Jumanne, 30 Desemba 2025

Tengeneza mambo ya nyumba yako!

 


2Wafalme 20:1-3 “Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana akasema, Nakusihi, Bwana, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.”


Utangulizi:

Moja ya wafalme na watawala wa ufalme wa Yuda aliyekuwa mwaminifu sana ni pamoja na Hezekia, Ni mfalme aliyemcha Mungu na kufanya mapinduzi makubwa ya uamsho ikiwa ni pamoja na kurejesha ibada ya Mungu wa kweli katika Hekalu lililokuwako Yerusalem na kukomesha kabisa ibada za kipagani, taarifa zake zinapatikana katika kitabu cha Wafalme wa pili, Nyakati wa pili na kitabu cha nabii Isaya, ambako kote anasifiwa kama mtawala mcha Mungu, ambaye alimtegemea Mungu hata wakati wa vita mbalimbali, Yeye alikuwa ni wa uzao wa Daudi na anayefikiriwa kama moja ya viongozi wacha Mungu sana, hata hivyo habari yake maarufu zaidi ni pamoja na habari zake za kuugua sana na akiwa katika kuugua huko akapokea onyo kali kupitia nabii Isaya kuwa atengeneze mambo ya nyumba yake kwani atakufa  na wala hatapona, jambo lilopelekea yeye kumlilia Mungu na kuomba kwa machozi.

Isaya 38:1-3 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.”

Mara kadhaa tumehubiri sana kuhusu kisa hiki na kuonyesha nguvu za maombi na hasa maombi ya kulia sana na machozi na tumehubiri vile vile kuhusu swala zima la Hezekia kuongezwa miaka 15, lakini ni vigumu sana kuwasikia wahubiri wakieleza ni kwa nini mfalme huyu mwaminifu alitakiwa atengeneze mambo ya nyumba yake? Na ni kwa nini alipewa karipio kali kuwa hatapona bali atakufa? Tena akiwa anaumwa! Na kwanini Mungu alikuwa ameahirisha mpango wake na kumuongezea miaka? Ni changamoto gani ilikuweko nyuma ya karipio hili ambalo kimsingi linaweza kuwa ndio sababu ya mkasa huu mzima! Leo Roho Mtakatifu anatuwekea wazi, kuhusiana na swala hilo. Tutajifunza somo hili tengeneza mambo ya nyumba yako kwa kuligawa katika vipengele vikuu vitatu muhimu vifuatavyo:-

 

·         Tengeneza mambo ya nyumba yako.

·         Sababu za kutengeneza mambo ya nyumba yako.

·         Jinsi ya kutengeneza mambo ya nyumba yako.


Tengeneza mambo ya nyumba yako.

Isaya 38:1 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.”

Hezekia aliyekuwa mfalme mwaminifu katika utawala wa Yuda, ambaye alisababisha mabadiliko makubwa sana ya kiimani na kuleta uamsho mkubwa sana, alitakasa Hekalu, na kuharibu madhabahu za kipagani na ibada za sanamu, na kurejesha ibada sahihi za Mungu aliye hai, na sikukuu za Pasaka tofauti na Ahazi baba yake, Hezekia alikuwa mtu wa imani na maombi, mtu aliyemtegemea sana Mungu kiasi ambacho aliwahi kushinda vita kwa kupiganiwa na Malaika baada ya kuitisha mfungo na Mungu akaingilia kati dhidi ya majeshi ya Waashuru chini ya Senakeribu.

2Nyakati 32:20-22 “Na kwa ajili ya hayo Hezekia mfalme, na Isaya nabii, mwana wa Amozi, wakaomba, wakalia hata mbinguni. Naye Bwana akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga. Ndivyo Bwana alivyomwokoa Hezekia, na wenyeji wa Yerusalemu, na mkono wa Senakeribu, mfalme wa Ashuru, na mikononi mwa wote, akawaongoza pande zote.”

Hezekia pia alijenga mradi wa maji maarufu kama mfereji wa Hezekia (Hezekiah’s tunnel) unaopitisha maji chini kwa chini katika mji wa Yerusalem wa zamani kama njia ya kujikinga na maadui endapo atazingirwa pande zote mfereji huo maarufu wa maji uko hata siku za leo, Anatambuliwa kama moja ya wafalme maarufu sana na mfano mzuri wa kuigwa akionyesha imani kwa Mungu na maombi na anatajwa katika ukoo wa masihi katika agano jipya kwenye kitabu cha Mathayo kama moja ya mababu waliomleta Yesu Kristo ulimwenguni kwa uzao wa Daudi. Ona:-

Mathayo 1:6-9 “Yese akamzaa mfalme Daudi. Daudi akamzaa Sulemani kwa yule mke wa Uria; Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa; Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia; Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia;

Hata pamoja na sifa hizi njema tunaona ghafla baadae alianza kuugua jipu baya sana na akiwa katika maradhi haya mabaya na katika hali ya kuugua na kuumwa, Isaya nabii anatumwa na Mungu kwenda kumpa ujumbe ya kwamba atakufa na wala hatapona na hivyo atengeneze mambo ya nyumba yake, kwa nini mfalme huyu mwadilifu anatamkiwa maneno makali hivi ya kutisha tena akiwa katika wakati wa kuumwa? Na kwa nini onyo alilopewa na nabii linaonekana kuwa ni onyo kali sana na kisha katika namna ya kushangaza baada ya kuomba kwake linaahirishwa kwa haraka baada ya maombi na anaongezewa miaka 15? Nini kilipelekea Hezekia apewe onyo hili kali Tengeneza mambo ya nyumba yako maana utakufa wala hutapona, tunajifunza nini kwenye hili?

Isaya 38:1 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.”

Sababu za kutengeneza mambo ya nyumba yako.

Mungu alimtuma nabii Isaya kumuonya Mfalme Hezekia na kumtaka atengeneze mambo ya nyumba yake, kwa ujumla sababu za kwanini onyo hili lilikuwa kali kiasi hiki haliko wazi sana katika Biblia Lakini unaweza kupata picha ya wazi kwamba Hezekia alikuwa na kiburi na ubinafsi uliopitiliza ambao ungeweza kuzuia mapenzi ya Mungu, alikuwa ni mtu aliyejihesabia haki kupita kawaida na hakuwa mtu mwenye kuamini haki ya wengine, Mfalme Hezekia alinyooshwa katika ugonjwa mzito na angekufa kweli, lakini Mungu hawezi kujipinga mwenyewe hivyo alimuongeza miaka 15 kwa sababu maalumu na za msingi sana ambazo tutaziangalia hapa:-

1.       Hezekia alikuwa ni mfalme ambaye hakuwa ameoa wala hakuwa anataka kuoa kwa mujibu wa maelezo ya tamaduni za kiyahudi Hezekia alikuwa anaogopa kuwa akioa na kuzaa mtoto anaweza kuzaa watoto wasio na haki na wasiomcha Mungu kama alivyo yeye na hivyo wangeweza kumuudhi Mungu, hivyo alijiamini mwenyewe na kujihesabia haki, akidhani kuwa wengine hawataweza kuwa kama yeye, kwa hiyo aliamini ni afadhali asioe kuliko kuoa na kuzaa watoto watakaomkosea Mungu, Mungu alichukizwa sana na mawazo ya Hezekia kwa sababu kama angelikufa bila kuzaa watoto, utawala wa Yuda ungekosa mfalme wa nasaba ya Daudi jambo ambalo lingevunja ahadi ya  mpango wa Mungu kwa utawala wa kudumu kwa uzao wa Daudi;-

 

2Samuel 7:12-16 “Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu; lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.”

 

Mwanzo 49:8-10 “Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia.Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemwamsha? Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.”

 

2.       Hezekia  alikuwa ni mfalme asiyetazama mbali; hata wakati anaumwa kwa muda mrefu bado alikuwa hafikirii lolote kuhusu uongozi ujao, alikuwa amejaa ubinafsi akijifikiri yeye mwenyewe, Mungu alimchungulia wakati anaumwa ikaonekana kuwa anafikiria kumaliza vizuri na Mungu lakini hakuwaza kamwe kuandaa kiongozi mwingine kwaajili ya kuendeleza uongozi ujao baada yake, wala hakuwaza kuwa watu wake wataongozwaje, alikuwa mfalme mwema na wa kiroho lakini mbinafsi, Mrithi alitakiwa kuandaliwa aone shughuli za kifalme na kujifunza maswala ya utawala hata kabla ya kifo chake lakini yeye hakuliangalia hilo, Neno tengeneza mambo ya nyumba yako katika lugha ya kiebrania ni “tsâvâh” ambalo maana yake kwa kiingereza ni appoint, au command au charge, set officially, arrange, determine, give orders, give instruction, show direction, chagua, Amuru, weka mtu mbadala, tangaza, andaa mrithi wako, amua, weka utaratibu, toa maelekezo, onyesha muelekeo lilikuwa ni agizo ambalo lingemfanya Hezekia akili zake zimrudie na afikiri kwa kina, nani anaweza kumrithi katika kiti cha ufalme baada yake,Kama yeye atakufa nini kitafuata, Sababu zake hazikuwa za msingi kwa Mungu, woga wake na hofu yake haikuwa na maana kwa Mungu, swala la uzao wake watakuaje watamcha Mungu au la, halikuwa linamuhusu  huwezi kuingilia na kuamua mambo ya Mungu ndani ya mtu mwingine ni kazi ya Mungu kujua nani atakuwa mwema au itakuwaje, ni wajibu wa Mungu kujua kuwa ajaye atafaa watu wake ama itakuwaje sio wewe, Kwa hiyo Hezekia alitakiwa kuoa na kuzaa na kumuandaa mfalme ajaye ili baada yake kazi ya Mungu iendelee, na uzao wa Daudi uendelee, yeye hakufanya hivyo, Musa aliandaa mtu ambaye angeshika madaraka baada yake  na Daudi aliandaa utaratibu wa mfalme ajaye na hata majukumu yake watu walijua baada ya Daudi nini kitafuata, Mungu alimuagiza hata Eliya kumuandaa Elisha kuwa nabii baada yake na alumuandaa hivyo mapema, kumbe viongozi huandaliwa:-

 

Hesabu 27: 18-23 “Bwana akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako; kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao. Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii. Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za Bwana; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia. Musa akafanya kama Bwana alivyomwamuru; akamtwaa Yoshua, akamweka mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote;kisha akaweka mikono yake juu yake, akampa mausia, kama Bwana alivyosema kwa mkono wa Musa.”

 

1Nyakati 28:1-9 “Kisha Daudi akawakusanya huko Yerusalemu wakuu wote wa Israeli, wakuu wa kabila, na maakida wa vikosi wenye kumtumikia mfalme kwa zamu, na maakida wa maelfu, na maakida wa mamia, na wenye kutawala juu ya mali na milki za mfalme, na za wanawe, pamoja na matowashi, na mashujaa, naam, waume mashujaa wote. Ndipo Daudi mfalme akasimama kwa miguu yake, akasema, Nisikilizeni, ndugu zangu, na watu wangu; Mimi nalikuwa na nia ya kuijenga nyumba ya kustarehe kwa ajili ya sanduku la agano la Bwana, na kiti cha kuwekea miguu yake cha Mungu wetu; hata nalikuwa nimeweka tayari kwa kujenga. Lakini Mungu akaniambia, Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umekuwa mtu wa vita, nawe umemwaga damu. Walakini Bwana, Mungu wa Israeli, alinichagua katika nyumba yote ya babangu kuwa mfalme juu ya Israeli milele, kwa kuwa amemchagua Yuda awe mkuu; na katika nyumba ya Yuda, alichagua nyumba ya babangu, na miongoni mwa wana wa babangu, aliniridhia mimi ili kunitawaza niwe mfalme juu ya Israeli wote; tena katika wana wangu wote (kwani Bwana amenipa wana wengi), amemchagua Sulemani mwanangu ili aketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wa Bwana, juu ya Israeli. Akaniambia, Sulemani, mwanao, ndiye atakayeijenga nyumba yangu na nyua zangu; kwa kuwa nimemchagua awe mwanangu, nami nitakuwa babaye. Na ufalme wake nitauweka imara milele, akijitia kwa bidii kuzitenda amri zangu na hukumu zangu, kama hivi leo. Basi sasa, machoni pa Israeli wote, hilo kusanyiko la Bwana, na masikioni pa Mungu wetu, angalieni na kuzitafuta amri zote za Bwana, Mungu wenu, ili mpate kuimiliki nchi hii njema, na kuwarithisha wana wenu baada yenu hata milele. Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa Bwana hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele.”

 

1Wafalme 19:15-17 “Bwana akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako.Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua.”

 

3.       Hezekia alikuwa anaamuriwa kuweka utaratibu, alikuwa ni kiongozi mzuri sana na mwema lakini alikuwa haandai utaratibu, angeacha mambo hayana hata muelekeo baada ya kifo chake, je hujawahi kuona viongozi wanaanzisha taasisi kisha wakifa wao nazo zinakufa? Watu wanaobaki wanakuwa hawajui hata la kufanya wote wanamtegemea yeye tu, Mungu ni Mungu wa utaratibu, Hezekia alikuwa hafiriki lolote kuhusu utaratibu utakuwaje baada yake wakati wenzake waliomtangulia walikuwa ni watu walioweka utaratibu yeye hata mke wa kuoa alikuwa anaogopa kuwa hatapata mke mcha Mungu na hivyo hatakuwa na watoto wazuri wala haonyeshi mrithi wake ni nani na nini kifanyike baada yake, kwa kufanya hivi ni kama alikuwa anazuia mpango wa Mungu wa baadaye, kila kiongozi kuanzia ngazi ya kifamilia anapaswa kukumbuka kuwa sisi ni wapitaji duniani, na baada ya kuongoza kwetu basi lazima aweko kiongozi mwingine na taratibu za baadae

 

Yehoshafati aliweka utaratibu mzuri sana wa kiserikali na kimaamuzi kabla ya kifo chake, Hezekia yeye alikaa kimya tu, anaugua na haweki mipango mingine vizuri, yalikuwa ni mawazo mabaya hakuwa kiongozi mbaya alimcha Mungu lakini hakuwa akifikiri zaidi ya mambo katika jicho la kiungu, hakuwaza kazi ya Mungu baada yake itakuwaje, kiongozi ambaye angemrithi angekosa hata pa kuanzia hajui aanzie wapi, hii ilikuwa changamoto yake ona mfano wa Yehoshafati yeye aliweka taratibu nzuri za kimaongozi na kiserikali ona!

 

2Nyakati 19:4-11 “Na Yehoshafati akakaa Yerusalemu; akatoka tena kwenda kati ya watu toka Beer-sheba mpaka milima ya Efraimu, akawarudisha kwa Bwana, Mungu wa baba zao. Akasimamisha makadhi katika nchi, katikati ya miji yote yenye maboma ya Yuda, mji kwa mji; akawaambia hao makadhi, Angalieni myafanyayo; kwa kuwa hammfanyii mwanadamu hukumu, ila Bwana; naye yupo pamoja nanyi katika neno la hukumu. Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu; angalieni mkaifanye; kwa maana kwa Bwana, Mungu wetu, hapana uovu, wala kujali nafsi za watu, wala kupokea zawadi.Tena katika Yerusalemu Yehoshafati akasimamisha wa Walawi na makuhani, na wakuu wa mbari za mababa wa Israeli wawe kwa hukumu ya Bwana, na kwa mateto. Nao wakarudi Yerusalemu. Akawaagiza, akasema, Ndivyo mtakavyotenda kwa hofu ya Bwana, kwa uaminifu, na kwa moyo kamili. Na kila mara watakapowajia na teto ndugu zenu wakaao mijini mwao, kati ya damu na damu, kati ya torati na amri, sheria na hukumu, mtawaonya, wasiingie hatiani mbele za Bwana, mkajiliwa na ghadhabu ninyi na ndugu zenu; fanyeni haya wala hamtakuwa na hatia.Tena angalieni, Amaria, kuhani mkuu, yu juu yenu kwa maneno yote ya Bwana; naye Zebadia, mwana wa Ishmaeli, jemadari wa nyumba ya Yuda, kwa maneno yote ya mfalme; Walawi nao watakuwa wasimamizi mbele yenu. Jitieni nguvu, mtende, naye Bwana awe pamoja nao walio wema.”

Hata hivyo jambo jema ni kuwa baada ya maonyo Hezekia aliutafuta uso wa Mungu, aligeukia ukutani na kutafuta uso wa Mungu, aliomba na kulia sana alijutia tabia yake na ubinafsi wake aliokuwa nao, alimkumbusha Mungu jinsi alivyotembea kwa uaminifu alilia na kujutia kosa lake na Mungu alimrehemu haraka na kumuongezea Muda wa kufanya maandalizi, ni katika muda huu wa nyongeza ndipo alipooa na ndani ya miaka mitatu alizaliwa Manase

Isaya 38:2-6 “Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la Bwana likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.”

Jinsi ya kutengeneza mambo ya nyumba yako

Kuna mambo kadhaa ya kujifunza kutoka kwa maisha ya Hezekia na mkasa huu, waalimu wa Kiyahudi wanaelezea ya kuwa Hezekia alioa haraka sana baada ya kuponywa na alimuoa mwanamke ambaye alikuwa ni binti wa nabii Isaya baada ya kukemewa na kuponywa, Nabii Isaya alimuelekeza jinsi ya kutengeneza mambo ya nyumba yake alitakiwa kuoa haraka hata bila kujali kuwa wazao wake watakuwa wema au wabaya, hakutakiwa kuogopa mambo yajayo wala kuharibu yanayobaki,alitakiwa kuweka utaratibu na kuandaa mrithi wa kifalme kwaajili ya Daudi mtumishi wa Mungu ili ahadi ya Mungu itimie, Mfalme Hezekia alimuoa “Hefsiba” ambaye alikuwa ni binti wa nabii Isaya  na miaka mitatu baada ya kuponywa kwake walifanikiwa kumpata mtoto aliyeitwa Manase, huyu akawa mfalme mpya hata hivyo akawa muovu sana kuliko wafalme wote katika Yuda, aliwahi kumtoa mwane sadaka ya kuteketezwa,akajihusha na waganga na wachawi na ibada za sanamu na kuabudu malaika na machukizo ya kila aina

Isaya 62:4-5 “Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula; kwa kuwa Bwana anakufurahia, na nchi yako itaolewa.Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.”

2Wafalme 21:1-6 “Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na mitano katika Yerusalemu, na jina la mamaye aliitwa Hefziba. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli. Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopaharibu Hezekia baba yake; akamjengea Baali madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia. Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya Bwana, napo ndipo alipopanena Bwana, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu. Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika behewa mbili za nyumba ya Bwana. Akampitisha mwanawe motoni, akatazama bao, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa Bwana, hata kumkasirisha.”

Mambo ya kujifunza:-  

1.       Hakuna mtu mwenye uhakika na kesho, kesho iko mikononi mwa Mungu tu, Hezekia ingawa alikuwa mwema lakini bado alikumbushwa kuwa kuna kifo na akapokea taarifa hizo bila kutarajia, kwa kawaida huwa tunajisahau kama wanadamu tunadhani tutaendelea kuwepo siku zote, uzima huu unatupa kiburi, pumzi hii inatufanya tufikiri ubovu ni wa wengine na kifo ni cha wengine, tunajifikiri sisi tu, hatufurahii kuandaa wengine, hatufikirii uhai wa taasisi wakati ujao, maisha ya mwanadamu ni kama mvuke tu, na kama ua la kondeni, usisahau kuwa kuna kifo, hata Musa alikumbushwa na Mungu akamuandaa Yoshua, Eliya alimuandaa Elisha, Paulo Mtume alimuanda Timotheo na wengine, wewe na mimi tunataka tukizimika wengine waone giza tu hicho ni kiburi na sio mpango wa Mungu.

 

Ayubu 14:1-2 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe

 

2.       Kutengeneza mambo ya nyumba yako sio agizo kwa Hezekia tu, ni agizo la kila mtu, iandae familia yako, andaa waandae kwaajili ya mambo yajayo, andaa mahusiano mazuri na watu, andaa  kwa kuondoa madeni ya kimwili na kiroho hakikisha yanalipwa, kumbuka kuweka maagizo, kumbuka kuna maisha baada ya kazi, kuna maisha baada ya kustaafu, kuna kutafuta kwa bidii kuwa na amani na watu wote, wewe na mimi hatutakuwepo milele tuache ubinafsi, Ondoa kinyongo chako moyoni, usijiweke katika nafasi ya Mungu, acha kuhukumu wengine na kudhani kuwa uko wewe peke yako Mungu anao watu wengi sana na anaweza kuwatumia, lakini ni wajibu wetu kuwaandaa na wengine waweze kutimiza hivyo Majukumu ya mbeleni.

 

Kutokujiayarisha kwa maswala ya Mungu kunaitwa upumbavu katika maandiko, lakini tukihesabu siku zetu fupi za kuweko duniani na tukazitumie vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa tayari tunaitwa wenye hekima na akili

 

Zaburi 90:10-12 “Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara.Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako? Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.”

 

Luka 12:15-21 “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.” 

 

3.       Fanya mambo yao yote kwa uaminifu, Hezekia alikuwa mwaminifu na uaminifu wake ulikuja kumkomboa baadaye, Mungu alimuongezea umri kwa sababu alikuwa mwaminifu na alikubali mapenzi ya Mungu baada ya kuponywa jipu lake sugu, kumbuka wakati wowote unaweza kufa, hata kama wewe u mwema usisubiri tangazo la kifo ndipo uanze kujiandaa, je umeandaa watoto wako wa kiroho, umeandaa viongozi wajao, ndoa yako iko vizuri, watoto wako wamefundishwa njia za Bwana, je umesamehe waliokukosea, je una Amani na watu wote, je kwa Mungu uhusiano wako uko salama, Geuka ukutani leo ujifanyie tathimini wewe na Mungu wako kama mambo yako yako sawa sawa au la kama kuna kwa kutengeneza tubu, tengeneza mambo ya nyumba yako

 

2Petro 3:9 “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.”

 

4.        Unyenyekevu ni nyenzo ya thamani kubwa, - Kuugua kwa Hezekia kulimkumbusha swala zima la unyenyekevu, alipopewa taarifa za kutokupona alionyesha ya kuwa anamtegemea Mungu, alijinyenyekeza kwa Mungu wake, ni mfalme lakini aliamini katika maombi, alitubu na hakujihesabia haki, alipopona na kuongezwa maiaka 15 aliitumia vema kukamilisha kazi iliyosalia mbele yake kwa uaminifu, Hezekia alijifunza wazi kuwa iko sauti ya Mungu wakati tunapougua, lazima tujifunze na kujua kuwa Mungu anataka jambo gani lifanyike wakati wa kuugua kwetu na Hezekia aliyajua mapenzi ya Mungu na alijua dhambi zake akatubu

 

Isaya 38:17-20 “Tazama; nalikuwa na uchungu mwingi kwa ajili ya amani yangu; Lakini kwa kunipenda umeniokoa na shimo la uharibifu; Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako. Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; Wale washukao shimoni hawawezi kuitarajia kweli yako. Aliye hai, naam, aliye hai, ndiye atakayekusifu, kama mimi leo; Baba atawajulisha watoto kweli yako.Bwana yu tayari kunipa wokovu. Basi, kwa vinubi tutaziimba nyimbo zangu, Siku zote za maisha yetu nyumbani mwa Bwana.”

Na. Rev, Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumamosi, 27 Desemba 2025

Kupata na kujuta!

 


1Timotheo 6:6-10 “Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”




Utangulizi

Bila shaka umewahi kushuhudia katika maisha haya kama mwanadamu kuwa unaweza kuwa na hamu au shauku ya kupata kitu fulani na ukapambana mpaka ukakipata na baada ya kuwa umekipata ukaanza kujuta moyoni, Hali hii inaweza ikatokea mara baada ya kufanya maamuzi kadhaa katika maisha yetu kisha baada ya maamuzi hayo unasikia hisia za majuto, unajiona kama umefanya maamuzi duni, ya kijinga na kipumbavu au kama umefanya makosa ya kiufundi umekosea malengo, au hujafanya maamuzi sahihi, wakati mwingine maamuzi ya aina hiyo yanaweza kuleta uchungu na hisia hasi na kuathiri afya na maendeleo ya mtu, kimwili, kiroho na kisaikolojia, ingawa kujuta pia kunaweza kujenga hisia chanya na kumfanya mtu kufanya maamuzi mazuri baadaye, maa na yake ni nini?, si kila kitu tunachikitaka na kufanikiwa kukipata duniani kinaweza kutuletea furaha, viko vitu vingine tunaweza tukavitamani sana lakini baada ya kuvipata vinaweza kuwa chanzo cha maumivu makubwa na huzuni na majuto, vitu hivyo inaweza kuwa mali, fedha, vyeo, mahusiano na kadhalika ambavyo tumevipigania kuvipata kwa shauku/tamaa lakini baadaye vinatuletea maumivu.

Yakobo 4:3 “Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.”

Watu wengi sana duniani wametamani sana kupata mali, vyeo, na hata mahusiano Fulani kwa tamaa zao, lakini baadaye walijuta na kulia machozi, ni muhimu sana kupata lolote tunalolitamani katika mapenzi ya Mungu na sio kwa tamaa ya kibinadamu, sio kila kitu tunachokitaka duniani kinaweza kutupa raha, na furaha, vingine vinaweza kutuletea maumivu, uchungu na majuto, mengi, wengi wamejilaumu wenyewe, kujikosoa na kujisikia vibaya au kukata tamaa kwa sababu ya hali hii “Getting and regretting” yaani kupata na kujuta kisaikolojia tendo hili linaitwa “Cognitive dissonance” ambalo ni tendo la kukosa raha, baada ya mambo kwenda kinyume na ulivyoamini!

Leo kwa msingi huo tutachukua muda kujifunza somo hili Kupata na kujuta kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-

·         Maana ya kupata na kujuta

·         Kupata na kujuta.

·         Jinsi ya kupata katika mpango wa Mungu


Maana ya kupata na kujuta

Kupata na kujuta ni tendo la kupata huzuni, kukata tamaa, kupata masononeko katika akili yanayokuja baada ya kupata jambo fulani ambalo ulitarajia kuwa litakupa furaha lakini ukajutia kuwa haikuwa kama ulivyokuwa unafikiri, na ukatamani kama ungelifanya vinginevyo, hii ni mojawapo ya sehemu ya kawaida katika maisha ambayo imewakumba watu wengi, aidha baada ya kupata nafasi fulani nzuri na kushindwa kuitumia au kupata nafasi fulani wakaitumia lakini isilete furaha au matarajio uliyoyafikiri, tendo hilo kisaokolojia linaitwa Cognitive dissonance – Psychological conflict resulting from incongruous beliefs and attitudes held simultaneously, kwa Kiswahili tunaweza kusema Majuto ni Matokeo ya mgogoro wa kisaikolojia unaotokana na kutokuenda sawa kwa kile ulichikiamini au kukitarajia sawa na mtazamo ulioufikiria, Kwa Kiebrania linatumika neno “Nâcham” naw- kham kimatamshi,  kwa kiingereza to sigh – physical and emotional response to strong feeling like grief, regret, repent Kwa mfano Mungu alipomuumba mwanadamu, aliatarajia wanadamu wataishi kwa shukurani na utii kwa Mungu, lakini badala yake  wanadamu wakaanza kuishi tofauti na kile Mungu alichokuwa amekitarajia kwa hiyo Mungu alijuta, aidha Mungu alijuta pia alipomtawaza Sauli akijua kuwa atatii yote anayomwagiza, lakini Sauli alirudi nyuma asifuate aliyoagizwa na Mungu

Mwanzo 6: 1-6 “Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za binadamu, wakazaa nao wana; hao ndiyo waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.”

1Samuel 15:10-11 “Ndipo neno la Bwana likamjia Samweli, kusema, Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia Bwana usiku kucha.”                

Katika maandiko yote hayo lugha ya kiebrania inayotumika ni “Nâcham” ikimaanisha kuwa Mungu alijuta baada ya kuwa alifanya jambo kwa nia njema lakini baadaye hakupata matokeo kama yale aliyokuwa ameyaamini au kuyategemea au kuyatarajia huu ni mfano sasa wa kupata na kujuta, Katika maisha, kupata na kujuta kumewatokea watu wengi sana na kunaendelea kuwatokea, Bwana ampe neema kila mmoja wetu asitembee katika maisha ya majuto na badala yake aweze kufurahia maisha, Mungu akupe akili hizo na ufahamu huo, isitokee ukaja kujuta katika maisha yako Ameeeeen

Kupata na kujuta.

Kila mwanadamu anapaswa kuwa makini sana katika maeneo yote ya maamuzi katika maisha yake kwani kanuni inayotumika hapo ndiyo ambayo inaweza kutuletea furaha au majuto, endapo maamuzi yetu yatafanyika yakiwa yanaongozwa na tamaa na misukumo ya kibinadamu bila kuzingatia ua kufikiri sana katika upana wake kwa njia za kiungu na kutimiza mapenzi ya Mungu tunaweza kujikuta tunaingia katika kundi la watu wanaojuta katika maisha yao, Neno llinatuasa:-

Mithali 3:5-7 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.”   

Maandiko yanaonyesha kuwa wako watu wengi sana ambao walitazama kitu kwa mitazamo yao na kukitamani lakini bila kuzingatia mapenzi ya Mungu na wakapata lakini walijuta sana baadaye

-          Hawa – Mwanzo 3:6-7 “Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.”

 

Adamu na Hawa walijutia sana katika maisha yao na vizazi vyao swala zima la kutokumtii Mungu na kufuata mapenzi yao kwa kula mti waliokatazwa na Mungu, wao waliutamani ule mti na katika fikira zao walifikiri wanaweza kupata furaha wakala kwa tamaa ya kufanana na Mungu, na kwa masikitiko makubwa wakagundua kuwa wameingia matatizoni na wamekuwa uchi kabisa, uamuzi wao uliwapa kujuta siku zote za maisha yao kupata na kujuta

 

-          Lutu – alifanya uamuzi wa kuchagua kuishi katika bonde la Sodoma ambalo kwa macho ya kawaida liloonekana kuwa kama bonde la Mungu, ardhi ilikuwa nzuri yenye kuvutia na akaamua kuishi huko nadhani pia alioa huko, alipata lakini alitoka na majuto kwani alipoteza kila kitu alichokuwa nacho na hata mkewe pia na kujikuta akiishi katika pango akiwa masikini na asiyekuwa na kitu, na kuishia katika uvunjifu mkubwa wa kimaadili uliochagiwa bintize.

 

Mwanzo 13:10-13 “Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari. Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao. Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma.Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA.”

 

Mwanzo 19:26-30 “Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi. Ibrahimu akatoka asubuhi kwenda mahali aliposimama mbele za BWANA, naye akatazama upande wa Sodoma na Gomora na nchi yote ya hilo Bonde, akaona, na tazama, moshi wa nchi ukapanda, kama moshi wa tanuru. Ikawa Mungu alipoiharibu miji ya Bondeni, Mungu akamkumbuka Ibrahimu, akamtoa Lutu katika maangamizi alipoiangamiza miji hiyo aliyokaa Lutu.Lutu akapanda kutoka Soari akakaa mlimani, na binti zake wawili pamoja naye, kwa sababu aliogopa kukaa katika Soari. Akakaa katika pango, yeye na binti zake wawili.”

 

-          Amnoni mwana wa Daudi alimpenda sana Tamari binti ya baba yake alimpenda sana mpaka akawa anakonda na kuumwa, alimtamani sana alimpenda mno ndio maandiko yanavyotueleza mpaka akapanga mikakati ya kumpata kwa hila, hata hivyo baada ya kumpata tu neno la Mungu linasema alimchukia machukio makuu sana kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza jambo hili lilimfanya apate lakini ajute

 

2Samuel 13:11-19 “Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye. Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako. Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa mabaya haya ya kunitoa ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa kumsikiliza. Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake. Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo mtumishi wake akamleta nje, akafunga mlango nyuma yake. Naye Tamari akatia majivu kichwani mwake, akairarua hiyo kanzu ndefu yake aliyoivaa, akaweka mkono kichwani akaenda zake huku akilia kwa sauti.”

 

 

-          Yuda Iskariote – alitamani sana fedha, alifahamu au kudhani ya kuwa anaweza kumsaliti Yesu Kwa vipande 30 vya fedha, akidhani kuwa labda Yesu angeliponyoka katika mikono ya adui zake, hakufikiri kwa kina zaidi ya tamaa zake lakini baadaye alijutia sana umauzi wake alizitupa fedha hizo na kwenda kujinyonga, kupata fedha sio kubaya lakini kutafuta fedha nje ya mapenzi ya Mungu au kufanya mambo kwa tamaa ni jambo baya sana linaloweza kutuletea majuto, Kwa hiyo Yusa alifanikuwa kupata fedha kwa kumsaliti yetu Lakini alijutia

 

Mathayo 26:14-16 “Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti.”

               

Mathayo 27:1-5 “Na ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu, wapate kumwua; wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato aliyekuwa liwali. Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia. Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe. Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga.”

Kusudi la Mungu ni kumtunza mwanadamu na maumivu mengi, kumlinda mwanadamu dhidi ya tamaa, kumkumbusha mwanadamu ya kuwa anapaswa sana kumtegemea Mungu katika maamuzi yake yote na njia zake zote, wanadamu wengi sana waliookoka na wale wasiookoka wamejikuta katika madhara makubwa kwa sababu ya kuongozwa na tamaa na matakwa yao wenyewe, ni vema kila unapofika wakati wa kufanya maamuzi watu wakawa wanautafuta uso wa Mungu kwa bidii ili kuyapata mapenzi ya Mungu badala ya kuzifuata njia zetu wenyewe ambazo baadaye zinaweza kutuletea majuto, Neno la Mungu linayo maelekezo ya kutosha ya namna ya kupata yale tuyatakayo katika mapenzi ya Mungu na ikiwa hivyo katika maisha yetu tutaepuka kwa kiwango kikubwa kujuta.

Mithali 14:12-14 “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti. Hata wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni; Na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo. Ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe; Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake.”

Jinsi ya kupata katika mpango wa Mungu

Maisha yamejaa majuto mengi sana wako watu wanajuta kwa sababu mbalimbali katika maisha walipata lakini wanajuta, ukifanya utafiti, wako watu wamechoka mno mioyo yao imejaa simamzi na uchungu kwa sababu walipata au walifanya jitihada za kupata lakini wanajuta kwa namna moja ama nyingine, yale waliyoyapigania ili wapate yalileta majuto badala ya furaha, yale yaliowapotezea muda mwingi sana wakawekeza huko yakawalipa mabaya wasiotarajia, sasa wanajuta, wako wanaojuta kwa sababu, Walipopata kazi, walifanya kazi kwa bidii na kwa kujituma sana lakini hawakutoa muda wa kutosha kwa familia zao, marafiki zao na ndugu na jamaa, wakati wote walikuwa bize na kazi zao lakini walipojikuta wako vitandani na wanakaribia kufa walijuta kwa sababu kazi walizipata  na fedha walizipata lakini walijikuta wanafanya kazi sana na kutumia masaa mengi makazini na wakakosa wakati muhimu wa kuwa na familia zao, nahata kuwaweka sawa watoto wao, wanakuja kubaini watoto wamepotoka, wamekuwa bila upendo wa baba na mama,

Wako waliokataa wachumba zao kwa sababu walichelewa kuwaoa kwa sababu ya umasikini, nitamsubiria mpaka lini, mtu akaamua kuolewa na kijana aliyejitokeza kwa sababu ana kazi nzuri na gari nzuri, na pesa bila kujiuliza alivipataje lakini baada ya maisha kuendelea maisha yalitoa majibu tofauti, walipoteza upendo wa dhati kwa sababu ya vitu vinavyoonekana kwa muda sasa wanajuta

Wako watu ambao hawakuishi maisha yao halisi, na badala yake waliishi maisha ya kuigiza, wakitaka kuwafurahisha wengine walifurahia kusifiwa na kutambuliwa na watu, hawakuchagua ndoto zao walichagua ndoto za wazazi wao, hawakuchagua waume au wake waliowapenda wakachagua wale waliopendekezwa kwao na wachungaji, mabosi wao na vinginevyo, hawakuchagua kazi zao na fani zao walichagua kile dunia inakitaka kwaajili yao na wakawekeza muda wao huko na sasa wanajuta

Wako watu ambao wanajuta kwa sababu hawakuwa na muda wa kutunza afya zao, waliishi maisha ya hovyo, mabaya, hawakuwa na muda wa kutengeneza na watu, waliharibu mahusiano, na watu, familia zao na kupuuzia mapatano, na sasa wanajuta, wako waliopuuzia  muda wa kulala, muda wa kufanya mazoezi, walikunywa misoda na mavitu ya Super-market na sasa wanagundua kuwa wameharibu kila kitu wana huzuni kwa sababu hawakufanya mazoezi, wana huzuni kwa sababu hawakuzingatia lishe bora, wana huzuni, kwa sababu hawakufanya mapatano, wana huzuni kwa sababu hawakuwa wanalala usingizi wa kutosha afya zimeharibika na sasa wanajuta, wako hata waliokuwa wakifunga kwa kusudi la kuutafuta uso wa Bwana lakini walifunga hovyo hovyo bila kuzingatia kanuni za afya na sasa wana madonda ya tumbo, na hawawezi kufunga tena na wanajuta

Wako watu ambao wanajuta kwa sababu hawakuwekeza, hawakuweka akiba za kutosha hawakufikiri mambo ya baadaye sasa ni masikini, hawana fedha, hawakuwekeza mashamba wala mifugo hawakujali tabia zao zitawaletea matunda gani ya baadaye na sasa wanajuta, hawakupanga wanazaa watoto wangapi na kwa kiasi gani, wao kila kilichotokea kiliwatokea kama bahati tu, wako wanaojuta kwa usaliti, kupigania vyeo wakavipata lakini baadaye wakajuta hata kwanini walipigania vyeo hivyo, kutaka umaarufu, kuoa au kuolewa na watu wasio sahihi na kadhalika na sasa wao wako Jehanamu ya moto wa ndoa zao wakati wengine wako Paradiso umepata lakini unajuta!, wako waliozalishwa wakiwa nyumbani, waliona raha kujirusha lakini sasa wanajuta, wako ambao wameolewa na kuachika, wako waliotoa talaka na wanajuta, wako waliodai talaka na sasa wanajuta  hii ndio hali halisi ya Dunia pale tunapofanya mambo na kuchagua mambo kwa kuyapa uthamani wa kwetu wenyewe machoni petu wenyewe na kufanya mambo ambayo yanaweza kutufurahisha kwa muda mfupi badala ya kuwaza yatakayotufurahisha kwa muda mrefu, chaguzi za namna hiyo ni chaguzi za kiesharati kwa mujibu wa maelekezo ya kimaandiko, mwesharati ni mtu anayewaza kumaliza haja zake za muda mfupi tu na ikamgharimu maisha yake, badala ya kufikiri mbele hii ilikuwa changamoto ya Esau ambaye alijuta sana baadaye baada ya kuuza urithi wake kwa sikumoja.

Waebrania 12:16-17 “Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja. Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi Baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi.”

Wewe hapo ulipo ulitamani nini na ukakitafuta na kukipigania kwa nguvu zako zote na ukakipata lakini sasa unajuta moyoni, wako watu wengi wenye majuto ya kila aina hapa duniani na wewe sio wa kwanza sisi kama wanadamu tunaweza kufanya maamuzi ambayo baadae yanaweza kutuletea majuto makubwa sana katika mioyo yetu! Tufanyeje tujiue, turudi nyuma hapana tunashauriwa cha kufanya Na maandiko  

Ufanyeje sasa ili usishi kwa majuto?

Mungu wakati mwingine anatutaka tuwe na subira, subira hupita njia ndefu na ngumu sana na ndio maana watu wengi hawaipendi njia hii, ni njia ngumu lakini inaweza kutuletea matokeo mazuri ya kiungu na kuiungwana unajua Mungu hufanya mambo kwa wakati, lakini mwanadamu hutaka matokeo ya haraka na ni vigumu kwetu kuvumilia na kusubiri wakati wa Mungu, kwa haraka zetu.

Muhubiri 3:11 “Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.”

Mungu anatutaka tutangulize faida za kiroho kabla ya zile faida za mwilini, wengi wanaopitia njia za majuto ni wale ambao tunafikiri kwa jinsi ya mwili, kwa kuangalia vinavyoonekana na kupuuzia vile visivyoonekana ambayo kwa asili ni vya milele na hutupa furaha ya kudumu, ni lazima tuutafute kwanza ufalme wa Mungu na haki yake na mengine yote tutazidishiwa

Luka 12:16-21 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”

Nadhani kila unapofikia wakati wowote katika maisha mahali ambapo tunataka kufanya uamuzi basi ni vema sana tukatafuta sana mapenzi ya Mungu na uongozi wa Mungu neno linasema usizitegemee akili zako mwenyewe bali katika njia zako zote mtegemee Mungu

Warumi 8:13-16 “kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;”

Mithali 3:5-7 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.”

Linda dhamiri yako wakati wote unapotaka jambo - unataka hicho unachokitaka kwa sababu gani? Mungu huangalia nia ya moyo na kuhukumu kulingana na nia ya moyo, kama kuna kitu unakihitaji lakini kwa tamaa unaweza usipewe au unaweza ukapewa lakini kikakutokea puani

Hesabu 11:18-20 “Kisha uwaambie watu hawa, Jitakaseni nafsi zenu kabla ya kesho, nanyi mtakula nyama; kwa maana mmelia masikioni mwa Bwana, mkisema, Ni nani atakayetupa nyama, tule? Maana huko Misri tulikuwa na uheri. Basi kwa sababu hiyo Bwana atawapa nyama, nanyi mtakula.Hamtakula siku moja, wala siku mbili, wala siku tano, wala siku kumi, wala siku ishirini; lakini mtakula muda wa mwezi mzima, hata hapo nyama hiyo itakapotoka katika mianzi ya pua zenu, nanyi mtaikinai, kwa sababu mmemkataa Bwana aliye kati yenu, na kulia mbele zake, mkisema, Tulitoka Misri kwa maana gani?

Hata kama tumemkosea Mungu na ikaleta majuto katika maisha yetu, ni Muhimu kwetu tukamrudia Mungu huyo huyo, kwa toba, kukiri, na kuutafuta uso wake tena, Upendo wa Mungu na rehema zake hauna mipaka, tukinyenyekea kwake atatupokea tena kama ilivyokuwa kwa mwana mpotevu, kupoteza kwetu sio mwisho wa maisha, kwani Baba wa rehema anayi nafasi nyingine, ttutafute uwepo wake naye atatutia nguvu na kuturejesha tena

Luka 15:17-20 “Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.”

Hitimisho:

Mpango wa kamili wa Mungu ni kila mmoja wetu kuyafurahia maisha, Mungu kama Baba aliye mwema anatufikiria mema na yuko kwaajili yetu, lakini pia yule muovu yuko, hata hivyo pamoja na kuweko kwa yule muovu, na majaribu mbalimbali mpango wa Mungu ni kuhakikisha ya kuwa anatubariki na kutupa mambo ya kudumu ambayo kimsingi hatachanganya nayo na huzuni wala majuto. Baraka za kweli kutoka kwa Mungu ni zile zinazokuja kwetu na hazituletei majuto, ukipata katika mpango wa Mungu bila ya hila, utaufurahia uwepo wa Mungu maisha yako yote, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa na Baraka za Mungu zisizo changamana na huzuni wala majuto. Amen

Mithali 10:22 “Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumapili, 14 Desemba 2025

Siku za miaka ya kusafiri kwangu!


Mwanzo 47:7-9 “Yusufu akamleta Yakobo babaye ndani akamweka mbele ya Farao. Yakobo akambariki Farao. Farao akamwuliza Yakobo, Je! Siku za miaka ya maisha yako ni ngapi? Yakobo akamjibu Farao, Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya baba zangu katika siku za kusafiri kwao.”




Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa maisha yetu hapa duniani yanafananishwa na safari, siku zetu za kuishi ni chache na tena zimejaa taabu sana, Maisha yetu yamejaa mabadiliko mengi sana na changamoto nyingi sana za kimwili na kiroho, kwa ujumla maisha yetu duniani ni ya kitambo kifupi sana ingawaje yana kusudi kubwa la Mungu na maana kubwa sana ya kiroho, Na ndio maana Yakobo alielewa wazi kuwa maisha yake duniani ni kama safari, anapita katika hii dunia kama mgeni na mpitaji tu, Yakobo alikuwa na ufahamu kuwa dunia hii sio nyumbani kwetu na kwamba hata kama ataishi maisha merefu kiasi gani bado miaka hiyo itakuwa ni miaka ya kusafiri kwake tu. Hivi ndivyo maandiko yanavyotukumbusha hata leo ili tuishi vizuri tukiwa na uhusiano mzuri na Amani kwa Mungu na wanadamu wote!

1 Petro 2:11-12 “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.”

Miaka ya kusafiri ni usemi (Metaphor) unaokazia kuwa maisha ni safari ya mchakato wenye kutupa uzoefu, mafunzo, kukua, kuelewa, kukomaa, kuongeza ufahamu na maarifa na kukutana na mambo chanya na mambo hasi, kutuchonga, kuuelewa ulimwengu na zaidi sana kuelewa kusudi la kuwepo kwetu, kwa utukufu wa Mungu Baba, hata hivyo maisha ni ya kitambo/yaani ni ya muda mfupi, sana na kwa sababu hiyo tunatiwa moyo kukabiliana na changamoto zote na kuzihesabu kuwa ni nafasi ya kipekee ya kutuandaa kwaajili ya maisha yajayo, Maisha ni safari kwa sababu hapa duniani sio mwisho na hatujafika na badala yake tunapita tu. Leo tutachukua muda basi kutafakari somo hili muhimu kwetu “Siku za miaka ya kusafiri kwangu” kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Siku za miaka ya kusafiri kwangu.

·         Siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu.

·         Wakristo kama wasafiri  
              

Siku za miaka ya kusafiri kwangu

Mwanzo 47:7-9 “Yusufu akamleta Yakobo babaye ndani akamweka mbele ya Farao. Yakobo akambariki Farao. Farao akamwuliza Yakobo, Je! Siku za miaka ya maisha yako ni ngapi? Yakobo akamjibu Farao, Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya baba zangu katika siku za kusafiri kwao.”

Ni muhimu kujifunza na kutafakari jinsi ambavyo Yakobo anayachukulia maisha kama safari, Maisha ni safari kweli ya kimwili na kiroho, Safari hii inakabiliwa na maswala mengi chanya na hasi lakini zaidi sana nyakati muhimu za kufanya maamuzi ambayo yataamua hatima yetu ya baadaye, ndani ya maisha tutapimwa imani, utii, na changamoto za kimaisha zitakazolazimisha maisha yetu yawe na mabadiliko kadhaa na kuzaa uvumilivu utakaotusaidia kuwa na uwepo wa Mungu na ukomavu.

Yakobo anaonyesha kuwa sio yeye tu alikuwa katika safari ya maisha lakini hata baba zake yaani Ibrahimu na Isaka nao walikuwa katika kusafiri kwao, hivyo Ibrahimu, na Isaka na Yakobo waliishi duniani kama wasafiri na wapitaji duniani, hawakuwa na makazi ya kudumu, waliishi kwa Imani, walijitambua kuwa hapa duniani wao ni wapitaji tu.

Waebrania 11:13-16 “Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi. Maana hao wasemao maneno kama hayo waonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurejea. Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji.”

Yakobo anahesabu miaka ya kukaa duniani kama miaka ya safari tu, Yeye na wazazi wake waliishi hivyo, hii ni kwa sababu hawakuishi katika nyumba za kudumu kama tunavyoishi leo, maisha yao yalikuwa ya kutanga tanga na kuhama hama (Nomads), kwa hiyo hawakuwa na makazi ya kudumu, waliishi duniani kama wapitaji wakiashiria ukweli halisi wa maisha ya kuwa maisha ni safari, na imejaa mabadiliko ya iana mbalimbali kimwili na kiroho, wakipitia changamoto nyingi na majaribu mengi, pamoja na baraka za Mungu, lakini maisha ya kawaida ya kibinadamu yana changamoto nyingi wao walikuwa ni mfano tu wa kutukumbusha sisi tunaoishi leo kwamba tuko safarini, na kuwa duniani tunapita tu, tuko hapa katika hali ya ugeni tu na dunia sio nyumbani kwetu kwa kudumu, maisha ya mwanadamu ni ya muda tu, ujumbe wake Yakobo na majibu yake kwa Farao yalikuwa  ni  mauhubiri tosha kumjulisha Farao kuwa wanadamu wote hapa dunia ni wanasafiri akiwepo yeye aliyekuwa na madaraka makubwa duniani kwa wakati ule, Yakobo alitaka hili lifike akilini kwa mtu huyu mkubwa kumkumbusha kuwa Pamoja na mamlaka yake kubwa na nguvu alizo nazo anapaswa kukumbuka kuwa siku za miaka yetu ni siku za miaka ya kusafiri kwetu tu na hakuna cha kudumu duniani!

Waebrania 11:8-9.“Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako. Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.”

Kila mwanadamu mwenye akili timamu anapaswa kukumbuka kuwa maisha haya ni “temporally” ni ya muda tu tunapita kwa kasi sana na kwa sababu hiyo hatuna budi kuishi kwa Amani na wenzetu na kuwafanyia watu mambo mema, tusiwafanyie watu ubaya, wala tusiwawekee watu kinyongo, na kujilimbikizia mali na madaraka kana kwamba sisi ni watawala wa kifalme, watu wengi hujisahau katika hili, Yakobo alikuwa amebarikiwa sana lakini hakusahau kuwa yeye ni msafiri, tuishi na watu vizuri, isifikie wakati watu wakafurahia kufa kwetu au kuugua kwetu, badala yake watuombolezee, siku hizi linaanza kuwa jambo la kawaida watu kufurahia kifo cha watu wengine kana kwamba wao hawatakufa, lakini sababu kubwa ni kuwa watu hao waliishi bila ya kujali wengine, au waliumiza wengine kwaajili ya ubinafsi na mafanikio yao, na wengine, walijisahau kuwa wao wanapita tu, kila kitu duniani ni cha muda tu na maisha kwa ujumla yana masomo mengi ya kutufunza! Na la muhimu sisi ni wasafiri na tuko duniani kwa muda!, acha kinyongo, acha kuhukumu wengine, acha ubinafsi, acha kinyongo, tafuta kwa bidi Amani na wote

Siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu.

Yakobo wakati anashuka Misri na kuonana na Farao wakati huu alikuwa na miaka 130 na mpaka anafariki alikuwa na umri wa miaka 147 tu, kwa msingi huo aliishi Misri kwa muda wa miaka kama  17 hivi, Yakobo anaziona siku hizi kuwa ni chache sana, Ibrahimu aliishi miaka 175, wakati Isaka aliishi miaka 180. Kwa hiyo Yakobo anayaona maisha yake kuwa mafupi na yaliyojaa taabu sana kuliko maisha ya baba zake, na pia ingawa hakuwa anajua ataishi umri gani lakini alijitabiria kuwa siku zake ni chache na zilizojaa taabu sana kuliko siku za baba zake, yaani Isaka na Ibrahimu, Yakobo alipanda milima na mabonde akipambana na maisha yaliyojaa ugumu wa maswala mbalimbali kama:

1.       Migogoro ya kifamilia – Yakobo alilazimika kukimbia nyumbani siku za maisha ya ujana wake na kuishi mbali na baba na mama kwaajili ya kumkimbia kaka yake, Esau, hayakuwa maisha ya kawaida, tabia yake ya hila na kuutumia upole wa kaka yake kwa faida zake mwenyewe uliweza kuongeza ugumu wa maisha na kumfanya kuwa mbali na wapendwa wake wa karibu uko uwezekano kuwa Yakobo Hakuonana na Rebeka tena mpaka kifo kwajili ya tukio hili.

 

Mwanzo 27:41-45 “Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo. Rebeka akaarifiwa maneno ya Esau, mwanawe mkubwa. Akapeleka mtu kumwita Yakobo, mwanawe mdogo, akamwambia, Tazama, katika habari zako Esau, ndugu yako, anajifariji moyo wake, maana anakusudia kukuua. Na sasa, mwanangu, sikia sauti yangu, uondoke, ukimbilie kwa Labani, ndugu yangu huko Harani; ukae kwake siku chache, hata ghadhabu ya ndugu yako igeuke; hata ikuondokee ghadhabu ya ndugu yako, akasahau uliyomtenda. Ndipo nitakapopeleka watu kukuchukua kutoka huko. Kwa nini nifiwe nanyi nyote wawili siku moja?”             

 

2.       Dhuluma na ukatili kutoka kwa mjomba – Yakobo alipokuwa akifanya kazi kwa mjomba wake, ni ukweli usiopingika kuwa Yakobo alikuwa na mjomba aliyejaa hila zaidi kuliko yeye, aliishi na mjomba katili, alimdanganya katika maswala ya ndoa na kuishia kumtumikisha, lakini alibadili-badili maswala ya mkataba wa mshahara wake zaidi ya mara kumi, siku chache zilizokadiriwa na kudhaniwa na Rebeka, zikawa ni miaka mingi ya kitumwa uko uwezekano kuwa alikaa ugenini kwa mjomba wake kwa miaka 20 akidhulumiwa tu

 

Mwanzo 29:18-27 “Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo. Labani akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa kwangu. Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile alivyompenda. Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu, maana siku zangu zimetimia; niingie kwake. Labani akakusanya watu wote wa mahali pale, akafanya karamu. Ikawa wakati wa jioni akamtwaa Lea, binti yake, akamletea Yakobo, naye akaingia kwake. Labani akampa Lea mjakazi wake Zilpa, awe mjakazi wake. Ikawa, kulipokuwa asubuhi, kumbe! Ni Lea. Akamwambia Labani, Nini hii uliyonitenda? Sikukutumikia kwa Raheli? Mbona umenidanganya? Labani akasema, Havitendeki hivi kwetu, kumtoa mdogo kabla ya mkubwa; timiza siku zake saba, nasi tutakupa huyu naye kwa utumishi utakaonitumikia, miaka saba mingine.”

 

Mwanzo 31:1-9 “Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote. Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi.  BWANA akamwambia Yakobo, Urudi mpaka nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe. Yakobo akatuma watu, akawaita Raheli na Lea waje nyikani kwenye wanyama wake. Akawaambia, Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama jana na juzi. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. Nanyi mmejua ya kwamba kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu. Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwacha kunidhuru. Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia. Hivi Mungu akamnyang'anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi.”

 

3.       Mateso katika familia yake – Yakobo alikutana na changamoto kutoka katika familia yake mwenyewe, watoto wake waliokuwa wakichukiana wao kwa wao, walimuuza ndugu yao Yusufu kijana wake mpendwa na kumdanganya kuwa amefariki, Yakobo aliomboleza sana akijua kuwa mwanae atakuwa amefariki, hii ilizidisha shida na huzuni kubwa katika maisha yake, nadhani walifanya msiba na kuzika nguo lakini kumbe alikuwa amedanganywa tena!

 

Mwanzo 37:31-35 “Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi. Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba yake akamlilia.”

 

4.       Njaa iliyosababisha safari Misri – Pamoja na mapito kadhaa wa kadhaa ilimlazimu kusafiri na kuiacha nchi ya ahadi akiwa na umri mkubwa 130, anakumbwa na njaa inayowalazimisha kushuka Misri kwaajili ya chakula na wito wa mwanaye Yusufu, Ingawa Abrahamu na Isaka walikutana na changamoto mbalimbali katika maisha, Yakobo anahisi maisha yake yalikuwa magumu zaidi kuliko wao  kwa sababu ya wingi wa mateso na maumivu na migogoro ya kifamilia aliyoipitia, Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida Mungu alimtia moyo kushuka Misri na aliambiwa na Mungu kuwa atakuwa pamoja naye, atafia huko mikononi mwa Yusufu

 

Mwanzo 46:2-4 “Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa. Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako.”

Wakristo kama wasafiri               

Kimsingi yako maswala mengi ya kujifunza kutoka kwa Yakobo na mtazamo wake wa maisha kama safari

1.       Tunajifunza kuwa maisha yetu ni ya muda – Haijalishi utaishi duniani kwa muda gani lakini vyovyote iwavyo maisha ni ya muda mfupi sana na maandiko yako wazi kuhusiana na jambo hili, na kuonyesha ufupi wa maisha ikionyesha mifano ya maua, mvuke, majani, usingizi na kadhalika

 

Zaburi 90:5-6 “Wawagharikisha, huwa kama usingizi, Asubuhi huwa kama majani yameayo. Asubuhi yachipuka na kumea, Jioni yakatika na kukauka.”

 

Yakobo 4:13-15 “Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi.”

 

2.       Tunajifunza kumtegemea Mungu na neno lake – Wakati wote wa mahangaiko yake Yakobo pamoja na safari zake alizokuwa akizunguka duniani Mungu alimtokea mara kwa mara na kumuonyesha dhahiri kuwa atakuwa pamoja naye, wakati mwingine katika maisha yako utahangaika huku na huko na unaweza ukafikiri kuwa labda Mungu hako pamoja nawe lakini nataka nikudhihirishie kuwa yuko pamoja nawe, haijalishi ulikoenda ni utumwani au unakutana na shida gani kama Mungu alivyomuongoza Yakobo atakuongoza na wewe pia katika safari yako ya maisha, changamoto za maisha na ugumu wake ni jambo la kawaida.

 

Mwanzo 28:10-15 “Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.”              

Mwanzo 46:2-4 “Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa. Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako.”

 

Zaburi 119:105 “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.”

 

3.       Tunajifunza kujitayarisha kwa Mungu – Kwa kuwa maisha ni ya muda tu maana yake pamoja na kupanga na kuweka maono na mikakati ya kibinadamu, kamwe tusiache kujitayarisha kwa Mungu, maandiko yanamuita mtun anayejiwekea mikakati ya kidunia na kuacha kujitayarisha kwa Mungu kama mtu mpumbavu, kwa sababu hiyo Mungu atupe moyo wa hekima ili tujue itupasavyo kuhesabu siku zetu.

 

Luka 12:16-21 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”

 

4.       Tunajifunza kuwa tayari kukabiliana na magumu – Kuwa mtu wa Mungu kamwe hakukufanyi wewe usikutane na magumu hapa duniani, Yakobo alikuwa mtu wa Mungu na Mungu alimbariki sana lakini hata hivyo maisha yake au miaka ya kusafiri kwake duniani ilijaa taabu kuliko ya siku za baba zake kama anavyosema, hii inatufundisha na kutuimarisha kuwa, kuwa mtu wa Mungu hakutazuia wewe kukutana na magumu, lakini pamoja na hayo tusiache kumcha Mungu na kuwa na uhusiano naye, Yakobo alikutana na changamoto nyingi lakini aliendelea kuwa na uhusiano na Mungu na kuwa mvumilivu na mwenye subira na Mungu akawa pamoja naye.  

 

Waebrania 13:5-6 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?

 

5.       Tunajifunza kuishi kwa viwango – Wasafiri na wapitaji hawaishi kwa viwango vya ugenini na badala yake huishi kwa viwango vya nchi zao, sisi wenyeji wetu uko mbinguni na kwasababu hiyo kamwe hatupaswi kuishi sawa na watu wa dunia hii, wala kufungwa na mambo ya dunia hii, badala yake tuishi sawa na viwango vya kule tunakokwenda.

 

Warumi 12:1-2 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.”        

 

Mathayo 6:19-21 “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.”              

 

Hitimisho

Maisha ya Yakobo yanatufundisha kuwa safari ya maisha yetu duniani inaweza kugubikwa na changamoto nyingi sana lakini hata hivyo, Bado Mungu atakuwa pamoja nasi, kwa msingi huo sisi kama wakristo hatupaswi kujisahau  na badala yake tuendelee kutumaini na kuwa na imani, uvumilivu, saburi na kuwa tayari kuongozwa na Mungu na neno lake ili kufikia malengo ya kuwa pamoja naye mbinguni, na hata kama maisha yatajaa taabu kama yale ya Yakobo, Neno la Mungu lina ahidi kuwa Mungu atakuwa pamoja nasi atatushika mkono na kututia nguvu hadi mwisho wa safari yetu, Siku za miaka ya kusafiri kwetu ni chache nazo imejaa taabu. Ilikuwa ushuhuda kwa Farao pia

Ayubu 14:1-2 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe.”

Isaya 41:8-10 “Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Ibrahimu, rafiki yangu; wewe niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa; usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Muungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!.