Jumamosi, 3 Septemba 2016

MADHARA YA KUWAGUSA MASIHI WA BWANA.


Mstari wa Msingi: Zaburi 105: 14-15 Biblia inasema “Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwaajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu wala msiwadhuru nabii zangu

Kupakwa mafuta kuliunganisha unganisho la Kiroho na uwezo wa kufanya kazi uliyoitiwa na Mungu

He allowed no man to do them wrong Amplified, He allowed no one to oppress NIV, He permitted no one to do them wrong NKJV

Kusudi la Somo:- (uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka  na kutii na kuwa tayari kwa kila kazi njema Tito 3:1)

Watu wote duniani waliookoka na wasiookoka wanapaswa kuwa na ufahamu na kuwa na hekima juu ya ujumbe huu muhimu katika maisha yao ili wasije wakajikuta wanapoteza Neema ya Mungu na kuwa na maisha yaliyojawa na mikosi na mapigo mazito yasiyoweza kuzuilika kwa sababu ya kutokuwa na ufahamu katika neno la Mungu na tukajikuta tunamchukiza Mungu, Bwana na ampe neema na hekima kila mmoja wetu kuwa na ufahamu katika somo hili katika jina la Yesu amen. Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vine vifuatavyo:-
 
·         Maana ya Neno  masihi
·         Onyo la kutokuwagusa masihi wa Bwana
·         Madhara ya kuwagusa masihi wa Bwana
·         Jinsi ya kufanya.

MAANA YA NENO MASIHI

Neno masihi limetokana na neno la kiibrania MESIAH au MESSIAS  na limejitokeza kwa mara ya kwanza katika 1Samuel 2:10, ambalo maana yake ni mtiwa mafuta au mwenye kuwekwa wakfu kwa kutiwa mafuta ili awe Kuhani, Mfalme au nabii, kwa kiyunani ni Kristo, Neno masihi mahali hapo linatumika katika mazingira tofauti sana na ile tunayoitumia kwa Bwana Yesu Kristo, Nyakati za Agano la kale mtu alipochaguliwa na Mungu kuwa kuhani, mfalme au nabii aliwekwa wakfu kwa kutiwa mafuta na hivyo kuitwa masihi, mafuta hayo yaliyomiminwa juu yao kwa jinsi ya mwili yaliwakilisha maswala muhimu katika jinsi ya kiroho 1Samuel 16:1-13, Roho Mtakatifu alishuka juu ya mtu aliyepakwa mafuta kumuwezesha mtu huyo, kuwa na uwezo wa kiungu na wa kupita kawaida katika kuyatimiza majukumu yake, ilifanyika hivyo katika nyakati za agano la kale kwa vile Roho Mtakatifu alikuwa hajaja maalumu bado, Nyakati za sasa hatutiwi mafuta katika namna ya kimwili, Lakini Roho wa Mungu mwenyewe ndiye anayemchagua mtu kwa utumishi alioukusudia  na kumpaka Mafuta Matendo 13:1-3, aidha pia katika agano jipya watumishi wa Mungu wanapowekewa mikono na kubarikiwa wanakuwa wametiwa mafuta katika namna ya rohoni, Kumbuka kuwa ni Mungu mwenyewe ndiye anayechagua “Nitengeeni Barnaba na Saul kwa kazi ile niliyowaitia” watu wa Mungu

Mafuta ilikuwa na hata sasa ni alama ya Roho Mtakatifu, mtu alipopakwa mafuta Roho alimuwezesha kuwa na vipaji vya kiroho vya kuweza kutimiza jukumu alilokabidhiwa, Mfano Yesu Kristo kama Masihi hakupakwa mafuta kwa jinsi ya mwili, lakini alijiliwa na Roho Mtakatifu na kuongozwa katika kuyatekeleza majukumu yake Luka 3:21-22,4:1,18-19 Kupakwa mafuta kwa Yesu Kristo kulimfanya awe na uwezo wa kipekee katika kuitimiza huduma yake hivyo Yesu ni Masihi ni mpakwa mafuta ni Kristo, Mtu anapomwamini Yesu kuwa bwana na mwokozi wamaisha yake Roho wa Mungu anakaa ndani yake kwa hivyo kibiblia mafuta yanakaa ndani yake 1Yohana 2:26-27, Yohana 14:25-26, hivyo watu waliookolewa ni wapakwa mafuta roho Mtakatifu anakaa ndani yetu 1Wakoritho 3:10, Hata hivyo kutoka miongoni mwao Roho Mtakatifu ambaye ndiye Bwana wa Mavuno, huwaita watu katika huduma Matedno 13:2, watumishi wa Mungu wanaoitwa katika huduma maalumu za utumishi, Roho wa Mungu anakuwa juu yao kwaajili ya kutimiza huduma waliyoitiwa, kwa hiyo nao huitwa wapakwa mafuta, wapakwa mafuta hao wanakuwa wametumwa na Mungu na hivyo huyanena maneno ya Mungu Yohana 3:24 wao huubiri kweli yote kwa ujasiri bila kuichakachua injili, watasimamia kweli yote huku wenyewe wakiwa kielelezo cha injili wanayoihubiri, watakemea, wataonya, watatia moyo na hawatahubiri khadihi za kutungwa na wanadamu Mathayo 5:48, watahubiri utakatifu 1Petro 1:13-16,Waebrania 12:14 watafanya na kutenda kama Yesu Kristo mwenyewe, Masihi wa Bwana wanaishi kwa haki na utauwa, bila kuwa na lawama zilizo na ukweli 1Wakoritho 1:11, 1Wathesalonike 2:10, Biblia inasema tutawatambua kwa matunda yao.

Aidha masihi wa Bwana watafanya kazi ya kulitetea jina la Bwana lisichafuliwe au kutukanwa, Manabii makuhani na manabii nyakati za agano la kale hawakujali sana watu maadui zao wanasema nini juu yao bali, walijali sana maaduin au watu waliokuwa wakitaka au kumkufuru Mungu.

Masihi wa Bwana watahubiri Utakatifu, Ni  muhimu kufahamu kuwa shetani hawezi  kuhubiri  utakatifu na ni rahisi kupambambanua kati ya mtumishi wa shetani na  Mtumishi wa Mungu, sifa  mojawapo ya Mtumishi wa shetani ni kuhubiri maneno yake. ( maneno yao) na  watajifanya ni watumishi  wa haki na watahubiri   mambo   ambayo ukiwauliza kwa wameyapata wapi au yameandikwa wapi, watakuambia  hii  ndiyo  sheria au desturi ya kanisa:  watajitungia mambo yao  na  hawataihubiri  neno, shetani kamwe hawezi   kuhubiri  utakatifu   na watumishi wa shetani  hawawezi  kamwe  kuishi  katika  utakatifu  na akawa  kielelezo  na hawezi  kuwafanya  watu waokolewe na  kukaa  katika  usafi  na utakatifu: (shetani hawezi kumtoa  shetani )

ONYO LA KUTOKUWAGUSA MASIHI  WA BWANA. Zaburi 105: 14- 15,  I Nyakati  16: 21-22
Ni muhimu kufahamu kuwa Maandiko matakatifu yanatoa maonyo na yamejaa mafundisho na mifano ya kutosha yanayotoa maonyo dhidi ya kuwagusa masihi wa Bwana

Kuwagusa huku ni pamoja  na kuwasengenya, kuwanena  vibaya, kuwachafulia huduma zao ili waonekane  wabaya  hawafai kama walivyomchafua  Yesu  kwa  kusema  anatoa pepo kwa Nguvu za mkuu wa pepo Bezelzebul, kuwadhalilisha, mbele za  watu  wengine  kuwalia huduma zao ,  kuwaua moja kwa moja  au kuwadhuru kwa mabaya au kuwatukana huko ni kuwagusa  masihi wa Bwana au kuwanyanyasa, kuwavunjia Heshima, kuwadhulumu, na kuwatendea mabaya  kumgeuza  mkewe, hata  kama ni mfalme  atashughulikiwa  atadhibitiwa na  Mungu Zakaria 2: 8  kuwagusa hawa ni kugusa  mboni  ya jicho la Mungu;  Hivyo hata kama sisi ni  wachungaji tunapaswa kuangalia walio juu  yetu  kwani wao  ni masihi wa Bwana. Kwa nini Biblia inaonya kutokuwagusa masihi wa Bwana au wapakwa mafuta?

1.       Wao ni Mawakili wa Mungu- Tito. 1:7,8,9 “Maana imempasa askofu(mwangalizi) awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa Mungu; asiwe mtu wa kujipenda nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu; bali awe mkaribishaji, mpenda wema,mwenye kiasi,mwenye haki, mtakatifu,mwenye kudhibiti nafsi yake, akilishika lile neno la imani vilevile kama alivyofundishwa,apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.”

2.       Hawajichukulii wenyewe heshima hii Waebrania 5:4 “Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe Heshima hii ila yeye aitwaye na Mungu kama vile Haruni

3.       Biblia imeagiza kuwatii na kuwanyenyekea wanaotuongoza Waebrania 13:17 “watiini wenye kuwaongoza  na kuwanyenyekea  maana wao wanakesha kwaajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua maana isingeliwafaa ninyi

4.       Mungu huwaheshimu watu wanaomtumikia Yohana 12:26 “Mtu akinitumikia na anifuate nami nilipo na mtumishi wangu atakakapokuwepo, tena mtu akinitumikia Baba atamheshimu

MADHARA YA KUWAGUSA MASIHI WA BWANA.

Muda usingetutosha kuweza kuangalia mifano  mmoja moja katika Biblia juu ya watu waliowagusa masihi wa Bwana na kushughulikiwa kwa makini na Mungu alivyoonyesha  ghadhabu juu yao hata hivyo tutaangalia mifano kadhaa:

1.       MARIAMU: (Hesabu 12: 1- 9) Miriamu alikuwa nabii mke lakini alinena vibaya juu ya uongozi wake Musa na  alishughulikiwa kwa kupigwa ukoma.

2.       FARAO:  Alichukua mke wa Ibrahimu kwa kutumia mamlaka ya kifalme alivyokuwa nayo na alishughulikiwa kwa mapigo mazito sana.( Mwanzo. 12: 14- 17

3.       ABIMELEKI:  Alipotamani kumchukua Sarai mke wa Ibrahim Mungu alimtandika( MWANZO 20: 1- 4, 6-8,14)

4.       YEROBOAMU: ( I Falme 13: 1- 4

5.       ASKARI WALIOTAKA KUMKAMATA  ELIYA  Bila kuonnyesha unyenyekevu  ( 2 Falme 1: 5- 15)

6.       WATU WALIOMFANYIA MZAHA ELISHA  yaani vijana waliomtania Upara wake (2 Falme 2: 23- 25)

7.       MWAMLEKI Aliyejidai kuwa ameuua  SAULI ( 2  Samwel 1: 1-16)

8.       Herode Baada ya Kumuua Yakobo Matendo 12: 1-4,20-24

JINSI YA KUFANYA.

-          Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu anaheshimu sana mafuta na kwa sababu hiyo si vema kupuuzia mafuta yaliyo juu ya watumishi wake kwani kwa kufanya hivyo kuna madhara yawezayo kutupata
-          Ni muhimu pia kufahamu kuwa kupakwa mafuta haipaswi kuwa sababu ya kuwafanya wapakwa mafuta hao kutokuishi sawa na maadili ya injili na Neno la Mungu
-          Ni muhimu kuomba kwa ajili ya wapakwa mafuta kwa sababu nao ni wanadamu

Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote
Nilijifunza kutoka kwa Bishop Zachary Kakobe, Miaka zaidi ya 20 iliyopita.

Hakuna maoni: