Mstari
wa Msingi: Matendo 6:3-5
“Basi ndugu,
chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na
Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba
na kulihudumia lile Neno.Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote;
wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na
Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;”
Mungu kamwe hamtumii mtu ambaye yuko
tupu, awaye yote ambaye yuko tupu ni rahisi kutumiwa na shetani na mapepo Mathayo 12: 43-45 “Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta
mahali pa kupumzika, asipate. Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu
nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa.Mara huenda,
akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao
huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya
kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya.”
Yesu Kristo mwana wa Daudi kutoka
katika ukoo wa Yese alitumiwa sana na Mungu kwa viwango kwa sababu Hakuwa tupu
alijaa Roho Mtakatifu katika ukamilifu wake
Isaya 11:1-2 “Basi litatoka chipukizi katika shina
la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya
Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho
ya maarifa na ya kumcha Bwana;”
Mungu
anataka kumtumia mtu aliyejaa mambo muhimu saba yafuatayo:-
1. “Kujaa utimilifu wa Mungu”Be
filled with the fullness of God.
Waefeso 3:14-19 “Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba
wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa
utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa
ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa
imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na
watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua
upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika
kwa utimilifu wote wa Mungu.”
Kwa
lugha nyepesi kusudi kubwa la Mungu ni kutupeleka katika hatua ya kuwa watu
wazima, kukomaa kutokuwa wachanga kiufahamu na kiroho, kuwa wakamilifu kama
Kristo Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii;
na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi
la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo
ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana
Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha
utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku,
na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata
njia za udanganyifu.”
Kujaa
utimilifu wa Mungu ni kujaa ujuzi kuhusu Mungu na kuigiza kila kitu na kila
tabia aliyokuwa nayo Yesu Kristo kwa sababu katika yeye na katika tabia zake na
mtindo wake wa maisha tunajifunza utimilifu wa Mungu Wakolosai 2:9 “Maana katika yeye unakaa
utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.”
Kama
utimilifu wa Mungu utajaa ndani yetu kuna faida kubwa sana nyingi tutakazoweza
kufaidika nazo
a. Tutajaaa upendo wenye kujitoa kwaajili
ya wengine Yohana 15:13 “Hakuna aliye na upendo
mwingi kuliko huu wa mtu kuutoa uhai wake kwaajili ya rafiki zake”
Upedno wenye kujidhabihu kwaajili yaw engine PHILEO, STORGE, EROS, AGAPE., Mother Teresa, Will Pooley and
Maximilian Kolbe. Ni mifano ya kuigwa duniani katika upendo wenye kujitoa
kwaajili ya watu wengine upendo wa aina hii hatuwezi kuwa nao kama hatujajaa
utimilifu wa uungu ndani yetu tuone mifano ya watu hao:-
Mama Teresa wa Culcuta India (1910-1997) anaheshimika sana duniani
kwa kuwahurumia wengine,alipewa nishani ya Nobel 1979,alianza akiwa masikini
lakini alianzisha vituo vya ukarimu kwa ajili ya kuwasaidia yatima na
wajane,wasiojiweza na wenye njaa, leo hii kuna matajiri wengi sana wasio na
huruma kwa wengine wanaongoza kwa dhuluma na ufisadi wewe utalifanyia nini taifa
upendo wenye kujitoa tu ndio unaweza
kukusaidia kuhisi maumivu ya wengine.
Daktari mmoja
wa Uingereza aitwaye Will Pooley
alikuwa ni moja ya madaktari waliokuwa mstari wa mbele Nchini “Sierra Leone” huko walikuwa na wenzake
wengi wakipambana na wagonjwa wa EBOLA na virusi vyake katika
harakati hizo Madaktari wengi sana na Manesi wengi sana wakiwemo wa
Afrika Magharibi waliambukizwa virusi vya ebola wakati walipokuwa wakiwauguza
wagonjwa na wengi wao walikufa
Ugonjwa utokanao na kirusi
cha Ebola ni ugonjwa hatari wenye uwezo wa kusababisha kifo kwa asilimia 90.
Shirika la afya duniani, WHO katikatovuti yake inasema kwa mara ya kwanza ulibainika mwaka 1976 huko
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Sudan. Chanzo cha kirusi hiki hadi
sasa hakijulikani lakini popo aina ya (Pteropodidae) wanaonekana kuwa wabebaji
wa kirusi hicho, kwa mujibu wa ushahidi uliopo sasa.
Maambukizi hupatikana kwa
kila aina ya majimaji yanayotoka katika mwili wa binadamu ni ugonjwa hatari na
unaoua kwa haraka na hauna tiba
Will Pooley alipoupata
ugonjwa huu alirejeshwa katika ndege maalumu na kuanza kutibiwa chini ya
uangalizi maalumu huko uingereza
Jambo la kushangaza ni kuwa
baada ya kupona kwa bahati tu Will Pooley alitangaza nia yake ya kurudi tena
Sierra Leone kusaidiana na wenzake kupambana na ugonjwa huo.
Mtu huyu aliwashangaza wengi
sana na kuwaogopedha wengi sana akiwa amepona kwa asilimia 100%alisema atarudi
Africa kusaidia zaidi maana alizaliwa kwaajili ya hayo, jambo hili lilimfanya
aandikwe kama shujaa na mwanadamu mwenye uwezo wa kujitoa kwa kiwango cha juu.
Maximilian
Kolbe alikuwa ni Padre aliyetokea Poland aliuawa kama mfungwa tarehe 14 August 14,1941, Jeshi la wa NAZI
waligundua kuwa baadhi ya wafungwa wamejaribu kutoroka na hivyo waliamua kuwaua
wafungwa kadhaa, walijaribu kuwaua kwa njia mbalimbali, na hivyo walichagua
wafungwa 10 ili wauawe na kifo chao kiliamuriwa kuwa kifo cha njaa, wafungwa
waliamuriwa kujitoa mmoja mmoja yeye mwenyewe na mfungwa wa kwanza kuchaguliwa
alijulikana kama Franciszek Gajowinczek
mfungwa huyu alipochaguliwa alilia kwa huzuni kubwa akimtaja mkewe, watoto wake
na familia yake na kusikitika kuwa hatowaona tena kutokana na swala hili
Maximillian alisimama na kusogea mbele na kuomba afe yeye kwa niaba ya
Franciszek ombi lake lilikubaliwa, wafungwa waliwekwa kizuizini kwa muda wa
siku kadhaa bila kula wengine walikunywa mikojo yao ili waweze kuishi,
Maximillian alikaa kwa wiki mbili bila kufa huku wengine wote wakiwa wamekufa,
walimchoma sindano ya kufa hakufa na hivyo waliamua kukata kichwa Pope John
Paul II alimtangaza kuwa Mtakatifu kutokana na moyo wake.
Hawa walijitoa maisha yao kwaajili ya wengine kutokana
na upendo wenye kujitoa na kujidhabihu, Yesu Kristo aliyatoa maisha yake
kwaajili yetu sisi nasi hatuna budi kujitoa kwaajili yaw engine katika upendo.
b. Tutajaa Unyenyekevu!
Yesu Kristo alikuwa mnyenyekevu lakini vilevile
alikuwa mtii, aliyatii mapenzi ya Mungu hata katika namna yenye kuumiza,
hakujihesabu kuwa ni Bora wala hakujikweza na hivyo Mungu alimheshimu sana Wafilipi 2:3-5 “Msitende
neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu
na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali
kila mtu aangalie mambo ya wengine.
Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo
Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa
sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana
utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena,
alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti,
naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia
Jina lile lipitalo kila jina;”
Njia ya kuinuliwa na kupelekwa juu na Mungu ni
unyenyekevu, kama tutajifikiri wenyewe kuwa ni bora kuliko wengine tutapoteza
neema ya Mungu kwetu Mungu huwapinga wenye kiburi bali huwapa wanyenyekevu
neema, Injili ilikuja kwaajili ya watu wanyenyekevu Luka 4:17-19 “Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta
mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta
kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa
kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka
wa Bwana uliokubaliwa.”
Watafasiri wa Biblia za kiingereza na kiswahili
walionukuu Yesu walikuwa na mawazo ya kufikiri kuwa Yesu alikuja kwa ajili ya
masikini hivyo walitumia neno “Poor”
hii haikuwa tafasiri sahii ya andiko hili kwa vile andiko hili lilinukuliwa
kutoka katika kitabu cha Isaya mwenyewe anazungumzia wanyenyekevu na sio
masikini, Isaya 61:1-3 “Roho ya Bwana
MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri WANYENYEKEVU
habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka
uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka
wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote
waliao;”
Ukweli wa kibiblia unaonyesha wazi kuwa Mungu anafanya
kazi na wanyenyekevu na anapendezwa nao na kuwapa neema na kuwaangalia Isaya 66:1-2 “Bwana asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha
enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna
gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani? Maana mkono wangu ndio
uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu
huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka,
atetemekaye asikiapo neno langu.”
Kama hatutakuwa wanyenyekevu ni vigumu kuhudumiana, ni
vigumu kutambua uweza alionao mtu mwingine endapo kila mtu atajifikiri kuwa ni
bora katika nafsi yake , lakini biblia pia inataka watu wenye umri mdogo
kuwaheshimu wenye umri mkubwa 1Petro 5:5 “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi
nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga
wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono
wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;”
Unyenyekevu ni nini hasa ?- unyenyekevu ni hali ya kutokujifikiri kuwa
wewe ni wa muhimu kuliko wengine, Humble or Humility ni hali ya kutokufikiri
kuwa wewe ni bora kuliko wengine, hali ya kutokutumia mamlaka uliyo nayo
kufanya lolote kwa mtu unayeweza hata kumdhuru.
Kwa Mungu hali hii inakubalika kama namna ya kujifunza
kutoka kwa Yesu Kristo.
c. Hakutakuwa na Mafarakano!
Kama hatutakuwa katika utimilifu wa Mungu, kutakuwa na
mafarakano kwetu, migawanyiko na hii ni dalili ya uchanga, nyakati za kanisa la
kwanza huko Koritho kulikuwa na migawanyiko, watu walisahau kuwa wao ni kitu
kimoja na wakaanza kushabikia wanadamu Paulo mtume aliwakemea 1Koritho 1:10-13a “Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote
mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri
moja. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani
mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila
mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa
Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo
amegawanyika?”
Paulo mtume aliyakemea mafarakano haya na kuwaeleza
wazi kuwa kama watu kanisa, familia, shirika lina mafarakano basi ni wazi kuwa
hawajakomaa 1Wakoritho 3:1-9 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na
watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na
watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa
kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi
ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si
watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana
hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je!
Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao
mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji;
bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali
Mungu akuzaye. Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila
mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe. Maana sisi
tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu.
kila mmoja katika mwili wa Kristo ana nafasi yake na hivyo hatupaswi kuwa na
mafarakano na kufikiri kuwa fulani ni bora kuliko mwingine”
2.
Kujaa
Roho Mtakatifu. “Be
filled with the Spirit.”
Hakuna jambo
muhimu katika maisha ya mwanadamu na maisha ya Ukristo kama kujaa Roho
Mtakatifu, katika maswala yaliyokaziwa sana na maandiko ni pamoja na kujaa Roho
Mtakatifu biblia inasema katika Waefeso 5:18 “Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe
Roho;” Kwa nini ni Muhimu kujaa Roho Mtakatifu? Mungu anatumia watu waliojaa Roho, ni muhimu sana
kukubali kwamba maisha yetu yaongozwe na Roho Mtakatifu, Roho Mtakatifu
akiyaongoza maisha yetu au akiachiwa aongoze maisha yetu tunakuwa na amani,
tutakuwa na furaha, tutakuwa na ujasiri, hatutapoteza tumaini, tutakuwa
wavumilivu, tutakuwa watu wema, tutakuwa wanyenyekevu au wapole. Na hakutakuwa
na bahati mbaya katika maisha yetu Luka
4:1-2 “Na
Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho
muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa
hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa.” Roho wa Mungu atatupa
maisha ya furaha na ushindi hata kama utakutana na changamoto za aina yoyote,
nyakati tulizonazo watu wengi sana wamekuwa wakilalamika na kushindwa kusimama
katika nafasi zao kwa sababu ya kumuacha Roho pembeni, hii haimaanishi kuwa
hawana Roho wa Mungu hapana, wanaye lakini hawataki kijizoeza maisha ya
kuongozwa na Roho mtakatifu na wanataka kujiongoza wenyewe na hivyo wanashindwa
na hivyo wanaishi maisha yasiyo na furaha, Mtu aliyejaa Roho wa Mungu
·
Atakupa ujasiri wa kuwa shahidi wa Yesu
Kristo hata kifo Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho
Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi
wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”
·
Anawezeshwa kufanya mambo ya kupita
kawaida Matendo 6:8 “Na Stefano,
akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.”
·
Anapewa ujasiri wa kupita kawaida na
kukuwezesha kushinda majaribu Matendo 4:8-13
“Ndipo
Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa
Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu,
jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina
la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua
katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye
jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la
pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina
jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.
Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na
elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja
na Yesu.”
·
Atakuongoza katika kweli ya neno la
Mungu ili kwamba mjaribu asikushinde Yohana
16:13 “Lakini
yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa
maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena,
na mambo yajayo atawapasha habari yake.”
·
Atakufariji na kukushauri wakati wa
maswala magumu Yohana 14:16 “Nami nitamwomba
Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; “
3. Kujazwa maarifa ya Mapenzi yake
“Be filled with the knowledge of His will”
Wakolosai 1:9
“Kwa sababu
hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa
ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa
rohoni;” Kuyajua mapenzi ya Mungu ni jambo la Muhimu,
watu wengi sana wanashindwa kujua kuwa wanachokifanya au walipo ni mapenzi ya
Mungu au hapana kwa kujaa neno lake na kulielewa na kulifahamu itatusaidia
kuyajua mapenzi ya Mungu, kila mmoja
anahitaji kujua maarifa ya mapenzi yake
Angalia
kwamba Paulo mtume anawaombea kanisa la kolosai ili wajazwe maarifa ya mapenzi
yake katika hekima yote na ufahamu wa Rohoni, kumbe kwamba pamoja na kuwa
tumeokolewa bado kuna maswala ya msingi tunapaswa kuyafahamu, mojawapo ni kujazwa
maarifa ya mapenzi yake, ni nini maana ya maarifa ya mapenzi yake?
Nyakati
za kanisa la kwanza katika Asia ndogo na ulaya kulikuwa na kiu kubwa sana
kuhusu kujaa maarifa na falsafa za aina mbalimbali, watu walijaa maarifa ya
maswala mbalimbali “Gnosticism” waliamini kuwa ukiwa na maarifa tayari umeokoka
na kukosa maarifa ni dhambi, kwa vile walikuwa wameiamini injili Paulo sasa
alitaka wajae maarifa ya mapenzi ya Mungu na waweze kuyaishi ni kama Paulo
anawaambia kuwa maarifa pekee hayatoshi, lakini mtu akiyajua mapenzi ya Mungu
atajua namna na jinsi ya kuenenda kwa hekima katika ulimwengu huu “Hekima ni matumizi sahii ya maarifa”
“wisdom is the application of Knowledge” kwamba kama watajaa maarifa ya
mapenzi ya Mungu na kuyatumia watakuwa na ufahamu wa maswala ya Rohoni pia kama
Paulo anavyowaombea wakolosai ni wazi kuwa moja ya maombi muhimu ambayo
tunaweza kuwaombea wenzetu ni pamoja na kujaa maarifa ya ujuzi wa mapenzi ya
Mungu.
4.
Be
filled with joy “Ujawe na Furaha”
2Timotheo 1:3-4
“Namshukuru
Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile
nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana. Nami natamani
sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha;”Ni
ukweli ulio wazi kuwa waraka huu Paulo aliandika akiwa kifungoni akiwa
anakaribia kunyongwa au kuuawa na huku ndugu wengi wakiwa wamemuacha huenda
jambo hili lilikuwa limemliza sana Timotheo ambaye aliishi vema na Paulo mtume
kama mtu na baba yakewakati huu Paulo anatamani sana kumuona Timotheo ili kwamba
aweze kujawa na furaha, Kujawa na futaha ni mapenzi ya Mungu hususani
tunapokuwa katika mapito ya aina mbali mbali Shetani anapenda kuona kwamba
tunahuzunika na kukata tamaa ni furaha ya maadui pia kuona machozi yako lakini
hupaswi kuhuzunika Biblia inasema kama tunafanya kwaajili ya Bwana basi furaha
ya Bwana ndio nguvu zetu Nehemia 8:10
“Kisha
akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena
mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu;
wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.” Biblia
inaamuru tuwe na furaha siku zote 1Wathesalonike 5:16 “Furahini siku
zote;” Shetani na maajenti wake siku zote watataka uwe na huzuni
usikubali hakikisha kuwa unapigania furaha yako kwa gharama yoyote.
5. “Jaa imani”Be filled with Faith
Mtualiyejaa
imani hi mtu wa kiwango kingine na kamwe hapotezi mwelekeo hata siku moja mtu
aliyejaa imani anaona kwa mlango wa sita wa fahamu ambao wengine hawaoni, mtu
wa imani anaona kuwa aliyekufa amelala tu, uwezo wa mtu wa imani ni tofauti na
uoni wa mtu wa mwilini, mtu wa imani anakuwa imara zaidi wakati wa maswala
magumu kwa vile anaona upenyo mahali ambapo wengine hawaoni, Stefano alikuwa
moja ya watu mashujaa waliokuwa tayari kufa kwaajili ya kristo kwa vile alikuwa
anaona kwa uhakika kuwa kifo ni hatua ya kumpeleka sehemu nyingine yeye
anasifiwa katika maandiko kuwa mtu aliyejaa imani Matendo 6:5 “Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote;
wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na
Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;”
Biblia inasema pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, Mungu anataka
mwenye haki wake aishi kwa imani na akisistasita roho yake haina furaha naye Habakuki 2:4 “Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu
ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake.”
Imani ni nini hasa? Waebrania 11:1 “Basi
imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo
yasiyoonekana.” Mungu anataka tujawe na imani imani
inaleta kujitegemeza kwa Mungu na kuonyesha nguvu ya mtu anayemtegemea Mungu na
huleta utukufu kwa Mungu.
6.
“ mjazwe Neema”Be
filled with Grace
Nyakati
za kanisa la kwanza walikuwa na ufahamu sana kuhusu umuhimu wa neema na hivyo
mara kwa mara moja ya Baraka kubwa sana iliyotolewa na mitume ilikuwa ni pamoja
na kuwatakiwa watu neema angalia 1Koritho 1:3 Neema na iwe kwenu, 2wakoritho 1:2 Neema na iwe kwenu,Wagalatia 1:3 Neema na iwe kwenu, Waefeso 1:2 Neema na iwe kwenu, Wafilipi 1:2
Neema na iwe kwenu, Wakolosai 1:2 Neema na iwe
kwenu,2Thesalonike 1:2 Neema na iwe
kwenu, Tito 1:4 Neema na iwe
kwako, Filemoni 1:3 Neema na iwe
kwenu, Je unadhani ni kwa nini Neema inaonekana kuwa ni kitu cha
Muhimu na Baraka kubwa sana ? neema ikiwa juu yako wewe sio mtu wa kawaida,
wewe utatenda maajabu na mambo ya kushangaza, watu wote na mashujaa wote wa
biblia walikuwa ni watu waliojaa neema, ukiwa na neema wewe una ngekewa, wewe
una bahati, wewe ni wa tofauti, utapata kibali kwa Mungu na wanadamu, Mungu
mwenyewe atakutumia kwa viwango vya kupita kawaida ni muhimu kwetu kumuomba
Mungu atujaze neema, neema itatuwezesha kutenda mambo makubwa chini ya uvuli na
msaada wa Mungu Yesu alijaa neema, Stefano alijaa Neema , Paulo mtume alijaa
neema, Musa alipata neema na wote walifanyamambo makubwa duniani na katika
mwili wa kristo
Matendo 6:8 “Na
Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika
watu. “ Luka 2;40 “Yule mtoto akakua,
akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.” Yohana
1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu;
nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba;
amejaa neema na kweli.” Ni
watu waliojaa neema tu ndio walioweza kutumiwa na Mungu kwa namna ya kutisha na
kushangaza, kama mtu anataka mafanikio ni muhimu kujitafutia neema ya Mungu,
ukijazwa neema wewe ni tajiri wa ajabu wewe utatenda mambo makuu na hakuna mtu
anaweza kushindana na mtu aliyepewa neema Paulo mtume alipewa neema kubwa sana
na Mungu na akafanya kazi kubwa sana ya kulijenga kanisa kwa mafundisho yake 1Wakoritho 3:10 “Kwa
kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima,
naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na
aangalie jinsi anavyojenga juu yake.” mwenyewe alitambua wazi kuwa
alikuwa amepewa neema kusimamia ujenzi wa kazi ya Mungu na kuweka msingi ambao
ni yesu Kristo. Musa alijaa neema Kutoka
33:12 “Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia,
Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami.
Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu.” Bwana na
ampe kila mmoja wetu kujaa neema katika jina la Yesu Kristo amen
7. “Ujazwe wema” Be
filled with goodness.
Warumi 15:14. “Ndugu
zangu, nimehakikishwa mimi mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi MMEJAA
WEMA, mmejazwa elimu yote, tena mwaweza kuonyana.” Paulo
mtume alikuwa badohajaonana na wakristo waliokuwa Rumi lakini alikuwa amesikia
sifa zao kuwa wamejaa wema , ni muhimu kwa kila mmoja kujiuliza katika maisha
yake kuwa amejaa nini? Watu wanasema nini kukuhusu, je wewe ni mwema? Mtumishi
wa Mungu Tito na mwenzake walikuwa watu
wema na sifa zao zilienea makanisani na
sehemu mbalimbali Munhgu anataka tujae wema wako watu wengine kila unakokwenda
unasikia habari zao aidha njema au mbaya , wengina hata kabla hujawaona
unasikia habari zao, je wewe umejaa wema una sifa za aina gani kila mahali,
wengine wana sifa mbaya, nimewahi kufika
mahali nikasikia watu waliomba yule hata akifa sitalia,yule afadhali afe hiki
ni kiwango kibaya sana cha sifa haiwezekani watu watatu au wane waseme
tunatamani afe Wakristo wanapaswa kuwa na sifa nzuri kila mahali 2Wakoritho 8:16-21 “Lakini ahimidiwe Mungu atiaye bidii ile ile kwa ajili yenu katika moyo
wa Tito. Maana aliyapokea kweli yale maonyo; tena, huku akizidi kuwa na bidii,
alisafiri kwenda kwenu kwa hiari yake mwenyewe. Na pamoja naye tukamtuma ndugu
yule ambaye sifa zake katika Injili zimeenea makanisani mwote. Wala si hivyo
tu, bali alichaguliwa na makanisa asafiri pamoja nasi katika jambo la neema
hii, tunayoitumikia, ili Bwana atukuzwe, ukadhihirike utayari wetu.
Tukijiepusha na neno hili, mtu asije akatulaumu kwa habari ya karama hii
tunayoitumikia; tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu, ila na
mbele ya wanadamu.”
Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuweza
kujawa na mambo haya ya msinhgi saba katika jina la Yesu Kristo
Na Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!