Alhamisi, 26 Mei 2016

Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele!.


Luka 19: 37-40 Biblia inasema Hivi:-  37. Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, 38. wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu.  39. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. 40. Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele.”


 Yesu Masihi akiingia Yerusalem Kwa shangwe!

Ndugu zangu wapendwa, wengi tunapolisoma andiko hilo kwa harakaharaka tunaweza kulikumbuka jinsi linavyotumika katika Jumapili ijulikanayo kama Jumapili ya mitende, tunapokumbuka na kuadhimisha kuingia kwa Yesu katika Jiji la Yerusalem kwa shangwe!, Jinsi watu walivyo muabudu na kumuheshimu Yesu na kuchukua matawi ya mitende na kutandaza nguo zao njiani wakimsifu Yesu Kristo kwa kusema “Hosanna” yaani tafadhali tuokoe na kumtukuza Mungu kuwa amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana!

Ni muhimu kufahamu kuwa kwanza kabisa Yesu alikuwa akiutimiza unabii wa Nabii Zekaria unaosema “Furahi sana Ee binti Sayuni: Piga kelele, ee Binti Yerusalem; Tazama mfalme wako anakuja kwako, Ni mwenye haki naye ana wokovu, Ni mnyenyekevu amepanda punda naam mwana punda, Mtoto wa pundaZekaria 9:9

Inaeleweka wazi kuwa safari hii ilikuwasafari ya mwisho ya masihi na punde alikuwa anaukabili msalaba na mateso makali, ili kwamba awakomboe wanadamu na sasa Yesu anashangiliwa na kutukuzwa sawa na unabii wa Zakaria, na Hapa wanaibuka watu wenye wivu, watu waliojikinai kuwa na haki wenye mawazo potofu wenye taratibu za kidini eti wanahesabu kinachofanyika ni kama upuuzi na wanaona ni kelele na wanamuamuru Yesu kunyamazisha watu wake Yesu anaitikia kwa kuwajibu Mafarisayo kwamba “Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele!” Luka 19:40 Yesu alikuwa akimaanisha nini hapa ndipo palipo na kitu cha kujifunza leo.!

Mawe ni Akina nani?
Kuna tafasiri kuu tatu kuhusu Mawe haya,
I. Israel ni Nchi ya mawe na ni wazi kuwa mahali alipokuwa anazungumza Yesu palikuwa na mawe, kwa sababu hiyo wengine hufikiri kuwa Yesu alikuwa akizungumza juu yam awe halisi kabisa kuwa yanaweza kumsifu Mungu endapo wanadamu wa kawaida watakataa kumsifu kwa vile ni lazima Yesu asifiwe! Ibada ya Kweli ya Kikristo inahusu Kumsifu Bwana Yesu ni lazima asifiwe tu hata na viumbe visivyo na uhahi.

II. Pili wako wanaofikiri kuwa Yesu alikuwa anazungumzia anguko la Yerusalem ambalo lingetokea Baadaye, kwamba kwa vile mji wa Yerusalem unakwenda kumkataa Masihi na ndio unakataa kumsifu kwa sababu hiyo Mungu anakwenda kuuhukumu na hakuta salia jiwe juu ya jiwe ama mawe ndiyo yatakayosikika yakitoa sauti kwa niaba ya watu waliomkataa Masihi

Hata hivyo hakuna ushahidi wa kibiblia kuhusu tafasiri hizo hapo juu mbili, wala  wa kihistoria kuwa mawe halisi yalifanya hivyo hata katika mwaka wa 70 Warumi walipoharibu kila kitu Israel
Lakini Biblia inazungumzia wazi kuhusu watu wanaokataa Kumuheshimu Yesu Kristo na kumtukuza wakiwa wazi kabisa wakiwakataza watu wengine waliokuwa wakimfuata Yesu wasimtukuze na kumsifu, Hivyo kuna ushahidi kuwa Yesu alikuwa anazungumzia watu

Kimsingi hawa viongozi wa dini ndio waliokuwa na kila sababu ya kumsifu na kumuheshimu na kumtukuza Yesu Masihi na kutambua umuhimu wake, kundi lingine la jamii ndio waliokuwa wakifanya hayo kwa mapenzi yao na kwa kutambua umuhimu wa Bwana na kazi anayokwenda kuifanya, hawa walikuwa wamemkubali kabisa Yesu kuwa ni Masihi, kitendo cha kuwanyamazisha watu ambao walikuwa tayari wamemkubali mwokozi kingeweza kumfanya Mungu kuinua Mawe yakamsifu na kumuheshimu na kumtukuza Mungu, kimsingi mawe ni watu wa namna gani

Mawe ni watu waliokuwa wakihesabika kuwa sio kitu, hawana maana ni jamii ya watu waliokataliwa na kufikiriwa kuwa sio wa kidini, waliwekwa katika makundi ya watu waliodharaulika, watu wasiofaa, hii ilijumuisha watu wote wasio wayahudi, watu walio nje na mapenzi ya Mungu, pia iliweza kuhusisha jamii ya watu kama watoza ushuru, wenye dhambi, na makahaba ambao miongoni mwao ndio walikuwa wakimfuata Yesu, makundi hayo ni makundi ambayo mafarisayo waliwadharau na kuwapuuza, Yesu alikuwa akiweka wazi kuwa kama jamii ya watu wanaojulikana kama wa Mungu wamekataa kumtukuza Mungu basi Mungu hashindwi watu waliokuwa wakifikiriwa kuwa si kitu kumtukuza Mungu

Lugha aliyoitumia Yesu mahali hapa ina ushahidi wa Kibiblia na ilitumiwa na Yohana mbatizaji alipokuwa akiwaonya mafarisayo Mathayo 3:9 Biblia inasema hivi :- “9. wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto.”

Ni wazi kabisa hili ndilo jambo ambalo Bwana amelifanya mimi nawe sio wayahudi lakini tuliokolewa tulisafishwa kwa Damu ya Yesu tulifanywa kuwa wana wa Mungu na sasa tunamsifu na kumuheshimu na kumuabudu Mungu, Mungu haogopi wala hashindwi kuachana na watu wanaoifanya mioyo yao kuwa migumu yeye sio Dikteta hawezi kulazimisha lakini yeye hubaki wa kuabudiwa Milele Ezekiel 36:26 “26. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama.” 

Lazima ufikie wakati watu wa Mungu waache kiburi na majivuno na kujifikiri kuwa wao ni watu maalumu zaidi, hakuna mtu mwenye hati miliki ya Mungu, Mungu ni wa kila mtu, Mungu yu aweza kumchagua awaye yote, Yako hata makanisa mengine ambayo hujivunia wakijifikiri kuwa wao ni maalumu na ndio wenye kweli peke yao, wengine hujifikiri kuwa ni kanisa kubwa na la kwanza Duniani, wengine hujifikiri kuwa ndio wana mapinduzi namba moja, wengine hujifikiri kuwa ndio namba moja duniani wakiwa na usahii, kuna viburi vya kimakanisa na kuna kiburi cha mtu mmoja mmoja kila mmoja akijifikiri kuwa ni Bora zaidi yaw engine Yesu alikuwa akiwaonya mafarisayo wasijifikiri kuwa  wao pekee ndio wenye haki ya kumsifu Mungu na kusikilizwa naye , wako watu wengine hujiona bora kutokana na mpangilio wa ibada zao kuwa za kimyakimya na kuwadharau wale wanaopiga kelele, kumbuka walimwambia nyamazisha watu wako labda wanafunzi wa Yesu walionekana ni wapiga Kelele tuLakini nabii Zekaria anasemaje Zekaria 9:9 “Furahi sana Eebinti Sayuni: Piga kelele, ee Binti Yerusalem; Tazama mfalme wako anakuja kwako, Ni mwenye haki naye ana wokovu, Ni mnyenyekevu amepanda punda naam mwana punda, Mtoto wa punda

Mungu ametuokoa na kutuita ili tumhudumie yeye japo tulihesabika kuwa sio kitu 1Petro 2:5, 10 Biblia inasema hivi,:- “Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.”

Biblia inawaita wakristo mawe yaliyo hai, sisi ndio mawe yale aliyoyasema Yesu, Yesu alitufia alituokoa kwa mateso yake makuu sasa tumepata rehema tumekuwa mawe yaliyo hai

Wajibu wa Mawe yaliyo hai:-

Ni muhimu kufahamu kuwa sasa tumepata rehema hatupaswi kuwa kama mafarisayo, Yesu atawapa injili yake watu wengine ni lazima tuhakikishe kuwa Yesu anatukuzwa kwa namna yoyote ile,Petro anaeleza wazi wajibu mkubwa tulio nao ili tusiweze kukataliwa 1Petro 2:9 “ Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;”

Mungu ametuita, ametuteua tupate kuzitangaza Fadhili zake, Kama wenzetu waliokuwa wakimtii Yesu na kusifu Hossana yaani Okoa lazima tuendelee kumuomba Mungu awaokoewatu wote Duniani, lazima tuhakikishe kuwa Mbinguni kunakuwa na amani na furaha kwa vile mapezi ya Mungu yanatimizwa Duniani, kuabudu na kusifu ni moja ya jukumu kubwa sana tulilonalo watu tuliookolewa ni muhimu kwetu, kuhakikisha kuwa tunalifanyia kazi hilo, kwa kuwa Yesu ni mfalme wa wafalme lazima tuhakikishe kuwa ufalme wake unatawala Duniani, Mataifa makubwa Duniani yaliyokuwa yanatarajiwa kuitetea injili leo kuna uozo mkubwa sana na mmommonyoko Mkubwa wa uadilifu Mungu sasa anaiangalia afrika kama mawakili wake, kama watu tuliozaraulika Duniani lakini tunaweza kulibeba kusudi hilo la Mungu na kulisambaza kote ulimwenguni, aidha kwa maisha yetu na mwenendo wetu tunapaswa kuutumia katika kumtukuza Mungu.

Mungu hashindwi hata kuyainua mataifa ya Kiarabu yakahubiri injili yake, Mungu hashindwi kuiinua hata China ikahubiri injili, Mungu ni wa watu wote,Tukijisahau hatashindwa kuwatumia wengine na kuwabariki wengine kwaajili ya utukufu wake yeye ni lazima atukuzwe tu wanaostahili kumtukuza wakishindwa atatukuzwa na wengineo ambao pia aliwaumba yeye.

Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele!

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni: