Ni muhimu kufahamu kuwa
kuwahudumia wakimbizi ni mpango wa Mungu!, Leo tutachukua Muda wa kutosha kwa
kina na upana na urefu kuangalia huduma muhimu kwaajili ya wakimbizi Duniani,
Mwaka 2004 pekee karibia watu milioni tatu na nusu walikuwa ni wakimbizi barani
Afrika pekee, ambao walikimbia na kuishi nje ya nchi zao, na wengine zaidi ya
milioni kumi walikuwa ni wakimbizi ndani ya nchi zao, wengi walikuwa hawakimbii
tumatukio ya majanga ya kiasili nlakini walikuwa wanakimbia matatizo ya
kisiasa, ugomvi wa kimadaraka, matatizo ya kidini, ukabila na maswala mengineyo
je neno la Mungu linasema nini kuhusu wakimbizi, kanisa limewahi kutafakari
nini kuhusu wakimbizi? Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu
vifuatavyo:-
·
Neno la
Mungu na wakimbizi
·
Mungu
anawajali wakimbizi
·
Wakimbizi
na mafundisho ya agano jipya
Neno la Mungu na wakimbizi:
Biblia inatambua kuweko kwa watu
ambao wamewahi kukimbia huko na huko mbali na Nchi zao, kaini alikuwa mtu wa
kwanza kufahamu madhara ya ukimbizi Mwanzo
4:12,”Utakapoilima
ardhi haitakupa mazao yake, utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao Duniani”
Neno utakuwa mtoro ni sawa na utakuwa mkimbizi. Yakobo na Familia yake
waliishimaisha ya ukimbizi kutokana na majanga ya njaa nchini kwao Mwanzo 47:3-4, “Farao akawauliza hao nduguze Kazi yenu ni nini?
Wakamwambia Farao, Tumekuja kukaa ugenini katika nchi hii, kwa sababu wanyama
wa watumwa wako hawana malisho, maana njaa ni nzito sana katika nchi ya
kanaani, Basi twakusihi uturuhusu sisi watumwa wako tukae katika nchi ya
gosheni” Yesu pia alikuwa mkimbizi huko Misri kwaajili ya kuokoa
Maisha yake yaliyokuwa yakitafuta na mfalme Herode Mathayo 2:13-14. “Na hao walipokwisha kwenda zao tazama malaika wa Bwana
alimtokea yusufu katika ndoto, akasema
Ondoka umchukue mtoto na mama yake , ukimbilie Misri, ukae huko hata
nikuambie kwa maana Herode anataka amwangamize, Akaondoka akamchukua mtoto na
mama yake usiku akaenda zake Misri” ziko sababu mbalimbali na
mazingira ya aina mbalimbali yanayoweza kusababisha kila mmoja wetu kuwa
mkimbizi kwa namna moja ama nyingine.
Mungu anawajali wakimbizi
Biblia iko wazi kuwa Mungu
anawajali wakimbizi, alionyesha kujalia sana maisha ya Kaini hata pamoja na
kuwa ukimbizi wake ulisababishwa na makosa yake mwenyewe Mwanzo 4:15. Mungu alimwambia Musa katika Torati kuandaa miji ya
makimbilio kwaajili ya wakimbizi watakaokimbilia kutokana na sababu mbalimbali
ama ambao watu wangelikuwa wanatafuta kuwaua, Kutoka 21:12-14, Hesabu 35:9-34,
Mstari 10-13 inasema hivi “Nena na wana wa
Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani,Ndipo
mtajiwekea miji iwe miji ya makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua
mtu, pasipo kukusudia kumwua, apate kukimbilia huko.Na hiyo miji itakuwa kwenu
kuwa makimbilio, kumkimbia mwenye kutwaa kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu,
hata atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe. Na hiyo miji mtakayowapa itakuwa
kwenu ni miji sita ya makimbilio”. Kumbukumbu 4:41-43, 19:3-13, Nyakati 6:42-55.
Mungu aliagiza pia kuwa wageni walioambatana na Israel pia wanahitaji
kuheshimiwa kimsingi tunapaswa kuwajali aina zote za wakimbizi waliokimbia nchi
zao kwa sababu zozote zile ziwe za kisiasa, vita uchumi njaa na ugumu mwingine wote wanapaswa kuheshimiwa
kuhifadhiwa kutunzwa vizuri, kupendwa na kuhifadhiwa,kwa heshima na usawa sawa
na raia wengine tukiwahesabu kuwa ni ndugu na jamaa zetu Walawi 25, Isaya 16:1-4, Ezekiel 47:21-23 Lawi 19:33-34. Isaya 16: 3-4
inasema “Lete shauri; kata neno; fanya kivuli chako
kuwa kama usiku kati ya mchana; wafiche waliofukuzwa; usiwachongee waliopotea. Watu
wangu waliofukuzwa waache wakae pamoja nawe; katika habari za Moabu, uwe sitara
kwake mbele ya uso wake anayeharibu; maana yeye atozaye kwa nguvu amekoma;
afanyaye ukiwa ametoweka; waliokanyaga watu wametoka katika nchi.”
Wakimbizi na mafundisho ya agano jipya
Agano jipya linasisitiza sana
kuwahudumia wageni kuwapenda na kuwajali wenye mateso na masikini Mathayo 25:35-40, “kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu,
mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa
mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki
watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au
una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u
uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia,
kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea
mimi”. tofauti ya ndugu na wakimbizi iliondolewa kabisa katika agano
jipya Yohana 13:34 kutokana na umoja
wa waamini Yohana 17:20-23 na
kutokana na udugu na wote kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo.
Hivyo ni muhimu kwa kanisa
kujihusisha na kuwahudumia wakimbizi punde linapotokea swala la wakimbizi na
kukutana na mahitaji yao ya muhimu haraka , kama usalama, upendo, chakula
mavazi, malazi, maji safi,madawa, Kumbuka kuwa Yesu atakuja kubagua Kondoo na
mbuzi kwa misingi ya namna tunavyowajudumia wengine au wenye uhitaji Mathayo 25:31-46, bila huduma hizi ni
vigumu kwa wakimbizi kuikubali injili, wanyarwanda wana usemi usemao “Inda irimo ubusa ntigira amatwi” yaani
tumbo tupu halina masikio, Ni muhimu kanisa likakumbuka hilo likakumbuka
kuwahubiri injili lakini pia kusikiliza injili kutoka kwao ikiwa wanauwezo wa
kuhudumu ili kuwalea na kukuza huduma zao punde warudipo au kuwa wamisionari
katika taifa letu, hivi ndivyo nyakati za kanisa la kwanza walivyofanya pia Matendo 8;1-4, 18:1-2, Hali hii itainua
heshima yao na kuwatia moyo, kanisa pia linapaswa kufanya kitu cha ziada sio tu
kuwaletea maji katika birika bali kuwaelekeza namna wanavyoweza kuchimba visima
wenyewe ili kujipatia maji, kanisa linapaswa pia kujihusisha katika swala zima
la kuangalia chanzo cha ukimbizi na kukishughulikia hii ina maana kuwa kanisa
linapaswa kujishughulisha na swala la kufanya upatanisho na kutafuta majibu ya
matatizo ili kuyatatua na watu waweze kurejea katika nchi zao kwa amani badala
ya kuiacha kazi hiiikafanywa na serikali zaidi, Kanisa ni lazima lisimamie
demokrasia, Haki, upatanisho na mswala ya uongozi kwa ujumla, unaweza kufikiri
kuwa kazi hii ni ya kiserikali zaidi nay a kijamii zaidi kuliko ya kiroho,
lakini nataka nikuambie kuwa ni ya Kiroho zaidi na inapaswa kanisa kuwa
sambamba na mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na
huduma kwa wakimbizi
Ni muhimu kuwahudumia vema
wakimbizi wao pia ni binadamu, kuna historia za kutisha kuwa sehemu nyingine
wakimbizi wanabakwa, wanakataliwa, wanawekewa uzio, au wanafanyiwa hila
wafe,n.k. hivi karibuni katika nchi ya Syria kutokana na vita kumekuwa na
wakimbizi wengi wanaokimbilia ulaya na wengine wanapitia Libiya lakini wengi
wamefanyiwa hila wakikimbia kuokoa maisha yao wengine wameuawa na mataifa
mengine yameingia hofu ya kuwapokea Mungu isaidie Dunia kuwa mahali panapofaa
kukaa ni wajibu wetu kupiga vita kila kinachosababisha watu kukimbia nchi zao
na kujaribu kutatua migogoro iliyoko Duniani ili kila Nchi ipate Ustawi
unaokusudiwa na Mungu.
Yeye aliye na sikio na alisikie
neno hili ambalo Roho aliambia kanisa.
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima