Jumapili, 5 Oktoba 2025

Namjua anayeishika kesho!


Mathayo 6:31-34 “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”



Utangulizi:

Mojawapo ya tatizo kubwa la kiroho na kisaokolojia linalowakumba wanadamu ni pamoja na tatizo la kuogopa kesho au wakati ujao, tatizo la kuhofia kuhusu kesho au wakati ujao kisakolojia linaitwa “Chronophobia” au “time anxiety”  hofu ya wakati hususani wakati ujao ambayo kitaalamu inafafanuliwa kama “a type of anxiety that involves  worrying about tomorrow or future”  yaani ni aina ya msongo wa mawazo unaohusisha kuogopa au hofu kuhusu kesho au wakati ujao,  Neno Chronophobia ni muunganiko wa maneno mawili ya kiyunani “Chronos” yaani muda na “phobos” yaani hofu kwa hiyo wanadamu wengi wanasumbuliwa na hofu kubwa sana kuhusu itakuwaje kesho, katika Afrika wanawake wengi huongoza kwa hofu hii na ndio maana wengi huogopa kufiwa na waume zao na utawasikia wakisema kuna leo na kesho hali itakuwaje? Na wakati mwingine watu huogopa kuwa huenda kuna jambo baya litawatokea na watu wengi wanaogopa magumu, wengine huogopa muda kwa kufungwa gerezani, masikini huogopa kwamba kesho itakuwaje, matajiri huogopa kufilisika, wenye vyeo huogopa kuviachia, wafanya biashara huogopa hasara, Wengine huogopa muda kwa kufikiri kuwa wamekawia katika maisha, Tatizo la hofu linaweza kuwako katika pembe nyingi,  Ingawa tatizo hili linaweza kuwa la kawaida lakini kuna wanadamu wengine tatizo hili huwa kubwa zaidi kwao na linaweza kufikia hatua likaathiri Imani yao na ni kwa sababu hii Neno la Mungu linamtaka kila mmoja wetu kutokuogopa kuhusu kesho au wakati ujao na badala yake kumtegemea Mungu.

Mathayo 6:34 “Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”

Kwa nini neno la Mungu linatuonya kutokuogopa kesho? Hii ni kwa sababu Mungu ndiye anayeishika kesho, kesho yako na wakati wako ujao uko mikononi mwa Mungu na ukilitambua hilo huwezi kuogopa lolote, Kwa msingi huu basi leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu juu ya somo hili “Namjua anayeishika kesho” kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Hofu ya wanadamu kuhusu kesho.

·         Neno la Mungu linasemaje kuhusu kesho.

·         Namjua anayeishika kesho.


Hofu ya wanadamu kuhusu kesho.

Mathayo 6:25-34 “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”

Katika hutuba yake ya mlimani Mwalimu wetu mkuu na mwokozi wa maisha yetu Yesu Kristo hakuacha kuzungumzia swala zima la hofu ya wanadamu kuhusu kesho, wanadamu wengi masikini kwa matajiri wote wanakabiliwa na hofu kuwa itakuwaje kesho au maisha ya baadaye, hofu hii inaweza ikawa sio tu kwa mahitaji ya kawaida nitakula nini na nitavaa nini, lakini inaweza kuwa zaidi ya hapo, itakuwaje nikifiwa na mume, itakuwaje nikifukuzwa kazi, itakuwaje nikifilisika, itakuwaje nikidaiwa kodi, itakuwaje nikiachwa! Itakuwaje nikiugua? Itakuwaje nikishindwa uchaguzi, itakuwaje nikifeli, nini kitatokea, itakuwaje uchumi ukiyumba? Na kadhalika hofu hii ni tatizo kubwa la kiroho na kisaikolojia na Mungu analijua vema, anajua kuwa hofu hizi zinaweza kumpelekea mtu akakosa Amani, akapoteza usingizi, na hatimaye akapoteza Imani na matumaini na Ndio maana Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kwamba hawapaswi kuogopa kuhusu kesho kwa sababu Baba wa mbinguni anajua mahitaji yetu na ndiye anayeishika kesho!.

Neno la Mungu linasemaje kuhusu kesho.

Neno la Mungu linatufundisha ya kuwa ni Mungu ndiye mwenye uwezo wa kudhibiti kesho ya kila mmoja wetu, na hakuna mwanadamu ambaye anaweza kujisumbua kuhusu kesho yake na akafanikiwa bila neema na kibali cha Mungu, hofu yako wasiwasi wako na hata maandalizi yako hayawezi kukuhakikishia kesho iliyo salama na kamili bila Mungu, kwa sababu kesho haiko katika mikono ya mwanadamu bali iko katika mikono ya Mungu mwenyewe, wako watu ambao walijisumbua sana kuhusu kesho na neno la Mungu likawatumia kama mifano ya kutuonya kuwa huwezi kufanya kitu kuhusu kesho na ukajithibitishia usalama bila ya Mungu! Kesho iko kwenye mapenzi ya Mungu! Mungu ndiye anayeishika kesho ili mwanadamu asiwe na kiburi, Tancredo Neves alikuwa mgombea urais wa Brazili mwaka 1985 wakati wa kampeni zake alisema nikipata kura 500,000 tu kutoka kwenye chama changu hakutakuwa na wa kuzuia nisiwe Rais hata Mungu hataweza kunizuia, Kwa kweli alipata kura hizo na akashinda uchaguzi, lakini aliugua ghafla na utumbo ulijikunja akafariki siku moja kabla ya kuapishwa kuwa raisi Tarehe 21/4/1985. Lazima kila mmoja kwa unyenyekevu akubali kuwa kesho iko mikononi mwa Mungu na sio mikononi mwa mwanadamu.

Yakobo 4:13-15 “Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi.”

Luka 12:15-20 “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?               

Maandiko yanatuonya wazi kuwa hakuna mwanadamu anayeweza kudai kwa sababu zozote zile kwamba anaweza kuwa na uhakika wa kesho, na hata hivyo hatupaswi kuiogopa kesho pia, lakini kesho iko katika mikono ya Mungu na kwa sababu hiyo neno la Mungu linatuonya kuiacha hofu ya kesho katika mikono ya Mungu, badala yake tunatiwa moyo kumuamini Mungu na kumtegemea yeye kwaajili ya mahitaji yetu ikiwepo kesho yetu,  Neno la Mungu halitutii moyo kuogopa kuhusu kesho kwaajili ya mahitaji yetu, wala halituhakikishii kuwa tunaweza kutengeneza usalama wetu wa kesho kwa kujilimbikizia ua kujiwekea akiba au kwa kutafuta sana kunakoambatana na hofu ya kesho na pia hakuna mwanadamu awaye yote wa ngazi yoyote ile anayeweza kujithibitishia kuwa na kesho iliyo njema nje ya uweza na mamlaka ya Mungu Mwenyewe. Kwa sababu hiyo hatupaswi kujivuna au kujisifia lolote kuhusu kesho!

Mithali 27:1-2 “Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja. Mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe; Mtu mgeni wala si midomo yako wewe.”

Neno la Mungu linaonyesha wazi kuwa mwenye kesho ni Mungu tu, siku moja tu inaweza kuzaa jambo na likabadilisha kila kitu katika maisha yetu, kwa sababu hiyo hatuna budi kuishi kwa unyenyekevu na kwa kumtegemea Mungu pake yake, hatupaswi kuiogopa kesho kama tunamwamini Mungu na wala hatupaswi kujihami kuhusu kesho kama iko mikononi mwa Mungu hii maana yake ni nini? Maana yake ni kuwa Mungu ndiye anayeishika kesho na ukimjua yeye hutaweza kuishi maisha ya hofu ya aina yoyote ile, ukiwa na uhakika kuwa kesho yako iko kwake!

Namjua anayeishika kesho.

Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna hofu wala woga utakaokutawala endapo tu utagundua kuwa ni Mungu ndiye anayeishikilia kesho yako, Mungu anaweza kubadilisha mambo kwa usiku mmoja tu, ukitambua kuwa ni Mungu ndiye anayeishikilia kesho yako hakuna mwanadamu atakayekutisha wala kukutetemesha kuhusu yajayo, kesho yako haiko katika mikono ya wanadamu, iko katika mikono ya Mungu, ukimjua yeye anayeshika kesho hautaogopa mabadiliko ya aina yoyote ile, utamtegemea yeye ambaye ni ngome iliyo imara  naye hatakuangusha, Mwandishi wa Zaburi hakuwahi kuogopa mabadiliko yoyote yale kwa sababu alikuwa anamjua Mungu na kutambua ya kuwa ndiye anayeshikilia kila kitu kwa hiyo lolote litokee haliwezi kututisha kwa sababu yeye Mungu ndiye mwenye kesho yake!

Zaburi 46:1-7 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake. Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu. Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema. Mataifa yalighadhibika, falme zikataharuki; Alitoa sauti yake, nchi ikayeyuka. Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.”

Mungu wetu ni Mungu asiyebadilika, Yeye ni Yeye yule jana leo na hata milele, Yu hai, na bado anaendelea kubarikia watu wake, anaendelea kulinda watu wake, anakomboa watu wake, bado ni mtawala wa mbingu na nchi majira na nyakati, ziko mkononi mwake, hajawahi kupoteza nguvu zake wala uwezo wake Yeye bado ni Bwana Mungu aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na vyote vilivyomo, Ndiye aliyeigawa bahari ya Shamu, akamzika Farao na majeshi yake, akawalisha watu wake kwa mana, akawanywesha maji kutoka katika mwamba, akawapigania dhidi ya adui zao, akatimiza ahadi zake kwa kuwapa nchi ya Mkanaani, nguvu zake hazijawahi kupungua, alimfufua Lazaro, alimtoa Petro na Paulo na Sila gerezani, hakuna nguvu inaweza kupingana naye, Yeye ndiye anayeishika kesho, kesho yako haiko kwa waganga wa kienyeji, kesho yako haiko kwa bosi wako, kesho yako haiko kwa wenye mamlaka au cheo, kesho yako haiko kwa wachawi, kesho yako haiko kwa wapiga ramli kesho yako inashikwa na Mungu aliye hai, muumba wa mbingu na nchi, uaminifu wake unazidi kizazi hata kizazi na yeye anatuwazia mema na yeye habadiliki ni Yeye Yule jana leo na hata milele, Hakuna mtu anayeweza kuichafua kesho yako, hakuna mtu anaweza kuizibia kesho yako, kesho yako iko katika mikono ya Mungu, ukimjua anayeishika kesho yako hutaogopa, hakuna wa kukurudisha nyuma, tunaweza tusijue lolote kuhusu kesho, lakini tunaweza kumjua anayeishika kesho! Naye ni mwenye nguvu!

Kama Mungu ndiye anayeishika kesho yako maana yake unaweza kumuamini yeye kuhusu kesho yako na kutokuogopa wakati ujao ukijua ya kuwa anatuwazia mema na ana mpango mzuri kwaajili yako:-

Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.”

Kama Mungu ndiye anayeishika kesho yako maana yake hupawi kuogopa endapo unazingirwa na maadui pande zote na wanakukusudia mabaya hawawezi kutimiza mpango wao kwa sababu mpango wao sio mkuu kama wa yule anayeishika kesho:-

Zaburi 31:13-15 “Maana nimesikia masingizio ya wengi; Hofu ziko pande zote. Waliposhauriana juu yangu, Walifanya hila wauondoe uhai wangu. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia.”

Kama Mungu ndiye anayeishika kesho yako maana yake ni yeye anayeweza kukulinda kwa nguvu zake na mkono wake kiasi kwamba hutakuwa na lolote la kuogopa, hutaogopa wachawi, hutaogopa Shetani, hutaogopa, laana, hutaogopa wanaoukutishia maisha Imani na tumaini litakuwa kubwa kwa Bwana Mungu wako na hutaogopa vita wala majeshi makubwa ya adui yajapojipanga kupigana nawe kwa sababu yuko anayeishika kesho yako!

Zaburi 27:1-5 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini. Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake. Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba.”

Kama Mungu ndiye anayeishika kesho yetu tunajengewa uhakika na matumaini ya kuwa anajishughulisha sana na mambo yetu, atakutana na mahiaji yetu, na tutaishi kwa kujiamini bila kuogopa tukijua ya kua kesho ni ya Baba mwenye upendo na rehema ataishughulikia, sina ada italipwa, sina chakula nitakula, sina nguo nitavaa, sina raha nitapewa, nina mizigo itapumzishwa, nina madeni yatalipwa, sioni njia ataniongoza, naona giza atakuwa nuru!

Kumbukumbu 8:11-16 “Jihadhari, usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako.”

Kama Mungu ndiye anayeishika kesho yako, maana yake ni kuwa haitakuja utishike na kuweweseka kwa sababu yeye yuko siku zote, alikuwako tangu mwanzo, habadiliki, hageuki wala hana kigeugeu, wala kwake hakuna kubadilika badilika Yeye ni Yeye yule jana leo na hata milele  Waebrania 13:8 “Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.”

Yakobo 1:17 “Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.”

Kama Mungu ndiye anayeishika kesho yetu basi ni wazi kuwa hakuna jambo lolote lile linaloweza kututenga na upendo wake, hakuna wa kutuhukumu, hakuna wa kututishia maisha, hakuna wa kututishia kuhusu kesho, hakuna wa kutupunguzia kitu, hakuna wa kutupokonya ushindi, hakuna wa kututisha kwa maana kesho iko mikononi mwake

Warumi 8:31-39 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: