Jumapili, 27 Aprili 2025

Kwa maana wamekufa waliokuwa wakiitafuta roho ya mtoto!


Mathayo 2:19-21 “Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli.”



Utangulizi:

Malaika wa Bwana alimwambia Yusufu maneno haya alipokuwa akali akiishi Misri, mahali alikokuwa ameelekezwa kwaajili ya kwenda kumficha mtoto Yesu baada ya kutafutwa kuuawa na Mfalme Herode mkuu, kwa hofu ya kutokutaka kuwepo kwa mfalme mpya wa Wayahudi, tabia ya Herode ilikuwa ni matokeo ya wivu wake na mpango wa kishetani wa kutaka kuharibu mpango na mapenzi ya Mungu kwaajili ya ukombozi wa mwanadamu kwa kutaka kumuua Yesu. Somo hili ni maonyo kwa watu wote wasio na mapenzi mema kwa kazi na mpango wowote wa Mungu, Mungu yuko tayari kuulinda mpango wake na makusudi yake kwa gharama yoyote ile, na hakuna mtu awaye yote anayeweza kuwa bora kuliko mpango na makusudi ya Mungu!

Mathayo 2:13 – 14 “Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri;”

Herode ambaye alitafuta kumuangamiza Yesu alikuwa amekwishakufa, Yesu alipaswa kukulia Nazareth katika inchi ya Israel inchi ya utumishi wake na aliyekuwa kipingamizi cha mpango huo alikuwa ameondolewa na Bwana mwenyewe hivyo Kristo angetekeleza mapenzi ya Mungu bila kizuizi, katika inchi ya Israel kwa sababu hiyo sasa malaika wa Bwana anatoa wito wa wao kurejea huku akiweka bayana sababu za kurejea ni kuwa wamekufa waliokuwa wakiitafuta roho ya mtoto!

Mathayo 2:22-23 “Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya, akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazorayo.”

Tutajifunza somo hili “Kwa maana wamekufa waliokuwa wakiitafuta roho ya mtoto” kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-

 

·         Hatari ya kuzuia mpango wa Mungu.

·         Kwa maana wamekufa waliokuwa wakiitafuta roho ya Mtoto.

 

Hatari ya kuzuia mpango wa Mungu

Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna jambo baya na la hatari sana duniani kama kujaribu kuzuia mapenzi ya Mungu au Mpango wa Mungu, mtu awaye yote wa mamlaka ya aina yoyote ile ambaye atasimama kuzuia kusudi la Mungu au kujaribu kusimamisha mpango wa Mungu juu ya kile alichokikusudia Mungu anajiweka katika hatari isiyoweza kusimulika, kuzuia makusudi ya Mungu wakati wowote na kwa sababu zozote zile ni kuingia katika mfumo wa Mungu. Mfalme Herode mkuu kwa ujumla hakufurahia taarifa za kuzaliwa kwa Masihi ambaye kimsingi ni mfalme wa wayahudi, na badala yake alianza mipango mikakati ya kutaka kumuua Yesu na kuharibu mpango wa Mungu wa ukombozi kwa mwanadamu, Kiburi cha kibinadamu na ulevi wa madaraka ulimfanya mfalme huyu mjinga kujifikiri ya kuwa yeye ni Muhimu kuliko mpango wa Mungu, na kwa akili zake ndogo alifanikiwa kusababisha misiba kwa wamama wa Bethelehemu waliokuwa na watoto wadogo chini ya miaka miwili.

Mathayo 2:3-8 “Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi? Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii, Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli. Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota. Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.”

Mathayo 2:16-18 “Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Sauti ilisikiwa Rama, Kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako.”

Mipango ya Herode na mikakati yake na kughadhibika kwake kunaonyesha Dhahiri nia ya moyo wake ilikuwa ni kuuufutilia mbali kabisa mpango wa Mungu, ni ujinga ulio wazi kuwa Herode aliweza hata kuita wakuu wa makuhani na kuuliza kuwa masihi anazaliwa wapi na akaelezwa kwa mujibu wa maandiko, lakini alikuwa amefanya upumbavu mkubwa sana kwani nadhani alipaswa pia kuwauliza makuhani hao hao kuwa kuna madhara gani anaweza kuyapata mtu anayejaribu kuzuia mapenzi ya Mungu?  Na neno la Mungu lingemjibu hivi:-

Isaya 14:26-27 “Hilo ndilo kusudi lililokusudiwa duniani mwote, na huo ndio mkono ulionyoshwa juu ya mataifa yote. Maana Bwana wa majeshi amekusudia, naye ni nani atakayelibatili? Na mkono wake ulionyoshwa, ni nani atakayeugeuza nyuma?

Ayubu 9:4 “Yeye ni mwenye hekima moyoni, na mwenye uwezo katika nguvu; Ni nani aliyejifanya kuwa mgumu juu yake, naye akafanikiwa?

Wakati wote, mahali popote na saa yoyote kila mtu wa Mungu ni lazima ahahakikishe kuwa linapokuja swala ambalo ni mapenzi ya Mungu, sisi kamwe tusiwe sababu ya kuharibu au kuzuia mpango huo kwani kwa kufanya hivyo tunaweza kujikuta tunapingana na mapenzi ya Mungu jambo ambalo ni hatari na linaweza kuleta madhara makubwa sana, tuache kiburi na kujifikiri ya kuwa sisi ni maalumu sana, umaalumu wetu unaweza kuwa na maana kama tuko kwaajili ya kutimiza mpango wake, lakini umaalumu wetu unaweza kupotea ikiwa tu tunasimama kama kizuizi cha ule mpango halisi wa Mungu neno linaonyeshqa huwezi kuwa mgumu kwa mapenzi ya Mungu kisha ukatoboa! 

Matendo 5:38-39 “Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.”

Maandiko yanaonya vikali swala zima la kujaribu kushindana na mapenzi ya Mungu, onyo linatolewa kuwa kama kazi imetokana na binadamu inaweza kuvunjwa lakkini ikiwa imetokana na Mungu huwezi kuvunja  na kinyume chake mtu utakuwa unajiingiza kwenye mfumo wa Mungu, nakumbushia kuwa Mungu habadiliki, Mungu yule yule wa agano la kale ndiye huyu huyu wa Agano jipya, Rehema zake zinadumu hata kizazi na kizazi kwa wamchao, lakini jicho lake li juu ya watenda mabaya aliondoe kabisa kumbukumbu lao duniani.

Zaburi 34:15-16 “Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.”

 

Kwa maana wamekufa waliokuwa wakiitafuta roho ya Mtoto

Herode alikuwa moja ya wafalme ambaye alishindana na kusudi la Mungu kuhusu Maisha ya Yesu, alikuwa anataka kumwangamiza, alisahahu kujifunza kutoka kwa Farao ambaye mara kadhaa alikuwa akikataa mpango wa Mungu wa kuwaachilia wana wa Israel waende katika nchi iliyokusudiwa na Mungu na matokeo yake Taifa la Misri lilipatwa na mapigo mazito yaliyosababisha hasara kubwa kwa Farao na raia wake na mwishoe msiba wa wazaliwa wote wa kwanza  wa binadamu na wanyama uliwapata Misri nzima na kama haitoshi Farao na majeshi yake wote walifutwa na Mungu katika bahari ya shamu, na hakukuweko mtu aliyesalia hata kupeleka habari ya kile kilichowakuta!

Yeye ni mwenye akili moyoni, na mwenye nguvu nyingi, ni nani aliyemwasi naye akasalimika? Herode aliyaasi mapenzi ya Mungu na hivyo uwezo wake wa kuwa salama uliondolewa, kumbukumbu lake duniani lilifutwa, huwezi kuufunga mpango wa Mungu kwa vizuizi vya kibinadamu, Herode aliyatafuta sana maisha ya Yesu Kristo Mwana wa Mungu ili kuyaangamiza na kwa dhamiri mbaya kabisa aliangamiza watoto wengi kule Bethelehemu ili yamkini ikiwezekana miongoni mwao awe ni Bwana wetu Yesu Kristo, Nini kilimtokea Herode maandiko yanaeleza tu kuwa alikufa ona:-

Mathayo 2:19-21 “Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli.”

Hata hivyo Maandiko hayajaelezea kwa kina yaliyomkuta Herode, lakini kwa taarifa za Mwandishi maarufu wa kihistoria  wa karne ya kwanza Myahudi Flavius Josephus  anaelezea kuwa mara baada ya kuagiza askari kuwaua watoto wadogo wasio na hatia kwa kusudi la kummaliza na Yesu, kule Bethelehemu Mfalme huyo aliandamwa  na maumivu makali sana yasiyokoma, kujinyonga kwa utumbo mwembamba na kupata maumivu makali sana, kubanwa na pumzi mfano wa mtu mwenye pumu, maumivu makali katika kila sehemu ya mwili wake, mashambulizi makali ya figo, kumomonyoka kwa seli za mwili wake (gangrene) na maambukizi mabaya katika via vyake vya uzazi, kwa maelezo ya Mwanahitoria huyu nguli wa kiyahudi anaeleza kuwa pia siku zake za mwisho akiwa na mashaka makubwa sana aliuwa baadhi ya watoto wake wa kiume kwa hofu kuwa wangeweza kumpindua, na  mwisho aliagiza kuwa wakamatwe viongozi muhimu wa kiyahudi na serikali yake na kuamuru kuwa wauawe siku atakayokufa akiwa na mashaka kuwa hakuna mtu atakayeomboleza msiba wake kwa vile alivyokuwa katili, kwa nini haya yalimkuta Herode? Kutokana na kupingana na mapenzi ya Mungu na Mungu alimfutilia mbali ili mpango wa ukombozi kupitia Yesu Kristo uweze kukaa katika njia yake na mapenzi ya Mungu yaweze kusimama!

Hitimisho:

-          Hakuna mwanadamu anaweza kuzuia mpango wa Mungu hata siku moja iwe ndani ya mtu au katika agenda za Mungu  nay ale ambayo watumishi wake manabii wamesema

-          Mungu ataendelea kuweka ulinzi dhidi ya wale anaowatumia kwa mapenzi yake, na kujaribu kuwaharibu au kuharibu kitu cha Mungu kilichomo ndani yao ni kujiweka katika wakati mbaya wa kuharibiwa wewe na Mungu mwenyewe, Mungu huangalia maslahi yake mapana zaidi kuliko tamaa zako finyu, na kutaka kwako kujijengea umaarufu acha kabisa kushindana na makusudi ya Mungu na mpango wake.

-          Mungu akikugundua kuwa wewe ni kikwazo kwaajili ya kazi yake atakuondoa kwa wakati wake ili mpango wake uweze kutimia, Maneno haya wamekufa waliokuwa wakiitafuta roho ya mtoto  yanadhihirisha wazi kuwa Mungu alisimamamia kifo cha Herode ili mpango wake na agenda yake ndani ya Yesu Kristo iweze kuendelea, Siku zote Mungu ataondoa kila kikwazo kinachosimama mbele ya watoto wake  ili makusudi yake yaweze kutimia, do not mess-up with the G.O.D of Israel, usimkosee Mungu wa Wayahudi hata siku moja 

 

-          Kutoka 14:13-14 “Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.”

 

-          Tunajifunza kuwa Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa neema wanyenyekevu

 

Yakobo 4:6 Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.”

Mtu yeyote anayezuia mapenzi ya Mungu na kazi ya Mungu na makusudi ya Mungu hatadumu Mungu ana mwisho wa kila Herode anayeitafuta roho ya mtoto aiangamize, ikiwa uko katika mpango wa Mungu usiogope, kwani wanaoyatafuta maisha yako ili kuyaharibu wanaharibu ya kwao na kwa ghafla kama ilivyokuwa kwa Herode kiburi chao kitafikia mwisho.               

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni: