Andiko la msingi: Zaburi 46:1-2 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na Nguvu, Msaada
utakaoonekana tele wakati wa mateso, kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi,
Ijapotetemeka milima moyoni mwa Bahari”
Utangulizi.
Kwa mujibu wa Mafundisho ya
kibiblia kuhusu Maombi, Biblia inatoa maelekezo kwamba imetupasa kumuomba Mungu
siku zote bila kukata tamaa Luka 18:1
“ Akawaambia
mfano ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote , wala wasikate tamaa”
kwa lugha nyingine imetupasa kumuomba Mungu siku zote bila kukoma 1Wathesalonike 5:17 “Ombeni bila kukoma”
ni wazi kuwa Biblia inatia moyo kuwa
waombaji na kila siku kumuomba Mungu na kushukuru, ni katika hali zote na kwa
namna yoyote imetupasa kuomba Maombi ni muhimu sana katika maisha yetu, na
katika kudumisha uhusiano wetu na Mungu, Yesu alikuwa Muombaji, hatuna budi
kuunganisha ucha Mungu wetu na maombi, kuacha maombi ni sawa na kuacha Ukristo!
Lakini kila mmoja anaweza
kujiuliza kwa nini leo mkuu wa wajenzi anataka au anazungumzia Umuhimu wa maombi wakati wa mambo Magumu, Kwa
ujumla maombi yanapaswa kuwa sehemu na tabia ya kila amwaminiye Yesu Kristo, Na
pamoja na hayo binafsi sipendi kuomba wakati wa mambo magumu, nafurahia sana
kuomba wakati wa amani, hata hivyo kibiblia wakati wa mambo magumu sio wakati
wa kuacha kuomba ni wakati wa kuongeza bidii katika kuomba. Biblia
inatufundisha kuwa nyakati za Kanisa la kwanza wakristo wa Karne ya kwanza
walikuwa waombaji, sehemu kuu ya ibada ya kawaida ya kanisa ilikuwa ni maombi,
waliomba Mungu siku zote, Biblia inasema walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja
katika kusali Matendo 2:14 “Hawa wote walikuwa
wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali,pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake
Yesu na ndugu zake” Unaona! Biblia inaonyesha kuwa wanafunzi na mama
yake Yesu na ndugu zake walidumu katika kuomba hii ndio ilikuwa tabia ya
nyakati za kanisa la kwanza.
Lakini hata hivyo tunaweza kuona katika
biblia Kanisa la kwanza wakiongeza Maombi zaidi wakati wa mambo magumu, kama
andiko la msingi pale juu linaonyesha kuwa Mungu kwetu sisi ni kimbilio na
nguvu, ni msaada utakaoonekana tele wakati wa Mateso, hii maana yake ni kuwa ni
lazima na ni muhimu kuliitia jina la bwana zaidi wakati wa mateso na majaribu Matendo 4:23-31 Biblia inasema
“23. Hata
walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote
waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. 24. Nao waliposikia, wakampazia
Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe
uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; 25. nawe ulinena
kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa
wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? 26. Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya
shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. 27. Maana ni kweli, Herode na
Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji
huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, 28. ili wafanye yote
ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. 29. Basi
sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako
kwa ujasiri wote, 30. ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike
kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. 31. Hata walipokwisha kumwomba Mungu,
mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena
neno la Mungu kwa ujasiri.”
Unaweza kuona Kumbe wakati wa majaribu
na mateso pia ni wakati mzuri wa kuongeza bidii na kumuomba Mungu kwa nguvu
zaidi, Muda usingeliweza kutosha kwa nyongeza ya mifano zaidi ya kibiblia
lakini biblia inaonyesha pia Paulo na Sila walipokuwa Gerezani yaani wakati wa
mateso waliendelea kukazia ibada Matendo
16:25 “Lakini
panmapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia
nyimbo za kumsifu na wafungwa wengine walikuwa wakisikiliza” unaona
ukiendelea kusoma utaweza kuona ni nini kilitokea Mungu alipowajibu maombi yao
hivyo Biblia inatufundisha kuwa tusikate tamaa na kuwa hata wakati wa mambo
magumu inatupasa kuomba
1. Kwa
nini inatupasa kumuomba Mungu hata wakati wa Mambo Magumu
2. Maombi
ni msaada kutoka kwa Mungu wakati wa mambo Magumu Zaburi 3:3-8;34:4
1.Bwana, watesi wangu wamezidi kuwa wengi, Ni wengi
wanaonishambulia, 2. Ni wengi wanaoiambia nafsi yangu, Hana wokovu huyu kwa
Mungu. 3. Na Wewe, Bwana, U ngao yangu pande zote, Utukufu wangu na mwinua
kichwa changu. 4. Kwa sauti yangu namwita Bwana Naye aniitikia toka mlima wake
mtakatifu. 5. Nalijilaza nikalala usingizi, nikaamka, Kwa kuwa Bwana
ananitegemeza. 6. Sitayaogopa makumi elfu ya watu, Waliojipanga juu yangu pande
zote. 7. Bwana, uinuke, Mungu wangu, uniokoe, Maana umewapiga taya adui zangu
wote; Umewavunja meno wasio haki. 8. Wokovu una Bwana; Baraka yako na iwe juu
ya watu wako.
3. Maombi
ndio njia ya Mungu ya kutulinda na nguvu na utendaji wa yule muovu Mathayo 6:13, Efeso 6:12.
4. Maombi
ndio njia pekee ya kutuletea amani tunapokutana na Magumu na hali za kutisha na
kukatisha tamaa Wafilipi 4:4-7
5. Maombi
yanaweza kupindulia mbali vikwazo vya aina zote Marko 11:23-24
6. Maombi
ndio njia ya kututia moyo wakati wa kuvunjika Moyo Wakolosai 1:9-11
7. Maombi
yana nguvu ya kuhairisha jambo baya Esta
4:15-17, Daniel 2:13-19
8. Maombi
ndio njia ya kupokea nguvu za kiroho na ujasiri wakati wa vita za kiroho Matendo 4:23-31
Bila shaka sasa
unaweza kuona na kuamini kupitia maandiko, kuwa wakati wa mateso na Mapito na
mambo magumu ya aina yoyote ile, huo sio wakati wa kukata tamaa na kuacha
kuomba ni wakati wa kuzidisha maombi na kumtegemea Mungu, Na Mungu hujitokeza kwa viwango vikubwa tukionyesha kumtegemea
yeye katika maombi wakati wa Mahitaji yetu katika wakati mgumu.
Rev. Innocent
Kamote
Mkuu wa wajenzi
mwenye Hekima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni