Matendo 27:20-25 “Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na
tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka. Na walipokuwa wamekaa
wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema,
Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata
madhara haya na hasara hii. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana
hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana
usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye
nimwabuduye, alisimama karibu nami,akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi
kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri
pamoja nawe. Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba
yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu
huwa anawatumia watumishi wake kwa namna mbalimbali katika kutuonya na
kutushauri kwa maswala mbalimbali katika maisha, Maandiko matakatifu
yanasisitiza kuwa tumwamini Mungu wetu, lakini vilevile tuwaamini manabii wake
ndipo tutakapothibitika na kufanikiwa, Lakini tatizo kubwa sana la watu wengi
tulionao katika kizazi hiki ni kuwa wanaamini katiika akili zao na uweza wao wa
kibinadamu jambo ambalo linawaletea madhara na kuwafanya wajifunze katika njia
ngumu sana, lakini kumbe njia rahisi ilikuwa ni kumsikiliza Mungu na
kuwasikiliza watumishi wake na wakati mwingine ushauri wanaotupa kama watumishi
wake ona
2Nyakati 20:20 “Wakaamka asubuhi na mapema,
wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati
akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini
Bwana, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo
mtakavyofanikiwa”
Hakuna jambo baya na linaloweza
kuleta madhara duniani kama kutokuyajua mapenzi ya Mungu na kutokutaka ushauri
kutoka kwa Bwana kisha tukazitumainia akili zetu wenyewe na uzoefu wetu wenyewe
katika maisha yangu Mungu wangu alinifundisha kwamba nimtegemee yeye hata
katika kiwango cha kutafuta sindano ya kushonea nguo inapokuwa imepotea au
imeanguka na siioni.
Mithali 3:5-6 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako
wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye,
Naye atayanyosha mapito yako.”
Kwa msingi huo kuna somo kubwa
sana katika maisha yetu kuhusu kumsikiliza Mungu na kumuamini na kuwasikiliza
watumishi wake katika kifungu cha msingi tulichokisoma hapo juu Paulo mtume
aliwahi kutoa ushauri Fulani wakati wa safari yao iliyokuwa ngumu sana na yenye
misuko suko mingi lakini hata hivyo ushauri wake ulipuuzwa na watu kutokana na
kudhani ya kuwa wao wana ujuzi na utaalamu kuliko yule mtumishi wa Mungu
aliyezungumza! Na matokeo yake walipata madhara makubwa sana kuliko madhara
yaliyokuwa yamekusudiwa !
Kupuuzia ushauri wa mtumishi wa Mungu!
Paulo mtume alikuwa miongoni mwa
wafungwa waliokuwa wanapelekwa Roma kwaajili ya kusimama mbele ya Kaisari
kutokana na Kesi iliyosababishwa na kazi zake za injili, akiwa amehesabiwa kama
wafungwa wengine tu Meli waliyokuwa wakiitumia kusafiria ilikutana na dhuruba
kali sana hali ilikuwa ngumu na kulikuwa na hatari kubwa na madhara makubwa
sana ambayo yangeweza kutokea wakati huu mtumishi wa Mungu ambaye kimsingi
alikuwa mfungwa tu aliamua kuwapa maonyo na tahadhari kuhusu safari ile kwa
Kamanda (Akida) wa kikosi cha safari ile lakini akida yule aliamua kumpuuzia
Paulo na akawasikiliza manahodha na
wenye meli na wakapuuzia kile alichikisema Paulo mtume na mfungwa wa Yesu
Kristo ona
Matendo 27: 6-13 “Na huko yule akida
