Yohana 11:32-44: 12:1-2
“32.Basi Mariamu alipofika pale alipokuwapo
Yesu, na kumwona, alianguka miguuni pake, akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo
hapa, ndugu yangu hangalikufa. 33. Basi Yesu alipomwona analia, na wale
Wayahudi waliofuatana naye wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake, 34.
akasema, Mmemweka wapi? Wakamwambia, Bwana, njoo utazame. 35. Yesu akalia machozi. 36. Basi
Wayahudi wakasema, Angalieni jinsi alivyompenda. 37. Bali wengine wao wakasema,
Je! Huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife? 38.
Basi Yesu, hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo
lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake. 39. Yesu akasema, Liondoeni
jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa;
maana amekuwa maiti siku nne. 40. Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba
ukiamini utauona utukufu wa Mungu? 41. Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua
macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. 42. Nami
nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu
wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma. 43.
Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. 44. Akatoka nje yule aliyekufa,
amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu
akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.”
“1.
Basi, siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alifika Bethania, alipokuwapo Lazaro,
yeye ambaye Yesu alimfufua katika wafu. 2. Basi wakamwandalia karamu huko; naye
Martha akatumikia; na Lazaro alikuwa mmojawapo wa wale walioketi chakulani
pamoja naye.”
Kaburi la Mtakatifu Lazaro huko Bethania Nchini Israel
Utangulizi:
Vifungu hivi vya Biblia ni moja ya vifungu
vya kushangaza sana katika Biblia,Ni kifungu kinachotupa wasomaji wa Biblia
nafasi ya kuona Nguvu, utukufu na fahari ya Yesu Kristo na Uweza wake, Hapa
tunamuona mtu anayeitwa Lazaro akifufuliwa toka mautini mpaka kukaa karamuni
mezani na Bwana.
Katika kifungu hiki tunaona kile ambacho Yesu
alikifanya kwa Lazaro, na hiki ndicho anachowqeza kukifanya pia kwa wale
waliopotea au kufia dhambini, Kifungu kinatuonyesha jinsi Yesu alivyo na uwezo
wa kukutoa katika hali mbaya na kukualika katika Karamu pamoja naye katika hali
yoyote ile uliyonayo yenye kuashiria kufa na kuharibika kwa kila kitu katika
hali ya mauti Yesu anao uwezo wa kukuleta katika furaha na uchangamfu.
Mstari
32-42 Hali ya Lazaro.
Alikuwa masikini na mtu aliyechakaa, aliugua
kwa muda mrefu na sasa amekufa hayuko hai tena, alikuwa sasa kaburini, Familia
ndugu na jamaa walikuwa wamekusanyika kwa msiba na maombolezo, Yeye hangeliweza
kuwasikia kwa vile amefariki, Hata Yesu alipolisogelea Kaburi lake asingeliweza
kusikia kitu wala kuhisi uwepo wa Bwana, hii inaweza kuwa hali ya kila mtu
ambaye hajamwamini Yesu ni mfu mbele za Mungu Waefeso 2:1 Nanyi
mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa yenu ndivyo Biblia isemavyo, Dhambi hutufanya
tusihisi uwepo wa Mungu, hatuwezi kumjibu mungu lolote katika hali ya uovu na
dhambi, wala hatuwezi kuwa na ushirika naye wala na wenzetu, Lazaro alikuwa
amekufa na amezikwa.
Alikuwa ameoza kwa mujibu wa Maelezo ya
Martha Lazaro alikuwa amekufa siku nne sasa alikuwa ameanza kuharibika, kama ni
hatua ya kifo imekwenda mbali zaidi, Yesu alikuwa amefufua watu kadhaa ambao
walikuwa wamekufa Luka 8
alimfufua binti wa Yairo na Luka 7 alimfufua kijana wa mjane huko naini, wote
hao walikuwa wamekufa lakini walikuwa hawaanza kuoza labda walikuwa wamekufa
saa chache tu, lakini sivyo ilivyo kwa Lazaro alikuwa amekufa na alikuwa
amezikwa na sasa ameoza, Wakati Yesu anafika Kaburini alikozikwa lazazo ilikuwa
zimepita siku nne sasa alikuwa ananuka, alikuwa amekufa kiasi ambacho kila mtu
alikubali kuwa amekufa,kifo cha kimwili nafuu yake ni mazishi tu na kifi cha
kiroho nafuu yake ni Jehanamu tu Warumi 6:23.
Lazaro
alikuwa ni maiti iliyoharibika.
Unapomsikiliza Martha na Mariam Mstari wa 21,32,36 unaweza
kupata wazo lililowazi kabisa kuwa Lazaro alikuwa ni maiti iliyofikia hatua
ambayo hakuna lingine linaloweza kufanyika na wote tunaweza kukubaliana kuwa
huo ndio uhalisia, kisayansi na kitaalamu, Lakini kitu cha kushangaza ni huyu
mwanaume anayeitwa Yesu, huyu yeye anauwezo wa kufanya mambo kuwa tofauti, watu
wanaweza kukuweka kaburini na hata kukukatia tamaa na inawezekana kabisa hata
ndugu zako wakakubaliana kabisa kuwa wewe mambo yako hayawezekani tena, tabia
zako, hali yako, mwenendo wako, Biashara zako, Masomo yako, magonjwa yako, ndoa
yako, kila mtu akasema haiwezekani tena, huinuki tena, hutoki tena,basi tena
wakakuweka kaburini, na kutokutaka kukusogelea huko wakaombolezea kwa mbali,
lakini yuk mmoja ambaye anaweze kubadilisha mazingira anaweza kumuinua myonge
kutoka jalalani, anaweza kufufua nafsi yako anaweza kurejesha matumaini
yaliyokufa, anaweza kufanya tofauti katika maisha yako, anaweza kufanya
yasiyowezekana yakawezekana, anaweza kugeuza huzuni yako kuwa furaha, msiba
wako kuwa Harusi,kunuka kwako kuwa kunukia, kukataliwa kwako kuwa kukimbiliwa,
kuchokwa kwako, kuwa kibali, kukimbiwa kwako kuwa kukimbiliwa Ni Yesu ni Yesu ni
Yesu pekee anayeweza kufanya tofauti katika maisha yako, kuna uwezekano ukawa
umekata tamaa na watu wakakukatia tamaa lakini habari njema leo ni kuwa Yesu
analikaribia kaburi lako, Yeye ndiye pekee anayeweza kufanya tofauti katika
matumaini yaliyokufa Matendo
4:12, Yohana 14:6, Yesu alilisogelea kaburi la mtu
aliyeachwa peke yake, ananuka, ameoza, ameshindikana yuko gizani na kubadilisha
mfumo wa Mambo.
43-44 Yesu
alimuita Lazaro.
Yesu alipokwenda Kaburini alimuita Lazaro tu,
najua kulikuwa na sababu maalumu angesema ewe uliyekufa amka njoo huku wafu
wote wangefufuka, Yesu alikuwa na akili sana alimuita yule aliyemkusudia tu,
wakati wote Mungu anapoita pia kupitia ujumbe maalumu kama huu, anamuita mtu
mmoja binafsi huyu ataguswa na mwito huu, wapezni wito wa Mungu sio wa
jumlajumla Mungu anamakusudi na kila mmoja wetu kwa jinsi yake ni imani yangu
kuwa Yesu anamakusudi na ujumbe huu kwa mtu Fulani na ni lazima aguswe, Mungu
anataka watu wote waokolewe 1Timotheo 2:4, na kila atakayeliitia jina la
Bwana ataokolewa Warumi
10:13, Ufunuo 22:17, mLakini yesu alikuja kuokokoa
kile kilichopotea Luka
10:19 yuko mtu ujumbe huu unamuhusu.
Yesu alimuita Lazazo na ni Lazaro aliyetoka
kaburini alipoitwa, Mungu anakuita katika wokovu, katika uponyaji, katika wito
wa kumtumikia Mungu, anakuita kutoka katika shida zako na mahitaji yako
anakuita wewe amekuona wewe anataka kukusaidia wewe Toka huku nje, ondoka
kaburini, ondoka gizani yuko Mwanaume anayekuita leo huyu ni Yesu
Lazaro
alipoitwa nini kilitokea?
·
Uhai ulirudi ndani yake
·
Aliwekwa huru baada ya
kufunguliwa sanda zake
·
Aliona nuru kuu kwani kaburini
ilikuwa giza
·
Aliishi maisha ya raha na alikuwa
na wakati wa kufurahia maisha sasa alialikwa karamuni na kula na Bwana Yesu
Yesu yuko tayari kumuita kila mmoja wetu toka
Kaburini mwake, swali la kujiuliza je tuko tayari kuhudumiwa naye, je tuko
tayari kuisikiliza Sauti yake?yuko tayari kukupa wokovu, kukuhudumia na
kukutumia yeye bado anaita, kama uhusiano wako nay eye umeharibika anakuita
mtengeneze ili akualike karamuni mwake naye atakutoa mautini mpaka mezani pake.
Mkuu wa
Wajenzi mwenye Hekima!
Rev.
Innocent Kamote
0718990796
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni