Jumatano, 19 Julai 2023

Iliwapasa kunisikiliza mimi kwanza!


Matendo 27:20-25Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka. Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami,akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.”


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu huwa anawatumia watumishi wake kwa namna mbalimbali katika kutuonya na kutushauri kwa maswala mbalimbali katika maisha, Maandiko matakatifu yanasisitiza kuwa tumwamini Mungu wetu, lakini vilevile tuwaamini manabii wake ndipo tutakapothibitika na kufanikiwa, Lakini tatizo kubwa sana la watu wengi tulionao katika kizazi hiki ni kuwa wanaamini katiika akili zao na uweza wao wa kibinadamu jambo ambalo linawaletea madhara na kuwafanya wajifunze katika njia ngumu sana, lakini kumbe njia rahisi ilikuwa ni kumsikiliza Mungu na kuwasikiliza watumishi wake na wakati mwingine ushauri wanaotupa kama watumishi wake ona  

2Nyakati 20:20 “Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini Bwana, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa

Hakuna jambo baya na linaloweza kuleta madhara duniani kama kutokuyajua mapenzi ya Mungu na kutokutaka ushauri kutoka kwa Bwana kisha tukazitumainia akili zetu wenyewe na uzoefu wetu wenyewe katika maisha yangu Mungu wangu alinifundisha kwamba nimtegemee yeye hata katika kiwango cha kutafuta sindano ya kushonea nguo inapokuwa imepotea au imeanguka na siioni.

Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”

Kwa msingi huo kuna somo kubwa sana katika maisha yetu kuhusu kumsikiliza Mungu na kumuamini na kuwasikiliza watumishi wake katika kifungu cha msingi tulichokisoma hapo juu Paulo mtume aliwahi kutoa ushauri Fulani wakati wa safari yao iliyokuwa ngumu sana na yenye misuko suko mingi lakini hata hivyo ushauri wake ulipuuzwa na watu kutokana na kudhani ya kuwa wao wana ujuzi na utaalamu kuliko yule mtumishi wa Mungu aliyezungumza! Na matokeo yake walipata madhara makubwa sana kuliko madhara yaliyokuwa yamekusudiwa !

Kupuuzia ushauri wa mtumishi wa Mungu!

Paulo mtume alikuwa miongoni mwa wafungwa waliokuwa wanapelekwa Roma kwaajili ya kusimama mbele ya Kaisari kutokana na Kesi iliyosababishwa na kazi zake za injili, akiwa amehesabiwa kama wafungwa wengine tu Meli waliyokuwa wakiitumia kusafiria ilikutana na dhuruba kali sana hali ilikuwa ngumu na kulikuwa na hatari kubwa na madhara makubwa sana ambayo yangeweza kutokea wakati huu mtumishi wa Mungu ambaye kimsingi alikuwa mfungwa tu aliamua kuwapa maonyo na tahadhari kuhusu safari ile kwa Kamanda (Akida) wa kikosi cha safari ile lakini akida yule aliamua kumpuuzia Paulo na akawasikiliza manahodha  na wenye meli na wakapuuzia kile alichikisema Paulo mtume na mfungwa wa Yesu Kristo ona

Matendo 27: 6-13 “Na huko yule akida akakuta merikebu ya Iskanderia, tayari kusafiri kwenda Italia, akatupandisha humo. Tukasafiri polepole kwa muda wa siku nyingi, tukafika mpaka Nido kwa shida; na kwa sababu upepo ulikuwa ukituzuia tukapita chini ya Krete, tukaikabili Salmone. Tukaipita kwa shida, pwani kwa pwani, tukafika mahali paitwapo Bandari Nzuri. Karibu na hapo pana mji uitwao Lasea. Na wakati mwingi ulipokwisha kupita, na safari ikiwa ina hatari sasa, kwa sababu siku za kufunga zilikuwa zimekwisha kupita, Paulo akawaonya, akawaambia, Wanaume, naona kwamba safari hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na ya maisha yetu pia. Lakini yule akida akawasikiliza nahodha na mwenye merikebu zaidi ya yale aliyoyasema Paulo. Na kwa sababu bandari ile ilikuwa haifai kukaa wakati wa baridi, wengi wao wakatoa shauri la kutweka kutoka huko ili wapate kufika Foinike, kama ikiwezekana, na kukaa huko wakati wa baridi; nayo ni bandari ya Krete, inaelekea kaskazini-mashariki na kusini-mashariki.Na upepo wa kusi ulipoanza kuvuma kidogo, wakidhani ya kuwa wamepata waliyoazimu kupata, wakang'oa nanga, wakasafiri karibu na Krete pwani kwa pwani.

Unaona kuna kitu cha kujifunza hapo, Akida na manahodha na wenye chombo walipuuzia maneno ya Paulo Mtume walimuhesabu kuwa ni mfungwa tu na kuwa hana mawazo wala kitu cha kuchangia, yeye sio mjuzi wa bahari, yeye aliwaonya kuwa kila kitu kingekuwa salama mizigo, pamoja na shehena na abiria kama tu wangetweka nanga na kutokuendelea na safari, Lakini Nahodha alitumia ujuzi wake na utaalamu wake na uzoefu wake wa kuijua bandari na hali ya hewa na kuwa hapafai kupiga nanga wakati wa baridi, hivyo waliamua kuendelea na safari na kumpuuzia kusikiliza habari za mfungwa mmoja maarufu tu, hawakujua ya kuwa mfungwa huyo ni Mtume wa Yesu Kristo hawakujua ya kuwa alikuwa ni wakili wa Mungu, hawakujua ya kuwa alikuwa kinywa cha Mungu, hawakujua ya kuwa Yesu alikuwa anamtumia, hawakujua ya kuwa Roho wa Mungu alikuwa anasema naye, hawakujua ya kuwa malaika wa Bwana wako pamoja naye wao walidhani wako na mjinga mmoja tu mfungwa na mtuhumiwa na mtu asiyekuwa na ujuzi kuhusu bahari kumbe Paulo alikuwa ni mtume wa Mungu aliyeziumba mbingu na nchi na ardhi na bahari, wao walifikiri ya kuwa wana dira na ramani na ujuzi na uzoefu kumbe Mwenye dira ujuzi na uzoefu ni Mungu mwenyewe aliyeziumba mbingu na nchi na matokeo yake walipata hasara kubwa sana walipoteza kila kitu walichokuwa nacho na mizigo na shehena na hata meli yanyewe ni wao tu ambao Mungu aliyaponya maisha yao kwa sababu ya mtume wake aliyekuwa katika safari ile wote walikata tama na kufikia ngazi ya kufikiri kuwa watakufa ona        

Matendo 27:14-20 “Baada ya muda mchache ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani, uitwao Eurakilo, merikebu iliposhikwa, na kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa. Na tukipita upesi karibu na kisiwa kidogo kiitwacho Kauda tukadiriki kuikweza mashua; lakini kwa shida. Walipokwisha kuikweza wakatumia misaada, wakaikaza merikebu kwa kupitisha kamba chini yake, nao wakiogopa wasije wakakwama katika fungu liitwalo Sirti, wakatua matanga wakachukuliwa vivi hivi. Na kwa maana tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, siku ya pili yake wakaanza kuitupa shehena baharini. Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao wenyewe. Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka.”

 Unaweza kuona ni muhimu kufahamu kuwa Licha ya kuwa na ujuzi na ufahamu katika maswala ya aina mbalimbali, Mungu ni Mungu na Mungu ni mwenye hekima na maarifa makubwa zaidi, yeye anajua yajayo sisi hatujui yatakayokuwako kesho kwa msingi huo ni vema kumsikiliza Mungu na watumishi wake na ni kweli tunaweza kufanikiwa sana kama tutamuhusisha Mungu na watumishi wake halisi katika kila Nyanja ya maisha yetu, Mungu yuko juu ya yote, hakuna kinachojitawala hapa duniani kila kitu kiko chini ya uweza wake hivyo hata kama tumesomea sayansi na jambo lolote lile bado kamwe tusiache kumuhusisha Mungu katika kila swala la maisha yetu ili tusiwe na majuto, wako watu wanaojifunza kutokana na makosa na wako watu wanaojifunza haraka kwa kutii ni vema kumtii Mungu na kuyafanya mapenzi yake ili tusijifunze kupitia mazingira magumu na yenye majuto, tunaposhauriwa na watu wa Mungu tusiwachukulie kama kwamba wao ni watu wapuuzi tu tukumbuke ya kuwa wao ni mawakili wa serikali na mamlaka iliyo juu ya mamlaka zote baada ya majuto mengi hatimaye sasa kila mmoja alimsikiliza Mtume na mtumishi wa Mungu ambaye aliwakumbusha hata kula sasa.

Iliwapasa kunisikiliza mimi kwanza!

Baada ya meli kupita katika madhara makubwa sana na kundi lile kupoteza kila walichokuwa nacho, wenye mali walipoteza shehena zote, lakini hata meli yenyewe ilivunjikia mbali, akida wa askari aliyekuwa na wafungwa alifikiri kuwaua wafungwa wote hakuna mtu aliweza kupika wala kula kila mmoja sasa alikuwa anajuta na kufikiri kuhusu uhai wake Ndipo Paulo mtume sasa anawakumbusha kuwa iliwapasa kumsikiliza, Yeye hakuwa mfungwa wa kawaida yeye alikuwa ni Mtumishi wa Mungu aliye hai wakati wao wanataabika huenda yeye alikuwa akiomba na alikuwa akipata mawasiliano na Mungu kuwa nini kinapaswa kufanyika, kwa hiyo ilikuwa sahihi wasingelipata hasara na taabu zile kama tu wangesikiliza kwanza lakini  baada ya taabu na dhuruba sasa ndio wanajua ya kuwa  kweli wangemsikiliza na sasa wanamsikiliza mtumishi wake ona  

Matendo 27:20-25Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka. Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema, Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata madhara haya na hasara hii. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami,akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.”

Unaweza kuona, watu hawa ambao walikosa kula na kunywa kwa muda wa siku 14 kila mmoja akihofia uhai wake na usalama wake tu, hali yao ikiwa tete huku wakiwa wamepata hasara ya kila kitu ndipo sasa wanajirudi na kukaa kimya na kumsikiliza Mtumishi wa Mungu, walikuwa wamepoteza Muda wao, walikuwa wamepigika na kupata hasara, meli, shehena chakula na kila kitu lakini sasa wanasikiliza, ukweli ilikuwa wote wafe lakini ashukuriwe Mungu kulikuwa na mmoja aliyekuwa anaomba, aliomba kwaajili ya Mabaharia, aliwaombea wenye meli, aliwaombea manahodha, aliwaombea askari, aliwaombea wafungwa, aliwaombea na abiria wengine  na Mungu akamtuma malaika wake na kumhakikishia kuwa hataacha mtu afe isipokuwa watapoteza kila kitu, wakati wote hatuna budi kumshukuru Mungu na kuwatumia watumishi wake na waombaji na kukubali kuwa wao ni sehemu muhimu sana katika maisha yetu, ushauri wao na nafasi yao isitazamwe kama ni ya kiwango cha chini wakati mwingine maisha yetu yamefungwa katika mikono yao, ramani na dira ya kweli kuhusu maisha na mwelekeo ulionyoooka uko kwa Mungu na watumishi wake uongezewe neema unapolitendea kazi somo hili katika jina la Yesu Kristo amen

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!  



Kivuli cha Mambo yajayo (typology):


Wakolosai 2:16-17 “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.”

Waebrania 10:1 “Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.”

1Wakorintho 10:11 “Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.”

 



Utangulizi:

Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina kuhusu kivuli cha mambo yajayo, ambayo ni picha kivuli cha picha halisi tunazokutana nazo katika agano la kale zikimzungumzia Yesu Kristo kwa kina na mapana na marefu, likiwemo kwa mfano tukio la Abrahamu kutaka kumtoa kijana wake Isaka kama sadaka ya kuteketezwa baada ya kupewa maagizo hayo na Mungu na kisha Malaika wa Bwana kumzuilia Abraham, na badala yake alimuonyesha kondoo aliyetolewa kwa niaba ya Isaka tunaangalia kwa kina kuwa swala hili lina maana gani na linatufundisha nini ukiacha tu kuwa Mungu alikuwa anamjaribu Abrahamu, Lakini tunajifunza pia kumbe tukio hili kiunabii linamuhusu Yesu Kristo kuyafuatilia matukio hayo kwa undani  tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Ufahamu kuhusu alama za kinabii

·         Mifano kadhaa ya alama za kinabii

·         Ishara ya  Abraham kumtoa Isaka

Ufahamu kuhusu alama za kinabii.

Ni muhimu kwa kila mwanafunzi wa neno la Mungu kuwa na ufahamu kuwa katika agano la kale kulikuweko na matukio ambayo kimsingi yalikuwa pia ni alama za kinabii, ambazo licha ya kutokea katika maisha halisi ya wahusika lakini pia yalikuwa yanatabiri maswala kadhaa yajayo katika maisha ya wahusika halisi kinabii, Mwalimu mkuu wa alama za kinabii kimsingi alikuwa ni Yesu Kristo mwenyewe alama hizi kitaalamu zinaitwa TYPOLOGY ambalo limetokana na neno la asili la kiyunani TYPOLOGIA  neno hilo typology maana yake katika kiingereza ni – The study and interpretation of types and symbol or events, originally especially from within the Bible.  (TYPOLOGIA two Greek terminology Types and Logos which means Studies about symbols) Kwa Kiswahili tunaweza kusema ni somo linalohusu tafasiri ya alama, ishara na matukio ya kinabii, yenye asili ya kibiblia hususani agano la kale ambayo yanahusu mambo yajayo kinabii. Kwa mfano Israel walimuasi Mungu Jangwani na Mungu akaleta hukumu ya nyoka za moto yaani nyoka wenye sumu kali na walianza kuwauma watu ona katika

Hesabu 21:6-9 “Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung'unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu. Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.”

Unaona kimsingi hili ni tukio ambalo lilikuwa tukio halisi kwa wana wa Israel walifanya dhambi walingung’unika Musa na Mungu akatuma nyoka kama adhabu na watu wengi wakafa lakini walipomlilia Musa Mungu alimuagiza Musa kutengeneza nyoka wa shaba na kumtundika juu ya msalaba na kila aliyeumwa na nyoka alipomwangalia yule nyoka alipona, sasa ingawa tukio hili ni halisi lakini Yesu analitafasiri kama ni alama ya kinabii kumuhusu yeye ona :-

Yohana 3:14-15 “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.”

Kwa msingi huo tunapata ufunuo kutoka katika mtazamo wa Yesu kuwa kuna matukio katika maandiko hususani agano la kale ambayo yalizungumza kumuhusu yeye  au kuhusu mambo yajayo japo yalikuwa ni matukio ya kawaida kutoka katika agano la kale lakini yalikuwa yanazungumza jambo kuhusu masihi Yesu, mwenyewe na matukio mengine muhimu ya kinabii, mfano mwingine tunajifunza kutioka kwa Yesu tena kuhusiana na tukio la Nabii Yona (Yunus) kumezwa na nyangumi ona tukio halisi na ona namna Yesu alivyokuja kulitumia

Yona 1:17 “Bwana akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku.”

Tunaona hapa tukio halisi la Nabii Yona (Yunus) kumezwa na nyangumi na kuweko ndani ya samaki mkubwa kwa siku tatu usiku na mchana kwetu sisi ni tukio halisi na la kawaida lakini tukio hili ni alama za kinabii linazungumza kuhusu kufa na kufufuka kwa Yesu Msalabani siku ya tatu  na ni Yesu mwenyewe ndiye aliyezungumza swala hilo ona

Mathayo 12:39-41 “Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona.”     

Mpaka hapo tunajifunza kuwa ingawa manabii na watu maarufu katika agano la kale waliishi maisha yao ya kawaida na kukatukia matukio ya kawaida kama stori tu za maisha yao, lakini kumbe kwa vile walikuwa ni manabii, Roho Mtakatifu alikuwa akiwatumia kutabiri au kutupa matukio na ishara muhimu kuhusu matukio muhimu yajayo na mengi kati ya hayo yalikuwa yanamuhusu Yesu Kristo, kwa hiyo ukishaweka hili akilini utagundua kuwa tukio la Ibrahimu Kumtoa Isaka kama sadaka ya kutekeketezwa na kisha kukatokea Kondoo akatolewa kama mbadala wa Isaka vilevile uko ujumbe katika shule za kinabii ya kuwa swala zima licha ya kuwa tukio la kawaida pia lilikuwa ni tukio la kinabii linalo muhusu Yesu Kristo. Kama tutakavyoweza kuliona tukio hilo kwa kina katika kipengele cha tatu;

Mifano kadhaa ya alama za kinabii.

Kwa hiyo kama tulivyojifunza ya kwamba kuna alama vivuli ambazo zinafunua mambo muhimu yajayo ni muhimu kufahamu ya kuwa kuna Unabii, manabii na alama vivuli na hizi zote zilitumiwa na Mungu Roho Mtakatifu ambaye ndiye mwasisi na msimamizi wa uandishi wa Biblia kufunua maswala kadhaa muhimu ya kinabii na mengi yakiwa na uhusiano na ujio wa Masihi Yesu Kristo ambaye ndiye wa Muhimu kuliko mambo yote, kwa hiyo watu, alama na unabii unaweza kuletwa kwetu kutoka katika agano la kale kutupa picha hizo za kinabii kama ninavyotaka kuonyesha baadhi ya nhizo hapa ambazo zote kitaalamu tunaziita alama vivuli (Typology) na maandiko yameweka wazi alama hizo na maana zake, Hata hivyo ni muhimu kufahamu kuwa katika alama hizo vivuli zimegawanyika katika makundi makuu mawili yaani Kivuli chanya na kivuli hasi (Type and Antitype) :-

Mfano:-

1.       Sikukuu za mwandamo wa mwezi (Iddi)  - Katika tamaduni za kiyahudi kulikuwa na sikukuu za kusheherekea mwezi mpya ambazo ziliitwa Rosh Chodesh au Rosh Hodesh ambazo tafasiri yake kwa kiingereza ni new moon, yaani mwezi mpya ni sikukuu walizozitumia kusheherekea mwanzo wa mwezi mpya katika kalenda ya kiyahudi na zilisheherekewa kwa siku moja au mbili kutokana na kuandama kwa mwezi kama mwezi ulikuwa na siku 29 au 30  sikukuu hii inatajwa katika

 

Hesabu 28:11 “Tena katika mianzo ya miezi yenu mtamsongezea Bwana sadaka ya kuteketezwa; nayo ni ng'ombe waume wadogo wawili, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, saba;”

 

2Wafalme 4:22-23 “Kisha akamwita mumewe, akasema, Tafadhali, uniletee mtu mmoja wa watumishi, na punda mmoja, ili nimwendee yule mtu wa Mungu kwa haraka, nikarudi tena. Akasema, Kwa nini kumwendea leo? Sio mwandamo wa mwezi, wala sabato. Akasema, Si neno.”              

 

Kwa hiyo utaweza kuona kuwa sikukuu hizo za mwandamo wa mwezi zilikuwepo, lakini sikukuu hizi zilikuwa na maana ya kinabii kuhusu ujio wa masihi na ndio maana Yesu alipokuja alijitambulisha kuwa yeye ndiye NURU YA ULIMWENGU

 

Yohana 8:12 “Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”

 

Kimsingi hapo Yesu alikuwa anaonyesha wazi kuwa mwandamo wa mwezi (Iddi) ilikuwa ni alama kivuli cha ujio wa masihi, mwezi uliingia gizani na watu walifurahia kuiona nuru kwa msingi huo basi Mwezi na mwandamo wa mwezi ni kivuli cha jambo halisi na jambo hilo ni Yesu Kristo mwenyewe, jambo hilimlinawekwa wazi na vizuri Zaidi na Paulo mtume akiwataka wakristo wasishituke watu wanapoandama mwezi na sikukuu nyingine kwani zote zilikuwa ni unabii kumuhusu masihi ona

 

Wakolosai 2:16-17 “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.”

 

Unaona kwa msingi huo mwandamo wa mwezi kwa wakristo hauna maana tena kwa sababu Nuru halisi ni Yesu, na sabato haija maana tena kwa sababu pumziko halisi ni Kristo kwa hiyo kupitia alama vivuli unapata neema ya kuuelewa ukristo katika agano jipya kwa namna njema Zaidi, kwa namna hiyo sharia nyingi, sikukuu, na baadhi ya stori au matukio katika agano la kale zilikuwa ni kivuli cha kumuhusu masihi, zilikuja kwa kusudi la kuwandaa wana wa Israel kuna na ishara zitakazosaidia kumtambua mwana wa Mungu ajaye ulimwenguni ambaye ni Bwana wetu Yesu Kristo.

 

Waebrania 10:1 “Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.”

 

2.       Adamu – Adamu huyu ndiye baba wa wanadamu wote kwa hiyo alikuwa ni kiongozi mkubwa sana duniani, ni mwanadamu wa kwanza kuwa na uhusiano wa karibu sana na Mungu, lakini yeye alisababisha dhambi na mauti kuingia ulimwenguni, ni nabii mkubwa sana lakini Yesu tofauti na Adam yeye aliishinda dhambi na mauti na kufanikiwa kuwaongoza wanadamu wote kuishi maisha ya haki na kuurithi uzima wa milelekwa hiyo Adamu ni kivuli kisicho na ukamilifu cha ujio wa Yesu Kristo aliye mkamilifu, kwa hiyo katika maandiko mitume wanamfananisha Adamu na Kristo katika mfanano kinzani (Antitype). Adamu asiye mkamilifu na Adamu aliye mkamilifu, adamu aliyesababisha mauti na adamu aliyesababisha uzima, Adamu mwenye asili ya udongo na Adamu mwenye asili ya mbinguni, Adamu aliyeleta mauti na Adamu aliyeleta Ufufuo.

 

1Wakorintho 15:45-48 “Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha. Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho. Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni.”

 

1Wakorintho 15:21-22   Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.”

 

Warumi 5:14 - 17 “walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja. Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.    Wala kadiri ya yule mtu mmoja aliyefanya dhambi si kadiri ya kile kipawa; kwa maana hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja ikaleta adhabu; bali karama ya neema ilikuja kwa ajili ya makosa mengi, ikaleta kuhesabiwa haki. Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo.”

 

Kwa hiyo Adamu ni alama kivuli –hasi, (Antitype) cha Yesu Kristo sio katika ulinganifu wa mfanano bali katika ulinganifu unaokinzana kutufundisha ya kwamba kama tutaishi kwa kumfuata mtu wa mwilini tutakufa na kama tutaishi kwa kumfuata mtu wa rohoni tutaishi na kuwa na uzima wa milele kimsingi Yesu ni Bora Zaidi kuliko Adamu.

 

3.       Abel – Abel naye ni moja ya alama kivuli kizuri sana kumuhusu Yesu Kristo, yeye ni mwana wa Adamu na aliuawa na ndugu yake aitwaye Kaini, kimsingi Yesu Kristo alipokuwa akijitaja kama Mwana wa Adamu kinabii alikuwa akimaanisha yeye ni mwana mpendwa wa Adamu atakayeuawa na ndugu zake na kumwaga Damu isiyo na hatia, Habili aliuawa na ndugu yake kwa sababu tu ya wivu na husuda lakini hakuwa ametendo kosa lolote Zaidi ya kutenda jema na kupata kibali kwa Mungu  ona

 

Mwanzo 4:9-11 “BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;”

 

Tunaona mfanano mkubwa sana ulioko kati ya mwana wa Adamu Abeli na Mwana wa Adamu Yesu Kristo, tofauti ni kwamba Damu yake Abeli ilipomwagika ilikuwa inadai haki yaani kisasi, wakati Yesu Kristo ambeye ni bora Zaidi kuliko Kaini, yeye tunaelezwa ya kuwa damu yake ilipomwagika ilidai Msamaha, rehema na kuleta wokovu badala ya laana 

 

Waebrania 12:24 “na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.”               

 

Waefeso 1:6-7 “Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.”

 

Kwa hiyo unaweza kuona na kuthibitisha kimaandiko kuwa Mwana wa Adamu Abel ni alama kivuli cha unabii cha Mwana wa Adamu Yesu Kristo ambao wote waouawa na ndugu zao na kumwaga damu zao  na damu zao kunena maswala tofauti kwa jamii ya wanadamu.

 

4.       Safina ya Nabii Nuhu – Safina hiii nayo inatajwa katika maandiko kama ishara ya mwokozi Masihi Yesu Kristo, yaani kama safina ile ilivyotumiwa na kumuokoa Nuhu na familia yake wakati Mungu alipouhukumu ulimwengu kwa gharika, sasa Mungu anawaokoa watu wote wanaomuamini Yesu Kristo, nje ya Yesu Kristo watu wote watashuhudia hasira ya Mungu ya milele ona katika

 

1Petro 3:20-21 “watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji. Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo.”

 

Neno mfano wa mambo hayo ni ubatizo linamaanisha kuwa kilichotokea ni mfano kwa maana ya safina iliyowaokoa ni Yesu Kristo na maji yaliyotumika kuwahukumu watu ni ubatizo kwa mambo yajayo, na hapa Petro anazungumzia ubatizo unaohusiana na kusafishwa kwa dhamiri, kwa wote wanaomuamini Yesu Kristo na kazi aliyoifanya Msalabani, wote wanaomuamini wamebatizwa katika kazi aliyoifanya Kristo kwa kufa na kufufuka.

  

1Wakorintho 12:12-13 “Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.”

 

Warumi 6:3-5 “Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake;”

 

5.       Melchizedeki – Melkizedeki anajitokeza katika maandiko kama Mfalme wa salem (jina la zamani la jiji la Yerusalem) na alikuwa kuhani wa Mungu aliyekutana na Abraham katika Mwanzo 14 na Ibrahimu alimuheshimu na kumpa sehemu ya kumi (Zaka) ya mateka yake

 

Mwanzo 14:17-20 “Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.”

 

Moja ya kitu kinacholeta upekee wa mfalme huyu Malkizedeki ni kuwa alikuwa Mfalme na kuhani wa Mungu aliye juu sana, katika tamaduni za Israel majukumu hayo yalitenganishwa, Mfalme hakuwa kuhani na kuhani hakuwa mfalme, Wafalme wa Kiyahudi walitoka katika ukoo wa Daudi tu, na Makuhani walitoka katika ukoo wa Haruni pekee, aidha maana na jina Melkizedeki tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani; hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu. Na Roho mtakatifu anaruhusu kuhani huyu katika agano la kale atokee tu bila kuelezea historia yake kwa undani maandiko pia yana maneno ya unabii wa kuja kwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki

 

Zaburi 110:1-4 “Neno la Bwana kwa Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako. Bwana atainyosha toka Sayuni Fimbo ya nguvu zako. Uwe na enzi kati ya adui zako; Watu wako wanajitoa kwa hiari, Siku ya uwezo wako; Kwa uzuri wa utakatifu, Tokea tumbo la asubuhi, Unao umande wa ujana wako. Bwana ameapa, Wala hataghairi, Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki.”

 

Unabii huo unamuhusu Yesu Kristo ambaye ana cheo cha Ufalme na ukuhani kwa pamoja, na unabii huo tafasiri ya jina la Melkizedeki na kitendo cha Abrahamu kumpa zaka kunathibitisha ya kuwa kuhani huyu ni wa ngazi ya juu sana na hivyo kinabii Malkizedeki ni alama kivuli cha Yesu Kristo ambaye ni kuhani mkuu aliyebora Zaidi ya Melikizedeki ona

 

 Waebrania 7: 14-17 “Maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika Yuda, kabila ambayo Musa hakunena neno lo lote juu yake katika mambo ya ukuhani.Tena hayo tusemayo ni dhahiri sana zaidi, ikiwa ametokea kuhani mwingine mithili ya Melkizedeki; asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na ukomo; maana ameshuhudiwa kwamba, Wewe u kuhani milele Kwa mfano wa Melkizedeki.”

 

Roho Mtakatifu hajatupa tena historia ya Melkizedeki kuzaliwa kwake na mwisho wake ili asimame kama alama ya kivuli cha kinabii kumuhusu Yesu kristo ambaye ni kuhani mkuu milele na mfalme kwa mfano wa Melkizedeki

 

6.       Ngazi ya Yakobo – Ngazi ya Yakobo nayo inasimama kama alama kivuli cha kinabii kumuhusu Yesu Kristo nah ii ni kwa mujibu wa ufafanuzi wa Yesu Kristo mwenyewe, awali tunaona katika maandiko kwamba Yakobo alipokuwa akienda Haran njiani alipokuwa amepumzika aliona maono kuwa kuna ngazi kubwa ambayo imeegamizwa mbinguni na katika ardhi aliyokuwa amepumzika na malaika walikuwa wakipanda na kushuka ona katika

 

Mwanzo 28:10-15 “Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.”

 

Unaweza kuona katika tulio ili iko ngazi iliyokuwa imesimamishwa juu ya nchi na ncvha yake inafika mbinguni,  na malaika walikuwa wakipanda na kushuka kama Yesu asingelisema lolote kungekuwa na tafasiri nyingi sana kuhusu ngazi ya Yakobo lakini kumbe Yesu alikuwa Mwalimu mzuri sana wa alama vivuli yeye alisema maneno haya

 

Yohana 1:47-51 “Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona. Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli. Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya. Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”

 

Kitendo cha Yesu kunukuu kuhusu tukio lile na kuwahakikishia wanafunzi wake hususani Nathanael kuwa Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya mwana wa Adamu hii ilikuwa ni Dhahiri kuwa Yesu alikuwa akiweka wazi kuwa ngazi ile ilikuwa ni alama kivuli kuhusu ngazi halisi ambaye ni Kristo unaona! Nathaniel na wanafunzi wengine wamekuzwa wakiwa wanafahamu stori za agano la kale na labda walielewa kuhusu hii ngazi kwa hiyo kwa haraka wanapata ujumbe kuwa Yesu ndiye njia ya mbinguni

 

Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”


                                               


7.       Yusufu - hakuna mtu amewahi kumtaja Yusufu, kama alama kivuli cha Yesu Kristo lakini kutokana na uzoefu wetu wa kujifunza neno la Mungu sasa unaweza kuelewa alama kivuli zote ambazo ziko katika maandiko hata kama hakuna mtu amezitaja mahali kwengineko katika maaandiko, unapoyachunguza maisha ya Yusufu utaweza kuona kuwa kuna maswala kadhaa ambayo yanafanania, Yusufu alichukiwa na Ndugu zake, na aliuzwa kule Misri, na alipokuwa Misri alisingiziwa mambo ya uongo na kufungwa, baada ya kutafasiri ndoto ya farao kuhusu maswala yajayo ndipo Farao akampandisha kuwa msaidizi mkuu wa mfalme, ambapo baadaye alikuja kuwa mwokozi wa familia yake  unawezaje kujua kuwa Yusufu alikuwa pia ni alama kivuli cha Yesu Kristo?

 

o   Alikuwa ni wa Uzao wa Ibrahimu ambaye kupitia yeye mataifa mengine walibarikiwa Mwanzo 41:53-57 “Miaka ile saba ya shibe ikaisha katika nchi ya Misri, ikaanza kuja miaka ile saba ya njaa, kama vile Yusufu alivyosema. Kukawa na njaa katika nchi zote, bali katika nchi yote ya Misri palikuwa na chakula. Na nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walimlilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote, Enendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni. Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri. Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote.”            

 

Mwanzo 22:16-18 “ akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.”

 

Leo hii Yesu mwana wa Ibrahimu amekuwa Baraka kubwa kwa mataifa yote, Yusufu alikuwa mwana mpendwa wa Yakobo baba yake, Yesu naye ni mwana mpendwa wa pekee Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”          

Yusufu alifanyika masikini, kama Kristo naye 2Wakorintho 8:9 “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”.

 

Yusufu alichukiwa na ndugu zake kwa sababu ya ndoto zake ya kuwa atawatawala na kuwa watamsujudia

 

Mwanzo 37:4-8 “Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani.Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake.”

               

Ilitokea hivyo kwa Yesu, Wayahudi walimchukia ili asiwatawale Luka 19:14 “Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.”

 

Hatimaye ndugu wa Yusufu walikuja kumsujudia ingawa hapo awali walimkataa na kumdhuru, hali kama hiyo ilimtokea Yesu Kristo ambaye wayahudi walimtoa mikononi mwa wenye dhambi ili auawe lakini maandiko yanasema wazi kuwa hatimaye siku moja watamkubali na kumuabudu wakiamini kuwa ndiye masihi wao

 

Zekaria 12:10 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.”

 

Warumi 11:26-27 “Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.”

 

Yusufu na Yesu wote walisalitiwa na ndugu zao (Wayahudi) na wote waliuzwa kwa vipande vya fedha

 

Mwanzo 37:28 “Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.”

 

Mathayo 26:15 akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha.”

 

Yusufu aliinuliwa sana huko Misri na kila kitu kiliwekwa chini ya utawala wake isipokuwa Farao tu

 

Mwanzo 41:40 “Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”

 

Tunaelezwa katika maandiko pia ya kuwa Yesu Kristo kama yanenavyo maandiko ameinuliwa juu ya kila kitu na kila kitu kimewekwa chini ya utawala wake

 

 1Wakorintho 15:27 “Kwa kuwa, Alivitiisha vitu vyote chini ya miguu yake. Lakini atakaposema, Vyote vimetiishwa, ni dhahiri ya kuwa yeye aliyemtiishia vitu vyote hayumo.”

 

Yusufu alilia kwaajili ya ndugu zake Mwanzo 45:2 “Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia.” Yesu Kristo naye alilia kwaajili ya Wayahudi Luka 19:41 “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia,”   

 

Yusufu aliokoa maisha ya wote waliomjia kwa msaada ikiwemo watu wa mataifa mengi ya dunia waliokutwa na njaa,

 

Mwanzo 41:57 “Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote.”

 

Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

Kwa hiyo tunaweza kukubaliana kuwa Maisha ya Yusufu yaakisi kuwa ni alama kivuli cha maisha yanBwana Yesu kwetu hata kama hakuna nukuu ya aina hiyo katika maandiko, hizi alama vivuli zimekuwepo na kadhaa zimefunuliwa ili kutusaidia kutufunulia aina nyinginezo kwa sababu unabii wote ulimuhusu Yesu Kristo.

 

8.       Musa nabii – Musa naye ni alama kivuli cha Yesu Kristo, yeye ni mjumbe wa agano la kale  wakati Yesu Kristo ni mjumbe wa agano jipya  na neno la Mungu linaweka wazi kuwa Mungu angeinua nabii mwingine mfano wa Musa na Mungu aliamuru asikilizwe

 

Kumbukumbu 18:15-19 “Bwana, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye.Kama vile ulivyotaka kwa Bwana, Mungu wako, huko Horebu, siku ya kusanyiko, ukisema, Nisisikie tena sauti ya Bwana, Mungu wangu, wala nisiuone tena moto huu mkubwa, nisije nikafa. Bwana akaniambia, Wametenda vema kusema walivyosema. Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. Hata itakuwa, mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake.”

 

Kwa kuwa nabii huyu alitabiriwa ni wazi kuwa wayahudi walikuwa wakimtazamia kama masihi na kumgojea kwa hamu kubwa sana

 

Yohana 6:14 “Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni.”

 

Katika ulinganifu wa ubora wa Musa na Yesu Kristo mwandishi wa kitabu cha Waebrania anamfananisha Musa kama mtumishi mwaminifu katika nyumba ya Mungu na Yesu kama Mwana mwaminifu katika nyumba ya Mungu

 

§  Musa alikuwa kama mtumishi mwaminifu katika nyumba ya Mungu wakati Yesu Kristo ni  Mwana muaminifu katika nyumba ya Mungu. Waebrania 3:5-6 “Na Musa kweli alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu kama mtumishi, awe ushuhuda wa mambo yatakayonenwa baadaye; bali Kristo, kama mwana, juu ya nyumba ya Mungu; ambaye nyumba yake ni sisi, kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya taraja letu mpaka mwisho.”   
                  

§  Musa kulinganishwa na Kristo ni sawa na kulinganisha  nyumba na mjenzi wa Nyumba Yesu ndiye mjenzi wa nyumba na ni Mungu Waebrania 3: 3-4 “.Kwa maana huyo amehesabiwa kuwa amestahili utukufu zaidi kuliko Musa, kama vile yeye aitengenezaye nyumba alivyo na heshima zaidi ya hiyo nyumba. Maana kila nyumba imetengenezwa na mtu; ila yeye aliyevitengeneza vitu vyote ni Mungu.” 

§  Musa alikuwa ni kiongozi mkuu mwenye kuheshimika sana mwenendo wake na mapito ya maidha yake ni alama kivuli cha maisha halisia na unabii halisia kumuhusu Yesu Kristo:- 

§  Ukuu wa Nabii Musa. 

Ø  Alikuwa mtoto wa kifalme (Nyumbani kwa Farao Misri)

Mrithi mtarajiwa wa Farao

Aliishi kama mtu maalumu (Prince) miaka 40 ikulu

Ø  Alikuwa mchungaji wa kondoo jangwani

Alijinyenyekeza

Alipata mateso magumu ya jangwani, upweke na kuwa mbali na ndugu

Aliishi kama tu duni miakla 40 jangwani

Ø  Alikuwa kiongozi wa taifa la Israel

Aliishi kama Mtumishi wa Mungu miaka 40.

Alionyesha njia,Nguvu za Mungu

Aliandika neno la Mungu (Sheria) Mungu ana tumia mtu duni. 

§  Ukuu wa Yesu Kristo. 

Ø  Alikuwa mtoto wa kifalme Mbinguni

Mrithi wa Mungu

Alikuwako tangu milele na milele

Ø  Alijinyenyekeza Duniani

Aliteswa Msalabani,alikuwa mpweke mpaka msalabani

Aliishi  kama mtu duni

Ø  Amekuwa kichwa cha Kanisa

Ametunukiwa jina lipitalo majina yoote

Ametupa Neno la uzima wa milele (Injili)..

 

Kufanana Kwa Musa na Yesu Kristo Kihuduma na kimapito

 

1.       Woote walikuwa viongozi 

2.       Woote walikataliwa na watu wao Kutoka 2: 14 “Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana., Yohana 1:11 “Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea.” 

3.       Woote walijaribiwa jangwani Hesabu 20: 3-4 Watu wakashindana na Musa, wakanena, wakisema, Ingalikuwa heri kama tungalikufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za Bwana! Mbona mmewaleta kusanyiko la Bwana hata jangwa hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu?”   Luka 4:1-2Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa.”

4.       Woote waliitwa Manabii na walifananishwa kinabii Torati 18:18 “Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.” Luka 24:19 “Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote;”

         

Pamoja na kuwa Yesu ana maswala yanayofanana na Musa kihuduma ama kimapito Bado mwandishi wa kitabu cha waebrania anawaonyesha wakristo wa kiebrania kuwa Yesu ni Bora zaidi ya Musa ambaye ni nabii kivuli cha Kristo..

 

9.       Kondoo wa Pasaka  - Mwana kondoo wa Pasaka aliyekuwa anachinjwa na jamii ya wayahudi pia alikuwa ni alama kivuli cha Yesu Kristo, hususani siku ile Wayahudi walipokuwa wanatolewa Misri, Mungu aliwahukumu wamisri kwa kuua kila mzaliwa wa kwanza kama tu hakukuwa na Damu ya mwana kondoo katika miimo ya malango yao, na wale waliokuwa wameweka alama ya damu ya mwana kondoo Malaika wa kuharibu alipoiona alama ya damu hakuleta madhara katika nyumba hiyo Angalia

 

Kutoka  12:3-14 “Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu.  Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani. Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto. Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya BWANA.  Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA.  Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa BWANA; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya mileleMwana kondoo huyu alikuwa ni alama kivuli cha ujio wa Yesu kristo ona

 

Yohana 1:29 “Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!

 

Katika siku ile ya pasaka  wana wa Israel hawakutakiwa kula au kupika au kuingiza chochote chenye chachu, Na Paulo mtume anaeleza moja kwa moja kuwa Yesu ndiye Kondoo wa pasaka aliyechinjwa kwa niaba yetu na kuwa tunapaswa kuondoa chachu yote chahu hapa inasimama kwa niaba ya dhambi

 

1Wakorintho 5:7 “Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo;”             

 

10.   Mana (Mkate ushukao kutoka juu) -  Wote tunakumbuka jinsi ambavyo Mungu aliwalisha nwana wa Israel kwa mikate au keki maalumu kutoka mbinguni walipokuwa safarini jangwani, baada ya malalamiko kuwa hawana chakula, Mungu aliwapa chakula hicho cha ajabu ambacho walikihoji kuwa hiki ni nini MANHU kwa kiebrania au MANNA maana yake hiki nini mkate huu ulioshuka kutioka mbinguni ulikuwa ni alama kivuli kumuhusu Yesu kristo 

 

Kutoka 16:4 “Ndipo BWANA akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo.”

 

Yohana 6:31-35 “Baba zetu waliila mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale. Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. Basi wakamwambia, Bwana, sikuzote utupe chakula hiki. Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe.”

 

Kama wana wa Israel walivyoishangaa mana ndivyo walivyoshangaa kuhusu Yesu Kristo awezaje nabii kutoka Galilaya? Aidha mana ilikuwa inafundisha kuwa ni Mungu ndiye anayeweza kuwapa watu mahitaji yao na kutunza maisha yao na ni kupitia Mungu tunapata wokovu na uzima wa milele kama tutamwamini Bwana Yesu, mana ilikuwa ni alama kivuli tu Yesu ndiye mkate wa uzima.    

 

11.   Kuhani mkuu - Kuhani mkuu katika agano la kale naye alikuwa ni picha au alama kivuli kumuhusu Yesu Kristo, makuhani katika agano la kale ndio waliokuwa wakifanya kazi ya upatanishi kati ya Mungu na wanadamu, waliwaombea watu, walitoa sadaka za kuteketeza, na miongoni mwa makuhani mmoja alikuwa nachaguliwa kuwa kuhani mkuu kutoka ukoo wa Haruni, Maandiko ynatuambia kuwa Yesu ndiye kuhani wetu mkuu na ndiye mpatanishi kati ya Mungu na wanadam, ingawa tofauti na makuhani wengine yeye alikuwa mkamilifu na hakutenda dhambi,  na Zaidi ya yote anaishi milele

 

Waebrania 4:15-16 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

 

Waebrania 7:26-27 “Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake.”

 

12.   Pazia la Hekalu - Pazia la patakatifu pa patakatifu ambalo lilitenganisha patakatifu pa Hekalu na mwanzio katika hema ya kukutania pia ni alama kivuli kumuhusu Yesu Kristo, Pazia hili lilipatenga patakatifu na Patakatifu pa patakatifu, yaani eneo ambalo kulikuwa na uwepo wa Mungu au mahali ambapo palikuwa na uwepo wa Mungu, kuhani mkuu angaingia mara moja kwa mwaka kutoa dhabihu ya dhambi siku ya upatanisho, Lakini siku aliyokufa Yesu Kristo moja ya jambo la kushangaza ni kuwa Pazia lile la Hekalu lilipasuka, kuashiria kuwa kizuizi cha kuufikia uwepo wa Mungu kimeondolewa,

 

Mathayo 27:51-54 “Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”

 

Kwa mujibu wa mwandishi wa kitabu cha Waebrania Pazia lile la Hekalu ni Mwili wa Yesu Kristo ambao uliposulubiwa ulitoa nafasi ya watu kuufikia uwepo wa Mungu ambao ulizuiwa katika nyakati za agano la kale

 

Waebrania 10:19-20 “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake;”        

Unaona kwa hiyo Pazia ni Alama kivuli cha kinabii kuhusu Mwili wa Kristo.

 

13.   Kiti cha Rehema - Kiti cha rehema ambacho kilikuwa juu ya sanduku la agano kimsingi nacho ni alama kivuli kumhusu Yesu Kristo, Kiti cha Rehema ndicho ambacho kilikuwa kinatoa rehema na upatanisho kati ya Wanadamu na Mungu

 

Warumi 3:25 “ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake,ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa.”       

 

Katika kiti cha Rehema kuhani mkuu angenyunyiza Damu ya Mwanakondoo na Mungu angeiona damu hiyo na angetoa ruhusa na kumkubali kuhani mkuu kuomba kwaajili ya watu, Yesu ndiye kiti cha rehema klwa sababu Mungu anapoiona damu yake aliyoimwaga pale Msalabani anatupa neema ya kukaribia katika kiti chake cha enzi na katika uwepo wake!      

 

14.   Siku ya sabato. - Sabato nayo ni moja ya alama kivuli kumuhusu Yesu Kristo na kazi yake aifanyayo kwa wanadamu na katika mioyo ya wanadamu, Sabato inaadhimishwa kuanzia ijumaa jioni na kuisha siku ya jumamosi jioni, Sabato iliwataka wayahudi wote kupumzika na kuacha kufanya kazi zao na kumuabudu Mungu

 

Kutoka 20:8-11 “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.”                

 

Lakini kwa habari ya sabato Paulo Mtume anasema hivi Wakolosai 2:16-17 “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.”

 

Kulikuwa na walimu wa uongo katika kanisa la Kolosai ambao waliwataka waamini kuendelea kuishika sabato, Paulo anawajulisha kuwa Sabato ilikuwa ni kivuli tu cha Yesu Kristo ambaye yeye ni pumziko la kweli la wanadamu na kwa kuwa Kristo amekuja ambaye ni picha halisi, wakristo hawahitajiki tena kusihika sabato, Sabato inatukumbusha kuwa sisi sio Mungu na hivyo hatuwezi kufanya kazi siku zote na tunahitaji mapumziko, na hivyo hatupaswi kuwa watumwa wa sabato

 

Marko 2:27-28 “Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato. Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.             

 

Kwa hiyo ni ndani ya Yesu Kristo ndiko ambako wanadamu wanaweza kupata pumziko halisi Mathayo 11:28-30 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”

 

15.   Miji ya makimbilio.

 

Miji ya makimbilio katiika agano la kale ilikuwa pia ni alama kivuli cha Yesu Kristo, Kwa mujibu wa Torati ya Musa, Mungu alimuelekeza kuwa atenge miji sita ili kwamba kama mtu ameua mtu mwingine kwa makusudi au kwa kutokukusudia akimbilie kwenyo moja ya mji wa makimbilio kwa usalama wake ili asije akauawa na watu wanaotaka kujilipizia kisasi cha damu kwa sababu maelekezo ya Mungu ni kuwa mtu atakayemwaga danu ya mwanadamu naye atauawa 

 

Mwanzo 9:5-6 “Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu. Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu.”

 

Kwaajili ya kuwalinda watu hao kabla kesi zao hazijajulikana kuwa waliua kwa bahati mbaya au kwa kukusudia iliwekaa miji ya makimbilia ambako mtu angekaa humo angekuwa salama na sii ryhusa kumuua isipokuwa kama atakuwa ametoka nje ya mji huo wa makimbilio

 

Hesabu 35:6 “Na hiyo miji mtakayowapa Walawi, itakuwa miji sita ya makimbilio, mtakayoweka kwa ajili ya mwenye kumwua mtu, ili akimbilie huko; pamoja na hiyo mtawapa miji arobaini na miwili zaidi.”        

 

Hesabu 35:11-13 “Ndipo mtajiwekea miji iwe miji ya makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua mtu, pasipo kukusudia kumwua, apate kukimbilia huko. Na hiyo miji itakuwa kwenu kuwa makimbilio, kumkimbia mwenye kutwaa kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu, hata atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe. Na hiyo miji mtakayowapa itakuwa kwenu ni miji sita ya makimbilio.”

 

Mwandishi wa kitabu cha waebrania anakuja kuweka wazi kuwa miji  hiyo ya makimbilia ilikuwa inamwakilisha Yesu kristo, kwamba usalama wetu unategemea sisi kuwa ndani ya Yesu na sio vinginevyo, nje ya Kristo ni rahisi kupatwa na madhara na ni rahisi kuuawa  ona

 

Waebrania 6:18-20 “ili kwa vitu viwili visivyoweza kubadilika, ambavyo katika hivyo Mungu hawezi kusema uongo, tupate faraja iliyo imara, sisi tuliokimbilia kuyashika matumaini yale yawekwayo mbele yetu; tuliyo nayo kama nanga ya roho, yenye salama, yenye nguvu, yaingiayo hata mle mlimo ndani ya pazia, alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.”

 

Mwandishi wa kitabu cha weaebrania anaonya hatari ya  kukengeuka na kuwa mbali na neema ya Mungu, na kisha baadaye anajadili ujasiri tulio nao endapo tutamkimbilia Bwana Yesu  ambaye ni bora Zaidi ya mji wa makimbilio, wote tunafahamu kuwa mshahara wa dhambi ni mauti bali karama yaani zawadi atoayo Mungu kama tunamuamini Yesu ni uzima wa milele

Warumi 6:23 “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

16.   Ule Mwamba    1Wakorintho 10:1-4 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.”

 

Paulo mtume anapoelezea kuhusyu mwamba wa roho uliowapa kinywaji cha roho wana wa Israel kule jangwani katika habari hii ambayo ilijulikana vizuri sana na wayahudi, kwamba Musa aliwapa wana wa Israel maji kutoka katika mwamba kwa maelekezo ya Mungu baada ya kuugonga mwamba

 

Kutoka 17:1-7 “Mkutano wote wa wana wa Israeli ukasafiri, kutoka bara ya Sini kwa safari zao, kama BWANA alivyowaagiza, wakatua Refidimu; napo hapakuwa na maji, watu wanywe. Kwa hiyo hao watu wakateta na Musa, wakasema, Tupe maji tunywe. Musa akawaambia, Kwani kuteta na mimi? Mbona mnamjaribu BWANA? Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung'unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu? Musa akamlilia BWANA, akisema, Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe.BWANA akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende. Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa. Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli. Akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu BWANA, wakisema, Je! BWANA yu kati yetu au sivyo?

 

Hesabu 20:2-13 “Na hapo hapakuwa na maji kwa ule mkutano; wakajikusanya juu ya Musa na juu ya Haruni.Watu wakashindana na Musa, wakanena, wakisema, Ingalikuwa heri kama tungalikufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za Bwana! Mbona mmewaleta kusanyiko la Bwana hata jangwa hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu? Na mbona mmetupandisha kutoka Misri ili kutuleta hata mahali hapa pabaya? Si mahali pa mbegu, wala tini, wala mizabibu, wala makomamanga; wala hapana maji ya kunywa. Musa na Haruni wakatoka pale palipokuwa mkutano, wakaenda hata mlangoni pa hema ya kukutania, wakaanguka kifudifudi; utukufu wa Bwana ukawatokea. Bwana akasema na Musa, akinena, Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao. Musa akaitwaa hiyo fimbo kutoka mbele za Bwana kama alivyomwamuru. Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu? Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia. Bwana akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa. Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa Israeli waliteta na Bwana, naye alijionyesha kuwa mtakatifu kati yao.”

 

Unaona ingawa wana wa Israel walikunywa maji halisi kutoka katika mwamba ule kwa muujiza uliofanywa na Musa baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa Mungu, Paulo mtume anasema mwamba ule ni Yesu, Mwamba huu uliowafuta na kuwapa Maji ulipigwa ili kutioa maji yaliyowapa uzima wana wa Israel ilikuwa ni Picha ya kusulubiwa Kwa Yesu Kristo ambako kumeleta ukombozi wa mwanadamu, Kwa hiyo ni wazi kuwa wakati wana wa Israel wanapewa maji kutioka katika mwamba huo uliokuwa ukiwafuata mwamba ule ulikuwa ni Yesu Kristo ambao wao walikuwa wakimtazamia kinabii, mwamba ni picha ya maandalizi ya ujio wa masihi.          

 

17.   Daudi.    -  Daudi naye anasimama kama alama kivuli cha kinabiii kumuhusu Yesu Kristo,  Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Yesu alitabiriwa kuwa mwana wa Daudi na anaitwa hivyo ilitabiriwa kuwa ni Mwana wa Daudi atakayetawala katika kiti cha Enzi cha Daudi baba yake katika Israel na ulimwengu mzima kwa ujumla, hata hivyo wakati mwingine katika maandiko pia Bado Yesu anaitwa Daudi ona Ezekiel 37;24 “Na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mfalme juu yao, nao wote watakuwa na mchungaji mmoja; nao wataenenda katika hukumu zangu, na kuzishika amri zangu, na kuzitenda.”

Kwaajili ya unabii huu wanatheolojia wengine wanadhani ya kuwa labda Mungu atamfufua Daudi aje atawale wakati wa utawala wa miaka 1000 duniani milemium, ingawaje hapa Mungu anatumia jina Daudi akimaanisha Masihi Yesu Kristo ambaye ni Mwana wa Daudi

 

Yeremia 23:5-6  Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi.Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu.”

 

18.   Sulemani – Sulemani naye anasimama kwa niaba ya Yesu Kristo kama alama kivuli, mapema Mungu alikuwa amefanya agano na Daudi  kwamba hatakosa mtu wa kukaa katika kiti chake cha enzi milele

 

1Wafalme 8:24-25 “Umemtimizia mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli machoni pangu, kama watoto wako wakiangalia njia zao, ili kuenenda mbele zangu kama wewe ulivyoenenda.”

 

1Nyakati 17:11-14 “Hata itakuwa, siku zako zitakapotimia, uende na babazo, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayekuwa wa wana wako; nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakifanya imara kiti cha enzi cha ufalme wake milele. Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; wala sitamwondolea fadhili zangu, kama nilivyomwondolea yeye aliyekuwa kabla yako; ila nitamstarehesha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele; na kiti chake cha enzi kitathibitishwa milele.”

 

Kimsingi mwana wa Daudi aliyeketi kwenye kiti cha enzi cha Daudi ni Sulemani katika namna nyembamba au fikira finyu lakini katika namna pana Mwana wa Daudi aliyeketi kwenye kiti cha Enzi milele ni Yesu Kristo, na nyumba ambayo suleimani aliijenga ni hekalu la  na Hekalu halisi ni watu waliookolewa yaani kanisa ambalo Mwamba na msingi wake ni Yesu Kristo

 

1Wakorintho 3:16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

 

1Petro 2:5 “Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo.”  

 

Hili ni hekalu la kiroho ambalo wanatheolojia wanaamini kuwa Kristo amelijenga na ingawa wako wanaoamini kuwa pia atajenga Hekalu halisi wakati wa utawala wa miaka 1000 duniani kama alivyotabiri Ezekiel katika Ezekiel 40-43 na Ufunuo 20, Yesu ni bora Zaidi kuliko Suleimani.

 

19.   Maombi ya Musa -  Israel walipokuwa jangwani kulitokea vita kati yao na wana wa amelekikatika vita hii Joshua ndiye alikuwa jemadari mpiganaji kiongozi wa vita na Musa na Haruni ha Huri wao walipanda mlimani na kumuombea Yoshua Maandiko yanaonyesha kuwa wakati mikono ya Musa ikidhoofika wakati anaomba aliinua mikono yake miwili kuelekea Mbinguni, mikono ikichoka amaleki walikuwa wanapata ushindi, lakini mikono yake ilipokuwa imara Yoshua na Israel walipata ushindi, picha au alama kivuli cha mUsa kupanua mikono yake na kusaidia na haruni na Huri inatupa alama ya kinabii ya siku aliposulubiwa Kristo ambapo alisulibiwa pale Golgotha na wahalifu wawili mmoja mkono wake wa kuume na mwingine mkono wake wa kushoto, haimaanishi kuwa Huri na haruni walikuwa waovu kama wale wanyang’anyi waliosulubiwa pamoja na Kristo lakini katika alama vivuli tunapata picha ya kinabii ya tukio husika ona


Kutoka 17:8- 13 “Wakati huo Waamaleki wakatokea, wakapigana na Israeli huko Refidimu. Musa akamwambia Yoshua, Tuchagulie watu, ukatoke upigane na Waamaleki; kesho nitasimama juu ya kilelekile, na ile fimbo ya Mungu nitakuwa nayo mkononi mwangu. Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima. Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda. Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa. Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga.”

 

Luka 23:32- 43 “Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye. Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto.Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura. Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki,huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe.Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa. Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.”

 

Ushindi wetu unapatikana kwa kazi iliyofanyika pale Msalabani, kwa Yesu aliyewambwa mikono yake msalabani akituombea ushindi kama Musa alivyomuombea ushindi Yoshua.

 

20.   Maombi ya Samsoni.

Samsoni ni moja ya watu ambao wanamwakilisha Yesu Kristo kwa namna nyingi sana huyu alikuwa mwamuzi katika Israel anawakilisha mtu mwenye nguvu nyingi sana nguvu kutoka Mbinguni, Mwanadamu huyu mwenye nguvu za kupita kawaida za kiasi cha kutosha sio kuongoza jeshi tu bali yeye pake yake kuwa na uwezo mkubwa sana wa kukabiliana na adui, yeye naye ni alama kivuli cha Kristo japo hakuna mtu ametaja hili lakini mimi nataja

 

-          Kuzaliwa kwa Samsoni kulitangazwa na malaika  Waamuzi 13:3-5 3 “Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.”

 

-          Kuzaliwa kwa Yesu Kulitangwazwa na malaika  Luka 1:26-31 “Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu.Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.”

 

-          Wote walisalitiwa na ndugu zao Wayahudi wakawafunga na kuwatia mikononi mwa wenye dhambi – Waamuzi 15:9-13 “Basi Wafilisti wakapanda wakapiga kambi yao katika Yuda, wakajieneza katika Lehi. Watu wa Yuda wakasema, Mbona mmekuja kupigana nasi? Wakasema, Tumepanda ili kumfunga Samsoni, kumtenda yeye kama alivyotutenda sisi. Ndipo watu elfu tatu wa Yuda wakatelemka hata ule ufa wa jabali la Etamu, wakamwambia Samsoni, Je! Hujui ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hii, basi, uliyotutenda? Akawaambia, Kadiri ile walivyonitenda mimi, ndivyo nilivyowatenda wao. Wakamwambia, Tumeshuka ili kukufunga, tupate kukutia katika mikono ya Wafilisti. Samsoni akawaambia, Niapieni ya kwamba ninyi wenyewe hamtaniangukia. Wakamwambia, wakisema, Vema, lakini tutakufunga sana, na kukutia katika mikono yao; lakini hakika hatutakuua. Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya, wakamchukua kutoka huko jabalini.”

 

-          Yesu Krito naye alisalitiwa na wayahudi na kukamatwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi – Mathayo 20:17-19 “Hata Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi, na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.”

 

-          Wote hawakuheshimika sana walipokuwa hai, lakini waliheshimika siku ya maziko yao Waamuzi 16:31 “Ndipo ndugu zake, na watu wote wa nyumba ya baba yake wakatelemka, wakamtwaa wakamchukua, wakamzika kati ya Sora na Eshtaoli, katika kiwanja cha kuzikia cha Manoa baba yake. Naye alikuwa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini.” Unaona miaka yote ya uhai wa Samsoni hakuonekana kuwa wa maana sana hakna mtu alimjali lakini siku ya kuzikwa kwake alizikika kadhalika Yesu alipata Heshima kubwa wakati wa maziko watu wakubwa wastahiki ndio waliokuja kumzika ona

 

Mathayo 27:57-60 “Hata ilipokuwa jioni akafika mtu tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu; mtu huyu alimwendea Pilato akauomba mwili wa Yesu. Ndipo Pilato akaamuru apewe. Yusufu akautwaa mwili, akauzonga-zonga katika sanda ya kitani safi, akauweka katika kaburi lake jipya, alilokuwa amelichonga mwambani; akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.”

 

Kuna kufanana kwingi kwa namna ya picha ya kinabii kati ya Samsoni na Yesu lakini picha kubwa Zaidi ni kuwa wmisho wao wote walikuwa wakiwa wamekunjua mikono katika nguzo mbili, Samsoni akisukuma nguzo mbili muhimu zilizokuwa zimeshikilia jingo la hekalu la Mungu Dagoni wa wafilisti na kuwafutilia mbali, na Yesu alikufa akiwa katika nguzo mbili za mti, yaani msalaba na hapa ndio kila mmoja akawa amekufa kifo cha ushindi dhidi ya adui zake

 

Waamuzi 16:26-31 “Samsoni akamwambia yule kijana aliyemshika mkono, Niache nizipapase nguzo ambazo nyumba hii inazikalia, nipate kuzitegemea. Basi nyumba ile ilikuwa imejaa watu waume kwa wake; na wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na juu ya dari palikuwa na watu elfu tatu waume kwa wake waliokuwa wakitazama, wakati Samsoni alipocheza. Samsoni akamwita Bwana, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili. Kisha Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo nyumba ile ilikaa juu yake, akazitegemea, moja kwa mkono wake wa kuume na moja kwa mkono wake wa kushoto. Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake. Ndipo ndugu zake, na watu wote wa nyumba ya baba yake wakatelemka, wakamtwaa wakamchukua, wakamzika kati ya Sora na Eshtaoli, katika kiwanja cha kuzikia cha Manoa baba yake. Naye alikuwa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini.”       

 

Hivyo unaweza kukubaliana name kwamba Samsoni na maisha yake sehemu kadhaa wa kadhaa anamwakilisha Yesu kama kivuli cha Picha Halisi.

Ishara ya Abraham kumtoa Isaka.

Ishara ya Abraham kumtoa Isaka – Isaka naye anasimama kama kivuli cha kinabii cha Yesu Kristo kwa namna pana Zaidi, kuna maswala mengi sana yanayofanana kumuhusu Isaka kumwakilisha Bwana Yesu, Isaka alikuwani mwana wa ahadi ambayo Mungu aliitoa kwa Abraham. Isaka alizaliwa kwa muujiza, wakati Abrahamu alipokuwa na umri wa miaka 100 na Sara akiwa na miaka 90. Baada ya tukio la kuzaliwa kwake tunaona Mungu akimjaribu ili kwamba Abrahamu amtoe mwanae huyu wa kipekee kuwa sadaka ya kuteketezwa, na Abrahamu alipokuwa katika kulitekeleza hilo tunaona kwa njia ya muujiza Mungu akiingilia kati na kumuokoa Isaka kwa namna ya kipekee, Mungu alimpa Abraham mwana kondoo ambaye alikuwa ni mbadala, tunaelezwa sababu kubwa ya Abrahamu kutii kufanya hivyo ni kwa sababu alimuamini Mungu kuwa anaweza kumfufua mwanae Isaka kutoka kwa wafu,

 

Waebrania 11:17-19 “Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee; naam, yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano.”

 

Kuna maswala mengi ya kujifunza kutoka katika kisa hiki cha Abraham na Isaka, ambayo yanatupa picha za kinabii katika tukio zima la kwenda kutolewa sadaka kwa Isaka.

 

a.       Abrahamu kukubali kumtioa mwana wake wa Pekee kuwa dhabihu – ni alama kivuli cha unabii wa Mungu baba kumtoa mwana wake wa Pekee Yesu Kristo kufa Msalabani kwaajili wa watu wote watakaomwamini.

 

b.      Kitendo cha Isaka kukubali baba yake amtoe sadaka – ni alama ya kukubali kwa Bwana Yesu kuyatoa maisha yake kwaaji ya watu akimtii Mungu

 

c.       Kitendo cha Isaka kubeba kuni ili akatolewe dhabihu juu ya kuni hizo ni alama kivuli cha kinabii cha Yesu kuubeba Msalaba ambao atakwenda kusulubiwa juu yake.

 

d.      Kitendo cha Isaka kuokolewa kwa Ibrahimu kupewa kondoo ni alama kivuli cha kinabii ya kwamba Yesu Kristo ndiye mwana kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu ona

 

Yohana 1:28-29 “Hayo yalifanyika huko Bethania ng'ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza.Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!”

 

e.      Kitendo cha yule mwana kondoo kwamba pembe zake zilikuwa zimenasa kwenye kichaka ona

 

Mwanzo 22:13. “Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.”

 

Unaona AMENASWA PEMBE ZAKE KATIKA KICHAKA – kitendo cha mwana kondoo huyu kunaswa pembe zake katika kichaka ni alama kivuli cha Kristo aliyesulubiwa akiwa amevikwa taji ya miiba kichwani ona

 

Yohana 9:2 “Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau.”

 

f.        Katika ujumla wake tendo hili zima la Isaka kutaka kutolewa na Abraham kama Sadaka lilikuwa ni unabii wa kazi nzima ya ukombozi ambayo Mungu baba na mwana wake wa peke Yesu Kristo waliifanya kwaajili ya ukombozi wa mwanadamu, najua wako waislamu ambao wanaamini kuwa tukio hili lilikuwa ni kati ya Abraham na Ishimael vyovyote vile mtu anavyoweza kudai  lakini unabii huu ulikuwa una uhusiano na ukombozi wa mwanadamu uliofanywa na Bwana Yesu pale Msalabani, Mungu alimtaka mwana wa pekee wa ibrahimu ona

 

Mwanzo 22:1-2 “Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”

 

Ibrahimu tunaambiwa kuwa alikuwa na wana wengi, lakini Mungu alikuwa maalumu sana kiuchaguzi, alikusudia wazi kabisa kuwa mtoto huyu awe ni Isaka, jumla ya watoto wa Ibrahimu walikuwa ni naneo ngoja nikuonyeshe na wengine

 

Mwanzo 25:1-2 “Ibrahimu alioa mke mwingine jina lake akiitwa Ketura. Akamzalia Zimrani, na Yokshani, na Medani, na Midiani, na Ishbaki, na Sua.”    

Unaona watoto wa Ibrahimu ZIMRANI, YOKSHANI, MEDANI, MIDIANI, ISHBAKI NA SUA NA WENGINE NI ISHMAEL NA ISAKA, Upekee wa Isaka unakuja kwa sababu yeye alizaliwa kwa muujiza alizaliwa kwa ahahdi alizaliwa kwa mapenzi ya Mungu na sio kwa mapenzi ya kibinadamu, Ibrahimu alimpenda sana Isaka kuliko watoto wengine kwa sababu hawa wengine walikuwa ni wana wa Masuria na sio watoto wa ndoa halali ya Ibrahimu na Sara na maandiko yako wazi ona

 

Mwanzo 25:5-6. “Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu.”

 

Wana wa Masuria hawezi kuwa wana wa pekee, wala hawawezi kuwa wanawapendwa kwa hiyo Mungu aliposema Mwana wako wa pekee alikuwa anamamisha Isaka na sio wana wa Masuria

 

Na Kama ilivyo kwa Isaka Mungu ana watoto wengi lakini mwana wake wa Pekee anayependezwa naye ni Bwana wetu Yesu Kristo

 

Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

 

Alitabiriwa na maandiko mara baada ya uumbaji, alizaliwa kwa Ahadi, alizaliwa kwa muujiza, zlizaliwa na mwanamke bikira, alikuwa ndiye sadaka halisi iliyochaguliwa na Mungu kwaajili yetu ndiye mwanakondoo halisi wa Mungu ambaye kwa kupigwa kwake sisi tumepona, kwa hiyo Isaka ni alama kivuli iliyo bora Zaidi ikimzungumia Kristo ambaye ni mwana pekee wa Mungu.                  

Muda usingeliweza kutosha kuangalia alama vivuli vyote vilivyomo katika agano la kale ambavyo vinatupa picha kamili ya shughuli mbalimbali alizokuja kuzitimiza bwana wetu Yesu Kristo, lakini tunapopitia alama vivuli ambavyo vinatoa picha ya kinabii tunapata picha kubwa sana ya namna Roho Matakatifu alivyoikatibu Biblia hata ikatiokea ya kuwa matukio na matendo na maneno ya manabii yalitabiri sasawa kabisa na matukio yote yaliyitimizwa na Bwana wetu Yesu, kumbuka hata mitume hawakumaliza alama vivuli vyote lakini wewe unaweza ukaongezea kwa jicho lako la mwanafunzi wa Biblia kumuona kristo katika matukio mbalimbali lakini tunajifunza kuwa

1.       Mungu ni Mungu wa Matukio na Historian a kuwa kupitia matukio na Historia ametuelekeza kumjua Kristo kwaajili ya utukufu wake

2.       Inatukumbusha kuwa Kweli Biblia ni neno la Mungu na kuwa kweli Mungu alichagua Yesu Kristo kuwa mkombozi wetu

3.       Unabii wote katika maandiko unamuhusu Yesu Kristo.

 

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

+255 718 99 07 96