Luka 7:19-23 “Ndipo Yohana alipowaita
wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule
ajaye, au tumtazamie mwingine? Nao walipofika kwake, walisema, Yohana Mbatizaji
ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Na saa
ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu
wengi aliwakirimia kuona. Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze
Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea,
wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini
wanahubiriwa habari njema. Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
ulimwengu tulio nao wakati mwingine wako watu ambao wangependa kujua uko wapi
na unafanya nini na ni kitu gani kinaendelea katika maisha yako, wakati wote
watu hao watataka kujua unaendeleaje, unafanya nini sasa na mbona siku hizi uko
kimya, wao ni kama hawana kazi nyingine lakini kazi yao ni kufuatilia tu maisha
ya watu na kutaka kujua uko wapi na unafanya nini na nini kinaendelea katika
maisha yako, watu hawa ni kama wasoma nyota tu, wana yao lakini wanataka kujua
habari zako, watataka kujua kama nyumba yako uliyojenga umemuachia nani,
watataka kujua una gari? Watataka kujua una watoto wangapi? Wanataka kujua
mwanao yuko wapi na anasoma shule gani, wanataka kujua hali ya mkeo ikoje,
wanataka kujua hata habari za rafiki zako fulani yuko wapi? Je mmewasiliana?
Yaani wao ni kutaka kufahamu tu kuwa unaendeleaje? Na kupeleleza kila
kinachoendelea katika maisha yako! Sijui kama umewahi kubaini wako watu wa
namna hii!. Leo tutachukua Muda kujifunza namna ya kuwajibu watu hao kutoka kwa
Yesu Kristo mwenyewe, kuna namna Yesu anatufundisha nzuri sana ya kuwajibu
wambeya na wapelelezi wanaotaka kujua maisha yako yanaendeleaje! Katika kifungu
cha maandiko Luka 7:21-23 Yesu
anaufunua moyo wake akionyesha asili yake Yeye ni nani na ametumwa kufanya
nini, “He was a man in mission” Yesu
alikuwa ni mtu wa kazi, kuna shughuli aliyokuwa ameandikiwa kuja kuifanya na
alikuwa akiifanya kwa uaminifu, Maandiko yanaonyesha wazi na mara kadhaa Yesu
aliweka wazi kuwa alikuja kufanya nini “He was an man with his assignment”
alikuwa ni mtu mwenye shughuli zake!
-
Kutangaza
habari njema na kuweka huru walioonewa Luka 4:18-19 “Roho
wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari
njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona
tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”
-
Kutafuta
na kuokoa kile kilichopotea Luka 19:10 “Kwa kuwa
Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”
-
Kuwa
fidia ya wengi kwaajili ya ukombozi wa mwanadamu Marko 10:45 “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali
kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”
-
Kuishuhudia
kweli Yohana 18:37 “Basi Pilato akamwambia, Wewe u
mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi
nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni,
ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.”
-
Kuwafanya
mataifa yote kuwa wanafunzi Mathayo 28:18-20. “Yesu
akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.
Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la
Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru
ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”
Kupitia maandiko hayo tunaweza
kuelewa kuwa Yesu alikuwa anajitambua yeye ni nani, na yuko duniani kwaajili ya
nini na kwa kweli alikuwa akitekeleza lile ambalo kwaajili ya hilo alizaliwa,
unapouliza swali kuhusu maisha ya mtu anayejitambua kama ilivyo kwa Yesu Kristo
basi ni vema utarajie majibu mazuri kama aliyoyapata Yohana Mbatizaji alipotaka
kujua kama Yesu ndiye yule ajae au tumtazamie mwingine? Tutajifunza somo hili Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia kwa
kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
·
Wewe
ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?
·
Nendeni
mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia
Wewe ndiwe yule ajaye au tumtazamie mwingine?
Ni muhimu kufahamu kuwa Yohana
Mbatizaji alikuwa amewekwa kizuizini yaani gerezani tena kwa uonevu tu katika
taabu zake na mashaka yake ya kuwekwa kizuizini huku akiwa na hofu kama haki itatendeka
au la anapatwa na mashaka sio ya kuhusu maisha yake na kufungwa kwake tu bali
hata kuhusu Yesu Kristo kama ni Masihi halisi au la? Yohana ndiye aliyemtangaza Yesu Kristo wazi
na kwa ujasiri kwa jamii na kuielezea jamii ya kuwa Yeye ajaye Nyuma yangu ana
nguvu kuliko mimi naye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.
Mathayo 3:11 “Kweli mimi nawabatiza kwa
maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala
sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na
kwa moto.”
Lakini sasa akiwa gerezani
Yoahana anawatuma wanafunzi wake wakaulize kwa Yesu kama kweli yeye ndiye yule
ajaye au tumtazamie mwingine? Swali hili
linaonyesha mashaka aliyokuwa nayo Yohana na matatizo aliyokuwa nayo kwenye
kichwa chake alipokuwa gerezani, pia swali linaonyesha kuwa Yohana naye hakuwa
ameifahamu vema huduma ya Kimasihi kwa wakati ule Yeye alikuwa akimtarajia
masihi ambaye atakuwa na nguvu kubwa sana za kisiasa na kijamii na kama masihi
ambaye angeleta mapinduzi makubwa ya
kikoloni na kuwaondoa warumi na utawala wao na Israel kupata uhuru wa kweli
kutoka kwa wakoloni hao, kama huduma hii ya kimasihi ingelikuwa ya namna hiyo
hata Yeye Yohana mbatizaji angeliweza kuwekwa huru kutoka katika magereza
iliyokuwa ikimkabili na mauti penginepo iliyokuwa ikimnyemelea. Yohana alikuwa
ameingia shaka kama kweli unabii uliosemwa katika maandiko kumuhusu Masihi
ulikuwa ndio huu, kwa maana nyingine alikuwa na mashaka na huduma aliyokuwa
akiifanya Yesu Kristo kama ilikuwa huduma sahihi au la? Yeye alikuwa anaona mbona
huyu jamaa yuko kimya niko gerezani mbona hafanyi kitu anachopaswa
kukifanya? Kwa hiyo alipata mashaka
kuhusu utendaji wa kimasihi!
Luka 7:21-20 “Ndipo Yohana alipowaita
wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule
ajaye, au tumtazamie mwingine? Nao walipofika kwake, walisema, Yohana Mbatizaji
ametutuma kwako, akisema, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?”
Swali hili lenye utata linajibiwa
na jibu lenye utata la Yesu Kristo ambalo kimsingi lina mambo ya kutufunza leo.
Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia
Jibu la Yesu Kristo kwa wanafunzi
wa Yohana na Yohana mwenyewe halikuwa la moja kwa moja Ndio au hapana na badala ayake kwanza walimkuta akiendelea
na kazi ambayo kazi yenyewe ilikuwa ndio ushahidi wa nini Yesu amekuja kukifanya,
Yesu kabla ya kujibu swali hilo kwanza alikuwa “busy” BIZE akishughulika na
kuhubiri injili, kufundisha lakini kama haitoshi
-
Aliwafungua vipofu na wengi wakafunguliwa na
kuona hapo hapo
-
Aliwafungua wenye ulemavu na wengi walitembea
hapo hapo
-
Alitakasa wenye ukoma na wengi walitakasika hapo
hapo
-
Aliwafungua waliokuwa viziwi na wengi walipata
kusikia hapo hapo
-
Alifufua wafu na wengi walioonekana na Misiba ilikomeshwa, pepo walikemewa na
kutoka na wagonjwa wengi sana walipokea
uponyaji wao
-
Alihubiria masikini habari njema na wengi
waliipokea injili
Baada ya kazi hii kubwa
aliyoifanya Yesu na wanafuzi wa Yohana Mbatizaji waliishuhudia, kwa macho yao
yeye mwenyewe ndipo akajibu kwa kuwaambia Nendeni mkamweleze Yohana hayo
mliyoyaona na kuyasikia.
Luka 7:21-23 “Na saa ile ile aliwaponya
wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia
kuona. Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona
na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma
wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari
njema. Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami.”
Swali kubwa la kujiuliza hapa ni
kwa nini Yesu alijibu swali la Yohana mbatizaji katika njia aliyoitumia? Na ya wazi?
1.
Wajibu
watu kivitendo – Siku zote watu wanapoingia mashaka na wewe hupaswi kwa
namna yoyote ile kujitetea lakini matendo yako na misheni yako uliyopewa na
Mungu itajibu kivitendo kwamba wewe ni mtu wa namna gani, Huduma ya kimasihi
ilikuwa imefunikwa na utendaji mkubwa wa kimiujiza na uwezo wake wa kuwahurumia
watu na kuwafungua kutoka katika vifungo vyao na mateso yao na misiba yao,
kimsingi Yesu alikuwa akiutimiza unabii kwa huduma yake vile vile kama manabii
walivyokuwa wametabiri na kupitia kazi alizikuwa akizifanya ilikuwa ni
udhihirisho wa wazi kuwa alikuwa ni mtu na shughuli zake.
Isaya 61:1-2 “Roho
ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri
wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo,
kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.
Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu;
kuwafariji wote waliao;”
Yohana 5:36 “Lakini
ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohana; kwa kuwa zile kazi
alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya
kwamba Baba amenituma.”
Yohana 10:37-38 “Kama
sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini
mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu,
nami ni ndani ya Baba.”
Yesu
anatufundisha kuwa ni kwa kufanya kazi na kwa kuonyesha kazi zetu tuzifanyazo
tutathibitika kwamba tunayatimiza mapenzi ya Mungu, kama mtu ana mashaka na
wewe mjibu kwa kazi za Mungu unazozifanya, namna njema ya kuondoa mashaka
katika huduma zetu ni kuonyesha kazi, wewe fanya kazi, ooo huyu vilienda
vikarudi waambie nionyeshe kazi, kazi zetu zinatushuhudia kama sisi ni wa Mungu
au la, wako watu ni hodari sana wa kuchafua wengine na ni kama wameumbwa wawe
wataalamu wa kuharibia wengine maisha lakini waambie waonyeshe kazi zao ni kazi
gani wanamfanyia Mungu? Wewe uchukiaye sanamu wateka mahekalu? Mungu
hataangalia uso wa mwanadamu Mungu ataangalia kazi tutapimwa na kuthibitika kwa
kazi, shuhuda zetu hazitegemei wanadamu zinategemea kazi, kazi itakusemea wewe
ni nani, kwa hiyo watu wanapokufuata fuata waonyeshe kazi, Yesu alionyesha kazi
ili kuondoa mashaka ya Yohana mbatizaji, Mbinguni tutapimwa kwa kazi fanya kazi
acha kupiga domo kazi, ee huyu sijui ilikuwa hivi ikawa vile acha upuuzi
onyesha kazi, Kazi ambazo wanafunzi wa Yohana waliziona yalikuwa ni majibu
tosha Yesu ni nani!
1Wakorintho 3:13-15 “Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika
moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi
ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea,
atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.”
Uthibitisho wetu
kuwa tumeitwa na Mungu tunatembea na Mungu na tunamtumikia Mungu ni kazi, ile
neema ya Mungu iliyoko juu yetu inatenda kazi na inatufanya tufanye kazi zaidi
ikiwezekana kuliko wote, watu watajaribu sana kukufanya ukose sifa kwa
kukukosoa na kukuchukia na kukuuatilia Lakini ifikie wakati kila mtu aonyesha
kazi, kwamba unachangia nini katika mwili wa Kristo kwa sababu kazi zetu
zitapimwa, watu wengi walikuwa wakimkosoa Paulo mtume na kumuweka katika
viwango vya chini na kumuona kama mtume asiye sahihi Lakini Kazi alizofanya
ndio zinajibu kuwa yeye alikuwa ni Mtume wa namna gani? Watu wanaokufuata fiata
waambie waangalie kazi
1Wakorintho 15:9-10 “Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa
mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu
nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali
nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya
Mungu pamoja nami.”
2.
Mtu
asikutaabishe – Wako watu ambao ukiwa kazini wanadhani hujui unalolifanya
kwa hiyo wanataka wakutaabishe, Maswali ya Yohana mbatizaji hayakumtoa Yesu Nje
ya Mstari, badala yake aliendelea kuifanya kazi, kutokujibu swali la wanafuzi
wa Yohana mbatizaji kwa haraka na kuanza kupiga kazi kwanza kulikuwa
kunamaanisha kuwa usikubali kutaabishwa fanya kazi ile uliyoitiwa wako watu
wataabishaji sana hapa duniani hawataki ufanye kile Mungu amekuitia au watataka
kukubabaisha ili uondoke katika lile uliloitiwa uanze kujibizana nao, achana na
magazeti ya udaku, achana na vyombo vya habari acha kujibizana na watu kwenye
mitandao ya kijamii, wewe weka uso wako katika kazi, mtu anayeondoa uso wake
katika kazi hafai katika ufalme wa Mungu wewe piga kazi usipoteze mwelekeo hata
kidogo, Yesu alipiga kazi, kazi zitajibu
Luka 9:59-62 “Akamwambia
mwingine, Nifuate. Akasema, Bwana, nipe ruhusa kwanza niende nikamzike baba
yangu. Akamwambia Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda ukautangaze
ufalme wa Mungu. Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe
ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia
mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.”
Wagalatia 6:17 “Tangu
sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu.”
Luka 13:31-32 “Saa
ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende
mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni,
mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa,
siku ya tatu nakamilika.”
Mtu anayejua
kusudi la Mungu, na kusudi la kuwepo kwake “a man with a mission” hawezi kutikiswa na kuacha kufanya lile
aliloitiwa, Kristo Yesu kwa majibu yake kivitendo alikuwa anatukumbusha kuwa na
msimamo katika shughuli zetu na wajibu wetu na yale mambo ambayo Mungu
ametuitia acha kusikiliza mambo ya pembeni, pembeni wewe angalia yale ambayo ni
mapenzi ya Mungu na ile kazi ambayo Mungu amekuitia kuifanya chukua chapa za
Kristo, fanya kazi mtu asikutishe! Wala asikutoe nje ya mstari.
3.
Heri
mtu yule asiye na mashaka nami - Naye
heri mtu ye yote asiyechukizwa nami, Yesu alikuwa anahitimisha jibu lake kwa
kutaka kumtoa shaka Yohana mbatizaji
kwamba asiye na mashaka naye wala asichukizwe naye, utendaji wake na
utoaji huduma zake ulikuwa sawasawa na mapenzi ya Mungu, lakini wakati mwingine
haungeweza kuwafurahisha wanadamu, kwa hiyo ingekuwa heri kama wangelikuwa na
Imani naye, unapofanya lile ambalo Mungu amekuitia wakati mwingine ni vigumu
kueleweka kwa ndugu zetu, jamaa zetu na hata marafiki zetu, kuna namna na jinsi
ambavyo watu wanatarajia uwe na utrende katika njia wanazozifikiria wao lakini
utendaji wa Mungu na mapenzi yake wakati mwingine unaweza usieleweke kwa
wanadamu na ukawakwaza Yesu aliwekwa kwaajili ya kuinuka na kuanguka wengi
katika Israel
Luka 2:25-34 “Na
tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye
haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu
yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya
kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi
walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria,
yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa,
Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu
yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa
mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye
walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki,
akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka
wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.”
Huduma ya
kimasihi ni yenye utata na yenye kufikirisha, na kuwakwaza wengi, utendaji wake
na mafundisho yake yangeweza kusababisha mgawanyiko mkubwa na upinzani mkubwa
utakaongoza wengi kujikwaa na wengi kuinuliwa katika Imani, Simeoni alimaanisha
Yesu angekuwa na huduma yenye utata na
hivyo kuwa ishara itakayonenwa, Matarajio yake Yohana mbatizaji kuhusu huduma
ya kimasihi kwake yangeweza kuwa kwazo kama bado angekuwa haelewi maandiko,
ilikuwa ni lazima huduma ya kimasihi ilete utata miongoni mwa jamii lakini ana
heri mtu yule ambaye angeamini ambaye hangekuwa na mashaka naye ambaye
hatakwazwa na yeye, kukwazwa na huduma ya kimasihi ilikuwa ni jambo la kawaida
na lilikuwa limetabiriwa na Isaya na pia Mzee Simeoni
Isaya 8:14-15 “Naye
atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa
kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu.
Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa.”
Yesu alitaka
kumsaidia Yohana Mbatizaji asiwe na mashaka naye aendelee kumuamini, hata kama Yesu
hatamtoa gerezani lakini hapaswi kuchanganyikiwa kuhusu Yesu, Yesu hakutaka
Yohana awe miongoni mwa wale wengi wataakaojikwaa juu yake, lakini alitaka
kumpa jibu thabiti kwamba awe na imani njia za Mungu za kiutendaji ziko juu
sana kuliko tunavyofikiri, usikwazike ukiona katika maisha yako ni kama Yesu
hashughuliki na wewe usimlaumu wala usiwe na mashaka naye endele kupiga kazi,
utendaji wa Mungu ni utendaji wa kipekee na wa ajabu na njia zake ziko tofauti
na matarajio yetu na utendaji wake.
Hitimisho:
Njia za Mungu za kiutendaji sio
njia zetu, utendaji wa Mungu unazidi utendaji wa fikra ya kawaida ya
kibinadamu, ni lazima tuwe tayari kufuata njia na mapenzi ya Mungu, wale watu
wanaotaka kujua kuwa tuko wapi tunafanya nini, tunaendeleaje, familia zetu
zikoje tuna watoto wangapi, tumejenga au la, tuna mashamba au la, tuna magari
au la! tuko wapi tuna ishu gani au la, tunamiliki fedha au la watu wanaofuatilia
maisha yako waambie Kazi za Mungu zinaendelea, waambie unachukua chapa za
Kristo waambie wasiwe na mashaka na wewe!, kuna wale waliokukwamisha pia
watatamani kujua uko wapi sasa na unaendeleaje, kuna wale waliokufukuza kazi,
kuna wale waliokuwekea fitina wakadhani ya kuwa utakwama, waambie waendelee
kutufuatilia katika mitandao ya kijamii wapitie kurasa zetu facebook na kwenye
blogu zetu waambie ya kuwa neno la Mungu linaendelea, waambie tunaendelea
kuihubiri injili vile vile na hatujawahi kukaa kimya, waambie tunaendelea
kufanya wanafunzi waambie kazi za Mungu zinaendelea kamakawaida, waambie watu
wanaokoka, waambie tunaendelea na wokobvu na wala hatuna mpango wa kurudi
nyuma, waambie kazi zinaendelea na
hakuna wa kutuzuia, pepo wanatoka, habari njema inahubiriwa, wafungwa
wanafunguliwa na vipofu wanapewa kuona, Nyaraka zinaandikwa na maisha
yanaendelea heri yake mtu yule asiye na
mashaka nami!, Heri yake mtu yule asioyechukizwa nami!
Rev. Innocent Samuel Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.
Maoni 1 :
Ahsante mchungaji
Chapisha Maoni