Ijumaa, 26 Agosti 2016

Jinsi ya kubadilisha Mfumo wa Maisha yako!


Andiko: 1Nyakati  4: 9-10 Biblia inasema hivi:-


“ Naye Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze; na mamaye akamwita jina lake Yabesi akisema; Ni kwa sababu nalimzaa kwa huzuni, Huyo Yebesi akamlingana Mungu wa Israel, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kwelikweli na kunizidishia hozi yangu na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu ili usiwe kwa huzuni yangu, Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba.”


Utangulizi:

Kitabu cha Mambo ya nyakati kinaanza kwa kutupa Historia ya ukoo wa Kabila la Yuda na Simeon, hasa katika sura ya 4:1-43, Hata hivyo katika namna ya kushangaza sana mwandishi anaonyesha kuwa katika ukoo huo kulikuwa na mtu anaitwa Yabesi na inaelezwa kuwa alikuwa ni mtu mwenye heshima kubwa sana kuliko ndugu zake wote, ni katika aya mbili tu yaani ya 9-10 tunapata maelezo yote kuhusu Yabesi, na inaonekana kabla ya kuwa mtu mwenye kuheshimiwa sana miongoni mwa ndugu zake, inaonekana alikuwa mwenye kudharauliwa na mwenue huzuni kubwa sana, Biblia inaonyesha kuwa mama yake alimpa jina hilo YABESI akimaanisha juu ya huzuni, kwa sababu alimzaa kwa huzuni. Hatufahamu kwa undani sana ninikilitokea katika nyakati zake, ni shida gani iliipata familia yake lakini ni wazi kuwa alikuwa na mfumo wa maisha ya huzuni na alizaliwa katika mfumo huo na alipewa jina la jinsi hiyo, Habari njema ni kuwa hata hivyo Yabesi alifanikiwa kubadili mfumo wa Maisha yake na hatimaye kuwa mtu mwenye heshima sana, na mwenye utajiri mkubwa na mwenye kutegemewa na ndugu zake na kuheshimika sana

Jinsi ya kubadili mfumo wa maisha

Yabesi anatufundisha jinsi alivyofanikiwa kubadili mfumo wa Maisha na kufanikiwa kutoka katika huzuni kuwa mwenye furaha, kutoka katika maisha yasiyo na heshima kwenda kwenye kuheshimika, kutoka katika maisha yaliyojaa umasikini kuelekea kwenye utajiri wa kweli ni namna gani Yabesi alibadili mfumo wa maisha yake kanuni alizozitumia Yabesi zinauwezo mkubwa sana wa kubadili mfumo wa maisha yetu pia

1.       Yabes akamlingana Bwana Mungu wa Israel.
Kumlingana Mungu wa Israel maana yake ni kumtafuta Mungu kwa njia ya maombi na kukubali kufuata sheria zake, kwa ufupi ni kuhakikisha kuwa anauhusiano wa kweli na Mungu wa kweli aliye hai, Mtu yeyote yule atakayekubali kuwa na uhusiano thabiti na Mungu aliye hai, atafanikiwa, Yabesi aliona namna pekee ya kuondoka katika hali ngumu aliyokuwa nayo kwanza ni kutembea na Mungu, ni kuwa na Mungu wa kweli, ni kutembea na Mungu aliye hai ni kushikamana naye awaye yote atakayedumisha uhusiano na Mungu atafanikiwa

2.       Yabesi aliomba kwaaajili ya hali yake aliyokuwa nayo.
Ni muhimu kufahamu kuwa jambo lingine lililomletea Yabesi Heshima alikuwa muombaji, alikuwa akimuomba Mungu na tunaelezwa kuwa “Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba” mtu awaye yote akidumisha uhusiano wake na Mungu atakuwa na maombi yenye matokeo, maombi yenye kujibiwa, Yabesi aliomba Mungu ambadilishie hali ngumu alizokuwa nazo,ni ukweli usiopingika kuwa Yesu alituambia kuwa ninyi mkikaa katika neno langu, na maneno yangu yakikaa nadi yenu ombeni mtakalolote nayi mtatendewa.


3.       Yabesi aliomba kwamba Mungu apate kumbariki.
Ni muhimu kufahamu kuwa hakuna Baraka za muhimu zilizo kuu kama Baraka za kiroho, huo ndio msingi wa mambo mengine ya kimwili, Baraka za Mungu ni halisi na ndizo zinageuka kuwa vitu halisi, unaweza kuwa na kila kitu lakini bila mkono wa Mungu ukakosa amani, Yabesi hakutaka mchezo na Mungu aliomba kwa kudhamiria Lau Kwamba Ungenibariki kweli kweli Biblia ya KJV “Oh that You would bless me indeed” NIV “Oh, that you would bless me” hapa napenda Tafasiri ya Mfalme James KJV kwamba ungenibariki kweli kweli, unibariki hasa

4.       Yabesi aliomba kwamba Mungu apanue HOZI yake.
Neno hozi linazungumzia umiliki, mipaka, mtaji, mali heshima, uthamani, Thamani yake ilikuwa chini na sasa anamuomba Mungu azidishe uthamani wake kama alikuwa anazaraulika katika jamii mungu aongeze heshima,kama alikuwa anamiliki kidogo amiliki zaidi, NIV-expand my territory!, NASB-enlarge my border, KJV-enlarge my border, hapa pia napendezwa na tafasiri ya KJV kukuza uthamani, ili kubadilisha mfumo wa maisha ni muhimu tukamuomba Mungu akuze uthamani, awaye yote asilidharau Taifa letu, shule yetu, familia yetu, jamii yetu, lugha yetu, tamaduni zetu na maisha yetu Mungu ayaongeze thamani, tunaweza kudharaulika kwa sababu ya umasikini tulio nao, elimu tulizo nazo lakini Mungu anaweza kubadilisha mfumo wa maisha yako kwa kumsihi azidisha Hozi yako.

5.       Yabesi aliomba kwamba Mkono wa Mungu uwe pamoja naye.
Ndugu yangu hakuna jambo baya sana duniani kama mkono wa Mungu ukiondoka juu yako, Naomi alielewa vizuri kuwa mkono wa Bwana ukitoka juu yako hakuna mafanikio mikozi na balaa vinaweza kukuandama , kila unalolifanya halifanikiwi Ruthu 1:11-14, mkono wa Bwana ukiondoka juu ya mtu, kinachofuata ni uchungu kilio na maombolezo na hasara, hakuna utakachokifanya kinaweza kufanikiwa, Yabesi alielewa kuwa mkono wa Bwana ukiwa juu yako kila kitu kitafanikiwa na ndio maana Yabesi alifahamu umuhimu wa mkono wa Mungu kuwa pamoja naye Mkono wa Bwana ukiwa juu ya mtu, maana yake Bwana atakuongoza, atakulinda, atakupa kibali,utapata fadhili na kufanikiwa katika mambo yote.

6.       Yabesi aliomba kwamba Mungu amlinde na Uovu.
Kulindwa na uovu kunakotajwa hapa kumekuwa na tafasiri mbali mbali, uovu unaotajwa hapa unaweza kumaanisha pia dhambi, lakini hapa Biblia nyingi katika tafasiri zake zimetumia maneno kama matatu ya kiingereza “Evil, Pain, Harm, Stresses” ikimaanisha uovu wenye kuleta Huzuni, ni wazi kuwa dhambi inasababisha huzuni katika maisha yetu na ni vema kumuomba Mungu akatulinda na kutuweka mbali nayo, lakini Biblia inazungumzia zaidi, uovu unaoleta huzuni yaani hasara na kulindwa na maadui au uonevu, kimsingi tunaweza kumuomba Mungu atulinde na Uovu wa dhambi, Uovu wa taabu na huzuni, uovu wa maadui na kuonewa uovu wenye kuharibu mafanikio yetu Mithali 10:22 “Baraka za Bwana hutajirisha wala hachanganyi huzuni nayo

Mungu alijibu Maombi ya Yabesi na kubadilisha mfumo wa Maisha yake, awaye yote ambaye anataka kubadili mfumo wa maisha yake kutoka katika hali yoyote ile isiyokupendeza unaweza kumuomba Mungu kama Yabesi na Mungu atakusikia na kukujalia uliyoyaomba. Bwana ampe neema kila mmoja wetu kubadili mfumo wa maisha yake katika Jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai amen!

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: