Jumamosi, 17 Agosti 2024

Sipora: Mwanamke mpatanishi!


Kutoka 4:24-26 “Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi.Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.”


Utangulizi

Mojawapo ya wanawake muhimu sana katika imani na ambaye ni kama umuhimu wake hauonekani ni Sipora aliyekuwa mke wa Musa ambaye aliozwa na Baba yake aliyekuwa kuhani mkuu wa Midian, Mwanamke huyu aliwahi kuyaokoa maisha ya Musa aliyetaka kuuawa na Mungu kutokana na kupuuzia maswala ya sheria ya tohara, na kwa namna ya haraka sana Sipora aliyefahamu sana mapenzi ya Mungu kwa kina na kwa huduma ya kikuhani yaani huduma ya upatanishi alimuokoa Musa na kutufundisha kuwa alikuwa mwanamke hodari, jasiri aliyejaa imani na aliyeyajua mapenzi ya Mungu, ni mwanamke aliyekuwa na huduma ya upatanisho alimpatanisha Musa kwa Mungu

2Wakorintho 5:18-19 “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho.”

Sipora ni mwanamke mwenye asili ya Afrika, Ethiopia ndiye ambaye leo Bwana anataka tujifunze kitu kupitia yeye na kuinua imani za wanawake wa Kikristo na kujifunza pia kupitia yeye katika maisha yetu ya imani, Tutajifunza somo hili Sipora mwanamke Mpatanishi kwa kuzingatia maswala kadhaa yafuatayo:-

·         Sipora ni nani?

·         Sipora mwanamke mpatanishi

·         Mambo ya kujifunza kutoka kwa Sipora  


Sipora ni nani?

Sipora alikuwa binti wa kuhani mkuu wa Midian aliyejulikana sana katika torati kama Yethro au (Reuel). Sipora aliolewa na Musa katika wakati mgumu wa maisha ya Musa, wakati Musa akiwa uhamishoni jangwani kufuatia kukimbia hasira ya Farao baada ya yeye kuua raia wa Misri, kwa hiyo ni katika wakati huo mgumu binti huyu alifanyika faraja kubwa sana kwa Musa

Kutoka 2:11-16 “Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. Basi akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha ndani ya mchanga. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako? Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana.Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima. Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao.”

Kutoka 2:17-22 “Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao.Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo? Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi. Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula. Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora.Huyo akamzalia mwana, akamwita jina lake Gershomu, maana alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni.”

Sipora anakuwa mfano wa wanawake wapatanishi aliyeokoa maisha ya Musa kupitia huduma yake ya kikuhani aliyoifanya kwa uamuzi wa kuokoa maisha ya Musa kwa haraka sana wakati Mungu alipotaka kumuua Musa kwa sababu za kutokuwatahiri watoto wake wa kiume ona

Kutoka 4:24-26 “Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.”

Tukio hili ni moja ya tukio muhimu liinalomuingiza Sipora katika orodha ya wanawake jasiri, wastahivu, wenye imani na ujasiri na upendo halisi kwa mume wake na ambaye alikuwa na uelewa wa juu sana wa kiungu, Sipora ni kama anaonekana alikuwa anamjua Mungu wa Musa, ambaye kimsingi pia alikuwa Mungu wa Yethro baba yake, na desturi zake kwa sababu alijua Hasira za Mungu huyo na namna ya kumtuliza na alijua namna ya kumkinga mumewe na watoto wake, Sipora alitoa dhabihu ya damu ya govi ya mwanae na kuzuia ghadhabu ya Mungu kumshukia Musa, ushujaa na ujasiri mkubwa na ujuzi kuhusu Mungu aliokuwa nao Sipora unatufundisha kuwa hakuna jambo la maana duniani kama wanawake kumjua Mungu, Mwanamke akimjua Mungu na sheria zake sio tu atakuwa mwokozi wa familia yake bali atakuwa mwokozi wa taifa na ulimwengu kwa ujumla, Kama Musa angeuawa ukweli kuhusu Historia ya Musa ungekuwa kwa mtu mwingine, tunajua Mungu angewaokoa wana wa Israel kutoka Misri, lakini labda sio kupitia Musa kama Sipora hangemuokoa katika tukio hili. Dunia nzima leo inafuata taratibu nyingi za sheria zilizoandikwa na Musa, hata wanasheria wanaposoma asili ya sheria duniani hawaachi kumtaja Musa kama moja ya waanzilishi wa sheria ambayo ilitoka kwa Mungu, hata hivyo nyuma ya mgongo wa Musa alikuwepo Sipora mwanamke mweusi wa ukoo wa kikuhani wa Yethro Mmidiani. Hii ndiyo inayotupa shauku katika siku ya leo kujifunza kwa kina na mapana na marefu na kutaka kumjua yeye na familia yake.

Sipora ni nani hasa? Ni vigumu sana kumjua Sipora vizuri kwa sababu habari zake hazikupewa umuhimu mkubwa na waandishi wa torati, penginepo ni kwa sababu ya jamii ya kiyahudi kutokuwapa umuhimu mkubwa wanawake, ama pia kwa sababu ya familia za kikuhani ambazo mara kadhaa ziliwataka wanaume kujitenga na wanawake kama sehemu ya usafi na utakatifu pale wanapofanya huduma zao kwa Mungu kwa mujibu wa sheria au torati

Kutoka 19:10-15 “BWANA akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao,wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu BWANA atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote.Nawe utawawekea mipaka watu hawa pande zote, ukisema, Jihadharini, msipande mlima huu, wala msiuguse, hata mapambizo yake; kila mtu atakayeugusa mlima huu, bila shaka atauawa. Mkono wa mtu awaye yote usimguse mtu huyo, ila hakika yake atapigwa kwa mawe, au kupigwa kwa mkuki; kwamba ni mnyama au kwamba ni mwanadamu, hataishi. Hapo panda itakapotoa sauti kwa kufuliza ndipo watakapoukaribia mlima. Musa akatelemka mlimani akawaendea watu akawatakasa, nao wakafua nguo zao. Akawaambia watu; Mwe tayari siku ya tatu; msimkaribie mwanamke.”

Sipora alikuwa Binti Mkubwa wa Yethro kuhani mkuu wa Midian ambaye anatajwa kuwa alikuwa na mabinti saba, Sipora alikuwa na uelewa mkubwa kuhusu Mungu kwa sababu alikuwa amejifunza sheria zote za ukuhani na kumjua Mungu wa baba yake, Baba wa Sipora alikuwani kuhani mkuu wa Midian kwa hiyo ni wa uzao wa Ibrahimu ni ndugu wa wayahudi pia, wote tunakumbuka kuwa Ibrahimu ukiacha ya kuwa alikuwa amemzaa Ishmael na Isaka pia alikuwa na watoto wengine wa kume sita aliowazaa kupitia Ketura na katika hao Midian ni mmoja wao ona:-

Mwanzo 25:1-6 “Ibrahimu alioa mke mwingine jina lake akiitwa Ketura. Akamzalia Zimrani, na Yokshani, na Medani, na Midiani, na Ishbaki, na Sua. Yokshani akamzaa Sheba, na Dedani; na wana wa Dedani walikuwa Waashuri na Waletushi, na Waleumi. Na wana wa Midiani walikuwa, Efa, na Eferi, na Hanoki, na Abida, na Eldaa. Hao wote walikuwa ni wana wa Ketura. Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu.”            

Kwa hiyo unaweza kuona kuwa katika hawa watoto wengine wa Ibrahimu wanaotajwa hapo juu Midiani ni wanne kati ya watoto sita aliozaa Ibrahimu kupitia Ketura unaona? Je watoto hawa wa Ibrahimu walimjua Mungu? Walijua kutenda haki? Waliyashika mafundisho yote ambayo Bwana alikuwa amemfundisha Ibrahimu? Jibu ni NDIO kwa herufi kubwa sana kwa nini kwa sababu Mungu alimchagua Ibrahimu kwa sababu alijua kuwa Ibrahimu atakuwa Mwalimu mzuri sana kwa watoto wake wote na wakazi wote wa nyumbani mwake na kuwa kupitia yeye wataishika njia ya Bwana na watafanya haki, na hukumu. Kwa hiyo watoto wote wa Ibrahimu walikuwa werevu na wajuzi wa sheria za Mungu na hukumu zake akiwepo Yethro kutoka ukoo wa Midian! Unaona?  

Mwanzo Mwanzo 18:17-19 “BWANA akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake.”

Kwa hiyo ni wazi kupitia Ibrahimu na uzao wake sasa kupitia Midiani na kuja kwa Yethro ni wazi kuwa Sipora na wadogo zake walimjua Mungu, na walifahamu utaratibu wote wa Mungu wa baba yao, Yethro alikuwa ni kuhani wa Mungu wa ngazi ya juu sana anapokuwepo Yethro sio rahisi Musa na Haruni kusongeza dhabuhi kwa Bwana kwa sababu Yethro alikuwa na ujuzi mkubwa zaidi na ni kuhani wa Mungu aliyejuu zaidi yao

Kutoka 18:8-12 “Musa akamwambia mkwewe mambo hayo yote BWANA aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na mambo mazito yote yaliyowapata njiani, na jinsi BWANA alivyowaokoa.Yethro alifurahi kwa ajili ya wema wote BWANA aliowatendea Israeli, kwa alivyowaokoa mikononi mwa Wamisri. Kisha Yethro akasema, Na ahimidiwe BWANA aliyewaokoa na mikono ya Wamisri, na mkono wa Farao; aliyewaokoa watu hao watoke mikononi mwa Wamisri.Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti.Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu.”

Kwa msingi huo utaweza kukubaliana nami kuwa Israel ambao wameishi Misri katika nyumba ya upagani mzito kwa miaka 430 tangu baba yao aliposhuka Misri na kizazi cha kina Yusufu, uwezo wao wa kumjua Mungu ni lazima ulikuwa umeathirika sana kumbuka wakati huo hakukuwa na Sheria bado, na hata Musa mwenyewe hangekuwa na ujuzi mkubwa wa kutosha kuhusu kumjua Mungu kama asingelipata muda wa kujifunza kutoka kwa Yethro, ni wazi kuwa Yethro na familia yake walikuwa wanamjua Mungu aliye hai, na walihusika sana kumsaidia Musa kujua maswala ya Mungu, huku Sipora akiwa binti hodari mwenye uwezo mkubwa wa kumjua Mungu na taratibu zake hata japokuwa alikuwa mwanamke na hakuwa nabii lakini alikuwa mshauri mkubwa sana wa Musa, Sio hivyo tu Sipora na familia yake wamekulia jangwani hivyo walilijua jangwa vizuri sana na ndio maana utaweza kuona alipokuja Yethro na kumleta Mke wa Musa pamoja na watoto, Musa sasa alikuwa akimsikiliza mkewe zaidi kuliko Miriam na Haruni ndio sababu Miriam aliona wivu na wakaanza kumteta na kumshambulia kwa ubaguzi wa rangi yake kama mwanamke Mkushi yaani mwanamke mwenye ngozi nyeusi (Ethiopian). Ona:-

Kutoka 18:1-7 “Basi Yethro, kuhani wa Midiani, mkwewe Musa, alisikia habari ya mambo hayo yote Mungu aliyokuwa amemtendea Musa, na Waisraeli watu wake, jinsi BWANA alivyowaleta Israeli watoke Misri. Ndipo Yethro mkwewe Musa akamtwaa Sipora, mke wa Musa, baada ya yeye kumrudisha, pamoja na wanawe wawili; katika hao, jina la mmoja ni Gershomu, maana alisema, Mimi nimekuwa mgeni katika nchi ya ugenini; na jina la wa pili ni Eliezeri, kwa kuwa alisema, Yeye Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa na upanga wa Farao. Basi Yethro, mkwewe Musa, pamoja na mke wa Musa na wanawe wawili wakamwendea Musa huko nyikani, hapo alipokuwa amepanga, kwenye mlima wa Mungu; naye akamwambia Musa, Mimi Yethro mkweo nimekuja kwako, na mkeo, na wanawe wawili pamoja naye. Basi Musa akatoka nje ili amlaki mkwewe, akasujudia na kumbusu; nao wakaulizana habari; kisha wakaingia hemani.”

Ujio wa Sipora kutoka nyumbani kwa Yethro kuungana na Musa mumewe na Musa kumpa kipaumbele unapelekea Haruni na Miriam kuona kama wanapoteza nafasi yao kwake na wakaanza kumsema vibaya jambo lililopeleka Mungu kuingilia kati na kuchukua hatua kali sana kwa Miriamu

Hesabu 12:1-13 “Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi. Wakasema, Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao. Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi. Bwana akanena ghafula na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje. Bwana akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili. Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, Bwana, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa? Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake. Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma. Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu nakusihi sana usituwekee dhambi juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi. Nakusihi, asiwe kama mmoja aliyekufa, ambaye nyama ya mwili wake nusu imelika hapo atokapo tumbo la mama yake. Musa akamlilia Bwana, akasema, Mpoze, Ee Mungu, nakusihi sana.”

Unaona nadhani sasa unapata Mwanga jinsi Sipora alivyokuwa wa muhimu, Sipora ni mwanamke Jasiri, mwanamke aliyejaa imani, mwanamke mwenye upendo, mwanamke kiongozi, mwanamke anayelijua jangwa vizuri, alikuwa na utulivu wa ajabu sana na ndio maana hata katika hali ngumu aliweza kufanya maamuzi sahihi na kutuliza hasira za Mungu dhidi ya mumewe, alikuwa mshauri mzuri wa Musa mpaka Miriam aliona wivu, alisengenywa lakini yeye na Musa walikaa kimya, unaweza kuchunguza kwa kina kuwa aliyekuwa anasemwa hapo sio Musa bali ni mwanamke huyu mwenye rangi nyeusi, hapa maandiko yanamtaja kama mwanamke mkushi neno kushi katika Biblia ni “Ethiopia” Ethiopia ni neno la kigiriki/kiyunani ambalo tafasiri yake ni “Of burned face” yaani watu weusi au walioungua uso na lilitumika kumaanisa watu wa Afrika hususani inchi iliyokuwa inafikika kwa bara bara kwa wakati huo ilikuwa ni Ethiopia kwa hiyo wakushi kimsingi walikuwa ni watu wenye ngozi nyeusi yaani mwafrika na walijulikana kwa ngozi yao nyeusi  katika maandiko ona

Yeremia 13:23 “Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.”

Kwa hiyo unaweza kupata picha kuwa Musa yeye alikuwa ameoa binti huyo Sipora aliyekuwa mweusi mtoto wa kuhani wa Midian. Lakini mwenye ujuzi mkubwa kuhusu Mungu, malezi mazuri, Jasiri, mwenye kujaa Imani, mwenye upendo na mpatanishi na mwenye kulijua jangwa ni mwanamke huyu ndiye tunajifunza habari zake leo.

Sipora mwanamke mpatanishi

Jinsi ambavyo Sipora alimuokoa Musa na kuwa mpatanishi kati ya Musa na Mungu ndio habari ya mjini katika siku hii ya leo, tukio hili lilikuwa ni tukio la namna gani, kwa sababu watu wengi wanashindwa kulibainisha lilivyokua lakini swala la msingi ni kuwa matendo na maneno ya Sipora yalimuokoa Musa katika tukio hilo hebu tulione tena katika maandiko

Kutoka 4:24-26 “Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.”

Ni tukio linaingizwa ghafla katika maandiko, Musa alipokuwa njiani akiwa pamoja na familia yake alikutana na Bwana na Bwana alitaka kumuua! Inaonekana kuwa kosa kubwa hapa ni kuwa Musa alikuwa hajawatahiri watoto wake na au alikuwa amepuuzia hivyo Mungu alichukizwa na hilo, hapa ndio tunajua kuwa Sipora alikuwa anajua umuhimu wa tukio hilo, kwani Musa huenda alishikwa na tatizo la ghafla na kwa ujasiri mkubwa mwanamke huyu alishika kisu cha jiwe gumu na kumtahiri mtoto na kuibwaga miguuni pake na kusema hakika wewe u bwana harusi wa damu kwangu mimi, Biblia ya kiingereza ya NRSV inasema aliikata govi ya mwanae wa kiume na kuitupa katika miguu ya Mungu na kusema maneno kwa kiebrania  (Dậm Chậthận) Baba mkwe wa Damu! Kwa hiyo aliitupa govi ya kijana katika miguu ya Mungu au aliiweka miguuni pa Mungu, na kwa sababu hiyo Musa na yeye wakawa wazima, bila tukio hili Musa angepigwa na Mungu kwa sababu ya kupuuzia agizo hili ambalo Mungu alimuamuru Ibrahimu, lakini kwa ushujaa wa Sipora na uelewa wake kuhusu tabia ya Mungu Musa aliokolewa na kuendelea na majukumu ya kazi ya ukombozi.

Sipora ni mwanamke wa kipekee na jasiri historia yake inatukumbusha kuwa hata katika hali ngumu wanawake wanaweza kujivika ujasiri, kutoka kwa Mungu, na kuwa wanaweza kuwa na ujuzi kuhusu Mungu na kusababisha wokovu mkubwa kwa familia yao na taifa na kufanikisha njia za Mungu, wanawake wanaweza kusimama kwa ujasiri na kuwapatanisha watu kwa Mungu, wanawake ndio waliokuwa wa kwanza kufika kaburini wakati Yesu amefufuka, na mwanamke msamaria aliwaleta wasamaria wengi kwa Yesu, Mungu anaweza kuwatumia wanawake na Imani ya kweli hukaa na wanawake na ndio maana Mungu hajawahi kuwapuuzia na aliwataka waisrael kutokuoa wanawake mabaradhuli, na wasiomcha Mungu kwani wanawake wanauwezo wa kugeuza moyo wa mwanaume hata kama ana hekima kiasi gani, hivyo kila mtumishi wa Mungu anapaswa kuoa mwanamke mcha Mungu kama alivyo Sipora mwanamke anayemjua Mungu na njia za Mungu na sio wanawake mabaradhuli wasio mcha Mungu.

1Wafalme 11:1-6 “Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, na wa mataifa Bwana aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda.Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo.Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni.Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu, kama Daudi baba yake.”

Wanaume wanapaswa kuwa makini ni aina gani ya mwanamke wanamuoa, ni ukweli usiozuilika kuwa hata uwe na hekima kiasi gani kama utapata mwanamke asiyemjua Mungu wala kuheshimu mambo ya Mungu na wito wako wa kiungu huduma yako itasambaratika, Huduma ya Musa iliweza kusimama na hata maisha yake kuwa salama kwa sababu alikuwa na mwanamke muelewa, wakati Sulemani aliharibikiwa kwa sababu ya wanawake, ni hatari hata kuoa mwanamke mchanga kiroho asiyelijua vema neno la Mungu wala hamjui Mungu wake inaweza kuleta madhara makubwa na kuwakosesha watu Baraka ambazo Mungu alizikusudia kwa watu wake, kama Sipora angekuwa mwanamke wa hovyo leo historia ya Israel na ushujaa wa Musa usingeliweza kuonekana, jina la Bwana na libarikiwe pia kwaajili ya malezi mazuri ya Yethro na ushauri  na mafunzo yaliyomsaidia Musa na wana wa Israel kwa ujumla.

Mambo ya kujifunza kutoka kwa Sipora

Je umewahi kukutana na hali ngumu ambayo kwa jiyo ulihitaji mwanamke jasiri kama wa Sipora? Unawezaje kuimarisha imani yako ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali? Unawezaje kuonyesha upendo usio na mipaka kwa wale tunaowapenda?

Sipora ni mfano na majibu kwa kila mmoja kwa sababu alitatua changamoto katika njia za kiungu, ameonyesha kuna faida kubwa sana katika kumjua Mungu aliye hai na njia zake, na anawakumbusha wanawake kujiamini katika Mungu

Kila mwanamke akumbuke kuwa anaweza kuwa mwenye nguvu na uwezo mkubwa, usiruhusu chochote kukuzuia kufikia malengo yako jifunzeni kutoka kwa Sipora na amini katika Mungu na kujijengea ujasiri na imani, hata kama watu hawamzungumzii sana Sipora, kama wanawake leo wanavyopuuziwa katika jamii nyingi, Roho Mtakatifu leo ametaka ujifunze kitu na uwe mwenye kumcha Mungu na kumjua Mungu  na kusifiwa kwa uchaji wa Mungu na kwa kufanya tukio lililo jema tafadhali kuwa mwema mche Mungu kama Sipora, uiokoe jamii yako na taifa stay blessed !   

Mithali 31:29-30 “Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote. Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa.”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima         

Jumamosi, 10 Agosti 2024

Vijana wamchao Mungu na ujasiriamali.


1Timotheo 4:11-13 “Mambo hayo uyaagize na kuyafundisha. Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi. Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha.”





Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa idadi ya watu nchi Tanzania kwa sasa inakadiriwa kufikia 61,741,120 yaani milioni 61 na katika idadi hii ya watu vijana ni asilimia 77% kati ya hao asilimia 35% wako chini ya umri wa miaka 35  kwa Msingi huo kuna wimbi kubwa sana la vijana katika taifa letu, na wimbi hili linaweza kuwa Baraka kubwa sana na kama kanisa na taifa tusiposhughulika nao wanaweza kuwa sababu ya changamoto kubwa sana endapo tu watakosa misingi itakayowapa muelekeo wa namna ya kuishi kwa Amani duniani na kujaribu kuishi kwa kujitegemea. Kwa msingi huo Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina namna na jinsi Vijana wanavyoweza kuyakabili maisha kupitia ujasiriamali kwa kuzingati misingi ya kibiblia tutajifuza somo hili kwa kuzigatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

·         Maana ya vijana na ujasiriamali

·         Misingi ya kibiblia kuhusu ujasiriamali

·         Mambo ya msingi ya kuyazingatia

 

Maana ya vijana na ujasiriamali

Neno vijana na ujasiriamali linapowekwa pamoja inaweza kuwa ngumu kuliona moja kwa moja katika mtazamo wa kimaandiko, lakini hili halimaanishi kuwa haliko, hapo kuna muunganiko wa maneno mawili 1 Vijana na 2 Ujasiariamali


1.       Vijana ni kundi la watu walio katika hatua ya ukuaji wa kijamii, kiuchumi na kiroho ambao bado wako kwenye mchakato wa kujitambua, kujitegemea na kutafuta muelekeo kwa lugha ya vijana ni watu wale ambao bado wanajitafuta, hawana utulivu mpaka wapate kile wanachokiota au kukitamani, ni kundi la watu wenye ndoto na maono na ni kundi ambalo kimsingi Mungu hajawahi kuwaacha anapokusudia kuwamwagia Baraka zake ni kundi ambalo liko katika mpangowa Mungu wa Baraka hivyo vijana hawapaswi kujifikiri kuwa wameachwa!  Mungu ametumia vijana na ana makusudi makubwa na vijana hivyo hawezi kuwapuuzia!

 

Yoeli 2:25-29 “Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu. Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la Bwana, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe. Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; wtena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.”

 

2.       Ujasiriamali – Ujasiriamali ni uwezo wa kuanzisha na kuendesha biashara au shughuli za kuzalisha mali na kutumia fursa zilizopo na tulizopewa na Mungu kwa ubunifu na kwa njia ya kipekee ili kutimiza malengo ya kiuchumi na kijamii kwa kawaida akili hii na uwezo huu wa ujasiriamali unatoka kwa Mungu

 

Kumbukumbu 8:18 “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo

 

Katika mtazamo wa Kikristo tunaelewa kuwa maisha yetu yapo mikononi mwa Mungu, na mwanadamu amewekwa Duniani na Mungu na msingi wa kwanza wa Mwanadamu kuwekwa Duniani ilikuwa ili afanye kazi, Mungu alimpa fursa mbalimbali mwanadamu na kumpa kila kitu, kwa sababu hiyo umasikini sio mpango wa Mungu, wala Mungu siye anayesababisha umasikini lakini Mungu anauwezo wa kutufunulia fursa ambazo tunaweza kuzitumia na kujipatia riziki zetu, pamoja na wale wote wanaotutegemea na wote wenye uhitaji wanaotuzunguka duniani.   

Misingi ya kibiblia kuhusu ujasiriamali

Ni muhimu kufahamu ya kuwa neno la Mungu limeweka wazi ya kuwa Misingi yote ya ujasiriamali imewekwa na Mungu na imeanzishwa na Mungu, Kumbuka Mungu ndiye aliyeumba na kutupa kila kitu, kwa hiyo uumbaji wa Mungu ni zawadi na mtaji wa hali ya juu kwa mwanadamu, kwa sababu Mungu alitangulia kuwekeza kwanza kisha akampa Mwanadamu umiliki wa kila kitu katika ulimwengu huu,

Mwanzo 1:26-28 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo.”

Mungu amempa mwanadamu kila kitu anachokihitaji, amempa akili, anga, ardhi, maji, wanyama, ndege, miche, miti, mbegu, madini na kila kitu na amembarikia na kumtaka akavitawale, kwa hiyo mwanadamu amepewa kila kitu na anamuwazia mema kila mwanadamu Mungu hafurahii maumivu yetu, kama tukimtegemea yeye atatufungulia macho yetu na kutuonyesha Fursa aliyoikusudia kwetu kwa sababu wakati wote Mungu anatuwazia mema lakini ili tufanikiwe kuna maswala kadhaa ambayo maandiko yanatuelekeza kuyazingatia:-

1.       Ufunuo kuhusu Fursa – Maandiko yanaonyesha kuwa wako watu wengi waliopitia shida ma mashaka makubwa sana, walioshi katika nyika, jangwa na kupitia maisha hatarishi sana lakini mafanikio yao yalikuja kupitia ufunuo wa kutumia Fursa walizofunuliwa na Mungu, Fursa ni nini? Neno Fursa kwa kiingereza ni Nafasi, au opportunity na Mungu ni Mungu anayetoa nafasi pale tunapomuomba na kumlilia, ukiona bado huioni fursa ujue bado hujabanwa ipaswavyo, lakini unapokuwa katika wakati mgumu sana mpaka ukawaza moyoni nitafanya nini ndipo utakapoona Mungu akikufungulia fursa au akikufanyia nafasi, Fursa ni nafasi au uwezekano wa mjasiriamali kuitumia nafasi inayopatikana ili kupata faida au manufaa ya kukufanikisha

 

a.        Mwanzo 21:14-20 “Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba.Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia.Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko.Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.” 

 

b.      Mwanzo 26:1-22 “Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari. BWANA akamtokea, akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia. Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako. Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia. Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu. Isaka akakaa katika Gerari. Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso. Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe. Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, Ni ndugu yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nalisema, Nisife kwa ajili yake. Abimeleki akasema, Ni nini hii uliyotutendea? Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani. Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima atauawa. Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika.Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.”

 

c.       Matendo 16:6-12 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia. Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa, wakapita Misia wakatelemkia Troa. Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie.  Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema. Basi tukang'oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli; na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha.”            

 

Maandiko yanaonyesha kuwa Mungu ni Mungu mwenye kuonyesha Fursa anatoa nafasi na kufungua mlango, wakati nafasi moja inapopotea, au mlango mmoja unafunga na unaona giza Mungu yeye yupo na hutuonyesha nini cha kufanya na wapi pa kuelekea, Hajiri na Ishmael walipofukuzwa, Mungu aliwaahidi kuwafanya taifa kubwa, walikimbilia jangwani, hali ilikuwa ni kame, maji yaliisha, chakula kikaisha, mtoto alizidiwa kiasi cha kufa lakini Mungu alimuonyesha Hajiri kisima, kisima ambacho kiliokoa maisha yao na bila shaka kilikuwa sababu ya makazi mapya, kijana akawa mwindaji na akaozwa na mke, vijana wengi hawana mke, hawana Mume na wana hali mbaya ya kiuchumi kwa sababu hawajafunuliwa fursa, Mungu akikufunulia Fusra utakuwa mtu mkubwa na utatajirika, Leo hii taifa la Kiarabu ni matajiri wakubwa wa Mafuta Duniani Mungu aliwaonyesha kisima katika Jangwa,

 

Isaka aliweza kugundua kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia kisima, wakati inchi ilikuwa na njaa Isaka hakuwa na njaa kwa sababu alinywesha mifugo yake kwa maji ya kisima na alibadili jangwa kua ardhi nzuri na kilimo, mifugo ilimpa mbolea, maji yalitunza mifugo na alimwagilia chakula cha wanadamu na wanyama, Chakula kilipatikana na akauza na hivyo alikuwa mtu mkubwa sana, wafilisti walipogundua walimuonea wivu, walifukia visima vyake, lakini alichimba vingine, hatimaye Bwana alimpa nafasi REHOBOTH.  Uko ufunuo, yako maono kwaajili ya biashara zako, mifugo, yako mashimo ya madini yako, genge lako, Huduma yako na kadhalika jambo kubwa na la msingi ni kuhitaji Maono kutoka kwa Mungu ili kwamba Bwana aweze kufungua nafasi na kubariki uchumi wako.

 

Mungu aliwafungulia mlango, Paulo mtume na Silas, na Timotheo na Luka, na wengineo wote wwliokuwa nao katika timu yao ya umisheni, kila walikotaka kwenda kwaajili ya injili milango ilifunga lakini hatimaye walimuona mtu kutoka Makedonia kwenye maono aliwaomba wavuke kwenda Makedonia, kwa hiyo Mungu aliwafungulia mlango wakufaa sana kwaajili ya injili.

 

Kila mmoja anahitaji neema ya Mungu ili aweze kupata maono na namna ya kuyainua macho ili uweze kuona fursa ambayo wengine wanaweza wasiione, Ni Mungu akupaye akili za kupata utajiri. Kila mmoja hana budi Kumuomba Mungu akuonyeshe fursa. Kwa mfano kunaposikika kuwa kuna mahafali mahali Fulani, utaona watu wanauza maua ya mataji, wanapiga picha, hawa wanatumia hilo tukio kunufaika kibiashara baada ya kujipanga kimkakati na kuhakikisha kuwa hawatapata hasara.

 

2.       Hekima na maarifa – Kutengeneza fedha na mali kunahitaji pia hekima na maarifa, hekima na maarifa ni nyenzo Muhimu inayotusaidia kuamua kwa busara biashara gani tuifanye, wapi ifanyike  na namna ya kufanya, tunaweza kupata hekima na maarifa kwa kujifuza katika mafundisho kama hivi, lakini vilevile tunaweza kusoma vitabu mbalimbali na vikatusaidia kuyapata maarifa Maandiko yanaonyesha  jinsi Hekima na maarifa ilivyo vyenzo ya Muhimu katika kujijenga kiuchumi, tunaweza kujifunza namna ya kufuga wanyama mbalimbali, na kukuza mazao ya namna mbalimbali hata kupitia mitandao ya kijamii na kwenye You tube, au kwa kutumia app za akili mnemba (Artificial Inteligences Apps) kwa kupata maarifa mbalimbali

 

a.       Mithali 24:3-5 “Nyumba hujengwa kwa hekima, Na kwa ufahamu huthibitika,Na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa Vitu vyote vya thamani na vya kupendeza. Mtu mwenye hekima ana nguvu; Naam, mtu wa maarifa huongeza uwezo;”

 

b.      Mithali 1:7 “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.”

 

c.       Yakobo 1:5 “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.”

 

Maandiko yanatuonyesha wazi kuwa tunaweza kuwa na mafanikio makubwa sana na kujijenga kiuchumi, kiroho, na kwa utajiri kama tu tutakuwa na Hekima na maarifa, kuja katika mafundisho kama haya au kusoma kunatupa maarifa, lakini hata hivyo maarifa ya msingi zaidi na ya muhimu yanapatikana kwa Mungu, kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa na sio hivyo tu tunaweza kupata hekima kwa kuomba, wote tunakumbuka jinsi Hekima ilivyokuwa sababu ya mafanikio makubwa sana kwa Mfalme Suleimani, watu wote unaowaona kuwa wamefanikiwa Mungu aliwapa hekima hii na ujuzi wa namna ya kufanikisha mambo yao, wakati mwingine hata bila kujali Imani yao mradi tu wamekaa katika kanuni zake na wanamtambua na kumkubali wakiishi kwa nidhamu kwa hiyo utaweza kukubaliana nami ya kuwa hatuwezi kumuweka Mungu pembeni linapokuja swala la ujasiriamali.

 

3.       Kufanya kazi kwa bidi - Siri nyingine kubwa mara baada ya Mungu kukuonyesha fursa yako na kukufunulia nafasi yako, na kukupa hekima na busara lazima uongeze bidii katika kile ambacho Mungu amekupa kukifanya, Ni muhimu kufahamu kuwa neno la Mungu linapiga vita uvivu, na linatutaka tufanye kazi kwa bidii na ukiweka bidii  maandiko yanasema utasimama mbele ya wafalme.

 

a.       Mithali 22:29 “Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme; Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo.”

 

b.      Mithali 6:6-11 “Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako? Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.”              

 

4.       Ujasiriamali unahitaji Imani, ujasiri na kuondoa aibu – kila kitu duniani kina vikwazo, moja ya kikwazo kikubwa cha ujasiriamali ni pamoja na kuwa na aibu, kukosa ujasiri na hata kukosa Imani ili tuweze kuwa na hayo na kufanikiwa na kuwa mbali na Hofu mfahamu ya kuwa tunamuhitaji Roho Mtakatifu pia, kama jinsi anavyotupa ujasiri kushuhudia habari za ufame tunamuhitaji pia katika biashara zetu, tuwe kama hatuoni, tuwe hatuna aibu tunapoamua kutafuta, watu wanaouza maduka, vitumbua, mikate, chapati, na kadhalika na vyakula kama mama nitilie na kadhalika huwa wanaweka woga kando, wanaweka mbali hofu na wanamuamini Mungu kuwa watauza

 

a.       2Timotheo 1:6-8 “Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu;”

 

Imani, ujasiri na kutokuwa na haya yaani kuona aibu sio fungu la mtu aliyeokolewa na anayejitafutia riziki, tunahitaji Imani kuwa Mungu atatuletea wateja kwa ile fursa aliyotufunulia na kwa lile wazo la kibiashara, au kilimo alilotupa, na lolote lile, leo hii wako wakina mama wengi wa kikristo ambao wanamiliki shule zao za awali, za msingi na sekondari, walipata mawazo, walianza kwa vikwazo lakini Mungu aliwasaidia na sasa wanamiliki uchumi mkubwa na ni vyombo vikubwa vya Mungu vya kuipeleka injili.

 

5.       Ujasiriamali unahitaji kutengenezewa mkakati – Mjasiriamali anapaswa wakati wote kukaa kimkakati, huku akihakikisha kuwa anakuwa makini na anakuwa tayari kwa kila nafasi itakayojitokeza wakati wowote kwa kusudi la kupata faida na kuhakikisha kuwa hapati hasara, Mpango mkakati huo pia unamuhitaji Mungu, wapendwa wengi wanadhani usemi ule mpe kaisari yaliyo ya kaisari na Mpe Mungu yaliyo ya Mungu ni kama umetenganisha Mungu na Biashara hapana unaenda na Mungu wako kwenye biashara huku ukimshirikisha yeye katika njia zako zote na yeye atakupa mkakati wa mafanikio usiomuondoe Mungu katika mkakati wako wa kibiashara na hivyo ndivyo neno la Mungu linavyotuelekeza, hakikisha kuwa unakuja kivingine, na unakuwa tofauti na wengine.

 

a.       Mwanzo 41:25-40 “Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja. Na wale ng'ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa. Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri.Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana. Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi. Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri. Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba. Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa. Neno hilo likawa jema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake wote. Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake? Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”

 

b.      Mwanzo 30:37-43 “Yakobo akatwaa fito za mlubna mbichi, na mlozi, na mwaramoni, akazibambua maganda, mistari myeupe ionekane ndani ya hizo fito. Akazisimamisha fito hizo alizozibambua katika mabirika ya kunyweshea maji, pale walipokuja wanyama wanywe; wakachukua mimba walipokuja kunywa.Wanyama wakapata mimba mbele ya hizo fito, wakazaa wanyama walio na milia, na madoadoa, na marakaraka. Na Yakobo akawatenga wana-kondoo, akazielekeza nyuso za makundi zielekee wale waliokuwa na milia, na kila aliyekuwa mweusi katika wanyama wa Labani. Akaweka kando wanyama wake mwenyewe, wala hakuwachanganya pamoja na wanyama wa Labani. Ikawa kila walipopata mimba wanyama wenye nguvu, Yakobo akaziweka zile fito mbele ya macho ya hao wanyama katika mabirika ili kwamba wachukue mimba kati ya zile fito, lakini wanyama walipodhoofika hakuziweka zile fito. Basi wale dhaifu walikuwa wa Labani, na wenye nguvu walikuwa wa Yakobo. Kwa hiyo mtu huyo akazidi mno, akawa na wanyama wengi, na vijakazi, na watumwa, na ngamia, na punda.”            

 

Mungu alimpa Yusufu kutafasiri ndoto na alimpa mkakati utakaomsaidia kuhifadhi chakula na kufanya biashara ya chakula hicho wakati wa njaa, kwa hiyo Farao aliona wazi kuwa hakuna mtu mwingine anayeweza kulisimamia jukumu hili isipokuwa yeye na kwa fursa hii Yusufu akawa msimamizi wa swala zima lililompa faida yeye na familia yake na ulimwengu kwa ujumla.

 

Yakobo hali kadhalika alipewa mpango mkakati wa namna ya kupata mshahara wake au kondoo wake na mbuzi na mifugo kama malipo yake kutoka kwa Labani na ilikuwa ni Mungu aliyeingilia kati kufanya hivyo, Kwa sababu Labani alikuwa amekusudia kumdhulumu Yakobo mara kadhaa lakini Mungu alimpa Yakobo njia ya kufanikiwa alimpa mkakati kwa njia ya ndoto

 

Mwanzo 31:7-12 “Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwacha kunidhuru. Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia. Hivi Mungu akamnyang'anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi. Ikawa, wakati wale wanyama walipochukua mimba, naliinua macho yangu nikaona katika ndoto, na tazama, mabeberu waliowapanda hao wanyama walikuwa na milia, na madoadoa, na marakaraka.Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa. Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda wanyama wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutendea Labani.”                

 

kwa hiyo ujasiriamali unahitaji mpango mkakati lakini wakati huo huo tukumbuke mkakati unatoka kwa Mungu. Kwa hiyo Yusufu na Yakobo walikaa kimkakati. Mungu anapokufunulia mpango Fulani wa kukufanikisha anakupa na mkakati wake, alimpa Nuhu vipimo vya kujengea Safina na alimuelekeza na aina ya mbao atakazotumia, alimpa Musa maelekezo ya kujenga sanduku la agano na alimpa vipimo na namna atakavyojenga, huwezi kumtenganisha Mungu na mipango mikakati katika kila kitu ikiwepo ujasiriamali.

 

6.       Ujasiriamali unahitaji kujenga Mahusiano – Ujenzi wa mawasiliano ni muhimu sio tu kwaajili ya ushirika kanisani, lakini hata katika biashara, Mahusiano mazuri, lugha nzuri na tabasamu lako ucheshi na namna unavyowahudumia watu vinaweza kujenga uhusiano Mzuri, unapojenga uhusiano Mzuri unapanua mipaka yako ya kushirikiana na wengine, kupata taarifa, kushauriwa, kujifunza na kujiongeza, wakati Mwingine hususani watu waliookoka wanafikiri kuwa siriasi, kununa nuna ndio kutaonyesha kuwa wako makini na kujilinda na wokovu na kama akicheka cheka ni kama amejirahisi na anadhani atarahisisha na mambo mengine. Mungu ametuumba na haiba na anatutaka tuwe na mahusiano mema kwa hiyo katika ujasiriamali tunamtegemea mtu aliye okoka kuwa bora zaidi kihuduma kuliko wale wasiomjua Mungu

 

a.       Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”

 

b.      Waebrania 13:2 “Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.”         

 

c.       Wagalatia 5:22-23 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.”

 

d.      Mithali 14:28 “Utukufu wa mfalme ni wingi wa watu wake; Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao.”

 

Wajasiriamali wanatakiwa kuwa na amani na watu wote, kwa sababu watu ndio mtaji wetu mkubwa, wajasiriamali wanapaswa kuwa na furaha, Amani, utulivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kujinidhamu na ukarimu kwa ujumla kwa sababu hayo yanawavutia watu, ni  jambo la kusikitisha sana kuwa mtu aliyeokoka anakuwa na lugha ya hovyo, amenuna na hatoi huduma bora na kuwachangamkia watu alafu watu wavutiwe, ukweli ni kuwa ukipoteza watu unapoteza ukuu wako wasambaa wanasema Zumbe ni Wanthu yaani nguvu ya mfalme ni watu wake usipoteze wateja, aidha tunda la Roho linamsaidia mjasiriamali wa kikristo kutokuwa na urasimu usio na maana katika kutoa huduma kwa wateja jambo ambalo litawavutia na kuimarisha uhusiano wako nao.

Mambo ya msingi ya kuyazingatia

Tumeona jinsi ambavyo Neno la Mungu yaani Biblia ina mawazo mengi sana yaliyonyooka ya kuwasaidia sio vijana pekee bali watu wote kuhusu ujasiriamali, lakini tunawalenga vijana kwa sababu ndio wengi na ndio wenye nguvu na wengi wao wako katika rika la utafutaji, kwa hiyo kanisa lina wajibu wa kuwafunulia ujuzi wa neno la Mungu  ili vijana wajitume, wamuamini Mungu, wawe na ujasiri na kufanya biashara, na shughuli nyingine za kujipatia kipato huku wakimtanguliza Mungu, Tumeona ya kuwa Mungu ana mpango mwema kwa ajili yao na hivyo hawana nafasi ya kumlaumu Mungu kwa ugumu wa maisha badala yake wanapaswa kujua ya kuwa Mungu anawapenda na anashughulika na mafanikio yao, Kwa wakristo masomo kama haya yanaweza kuwa kitu kipya lakini haikuwa hivyo katika jamii ya Wayahudi na nyakati za Kanisa la Kwanza

1.       Kujifunza kutoka kwa Wayahudi – Wayahudi walikuwa na njia maalumu za kuwaandaa vijana wao kiimani na pia waliwafundisha kujitegemea kwa hiyo swala la kujituma na kufanikiwa halikuwa geni katika jamii ya kiyahudi wao walifanya maswala kadhaa yafuatayo:-

 

a.       Waliwandaa kiimani

 

i.                    Kila kijana wa kiyahudi alifundishwa neno la Mungu na kukaziwa kujifunza neno la Mungu hususani torati, walikaziwa wazi kabisa kuwa siri ya mafanikio yao ni kusoma torati kuishika na kumjua Mungu

 

a.       Yoshua 1:8 “Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako,bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.”

 

b.      1Wafalme 2:1-3 “Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema, Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume;uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;”

 

c.       Ezra 7:10 “Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Bwana, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli.”

 

Kwa hiyo Neno la Mungu kwao lilikuwa ni Msingi wa mafanikio yao, mkazo mkubwa uliwekwa hivyo kuwa bila sheria ya Mungu hawawezi kutoboa lakini kama wanataka kusitawi sana na kufanikiwa katika kila kitu wanapaswa kumuweka Mungu kwanza na Mungu angewafanikisha katika maswala yao yote swa na tu na Kristo alivyotufundisha kuwa ili tuzidishiwe mambo mengine lazima tumuweke Mungu mbele na kumpa yeye kipaumbele kwa hiyo tuseme wote bila wewe Mungu mimi sitoboi haleluya

 

Mathayo 6:31-33 “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”

 

Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa wapagani na watu wasiomjua Mungu au wanaoabudu miungu hufunga maduka yao saa za ibada zao na kutoa kipaumbele kwa miungu yao kuliko wale wenye Mungu wa kweli aliyehai, sisi tunapaswa kuwa mstari wa mbele kuliko wao

 

b.      Walifunzwa umuhimu wa maombi na ibada

 

i.                     Vijana wa kiyahudi walifundishwa umuhimu wa kushiriki ibada na maombi, hivyo walishiriki ibada kuanzia ngazi ya kifamilia na ibada za kijamii, walitumia ibada kama njia ya kuonyesha ya kuwa wanamtegemea Mungu walijiimarisha kiimani na iliwajengea ujasiri kuwa Mungu ni kila kitu katika maisha yao.

 

a.       Daniel 6:10 -11“Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.”

 

b.      1Nyakati 4:9-10 “Naye Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze; na mamaye akamwita jina lake Yabesi, akisema, Ni kwa sababu nalimzaa kwa huzuni. Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.”

 

Vijana wa kiyahudi hawakuacha kuomba kwa sababu zozote zile, waliamini kuwa maombi yanaweza kuingilia kati shughuli zao, kazi zao, maisha yao, na kilimo, ufugaji na biashara na kwa kweli Mungu aliweza kuingilia kati mahitaji yao na walifanikiwa sana, kijana wa kikristo akifanikiwa Mungu anapoteza maana na ibada na maombi zinapoteza maana hayo hayakuwa msingi wa tamaduni za kiyahudi.

 

c.       Waliwafunza Historia yao

 

i.                     Wayahudi walihakikisha kuwa vijana wanajifunza historia ya taifa lao na kwa sababu hiyo walizitumia sherehe za kidini kama Pasaka, sikukuu ya vibanda na nyinginezo ili kuwakumbusha Israel matendo makuu ya Mungu

 

a.       Kutoka 12:26-27 “Kisha itakuwa, hapo watoto wenu watakapowauliza, N'nini maana yake utumishi huu kwenu? Ndipo mtawaambia, Ni dhabihu ya pasaka ya BWANA, kwa kuwa alipita juu ya nyumba za wana wa Israeli huko Misri, hapo alipowapiga Wamisri, akaziokoa nyumba zetu. Hao watu wakainama vichwa na kusujudia.”

 

Hayo yalikuwa maswala ya msingi ambayo jamii ya kiyahudi iliipandikiza kwa vijana wao ili wamtangulize Mungu, wajue kuwa Mungu ndiye kila kitu katika maisha yao kabla ya kuwafunza maswala mengine walihakikisha vijana wao kwanza wanamjua Mungu, wanamuabudu Mungu, wanamuomba Mungu wanamtegemea Mungu na wanaheshimu ibada na kila kitu kwenye taifa lao kilionyesha jinsi Mungu alivyowapigania.

 

d.      Walitoa mafunzo ya ujasiriamali

 

i.                     Baada ya kuweka Msingi katika torati, maombi na historia ya taifa lao, wakati huo huo pia vijana wa kiyahudi walifundishwa ujasiriamali, wayahudi waliamini kuwa usipowafundisha vijana kufanya kazi kwa mikono yao wenyewe unawaandaa kuwa wezi, kwa hiyo waliandaliwa kujitegemea, hivyo kulikuwa na stadi za maisha na maswala kadhaa za kufanya ambazo wazazi waliwazoesha ili kuwa wasimamizi wa mali zao na kujitegemea kifedha na kimaisha

 

a.       Mwanzo 37:2 “Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya.”

 

b.      Marko 6:2-3 “Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake.”

 

c.       Matendo 9:36-39 “Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa.Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao.”

 

d.      Matendo 18:1-3 “Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho.Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzalia wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Prisila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafikilia kwao; na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema.”

 

Maandiko yanaonyesha kuwa vijana wa kiyahudi waliandaliwa vizuri kwaajili ya kujikimu kwa mahitaji yao, Yusufu aliandaliwa kuwa msimamizi wa mifugo ya Yakobo, Yesu aliandaliwa kuwa Seremala (Mjenzi) na Dorkas aliandaliwa kuwa mfumaji wa nguo, Paulo, Prisila na Akila walikuwa washona mahema, Ishmael na Esau waliandaliwa kuwa wawindaji.

Kwa hiyo Jamii ya kiyahudi iliwandaa vijana wao kwaajili ya maswala ya kiroho, lakini vile vile kwaajili ya maisha ya kujitegemea na kuwapa stadi mbalimbali za muhimu za maisha Maswala haya yanawawezesha vijana kukua wakijitegemea huku wakiwa na misingi imara ya kiimani na kiuchumi hakuna jambo la kusikitisha duniani kama kuomba au kuwategemea watu kwaajili ya mahitaji yetu na ndio maana Paulo Mtume alifanya kazi kwaajili ya kuwafundisha watu waache uvivu na wasimuelemee mtu

2Wathesalonike 3:7-9 “Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote.Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate.”

Kumbuka: usiilete biashara yako mahali pa ibada! Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Yesu hakupendezwa kabisa na watu waliopageuza mahali pa ibada kuwa sehemu ya biashara kwa faida zao binafsi, kusudi kuu la mahali pa ibada ni kwaajili ya kumuabudu Mungu.

Yohana 2:14-16 “Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng'ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng'ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara.”

Ni halali kufanya biashara kanisani? jibu ni moja kwa moja hapana, kulingana na mafundisho ya Bwana Yesu, Maandiko yanasisitiza utakatifu wa mahali pa ibada, kila nyumba iliyojengwa kwa kusudi la ibada linapaswa kutumika kwa makusudi ya ibada, kuleta bidhaa zako zozote katika nyumba ya Mungu ni ukosefu wa adamu kwa Yesu Kristo mwenyewe,  kwa sababu nyumba yake inageuzwa kuwa soko, kanisani ni mahali maalumu kwaajili ya kuhudumia watu, kiroho na kimwili, kuwafundisha watu neno la Mungu na kuwasaidia kukua kiimani, unapoleta biashara kanisani maana yake ni kuwa unazingatia zaidi faida za kifedha kuliko mahitaji ya waamini, Yesu alikasirishwa san asana mpaka akatengeneza kikoto cha mkambaa kufukuza wote wanaofanya biashara nyumbani mwake kama una msimamo kumshinda Yesu basi leo ujue kuwa mtazamo wa Yesu ni mtazamo wa Mungu, shughuli za kibiashara zinazotakiwa kufanyika kanisani ni zile tu zinazohusiana na faida za kikanisa na injili, kanisa linaweza kuwa na miradi kwa kusudi la kutoa huduma kwa wahitaji, kama hospitali, shule, vituo vya watoto, Mauzo uya biblia na vitabu vya kiroho katika uatartibu maalumu, lakini swala la kufanya biashara la moja kwa moja kanisani hata kama ni baada ya ibada halikubaliki, kanisa linaweza kushiriki katika maswala ya kiuchumi kwaajili ya kufadhili kazi zake za kihuduma

Lakini ni marufuku kuchanganya biashara na kanisa, shughuli za kanisa zinapaswa kulenga kuimarisha Imani na huduma za kijamii na sio kwa sababu ya manufaa ya mtu binafsi, Mtu anayekuja kuabudu akiwa na biashara na anayekuja kuabudu kwa huku moyoni ana mpango wa kununua kitu ulani kwa faida yake moyo wake katika ibada utagawanyika

Luka 10:27  Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.”                          

Ni imani yangu kuwa somo hili litamsaidia kila kijana wa kanisani, kujifunza ujasiriamali na kuelekwa umuhimu wa kujitegemea na kufanya kazi kwa bidii, kwa uaminifu, kwa wema, na kwa sifa muhimu zinazojenga mahusiano na kujenga mtandao mzuri wa kibiashara na kufanikiwa neema iwe juu yako!, Bila kuathiri uhusiano wetu na Mungu!

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima.

+255 718 990 796