Jumapili, 19 Oktoba 2025

Na tazama, pazia la hekalu likapasuka!


Mathayo 27:50-54 “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”




Utangulizi:

Mojawapo ya matukio makubwa ya kutisha na kushangaza yaliyoambatana na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo pale Msalabani ni pamoja na tukio la kupasuka kwa pazia la hekalu, tukio hili lina tupa ishara madhubuti juu ya umuhimu wa kifo cha Yesu Kristo na nguvu ya upatanisho iliyofanywa na kifo chake kwa wanadamu wote wakiwemo Wayahudi pia, Njia ya kuufikia uwepo wa Mungu ilikuwa sio rahisi wakati wa agano la kale na ni watu wachache sana waliokuwa na ruhusa ya kuukaribia uwepo wa Mungu. Pazia kubwa zito lilitenganisha mahali patakatifu sana palipokuwa na kiti cha rehema na uwepo wa watu wa kawaida hivyo kuwanyima watu fursa ya kukutana na Mungu bila mtu wa kuingilia kati. Pazia hili lilitengenezwa kwa maelekezo ya Mungu kwa Musa, likizuia eneo la Sanduku.

Kutoka 26:30-33 “Nawe utaisimamisha hiyo maskani sawasawa na mfano wake ulioonyeshwa mlimani. Nawe fanya pazia la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na nguo za kitani nzuri zenye kusokotwa, litafumwa na kutiwa makerubi, kazi ya fundi stadi; kisha litungike katika nguzo nne za mti wa mshita zilizofunikwa dhahabu, vifungo vyake vitakuwa vya dhahabu, katika matako ya fedha manne. Nawe tungika lile pazia chini ya vile vifungo, nawe lete lile sanduku la ushuhuda na kulitia humo nyuma ya pazia; na lile pazia litawagawanyia kati ya patakatifu, na mahali patakatifu sana.”

Leo tutachukua muda kiasi kujifunza umuhimu wa pazia hili kupasuka wakati wa kifo cha Yesu Kristo na maana yake kubwa sana kwetu ambayo kimsingi inatupa tiketi ya kuuendea uwepo wa Mungu na kuufurahia ushirika na Mungu bila kupata madhara ya aina yoyote na bila ya kupitia kwa mtu yeyote, tutajifunza somo hili, Na tazama, Pazia la hekalu likapasuka kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-


·         Kazi ya Pazia la hekalu.

·         Na tazama pazia la hekalu likapasuka.

·         Faida za kupasuka kwa pazia la hekalu.


Kazi ya pazia la Hekalu!

Pazia la Hekalu ilikuwa ni nguo maalumu iliyotengenezwa kwa nyuzi za kitani zilizofumwa kwa ustadi kwa rangi mchangayiko wa aina tatu, rangi ya samawi, yaani mbingu, rangi ya zambarau na nyekundu, Pazia hili lilikuwa na ukubwa kwa maana ya urefu wa futi sitini (Sawa na mita 18) na upana wa futi 30 (sawa na mita 9) na unene wake ulikuwa kati ya inchi 4 mpaka sita yaani kati ya sentimita 10-15. Aidha lilifumwa pia likiwa na picha ya makerubi mfano wa ulinzi kwaajili ya patakatifu pa patakatifu, Pazia hili lilikuwa na kazi ya kupafunika au kutenganisha mahali patakatifu na patakatifu sana. Pazia hili lilitengenezwa kwa ustadi kufuata maelekezo yaliyotolewa na Mungu.

Kutoka 36:35-38 “Kisha akafanya hilo pazia la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri zilizosokotwa; akatia na makerubi kazi ya fundi stadi, ndivyo alivyofanya. Naye akafanya kwa ajili yake nguzo nne za mti wa mshita, akazifunika dhahabu; na kulabu zake zilikuwa za dhahabu; naye akasubu kwa ajili yake matako manne ya fedha. Kisha akafanya pazia la sitara kwa ajili ya mlango wa Hema, la nguo ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na nyekundu, na nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, kazi ya mwenye kutia taraza, na nguzo zake tano pamoja na kulabu zake; naye akavifunika dhahabu vichwa vyake na vifungo vyake; na matako yake matano yalikuwa ya shaba.”

Kazi kubwa ya Pazia hili ilikuwa ni kutenganisha mahali patakatifu na patakatifu sana, hekalu lilikuwa na sehemu kubwa tatu, Patakatifu sana au patakatifu pa patakatifu mahali ambapo lilikaa sanduku la agano la Bwana, na patakatifu mahali ambapo palikuwa na madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba, taa ya vinara saba na meza ya mikate ya wonyesho, eneo hili kuhani aliingia kwaajili ya kufukiza uvumba, kila siku na kisha eneo la tatu ulikuwa ni uwa wa kawaida ambapo Wayahudi walikaa, na Mataifa wasio Wayahudi walikaa mbali zaidi katika uwa wa wamataifa. Pazia lilitenganisha mahali lilipokuwepo sanduku la agano ambalo juu yake kulikuwa na kiti cha rehema,  mahali hapa kuhani mkuu aliingia mara moja tu kwa mwaka kufanya upatanisho kwa watu na Mungu, siku ya upatanisho tena akiwa amejitakasa kweli kweli (siku saba maalumu kabla ya kuingia katika ibada hiyo), Pazia hili ni alama ikiwa na fundisho kuwa Mungu ni MTAKATIFU SANA na sio rahisi mwanadamu wa kawaida kumsogelea bila kupata madhara, Pazia hili zito lilikuwa ni katazo kuwa huwezi kuufikia uwepo wa Mungu wala kuona ukawa salama, Kuhani mkuu mwenyewe aliingia hapa mara moja kwa mwaka wala si pasipo damu tena siku ya upatanisho (Yom Kippur) kutoa dhabihu ya dhambi kwaajili yake, familia yake na watu wa taifa zima! Kinyume chake kifo kingehusika.

Kutoka 30:10 “Naye Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe zake mara moja kila mwaka; kwa damu ya ile sadaka ya dhambi ya kufanya upatanisho, mara moja kila mwaka ataifanyia upatanisho, katika vizazi vyenu vyote; ni takatifu sana kwa BWANA.”

Waebrania 9:1-9 “Basi hata agano la kwanza lilikuwa na kawaida za ibada, na patakatifu pake, pa kidunia. Maana hema ilitengenezwa, ile ya kwanza, mlimokuwa na kinara cha taa, na meza, na mikate ya Wonyesho; ndipo palipoitwa, Patakatifu. Na nyuma ya pazia la pili, ile hema iitwayo Patakatifu pa patakatifu, yenye chetezo cha dhahabu, na sanduku la agano lililofunikwa kwa dhahabu pande zote, mlimokuwa na kopo la dhahabu lenye ile mana, na ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya agano; na juu yake makerubi ya utukufu, yakikitia kivuli kiti cha rehema; basi hatuna nafasi sasa ya kueleza habari za vitu hivi kimoja kimoja. Basi, vitu hivi vikiisha kutengenezwa hivyo, makuhani huingia katika hema hiyo ya kwanza daima, wakiyatimiza mambo ya ibada. Lakini katika hema hiyo ya pili kuhani mkuu huingia peke yake, mara moja kila mwaka; wala si pasipo damu, atoayo kwa ajili ya nafsi yake na kwa dhambi za kutokujua za hao watu. Roho Mtakatifu akionyesha neno hili, ya kwamba njia ya kupaingia patakatifu ilikuwa haijadhihirishwa bado, hapo hema ya kwanza ilipokuwa ingali ikisimama; ambayo ndiyo mfano wa wakati huu uliopo sasa; wakati huo sadaka na dhabihu zinatolewa, zisizoweza kwa jinsi ya dhambi kumkamilisha mtu aabuduye,”

Kwa sababu hii watu wa kawaida hawakuweza kabisa kupakaribia mahali hapa, kwani hata kuhani alivalishwa kengele (njuga) maalumu kiunoni na mguuni na kufungwa kamba maalumu ili kama atapigwa na Mungu na kufa wamvute nje, watu wengine wote, wangekuwa nje mbali wakiwa wametengwa mbali na mahali hapo patakatifu sana kwaajili ya dhambi na matakwa ya kisheria, hivyo pazia lilikuwa linawakilisha ugumu wa kuufikia uwepo wa Mungu, Pazia lilikuwa linawakumbusha wakati wote kuwa Mungu ni MTAKATIFU SANA na sisi wengine wote hatustahili, dhambi ilikuwa imetufarakanisha mbali na Mungu na hakuna jitihada yoyote ya kibinadamu inayoweza kutuunganisha, utaratibu wote huu ulikuwa pia unafundisha ya kwamba tunahitaji mtu wa kutupatanisha na Mungu, hakuna mwanadamu yeyote aliruhusiwa kupita kwenye pazia hili, maovu ya mwanadamu yalimfarikisha na Mungu.

Isaya 59:1-2 “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.”             

 

Na tazama pazia la hekalu likapasuka.

Katika namna ya kushangaza sana na isiyoweza kubuniwa kibinadamu Neno la Mungu katika agano jipya linatufahamisha katika injili zifafanazo zote kuwa pazia hili lililokuwa na unene wa nchi 4-6 hivi kwa njia ya muujiza mkubwa usiokuwa wa kibinadamu mara Yesu alipokata roho na kufa msalabani pazia hili la hekalu lilipasuka katikati vipande viwili kutoka juu hata chini! Muujiza huu usiokuwa wa kawaida ulirekodiwa katika injili zote tatu zifananazo.

Mathayo 27:50-51. “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;”

Marko 15:37-38 “Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho. Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini.”

Luka 23:44-45 “Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati.”

Kwa nini tukio hili linakuwa la muhimu kiasi hiki mpaka kila mtume anarekodi habari hii, kwa ujumla hili sio jambo dogo, lina kitu cha muhimu cha kutufundisha, Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anaeleza kwamba sababu kubwa ni kuwa Yesu Kristo mwana wa Mungu alifanyika Mwana kondoo mkamilifu, aliyejitoa mwenyewe kama sadaka ya kudumu ya milele na kwa damu yake kuwa mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu, Mwandishi anafafanua kuwa lile pazia linawakilisha mwili wa Yesu Kristo, kwa hiyo wakati mwili ule unasulubiwa kwa ajili ya dhambi zetu, Kristo anafanyika kuwa mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu na hivyo hatuhitaji tena kuhani wa kuingia katika kiti cha rehema kwaajili yetu, na ukuta uliotutenganisha na Mungu umebomolewa, kusulubiwa kwa Yesu Kristo kumeleta uponyaji mkubwa sana kwetu wa kimwili na kiroho, na hatuhitaji tena mtu awaye yote ajifanye “dalali” wa kiroho, au ajifanye kuwa yeye  anaweza kutupatanisha na Mungu ni ukweli ulio wazi kuwa mpatanishi ni mmoja tu. Yesu Kristo!

Waebrania 10:19-21 “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu;”

Isaya 53:2-5 “Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”

1Timotheo 2:5-6 “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.

Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”            

1Petro 2:9-10 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.”

1Wakorintho 6:19 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe;”      

 

Faida za kupasuka kwa pazia la hekalu

Kupasuka kwa Pazia la hekalu kunatupa faida lukuki ambazo muda usingeliweza kutosha kuelezea yote lakini njia ya kumuendea Mungu na kufanya ushirika naye leo imekuwa wazi kwa kila aaminiye, kutoka kokote kule duniani!

-          Tunaweza kumuendea Mungu kwa maombi na kuzungumza naye moja kwa moja bila dalali huku tukiwa na uhakika kuwa Mungu anatusikia  Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”

 

-          Tunaweza kumuendea kwa ibada na kumuabudu kwa kumsifu na kumshukuru tukiwa na uhakika kuwa yeye ni Bwana Mungu wetu kwani tuna uwezo wa kuingia malangoni mwake Zaburi 100:4-5 “Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; Nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini jina lake; Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; Rehema zake ni za milele; Na uaminifu wake vizazi na vizazi.”

 

-          Tunaweza kulifurahia neno lake ambalo kimsingi zamani ni makuhani pekee ndio waliokuwa na uwezo wa kulisoma na kulifafanua kwa watu, Neno la Mungu sasa ni kwaajili ya kila mtu na linaeleweka kwa kila amtafutaye Mungu

 

2Timotheo 3:16-17 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”

 

-          Tunaweza kuufurahia uwepo wa Mungu pamoja na wengine kwani kila tunapokutana na kukusanyika kwa jina lake yeye naye anaungana nasi na kuwa kati kati yetu.

 

Mathayo 18:18-20 “Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.”

 

-          Tunaweza kuziungama dhambi zetu wenyewe moja kwa moja na Mungu akatusamehe bila kupitia kwa kuhani wa kibinadamu kama ilivyo katika baadhi ya dini ambapo makuhani hutaka kuwatawala wanadamu na kuwanyanyasa kisaikolojia kwa sababu wanataka kusikiliza dhambi zao, au wanafanya kazi ya upelelezi

 

1Yohana 1:8-9 “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.”            

 

Kupasuka kwa pazia la hekalu ni tukio la kusangaza sana na si la kihistoria tu bali ni kazi kubwa ya Mungu yenye kumaanisha kuwa Mungu anatoa mwaliko kwa kila mmoja kuukaribia uwepo wake haijalishi umetoka katika historia gani,  na wa kabila gani, Mungu sasa haishi nyuma ya pazia wala hafikiwi kupitia mtu, kuhani au dalali, lakini kupitia Bwana wetu Yesu Kristo mlango ulio wazi umefunguliwa kwa jamii nzima ya aina binadamu duniani kuwa huru na kuufikia uwepo wa Mungu, hakuna wa kujidai katikati yetu badala yake tunasaidiana na kujengana huku tukitiana moyo kwamba leo uiamini kazi  yake Bwana aliyoifanya msalabani kwamba imefungua njia kwaajili yako na yangu na Wayahudi wote duniani kokote waliko kwamba Mungu yuko tayari kukutana na kila mtu anayemjia katika jina la Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai Amen

               

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: