Jumamosi, 10 Desemba 2016

Mungu wa Faraja yote. (God of all Comfort).



Andiko: 2Wakoritho 1: 3-7

3. Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote

Utangulizi:

Neno Mungu wa faraja yote linalojitokeza hapa na sehemu nyingine katika agano jipya limetokana na neno la asili la kiyunani “Paraklesis” ambalo maana yake ni wakili au mtetezi au mtu anayesimama karibu na mtuhumiwa ili kumtetea na kumsaidia,Neno hili limetumiwa mara nyingi sana na Paulo mtume katika nyaraka zake, na Mwandishi Luka na baadhi ya waandishi n wengine wa nyaraka na katika waraka wa Waebrania, ambapo neno hilo hujitokeza Mara 12 au kwa maneno yanayofanana na hilo mara 28

Neno hili ni la muhimu sana kwa wakristo wanaopitia magumu na mapito ya aina mbalimbali lakini zaidi sana mapito a taabu zinazotokana na kazi ya injili, ni muhimu sana kufahamu kuwa maisha ya ukristo yanajumuisha pamoja na kuteseka kwaajili ya Kristo biblia inasema tumeitwa si kumwamini tu bali kuteseka pamoja na Kristo, lakini hata pamoja na mateso hayo wakati huu Mungu hujihusisha kwa namna ya kipekee katika kufariji na hiki ndicho Paulo anakikazia katika kifungu hiki tunachojifunza leo.



Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia maswala ya msingi yafuatayo:-

·         Ahimidiwe Mungu. Mstari 3
·         Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo Mstari 3
·         Baba wa Rehema Mstari wa 3
·         Mungu wa Faraja yote Mstari wa 3

Ahimidiwe Mungu.

Neno Ahimidiwe Mungu katika Biblia ya kiingereza ya NIV linasomeka “Praise be to the God” na Biblia ya kiingereza ya KJV ambaoyo ndiyo iliyotumika kutafasiri Biblia ya Kiswahili ya Union Version linasomeka katika lugha hiyohiyo ambayo Kiswahili chake kingesomeka “Abarikiwe Mungu” Hata hivyo Biblia ya kilatili Vulgate inatumia neno “Benedictus” ambalo kiingereza chake lingesomeka “Heartfelt thanks be to the God” ambalo lingesomeka kwa Kiswahili rahisi  Atukukuzwe au Ashukuriwe sana Mungu, unaweza kuona vema katika Waefeso 1:3 “Atukuzwe Mungu

Salamu hizi kwa ujumla zinafunua moyo wa Paulo mtume ambaye alikuwa amejawa na wingi wa shukurani, na hivyo anaonyesha kufurahi na kushukuru kwa kiwango cha juu sana kwa Mungu, kwa nini Paulo anajawa na wingi wa shukurani kiasi hiki kwa Mungu? Paulo alikuwa ni mtu mwenye mzigo na kazi ya Mungu, alikuwa ni mtume mwenye moyo wa kichungaji, alikuwa na mambo mengi sana ya kuwaonya na kuwafundisha wakoritho hasa baada ya kanisa kumuandikia na kumsimulia yale waliokuwa wakiyapitia wakati akiwa hayupo, na aliwajibu kwa kuandika waraka wa Wakoritho ule wa kwanza sasa anapata taarifa kuwa Kanisa la Koritho sasa linaendelea vizuri, Paulo mtume alikuwa amekemea mambo mengi katika waraka wake wa kwanza ambao ulileta huzuni na toba kwa kanisa la Koritho na waliweza kufanya marekebisho mengi, sasa Paulo amesikia taarifa kuwa Kanisa linaendelea vema na sasa anafarijika na kufurahi sana kutokana na maendeleo mazuri ya Kanisa la Koritho, habari za maendeleo mazuri Paulo alizipata kutoka kwa Tito aliyekuwa akisimamia makanisa ya Akaya au Macedonia 2Wakoritho 7:8-10,12-16, Ni kwasababu hii Paulo mtume anamtukuza Mungu, anafurahi anamhimidi Mungu, ni kama mtu uliyekuwa na mgonjwa kisha ukapewa taarifa kuwa mgojwa huyo sasa anaendelea vema, au ameruhusiwa, kila mchungaji mwenye mapenzi ya kweli na kanisa hawezi kufurahi kanisa linapoharibika, hafurahii watu wakienenda katika njia isiyopasa, lakini watu wanapoendelea vizuri kunakuwa na furaha kubwa sana hali kadhalika walimu watafurahi kusikia wanafunzi wao wanaendelea vizuri wanafanya vizuri, madaktari na manesi hawafurahii kuona wagonjwa wakipoteza maisha wanapenda kuona wagonjwa wanapona

Huu ndio ulikuwa moyo wa Paulo Mtume anafurahi, anamtukuza Mungu anamhimidi bwana Mungu anamsifu anaonyesha moyo wa kufurahi, mambo yanapokwenda vema, kila mmoja anapaswa kufurahia mabadiliko mema ya kila mmoja wetu katika kumpenda Mungu, hatutarajii watu watasababisha huzuni, kila mmoja ataonyesha ukomavu, maendeleo katika kila Nyanja ni jambo hilo linaleta faraja kubwa sana, hakuna mama anayefurahia kuwa na mtoto asiyekua, lakini kila mtoto anapopiga hatua kina mama hushangilia sana anakaa, anatambaa, anaota meno, anasimama, anatembea anazungumza na hatua nyinginezo zote huleta faraja kubwa sana kwa kina mama wanaofanya malezi ya watoto.

Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo Mstari 3

Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo – Mahali hapa Paulo anamtaja Mungu lakini anaunganisha Mungu Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, kwa nini ? sababu kubwa ni kuwa hakuna mtu anaweza kuunganishwa na rehema za Mungu baba pasipokuweko kwa Yesu Kristo, Ni muhimu kufahamu kuwa watu wengi sana duniani hata wapagani wanafahamu sana Mungu kama Baba wa rehema lakini tatizo kubwa ni kuwa hawa wanataka kwa vinywa vyao tu hawajui kuwa rehema hizi za Mungu zimepitia kwa Yesu Kristo, ni kwa mateso ya yesu Kristo tu, ni kwa kusulubiwa kwake tu ni kwa kuiamini kazi aliyoifanya Yesu Kristo tu ndipo watu wanaweza kufaidika na rehema za Mungu baba  na upendo wake hakuna njia nyingine, Upendo wa Mungu umeunganishwa kwa mwana wake wa pekee Yesu Kristo na hakuna namna nyingine, kama tunapitia mateso katka imani yetu ni kupitiamateso ya Kristo 2Wakoritho 1:5 kama tunafarijika faraja hiyo ni kwaajili ya Yesu Kristo tu, Pasipo Kristo hatuwezi kufanya neno lolote. Shukurani anazozitoa Mtume Paulo kwa Mungu baba pia zinaunganishwa na Yesu Kristo yeye pekee ndio kipatanisho cha kweli kati ya Mungu na wanadamu

Baba wa Rehema Mstari wa 3

Baba wa Rehema – Ni muhimu kufahamu kuwa Paulo mtume alikuwa Mwebrania na ingawa aliandika waraka huu kiyunani, ni wazi kuwa alikuwa anawaza kiebrania, katika tamaduni za Kiibrania neno Baba lilitumika pia kumaanisha MWANZILISHI au chanzo kwa msingi huo linapotumika hapa linamaanisha Rehema zinatoka kwa Mungu, asili yake ni kutoa Rehema  na ndiye mwenye kuitunza rehema, 

Rehema ni sifa kuu ya Mungu, Ndani ya rehema kuna huruma, neema uvumilivu usioelezeka tunaita Mungu wa Rehema na neema , mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli Zaburi 86: 15 na ni kupitia sifa hizo ndio Mungu husaidia na kufariji, Vitabu vya tamaduni za kiyahudi Talmud vinaeleza kuwa ndiye yeye huanza kwa rehema na kumaliza kwa rehema, kila sura ya Quran isipokuwa moja tu zinaanza kwa kusema Mungu ni mwingi wa Rehema, hii ilikuwa ni salamu ya kawaida kwa waru wa mashariki ya kati kuhusu tabia ya Mungu kwa kiibrania “RACHAMIM” likimaanisha huruma au rehema Warumi 12:1 ni kutokana na tamaduni hizi na sifa hii ya kweli ya Mungu ilikuwa ni utaratibu wa kawaida kwa nyakati za kanisa la kwanza kumtaja Mungu kama Baba wa rehema

Mungu wa Faraja yote Mstari wa 3

Neno hili Mungu wa faraja yote ndio nenola Muhumu sana key word dhidi ya maneno yote katika kifungu hiki ni wazi kuwa kutoka mstari wa 3-7 neno faraja limetajwa mara kumi likiunganishwa na neno Mateso mara nne hivi au dhiki 

Mahali hapa panatupa matumaini yalkiyo wazi kuwa katika dhiki ya aina yoyote na mateso ya aina yoyote kamwe Mungu hawezi kutuacha wala kujitenga na upendo wake, Paulo ameona katika uzoefu wake kuwa wakati wote walipopita katika magumu Mungu alikuwa ni faraja , kwa msingi huo Mungu anafaraja yote, Mungu anaweza kuruhusu sisi kupita katika mateso na dhiki ili tuweze kuwafunza wenzetu jinsi Mungu alivyo mwema tuwe na ujasiri wa kuwashuhudia wengine upendo na neema ya Mungu, 

Mungu singeliweka faraja zake tungelikata tamaa, Dunia ni ngumu lakini kwaajili ya faraja zake tumejifunza kuvumilia kwa kuwa na tumaini Mungu anatufariji kwa Roho wake Mtakatifu, Paulo anaiona faraja nyingine kuwa ni kuendelea mbele na kukua wa kanisa la Koritho ambalo alilitaabikia, likaingiliwa na waalimu wa uongo, likaonyesha dalili mbaya akakemea ingawa alitumia waraka wake wa kwanza sasa wanaendelea vizuri, wanakua kiroho kwa kasi, kwa Paulo mtume hii ni aina ya faraja, Mungu anatufariji kwa viwango vikubwa anajua kutufariji katika kila aina ya dhiki na mateso, kila aina ya pito lisilo jema unalolipitia kumbuka kuwa Yuko Mungu wa faraka yote

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi.

Jumapili, 4 Desemba 2016

Mungu wa Kisasi Uangaze!



Andiko : Zaburi 94:1-3

“1. Ee Bwana, Mungu wa kisasi, Mungu wa kisasi, uangaze, 2. Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze, Uwape wenye kiburi stahili zao. 3. Bwana, hata lini wasio haki, Hata lini wasio haki watashangilia?



Utangulizi:

Je wewe umewahi kuona watu wakidhulumiwa? Umewahi kuona mahali haki haitendeki? Je hujawahi hata kusikia mahali watu wakionewa, wakiteswa, wajane na yatima na hata wageni au wakimbizi na wanyonge wakikandamizwa na kuonelewa huku wale wanaofanya dhuluma wakishangilia na kufurahi? Na hata wakidharau kuweko kwa Mungu na utetezi wake?

Jambo hili ndio hali halisi katika zaburi hii iliyoandikwa na Daudi, Hatuwezi kujua kuwa Daudi wakati huu alikuwa ameshuhudia nini katika mazingira yake, lakini kile anachokizungumza na kukililia katika zaburi hii kinafunua wazi aidha jambo ambalo amelishuhudia katika uzoefu wake wa maisha ama limewahi kumkuta, vyovyote vile iwavyo maswala haya yanaikumba hata jamii inayotuzunguka leo na Biblia hapa kupitia kinywa cha Mfalme Daudi ambaye pia Roho wa Kinabii alikaa ndani yake kuna mswala kadhaa muhimu ya kujifunza ambayo tutajifunza katika vipengele vifuatavyo:-

·         Kumuita Bwana kwaajili ya Haki (Zaburi ya 94:1-4)
·         Kushitaki kile wanachikifanya wadhalimu (Zaburi 94:5-7)
·         Kushangazwa na ujinga wa wadhalimu (Zaburi 94:8-11)
·         Baraka za kupitia katika magumu (Zaburi 94:12-13, 14-15)
·         Hatima ya kucheza na mwenye haki (Zaburi 94:16-23)

Kumuita Bwana kwaajili ya Haki (Zaburi ya 94:1-4)

Daudi anaiimba Zaburi hii katika mtazamo wa watu wanaoonewa, wanoteswa na kudhulumiwa na kutokutendewa haki watu hao wakimuangalia Mungu kama Jaji mkuu mwenye uwezo wa kutoa hukumu ya mwisho, wakati wengine wote wameshindwa kutoa msaada, Daudi anamuonyesha Mungu kuwa ndio mahakama ya juu zaidi tunayoweza kukata rufaa na tena mahakama hii ya juu zaidi inauwezo wa kutulipia Kisasi, Daudi anamtaka Mungu huyu mwenye uwezo wa kulipiza kisasi dhidi ya maadui zetu  aangaze, yaani aangalie kila kinachofanyika na kutoa haki

Wewe na mimi tumewahi kushuhudia kile ambacho Daudi alikishuhudia na kukililia katika Zaburi hii, inawezekana umewahi kushuhudia mume akifariki na kuacha mjane na yatima na Ndugu wa Mume wakiingilia kati na kudhulumu mali za yatima na kumuacha mjane huyo akiwa mikono mitupu wakiishi maisha ya dhiki, tumewahi kushuhudia wanawake wakorofi wakipora mali za waume zao na kujimilikisha, ndugu jamaa na hata watoto wakigombea hati za viwanja, kadi za magari, watu wakichongeana makazini na kusababisha wenngine wafukuzwe kazi, na kushangilia mafanikio ya anguko la mwingine, watu wakichafuana kwa faida na maslahi yao wenyewe na hila za aina nyingi zikifanyika duniani zinazofanana na hayo

Biblia inatufundisha kuwa endapo tumezulumiwa kila tunachokistahili na hakuna wa kututetea pako mahali ambapo tunaweza kudai haki zetu, Yesu alifundisha kwa msisitizo kuhusu madai ya haki zetu kwa Jaji mkuu wa majaji wote duniani, Mfalme wa wafalme mwenye uwezo sio tu wa kutoa haki bali pia kulipiza kisasi kwa watakaotudhulumu 

Luka 18: 1-81. Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. 2. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. 3. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. 4. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, 5. lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. 6. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. 7. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? 8. Nawaambia, atawapatia haki upesi;”

Daudi anamuomba Mungu haki iweze kupatikana, Yesu anatufundisha kuendelea Kumuomba Mungu mpaka haki yetu iweze kupatikana Yeye ni Jaji mkuu, ni Hakimu wa Dunia nzima, tunaweza kuimuendea yeye kwa ujasiri atupatie haki yetu, hatuhitaji kulalamika Yuko Mungu wa kisasi mwenye kuihukumu inchi na kuwapa stahili zao wenye kiburi, Yeye atawahukumu watu wote na pia ndiye mwenye kulipiza kisasi kwa wadhalimu na ndiye anayeteua majaji Warumi 13:4

Biblia inatufundisha kuwa tunapodhulumiwa tumuombe Mungu na kumsihi aangazie kile kinachoendelea, Hatupaswi kutumia njia yoyote ile yenye kutaka kujilipia kisasi wenyewe ni muhimu kumuachia Mungu yeye ndiye atakayetulipia kisasi.

 Warumi 12:19Wapenzi, Msijilipizie kisasi, Bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa Kisasi ni juu yangu mimi nitalipa anena Bwana

Kushitaki kile wanachikifanya wadhalimu (Zaburi 94:5-7)

Daudi mwandishi wa Zaburi anaendelea kumwambia Mungu kilie wanachokifanya wadhalimu, wote tunajua kuwa Mungu anafahamu kila kinachoendelea lakini Daudi anataka kufafanua, kuchamganua kile ambacho ameona kinaendelea na anataka Mungu akiangazie 

5. Ee Bwana, wanawaseta watu wako; Wanautesa urithi wako; 6. Wanamwua mjane na mgeni; Wanawafisha yatima. 7. Nao husema, Bwana haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri.”

Daudi anaelezea jinsi sifa ya wadhalimu hao walivyo, hawana huruma, wana kiburi na wanazungumza kwa kejeli na kiburi cha hali ya juu, hawajali hata kile wanachokizungumza, wanazungumza vibaya na wengine, sio watu wa dini wala hawamjali Mungu, wanajiamini wanajitegemea, wanavunja watu mioyo, wanagawa watu, wanawaua watu,hawajali huyu mjana wala yatima, wanajisemesha kuwa nani atatwatetea nani atawaokoa na uwezo walio nao ni makatili, hawajali wageni wala wakimbizi, Daudi aliwasoma vema maadui hawa na kuwaona jinsi walivyo wabaya na wakatili na alieleza Moyo wake kwa Mungu kuwahusu, wako watu Duniani ni wabaya na hawana haya unaweza kujiuliza ni roho ya namna gani waliyonayo na usipate majibu kwamba wanaongozwa na ibilisi au vipi wakati mwingine unaweza kuona ukatiliwao unazidi hata ule wa ibilisi mwenyewe Mungu atulinde na watu wa aina hii 

Kushangazwa na ujinga wa wadhalimu (Zaburi 94:8-11)

8. Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? 9. Aliyelitia sikio mahali pake asisikie? Aliyelifanya jicho asione?         10. Awaadibuye mataifa asikemee? Amfundishaye mwanadamu asijue? 11.  Bwana anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili.”

Daudi anashangwazwa na jinsi wadhalumu hao walivyojawa na roho ya udanganyifu wanafanya uovu mkubwa kwa kujiamini kiasi cha kupofuka macho na kuwa wajinga na wasiofikiri wala kuwa na akili Daudi anauzoefu kuwa Mungu Jaji mkuu atafanya kitu haiwezekani Yeye aliyemuumba mwanadamu awe na sikio kisha yeye mwenyewe asisikie, Yeye aliyemuumba mwanadamu kuwa na jicho kisha asiione yanayotendeka, yeye anayeshikisha watu adabu asikemee udhalimu unaoendelea, yeye anayewafundisha wanadamu sheria na jinsi iwapaswavyo kuenenda asijue uharibifu unaoendelea, anahitimisha kuwa Mungu anayajua mawazo ya wanadamu na anatambua kuwa ni ya ubatili

Wako watu wameharibika mioyo kiasi cha kutokutambua kuwa yuko Mungu anayeona na kusikia, wako watu wanafanya uovu kana kwamba wao ndio Miungu na hakuna awaye yote aliye juu yao, Daudi anasema huu ni ujinga wa watu na unaweza kufanywa na watu wasiofikiri, tena anawaita wapumbavu na anajiuliza ni lini watakapopata akili

Baraka za kupitia katika magumu (Zaburi 94:12-13, 14-15)

12. Ee Bwana, heri mtu yule umwadibuye, Na kumfundisha kwa sheria yako; 13. Upate kumstarehesha siku za mabaya, Hata asiye haki atakapochimbiwa shimo.14. Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake, Wala hutauacha urithi wake, 15. Maana hukumu itairejea haki, Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata.

Daudi anatumia mistari hii kumuita heri mtu anayepitia katika majaribu kwake yeye kupitia katika hali ngumu ni kuadibishwa na Mungu ni kufundishwa sheria na kanuni za Mungu na kuwa hatima ya Mungu ni kuja kutupa starehe wakati wa mabaya na kuwa mwisho wa adui upon a tutawaona adui zetu wakizikwa wakichimbiwa shimo, Daudi aonyesha ya kuwa Mungu hatawatupa watu wake hawezi kutuacha maana kila anayemcha yeye ni urithi wake, ana uhakika kuwa Mungu atafanya hukumu atarejea  na haki itapatikana na waliowanyofu wa moyo watanufaika nayo

Dhuluma zinazoendelea Duniani hazitadumu, uko wakati Mungu atakomesha , atahukumu kwa haki na kuwasterehesha wote walioonewa na mwisho wa wabaya tutauona Ndugu yangu kama asemavyo Daudi na kama lisemavyo neno la Mungu Bwana hatawatupa watu wake hawezi kuuachia Urithi wake 

Hatima ya kucheza na mwenye haki (Zaburi 94:16-23)

16. Ni nani atakayesimama Kwa ajili yangu juu ya wabaya? Ni nani atakayenisaidia Juu yao wafanyao maovu? 17. Kama Bwana asingalikuwa msaada wangu, Nafsi yangu kwa upesi ingalikaa penye kimya. 18. Niliposema, Mguu wangu unateleza; Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza. 19. Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako zaifurahisha roho yangu. 20. Je! Kiti cha udhalimu kishirikiane nawe, Kitungacho madhara kwa njia ya sheria? 21. Huishambulia nafsi yake mwenye haki, Na kuihukumu damu isiyo na hatia. 22. Lakini Bwana amekuwa ngome kwangu, Na Mungu wangu mwamba wangu wa kukimbilia. 23. Naye atawarudishia uovu wao, Atawaangamiza katika ubaya wao, Naam, Bwana, Mungu wetu, atawaangamiza

Mwandishi wa zaburi anahitimisha kwa kuuliza swali nani atasimama kunitetea dhidi ya adui zangu? Na ni atanisaidia dhidi ya waovu au wadhalimu? Kisha anaonyesha kuwa Bwana ni Msaada na kama asingelikuwa msaada waovu waneipoteza nafsi yake, Lakini fadhili za Bwana ni njema na zilimtegemeza Mungu alifanyika faraja kubwa  pamoja na udhalimu wanaoufanya Mungu akikimbiliwa anakuwa mwamba na atawarudisha waovu hawezi kukaa nao kiti kimoja atawaangamiza katika ubaya wao na hakika atawaangamiza 

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu anaona kila aina ya uonevu unaoendelea katika ulimwengu, inatupasa kukata rufaa na kudai haki zetu kwa dua sala na maombi, Mungu atatutetea, ataingilia kati jambo kubwa la msingi ni kumwambia mlipiza kisasi aangaze Tumuombe Mungu wa kisasi aangaze amulike aangalkie aone atazame na kukemea kila aina ya ubaya , uovu  na udhalimu wa watu walioota sugu walioharibika mioyo wasiojali wanaodhulumu, wanaoibia watu wakidhani kuwa hakuna utetezi dhidi ya wanyonge Bwana ana aliangalie jambo hilo na kulikemea Katika Jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!

+255718990796

Jumanne, 15 Novemba 2016

Kumuweka Bwana mbele Daima!



Andiko la Msingi: Zaburi 16:8

Nimemweka Bwana mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.

Utangulizi:

Zaburi hii ni zaburi iliyotungwa na kuimbwa na Daudi, Ni zaburi ya kimasihi hasa kutokana na unabii unaomuhusu Yesu Kristo moja kwa moja, hata hivyo kupitia zaburi hii bado kuna mambo ya muhimu ya kujifunza kutokana na maisha ya Daudi, na uwezo wake aliokuwa nao katika kumtegemea Mungu na faida zake Daudi anatufunulia siri mojawapo kubwa ya ushindi na mafanikio yake katika kudumisha uhusiano na Mungu, katika mstari huu wa nane kuna maswala ya msingi matatu ya kujifunza

·         Kumuweka Bwana mbele Daima
·         Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu
·         Sitaondoshwa!

Kumuweka Mungu mbele Daima.

Moja ya siri kubwa ya ushindi katika maisha ya Daudi ilikuwa ni pamoja na kumuweka Mungu mbele, Katika biblia ya kiingereza neno kumuweka Mungu mbele linasomeka hivi “I have set the Lord always before meNeno “SET” la kiingereza linalotumika hapo liko sawa na neno la kiebrabia “SAWA” kwa msingi huo tafasiri rahisi ya mstari wa aya hiyo katika kiingereza inaweza kusemeka hivi “I have equally set” ambalo katika Kiswahili tunaweza kutumia neno Nimekwenda sambamba na Mungu, au nimetembea sawasawa na Mungu, au kwenda pamoja na Mungu, au kuendenda kwa jinsi ya Mungu lugha hii ya kibiblia ndiyo ambayo imetumika katika Mwanzo 5:22,24 ikionyesha jinsi “Henoko akaenda pamoja na Mungu” kwa hiyo duniani kuna aina tatu za mwenendo, kwa jinsi ya Mungu, kwa jinsi ya kishetani na kwa jinsi ya kibinadamu.

1Wakoritho 3:3 “Kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini, maana ikiwa kwenu kuna husuda, na fitina Je si watu wa tabia ya mwilini; tena mnaendenda kwa jinsi ya kibinadamu

Daudi alidhamiria katika maisha yeke kuenenda kwa jinsi ya Mungu siku zake zote. Hakutaka kuendenda kwa jinsi nya mwili wala ya kishetani aliamua maisha yake yote kumuweka Mungu mbele hii ilikuwa siri ya maisha ya ushindi kwa daudi siku zote za maisha yake.

Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu.

Mkono wa kuume yaani mkono wa kulia kama unavyojulikana sana kwa lugha ya Kiswahili ni kuwekwa mahali pa Heshima kubwa sana, ni sawa na kutawala pamoja, au kukaa katika meza ya kifalme, kuamua pamoja naye, kula pamoja naye kushauriana na kufanya maamuzi ya pamoja, hivyo mtu alipomuweka mtu mkono wake wa kuume maana yake kumuweka mahali pa heshima kubwa
 2Samuel 9:1-9, “1. Kisha Daudi akasema, Je! Amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani? 2. Palikuwa na mtumishi mmoja wa nyumba ya Sauli, jina lake Siba, basi wakamwita aende kwa Daudi; na mfalme akamwuliza, Wewe ndiwe Siba? Naye akasema Mimi, mtumwa wako ndiye. 3. Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu ye yote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu. 4. Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. 5. Basi mfalme Daudi akatuma watu, akamwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. 6. Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumwa wako! 7. Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima. 8. Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi? 9. Ndipo mfalme akamwita Siba, mtumwa wa Sauli, akamwambia, Mali yote yaliyokuwa ya Sauli na ya nyumba yake nimempa mwana wa bwana wako. 10. Nawe utamlimia nchi hiyo, wewe, na wanao, na watumwa wako; nawe utamletea mwana wa bwana wako matunda yake, apate chakula ale; lakini Mefiboshethi, mwana wa bwana wako, atakula chakula mezani pangu sikuzote. Basi huyo Siba alikuwa na wana kumi na watano na watumwa ishirini. 11. Ndipo Siba akamwambia mfalme, Mimi, mtumwa wako, nitatenda hayo yote kama bwana wangu, mfalme, alivyoniamuru. Na kwa habari za Mefiboshethi, mfalme alisema, Atakula mezani pangu, kama mmojawapo wa wana wa mfalme. 12. Huyo Mefiboshethi alikuwa na mwana mdogo, jina lake akiitwa Mika. Na watu wote waliokaa nyumbani mwa Siba walikuwa watumwa wa Mefiboshethi. 13. Basi Mefiboshethi akakaa Yerusalemu; maana alikuwa akila chakula sikuzote mezani pa mfalme; naye alikuwa na kilema cha miguu yote miwili.

Watu wa nyakati za agano jipya walifahamu vizuri umuhimu wa swala hili, swala la kumuweka mtu mkono wa kuume lilimaanisha kumuheshimu mtu huyo kwa kiwango kikubwa na cha hali ya juu, katika serikali kumuweka mtu mkono wa kuume ni sawa na kumfanya kuwa makamu wa rais, wana wa  Zebedayo kupitia mama yao waliwahi kumuomba Yesu wapewe nafasi hii lilikuwa ni ombi la ajabu sana ambalo gharama yake ilikuwa ni kupitia mateso na aibu ileile aliyoipitia Yesu Kristo  Mathayo 20:20-23

Biblia inasema:- 20. Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. 21. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako. 22. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza. 23. Akawaambia, Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.”

Aidha kumuweka mtu mkno wa kuume maana yake ni kumfanya kuwa msaada wako, na ngao yako au mlinzi wako au mtetezi wako.

Daudi kutokana na kumtegemea kwake mungu na kutembea naye alikuwa na uhakika kuwa Mungu yuko mkono wake wa kuume ndiye anayemshauri, ndiye anayemlinda na ndiye anayemtegemea na kwa sababu hiyo alikuwa na uhakika kuwa hatoondoshwa.

Sitaondoshwa!

Kutokuondoshwa kunakotajwa mahali hapo, maana yake ni kuwa salama, kutokusumbuliwa na maadui, kutokuogopa, kutokutikiswa, kulindwa dhidi ya maadui, kuokuingia matatani, kutokuwamo taabuni Zaburi 10:6, kudumu milele Zaburi 15:5, kutokutetemeshwa Zaburi 46:5, Hutotikisika
Kwa ufupi Daudi anatufundish.

1.       Kumuweka Mungu mbele siku zote za maisha yetu
2.       Kumfanya kuwa ngao yetu
3.       Kumfanya kuwa kinga yetu
4.       Kumfanya kuwa tegemeo letu
5.       Kumfanya kuwa mwangalizi wetu
6.       Kumueshimu na kutembea naye
Na tukiyafanya hayo
1.       Tutakuwa na furaha
2.       Hatutatikisika milele
3.       Mungu atakuwa tegemeo letu na ngao yetu

Taifa lolote, chama chochote, mtu yeyote na taasisi yoyote kama tumedhamiria kumuweka Mungu mbele katika maisha yetu mafanikio ni lazima, furaha ya Bwana ndio nguvu zetu, amani ya Mungu ndio nguvu yetu kubwa sana, kama ukimuweka Mungu, katika mitihani, katika maisha ya kila siku, katika kazi zetu, katika ndoa zetu, katika dua zetu na ibada na maombi yetu kila kitu mfanye Mungu kuwa mkono wako wa kuume na utakuwa msindi na zaidi ya kushinda.

Hivi karibuni katika uchaguzi wa Marekani watu wengi sana walishangazwa na matokeo ya uchaguzi huo uliompa Ushindi mkubwa Muheshimiwa Donal Trump wa Republican na ambaye ni kama alikuwa hakubaliki wala kuongoza katika kura za Maoni, na kuking'oa chama cha Democtratic lakini siri kubwa ya Ushindi wa Trump bila kujali madhaifu yake alimuweka Mungu mbele, wakati Democratic walifanya maovu yafuatayo

1. Waliondoa Amri kumi na alama ya Biblia iliyowekwa na George Washington kutoka ikulu ya Marekani

2. walifungisha ndoa za jinsia moja kwa wafanyakazi wa ikulu ya Marekani
Makamu wa Rais wa Marekani wa Chama cha Democratic Joe Biden akifungisha ndoa ya Mashoga ambao ni wafanyakazi wa ikulu ya Marekani jijini Washington DC

3. Uhusiano na Israel wakati wa utawala wa Obama na Chama chake cha  Democratic ulipoa na ulikuwa wa kinafiki

Sriri ya ushindi wa Donal Trump wa Republican

1. Alumuweka Mungu mbele na kuchukizwa na uovu unaofanyika Washington DC ikulu


2. Ana uhusiano mzuri na Israel na ameahidi kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv Jaffa kwenda Mji mkuu wa milele wa kiyahudi Yerusalem


3 baada ya kuteuliwa alifanyiwa maombi na watumishi wa Mungu kuonyesha kumtanguliza Mungu katika kila jambo
Katika mifano hii iliyohai utakuwa umejifunza kwamba kumuweka Mungu mbele na kumuheshimu kutakufanya usiondoshwe milele


Rev. Innocent Kamote
“Mkuu wa Wajenzi mwenye hekima”