2Timotheo 2:8-9 “Mkumbuke
Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili
yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno
la Mungu halifungwi. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya
wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na
utukufu wa milele.”
Utangulizi
Kauli
ya kuwa Neno la Mungu halifungwi, ilitamkwa na Mtume Paulo ambaye wakati huu
alikuwa kifungoni, Paulo alifungwa na kupitia mateso kwa sababu alikuwa
akiihubiri injili na kufundisha watu Neno la Mungu ambalo alikuwa na Imani
kwamba litawafungua watu kutoka dhambini na kuwaelimisha, Hata hivyo kutokana
na njama za shetani Paulo mtume mara kadhaa aliwekwa kizuizini na kufungwa
gerezani shetani akifikiri ya kuwa kwa kufanya hayo ataweza kuzia kasi ya
injili na utendaji wa Roho Mtakatifu katika maisha ya muhubiri huyu Mashuhuri
wa karne ya Kwanza, Hata hivyo Paulo Mtume alikuwa na ujuzi na uzoefu ya kuwa Neno la Mungu halifungwi!, vizuizi
kwa Paulo mtume kamwe havikuweza kudhoofisha Nguvu ya injili, kwani wakati
mwingine aliweza kuhubiri akiwa kifungoni na kuwafikia wengi huko na zaidi ya
yote alipata nafasi ya kuandika mafundisho ambayo kimsingi yaliweza kuinua kwa
kiasi kikubwa maisha ya waamumini wa makanisa wa nyakati za kanisa la Kwanza
hata leo, kwa hiyo tunajifunza ya kuwa licha ya mateso, vikwazo na vifungo
mbali mbali ambavyo tunakutana navyo kwaajili ya injili kumbe Neno la Mungu
halifungwi!
2Timotheo 2:9 “Nami
katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu
halifungwi.”
Kwa
Msingi huo leo tutachukua Muda kujifunza kwa undani usemi wa Paulo kuwa neno la
Mungu Halifungwi kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Injili ina
nguvu kuliko vifungo vya gerezani
·
Mifano ya
watu waliofungwa kwaajili ya injili
·
Neno la
Mungu halifungwi!
Injili ina nguvu kuliko vifungo vya
gerezani
Wote
tunafahamu kuwa habari njema za Yesu Kristo zina nguvu kubwa sana ya kuwafungua
watu na kuwaweka huru kutoka katika vifungo mbalimbali vya shetani pamoja na
utumwa wa dhambi, ni ukweli usiopingika kuwa injili ni uweza wa Mungu uletao
wokovu, kwa kila aaminiye bila kujali anatokea katika utamaduni wa aina gani,
wala bila kujali hekima au elimu aliyonayo mtu.
Warumi 1:14-16 “Nawiwa
na Wayunani na wasio Wayunani, nawiwa na wenye hekima na wasio na hekima. Kwa
hiyo, kwa upande wangu, mimi ni tayari kuihubiri Injili hata na kwenu ninyi
mnaokaa Rumi. Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu
uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.”
Kwa
utambuzi na uzoefu wa namna Paulo alivyoona injili ikiwasaidia wengi na
kuwafungua kutoka katika vifungo vya giza na dhambi, Paulo aliendelea kushikwa
na shauku ya kuihubiri injili kila mahali na kila wakati, hata hivyo katika
namna ya kushangaza sana Paulo mtume mara kadhaa alikamatwa na kutiwa gerezani,
kama muhalifu/au mtenda mabaya kwa sababu ya injili aliyokuwa anaihubiri, Paulo
alitamani sana kuwa huru ili aweze kuieneza injili, Lakini Ibilisi alikusudia
kumzuia na sio tu kuwa aliwekwa gerezani lakini pia alilindwa na askari na
kufungwa kwa minyororo kama moja ya wahalifu hatari sana, kwa hiyo mara
nyingine aliwaandikia makanisa mbalimbali wamuombee, ili afunguliwe kinywa na
kuihubiri injili kwa ujasiri mkubwa, Lakini hata hivyo alikuwa amefungwa
Waefeso 6:18-20 “kwa
sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na
kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe
usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili;
ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri
katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena.”
Katika
hali ngumu kama hiyo, akiwa gerezani, na katika vifungo na chini ya mikatale
akiwa mfungwa au mjumbe wa minyororo bado anawaomba kanisa kumuombea ili apewe
ujasiri aendelee kulisema neno la Mungu, Paulo alifanya hivyo akiihubiri injili
kwa wafalme, wafungwa na wakuu wa magereza ambao kimsingi walifunguliwa na
walipata neema ya kusikia habari njema licha ya kuwa Mtumishi wa Mungu alikuwa
katika minyororo, aliendelea kuhubiri kwa ujasiri mahakamani, kwa mahakimu na
wasikilizaji lakini pia aliendelea kuandika nyaraka mbali mbali ambazo zilikuwa
na mafundisho mazuri na ya msingi akiyatia moyo na kuwajenga wale aliokuwa
amewahubiri injili pamoja na mwili wa Kristo kokote uliko ulimwenguni.
Matendo 26:27-29 “Mfalme
Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini. Agripa akamwambia
Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo. Paulo akamjibu,
Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na
hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa vifungo hivi.”
Vifungo
havikumzuia Paulo Mtume kuihubiri injili, alihubiri kwa ujasiri wote, alihubiri
wafalme mahakamani na wasikilizaji wa kesi wote akiendelea kuwashawishi waijuie
injili na kumuamini Mwana wa Mungu, Paulo hakujali injili inahubiriwa wapi,
alikuwa gerezani lakini alitamani watu wote wabadilike wawe kama yeye isipokuwa
vifungo vyake tu, kwa maneno yake na matendo yake inatufundisha kuwa injili ina
nguvu kuliko magereza, magereza ilikuwa shimoni, mwanga ukiwa hafifu sana
lakini Moyo wa Paulo uliendelea kumuwaka akiwa na shauku ya kuisema injili,
kufungwa kwake kulitumiwa na maadui kama njia ya kuhubiri kwa fitina injili
isiyofaa lakini kulitumiwa na watu wazuri kuwapa ujasiri wa kuisema injili kwa
nguvu kubwa huku yeye akiendelea kuandika nyaraka za kuwatia moyo makanisa
mbalimbali na mwili wa Kristo.
Wafilipi 1:12-13 “Lakini,
ndugu zangu, nataka mjue ya kuwa mambo yote yaliyonipata yametokea zaidi kwa
kuieneza Injili; hata vifungo vyangu vimekuwa dhahiri katika Kristo, miongoni
mwa askari, na kwa wengine wote pia. Na wengi wa hao ndugu walio katika Bwana,
hali wakapata kuthibitika kwa ajili ya kufungwa kwangu, wamezidi sana kuthubutu
kunena neno la Mungu pasipo hofu.”
Neno
la Mungu limedhihirika kuwa na nguvu sana kuliko mipaka ya kibinadamu na
utendaji wa shetani, Injili ina nguvu kuliko vifungo vya gerezani, ina nguvu
kuliko vizuizi vya shetani, ina nguvu kuliko vifungo vya kidini, ina nguvu
kuliko wivu wa wanadamu na husuda zao, injili haiwezi kuzuiwa na mtu yeyote,
wala haiwezi kuziwa na vita vya kijinga vya maadui wa injili, Injili itaendelea
kuhubiriwa hata kwa kalamu, itapelekwa kwa mitandao ya kijamii, itapenya kwa
sauti za Redio na televisheni, hakuna dhehebu, wala dini, wala taifa, wala
ufalme, wala bara, wala kisiwa ambacho kitaweza kuizuia injili, nguvu za giza
haziwezi, mapepo na majini hayawezi, mila na desturi haziwezi injili ina nguvu
kuliko maregeza yoyote ile, inaweza kupenya kwa askari, inaweza kupenya kwa
daktari, inaweza kupenya kwa mkulima, inaweza kuwafikiwa wachimba madini,
inaweza kuwafikia wanasiasa, inaweza kumfikia yeyote yule kwa njia yeyeote ile,
Paulo alitumia mateso yake na vifungo vyake kumkumbusha Timotheo na kumtia moyo
kwamba asiogope kwani Yesu aliteseka pia kwaajili ya injili, lakini alifufuka,
hakuna mateso yanayoweza kuizuia injili, wala hila, wala vifungo neno la Mungu
litaendelea mbele, wapinzani watakufa lakini neno la Mungu halifi, hivyo kila Muhubiri
wa injili hapaswi kuogopa kuisema kweli ya Mungu kwa sababu watu wa Mungu
watafunguliwa kwa injili ya kweli na sio injili ya hila na uongo hubiri kweli
saidia watu kuwa huru na unaweza kwa injili.
Mifano ya watu waliofungwa kwaajili ya
injili
Ni
muhimu kufahamu kuwa tunapaswa kuihubiri injili katika mazingira yoyote yale
yawe magumu yawe laini, bila kujali kwamba kuna vikwazo vya aina gani, kumbuka
kuwa kwa kadiri siku zinavyokwenda mbele upinzani wa kiinjili unaendelea
kuchukua sura mpya, shetani sasa anaweza kuwatumia viongozi wa kidini na kidhehebu
kuhakikisha kuwa wanakuziba kinywa ili usihubiri injili, kumbuka tu kuwa
watakatifu waliotutangulia wote waliopewa maagizo ya neno la Mungu walipitishwa
katika nyakati ngumu na kufungwa na kuzibwa vinywa vyao kwaajili ya injili hata
hivyo bado tunaonyeshwa ya kuwa neno lilisimama na wale waliokuwa huru
waliisema injili kila mahali.
1.
Paulo
na Sila walipokuwa wakiihubiri injili ambayo ilifungua watu na zaidi sana
mwanamke mwenye pepo wa uaguzi, mji ulitaharuki, wakafanyiwa ghasia,
wakapelekwa mahakamani, wakisingiziwa kesi ya kuchafua mji, wakavuliwa nguo,
wakapigwa kwa bakora, wakatupwa gerezani wakafungwa miguu yao kwa mikatale
wakiwa wamepokea mapigo mengi, hawakuweza kutulia walipokuwa ndani gerezani
wakifungwa kama wahalifu hawakukata tamaa, wala hawakunyamaza, waliendelea
kuisema injili walimwimbia Mungu na kuomba usiku kucha, Na Mungu akatuma
tetemeko kubwa gereza na vifungo vyote vya watu wote vikaaachia na hatimaye
mkuu wa gereza na nyumba yake wakaokoka, shetani kwa ujinga wake alifikiri kwa
kumuweka Paulo na sila kizuizini ataizuia injili na badala yake injili
iliwafikiwa wafungwa wote na mkuu wa gereza na familia yake wote waliokoka na
kubatizwa
Matendo 16:19-34 “Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao
limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya
wakuu wa mji; wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji
wetu, nao ni Wayahudi; tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali
kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi. Makutano wote wakaondoka
wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa
bakora. Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru
mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika
chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane
Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na
wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi,
hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo
vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa
milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa
wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema,
Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani,
akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema,
Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana
Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na
watu wote waliomo nyumbani mwake. Akawakaribisha saa ile ile ya usiku,
akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo.
Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na
nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu.”
2.
Petro
na Yohana - Waliwekwa gerezani na
wakuu wa makuhani na masadukayo kwaajili ya wivu walipokuwa wakiihubiri injili
na kuijaza Yerusalemu mafundisho yao, wakuu wa makuhani na wazee wa dini
waliwakataza wasihubiri kwa jina la Yesu wala nguvu zake za ufufuo na kuamua
kuwaweka gerezani, lakini malaika wa Bwana alikuja kwa muujiza na kuwafungua na
kuwaagiza tena wakaseme habari njema na kuendelea kuwafundisha watu
Matendo 4:1-20 “Hata walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida
wa hekalu na Masadukayo wakawatokea, wakifadhaika sana kwa sababu
wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu. Wakawakamata,
wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni. Lakini wengi
katika hao waliosikia lile neno waliamini; na hesabu ya watu waume ikawa kama
elfu tano. Hata asubuhi wakubwa na wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu,
na Anasi Kuhani Mkuu, na Kayafa pia, na Yohana na Iskanda, na wote wale
waliokuwa jamaa zake Kuhani Mkuu. Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu
gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya? Ndipo Petro, akijaa Roho
Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama
tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi
alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la
Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika
wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe
lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni.
Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine
chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. Basi walipoona
ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na
maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu. Na
wakimwona yule aliyeponywa akisimama pamoja nao hawakuwa na neno la kujibu.
Wakawaamuru kutoka katika baraza, wakafanya shauri wao kwa wao, wakisema,
Tuwafanyie nini watu hawa? Maana ni dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya
kwamba ishara mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana. Lakini neno hili
lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa
jina hili. Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la
Yesu. Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu
kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi
kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.”
Matendo 5:18-25 “wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza; lakini
malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni
mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu. Nao waliposikia
wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha. Akaja Kuhani Mkuu nao
waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa
Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete. Hata watumishi walipofika
hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa habari, wakisema, Gereza tumeikuta
imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua
hatukukuta mtu ndani. Basi jemadari wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia
haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo. Mtu mmoja akaja
akawapasha habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya
hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu.”
3.
Yeremia
nabii alifungwa lakini neno la Mungu lilienea - Historia na tabia ya Mungu
inaonyesha ya kuwa neno lake halijawahi kufungwa wala kuwekwa kizuizini,
shetani anaweza kutumia hila kuwatesa na kuwaweka kizuizini watumishi wa Mungu
lakini Historia inamuhukumu kuwa hajawahi weza kushidana na Roho wa Mungu na
Hekima aliyo nayo Mungu katika kuyahifadhi mapenzi yake, Yeremia yeye alitiwa
Gerezani kwa sababu ya kuwaonya watu kuhusu kuharibiwa kwa Yerusalem na hekalu
pia, lakini pamoja na kufungwa aliendelea kupenyeza ujumbe wa Mungu kwa mfalme
na unabii wa ujumbe wa Mungu kwa watu wake uliendelea
Yeremia 37:15-17 “Nao wakuu wakamkasirikia Yeremia, wakampiga, wakamtia
gerezani katika nyumba ya Yonathani, mwandishi; kwa maana ndiyo waliyoifanya
kuwa gereza. Basi, Yeremia alipokuwa ameingia katika nyumba ya shimo, na katika
vyumba vya ndani; na Yeremia alipokuwa amekaa humo siku nyingi; ndipo Sedekia,
mfalme, akatuma watu wamlete; naye mfalme akamwuliza kwa siri ndani ya nyumba
yake, akasema, Je! Liko neno lililotoka kwa Bwana? Yeremia akasema, Liko.
Akasema pia, Utatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli.”
4.
Yesu
Kristo aliuawa kwaajili ya injili – Wakuu wa dini na makuhani walipanga
njama za kummaliza Yesu, walifikiri kwa ufupi ya kuwa wakimmaliza basi watakuwa
wameondoa ujumbe wake na kupunguza kadhia ya kusikia Yesu akiwa maarufu siku
hadi siku, walimsingizia mengi, walimtesa, aliteswa sana alipigwa mijeledi
mikali, walimdhihaki na kumsulubisha msalabani, hawakujua ya kuwa huo ndio
ulikuwa mwanzo wa mapinduzi makubwa ya kiinjili, Mwanaume huyu mmbora alifufuka
siku ya tatu na habari zake zilihubiriwa mpaka leo na yeye ameamuru habari hizi
na mafundisho yake yahubiriwe na kufundishwa kwa wanafunzi wa mataifa yote
1Wakorintho 2:6-8. “Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si
hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika; bali
twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu
aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu; ambayo wenye kuitawala dunia hii
hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa
utukufu;”
Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa
mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa
wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na
kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja
nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”
Yohana 12:24 “Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika
nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.”
Kifo cha Yesu Kristo cha mateso, kileleta ukombozi mkubwa sana
kwa wanadamu na kusababisha neno la Mungu kuenea kwa kasi kubwa duniani,
tunajifunza hapa kuwa neno la Mungu sio tu kuwa halifungwi lakini halizikwi, ni
kukosa hekima na ni ujinga mkubwa kujaribu kuizuia injili kwa sababu zozote
zile, kila wakati shetani anapojaribu kuleta vikwazo kuizuia injili anakuwa
kama mtu anayechochea moto na kusababisha chakula kiive haraka, upinzani mkubwa
ulisababisha kazi kubwa na ueneaji mkubwa wa injili, Ndugu haijalishi
wanaoizuia injili ni makuhani, au wakuuwa dini au mafarisayo au masadukayo au
wanasiasa vyovyote iwavyo Neno la Mungu litaendelea na hakuna mwanadamu anayeweza kizuia injili. Mtu
akiifunga injili malaika wa Bwana watakunong’oneza kwa kukuambia Enendeni
mkasimame mkawaambie watu maneno yote ya uzima huu!
Matendo 5: 18-21b “wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya
gereza; lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa,
akasema, Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu. Nao
waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha
Neno la Mungu halifungwi!
Tumeona
na sasa unaweza kukubaliana na ukweli wa maneno ya Paulo mtume ya kuwa neno la
Mungu halifungwi, Katika historia nzima ya dunia tumeona shetani akiwatumia
watu na wafalme na mataifa mbalimbali kuzizuia habari za Yesu, lakini pia
madhehebu na viongozi wa dini wakiwa sababu ya kuizuia injili lakini daima
shetani na maajenti wake wote wamethibitisha kufeli, usikubali kupoa, usikubali
moto wa injili uzimike katika maisha yako, ni lazima tuhakikishe ya kuwa tunakirithisha
kijiti hiki au mwenge huu au nuru hii kwa kizazi kingine waipeleke injili bila
kujali vikwazo wanavyokutana navyo, Mateso, upinzani na vifungo kamwe
havijawahi kuwa sababu ya kuizuia injili na badala yake kama upinzani wa upepo
kwa ndege inayotaka kupaa ndio ulivyo upinzani wa injili husababisha moto uwake
na kukolea zaidi.
2Timotheo 2:8-9 “Mkumbuke
Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili
yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno
la Mungu halifungwi. Kwa ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya
wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na
utukufu wa milele.”
Tunao
ushuhuda ya kuwa mataifa mengi, wafalme wengi na wenye mamlaka wengi wamejaribu
kuipinga injili lakini injili imeenea kila mahali ulimwenguni, yako maeneo
ambayo Biblia imepigwa marufuku lakini uthibitisho tulio nao leo duniani ni
kuwa bado ndicho kitabu kinachoongozwa kwa kusomwa zaidi duniani, Yako makanisa
yamefungwa na wako wakristo ambao wako katika mateso ya aina mbalimbali, lakini
hayo hajayasaidia kuifanya injili isisonge mbele, wewe nawe mtu wa Mungu
unaweza kuwa unapitia vikwazo vya namna mbalimbali, wakuu wa dini
wanakukandamizia, hawataki uibuke, wanataka upotee kwa sababu una mafundisho
sahihi, una injili iliyo sahihi wewe bado ni wa moto nataka kukutia moyo ya
kuwa unayoyapitia hayawezi kukufanya unyamaze neno la Mungu litaendelea kila kitu duniani kitapia lakini maneno ya
Mungu hayatapita kamwe, Kama makusudi ya Mungu hayawezi kuzuilika kumbuka ya
kuwa kusudi kubwa la Mungu ni injili hakuna mtu anayeweza kuizuia injili
lihubiri neno bila kujali wakati unaofaa na wakati usiofaa hubiri neno!
Isaya 40:7-8 “Majani
yakauka, ua lanyauka; Kwa sababu pumzi ya Bwana yapita juu yake. Yakini watu
hawa ni majani. Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu litasimama
milele.”
Hitimisho;
Neno la Mungu halifungwi, Paulo mtume alikuwa na ufahamu huo ya kwamba hata
ingawa yeye yuko kifungoni, hekima ya shetani imeshindwa kwa hekima ya Mungu,
shetani hakuweza kuzuia kabisa ujumbe wa kitume usiwafikie watu, watu
hawakuweza kuisikia sauti yake lakini mafundisho yenye uzima yaliwafikiwa watu
kupitia nyaraka zake, hakuna mwanadamu anayeweza kulifunga neno la Mungu na
kufanya hivyo ni upuuzi na hekina ya kibinadamu na ya shetani, Shetani hawezi
kuzuia mpango wa Mungu, kila wakati mipango ya giza imehibitisha kufeli vibaya,
mateso na vifungo havujawahi kuwa mwisho wa kazi ya Mungu, badala yake imekuwa
njia ya kuonyesha utukufu wake na nguvu, injili itaendelea kuhubiriwa na kufundishwa
pasipo hofu hata kama tutakutana na vikwazo, Mungu atafanya kila njia ili
kwamba neno lake lizidi kukua na kuenea
Je umekuwa unakabiliwa na hofu kama Timotheo kwaajili ya vikwazo? Usiogope neno
la Mungu halifungwi!
Marko 13:31 “Mbingu na nchi zitapita;
lakini maneno yangu hayatapita kamwe.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni