigamba. Hivi ndivyo tunavyoonywa hata katika maandiko. 


Muhubiri 7:15 “Mambo hayo yote nimeyaona mimi katika siku za ubatili wangu, yuko mwenye haki apoteaye katika haki yake, yuko na mtu mwovu azidishaye maisha yake katika udhalimu wake. Usiwe na haki kupita kiasi; Wala usijiongezee hekima mno; Kwani kujiangamiza mwenyewe?


Warumi 9:14-16 “Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha! Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.”


Mathayo 7:21-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”


Endapo utaishi katika hayo na kutembea kwa unyenyekevu, na kukaa katika upendo wa Mungu basi kumbuka kuwa Mungu katika rehema zake atatukaribisha kwake na tutakuwa imara katika imani zetu, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kujijenga katika Imani tukingojea rehema za Bwana wetu hata tupate uzima wa milele Amen “ukiyajua hayo heri wewe ukiyatenda” 


Na Rev. Innocent Samuel Kamote 

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima

  

Hakuna maoni: