Isaya 63:7-9 “Nitautaja wema wa Bwana, sifa za Bwana kwa yote aliyotukirimia Bwana; na wingi wa wema wake kwa nyumba ya Israeli, aliowakirimia kwa rehema zake, na kwa wingi wa wema wake. Maana alisema, Hakika ndio watu wangu hawa, wana wasio na hila; akawa Mwokozi wao.Katika mateso yao yote yeye aliteswa, na malaika wa uso wake akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake, aliwakomboa mwenyewe; akawainua, akawachukua siku zote za kale.”
Utangulizi:
Tuwapo duniani wanadamu wote
tunakutana na maumivu ya aina mbalimbali katika maisha, maumivu haya yanaweza
yasilingane lakini kila mmoja anaweza kuhisi maumivu kwa jinsi yake, ziko
nyakati maisha yanakuwa magumu, ziko nyakati tunaumia moyo, ziko nyakati
tunalia machozi, ziko nyakati matumaini yanavunjika, ziko nyakati roho zinauma,
kwa ujumla kunakuwa na maswali mengi sana hususani wakati tunapopitia maumivu
haya, moyoni unaweza kuhisi kuwa labda Muumba naye angehisi maumivu haya,
tunajiuliza anasikia na anaumia kama ninavyoumia? Mungu wetu anajali kweli? Neno
la Mungu linaonyesha ya kuwa Mungu sio tu kuwa anayaona mateso yetu lakini pia
anaumia pamoja nasi kama baba anavyowahurumia watoto wake ndivyo Mungu wetu
anavyotuhurumia Maumivu yako ni maumivu yake!
Zaburi 103:11-14 “Maana mbingu zilivyoinuka
juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. Kama mashariki
ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. Kama vile
baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. Kwa maana
Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.”
Mungu anatupenda mno, anaweza
kuyatumia maumivu yetu kutimiza makusudi yake fulani fulani katika maisha yetu,
lakini hata hivyo yeye hafurahii maumivu yetu na anapatwa na uchungu ule ule
unaotupata sisi wakati wa maumivu yetu, anashiriki machozi yetu na anakaa nasi
wakati wa mambo magumu na kutukomboa kuhakikisha usalama wetu na furaha yetu
inakuwa kamilifu, Leo basi tutachukua muda kujifunza somo hili “Maumivu yako maumivu yake” kwa
kuzingatia yafuatayo:-
·
Maana ya
maumivu yako maumivu yake.
·
Mifano ya
watu ambao Mungu alioshughulika na maumivu yao.
·
Maumivu
yako maumivu yake.
Maana ya maumivu yako maumivu yake.
Usemi maumivu yako maumivu yake
unatokana na maelezo ya unabii wa Isaya katika mstari wetu wa msingi tuliousoma
ambao unaashiria kuwa, Mungu anaguswa sana na maumivu yetu, na ya kuwa
anateseka pamoja na wanadamu wanaoteseka anasikia uchungu kama wanavyosikia
uchungu, anahisi maumivu kama wanavyohisi maumivu, anaumia pale watoto wake
wanapoumia, na Analia pale watoto wake wanapolia hii ndio maana kubwa
tunayoipata katika mstari wa Msingi kutoka ktk
Isaya 63:9 “Katika mateso yao yote yeye
aliteswa, na malaika wa uso wake akawaokoa; kwa mapenzi yake, na huruma zake,
aliwakomboa mwenyewe; akawainua, akawachukua siku zote za kale.”
Neno katika mateso yao yote yeye
aliteswa, Neno aliteswa katika lugha ya Kiebrania linasomeka kama “tsar tsar” ambalo katika kiingereza
ni sawa na neno “Affliction” kwa
hiyo katika kiingereza maneno Katika mateso yao yote yeye aliteswa yanasomeka “in all their affliction he was afflicted”
neno hili ni sawa na kusema “Maadui
zao wakawa maadui zake” au “Maumivu
yao yakawa maumivu yake” au “Maumivu
yako maumivu yake” au “Katika taabu
zao alitaabika”hii maana yake ni kuwa Mungu anajua maumivu yako, anashiriki
taabu zako na mashinikizo yako, anasikia uchungu wako kama mtu awaye yote
mwenye huruma anavyohisi uchungu wa maumivu yako, wakati wote kama baba zetu wa
duniani wanaposikia uchungu kwa habari ya maumivu ya watoto wao, Mungu wetu wa
Mbinguni ambaye ni Baba anaguswa zaidi na maumivu yetu kuliko wanadamu ambao ni
waovu, maandiko yanaonyesha ya kuwa Mungu ni Baba anayejali watoto wake kuliko,
zaidi ya baba zetu wa duniani, ikiwa wao wanaumia kwaajili yetu, Mungu yeye
Maumivu yako, ni maumivu yake!
Luka 11:11-13 “Maana ni yupi kwenu aliye
baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki
atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua
kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho
Mtakatifu hao wamwombao? ”
Mifano ya watu ambao Mungu alioshughulika na maumivu yao.
Biblia imejaa mifano mingi
inayoonyesha jinsi ambavyo Mungu hakuwahi kuvumilia maumivu ya watu wake kwa
sababu zozote zile, aliyajua maumivu, hofu na changamoto walizokuwa wanazipitia
watu wake, alifahamu mashinikizo yao katika maisha na katika hekima yake na
huruma zake aliweza kuwajali na kushughulikia kwa haraka, changamoto hizo kabla
hawajamezwa kwa huzuni.
1.
Hajiri
– Aliteswa na Sara Bibi yake kiutawala alimuamuru Abrahamu kumtupa na
kumfukuzilia mbali majazi huko jangwani, Hajiri alikimbilia jangwani akiwa na
mwanae ambaye alikuwa anakaribia kufa kwa kiu ya maji, walianza kulia katika jangwa,
alimweka mtoto chini na kukimbilia mbali ili asimuone mtoto akifa, akalia kwa
uchungu Mungu aliguswa na mateso na kilio cha mtoto na mama yake na akaleta
ufumbuzi katika maisha yao
Mwanzo 21:14-19 “Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana.”
2. Israel Utumwani – Wote tunafahamu kuwa Israel walipata mikandamizo mingi na kuonewa na wasimamizi wao huko jangwani, hali ilikuwa mbaya kiasi ambacho Mungu alilazimika kuingilia kati kwaajili ya wokovu, ni ukweli ulio wazi kuwa Maumivu yao yalikuwa magumu na waliugua na kuumwa na shinikizo lile la utumwa usio wa kiungwana Maumivu yao yakawa maumivu yake Mungu ambaye kimsingi aliguswa na kushuka akipanga wokovu wao
Kutoka 3:7-10 “BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri.”
3. Mjane – Huyu mwanamke huko katika mji wa Naini alikuwa mjane, lakini licha ya kuwa mjane alikuwa na mwane mmoja kijana wa pekee, Neno la Mungu halisemi kulikuwa na mazingira gani kijana huyu alikufa na watu wa mji walitoka kwenda mazikoni, Yesu alipomuona mama huyu alimuhurumia maumivu yake yakawa maumivu ya Kristo, na akisukumwa na upendo wake na maumivu ya huruma zake Yesu alimfufua kijana yule mara!
Luka 7:11-15 “Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake.”
4. Lazaro – Alikuwa rafiki wa Yesu Kristo pamoja na dada zake Martha na Mariamu, Lazaro aliugua na baadaye akafa, Yesu alihudhuria msiba huu akiwa Mungu katika mwili aliguswa sana na maumivu ya dada zake Lazaro, ambao walilia wakiwa wamekata tamaa ya uhai, wakitarajia kuwa uwezekano wa kufufuka kwa Lazaro ni labda katika siku ya mwisho lakini akisukumwa na huruma maumivu yao yakawa maumivu yake Yesu akafanya tukio akamfufua
Yohana 11: 32-35 “Basi Mariamu alipofika pale alipokuwapo Yesu, na kumwona, alianguka miguuni pake, akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Basi Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliofuatana naye wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake, akasema, Mmemweka wapi? Wakamwambia, Bwana, njoo utazame. Yesu akalia machozi.”
Yohana 11:43-44 “Naye
akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje
yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa
leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.”
Maumivu yako maumivu yake.
Tunajifunza kupitia neno la Mungu
la msingi na mifano iliyopo katika maandiko ya kwamba Mungu wetu huwa anajishughulisha
sana na mambo yetu na kwa sababu hiyo pia ni muhimu kufahamu kuwa maumivu yetu
ni maumivu yake, kwa sababu hiyo hatakuacha ujaribiwe kupita uwezavyo, yuko
tayari kabisa kutoa mapumziko kwa wote wanaaonewa na kukandamizwa na Shetani
kwa sababu zozote zile. Usifikri hata kidogo kuwa tuna Mungu asiyejali, Maumivu
yako ni maumivu yake!
1Petro 5:6-7 “Basi nyenyekeeni chini ya
mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye
fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”
Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote
msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.”
Mathayo 8:16-17 “Hata kulipokuwa jioni,
wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote
waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema,
Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.”
Ni muhimu kwa sababu hiyo
kukumbuka kuwa maumivu yako ni maumivu yake, Maumivu yako si dalili ya kuwa
Mungu amekutupa bali ni njia ya kuthibitisha ya kuwa yuko pamoja nawe na
anakujali sana, wakati wewe unalia kumbuka Mungu analia pamoja nawe, Mungu
anayabeba maumivu yako kuliko yanavyobebwa na mwanasaikolojia yeyote yule, na
sio hivyo tu yeye atakupa nguvu na kukuwezesha kwa msaada wa Roho wake Mtakatifu,
kilio chako wakati wowote kinaweza kugeuka kuwa mbegu ya furaha na mafanikio
yako, uchungu wako unatambuliwa na Mungu kwa hiyo kama alivyosema katika mateso
yako yote yeye anateseka pamoja nawe kwa hiyo leo ishi ukifahamu ya kwamba
maumivu yako ni maumivu yake, ole wake anayekuumiza anamuumiza Mungu, ole wake
anayekulaani anamlaani Mungu, ole wake anayekugusa anamgusa Mungu.
Zekaria 2:8-10 “Kwa maana Bwana wa majeshi
asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi;
maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake. Kwa maana, tazama,
nitatikisa mkono wangu juu yao, nao watakuwa mateka ya hao waliowatumikia;
nanyi mtajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma. Imba, ufurahi, Ee binti
Sayuni; maana, tazama, ninakuja, nami nitakaa kati yako, asema Bwana.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni