Jumanne, 27 Juni 2023

Inzi wanaposumbua Nyumba yako.


Kutoka 8:20-22 “BWANA akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, BWANA asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi. Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta wingi wa mainzi juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na wingi wa mainzi, na nchi nayo ambayo wa juu yake. Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi BWANA kati ya dunia.” 

 




Utangulizi:

Watu wengi sana huwa wanachukizwa sana na wakati mwingine wanapata hasira wanaposumbuliwa na Inzi katika nyumba zao, hii ni kwa sababu inzi katiika jamii nyingi wanahusishwa na uchafu, na wakati mwingine pia kusambaza magonjwa hivyo kimsingi inzi hawapendwi na ni machukizo kwa watu wengi sana duniani, wakati mwingine nzi wanaweza hata kutoa milio Fulani ya kuudhi au kujazana mahali, Jambo ambalo linakera na linaleta maudhi na wakati mwingine kuruka ruka katiika miili ya watu! Hata hivyo katika lugha ya kinabii inzi wanapotokea katika nyumba yako wana habari Fulani njema au mbaya ya kukupasha, katika ulimwengu wa kiroho, na hivyo ni muhimu kuwa na usikivu wa rohoni mainzi yanapotawala katika nyumba yako! Tutajifunza somo hili Inzi wanaposumbua nyumba yako kwa kuzingatia maeneo manne yafuatayo:-

i.                    Inzi katika mtazamo wa kibiblia

ii.                  Inzi wakiwa ni ishara njema

iii.                Inzi wakiwa ni ishara mbaya

iv.                 Mambo ya msingi yakupasayo kufanya

Inzi katika Mtazamo wa kibiblia

Hatunabudi kufahamu kuwa nzi ukiacha kwamba ni wadudu wa kawaida lakini pia wanatazamwa tofauti katika mtazamo wa kibiblia kwanza wanawakilisha malaika waovu au pepo wachafu, na dhana hii iko katika maandiko agano la kale na jipya ambapo hata mkuu wao aliitwa Beelzebubu ona mfano katika

Luka 11:14-15 “Naye alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu. Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo.”

Katika kifungu hicho cha maandiko Wayahudi walimshutumu Yesu wakidhani ya kuwa anatumia nguvu za mkuu wa pepo Beelzebuli kutoa Pepo, kumbe yeye alitoa pepo kwa uweza wa Roho Mtakatifu na alifafanua kuwa shetani hawezi kumtoa shetani, sio kusudi langu kufafanua jambo hilo kwa undani kwani ninachikitaka hapa ni kufafanua tu huyu BEELZEBULI ni nani ?  Kimsingi jina hili Wayahudi walitoka nalo huko ukaldayo na hapa limeandikwa kwa lugha ya Kiyunani, kiyunani ni BEELZEBOUL ambalo tafasiri yake ni mkuu wa Pepo wachafu, au mfalme wa pepo wachafu jina ambalo kimsingi linamuhusu shetani,  aidha katika maandiko pia huko katika nchi ya wafilisti katika mji ulioitwa Ekron kulikuwa na mungu baali ambaye alikuwa anahusishwa na swala la kufukuza Inzi huyu aliitwa Baal-Zebub mungu wa Ekron ona katika

2Wafalme 1:2-4 “Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu. Lakini malaika wa Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi sasa, Bwana asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka.”

Mungu huyu wa wafilisti aliitwa BAAL ZEBUBU jina ambalo kwa kiingereza humaanisha “BAAL OF FLIES”  yaani mungu wa mainzi, mungu huyu alisadikiwa kuwa na uwezo wa kufukuza mainzi, Hakuna uhakika sana kama kuna muununganiko wa kimaana kwa majina hayo na lile la agano jipya lakini huyu pia alikuwa ni shetani kwa hiyo bado tunaweza kuona Mapepo na mashatani yakihusishwa na mainzi, kwa sababu ya uchafu. Au jina lile pepo wachafu.

Huko Misri nako wakati wa hukumu ya Mungu dhidi ya Farao ili awaachie wana wa Israel Mungu aliipiga Misri kwa hukumu ya pigo la mainzi

Kutoka 8:20-22 “BWANA akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, BWANA asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi. Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta wingi wa mainzi juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na wingi wa mainzi, na nchi nayo ambayo wa juu yake. Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi BWANA kati ya dunia.”

Kimsingi pigo hili pia ilikuwa sio hukumu kwa Farao na wamisri tu bali pia kwa miungu ya wamisri, mungu aliyekuwa anahukumiwa hapa kwa wamisri ambao walikuwa na miungu wengi mmoja wapo ni  mungu aliyekuwa anajihusisha na kufukuza inzi, kwa uweza wa Mungu alikuwa akionyesha kuwa kama Mungu akiwatumia inzi kama sehemu ya hukumu miungu hiyo haiwezi kuzuia kusudi kuu likiwa lile lile Farao aweze kujua ya kuwa Yehova ndiye Mungu pekee duniani.

Kwa hiyo tunaweza kukubaliana wazi na wazo la kibiblia kuwa inzi wanawakilisha pepo wabaya na mkuu wao ni shetani, katika lugha ya kinabii, hata hivyo ni muhimu kufahamu kuwa kinabii inzi wa kawaida wanapoanza kuiandama nyumba yako huwa kunakuwa na maana za msingi za kiroho zinazowakilishwa maana hiyo inaweza kuwa ya hatari na mbaya au maonyo ya kutokupuuzia maeneo Fulani muhimu katika maisha yetu. Inzi kinabii pia wanawakilisha chuki, uovu, au lawama kwa sababu wanaruka ruka hovyo na kubughudhi watu, wanawakilisha pia tabia mbaya, kukosa kiasi na hisia mbaya, lakini pia wanawakilisha mambo mazuri kama tunavyoweza kujifunza katika vipengele vifuatavyo:-

Inzi wakiwa ni ishara njema

Inzi wakiwa na ishara njema huwa wanabeba maana zifuatazo:-

1.       Inzi wanashiria kuwa kuna mambo unapaswa kuyafanyia maamuzi magumu  - Inzi wanapokufuata futa katika nyumba yako wanakupa ujumbe kuwa kuna maamuzi magumu unapaswa kuyafanya ili kuleta mabadiliko makubwa katika maisha yako, yako mambo aidha unapaswa kuachana nayo, au kuna jambo unapaswa kuliachia kabisa katika maisha yako, kama iko tabia mbaya ambayo inachangia kwa kiwango kikubwa kuharibu maisha yako tabia hiyo iachwe mara moja, kama yuko mtu anakusababishia kufanya mambo mabaya mtu huyo uachane naye haraka, au mara moja, kuna ujumbe wanaokupa nzi kuwa kitu hicho kibaya kiondoke katika maisha yako, hivyo utapaswa kujitafakari na kuangalia ndani yako na mazingira yako na kile utagundua kuwa ni sababu ya wewe kutokuendelea au kuharibikiwa basi utapata jibu kuwa unatakiwa kukifukuzilia mbali kama vile tunavyotafuta kuachana na nzi, tahadhari hapa usichukue maamuzi bila kufikiri kwa kina na ukijisikilizia kwa ndani ndipo utagundua ni kitu gani watu au mtu gani mbaya anakusababishia mkwamo katika maisha kisha utatafuta njia mbadala za kuachana na jambo hilo kwa amani!

 

2.       Inzi wanakupa taarifa ya jambo jipya kutokea katika maisha yako – Ishara ya nzi sio tu wakati wote ni mbaya kama watu wanavyodhani lakini wanapokuandama inamaanisha kuwa kuwa kuna kitu kinaenda kuisha au kufikia mwisho katika maisha yako  na jambo jipya kabisa linaenda kutokea katika maisha yako, ni ishara ya kuisha kwa jambo Fulani katika maisha yako na kuanza kwa jambo jipya kabisa, hivyo kuwaona inzi wazi wazi kabisa au kwenye ndoto  ni ujumbe ambao unakueleza kuangalia jambo jipya kabisa katika maisha yako, a kulipokea vizuri kwani mabadiliko hayo yanaweza kuleta  nafasi usiyoitarajia.

 

3.       Inzi wanakupa taarifa ya kwamba kuna jambo linalokuondolea umakini - aidha unalijua au hulijui kama ni mtu aidha unamjua au humjui anakunyima usingizi, anakusumbua au ndio sababu ya kuharibikiwa kwako na kukuletea migandamizo katika moyo , unapoona inzi fikiria kwa kina kama kuna mtu katika maisha yako uwe unamjua au humjui anasababisha mabaya katika maisha yako iwe unajua au hujui, mtu huyo lazima umfanyie mkakati wa kumuacha au kuharibu nguvu anayoitumia kuharibu maisha yako mtu huyo aondoke au uache mawasiliano naye katika maisha yako kabisa. Kumbuka isiwe kwa ugomvi Mungu ametuita katiia mani.

 

4.       Inzi wana ujumbe kuwa kuna watu au mtu unampuuzia  kama unavyoona inzi wanapotusumbua huwa tunawapuuza, na kuwafukuza kwa dharau japo nzi hao hawataenda mbali na wataendelea kutusumbua hii ni ishara kuwa kuna watu wanakuhitaji lakini unawapuuzia hujawapa kipaumbele, ni mtu au watu wanaokupenda sana lakini umewapuuzia, au ni marafiki wa maana sana lakini umewapuuzia, inawezekana hata wakituma ujumbe unawapuuzia hujibu,  anza kujihoji kwa makini, na kwa uangalifu mkubwa kama umepuuzia na kuharibu urafiki na watu muhimu katika maisha yako au umeshindwakugundua umuhimu wa watu hao tunza na kurudisha urafiki haraka imarisha mahusiano na wote walio muhimu kwenye maisha yako

 

5.       Inzi wanakupa taarifa wazi kuwa unakabiliwa na hofu – Hofu hii ni hofu ya kupoteza mtu wa karibu sana umpendaye au kupoteza kazi, labda mambo hayaendi vizuri kazini na una mashaka ya kupoteza kazi hivyo kuna hofu inaanza kujengeka ndani yako, inzi wanakutaarifu kuhusu hofu yako ili uweze kujihami mapema kwa kufikiri kuondoka kazini au kutafuta kazi nyingine ambayo itaendana na hisia zako na kuachana na ile inayokupa mikandamizo ya moyo.

 

6.       Inzi wanawakilisha uwezo wako wa kukabiliana na mazingira – Inzi wanakupa ujumbe kwamba wewe sio wa kupuuzwa kuna nguvu kubwa ndani yako ya kukabiliana na mazingira nzi wanauwezo wa kuishi kokote na katika mazingira yoyote yawe mazuri au mabaya, wanauwezo wa kujipatia chakula hata katika mazingira yanayofikiriwa kuwa hayafai,  wana wanakupa ujumbe kuwa hata wakikutupa kama taka taka wewe ni hazina kwa wengine, inzi wanakupa ujumbe wa kufanikiwa, kuwa na vingi sana kuwa tajiri, kuwa na uwezo mkubwa wa kuhamasisha watu kuwa na uwezo wa kuishi katika mazingira hata ya kukataliwa, uwezo mkubwa wa kuvumilia magumu, huku ukiendelea na maisha na kujitafutia chakula , inzi wanakukumbusha kuwa wewe ni mtu mgumu sana  na unaweza kukabiliana na mazingira yoyote yanayobadilika, yawe mazuri au mabaya.

 

7.       Inzi wanakukumbusha kuwa una hasira -  na kwamba unatakiwa kumudu hasira yako, katika maisha, inzi hatuwezi kuwadhibiti sisi wenyewe  kwa msingi huo, hata hasira lazima tujifunze namna ya kuidhibiti ili isituletee madhara

Inzi wakiwa ni ishara mbaya

Inzi pia wana ujumbe mbaya na wa kuvunja moyo

1.       Inzi wanaujumbe wa kukutaarifu kuwa kuna jambo baya. – kuna jambo baya lisilopendeza, la kuudhi au lenye kuingilia mipango yako na kukuharibia kama vilevile tunavyoona inzi wakiwa wasumbufu, wenye maudhi na kutua tua katika mazingira tusiyoyapenda ndivyo wanavyoashiria kuwa kuna tukio litaingilia kati katika maisha yako kulete usumbufu, kukuharibia kukukatisha kukuudhi na kadhalika au jambo la kukuondolea amani, na au kukupa fadhaa, kiroho unajua nini unachopaswa kukifanya kuifuta hali hiyo.

 

2.       Inzi ni taarifa ya kifo – Kwa kawaida inzi pia wanapenda kitu kilichokufa au kilichooza au chenye harufu mbaya au shombo, nzi wanapoonekana katika ndoto au halisi wakiwa nyumbani kwako huashirikia kifo cha mtu aliye karibu sana na wewe ambaye hungependa afe  hata hivyo Inzi pia wana ishara ya ufufuo, kwa kuwa huzaliwa kama yai kisha buu kisha inzi hutokea kwa hiyo kuna ishara ya maisha mapya.

 

3.       Uwepo wa Inzi pia huashiria kuvunjika kwa mahusiano, - kwa hiyo watu wanapaswa kuzungumzia mahusiano yao ili ikiwezekana wayajenge kama wanaweza kuimarisha uhusiano wao na kila mmoja ajali hisia za mwenzake, kama watu hawataimarisha mahusiano yao ni dalili inayoonywa na nzi kuwa uhusiano unakwenda kuvunjika, inzi wanakupa ishara mbaya ya matukio mabaya ya kiroho, hivyo tunapowaona tunaweza kurekebisha hali ya mambo isiwe mbaya vinginevyo kitu kibaya kinakwenda kutokea na watu watafukuzana kama unavyofukuza inzi.

 

4.       Inzi wanashirikia haribiko – inaweza kuwa haribiko ambalo limekwishatokea au linalokwenda kutokea, labda ulikuwa ukifanya kazi na kuwafurahisha wanaokuzunguka na kukuajiri na umesahahu jambo muhimu sana unalotakiwa kulifanya sasa unapaswa kuangalia kile unachotakiwa kukifanyia kazi na kile kinachohusina na maisha yako, panga mipango yako mwenyewe na kaa katika hiyo ili uweze kufikia malengo, vunja malengo makubwa na angalia madogo ambayo unayamudu inaweza kuwa jambo sahihi kwako, kama unagundua kuwa umetoka katika mpango  anza kujipanga sasa panga mpango utakaokufaa ni rahisi kuwa kutokujisikia vizuri lakini itakusaidia kufanya mambo ya muhimu.

 

 

5.       Huwezi kufanya lolote – Inzi wanakupa ujumbe kuwa mambo yanayokutokea au yatakayokutokea  yako nje ya uwezo wako huwezi kuyadhibiti kinachokutokea kiko nje ya uwezo wako kama unavyoona inzi hujawaleta wewe unawaona tu na wanakuletea usumbufu ndivyo ilivyo katika maswala yanayokutokea au yatakayokutokea  kwa imani kumbuka tu kuwa Mungu anatawala.

Mambo ya msingi yakupasayo kufanya

Hakuna sababu ya kuogopa unapoona inzi katika nyumba yako, hawako hapo kwa makusudi ya kukutisha lakini wako hapo kukupa ujumbe kuhusu mambo yajayo, hivyo jipange jipe moyo kaa tayari kukabiliana na lolote litakalokusibu, weka moyo wako kwenye mipango yako, wasiliana na watu muhimu sana katika maisha yako, fanya kazi kwa bidii weka mahusiano yako vizuri, usiogope jambo baya wala taarifa mbaya jiandae kukabiliana na lolote gumu litakalokukabili, Muombe sana Mungu kwa kuahirisha mambo mabaya na kumshihi Mungu alete mambo mema siku zote za maisha yako, hakikisha kuwa unakuwa safi kwani kama jinsi ambavyo inzi wanavutiwa na uchafu, lisiwepo ovu katika maisha yako litakalokuchafua.

KUMBUKA. Mafundisho haya ya katika shule za kinabii na kama imani yako inakinzana usitilie maanani wala usifundishe kanisani kwako!

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Ijumaa, 16 Juni 2023

Basi Ninyi mtakuwa wakamilifu


Mathayo 5:43-48 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya msingi mkuu wa malengo ya Mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo ilikuwa ni kuwafanya watu wote waliomuamini kuwa wakamilifu, katika tabia na mwenendo, Kwa bahati mbaya kanisa la Mungu katika nyakati za leo tumeacha kukazia mafundisho yetu katika uadilifu kama ilivyokuwa kwa Yesu na Mitume na badala yake kuwaelekeza watu katika maswala mengine!. Pamoja na kuwa agizo la Mungu ni pana sana lakini ni muhimu vile vile tusiache kabisa kurudi katika msingi na kuwakumbusha watu kulenga katika kukua kiroho, kimaadili na mwenendo! Hili ndio kusudi mojawapo kubwa la kuwepo kwa kanisa.

Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;”         

Nadhani unaweza kupata picha iliyo wazi kusudi la Kristo kulipa kanisa Mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji na walimu ni ili watu wa Mungu wajengwe kwa mafundisho na maelekezo wakue na kukomaa na hatimaye waweze kuwa na tabia na mwenendo na sifa sawa na zile alizokuwa nazo Kristo, hakuna gharama kubwa kama hii ya kutokuwa na wakristo waliokomaa kiroho, wasio na ufahamu wala ujuzi wa neno na wanaoacha kukua kiroho na kiuelewa na kubaki katika udumavu, uchanga na kutokuwa na tabia na mwenendo unaofanana na baba yetu wa Mbinguni, tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-

*      Maana ya neno ukamilifu

*      Kipimo cha mtu aliyekomaa kiroho, kimaadili na kimwenendo.

Maana ya neno Ukamilifu.

Unapoyachunguza mafundisho ya Yesu na Mitume kuhusu ukamilifu utaweza kuona kuwa kuna jambo walilolokuwa wakililenga zaidi katika mafundisho yao, Kwa kawaida mwanadamu hawezi kuwa mkamilifu kama Mungu, Mungu anatajwa kuwa mkamilifu na muadilifu na kuwa hakuna uovu wowote ndani yake ona:-

Kumbukumbu 32:3-5 “Maana nitalitangaza Jina la Bwana; Mpeni ukuu Mungu wetu. Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; Maana, njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye haki na adili. Wametenda mambo ya uharibifu, Hawawi watoto wake, hii ndiyo ila yao; Wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka.”

Mwanadamu alikuwa na ukamilifu wa uadilifu, haki na kutokuwa na uovu mara alipoumbwa na Mungu katika bustani ya Edeni na ndio maana alikuwa na uhusiano na Mungu wa karibu kama Baba na Mwana wake, Hata hivyo baada ya anguko la mwanadamu, Mwanadamu alipungukiwa kila eneo  la maisha yake, alipoteza haki, alipungukiwa na uadilifu na kupoteza ushirika na Mungu wa moja kwa moja ona:-

Warumi 3:23 -24 “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;”

Mwanadamu aliyemuamini Yesu Kristo na kazi yake ya ukombozi iliyofanyika pale Msalabani, kama akifunzwa vyema katika kanisa analokuweko anaweza kuwa mkamilifu katika uadilifu kama alivyo Mungu, ukamilifu huu ambao umetajwa katika maandiko tunaweza kujifunza maana zake kama ifuatavyo:-

Mathayo 5:48 “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Neno hilo Nanyi mtakuwa wakamilifu katika maandiko ya kiyunani yanasomeka kama “TELEIOS”  neno hilo linasomeka kama “PERFECT” katika kiingereza, lakini hata hivyo neno hilo halitoshelezi katika kuelezea ukamilifu unaokusudiwa kwa kiyunani neno hilo teleios maana yake ni complete or application of labor growth, mental and moral character  na katika maana nyingine pia ni full of age,  kwa hiyo ukamilifu unaozungumzwa hapo ni kufikia kwenye uwezo wa kujitambua (Maturity), kuacha ujinga, kukomaa kimaadili, na kitabia na kimwenendo  na maandiko yanaonyesha kuwa jambo hili linawezekana kabisa kwa kila mkristo aliyeitwa na Mungu kwa kuokolewa

1Petro 1:14-16 “Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

Unaweza kuona! kumbe kama mtu ameokolewa na amekuwa mwanafunzi waYesu na kisha bado akawa anaenenda kama kwanza yaani kama ilivyokuwa kabla ya kuokolewa anafanya ujinga, HAJAJITAMBUA, kwa hiyo ni lazima kila mtu aliyeokolewa afunzwe aondoke katika ujinga awe na akili abadilike katika tabia na mwenendo na kuwa na tabia ya uungu, yaani kuwa kama Mungu, unaona utakatifu unaozungumzwa hapo katika waraka wa Petro wayunani  wanautaja kwa kutumia neno HAGIOS  ambalo pia linazungumzia Morally Blemeless  yaani kufikia ngazi ya kutokuwa na lawama kimaadili  na kujiweka wakfu kama wafanyavyo makuhani ona

Waebrania 7:6 “Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu;”             

Kwa namna Fulani Mungu anataka wanafunzi wakristo, wakue wakamilike, wakomae, wakue waondoke katika maswala na tabia za kitoto na za kijinga, kutokukua kiroho kunatupelekea kuwa na kanisa yaani watu ambao wameokolewa kwa kumuamini Bwana Yesu lakini wakiwa na tabia mbaya kama tu watu wa kawaida wasiomjua Mungu, watu ambao Hawajajitambua, Paulo mtume anawaita wakristo wa namna hii kama wakristo wenye tabia ya mwilini ona

1Wakorintho 3:1-3 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu?

Watu wenye tabia ya mwilini katika kiingereza wanaitwa  “CARNAL”       neno hili la kingereza linalotumika hapo katika kiyunani linatumika neno “SARKIKOS” ambalo maana yake ni tabia za KINYAMA  hii maana yake ni kuwa katika kanisa la Korintho japo wakristo walikuwa wameokoka na kumuamini Yesu kama Bwana na Mwokozi, bado kulikuwa na ukosefu mkubwa wa huduma ya mafundisho ya kichungaji na kitume, kwa msingi huo wakristo wa Korintho japo walibarikiwa sana kuwa na karama za Rohoni lakini vilevile tunaona kuwa kanisa hili lilikuwa limejaa tabia za kinyama  mfano:-

-          Kulikuwa na Mafarakano na ushabiki wa wahubiri wa injili - kama tu ilivyo leo 1Wakorintho 3:4-9 “Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye. Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe. Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu

 

-          Kulikuwa na husuda na fitina – sio jambo la kushangaza leo katika jumuiya ya Kikristo kuona watu wakiwa wamejaa fitina majungu na mafarakano, wakristo wakisingiziana mambo makubwa ya uongo bila hata kuchomwa mioyo katika dhamiri zao ona 1Wakorintho 3:3 “kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? wakristo katika nyakati za siku hizi wamefikia ujinga wa hata kuchomekeana mambo mabaya, kuuana, kuwekeana sumu au kutumiana watu wasiofaa kitu kufanya mauaji, na kutengeneza keshi na skendo za kuchafuana  sio kiu cha ajabu


-          Kulikuwa  na zinaa za kupita kawaida -  yaani kulikuwa na watu waliozini mpaka na wake za baba zao, yaani zinaa zisizokuweko hata katika mataifa ona 1Wakorintho 5:1-3 “Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo. Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo.” Leo hii watu kuzini na wachungaji, wake za wachungaji, wazee wa kanisa na watu wenye sifa katika kanisa limekuwa jambo la kawaida watu wanakula stori za zinaa kama jambo la kawaida tu hofu na hali ya kumcha Mungu imeondoka na neema ya Mungu imechukuliwa kama njia ya kujihurumia katika kuteda dhambi na kuzihalalisha, mwenendo wetu haufanani tena na makusudi ya kuwepo kwa kanisa la kristo duniani

 

-          Watu wasiokubali kuachilia – Katika Kanisa la Kristo kule Korintho na kama ilivyo leo kulikuwaweko watu wasiotaka kupoteza, kila wakati walitaka kuonekana kuwa ni washindi, katika Kristo tumepewa sio kumwamini tu bali na kuteswa kwaajili yake, watu waliokomaa kiroho sio lazima kila kitu washinde, wakati mwingine iko haja ya kuachia na kupoteza Korintho watu walipelekana mahakamani ona 1Wakorintho 6:1-8 “Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu? Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya? Basi, mkiwa na mahali panapohukumiwa mambo ya maisha haya, mwawaweka kuwa waamuzi hao waliohesabiwa kuwa si kitu; katika kanisa? Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake? Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini. Basi imekuwa upungufu kwenu kabisa kwamba mnashitakiana ninyi kwa ninyi. Maana si afadhali kudhulumiwa? Maana si afadhali kunyang'anywa mali zenu? Bali kinyume cha hayo ninyi wenyewe mwadhulumu watu na kunyang'anya mali zao; naam, hata za ndugu zenu.” Je katika siku za leo hujawahi ona watu wakristo wakidhulumiana je hujawahi ona wakristo wakipelekana mahakamani? Wakisingiziana wakitakiana mabaya maswala kama haya yanaweza kutokea tu kama watu hawatatafuta kuwa wakamilifu kama baba wa Mbinguni, niliwahi kumsikia Mkristo mmoja aliyekuwa anahusika na kuajiri watu mahali Fulani akitamka kuwa nitahakikisha huyu kijana (mwajiriwa wake) ananyooka na kukimbia na kurudi kijijini, ni matamshi hatari sana sio ya mwajiri wa kawaida wa dunia hii ni Mkristo akihakikisha kuwa anaharibu maisha ya mtu mpaka mtu huyo akimbie mjini?  Nimewahi kumsikia Mkristo mmoja akipanga njama ya kuharibu kibali cha mtu na akiwa na nia hata ya kusambaza skendo kwa kuhakikisha kuwa anamuandika mtu gazetini ili kumuharibia kibali chake wivu husuda na dhuluma na masingizio leo imekuwa ni tabia ya kawaida ya Wakristo, nataka nikuhakikishie kuwa hakuna jambo baya sana duniani kama kuwa na Kanisa la watu walioharibika, waliodumaa kiroho na wasiokua kiroho na kimaadili na wasiojitambua, wanageuka na kuwa wanyama kabisa, Mkristo anadhulumu wenzake na anaendelea kuabudu bila wasiwasi huku akiwatishia wale aliowadhulumu, Wakristo ambao wamedumaa kiroho na kutokukomaa na kukua ni tatizo kubwa sana na linasumbua sana jamii ya Wakristo na makanisa tuliyonayo leo.

 

-          Kuweko kwa wakristo wasio na faida – Waebrania 5:11-14 “Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia. Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.” Mwandishi wa kitabu cha waebrania anasikitishwa na wakristo walio na miaka mingi kanisani lakini wamedumaa hawakui Kiroho muda mwingi umepita lakini hawawezi kuwa walimu maana yake hawajakua kufikia hata ngazi ya kuweza kuwafundisha na wengine kwa kuhudumu katika kufundisha neno la Mungu lakini pia hata wao wenyewe kushindwa kuwa somo, kuwa kielelezo leo tuna wakristo wana miaka mingi sana katika imani lakini ni wabovu katika kiwango ambacho huwezi kujifunza kitu kutoka kwake, huwezi kuona tofauti yake na watu wa duniani  na wakati mwingine hata wale wa duniani huonekana kuwa wana nafuu, changamoto hii inatokana na kutokujali swala la kuwa wakamilifu katika mwenendo wetu yaani kuwa na tabia ya Kristo!

 

-          Kuwepo kwa karama na miujiza mingi lakini tabia mbaya – Kanisa la korintho lilikuwa ni kanisa lililokuwa na neema ya kuwa na vipawa vingi na karama nyingi na watu wengi sana waliokuwa wakinena kwa lugha lilijaliwa vipawa vingi sana vya rohoni lakini pia kulikuwa na changamoto nyingi za kimaadili kwa kanisa hilo, unaona Paulo anawafundisha namna bora ya kutumia karama za rohoni lakini vilevile akiwafundiaha njia iliyo bora ambayo ni upendo, kama ilivyokuwa kwao nyakati za leo tuna watu wenye vipawa vingi na Mungu anawatumia sana na watu wanawafuata lakini wana tabia mbaya hakuna uadilifu kuanzia namna wanavyofanya huduma bila adabu, lakini wakiwa na tabia zisizovutia na wakristo wajinga waochukuliwa na mawimbi ya watenda miujiza wakidhani kuwa kila mtenda miujiza ni wa Mungu, Kipimo cha ukomavu wa mtu kiroho sio miujiza bali ukomavu katika uadilifu na upendo, Kristo atawakataa wahubiri wote, na watumishi na manabii ambao kweli kwa jina lake watafanya miujiza na kutoa unabii lakini tabia na mwenendo wao kwa vipimo vyake hauonekani kuwa wenye kufaa.

 

Mathayo 7:21-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”

 

Kipimo halisi cha kiroho sio mkutenda miujiza bali kuishi maisha ya utakatifu na kuzaa matunda ya roho, mtu mmoja alisema mnadhani waislamu huenda msikitini kwaajili ya miujiza? Wao huacha maduka yao na biashara zao na kukimbilia katika nyumba za ibada kwaajili ya kusali na kuabudu tu, Wakristo wa leo ni kama wasipoona muujiza kabisa wanadhani kuwa Mungu hayuko mahali hapo Yesu alikisikitishwa na watu ambao hawawezi kumuamini hivihivi tu mpaka ziweko ishara

 

Yohana 4:46-48 “Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; kwa maana alikuwa kufani.Basi Yesu akamwambia, Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?

 

Wakristo wasiokomaa na kukua katika uadilifu na mwenendo hukimbizana huku na huko wakitaka kuona miujiza na ishara hawawezi kumuamini Mungu pasipo miujiza, je unadhani ukuu wa Muhubiri ni miujiza tu hapana! Hatusomi kokote pale ambapo Yohana mbatizaji alifanya muujiza wowote lakini Yesu alimsifika kuwa katika uzao wa mwanamke hakuna aliye mkuu kama Yohana Mbatizaji ona

 

Luka 7:24-28 “Basi, wajumbe wa Yohana walipokwisha ondoka, alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Jueni, watu wenye mavazi ya utukufu, wanaokula raha, wamo katika majumba ya kifalme. Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye zaidi ya nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. Nami nawaambia, Katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana; lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye.”

 

-          Watu wanaochukuliwa na upepo wa kila aina ya Elimu – Waefeso 4:11-15 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, KristoNeno la Mungu limemaliza kila kitu kuna upepo wa kila namna wa Elimu na hila za watu na ujanja na njia za udanganyifu hizi zipo, kukosekana kwa Elimu sahihi ya neno la Mungu kumewafanya wakristo wa leo kuchukuliwa na hizi pepo biblia ya NIV inatumia neno “WAVES” yaani neno la Mungu linatambua kuweko kwa mawimbi,  au pepo katika maswala ya neno la Mungu  na kazi zake wakati mwingine hutokea amsho za aina mbalimbali za huduma au watu wengine ni watumishi halisi wa Kristo lakini wengine huangukia katika hayo mawimbi ambayo kimsingi huinuka na kutoweka, kama wakristo hawajaimarishwa vizuri wakabaki wachanga kila wakati  linapotokea wimbi la aina moja utaweza kuona wakristo hao wakristo hao wakiruka na wimbi hili na lile badala ya kukua, kukomaa na kufikia ngazi ya kutumika kwa uaminifu katika eneo lako uliloitiwa. Kwa ujumla tunajifunza na kuona kuwa kuna hasara kubwa sana ya kuwa na wanafunzi wa Bwana Yesu wasiokuwa na moyo wa kutafuta ukamilifu!

 

-          Kubadili neema ya Mungu kuwa ufisadiYuda 1:4 “Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo.”

 

Moja ya changamoto kubwa pia inayolifanya kanisa la leo kushindwa kuishi maisha ya ukamilifu ni matumizi mabaya au tafasiri mbaya ya mafundishio kuhusu neema, kupitia mkazo mkubwa na wa kijinga kuhusu neema ya Mungu watu wengi wamejikuta wakiishi maisha ya dhambi na kutokubadilika kwa kisingizio tu kuwa Mungu ametupa neema na tunaishi wakati wa neema, lakini Paulo mtume akifundisha kuhusu Neema ya Mungu aliweka mkazo ulio wazi kuwa neema sio tiketi ya kuishi maisha ya dhambi ona

 

Warumi 6:1 -2 “Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? ”  

 

Neema ya Mungu kazi yake ni kuturahisishia kuishi maisha ya haki na utauwa bila kutumia nguvu kama wakati wa sharia, neema inasaidia kuwa kama Kristo alivyo na kama Mungu wa mbinguni alivyo ni neema ya Mungu inayotusaidia kuwa wazuri, wenye maisha ya kiasi na sio kuishi maisha mepesi ya dhambi. Ndani ya neema ya Mungu kuna uweza wa kiungu wa kutuwezesha kuishi maisha ya kumpendeza Mungu  nay a viwango ona

 

Tito 2:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;”

 

Unaona neema sahihi inatusaidia kukataa tama na ubaya, kukataa tamaa za kidunia, kutupa uwezo wa kuishi maisha ya kiasi, haki na utauwa katika ulimwengu huu huu, kwa hiyo hakuna neema inayokuelekeza kuishi maisha ya dhambi, lakini kutokana na mafundisho mabaya kuhusu neema kanisa la leo linachukulia dhambi kama jambo poa na lisilo la ajabu. Ni neema ya Mungu ndiyo inayotusaidia kubadilika na kuwa na tabia kama ya baba wa Mbinguni nanyi mtakuwa wakamilifu, ukamilifu huu hauwezekani bila neema sahihi, kama utafundishwa kuwa kuna neema na inakusaidia kuona uko sawa dhambini hiyo itakuwa ni injili nyingine neema ya Mungu itaachilia hukumu ndani yako itakayokuleta katika toba wala sio kuishi dhambini, Moja ya changamoto inayowafanya wanafunzi wa Yesu leo kutokuwa wakamilifu kama baba wa mbinguni ni mafundisho kuhusu neema iliyopitiliza, ambayo inakufanya udumae na sio upokee mabadiliko

                               

-          Kufilisika kiroho  - Kanisa linapopoteza mwelekeo sahihi hususani katika fundisho la kuwa na tabia njema na mwenendo mwema na kuwa wakamilifu na kuishi maisha ya utakatifu na tukakazia maswala mengine  yasiyo na  umuhimu kama kutajirika tunaweza kujikuta kuwa tuna changamoto nyingine mbili, jina la kuwa tajiri, lakini ni masikini yaani kanisa limekuwa na utajiri wa mali za kawaida lakini limekuwa masikini na limepungukiwa na kuwa na umasikini wa tabia za uungu, kanisa lina jina la kuwa hai lakini limekufa  lina mali lakini liko uchi ona

 

Ufunuo 3:1 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa.”

 

Ufunuo 3:16-17 “Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.”  

 

Unaona hali ya kanisa la watu wasiolenga kukamilika hubaki katika kusheherekea mafanikio ya kimwili huku nguvu za rohoni zikiwa zimefilisika, niliwahi kumsikia askofu wa kanisa Fulani msomi mkubwa akinieleza ya kuwa kulikuwa na wachawi kanisani kwake na walikuwa wakikopera sadaka mpaka aliposimama na kuwakemea waache tabia hizo? Ndipo wachawi wakapunguza kukopera sadaka, Kama kweli kanisa la Mungu linaweza kufikia hatua ya kuweza kuwa na wachawi  ndani na wakahudhuria ibada  na wanaamini na kuweza kufikia ngazi ya kukopera sadaka haiingiia akilini kuendelea kufikiri kuwa kanisa lina uhai, afadhali kidogo kama ningesikia kuwa kuna waizi wanaiba sadaka wakati wa kuhesabu na tumewakamata kupitia ccctv Camera kidogo ingeweza kuingia akilini kufikiri hivyo lakini kama zinakoperwa ni wazi kuwa tunahitaji kuwa na uamsho na kuruhusu nguvu za Mungu kutamalaki na kuweka msisitizo mkubwa wa kuweko kwa tabia ya ukamilifu kama baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Bado tunaweza kushuhudia na kuelewa kuwa hakuna jambo baya sana duniani kama kutokulifundisha kanisa kuwa na tabia na mwenendo ulio mkamilifu, tungeweza kuchambua mambo kadhaa wa kadhaa yanayodhihirisha kuwa tunamuhitaji Mungu na tunahitaji kukua kiroho na kuwa wakamilifu lakini nadhani kwa maswala hayo machache umeweza kuona kuwa msisitizo wa kuwa na kanisa lenye ukamilifu kama baba yetu wa mbinguni unahitajika sana katika karne yetu. Sasa ni namna gani tunaweza kujikwamua kutoka katika tatizo hili? Kwanza hatuna budi kujipima kama tunakomaa kiroho, kimaadili na mwenendo.

 

Kipimo cha mtu aliyekomaa kiroho, kimaadili na kimwenendo.

 

1.       Ni jukumu la mtu mmoja mmoja kutamani kuwa mkamilifu kama alivyo baba wa Mbinguni – Neno la Mungu linatuonyesha kuwa tunaweza kuwa wakamilifu kama baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu kwa msingi huo ni vema sasa kila mmoja wetu akawana na shauku ya kuwa kama Kristo ambaye ni kiongozi mkuu wa wokovu wetu na ambaye ametuachia kielelezo tukifuate Mathao 5:6 “Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.”

2.       Ni jukumu la kila mmoja kutamani kuuweza mwili wake na hisia zake katika utakatifu 1Wathesalonike 4:3-4 “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;”

3.       Ni jukumu la kila mmoja kuwa na Upendo kwa Kristo mwenyewe alisema mkinipenda mtazishika mari zangu Yohana 14:15 “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”

4.       Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa najijengea upendo wa kupenda maswala ya kiroho yanayochangia ukuaji wa kiroho mfano kujisomea neno la Mungu, kuomba, kusikiliza mahubiri, kuhudhuria ibada, kufunga, kujitoa kwa Mungu na kutimiza agizo kuu

5.       Ni jukumu la kila mmoja kutamani kukaa katika uwepo wa Mungu na kuimarisha uhusiano wako na Yesu Kristo

6.       Kukubali kusamehe na kuachilia au kushindwa na kupoteza haki zetu kwa faida ya ufalme wa Mungu

7.       Kukubali kuwa na maisha ya mfano na kuhubiri kile ambacho sisi wenyewe tunakifanyia kazi 1Wakoritho 11:1 “Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo.”

8.       Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa anajaa Roho Mtakatifu na kuwa na maisha yaliyojaa muongozo wa Roho Mtakatifu Waefeso 5:18 -20 “Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho; mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu; na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo;”

9.       Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha nya kuwa anakubali maonyo makemeo na marekebisho kutoka kwa watu wanaoaminika kuwa wamekomaa kiroho na kama wameona kuwa kuna jambo sahihi la kukemea katika maisha na mafundisho yetu

10.   Ni jukumu la kila mmoja wetu kukubali kufundishika na kukiri makosa yetu pale tunapokuwa tumekosea

11.   Ni jukumu la kila mmoja wetu kutambua na kukubali ya kuwa hatujui kila kitu 1Wakorintho 8:2 “Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.”      

12.   Ni jukumu la kila mmoja wetu kujilinda na kiburi na majivuno pamoja na kuchukua utukufu wa Mungu

13.   Kukubali kujifunza kutoka kwa wengine na kutambua huduma na ubora wa wengine katika eneo Fulani la maisha yetu

14.   Kuamini kuwa neno la Mungu ndio mamlaka ya mwisho na ya kuwa hakuna mtu aliyejuu ya neno la Mungu

15.   Kukubali kuitambua na kuelewa na kupambanua ili kuitii na kuifuata sauti halisi ya Roho Mtakatifu na mapenzi ya Mungu

16.   Kuwa na uhusiano ulioshiba na Roho Mtakatifu

Siku hadi siku katika maisha yetu kama tutayatendea kazi maswala kadhaa tunayojifunza hapo juu uwezekano wa kuishi maisha ya ukamilifu na kuwa na tabia alizosema Kristo, uwezo wa kusamehe maadui na kuwaombea, uwezo wa kuvumilia, kuwasalimia hata wale wasiotupenda na kadhalika, hakuna jambo zuri na la kupendeza ni kuwa kama baba yetu wa Mbinguni alivyo.

Rev. Innocent Mkombozi Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima