Marko 16:15-18 “Akawaambia, Enendeni
ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa
ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio;
kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa
lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru
kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”
Utangulizi:
Kunena kwa lugha ni moja ya
kipawa cha Roho Mtakatifu kinachotolewa kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu
huyo, kuwa na uwezo wa kuzungumza lugha nyingine ya wanadamu au malaika kwa
uwezo wa Roho Mtakatifu, kipawa hiki kinatajwa na kuelezewa mara kadhaa katika
maandiko hususani ya Agano Jipya na kwa sababu hiyo ni muhimu kwetu, kuchukua
muda na kujifunza kwa kina na mapana na marefu, ili tuweze kuelewa umuhimu
wake, faida zake na uhalisia wake, hii ni kwa sababu kama ilivyo kwa fundisho
la utatu, na uungu wa Yesu, na hata uwepo wa Roho Mtakatifu, kitheolojia yamekuwa
na mijadala mikubwa sana ambayo inapelekea watu kutilia shaka kuhusu mafundisho
hayo hali kadhalika swala la kunena kwa Lugha. Na hivyo kupelekea kuwepo na
upungufu wa kuzingatia umuhimu na faida za karama hii ya kunena kwa lugha,
Bwana ampe neema kila mmoja wetu kufuatilia na kuelewa kwa kina ili tuweze
kufaidika na uwepo wa kipawa hiki kwa faida ya ufalme wa Mungu: Tutajifunza
somo hili Umuhimu kwa kunena kwa lugha kwa
kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
·
Ukweli kuhusu kunena kwa lugha.
·
Umuhimu wa kunena kwa lugha.
Ukweli kuhusu kunena kwa lugha.
Ni muhimu kufahamu kuwa swala la
kunena kwa lugha sio swala la mzaha na dhihaka kama watu wengine wanavyofikiri,
kunena kwa lugha ni ishara kamili na ni kipawa kamili kutoka kwa Baba wa mianga
kama jinsi ambavyo Yesu Kristo mwenyewe alivyoahidi na kusema kuhusu swala
hilo, sio hivyo tu, maandiko yamelitaja swala la kunena kwa lugha katika
mazingira toshelevu ya kuwa na uwezo wa kufanya fundisho kupitia swala hilo:-
Marko 16:15-18 “Akawaambia, Enendeni
ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa
ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio;
kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa
lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru
kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”
Yakobo 1:16-17 “Ndugu zangu wapenzi,
msidanganyike.Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili,
hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli
cha kugeuka-geuka.”
Kunena kwa lugha kupo, na ni
karama au kipawa kutoka kwa Mungu, maandiko hayo hayako kwa bahati mbaya, Yesu
mwenyewe aliahidi ya kuwa wale wanaomuamini watafuatiwa na ishara mbalimbali, ikiwemo
hii ya kunena kwa lugha mpya, hiki ni kipawa kamili kutoka kwa baba wa mianga
ambaye kwake hakuna kivuli cha kugeuka geuka, kwa msingi huo ni ukweli
usiopingika kuwa zawadi hii ya kunena kwa lugha ipo na imethibitishwa katika
maandiko, bahati mbaya Makanisa mengi na
baadhi ya madhehebu wana maoni tofauti tofauti kuhusu kunena kwa lugha hata
hivyo eneo pekee ambalo tunaweza kujifunza na kuelewa kwa kina kuhusu karama
hii ni kwenye neno la Mungu tu.
-
Matendo
2:3-4 “Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama
ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho
alivyowajalia kutamka.”
-
Matendo
10:44-46 “Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho
Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.Na wale waliotahiriwa,
walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu
Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu.
Ndipo Petro akajibu,”
-
Matendo
19:1-6 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo,
akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha
wa kadha huko; akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu,
La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia. Akawauliza, Basi
mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema,
Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja
nyuma yake, yaani, Yesu.Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.Na
Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.”
-
1Wakorintho
14:2 “Maana yeye
anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna
asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.”
-
1Wakorintho
13:1 “Nijaposema
kwa lugha za wanadamu na za malaika,
kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.”
Kwa ushahidi wa maandiko kadhaa
hapo tunaweza kukubaliana ya kuwa maandiko yanatambua kuwa iko ishara ya kunena
kwa lugha na nyakati za kanisa la kwanza ilikuwa ni jambo la kawaida kwa wakristo
waliobatizwa kwa Roho Mtakatifu kunena kwa lugha, na maandiko yameweka wazi hilo,
kwa hiyo hatuwezi kupingana na neno kuhusu hili.
Umuhimu wa kunena kwa lugha
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
makanisa mengi sana watu wengi wanapuuzia swala zima la kunena kwa lugha kwa
sababu wanadhani au kufikiri kuwa neno la Mungu linasema kuwa kunena kwa lugha
kutakoma, lakini hiyo haimaanishi tukiwa ulimwenguni, kunena kwa lugha kutakoma
tutakapofika mbinguni, kwa sababu tukifika mbinguni kunena kwa lugha kutapoteza
umuhimu wake kwa sababu kule kila kitu kitakuwa kamili au kitakamilika kwa Mungu
1Wakorintho 13:9-12 “Kwa maana tunafahamu
kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili,
iliyo kwa sehemu itabatilika.Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto
mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea
hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto.Maana wakati wa sasa
tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa
sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa
sana.Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo
lililo kuu ni upendo.”
Wako pia wale wanaoamini katika
kunena kwa lugha lakini pia hawaoni umuhimu wa kuendelea kunena kwa lugha aidha
kwa kufikiri kuwa kunena kwa lugha hakuna umuhimu, hapa sizungumzii karama ya
aina za lugha, nazungumzia kunena kwa lugha ambako ni fungu la kila mtu
aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu, Kunena kwa lugha hakutokei mara moja pale tu
mtu anapokuwa amebatizwa kwa Roho Mtakatifu lakini linapaswa kuwa swala endelevu
ambalo lina faida kubwa sana, hapa yako maswala kadhaa yanayosisitiza umuhimu
wa kunena kwa lugha sawa na neno la Mungu.
1.
Kusema
na Mungu. - Kunena kwa lugha uwe
unajua hiyo lugha au huitambui lakini kuna kupa neema ya kuzungumza na Mungu na
sio wanadamu, kwa hiyo kunena kwa lugha ni mawasiliano ya siri kati ya mtu na
Mungu ambayo mwanadamu hawezi kuyaelewa, kwa hiyo roho ya mtu aliyeokoka na
kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, inawasiliana na Mungu moja kwa moja japokuwa
huwezi kupanga kuhusu kunena kwa lugha lakini hatuna budi kuchochea kwa kina
swala zima la kunena kwa lugha kutokana na umuhimu wake.kwani Mtu anaponena kwa
lugha anazungumza na Mungu moja kwa moja maswala yote ya siri katika roho yake.
1Wakorintho 14:2 “Maana
yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna
asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika
roho yake.”
2.
Kujijenga
kiroho - Kunena kwa lugha pia
kunamjenga kiroho, yeye anenaye kwa lugha, kujijenga kiroho kuna maanisha nini
kunamaanisha kuwa unaponena kwa lugha unaimarisha imani yako na kuijimarisha
kiroho wakati huo akili yako haina matunda yaani haijui kile unachokizungumza
lakini roho yako ndani yako inaomba katika kiwango kilicho bora zaidi, ambacho
kimsingi kinaimarisha hali yako ya kiroho unajijenga. Kumbuka pia kunena ka
lugha pia kunaitwa kuomba kwa roho katika maandiko.
1Wakorintho 14:3-4 “Bali yeye ahutubuye, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji,
na kuwatia moyo.Yeye anenaye kwa lugha
hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa.”
Yuda 1:20 “Bali
ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani
yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika
Roho Mtakatifu,”
1Wakorintho 14:14-15 “Maana nikiomba kwa lugha, roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda. Imekuwaje, basi?
Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; mtaimba kwa roho, tena nitaimba
kwa akili pia.”
3.
Kumwadhimisha
Mungu – Kunena kwa lugha kunakufanya umwadhimishe Mungu yaani umuabudu Mungu
katika namna ya ndani sana, Na kumshukuru, Roho Mtakatifu anatusaidia kumuabudu
Mungu katika namna ambayo kibinadamu ni ngumu kuelezea naweza kusema ni kama
mnenaji kwa lugha ni kama anazungumza akiwa mbinguni katika ulimwengu wa roho,
na ndio maana tunaambiwa katika maandiko kuwa mara baada ya Kornelio na watu wa
nyumbani mwake kubatizwa katika Roho Mtakatifu walianza kumwadhimisha Mungu
yaani kuuabudu kwa ndani na kumshukuru Mungu, lugha inakusaidia kumuabudu Mungu
kwa usahihi.
Matendo 10:44-47 “Petro
alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile
neno. Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja
pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.
Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na
kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu, Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa
wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?”
4.
Mlango
wa maisha ya ushindi – Moja ya siri kubwa sana ya mafanikio ya kunena kwa
lugha ni pamoja na kukupa maisha ya ushindi, na kukupandisha kiroho pamoja na
kuchochewa kwa karama za Rohoni, Kama unataka kuona hayo katika maisha yako
chochea zoezi hili la kunena kwa lugha na utakuja kukubaliana nami kuwa kadiri
unavyonena kwa lugha sana utagundua kuwa unapanda juu sana kiroho na kuchochea
karama nyingi sana za rohoni, na kadiri unavyoacha utaona upungufu, watu wa
Korintho walikuwa wananena kwa lugha na walikuwa na karama nyingi sana za
rohoni lakini Paulo Mtume aliwaambia watamani sana karama zilizo kuu, karama
zilizokuu maana yake kadiri mtu anavyotumia lugha katika mawasiliano na Mungu
anajiweka katika nafasi ya kuchochea uwepo wa Mungu na karama za Roho na
kutumiwa na Mungu zaidi.
1Wakorintho 14:1 “Ufuateni
upendo, na kutaka sana karama za rohoni, lakini zaidi kwamba mpate kuhutubu.”
1Wakorintho 12:31 “Takeni
sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora.”
Kunena kwa lugha
ni njia ya kipekee sana ambayo Mungu ametupa kwaajili ya kujijenga binafsi,
kujenga roho zetu, hii ni njia ya kujiimarisha kiroho na kuimarisha mahusiano
yetu, na kumuabudu Mungu, tunapoomba kwa roho yaani kunena kwa lugha roho
iliyoko ndani yetu na Roho wa Mungu yaani Roho Mtakatifu anatusaidia kutuombea
na kujiweka katika nafasi nzuri kwaajili ya mambo yajayo kwani yeye anayajua
Yohana 16:13-14 “Lakini
yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa
maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena,
na mambo yajayo atawapasha habari yake.Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa
katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.”
1Wakorintho 2:19-15 “Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho
Huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana Ni nani katika binadamu ayajuaye
mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo
ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya
dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na
Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu,
bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya
rohoni. Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu;
maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa
jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na
mtu.”
5.
Kuomba
kwa usahihi zaidi – Kunena kwa lugha kunamsaidia mnenaji kuomba kwa njia
inayomlingana Mungu, na hasa kuomba sawa na mapenzi ya Mungu kwa sababu kwa
akili zetu na nguvu zetu kibinadamu hatujui kuomba kama jinsi itupaswavyo
kuomba, kwa hiyo tunapoomba katika Roho Mtakatifu yaani kwa kunena kwa lugha
tunajiweka katika nafasi ya kuomba kwa usahihi na kuboresha maisha ya maombi,
bila Roho Mtakatifu ni vugumu kuwa waombaji lakini ni Roho wa Mungu ndani yetu
na kupitia kunena kwa lugha tunaweza kuboresha kwa kiwango kikubwa sana maisha
ya maombi, na kuongezea neema ya kuwa waombaji wenye maombi yenye kutosheleza
na yenye kutuletea majibu na utaratibu ulio sahihi zaidi.
Warumi 8:26-27 “Kadhalika
Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo,
lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye
aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama
apendavyo Mungu.”
Zecharia 12:10 -11 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu,
roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao
watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona
uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake
wa kwanza.Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama
maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.”
6.
Kuimarisha
uhusiano wetu na Mungu - Wote tunafahamu jinsi lugha yoyote duniani
ilivyo ya muhimu, iwe ni ya kuzungumza, au ya alama, au ya kimatendo, wote
tunafahamu kuwa ubora na uzuri mkubwa wa lugha ni katika kuwasiliana na kujenga
uhusiano, lugha ndiyo inayoruhusu kujielezea, na kuelezea hisia zetu, mawazo
yetu shauku yetu na matakwa yetu. Kama hatuna ujuzi wa mawasiliano ni vigumu
kwetu kueleweka ipaswavyo, ndani ya lugha kuna msingi wa mawasiliano, uhusiano,
utamaduni, ukaribu, silaha, usalama, na nafasi, na kuunganisha, hii ndicho kinachotokea
kati ya mtu aliyeokoka na Mungu pale tunaponena kwa lugha tunaimarika kila kitu
katika uhusiano wetu na Mungu, hii haimaanishi kuwa Mungu hasikii lugha
nyingine hapana lakini kwa njia rahisi tunaweza kusema kunena kwa Lugha ni
lugha ya rohoni au ni lugha ya Mungu, ni Lugha ya Roho Mtakatifu, wote
tunafahamu pale inapotokea ukikutana na mtu wa ngozi yako, rangi yako na lugha yako
katika eneo la ugenini, jinsi inavyoleta msisimko mkubwa sana na kutaka kujuana
na kuwasiliana ndicho kinachotokea pale unapozungumza na Mungu kwa kunena kwa
lugha.
1Wakorintho 14:2 “Maana
yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna
asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake.”
7.
Kukabiliana
na changamoto za kiroho – Kunena kwa lugha kunazalisha nguvu na nguvu mpya
na kunazalisha upako kutoka kwa Roho Mtakatifu unaotusaidia kukabiliana na changamoto
zozote za kiroho, Paulo mtume alikabiliana na changamoto nyingi sana, alifanya
kazi kuliko mitume wote, alitumiwa na Mungu kwa viwango vikubwa sana lakini
moja ya sababu kubwa ya yeye kuwa imara sana ni kwa sababu alinena sana kwa
lugha, kunena kwa lugha sana au kuliko wengine ni wazi kuwa pia alikuwa na
maisha ya maombi sana kuliko wengine na unaweza kuona utajiri wa kila karama
aliokuwa nao, na utendaji au kutumiwa na Mungu kwa viwango vikubwa zaidi.
Yuda 1:20 “Bali
ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani
yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika
Roho Mtakatifu,”
1Wakorintho 14:18-19 “Namshukuru Mungu ya kuwa
nanena kwa lugha zaidi ya ninyi nyote; lakini katika kanisa napenda kunena
maneno matano kwa akili zangu, nipate kuwafundisha wengine, zaidi ya kunena
maneno kumi elfu kwa lugha.”
1Wakorintho 15:9-10 “Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa
mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu
nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali
nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya
Mungu pamoja nami.”
Matendo 19:11-12 “Mungu
akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa
wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea,
pepo wachafu wakawatoka.”
Unaweza kuona
muunganiko ulioko kati ya kunena kwa lugha sana, kufanya kazi sana na kutumiwa
na Mungu sana siri ya kutumiwa na Mungu katika neema yake na kumsaidia mtu
kuishi maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu, na kumtumikia Mungu sana na
kutumiwa sana katika ishara na miujiza iko katika kunena kwa lugha sana.
8.
Kupokea
maelekezo ya kiroho – kwa kuwa kunena kwa lugha kunaimarisha uhusiano wetu
na Mungu ni wazi kuwa kila anayenena kwa lugha anazungumza na Mungu na kwa
sababu hiyo ni rahisi kupokea maelekezo, mafunuo, Elimu na hata unabii na
maelekezo ya kimafundisho, kwa hiyo kunena kwa lugha hutuletea ufunuo mkubwa
sana na maelekezo kutoka kwa Mungu ambayo yatatusaidia katika maisha yetu na
huduma na utumishi kwa Mungu.
1Wakorintho 14:5-6 “Nami nataka ninyi nyote mnene kwa
lugha, lakini zaidi sana mpate kuhutubu, maana yeye ahutubuye ni mkuu
kuliko yeye anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi kanisa lipate
kujengwa. Ila sasa, ndugu, nikija kwenu na
kunena kwa lugha, nitawafaidia nini, isipokuwa nasema nanyi kwa njia ya
ufunuo, au kwa njia ya elimu, au kwa njia ya hotuba, au kwa njia ya fundisho?”
9.
Kwaajili
ya kuyatimiza maandiko – Hakuna jambo la msingi na la muhimu kama kutii
maandiko, wakati mwingine utii unaleta Baraka kubwa sana hata kama jambo
tulifanyalo linaonekana kama la kipuuzi, tukumbuke tu kuwa upumbavu wa Mungu
una hekima kuliko maarifa ya kibinadamu, maandiko yanapotutaka tujae Roho, tutembee
kwa Roho, tuishi kwa Roho, tuabudu katika roho na kweli hayo yote hayawezi
kukamilika kama tutaachia nje swala hili la msingi sana la kunena kwa lugha.
Yohana 4:23-24 “Lakini
saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho
na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao
wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”
Warumi 8:11-16 “Lakini,
ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye
aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali
ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu. Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu
wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, kwa maana kama tukiishi
kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili
kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana
wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea
roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba.Roho mwenyewe
hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu”
Wagalatia 5:16-18 “Basi
nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.Kwa sababu
mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi
zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.Lakini mkiongozwa na Roho, hampo
chini ya sheria”
Waefeso 5:18 “ .Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna
ufisadi; bali mjazwe Roho;”
10.
Kwaajili
ya vita vya kiroho – Kunena kwa lugha ni silaha, tunawasiliana kwa siri na
Mungu na kwa sababu hiyo roho zetu huelewana vizuri na Mungu, na kwa sababu
hiyo kutusaidia kupigana vita vya kiroho tukisaidiwa na Mungu kwa namna ya
ajabu sana, kuomba katika roho yaani kunena kwa lugha kumetajwa na Paulo mtume
kama miongoni mwa silaha za Rohoni zinazotusaidia kupata ushindi katika vita
vyetu dhidi ya giza
Waefeso 6:10-18 “Hatimaye,
mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.Vaeni silaha zote
za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.Kwa maana kushindana kwetu
sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa
giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu
hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na
mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli
viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa
Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza
kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu,
na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa
jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”
Aidha utafiti wa
kisayansi uliofanyika mnamo mwaka 2006
na kuandikwa katika gazeti la The new York Times limethibitisha kuwa
watu wanaonena kwa lugha ni mara chache sana kupatwa na tatizo la kiakili, kule
uingereza katika utafiti uliofanywa kwa watu 1000 wanaonena kwa lugha
ilibainika kuwa watu wanaonena kwa lugha wako sawa kihisia kuliko wale
wasionena kwa lugha, na huku kundi linalofuata likiwa ni wale wanaokaa kimya na
kufanya tafakari, kwa hiyo kunena kwa lugha licha ya kukupa ushindi dhidi ya
nguvu za giza unakufanya uwe imara kihisia na kiakili, kisaikolojia na
kukufanya uishi maisha yaliyo sahihi. Kwa hiyo ile hali ya kufikiriwa kuwa
wanaonena kwa lugha labda hawako sawa kiakili imebainika kuwa sio dhana sahihi.
Kwa msingi huo wote tunakubaliana
ya kuwa swala hili ni swala la Muhimu sana, kwamba kunena kwa lugha kuna faida kubwa
sana za kiroho, kwa kila Mkristo aliyebatizwa kwa Roho Mtakatifu kwani
kunatujenga kiroho, kunatufanya kuomba kwa usahihi, kunaimarisha ushirika wetu
na Mungu, kunatupa mafunuo, kunajenga mahusiano na mawasiliano, na Ndio maana
Paulo mtume aliitumia sana zawadi hii ya kunena kwa lugha wewe na mimi
hatunabudi kuhakikisha ya kuwa tunauiga mfano wa Paulo mtume na kuliweka swala
hili katika vitendo kwa kumuhitaji sana Roho Mtakatifu katika kunena kwa lugha
na kuimarisha uhusiano wetu na Mungu na kupata faida zote zinazoambatana na
kunena kwa lugha. Ni kawaida yangu tu kufundisha neno la Mungu bila kuweka
shuhuda lakini nnazo shuhuda nyingi zinazoashiria kunena kwa lugha
kunabadilisha mfumo wa maisha yetu jambo la msingi tu lifanyie kazi neno hili
na utabaini kuwa nisemayo ni kweli.
Yakobo 1:22-24 “Lakini iweni watendaji wa
neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.Kwa sababu mtu akiwa
ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso
wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi
alivyo.”
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!