Andiko la Msingi: 1 Wafalme 21:1-4
“1. Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli
alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya
Ahabu mfalme wa Samaria. 2. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba
lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu;
nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda,
nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. 3. Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana
apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. 4. Basi Ahabu akaenda nyumbani
kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na
Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani
pake, akageuza uso wake, akakataa kula.”
Naboth aliuawa akijaribu kuutetea urithi wa Baba zake kutokana na tamaa ya mfalme Ahabu na malikia muovu Yezebeli
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa Biblia
inazungumzia kwa undani sana kuhusu UMUHIMU WA URITHI, Katika Israel Urithi
ulitambuliwa kama moja ya maswala muhimu sana na kama mtu aliuza urithi
alizarauliwa sana katika jamii ya kiebrania na kuitwa jina la dharau kama mtu
asiyemcha Mungu au mwesharati Katika Waebrania angalia kwa mfano Waebrania 12: 16-17 Biblia
inasema hivi;-
“16. Asiwepo mwasherati wala asiyemcha
Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya
chakula kimoja. 17. Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi
baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana
kwa machozi.”
Angalia kwa makini jinsi Esau alivyoitwa katika maandiko,
alidharaulika kama mtu asiyemcha Mungu na mwesharati kwa nini? Kwa sababu
aliuza urithi wake
Ni nini maana ya neno
Urithi?
Urithi kwa asili ni Baraka kutoka
kwa Mungu, ambazo zinaweza kutafasirika katika ulimwengu wa kimwili na
kuhusisha fedha, mali, mashamba, mtaji karama, vipawa, maisha yako ya baadaye,
Elimu, Kazi, Mume, mke watoto,zawadi na kadhalika.
Baraka hizo zinaweza kuweko
duniani au kwa mtu toka kizazi hata kizazi, mtu anaweza kupokea urithi kutoka
kwa Mungu, Roho Mtakatifu, wazee wetu, na Baraka hizo na mali zikadumu, urithi
kwa kawaida hauwi mali ya mtu mmoja unakuwa ni mali ya familia, watu wako au
jamii yako, urithi unaambatana na Heshima mfano Mgombe urais wa republican
Donald Trump ambaye ni tajiri mkubwa sana duniani mwenye kuheshimika sana
lakini inajulikana wazi kuwa utajiri wake na heshima yake inatokana na urithi
wa utajiri wa Majumba kutokakwa Baba yake, na kwa mujibu wa maandiko katika
torati Mungu alikataza kabisa kuuza urithi soma Hesabu 36:7 Biblia inasema haya:-
“Hivyo hapana urithi wo wote wa wana wa
Israeli utakaotoka kabila hii kwenda kabila hii; kwa kuwa wana wa Israeli
watashikamana kila mtu na urithi wa kabila ya baba zake.”
Unaweza kuongezea na andiko kama Walawi 25:23 “Nayo
nchi haitauzwa kabisa kabisa; kwani nchi ni yangu mimi; maana ninyi ni wageni
na wasafiri wangu”
Unaweza kuona Mungu alikataza
kabisa kuuzwa kwa urithi lakini alikataza pia kuuza nchi, mtu aliyeuza
alihesabiwa kama mtu asiyemcha Mungu au mwesharati, mtu anayefanya ukahaba ni
tofauti na mtu anayefanya uasherati, makahaba huuza miili yao ili kupata
kipato, wanatoa miili yao kwa mapatano ya kupata faida, anayefanya uasherati
anatoa mwili wake bure, anautoa akitarajia kuwa hatimaye ataolewa mwisho wa
siku anajikuta amechezewa lakini haolewi, anakuwa amepoteza tumaini, amepoteza
muda na huku amesha chezewa vya kutosha na hakuna alichoambulia, mtu
anayechezea urithi anachezea maisha yake ya baadaye naya jamii yake, shetani
wakati wote ataangalia mbele katika mfumo wa maisha yako na kuanza kupambana na
mafanikio yako ya baadaye, kumbuka alipambana na Yusuphu kwa sababu ya ndoto
zake akitumia wivu wa kaka zake,
Watanzania kamwe tusikubali kuuza
ardhi, wala wanyama wetu, tusikubali kuwaachia wakawa mawindo wala kuwauza
katika nchi zao kwani baadaye hawatasafiri kuja kwetu kuangalia urithi tuliopewa
na Mungu, tusikubali madini na malighafi nyinginezo kuchukuliwa hovyo
Katika 1Wafalme 21:1-4 Tumeona
Jinsi Naboth alivyokuwa na msimamo, Mfalme Ahabu alitamani sana kulinunua
shamaba la mizabibu la Nabothi , Jambo hili lilikuwa kinyume na Torati, Kama
tulivyosoma, Nabothi alielewa vizuri sana swala hilo, na alijitia nguvu kumjibu
mfalme kwa ujasiri
“BWANA APISHIE MBALI NIKUPE WEWE URITHI WA BABA ZANGU?”
Ingawa majibu ya Nabothi
yaligharimu maisha yake na familia yake kwani wote waliuawa na mfalme ili
kujipatia shamba hilo kupitia mkewe muovu Yezebeli , Hata hivyo Nabothi anabaki
kuwa mtushujaa na jasiri na mwenye imani na mcha Mungu kwani alijua umuhimu wa
kuutunza urithi wa Baba zake, Mungu akupe neema na ampe neema kila mmoja wetu
kuhakikisha kuwa kwa gharama yoyote anatunza na kuutetea urithi wa taifa letu,
jamii yetu, ndugu zetu na wazazi wetu.
Ukiyajua hayo heri wewe
ukiyatenda!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni