Kutoka 4:24-26 “Ilikuwa walipokuwa njiani
mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika
jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake
akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi.Basi akamwacha. Ndipo
huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.”
Utangulizi
Mojawapo ya wanawake muhimu sana
katika imani na ambaye ni kama umuhimu wake hauonekani ni Sipora aliyekuwa mke
wa Musa ambaye aliozwa na Baba yake aliyekuwa kuhani mkuu wa Midian, Mwanamke
huyu aliwahi kuyaokoa maisha ya Musa aliyetaka kuuawa na Mungu kutokana na
kupuuzia maswala ya sheria ya tohara, na kwa namna ya haraka sana Sipora
aliyefahamu sana mapenzi ya Mungu kwa kina na kwa huduma ya kikuhani yaani
huduma ya upatanishi alimuokoa Musa na kutufundisha kuwa alikuwa mwanamke
hodari, jasiri aliyejaa imani na aliyeyajua mapenzi ya Mungu, ni mwanamke aliyekuwa
na huduma ya upatanisho alimpatanisha Musa kwa Mungu
2Wakorintho 5:18-19 “Lakini vyote pia
vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye
alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo,
akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia
ndani yetu neno la upatanisho.”
Sipora ni mwanamke mwenye asili
ya Afrika, Ethiopia ndiye ambaye leo Bwana anataka tujifunze kitu kupitia yeye
na kuinua imani za wanawake wa Kikristo na kujifunza pia kupitia yeye katika
maisha yetu ya imani, Tutajifunza somo hili Sipora mwanamke Mpatanishi kwa
kuzingatia maswala kadhaa yafuatayo:-
·
Sipora ni nani?
·
Sipora mwanamke mpatanishi
·
Mambo ya kujifunza kutoka kwa Sipora
Sipora ni nani?
Sipora alikuwa binti wa kuhani
mkuu wa Midian aliyejulikana sana katika torati kama Yethro au (Reuel). Sipora
aliolewa na Musa katika wakati mgumu wa maisha ya Musa, wakati Musa akiwa
uhamishoni jangwani kufuatia kukimbia hasira ya Farao baada ya yeye kuua raia
wa Misri, kwa hiyo ni katika wakati huo mgumu binti huyu alifanyika faraja
kubwa sana kwa Musa
Kutoka 2:11-16 “Hata siku zile, Musa
alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao.
Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. Basi akatazama
huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha
ndani ya mchanga. Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania
walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga
mwenzako? Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu
yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa,
akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana.Basi Farao alipopata habari, akataka
kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya
Midiani; akaketi karibu na kisima. Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti
saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi
la baba yao.”
Kutoka 2:17-22 “Wachungaji wakaja
wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi
lao.Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema
leo? Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi
ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi. Akawaambia binti zake, Yuko wapi
basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula. Musa akawa radhi kukaa
kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora.Huyo akamzalia mwana,
akamwita jina lake Gershomu, maana alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni.”
Sipora anakuwa mfano wa wanawake
wapatanishi aliyeokoa maisha ya Musa kupitia huduma yake ya kikuhani
aliyoifanya kwa uamuzi wa kuokoa maisha ya Musa kwa haraka sana wakati Mungu
alipotaka kumuua Musa kwa sababu za kutokuwatahiri watoto wake wa kiume ona
Kutoka 4:24-26 “Ilikuwa walipokuwa njiani
mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika
jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake
akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi akamwacha. Ndipo
huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.”
Tukio hili ni moja ya tukio
muhimu liinalomuingiza Sipora katika orodha ya wanawake jasiri, wastahivu,
wenye imani na ujasiri na upendo halisi kwa mume wake na ambaye alikuwa na
uelewa wa juu sana wa kiungu, Sipora ni kama anaonekana alikuwa anamjua Mungu
wa Musa, ambaye kimsingi pia alikuwa Mungu wa Yethro baba yake, na desturi zake
kwa sababu alijua Hasira za Mungu huyo na namna ya kumtuliza na alijua namna ya
kumkinga mumewe na watoto wake, Sipora alitoa dhabihu ya damu ya govi ya mwanae
na kuzuia ghadhabu ya Mungu kumshukia Musa, ushujaa na ujasiri mkubwa na ujuzi
kuhusu Mungu aliokuwa nao Sipora unatufundisha kuwa hakuna jambo la maana
duniani kama wanawake kumjua Mungu, Mwanamke akimjua Mungu na sheria zake sio
tu atakuwa mwokozi wa familia yake bali atakuwa mwokozi wa taifa na ulimwengu
kwa ujumla, Kama Musa angeuawa ukweli kuhusu Historia ya Musa ungekuwa kwa mtu
mwingine, tunajua Mungu angewaokoa wana wa Israel kutoka Misri, lakini labda
sio kupitia Musa kama Sipora hangemuokoa katika tukio hili. Dunia nzima leo
inafuata taratibu nyingi za sheria zilizoandikwa na Musa, hata wanasheria
wanaposoma asili ya sheria duniani hawaachi kumtaja Musa kama moja ya
waanzilishi wa sheria ambayo ilitoka kwa Mungu, hata hivyo nyuma ya mgongo wa
Musa alikuwepo Sipora mwanamke mweusi wa ukoo wa kikuhani wa Yethro Mmidiani. Hii
ndiyo inayotupa shauku katika siku ya leo kujifunza kwa kina na mapana na
marefu na kutaka kumjua yeye na familia yake.
Sipora ni nani hasa? Ni vigumu
sana kumjua Sipora vizuri kwa sababu habari zake hazikupewa umuhimu mkubwa na
waandishi wa torati, penginepo ni kwa sababu ya jamii ya kiyahudi kutokuwapa
umuhimu mkubwa wanawake, ama pia kwa sababu ya familia za kikuhani ambazo mara
kadhaa ziliwataka wanaume kujitenga na wanawake kama sehemu ya usafi na
utakatifu pale wanapofanya huduma zao kwa Mungu kwa mujibu wa sheria au torati
Kutoka 19:10-15 “BWANA akamwambia Musa,
Enenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao,wawe tayari
kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu BWANA atashuka katika mlima wa Sinai
machoni pa watu hawa wote.Nawe utawawekea mipaka watu hawa pande zote, ukisema,
Jihadharini, msipande mlima huu, wala msiuguse, hata mapambizo yake; kila mtu
atakayeugusa mlima huu, bila shaka atauawa. Mkono wa mtu awaye yote usimguse
mtu huyo, ila hakika yake atapigwa kwa mawe, au kupigwa kwa mkuki; kwamba ni
mnyama au kwamba ni mwanadamu, hataishi. Hapo panda itakapotoa sauti kwa
kufuliza ndipo watakapoukaribia mlima. Musa akatelemka mlimani akawaendea watu
akawatakasa, nao wakafua nguo zao. Akawaambia watu; Mwe tayari siku ya tatu;
msimkaribie mwanamke.”
Sipora alikuwa Binti Mkubwa wa Yethro
kuhani mkuu wa Midian ambaye anatajwa kuwa alikuwa na mabinti saba, Sipora
alikuwa na uelewa mkubwa kuhusu Mungu kwa sababu alikuwa amejifunza sheria zote
za ukuhani na kumjua Mungu wa baba yake, Baba wa Sipora alikuwani kuhani mkuu
wa Midian kwa hiyo ni wa uzao wa Ibrahimu ni ndugu wa wayahudi pia, wote
tunakumbuka kuwa Ibrahimu ukiacha ya kuwa alikuwa amemzaa Ishmael na Isaka pia
alikuwa na watoto wengine wa kume sita aliowazaa kupitia Ketura na katika hao
Midian ni mmoja wao ona:-
Mwanzo 25:1-6 “Ibrahimu alioa mke mwingine
jina lake akiitwa Ketura. Akamzalia Zimrani, na Yokshani, na Medani, na
Midiani, na Ishbaki, na Sua. Yokshani akamzaa Sheba, na Dedani; na wana wa
Dedani walikuwa Waashuri na Waletushi, na Waleumi. Na wana wa Midiani walikuwa,
Efa, na Eferi, na Hanoki, na Abida, na Eldaa. Hao wote walikuwa ni wana wa
Ketura. Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. Lakini wana wa masuria
aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali
alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka
nchi ya Kedemu.”
Kwa hiyo unaweza kuona kuwa
katika hawa watoto wengine wa Ibrahimu wanaotajwa hapo juu Midiani ni wanne
kati ya watoto sita aliozaa Ibrahimu kupitia Ketura unaona? Je watoto hawa wa
Ibrahimu walimjua Mungu? Walijua kutenda haki? Waliyashika mafundisho yote
ambayo Bwana alikuwa amemfundisha Ibrahimu? Jibu ni NDIO kwa herufi kubwa sana kwa nini kwa sababu Mungu alimchagua Ibrahimu
kwa sababu alijua kuwa Ibrahimu atakuwa Mwalimu mzuri sana kwa watoto wake wote
na wakazi wote wa nyumbani mwake na kuwa kupitia yeye wataishika njia ya Bwana
na watafanya haki, na hukumu. Kwa hiyo watoto wote wa Ibrahimu walikuwa werevu
na wajuzi wa sheria za Mungu na hukumu zake akiwepo Yethro kutoka ukoo wa
Midian! Unaona?
Mwanzo Mwanzo 18:17-19 “BWANA akanena, Je!
Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari,
na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba
atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye
haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake.”
Kwa hiyo ni wazi kupitia Ibrahimu
na uzao wake sasa kupitia Midiani na kuja kwa Yethro ni wazi kuwa Sipora na
wadogo zake walimjua Mungu, na walifahamu utaratibu wote wa Mungu wa baba yao,
Yethro alikuwa ni kuhani wa Mungu wa ngazi ya juu sana anapokuwepo Yethro sio
rahisi Musa na Haruni kusongeza dhabuhi kwa Bwana kwa sababu Yethro alikuwa na
ujuzi mkubwa zaidi na ni kuhani wa Mungu aliyejuu zaidi yao
Kutoka 18:8-12 “Musa akamwambia mkwewe mambo hayo yote BWANA aliyomtenda
Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na mambo mazito yote yaliyowapata
njiani, na jinsi BWANA alivyowaokoa.Yethro alifurahi kwa ajili ya wema wote
BWANA aliowatendea Israeli, kwa alivyowaokoa mikononi mwa Wamisri. Kisha Yethro
akasema, Na ahimidiwe BWANA aliyewaokoa na mikono ya Wamisri, na mkono wa
Farao; aliyewaokoa watu hao watoke mikononi mwa Wamisri.Sasa najua ya kuwa
BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa
unyeti.Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na
Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa
mbele za Mungu.”
Kwa msingi huo utaweza kukubaliana
nami kuwa Israel ambao wameishi Misri katika nyumba ya upagani mzito kwa miaka
430 tangu baba yao aliposhuka Misri na kizazi cha kina Yusufu, uwezo wao wa
kumjua Mungu ni lazima ulikuwa umeathirika sana kumbuka wakati huo hakukuwa na
Sheria bado, na hata Musa mwenyewe hangekuwa na ujuzi mkubwa wa kutosha kuhusu
kumjua Mungu kama asingelipata muda wa kujifunza kutoka kwa Yethro, ni wazi
kuwa Yethro na familia yake walikuwa wanamjua Mungu aliye hai, na walihusika
sana kumsaidia Musa kujua maswala ya Mungu, huku Sipora akiwa binti hodari
mwenye uwezo mkubwa wa kumjua Mungu na taratibu zake hata japokuwa alikuwa
mwanamke na hakuwa nabii lakini alikuwa mshauri mkubwa sana wa Musa, Sio hivyo
tu Sipora na familia yake wamekulia jangwani hivyo walilijua jangwa vizuri sana
na ndio maana utaweza kuona alipokuja Yethro na kumleta Mke wa Musa pamoja na
watoto, Musa sasa alikuwa akimsikiliza mkewe zaidi kuliko Miriam na Haruni ndio
sababu Miriam aliona wivu na wakaanza kumteta na kumshambulia kwa ubaguzi wa
rangi yake kama mwanamke Mkushi yaani mwanamke mwenye ngozi nyeusi (Ethiopian).
Ona:-
Kutoka 18:1-7 “Basi Yethro, kuhani wa
Midiani, mkwewe Musa, alisikia habari ya mambo hayo yote Mungu aliyokuwa
amemtendea Musa, na Waisraeli watu wake, jinsi BWANA alivyowaleta Israeli
watoke Misri. Ndipo Yethro mkwewe Musa akamtwaa Sipora, mke wa Musa, baada ya
yeye kumrudisha, pamoja na wanawe wawili; katika hao, jina la mmoja ni
Gershomu, maana alisema, Mimi nimekuwa mgeni katika nchi ya ugenini; na jina la
wa pili ni Eliezeri, kwa kuwa alisema, Yeye Mungu wa baba yangu alikuwa msaada
wangu, akaniokoa na upanga wa Farao. Basi Yethro, mkwewe Musa, pamoja na mke wa
Musa na wanawe wawili wakamwendea Musa huko nyikani, hapo alipokuwa amepanga,
kwenye mlima wa Mungu; naye akamwambia Musa, Mimi Yethro mkweo nimekuja kwako,
na mkeo, na wanawe wawili pamoja naye. Basi Musa akatoka nje ili amlaki mkwewe,
akasujudia na kumbusu; nao wakaulizana habari; kisha wakaingia hemani.”
Ujio wa Sipora kutoka nyumbani
kwa Yethro kuungana na Musa mumewe na Musa kumpa kipaumbele unapelekea Haruni
na Miriam kuona kama wanapoteza nafasi yao kwake na wakaanza kumsema vibaya
jambo lililopeleka Mungu kuingilia kati na kuchukua hatua kali sana kwa Miriamu
Hesabu 12:1-13 “Kisha Miriamu na Haruni
wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa
amemwoa mwanamke Mkushi. Wakasema,
Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia
maneno yao. Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote
waliokuwa juu ya uso wa nchi. Bwana akanena ghafula na Musa, na Haruni na
Miriamu, na kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania.
Basi hao watatu wakatoka nje. Bwana akashuka katika nguzo ya wingu akasimama
pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote
wawili. Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu,
Mimi, Bwana, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo
ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote;
Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la
Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo
Musa? Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake. Kisha hilo wingu
likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma,
mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma.
Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu nakusihi sana usituwekee dhambi
juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi. Nakusihi, asiwe
kama mmoja aliyekufa, ambaye nyama ya mwili wake nusu imelika hapo atokapo
tumbo la mama yake. Musa akamlilia Bwana, akasema, Mpoze, Ee Mungu, nakusihi
sana.”
Unaona nadhani sasa unapata
Mwanga jinsi Sipora alivyokuwa wa muhimu, Sipora ni mwanamke Jasiri, mwanamke
aliyejaa imani, mwanamke mwenye upendo, mwanamke kiongozi, mwanamke anayelijua
jangwa vizuri, alikuwa na utulivu wa ajabu sana na ndio maana hata katika hali
ngumu aliweza kufanya maamuzi sahihi na kutuliza hasira za Mungu dhidi ya
mumewe, alikuwa mshauri mzuri wa Musa mpaka Miriam aliona wivu, alisengenywa
lakini yeye na Musa walikaa kimya, unaweza kuchunguza kwa kina kuwa aliyekuwa
anasemwa hapo sio Musa bali ni mwanamke huyu mwenye rangi nyeusi, hapa maandiko
yanamtaja kama mwanamke mkushi neno kushi katika Biblia ni “Ethiopia” Ethiopia ni neno la kigiriki/kiyunani ambalo tafasiri yake
ni “Of burned face” yaani watu weusi au walioungua uso na lilitumika kumaanisa
watu wa Afrika hususani inchi iliyokuwa inafikika kwa bara bara kwa wakati huo
ilikuwa ni Ethiopia kwa hiyo wakushi
kimsingi walikuwa ni watu wenye ngozi nyeusi yaani mwafrika na walijulikana kwa
ngozi yao nyeusi katika maandiko ona
Yeremia 13:23 “Je! Mkushi aweza kuibadili
ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda
mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.”
Kwa hiyo unaweza kupata picha kuwa
Musa yeye alikuwa ameoa binti huyo Sipora aliyekuwa mweusi mtoto wa kuhani wa
Midian. Lakini mwenye ujuzi mkubwa kuhusu Mungu, malezi mazuri, Jasiri, mwenye
kujaa Imani, mwenye upendo na mpatanishi na mwenye kulijua jangwa ni mwanamke
huyu ndiye tunajifunza habari zake leo.
Sipora mwanamke mpatanishi
Jinsi ambavyo Sipora alimuokoa
Musa na kuwa mpatanishi kati ya Musa na Mungu ndio habari ya mjini katika siku
hii ya leo, tukio hili lilikuwa ni tukio la namna gani, kwa sababu watu wengi
wanashindwa kulibainisha lilivyokua lakini swala la msingi ni kuwa matendo na
maneno ya Sipora yalimuokoa Musa katika tukio hilo hebu tulione tena katika
maandiko
Kutoka 4:24-26 “Ilikuwa walipokuwa njiani
mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika
jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake
akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. Basi akamwacha. Ndipo
huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.”
Ni tukio linaingizwa ghafla
katika maandiko, Musa alipokuwa njiani akiwa pamoja na familia yake alikutana
na Bwana na Bwana alitaka kumuua! Inaonekana kuwa kosa kubwa hapa ni kuwa Musa
alikuwa hajawatahiri watoto wake na au alikuwa amepuuzia hivyo Mungu
alichukizwa na hilo, hapa ndio tunajua kuwa Sipora alikuwa anajua umuhimu wa
tukio hilo, kwani Musa huenda alishikwa na tatizo la ghafla na kwa ujasiri
mkubwa mwanamke huyu alishika kisu cha jiwe gumu na kumtahiri mtoto na kuibwaga
miguuni pake na kusema hakika wewe u bwana harusi wa damu kwangu mimi, Biblia
ya kiingereza ya NRSV inasema
aliikata govi ya mwanae wa kiume na kuitupa katika miguu ya Mungu na kusema
maneno kwa kiebrania (Dậm
Chậthận)
Baba mkwe wa Damu! Kwa hiyo aliitupa govi ya kijana katika miguu ya Mungu au
aliiweka miguuni pa Mungu, na kwa sababu hiyo Musa na yeye wakawa wazima, bila
tukio hili Musa angepigwa na Mungu kwa sababu ya kupuuzia agizo hili ambalo
Mungu alimuamuru Ibrahimu, lakini kwa ushujaa wa Sipora na uelewa wake kuhusu
tabia ya Mungu Musa aliokolewa na kuendelea na majukumu ya kazi ya ukombozi.
Sipora ni mwanamke wa kipekee na jasiri
historia yake inatukumbusha kuwa hata katika hali ngumu wanawake wanaweza
kujivika ujasiri, kutoka kwa Mungu, na kuwa wanaweza kuwa na ujuzi kuhusu Mungu
na kusababisha wokovu mkubwa kwa familia yao na taifa na kufanikisha njia za
Mungu, wanawake wanaweza kusimama kwa ujasiri na kuwapatanisha watu kwa Mungu,
wanawake ndio waliokuwa wa kwanza kufika kaburini wakati Yesu amefufuka, na
mwanamke msamaria aliwaleta wasamaria wengi kwa Yesu, Mungu anaweza kuwatumia
wanawake na Imani ya kweli hukaa na wanawake na ndio maana Mungu hajawahi
kuwapuuzia na aliwataka waisrael kutokuoa wanawake mabaradhuli, na wasiomcha
Mungu kwani wanawake wanauwezo wa kugeuza moyo wa mwanaume hata kama ana hekima
kiasi gani, hivyo kila mtumishi wa Mungu anapaswa kuoa mwanamke mcha Mungu kama
alivyo Sipora mwanamke anayemjua Mungu na njia za Mungu na sio wanawake
mabaradhuli wasio mcha Mungu.
1Wafalme 11:1-6 “Mfalme Sulemani akawapenda
wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa
Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, na wa mataifa Bwana
aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa
hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa
kuwapenda.Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao
wakeze wakamgeuza moyo.Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake
wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu
kwa Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake.Kwa kuwa Sulemani akamfuata
Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni.Sulemani
akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, wala hakumfuata Bwana kwa utimilifu,
kama Daudi baba yake.”
Wanaume wanapaswa kuwa makini ni
aina gani ya mwanamke wanamuoa, ni ukweli usiozuilika kuwa hata uwe na hekima
kiasi gani kama utapata mwanamke asiyemjua Mungu wala kuheshimu mambo ya Mungu
na wito wako wa kiungu huduma yako itasambaratika, Huduma ya Musa iliweza
kusimama na hata maisha yake kuwa salama kwa sababu alikuwa na mwanamke
muelewa, wakati Sulemani aliharibikiwa kwa sababu ya wanawake, ni hatari hata
kuoa mwanamke mchanga kiroho asiyelijua vema neno la Mungu wala hamjui Mungu
wake inaweza kuleta madhara makubwa na kuwakosesha watu Baraka ambazo Mungu
alizikusudia kwa watu wake, kama Sipora angekuwa mwanamke wa hovyo leo historia
ya Israel na ushujaa wa Musa usingeliweza kuonekana, jina la Bwana na
libarikiwe pia kwaajili ya malezi mazuri ya Yethro na ushauri na mafunzo yaliyomsaidia Musa na wana wa
Israel kwa ujumla.
Mambo ya kujifunza kutoka kwa Sipora
Je umewahi kukutana na hali ngumu
ambayo kwa jiyo ulihitaji mwanamke jasiri kama wa Sipora? Unawezaje kuimarisha
imani yako ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali? Unawezaje kuonyesha
upendo usio na mipaka kwa wale tunaowapenda?
Sipora ni mfano na majibu kwa
kila mmoja kwa sababu alitatua changamoto katika njia za kiungu, ameonyesha
kuna faida kubwa sana katika kumjua Mungu aliye hai na njia zake, na
anawakumbusha wanawake kujiamini katika Mungu
Kila mwanamke akumbuke kuwa
anaweza kuwa mwenye nguvu na uwezo mkubwa, usiruhusu chochote kukuzuia kufikia
malengo yako jifunzeni kutoka kwa Sipora na amini katika Mungu na kujijengea
ujasiri na imani, hata kama watu hawamzungumzii sana Sipora, kama wanawake leo
wanavyopuuziwa katika jamii nyingi, Roho
Mtakatifu leo ametaka ujifunze kitu na uwe mwenye kumcha Mungu na kumjua
Mungu na kusifiwa kwa uchaji wa Mungu na
kwa kufanya tukio lililo jema tafadhali kuwa mwema mche Mungu kama Sipora,
uiokoe jamii yako na taifa stay blessed !
Mithali 31:29-30 “Binti za watu wengi
wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote. Upendeleo hudanganya, na uzuri ni
ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni