Jumanne, 14 Mei 2024

Mimi ndimi BWANA nikuponyaye !


Kutoka 15:25-26 “Naye akamlilia BWANA; BWANA akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko; akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye.”


 


 

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa uponyaji wa kimungu ni mojawapo ya sehemu muhimu sana ya Injili, Haiwezekani kwa namna yoyote ile ukamuhubiri Yesu Kristo ukaacha huduma ya uponyaji, Huduma ya uponyaji tangu zamani ilikuwa ni sehemu muhimu sana ya kazi ya uungu, Maandiko yamejaa ahadi nyingi sana za Mungu kuhusu uponyaji, kile kifurushi cha wokovu wa mwanadamu na ukombozi wa mwanadamu kinakwenda sambamba na uponyaji wa mwili nafsi na roho, na kwa sababu hiyo uponyaji ni haki ya kila mwanadamu anayehitaji msaada kutoka kwa Mungu kwaajili ya changamoto anayokutana nayo:-

Zaburi 103:2-5 “Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema, Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai;”

Mathayo 4:23-24 “Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu. Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya.”

Kama huduma ya uponyaji ingekuwa haina maana na si ya Muhimu kwa vyovyote vile mwana wa Adamu Yesu Kristo asingejishughulisha na kazi ya kuhubiri habari njema na kufungua watu, Moja ya sababu kubwa ya Mungu kuwapaka mafuta watumishi wake ni ili pia wawasaidie watu kutoka katika udhaifu vifungo na magonjwa ya aina zote, kwa sababu hiyo watu wote ni lazima wakumbuke kuwa Mungu anaponya, na yeye yuko tayari kufanya hivyo na anawapaka mafuta watumishi wake ili pamoja na mambo mengine wafanye kazi ya kuwafungua watu kutoka katika changamoto zao.

Luka 4:17-19 “Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye

Leo tutachukua muda kwa msingi huo kujikumbusha tena msingi wa uponyaji wa kiungu na umuhimu wa huduma za uponyaji na jinsi ya kuhakikishakuwa uponyaji inakuwa ni sehemu ya huduma ya maisha yetu ya kila siku, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

·         Umuhimu wa huduma ya uponyaji.

·         Vizuizi vya nguvu za uponyaji.

·         Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.

 

 

Umuhimu wa Huduma ya Uponyaji:

Wokovu wa mwanadamu na ukombozi wake unahusisha mwili nafsi na roho, na Mungu yuko tayari kuwasaidia wanadamu wote katika changamoto zao ikiwa ni pamoja na kuwaponya magonjwa yao, Mungu anataka tuwe na mafanikio yote ya kimwili na kiroho, na ndio maana unaweza kuona kuwa katika huduma ya Kimasihi ya Yesu Kristo hakupuuzia uponyaji, Yesu aliwaponya wagonjwa wote wenye changamoto za kila aina.

Mathayo 8:14-17 “Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa. Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.”            

Kristo Yesu alilipa kanisa au wanafunzi wake mamlaka hii ya kuhubiri injili, kufundisha lakini alijumuisha pia huduma ya kutoa pepo na kuponya magonjwa yote, maandiko yanaonyesha kuwa mojawapo ya ishara ya kuwa tunamuamini Yesu, ni pamoja na kuombea wagonjwa na kuwa nao watapata afya, kwa hiyo ikiwa tunamfuata Yesu ambaye ametupa kielelezo, kwa sababu zozote zile hatuwezi kupuuzia moja kwa moja huduma za uponyaji.

Mathayo 10:1, 7-8 “Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina., 7-8. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.”

Marko 6:7,13 “Akawaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; 13 Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.”

Luka 10:9 “waponyeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia.” Marko 16:17-18 “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

Kwa nini Yesu aliweka agizo la kuhubiri injili pamoja na kazi ya uponyaji kwa kanisa na kuagiza wanafunzi na kanisa kuifanya kazi hii ikiwa ni pamoja na kuihubiri injili? Hii ni kwa sababu Yesu anajua kuwa magonjwa na madhaifu yanawasumbua wanadamu na kuwa magonjwa na udhaifu wa kila aina ni kazi ya shetani, Magonjwa ni moja ya silaha ya ibilisi kuwanyima wanadamu furaha na kuwatesa na kuwaonea, maandiko yanathibitisha kuwa kila aina ya magonjwa na uonevu wowote wa kiafya ni kazi ya shetani. Na Yesu alidhihirishwa ili azivunje kazi za ibilisi.

Luka 13:11-16 “ Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu. Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. Lakini Bwana akajibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng'ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha? Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato?”

 Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye

1Yohana 3:8 “atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.”

Kanisa linapaswa kuwa mstari wa mbele katika kukemea na kukataa uonevu sio tu katika jamii lakini vile vile katika miili ya wanadamu wanaoonewa na ibilisi, tangu nyakati za agano la kale Mungu alikuwa akijihusisha na uponyaji wa watu wake, na katika nyakati za agano jipya huduma za uponyaji ni muhimu sana, na zinaendelea, wote tunajua ya kuwa Yesu Kristo ni yeye yule jana leo na hata milele na hivyo huduma hii inaendelea, kazi ya ukombozi wa mwanadamu pale msalabani ilihusisha sio dhambi zetu tu bali na magonjwa ambapo Yesu aliposulubiwa pia alikuwa akihusika na kuharibu nguvu za magonjwa, alidhihirishwa ili azivinje kazi za ibilisi.

Isaya 53:4-5 “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”

Mathayo 8:16-17 “Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.”

Kwa hiyo neno la Mungu linaonyesha wazi kuwa uponyaji ni sehemu ya mapenzi kamili ya Mungu, Mungu aliponya katika wakati wa agano la kale na aliahidi kuwaponya watu wake, akijiweka wazi kuwa yeye ni Bwana aponyaye, Yesu ni udhihirisho wa Mungu ulio wazi, alipokuwa duniani alikuwa akifunua tabia ya uungu, na kutuonyesha mapenzi ya Mungu baba, na hivyo yeye mwenyewe aliponya, na sio hivyo tu aliagiza wanafunzi wake kuponya, na sio hivyo tu alitoa na vipawa na karama za uponyaji na matendo ya miujiza kwa kanisa hii maana yake ni nini? Mbingu zinaona kuwa uponyaji ni swala la Muhimu, kanisa likipuuzia huduma hii maana yake litakuwa limempa nafasi na kibali shetani kuendelea kuwaonea watu, Agizo la Kristo linatufundisha kuwa ni mapenzi ya Mungu kwa kila mtu kuponywa, Mfano wa Yesu Kristo unatukumbusha kuwa huduma ya uponyaji ni sehemu muhimu ya injili, na kuteseka kwake msalabani kunaonyesha umuhimu wa uponyaji wa mwanadamu, katika nafsi, mwili na roho, kwa kupigwa kwake!  Sisi tumeponywa ! kwa msingi huo kila mtumishi wa Mungu anapaswa kujikumbusha kuwa huduma ya uponyaji ni sehemu ya kazi tuliyopewa au kuitiwa na Mungu, ni sehemu ya agizo kuu, na ni wazi kuwa tunamuamini Mungu aponyaye na ambaye yuko tayari kuwaponya watu wake hata sasa!  Katika mahitaji yao yote, kimwili, kiroho, nafsi na uchumi.

Vizuizi vya nguvu za uponyaji

Ni muhimu kufahamu na kukumbuka kuwa ni mapenzi ya Mungu kuwaponya watu wake, na kuwa Mungu yuko tayari kuponya, lakini huduma hii ya uponyaji ina vizuizi kadhaa ambavyo ni muhimu kushughulika navyo ili kanisa liweze kuwa makini na kujiepusha navyo, aidha shetani pia anaweza kupingana na huduma za aina hii kwa sababu hataki watu wafunguliwe na kwa sababu hiyo anaweza kutumia fahamu zetu zilizopotoka kuhakikisha kuwa hatukumbuki kutoka kipaumbele kwa huduma za uponyaji, hata hivyo ninapokazia swala zima la umuhimu wa huduma hii, ni muhimu kujikumbusha kuwa agizo la Mungu ni pana sana na watumishi wa Mungu wanapaswa kutoa MLO KAMILI yaani “balance diet” tunapoifanya kazi hii ya Mungu, yaani tuwe na kiasi katika kuwahudumia watu, tuwahudumie kiakili, kimwili na kiroho. Tuwafundishe neno, tuhudumie miili yao kwa huduma za kiponyaji, na sio vema kuelemea upande mmoja, kwa hiyo huduma zetu zinahitaji mzani, kufundisha, kuhubiri, kutia moyo, kushauri, kutembelea na huduma za maombezi na uponyaji.  Kwa hiyo mpangilio wako wa ibada katika kanisa lako ni wa muhimu, unaweza kuitumia siku ya maombi na maombezi kwa kazi za uponyaji, na unaweza kuitumia siku ya mafundisho kufundisha watu Biblia yaani neno la Mungu na unaweza kuitumia siku nyingine kwa kuimarisha watu, kumbuka mitume walifundisha, waliomba, walifanya miujiza na walifundisha watu neno la Mungu na kuhubiri, huduma yako isielemee upande mmoja kwa sababu vyote vinahitajika kwa kusudi la kuwajenga watu, usifanye huduma ya maombezi tu ukaaacha kuwaelekeza watu kwa Yesu, na kuwafunza. Sasa basi vizuizi vya uponyaji ni vipi?

1.       Kutokuamini - kumekuwepo na sababu nyingi sana zinaoainishwa kwa nini watu wengine hawaponywi, lakini mojawapo ya sababu kubwa ni KUTOKUAMINI  Kutokuamini pia kunahusika katika hali ya kutokujibiwa maombi, tatizo la kutokuamini linaweza kuwa kwa pande mbili anayekuombea na anayeombewa,  Ni mapenzi ya Mungu watu kuponywa kwa sababu hiyo kila anaemwendea Mungu kwaajili ya uponyaji ni lazima awe na Imani aaamini kuwa Mungu yuko na yuko tayari kuponya na ataponya bila kutia shaka!

 

Yakobo 1:6-8 “Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana. Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote.”  

 

Watu wanaotoa huduma ya maombezi na watu wanaoombewa wanapaswa kuwa na imani ya kuwa ni mapenzi ya Mungu kamili kwamba watu waponywe, na tunapoomba jambo lolote kwa imani yaani kuliamini Neno la Mungu na kuwa na uhakikika kuwa uponyaji ni sehemu ya haki yetu na ni sehemu ya mapenzi ya Mungu na kuwa Mungu anataka kutuponya ufahamu huo pekee ni Imani tosha kuwa Mungu anaweza kutusaidia na hivyo ataleta uponyaji wake, lakini tukiwa na shaka, tunajiwekea kizuizi cha kupokea kutoka kwa Bwana.

 

Marko 9:23-24 23. “Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye. Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu.”

 

Mathayo 17:19-20 “Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.”

 

2.       Kutokusamehe – Wakati mwingine ni muhimu kuwafundisha kwanza wale wanaohitaji maombezi umuhimu wa kusamehe, au umuhimu wa kutubu dhambi zetu,  kama iko dhambi haijatubiwa au uko moyo ambao una uchungu kiroho, uchungu na kutokusamehe kunamuweka mtu gerezani na kunampa shetani haki ya kuendelea kukutesa na magonjwa yako!

 

Yohana 5:11-15 “Akawajibu, Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, Jitwike godoro lako, uende. Basi wakamwuliza, Yule aliyekuambia, Jitwike, uende, ni nani? Lakini yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; maana Yesu alikuwa amejitenga, kwa sababu palikuwa na watu wengi mahali pale. Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi. Yule mtu akaenda zake, akawapasha habari Wayahudi ya kwamba ni Yesu aliyemfanya kuwa mzima.”

 

Yakobo 5:15-16 “Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.”

 

Marko 11:24-25 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.”

 

Watu wengi sana wanatafuta uponyaji, na uponyaji ni kwaajili ya wanadamu wote, lakini tunapomjia Mungu kwa uponyaji tunapaswa kuachilia, tunapaswa kuwasamehe waliotukosea ili Mungu aweze kuturehemu, maombi yetu hayapaswi kuwa na mtu tuliyemfungia moyoni, hayapaswi kuwa na mtu ambaye tuna kinyongo naye, lazima tuhakikishwe kuwa tuko huru kabisa kutoka kwenye uchungu na wanadamu wenzetu, tafadhali sana kusamehe ni kwaajili ya afya zetu, tusiposamehe sisi tunajiumiza wenyewe.  Na kujiacha kwenye gereza la mateso ona :-

 

Mathayo 18:21-35 “Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia.  Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.”

 

Katika mfano huo hapo juu unaohusiana na kusamehe, sehemu ya mwisho inaonyesha kuwa yile mtumwa aliyeshindwa kusamehe, Bwana wake aliamuru kuwa apelekwe kwa watesaji, hata atakapolipa deni ya mwisho maana yake hata atakapoweza kusamehe, au hata atakapoweza kuachilia ndipo na yeye anaweza kuachiliwa, katika maswala ya uponyaji ni wazi kuwa watu wenye uchungu na wanadamu wengine na wasiosamehe hawawezi kupokea kitu kutoka kwa Mungu isipokuwa mpaka wamesamehe kwanza. Na hiyo ni kanuni ya Mungu mwenyewe!

 

3.       Kutokutii – Wale wanaofanya huduma za maombezi watakubaliana nami kuwa Roho Mtakatifu huwa anatoa miongozo mbalimbali jinsi na namna ya kuwahudumia watu, huduma za maombezi huwa hazina aina moja ya kanuni, tangu zamani tunaona kuwa Mungu aliponya watu wake kwa jinsi na namna mbalimbali kwa kupitia jina lake, wakati mwingine ili Mungu amponye mtu inahitajika utii tu na kukubali kunyenyekea basi.

 

2Wafalme 5:1-3, 8-14 “1-3 Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake. 8-14 “Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli. Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi. Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la Bwana, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma. Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira. Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.”

 

Luka 17:11-14 “Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya. Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.”

 

Yohana 9:6-11 “Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho, akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona. Basi jirani zake, na wale waliomwona zamani kuwa ni mwombaji, wakasema, Je! Huyu siye yule aliyekuwa akiketi na kuomba? Wengine wakasema, Ndiye. Wengine wakasema, La, lakini amefanana naye. Yeye mwenyewe alisema, Mimi ndiye. Basi wakamwambia, Macho yako yalifumbuliwaje? Yeye akajibu, Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka macho akaniambia, Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona.”

 

Katika vifungu hivyo utaweza kuona kuwa uponyaji unajitokeza kwa sababu ya maagizo, walioponywa wote waliagizwa kitu cha kufanya, mmoja aliambiwa akajichovye Jordani mara saba na mwingine alipakwa tope akaagizwa akanawe katika kisima kiitwacho Siloamu na wakoma waliagizwa wakajionyeshe kwa makuhani, Kwa hiyo Mungu anachotaka kukiona ni utii tu na kupitia utii wako analeta uponyaji, kwa hiyo wakati wa huduma ya uponyaji Muhudumu sikiliza maelekezo ya Roho Mtakatifu na muhudumiwa fuata maelekezo unayopewa na anayekuhudumia kwa utii wako unapokea uponyaji. Maana yake ni nini kutokutii au kufuata maelekezo wakati mwingine kunaweza kutunyima uponyaji. Kumbuka neno lile

 

…..Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye

 

4.       Ndoa yenye mafarakano - wako wanandoa ambao ugomvi kwao ni swala la kawaida sana wanagombana mno, Mafarakano ni moja ya silaha muhimu sana anayoitumia shetani kuharibu ndoa, taasisi na kanisa, shetani anapotaka kupigana na huduma iliyoko ndani yako anaanzia kwenye ndoa, anatingisha kwenye ndoa lakini sio hivyo tu akitaka kukunyima miujiza, na uponyaji mafarakano ni moja ya njia anayoitumia shetani kuondoa Baraka na kukunyima kujibiwa maombi.

 

1Peter 3:6-7 “Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote. Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.”

 

Wanandoa wengine pia wanatumia tendo la ndoa kama njia ya kuadhibiana na kutesana, kunyimana tendo la ndoa kunaweza kukuletea balaa za kimwili na kiroho na kufungua mlango wa shetani kupata nafasi na kuharibu taasisi ya ndoa na familia  na kusababisha shetani apate mlango wa kupenyeza mambo yake yakiwepo magonjwa, lakini sio hivyo tu kukufunga na kukunyima uponyaji, kunyimana tendo la ndoa ni dhambi kwa sababu ni kinyume na maagizo ya Mungu, pia kunavunja umoja ambao Mungu aliukusudia kwa wana ndoa na kunatoa mlango mpana sana wa kusababisha majanga makubwa, ikiwa Yesu alisema ole wake mtu yule asababishae makwazo, ni afadhali afungiwe jiwe kubwa shingoni na kutoshwa baharini, maana yake kukoseshana kunakotokea kupitia tendo la Ndoa kunaleta madhara yanayofanana na mauti, kubwa zaidi kunazuia uponyaji kwa muhitaji wa maombezi.

 

1Wakorintho 7:3-5. “Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.”    

 

 

5.       Kushiriki meza ya Bwana isivyostahili -  watu wafundishwe vizuri kuhusu meza ya Bwana na uwepo wa Mungu unaokuwepo kwenye meza ya Bwana, meza ya Bwana ni mojawapo ya njia ya uponyaji, lakini watu wakishiriki meza ya bwana bila kutubu dhambi, au bila kuipa heshima inayostahili meza hiyo inaweza kusababisha magonjwa na magonjwa hayo yakawa hayawezi kupona kwa maombezi wala njia nyinginezo

 

1Wakorintho 11:27-30 “Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala.”          

 

6.       Kutokuomba – Yakobo 4:2 “Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!

 

Kanuni ya kimaandiko inatutaka tuombe, kila kitu tunachokihitaji, katika ulimwengu wa kiroho kinapatikana kwa kuomba kwa hiyo katika huduma za uponyaji muhudumu anapaswa kuwa na muda wa kuomba, omba karama za uponyaji, omba Mungu ajidhihirishe, omba Mungu alithibitishe neno lake kwa ishara na maajabu, omba Mungu ishara na miujiza itendeke kwa jina la mtumishi wake Yesu, lakini vile vile wanaoombewa wapate muda wa kuomba, kumbuka Yesu aliwauliza watu aliowahudumia wakati mwingine wataka nikufanyie nini, kwa hiyo muombewaji ana haki ya kuomba hata kwa ufupi, ili kwamba Mungu aweze kumponya, zamani sana nilisoma kitabu kimoja kiitwacho Edmundi John Mtu wa Mungu, Mtumishi huyu alikuwa ni mshirika wa kanisa la Anglican ambaye Mungu alimtumia sana zamani, inasemekana alikuwa na undugu na Askofu Sepeku wa kanisa la Anglican wakati huo, kiufupi Edmund alikuwa akifanya maombezi siku za ijumaa katika makanisa na alikuwa akifunga siku ya ijumaa na wakati huo huo aliwataka waliokuwa wanataka maombezi pia nao kufunga kwa hiyo yeye aliomba kwaajili ya uponyaji na waombewaji waliomba kwaajili ya kuponywa na ulipofika muda wa maombezi, Mungu alifanya miujiza Mikubwa sana na watu waliponywa sana, kwa hiyo maombi ni nyenzo Muhimu sana kwaajili ya huduma za uponyaji, hamna kitu kwa sababu hamuombi!

 

Matendo 4:29-31 “Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.”

 

7.       Kuwepo kwa nyenzo za utendaji wa ibilisi – ufunguliwaji wa uponyaji wa aina mbalimbali hauko mbali sana na ufunguliwaji wa changamoto za kipepo, kuna uhusiano Fulani wa uwepo wa ugonjwa na pepo kuna wakati ugonjwa Fulani unaweza kuwepo kama dalili ya kuwepo kwa pepo wenye kusababisha aina hiyo hiyo ya ugonjwa kwa mfano

 

Mathayo 22:12 “Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona.”

 

Unaona huyu alikuwa kipofu yaani haoni na pia alikuwa hasemi Sehemu nyingine anaonyeshwa alikuwa bubu na kiziwi pia lakini Mathayo anaonyesha kwamba sababu hizo zilisababishwa na Pepo na Yesu alipolikemea ewe pepo bubu na kiziwi toka mtu huyu alipokea uponyaji wake wote

 

Marko 9:25-27 “Naye Yesu akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena. Akalia, akamtia kifafa sana, akamtoka; naye akawa kama amekufa; hata wengi wakasema, Amekufa. Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua naye akasimama.”

 

Katika uponyaji wa Mtu huyu Yesu anapolikemea pepo tunaona akiweka na amri wala usimuingie tena, Yesu alikuwa anajua kuwa ni desturi na ni kawaida kuwa pepo wana tabia ya kurudi tena na ndio maana sehemu nyingine Yesu alionya kuwa ili uponyaji wa mtu uweze kuwa kamili, asiruhusu tena nyenyo za utendaji wa shetani, nyenzo hizo Yesu aliziita mapambo na pia dhambi, hivi vikirudiwa tena vinampa haki shetani ya kurudi tena na kusababisha tatizo endelevu au hata kuleta janga baya zaidi

 

Mathayo 12:43-45 “Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate. Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa. Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya.”               

 

Yohana 5:13-14 “Lakini yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; maana Yesu alikuwa amejitenga, kwa sababu palikuwa na watu wengi mahali pale. Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.”

 

Unaona kwa msingi huo ili mtu aweze kupokea uponyaji kamili hana budi kuhakikisha kuwa anaondoa mapambo na kuacha kuifanya dhambi iliyosababisha apatwe na ugonjwa huo mapambo katia kiyunani linatumika neno Kosmeō  kwa kiingereza Decoration ni lugha ya mficho aliyoitumia Yesu ikimaanisha nyenzo za kishetani kama hirizi au vifaa vya kiganga na kichawi ambavyo ulipewa kama njia ya ulinzi, pembe, chungu, hirizi, na kadhalika hivyo vinapaswa kuharibiwa kwaajili ya uponyaji kamili wa kiungu, aidha kabla ya uponyaji au baada vinginevyo utaweza kuona hali ile ya kwanza ikijirudia rudia hii inaweza sana kuwahusu wale waliofunguliwa kutoka kwenye mapepo. Na ndio maana watu wa Efeso walipolipokea neno walichoma vitu vyote walivyokuwa wakivitumiwa kwa uganga na uchawi hata kama vilikuwa na thamani

 

Matendo 19:18-19 “Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.”

 

Kwa hiyo uko umuhimu wa kuharibu kila nyenzo za utendaji wa ibilisi, ili kutokumpa nafasi na kibali cha kurudia vifaa vyake vya kiibada vinavyompa mamlaka ya kukuonea na kukufikia tena na tena, jambo hili linampa Mungu nafasi ya kuifanya kazi kamili ndani ya mwili wako, nafsi yako na roho yako kama mponyaji.

 

8.       Vikwazo vya mitazamo ya Kitheolojia - Mungu yuko tayari kuwaponya watu wake na ni mapenzi yake kamili kuponya, na Mungu hana upendeleo yeye anajiita mimi ndimi Bwana nikuponyaye maana yake yeye ni mponyaji, JEHOVAH RAPHA, watu wanaumwa na Mungu anataka kuwaponya wote, Mungu hana upendeleo hawezi kumponya huyu kisha akamuacha huyu, kama tumezingatia ukweli kuhusu neno lake na matakwa yake yote ya uponyaji kwanini asikuponye?  Lakini moja ya changamoto kubwa sana katika huduma za uponyaji utaweza kuona  ni pamoja na vikwazo vya mitazamo ya kitheolojia,  na hasa wanatheolojia waliosoma vyuo vya Biblia, unapofanya utafiti mdogo tu unaweza kugundua watu wengi wanaotumiwa na Mungu katika huduma za uponyaji wengi wao sio wote ni wale ambao labda hawajaenda vyuo vya biblia, Elimu tunazopata zinapaswa kuwa msingi wa kutufungua macho zaidi, na kupanua uwezo wetu wa kuitawala dunia na kufanya huduma zetu katika ubora unaokusudiwa, kwa bahati mbaya sana Elimu nyingi za dunia zinawafunga watu katika boksi na kuwawekea mipaka, kwa hiyo utashangaa mtu anakuja na somo lake KWANINI WENYE HAKI WANATESEKA?  Somo hilo litakupa sababu kadhaa wa kadhaa zinazopelekea kuweko kwa mateso katika maisha ya mwanadamu, ukiangalia kwa makini somo hilo ni kama linataka kutoa uhalali wa watu kuteseka na wakati mwingine kufikiria kuwa labda ni mapenzi ya Mungu mtu ateseke, kwa hiyo kunakuwepo na Labda tatizo hili limetokana na sababu hii au ile labda labda zinakuwa nyingi sana, na ndio maana leo hii Dunia imekuwa na magonjwa mengi sana, na watu wanateseka sana na nguvu za uponyaji katika makanisa mengi zimepungua, na watu wanakabiliwa na changamoto nyingi na za aina mbalimbali,  pamoja na maendeleo makubwa ya kisayansi katika tiba ya afya, bado watu wanateseka na sasa makanisani tunashuhudia magonjwa makubwa sana na ya kutisha sasa yako kwa washirika na wachungaji, sasa maelefu ya washirika na wakristo wanaumwa, siku hizi sio ajabu kusikia, kansa, figo, sukari, presha, migandamizo ya mawazo, moyo,  na michangamoto kibao iko makanisani, sababu kubwa ni misimamo ya kitheolojia waliyo nayo watumishi wengi wa Mungu, watu wanaweza kuja na neno la kukutia moyo tu  na kukuhurumia,  na wakati mwingine wakisema ugonjwa huu au tatizo hili ni mapenzi ya Mungu, na wengine utasikia hakuna sababu ya kujiuliza kwa nini?, hii ni mpango wa Mungu  na wengine utasikia ugonjwa huu ni mwiba, au inawezekana ni Mungu anakunyenyekesha ili uwe karibu naye kwa hiyo Mungu anaruhusu eti atulete karibu kupitia magonjwa na matatizo yaliyosababishwa na wanadamu, Mungu asingejiita yeye ni Bwana mponyaji kama asingelikuwa na mpango wa kutuponya, mojawapo ya sehemu ya Mungu kuonyesha upendo wake kwetu ni pamoja na uponyaji, kwa hiyo mojawapo ya sababu kubwa sana wakristo kuteswa na magonjwa leo inachangiwa na elimu zetu kuhusu Mungu, kama tukimuamini Mungu, na kukumbuka ya kuwa aliahidi uponyaji na kuwa yeye si mtu hata aseme uongo uponyaji wa wagonjwa itakuwa ni kama kupumua tu

 

 Zaburi 103:3 “Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote,” Hesabu 23:19 “Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?

 

Waebrania 6:16-18 “Maana wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao; na kwao ukomo wa mashindano yote ya maneno ni kiapo, kwa kuyathibitisha. Katika neno hilo Mungu, akitaka kuwaonyesha zaidi sana warithio ile ahadi, jinsi mashauri yake yasivyoweza kubadilika, alitia kiapo katikati; ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo MUNGU HAWEZI KUSEMA UONGO, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu;”

 

Isaya 55:10-11 “Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”                 

 

Yeremia 1:11-12 “Tena neno la Bwana likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, Naona ufito wa mlozi. Ndipo Bwana akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize.”

 

Maswala ya uponyaji yako kwenye ahadi za Mungu kwetu, na kwa sababu hiyo yeye hawezi tu kututia moyo kwenye neno lake kuhusu uponyaji kisha asifanye, kwa hiyo ni lazima kwetu kuweka uwiano mzuriwa elimu zetu za kitheolojia katika kuamini uponyaji wa kiungu, na tusiuchepushe kwa namna yoyote Mungu ni mponyaji na ameahidi katika neno lake na hawezi kusema uongo!    

 

Wanatheolojia wengine wanaamini kuwa Maswala yote ya uponyaji wa kimiujiza yalikuwa zamani, nyakati za mitume tu na kuwa siku hizi Mungu hashughuliki tena na uponyaji wa kimiujiza kwa hiyo makanisa yao yana waamini ambao kwa miaka mingi sana wamekosa kuona Mungu akishughulika na uponyaji wa kimiujiza,inasikitisha sana kuona kuna ujinga mwingi sana wengine wanasoma hata maandiko yakionyesha kuwa Paulo mtume aliacha Ndugu mmoja ambaye alikuwa anaumwa, wanaamini hata Paulo mwenyewe alikuwa na tatizo ambalo Mungu hakumponya mwenyewe alilita mwiba wake ambao unasadikiwa kuwa yalikuwa macho mabovu, vyovyote iwavyo kumbuka Paulo mtume alijibiwa maombi yake Mungu alisema naye kuwa anaweza kumtumia kwa neema yake bila kujali udhaifu aliokuwa nao ambao aliomba aponywe, lakini hii haimaanishi hata kidogo kuwa Mungu haponyi, na wewe sio Paulo Mtume yeye alipewa mwiba huo kusudi asijivune kwa sababu ya mafunuo makubwa sana aliyopewa ambayo wewe na mimi hatuna !

 

2Timotheo 4:20 “Erasto alikaa Korintho. Trofimo nalimwacha huko Mileto, hawezi.”

 

2Wakorintho 12:7-9 “Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.”               

 

Wagalatia 4:13-15 “Lakini mwajua ya kuwa naliwahubiri Injili mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili; na jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu. Ku wapi, basi, kule kujiita heri? Maana nawashuhudu kwamba, kama ingaliwezekana, mngaling'oa macho yenu, mkanipa mimi.”        

 

Kwa hiyo ujuzi wetu wa kiungu (Theolojia) ina nafasi kubwa sana katika utendaji wa huduma za uponyaji, kutokana na mitazamo mbalimbali ya kitheolojia wako watu wanafaidika na uponyaji katika makanisa yao na wako watu wasiofaidika na uponyaji katika makanisa yao kwanini ni kutokana na jinsi mtu anavyomuwekea Mungu mipaka,  na athari za namna anavyoamini na namna anavyojaribu kulitendea kazi neno la Mungu au kile alichokisikia au kuaminishwa, kama Imani yetu inasadiki katika swala la uponyaji wa kimungu basi kumbuka ya kuwa Mungu anaponya hata sasa, na tuache woga wa kuombea wagonjwa, nimefanya utafiti katika makanisa mengi sana siku hizi kuna janja janja nyingi sana katika maombezi, watu wamepoteza ujasiri  wa kufanya maombezi kwa waamini na hii ndio inasababisha watu wasafiri kwenda mbali kutafuta uponyaji wa kiungu mbali sana badala ya kupata msaada wa karibu kutoka kwa kwa watumishi wa Mungu walioko karibu katika miji yao, kumbuka hapo ulipo Mungu amekuweka ili watu watafute msaada kutoka hapo karibu na sio wasafiri mpaka mbali.

 

Mimi ndimi Bwana nikuponyaye

Kutoka 15:25-26 “Naye akamlilia BWANA; BWANA akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko; akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye.”

Mimi Ndimi Bwana nikuponyaye! Mungu anapojitambulisha kama mponyaji kwa wana wa Israel, anajifunua kwetu pia watu wa mataifa kuwa yeye ni Mponyaji wa ulimwengu mzima na mponyaji wa kila mtu, Yesu alipokuja duniani alikuja kufanya mapenzi ya baba yake, kwa sababu hiyo alipokuwa akiponya pia alikuwa akifanya mapenzi ya Mungu, kwa sababu kila kitu alichokifanya alikuwa ameandikiwa kukifanya, kwa hiyo uponyaji ni mapenzi ya Mungu kamili.

Waebrania 10:5-7 “Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu.”

Sisi nasi tunapaswa kufanya vile vile kama Yesu alivyofanya, na Kristo aliahidi kuwa kazi alizozifanya sisi tutafanya naam na kubwa kuliko hizo alizozifanya

Yohana 14:12-13 “Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.”

Kwa hiyo uponyaji ni mapenzi  kamili ya Mungu, Mungu anataka kutuponya,  wako watu wengine wanaofikiria kuwa labda huenda Mungu hataki kuwaponya, hii ni kwa sababu tu ya moyo wa kukata tamaa, mkoma mmoja alimjia Yesu akiwa na ukoma wake, alifikiri ni mapenzi ya Mungu yeye kuwa na ukoma, kwa sababu ukoma ulionekana kama ni pigo kutoka kwa Mungu, hawakuwa wanajua kuwa mateso na magonjwa ni kazi ya shetani, Mungu katika wema wake na upendo wake mkuu hawezi kutuadhibu kwa magonjwa kwa hiyo katika Kuomba kwake aliomba kama ukitaka waweza kunitakasa na Yesu alipojibu kuwa nataka takasika, alikuwa akionyesha kuwa anataka uponyaji na uzima kwa  wote.  Je Mungu anataka kukuponya? Jibu ni ndio Mungu anataka kukuponya amini katika uponyaji wake

Marko 1:40-42 “Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.”

Kwa hiyo swala la uponyaji sio Mungu akitaka, hapana Mungu anataka ni mapenzi yake kumponya kila mtu, lakini katika shughuli za uponyaji Mungu hutumia njia mbalimbali katika uponyaji kwa jina lake hizi nazo ni muhimu kuzijua

1.       Uponyaji kupitia neno la Mungu - njia mojawapo ya kuleta uponyaji ni kupitia neno la Mungu, Neno la Mungu huwa linaambatana na nguvu za uponyaji, Mungu anasema ya kuwa neno lake halitamrudia bure na kuwa litatimiza mapenzi yake, kwa hiyo Mungu hulitumia neno lake kusababisha uponyaji na kuwaondoa watu kutika katika maangamizo. 

 

Isaya 55:10-11 “Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”

 

Zaburi 107:19-20 “Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.”

 

Uponyaji wa kutumia neno la Mungu unafanyika kupitia ibada maalumu za maombezi, katika ibada hiyo, ambayo inaweza kutanguliwa na sifa na kuabudu, kisha linakuja neno la Mungu, neno hilo linakusudia kuelezea jinsi Mungu anavyowaponya watu wake, litaonyesha nguvu za Mungu za uponyaji, na jinsi alivyoponya watu mbalimbali, kwa hiyo wakati llikizungumzwa katika upako na uwepo wa Roho Mtakatifu Imani za watu zitapanda kwa sababu Imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo Imani ya watu itapanda na watu watakuwa tayari kupokea uponyaji na miujiza yao wakati wa maombezi.

 

Warumi 10:10,17 “Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. 17 Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.”

 

Matendo 14:8-10 “Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa. Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda.”

 

Neno la Mungu linapohubiriwa katika mamlaka ya kutia moyo na kuinua Imani kwaajili ya uponyaji linapandisha Imani ya wasikiaji na hivyo kusababisha uponyaji, kwa hiyo baada ya neno la Mungu mtumishi anaweza kualika watu mbele au kupita akiwasaidia na kuwaombea watu na utaweza kuona wakifunguliwa, huduma ya uponyaji inakwenda sambamba na kufukuza pepo wenye kusababisha udhaifu wa namna mbalimbali.

 

2.       Uponyaji kwa kuwekea mikono – Kuwekea mikono wagonjwa ni moja ya sehemu ya njia ya kufanya maombezi kwa wagonjwa na wakaweza kupokea uponyaji wao, njia hii ni ya kimaandiko na ilifanywa na Kristo mwenyewe na imeahidiwa kwa waamini wote.

 

Luka 4:40-41 “Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbali mbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya. Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo.”

 

Yesu Kristo aliwaponya wagonjwa wengi sana kwa kuwawekea mikono, kwa msingi huo kuweka mikono ni mojawapo ya njia sahihi ya kupitisha neema ya Mungu kwa watu wake kutoka kwa watumishi wa Mungu, njia hii inakubalika sana kama njia ya upendo kwa sababu unaweka mkono juu ya mgonjwa na kumuombea ukimtamkia afya njema  kwa jina la Yesu. Ni njia inayokubaliwa na wanatheolojia wengi Yesu aliitumia na kisha na yeye pia alituagiza kuitumia, aliamini kuwa waamini wataweka mikono juu ya wagonjwa nao watapata afya

 

Marko 16:17-18 “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

 

Tunapoweka mikono juu ya mtu mwenyye udhaifu na kuanza kumuombea kwaajili ya muhusika tunafanya hivyo tukiamini ya kuwa Roho wa Mungu atapitisha neema yake na kumpa mgonjwa nafasi ya kupona, maombi hayo huambatana na kulitaja jina la Yesu, tendo la uwekaji mikono pia hutumiwa na kanisa kama njia ya Kuruhusu Roho Mtakatifu kupitisha neema yake sio tu ya uponyaji bali ya uongozi na pia kazi na majukumu mbalimbali ya kikanisa

 

Matendo 6:5-6 Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao.”

               

Matendo 8:14-19 “Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohana; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu. Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu.”

 

Matendo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.”

 

Kuwekea mikono sio tu ilikuwa kwaajili ya wagonjwa lakini pia ilikuwa njia ya kuwaombea watu wapokee Roho Mtakatifu, na vile vile kuweka wakfu viongozi, kwa hiyo Mungu kwa vile ni Roho hufanya kazi na wanadamu katika kuipitisha neema yake kupitia mikono wanayoweka juu ya wagonjwa kwa makusudi ya kuleta afya, na vile vile kwaajili ya kuombea neema nyinginezo, kama ujazo wa Roho, hekima, uongozi, busara na kadhalika.

 

3.       Uponyaji kwa njia ya Maombezi – Mungu ndiye mponyaji, uponyaji ni mali yake na unatoka kwake hata hivyo Mungu huweza kuponya kupitia mawakala wake yaani watumishi wake kwa sababu Mungu ni ROHO na hivyo sio rahisi kumuona kwa macho, kwa hiyo kunapotokea changamoto Mungu huwatumia watumishi wake kwaajili ya kuomba au kuombea na kwa mamlaka aliyowapa uponyaji hutokea

 

Mwanzo 20:17-18. “Ibrahimu akamwomba Mungu, Mungu akamponya Abimeleki, na mkewe, na wajakazi wake, nao wakazaa wana. Maana BWANA alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa nyumbani mwa Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Ibrahimu.”

 

Mwanzo 25:21 “Isaka akamwomba BWANA kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye BWANA akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba.”    

 

2Wafalme 20:4-7. “Ikawa, kabla Isaya hajatoka katika mji wa kati, neno la Bwana likamjia, kusema, Rudi, ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wangu, Bwana, Mungu wa Daudi baba yako asema hivi, Nimeyasikia maombi yako, na kuyaona machozi yako; tazama, nitakuponya; siku ya tatu utapanda nyumbani kwa Bwana. Tena, nitazizidisha siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano, nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu. Naye Isaya akasema, Twaeni mkate wa tini. Wakautwaa, wakauweka juu ya jipu, naye akapona.”

 

4.       Uponyaji kwa njia ya Karama za Roho. – Katika kanisa Mungu ametoa karama za aina mbalimbali kwaajili ya kuujenga mwili wa Kristo ziko karama nyingi, Paulo mtume ametaja karama za Roho Mtakatifu kama tisa ambazo huwa tunazigawa katika makundi makuu matatu.

 

·         Karama za Usemi – Aina za lugha, tafasiri za lugha na Unabii

·         Karama za Mafunuo – Neno la hekima, Neno la Maarifa na kupambanua roho

·         Karama za Uweza – Neno la Imani/neno la Mamlaka, Miujiza, na Karama za uponyaji

Kwa kawaida karama zinazohusika katika kuwahudumia watu kwa uponyaji ni karama za uweza yaani Imani, Miujiza na Uponyaji, hizi ni karama zinazowekwa na Roho Mtakatifu kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kuwa na uwezo maalumu wa kuamini katika Mungu na kuomba kwa Imani na kusababisha ukarabati katika mwili (Uponyaji) au miujiza, somo kuhusu karama ni pana lakini  (mimi nataka kuzungumzia kwa ufupi sana za uweza) mtumishi mwenye Karama hizi kwa kawaida anatumiwa na Mungu katika kiwango cha juu na cha tofauti  katika kufanya kazi za kimiujiza na uponyaji, kila mtu aliyeokoka anaweza kuombea mwingine na hata asiyeokoka anaweza kuomba kwaajili ya mgonjwa na Mungu akajibu, hata hivyo mwenye karama anakuwa na umaalumu zaidi katika kutumiwa na Mungu kwa eneo hilo zaidi ya wengine.

1Wakorintho 12:4-11  Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.”

Kwa msingi huo pamoja na kuwepo kwa uponyaji kwa njia ya maombezi, lakini wote tunakubaliana ya kuwa Mungu kwa kutumia karama au watu aliowapa karama za uponyaji anaponya watu wake, karama za Roho Mtakatifu ziko miongoni mwa mwili wa Kristo, watumishi wa Mungu hawana budi kumuomba Mungu awape karama hizi kwaajili ya mahitaji ya watu wetu walioko duniani na makanisani ambao wanahitaji uponyaji.  Karama hizi unaweza kuzitaka na unaweza kupewa kwa kuomba hata hivyo Mungu hutoa karama hizi kama apendavyo yeye Mwenyewe.

1Wakorintho 12:31Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora” 1Wakorintho 12:11 “lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.”

 

5.       Uponyaji kwa njia ya kupaka Mafuta -  Uponyaji kwa njia ya kupaka mafuta umekuwa maarufu sana katika nyakati za leo na kuliacha kanisa likiwa katika vipande viwili, wale wanaopinga uponyaji kwa njia ya kupaka mafuta na wale wanaokubali, Maandiko tangu mwanzo yanaonyesha kuwa uponyaji wa kimungu haujawahi tu kuwa katika mfumo wa aina moja, hata karama za uponyaji, haiitwi karama ya uponyaji inaitwa karama za Uponyaji kwa sababu ya utendaji tofauti tofauti lakini kwa Roho Yeye yule mmoja, Biblia inasema nini kuhusu uponyaji kwa njia ya kupaka mafuta? Hakuna ubaya kutumia mafuta katika kumuombea Mgonjwa, mafuta yanatumika sana lakini Maombi ya Imani ndio njia ya juu zaidi inayoleta uponyaji, Yesu alipowatuma wanafunzi wake katika maagizo yake ya uponyaji aliagiza maswala kadhaa ikiwepo kuombea wagonjwa na kuwapaka mafuta.  

 

Marko 6:12-13 “Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.”

 

Yakobo 5:14-15. “Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.”

 

Ni muhimu kufahamu hata hivyo kuwa njia ya upakaji mafuta ni lazima ihusishe maombi na mafuta haya ni yale yaliyotokana na zeituni, ambayo zamani yalitumika kuweka wakfu viongozi, ili waweze kuwaokoa watu mafuta haya yaliwakilisha uwepo na neema ya Roho Mtakatifu kwaajili ya kuharibu vifungo mbalimbali vya kikoloni na kutoka kwa waonevu, na ndio maana Isaya alitabiri ushindi mkubwa wa Hezekia dhidi ya wababiloni, kwamba kwaajili ya kutiwa kwake mafuta atavunja nira, ile nira inavunjwa na Roho Mtakatifu ambaye aliwakilishwa na mafuta wakati wa agano la kale.

 

Isaya 10:27 “Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.”

 

Yesu alipokuja Duniani yeye ni mpakwa mafuta ndio masihi, hata hivyo yeye hakupakwa mafuta halisi kutoka katika pembe au kichupa bali Mungu alimpaka mafuta yaani alimjaza kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwa msaada kwa watu, kwa hiyo mafuta ni njia ya kupitisha neema ya Mungu sawa tu na kuwekea mikono, hata hivyo Roho wa neema anaweza kushusha neema bila hata ya kuwekea mikono au bila hata ya kupakwa mafuta halisi.

 

Luka 4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

 

Luka 3:21-22 “Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”  

 

kimsingi huduma hii inaweza kufanyika kwa wagonjwa wengine(hapa sio lazima wale ambao wako kitandani) na inafanya kazi tatizo kubwa ni kuwa wale wanaokataa fundisho hili hawajawahi kulitii hata mara moja wanapinga tu kwa sababu wameambukizwa kipinga, au wana mtazamo mdogo katika theolojia zao kuhusu uponyaji kwa njia hii ama na inawezekana wamekosa tu uzoefu au zoezi la kufanyia kazi hili (Exiperimental Theology) kama hii haifanyi kazi jaribu uone paka watu mafuta omba na kukemea kwa jina la Yesu, isipofanya kazi  achana nayo, ikifanya kazi endelea nayo haitakuwa umefanya dhambi Wathesalonike 5:21 “Jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema;iwapo jambo hili halitafanya kazi nimekaa pale niite mzushi na ikifanya kazi tubu na uache kuanzia sasa kuwashutumu wale wanaotumia mafuta katika uponyaji, kibiblia hata kuwekea mikono tu pekee ni sawa na kuweka mafuta kwa sababu Mungu huitumia mikono kupitisha neema yake, lakini wagonjwa wakiwa na imani wanaweza kupokea miujiza yao na uponyaji wao bila kuwekewa mikono wala kupakwa mafuta, Mafuta zamani yalitumika kuweka wakfu viongozi, na Roho wa Mungu alikuja juu yao, Mafuta yanatumika kuwaombea watoto neema, kuweka wakfu makasisi katika makanisa yasiyo ya kipentekoste, pia kuombea wagonjwa ambao hawawezi hata kuinuka  ndio maana unaweza kuona Lugha ya Yakobo Na awaite wazee… Lugha hii awaite wazee akiwa hawezi maana yake inahusu zaidi mgonjwa aliyeteseka mno kitandani, lakini hii haimaanishi kuwa isitumike kwa wagonjwa wengine, kumbuka yakobo pia anasema Mtu wa kwenu amekuwa hawezi, kiingereza Is any sick amongo you? Yaani yeyote ambaye anaumwa miongoni mwenu kwa hiyo kanisa lisitumie nguvu sana kushindana na agizo hili, washirika wako watakuona mjinga pale unapokemea mafuta ili hali wao wamehudumiwa kupitia mafuta na wanaendelea vizuri. Kitu ambacho kanisa linaweza kukemea ni matumizi ya kupita kawaida ya mafuta au sura ya kibiashara kupitia mafuta hayo, lakini kitheolojia ushahidi wa kimaandiko unaonyesha kuwa hakuna shida kuyatumia mafuta katika kuombea wagonjwa kwa sababu mafuta hayo yanapakwa kwa jina la Bwana Yesu na kimaandiko uko ushahidi wa zaidi ya andiko moja,  

 

Mathayo 18:16 “La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike.”

               

2Wakorintho 13:1 “Hii ndiyo mara ya tatu ya mimi kuja kwenu. Kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno litathibitishwa.”

 

1Timotheo 5: 19 “Usikubali mashitaka juu ya mzee, ila kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu.”  

 

Kwa mujibu wa kanuni za kutafasiri maandiko, ni kwamba huwezi kufanya fundisho kwa kupitia jambo ambalo limesemwa katika ushahidi wa mstari mmoja tu au tukio moja tu ambalo halijajirudia mara mbili kwa hiyo kitaalamu matumizi ya mafuta kwa kuwa yametajwa mara kadhaa katika maandiko ni halali, jambo ambalo linahitajika katika kila kitu ni kiasi tu. Mtumishi aliyetumiwa sana na Mungu katika miujiza na uponyaji T.L. Osborn   katika kitabu chake kiitwacho Healing the sick chapter 7 page 26 anaeleza kuhusu maombezi ya kupaka mafuta kama  Nanukuu “This is an unmistakably clear Promise of healing for the sick” mwisho wa kunukuu kwa tafasiri yangu isiyo rasmi  anasema “hii ni  wazi au sahihi ahadi isiyo na dosari kwa uponyaji wa wagonjwa” ni ahadi ya uhakika so bnafsi nakubaliana naye kuwa hakuna shida kutumia mafuta kuwaombea waonjwa.             

 

6.  Uponyaji kwa njia ya Hospital - Uponyaji wa hospitalini ni mojawapo ya njia ambayo Mungu ameiweka kwa wanadamu wote, kupitia akili na maarifa ambayo Mungu amewapa watu wake na uwezo mkubwa wa wanasayansi katika kufanya utafiti, na kuvumbua madawa ya kisasa imekuwa ni njia ya uponyaji wa wanadamu ya kawaida, Mungu anauwezo wa kuponya moja kwa moja kwa njia ya Imani, lakini pia anaweza kutumia vyanzo vingine kama njia ya kuleta uzima,  Katika historia ya kanisa la Kwanza Mtumishi wa Mungu Timotheo alikuwa akisumbuliwa na vidonda vya tumbo, na kutokana na taratibu za kitabibu za wakati ule Paulo alimshauri Timotheo kutumia mvinyo kidogo

 

1Timotheo 5:23 “Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara.

 

Aidha pia Mwandishi wa kitabu cha Matendo ya Mitume na injili ya Luka, yaani Doctor Luka ambaye alikuwa katika timu moja ya umisheni na Paulo Mtume mtu huyu alikuwa na taaluma ya udaktari (tabibu) kwa Kiswahili cha zamani Wakolosai 4:14 “Luka, yule tabibu mpendwa, na Dema, wanawasalimu.” Hii maana yake ni kuwa walikuwepo matabibu wa kawaida na lugha ya matabibu ipo kwa wingi katika sehemu nyingi ikiashiria walikuwepo na walikuwa wakifanya kazi za kitabibu,  na ndio maana hata Yesu alitumia mifano ya walio na afya hawahitaji tabibu

Mathayo 9:12 “Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi.” Marko 2:17 “Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”             

 

7.       Uponyaji kwa njia nyingine mbalimbali – Ziko njia nyingine mbalimbali ambazo kimsingi haziwezi kutengenezewa fundisho kwa sababu hazina ushahidi wa maandiko mengine, na hazina tukio la kujirudia rudia au hakuna ushahidi wa andiko zaidi ya moja, lakini ni njia ambazo Mungu alizitumia kuponya watu naziweka hapa kwa faida tu ya kuoanua ufahamu lakini sitoi idhini ya kutumiwa kwa njia hizo kwa sababu hazithibitishwi mara zaidi ya mbili katika maandiko lakini iko haja  ya kuzijua na kujifunza kwa kuwa zimetajwa mara moja, tu katika maandiko.

 

a.       Nyoka wa Shaba - Watu walikuwa wamemuasi Mungu na manung’uniko na hivyo Mungu aliruhusu nyoka za Moto yaani Nyoka wenye sumu, waliokuwa wakiwaadhibu, wakati watu walipotafuta suluhu Mungu alimuelekeza Musa kuweka nyoka wa shaba, na ya kuwa kila atakayeumwa na nyoka atapaswa kuangalia nyoka yule wa shaba, na angepata nafuu

 

Hesabu 21:8-9 “Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.”

 

Tunajua kuwa Nyoka huyu wa shaba alitumika kama alama kivuli kuonyesha Kuwa Yesu atawaponya watu watakaomtazama yeye, lakini kwa wakati huo ilikuwa ni ishara halisi ya uponyaji na Israel waliponywa kwa wakati ule.

 

Yohana 3:14-17 “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.”

 

b.      Uponyaji kwa kutumia matope na mate – Yohana 9:6-7 “Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho, akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona.”                    

c.       Uponyaji kwa kugusa upindo wa vazi (Talit) – Luka 6:19 “Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote”. Marko 5:25-29 “Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule.”

 

d.      Uponyaji kwa njia ya vitambaa na nguo – Matendo 19:11-12 “Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.”

 

e.      Uponyaji kwa njia ya kivuli – Matendo 5:15 “hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao.”         

 

f.        Uponyaji kwa njia ya Mkate wa tini – Isaya 38:21 “Maana Isaya amesema, Na watwae mkate wa tini, wakauweke juu ya jipu, naye atapona.”

 

g.       Uponyaji kwa njia ya chumvi – 2Wafalme 2:19-22 “Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza. Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea. Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, Bwana asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza. Hivyo yale maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena.”

 

h.      Uponyaji kwa njia ya kijiti – Kutoka 15:25 “Naye akamlilia BWANA; BWANA akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko;”

 

i.        Uponyaji kwa njia ya tiba mbadala – Yeremia 51:8 “Babeli umeanguka na kuangamia ghafula; mpigieni yowe; twaeni zeri kwa maumivu yake; ili labda apate kuponywa.” Yeremia 8:21-22 “Kwa sababu ya maumivu ya binti ya watu wangu nimeumia mimi; nimevaa kaniki; ushangao umenishika. Je! Hapana zeri katika Gileadi? Huko hakuna tabibu? Mbona, basi, haijarejea afya ya binti ya watu wangu?

Hakuna jambo Muhimu katika maisha ya mwanadamu kama Afya, Na ndio maana mwanadamu anaweza kufanya lolote analoweza kulifanya ilimradi tu aweze kuwa na uzima, uzima wa afya ya mwili ndio unaoamua ustawi wa kimwili nafsi na roho, shetani alikuwa na uhakika kuwa mwanadamu akiguswa kwenye afya anauwezo hata wa kumkufuru Mungu ilimradi tu atakuwa mzima,

Ayubu 2:4-6 “Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake. Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako.Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake.”

Marko 5:25-26 “Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya               

Maandiko yanaonyesha kwamba mwanadamu anaweza kutoa kila kitu alicho nacho endapo tu afya yake itaguswa, Shetani alitoa hoja hiyo alipokuwa akizungumza na Mungu kuhusu Ayubu, na Marko anatuonyesha mwanamke ilimgharimu vitu vyote alivyo navyo kwaajili ya uzima wake, kwa hiyo unaweza kuona kuwa hakuna mwanadamu anayependa kuteseka, Na ndio maana Mungu katika hekima yake ameahidi kuwaponya wanadamu, anajua umuhimu wa afya kwa mwanadamu, yeye ni Mungu mwenye wivu mkubwa sana hataki watu watafute msaada kwa waganga na wenye pepo wa utambuzi, jambo hilo linamuuzunisha sana.

Walawi 19:31 “Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.”                

2Wafalme 1:16-17 “Akamwambia, Bwana asema hivi, Kwa kuwa umetuma wajumbe waulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, uulize Neno Lake? Kwa hiyo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Basi akafa, sawasawa na neno la Bwana alilolinena Eliya. Na Yoramu alianza kutawala mahali pake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda; kwa kuwa yeye hakuwa na mwana.”

Watu wanaweza kwenda kwa waganga na wachawi au miungu kwa sababu tu ya kutafuta uponyaji na msaada, Mungu ni Mungu mwenye wivu, hataki tutegemee miungu mingine wala wanadamu kwa hiyo anapojitambulisha kuwa ni Mungu mponyaji, maana yae uponyaji ni swala la uhakika, kwa Msingi huo na kwa namna yoyote ile kanisa halina budi kuutafuta uso wa Mungu, uwepo wa Mungu, karama za uponyaji na miujiza kwa kusudi la kuwasaidia watu kwa sababu Mungu yuko tayari na ahadi zake ni ndio na kweli yeye si mtu hata aseme uongo.

Kwa habari ya njia za uponyaji ambazo hazina andiko zaidi ya moja la ushahidi, kanuni za utafasiri maandiko haziruhusu kutumia tukio ambalo halijajirudia zaidi ya mara mbili kutumika kama fundisho lakini jambo la Msingi linaonyesha kuwa mwanadamu anauwezo wa kufanya lolote waajili ya uzima wake na hivyo kanisa lisipokuwa msaada wanadamu hao wanaweza kuutafuta msaada huo nje ya kanisa, au katika mikono ya watu wasiokuwa salama kwao, Agizo la Yesu Kristo kwa kanisa ni pamoja na kuifanya kazi hii ya kuwafungua watu, agizo hilo la Kristo limekataza kabisa kufanya biashara kwaajili ya uponyaji.

Mathayo 10:7-8 “Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.”

Kwa hiyo kibiblia ni marufuku kuutumia uponyaji wa kiungu kama biashara kwa kuwa Mungu ndiye mponyaji mkuu na huponya kwa kutumia wanadamu lakini wa jina lake na kwa nguvu zake, wala wanaoponywa wenyewe bila kushurutishwa na Mtu wanaweza kuguswa na Mungu, kumtumza mtumishi wa Mungu na kusaidia huduma yako kwa vile tu waliguswa wenyewe kuona umuhimu wa huduma ya uponyaji, wako wanawake ambao waliisaidia huduma ya Yesu kwa sababu walikumbuka tu jinsi Mungu alivyowarehemu kupitia mtumishi wake lakini swala hilo sio sharti ni shukurani tu kwa wale ambao Mungu amewatendea na kwa hiyari yao wenyewe

Luka 8:1-3 “Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.”

Wanawake wengi waliokuwa wameponywa na Yesu, kutokana na kuelewa umuhimu wa huduma za uponyaji waliyatoa maisha yao kumsaidia na kumtunza mtumishi wa Mungu kwa mali zao, walifanya hivyo kwa hiyari yao na kwa mioyo yao na kwa shukurani zao, ili Yesu aendelee kuwahudumia wengine, kwa hiyo waamini walioponywa na waliookolewa wanapaswa kuwa na ufahamu kuwa ili kujitoa kufanya huduma hii watumishi wa Mungu watahitaji muda mrefu, wa kuutafuta uso wa Mungu na uwepo wake na nguvu za Mungu na hivyo watahitaji kutunzwa bila ya kutumia janja janja.

               

Rev. Innocent Mkombozi Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!