akakuta merikebu ya Iskanderia, tayari kusafiri kwenda Italia, akatupandisha
humo. Tukasafiri polepole kwa muda wa siku nyingi, tukafika mpaka Nido kwa
shida; na kwa sababu upepo ulikuwa ukituzuia tukapita chini ya Krete, tukaikabili
Salmone. Tukaipita kwa shida, pwani kwa pwani, tukafika mahali paitwapo Bandari
Nzuri. Karibu na hapo pana mji uitwao Lasea. Na wakati mwingi ulipokwisha
kupita, na safari ikiwa ina hatari sasa, kwa sababu siku za kufunga zilikuwa
zimekwisha kupita, Paulo akawaonya, akawaambia, Wanaume, naona kwamba safari
hii itakuwa na madhara na hasara nyingi, si ya shehena na merikebu tu, ila na
ya maisha yetu pia. Lakini yule akida akawasikiliza nahodha na mwenye merikebu
zaidi ya yale aliyoyasema Paulo. Na kwa sababu bandari ile ilikuwa haifai kukaa
wakati wa baridi, wengi wao wakatoa shauri la kutweka kutoka huko ili wapate
kufika Foinike, kama ikiwezekana, na kukaa huko wakati wa baridi; nayo ni
bandari ya Krete, inaelekea kaskazini-mashariki na kusini-mashariki.Na upepo wa
kusi ulipoanza kuvuma kidogo, wakidhani ya kuwa wamepata waliyoazimu kupata,
wakang'oa nanga, wakasafiri karibu na Krete pwani kwa pwani. ”
Unaona kuna kitu cha kujifunza
hapo, Akida na manahodha na wenye chombo walipuuzia maneno ya Paulo Mtume
walimuhesabu kuwa ni mfungwa tu na kuwa hana mawazo wala kitu cha kuchangia,
yeye sio mjuzi wa bahari, yeye aliwaonya kuwa kila kitu kingekuwa salama
mizigo, pamoja na shehena na abiria kama tu wangetweka nanga na kutokuendelea
na safari, Lakini Nahodha alitumia ujuzi wake na utaalamu wake na uzoefu wake
wa kuijua bandari na hali ya hewa na kuwa hapafai kupiga nanga wakati wa
baridi, hivyo waliamua kuendelea na safari na kumpuuzia kusikiliza habari za
mfungwa mmoja maarufu tu, hawakujua ya kuwa mfungwa huyo ni Mtume wa Yesu
Kristo hawakujua ya kuwa alikuwa ni wakili wa Mungu, hawakujua ya kuwa alikuwa
kinywa cha Mungu, hawakujua ya kuwa Yesu alikuwa anamtumia, hawakujua ya kuwa
Roho wa Mungu alikuwa anasema naye, hawakujua ya kuwa malaika wa Bwana wako pamoja
naye wao walidhani wako na mjinga mmoja tu mfungwa na mtuhumiwa na mtu
asiyekuwa na ujuzi kuhusu bahari kumbe Paulo alikuwa ni mtume wa Mungu
aliyeziumba mbingu na nchi na ardhi na bahari, wao walifikiri ya kuwa wana dira
na ramani na ujuzi na uzoefu kumbe Mwenye dira ujuzi na uzoefu ni Mungu
mwenyewe aliyeziumba mbingu na nchi na matokeo yake walipata hasara kubwa sana
walipoteza kila kitu walichokuwa nacho na mizigo na shehena na hata meli
yanyewe ni wao tu ambao Mungu aliyaponya maisha yao kwa sababu ya mtume wake
aliyekuwa katika safari ile wote walikata tama na kufikia ngazi ya kufikiri
kuwa watakufa ona
Matendo 27:14-20 “Baada ya muda mchache
ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani, uitwao Eurakilo, merikebu
iliposhikwa, na kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa. Na
tukipita upesi karibu na kisiwa kidogo kiitwacho Kauda tukadiriki kuikweza
mashua; lakini kwa shida. Walipokwisha kuikweza wakatumia misaada, wakaikaza
merikebu kwa kupitisha kamba chini yake, nao wakiogopa wasije wakakwama katika
fungu liitwalo Sirti, wakatua matanga wakachukuliwa vivi hivi. Na kwa maana
tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, siku ya pili yake wakaanza kuitupa
shehena baharini. Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao
wenyewe. Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu
ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka.”
Unaweza kuona ni muhimu
kufahamu kuwa Licha ya kuwa na ujuzi na ufahamu katika maswala ya aina
mbalimbali, Mungu ni Mungu na Mungu ni mwenye hekima na maarifa makubwa zaidi,
yeye anajua yajayo sisi hatujui yatakayokuwako kesho kwa msingi huo ni vema
kumsikiliza Mungu na watumishi wake na ni kweli tunaweza kufanikiwa sana kama
tutamuhusisha Mungu na watumishi wake halisi katika kila Nyanja ya maisha yetu,
Mungu yuko juu ya yote, hakuna kinachojitawala hapa duniani kila kitu kiko
chini ya uweza wake hivyo hata kama tumesomea sayansi na jambo lolote lile bado
kamwe tusiache kumuhusisha Mungu katika kila swala la maisha yetu ili tusiwe na
majuto, wako watu wanaojifunza kutokana na makosa na wako watu wanaojifunza
haraka kwa kutii ni vema kumtii Mungu na kuyafanya mapenzi yake ili tusijifunze
kupitia mazingira magumu na yenye majuto, tunaposhauriwa na watu wa Mungu
tusiwachukulie kama kwamba wao ni watu wapuuzi tu tukumbuke ya kuwa wao ni
mawakili wa serikali na mamlaka iliyo juu ya mamlaka zote baada ya majuto mengi
hatimaye sasa kila mmoja alimsikiliza Mtume na mtumishi wa Mungu ambaye
aliwakumbusha hata kula sasa.
Iliwapasa
kunisikiliza mimi kwanza!
Baada ya meli kupita katika
madhara makubwa sana na kundi lile kupoteza kila walichokuwa nacho, wenye mali
walipoteza shehena zote, lakini hata meli yenyewe ilivunjikia mbali, akida wa
askari aliyekuwa na wafungwa alifikiri kuwaua wafungwa wote hakuna mtu aliweza
kupika wala kula kila mmoja sasa alikuwa anajuta na kufikiri kuhusu uhai wake
Ndipo Paulo mtume sasa anawakumbusha kuwa iliwapasa kumsikiliza, Yeye hakuwa
mfungwa wa kawaida yeye alikuwa ni Mtumishi wa Mungu aliye hai wakati wao
wanataabika huenda yeye alikuwa akiomba na alikuwa akipata mawasiliano na Mungu
kuwa nini kinapaswa kufanyika, kwa hiyo ilikuwa sahihi wasingelipata hasara na
taabu zile kama tu wangesikiliza kwanza lakini baada ya taabu na dhuruba sasa ndio wanajua ya
kuwa kweli wangemsikiliza na sasa
wanamsikiliza mtumishi wake ona
Matendo 27:20-25 “Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na
tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka. Na walipokuwa wamekaa
wakati mwingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao, akasema,
Wanaume, iliwapasa kunisikiliza mimi na kutokung'oa nanga huko Krete, na kupata
madhara haya na hasara hii. Sasa nawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwa maana
hapana hata nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea, ila merikebu tu. Kwa maana
usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye
nimwabuduye, alisimama karibu nami,akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi
kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri
pamoja nawe. Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba
yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.”
Unaweza kuona, watu hawa ambao
walikosa kula na kunywa kwa muda wa siku 14 kila mmoja akihofia uhai wake na
usalama wake tu, hali yao ikiwa tete huku wakiwa wamepata hasara ya kila kitu
ndipo sasa wanajirudi na kukaa kimya na kumsikiliza Mtumishi wa Mungu, walikuwa
wamepoteza Muda wao, walikuwa wamepigika na kupata hasara, meli, shehena
chakula na kila kitu lakini sasa wanasikiliza, ukweli ilikuwa wote wafe lakini
ashukuriwe Mungu kulikuwa na mmoja aliyekuwa anaomba, aliomba kwaajili ya
Mabaharia, aliwaombea wenye meli, aliwaombea manahodha, aliwaombea askari,
aliwaombea wafungwa, aliwaombea na abiria wengine na Mungu akamtuma malaika wake na
kumhakikishia kuwa hataacha mtu afe isipokuwa watapoteza kila kitu, wakati wote
hatuna budi kumshukuru Mungu na kuwatumia watumishi wake na waombaji na
kukubali kuwa wao ni sehemu muhimu sana katika maisha yetu, ushauri wao na
nafasi yao isitazamwe kama ni ya kiwango cha chini wakati mwingine maisha yetu
yamefungwa katika mikono yao, ramani na dira ya kweli kuhusu maisha na mwelekeo
ulionyoooka uko kwa Mungu na watumishi wake uongezewe neema unapolitendea kazi
somo hili katika jina la Yesu Kristo amen
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni