Jumamosi, 25 Machi 2017

Ujumbe: Kataa kudhalilishwa kwa Jamii yako!



“Reject any insult in your society” 

Mstari wa Msingi: 2Samuel 10:1-5,17-19.

“Ikawa baadaye, mfalme wa wana wa Amori akafa, akamiliki Hanuni, mwanawe, mahali pake. Naye Daudi akasema, Nitamtendea wema Hanuni, mwana wa Nahasi, kama babaye alivyonitendea wema mimi. Basi Daudi akatuma kwa mkono wa watumishi wake, ili kumtuliza kwa habari za babaye. Wakaja watumishi wa Daudi katika nchi ya wana wa Amoni. Lakini wakuu wa wana wa Amoni wakamwambia Hanuni, bwana wao, Je! Waona ya kuwa Daudi amemheshimu babayo kwa kutuma kwako wafariji? Je! Daudi hakuwapeleka watumishi wake kwako ili kuuangalia mji, na kuupeleleza, na kuuangamiza? Basi Hanuni akawatwaa hao watumishi wa Daudi, akawanyoa nusu ya ndevu zao, akawakatia nguo zao katikati, hata matakoni, akawatoa waende zao. Watu walipomwambia Daudi habari hizo, akatuma watu kuwalaki; kwa sababu watu hao walikuwa wametahayarika sana. Mfalme akasema, Ngojeni Yeriko, hata mtakapoota ndevu zenu, ndipo mrudi.” 

“Alipoambiwa Daudi, akakusanya Israeli wote, akavuka Yordani, akaja Helamu. Nao Washami wakajipanga kinyume cha Daudi, wakapigana naye. Wakakimbia Washami mbele ya Israeli; naye Daudi akawaua katika Washami, watu wa magari mia saba, na wapanda farasi arobaini elfu, naye akampiga huyo Shobaki, jemadari wa jeshi lao, hata akafa huko. Na wafalme wote waliomtumikia Hadadezeri walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, walifanya amani na Israeli, wakawatumikia. Basi Washami wakaogopa kuwasaidia wana wa Amoni tena.”                
Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Daudi alikuwa na kiongozi mwenye moyo wa ajabu sana, aliwapenda watu wake aliwapenda jirani zake, alipenda haki alilipa mema, lakini Daudi alichukia sana Udhalilishaji, Biblia inaonyesha katika kifungu tulichosoma Jinsi Israel walivyopigana vita na wana wa amoni na washami sababu kuu ikiwa ni Udhalilishwaji wa watumishi wake

Maana ya udhalilishaji
Neno udhalilishaji kwa kiingereza Insult au offend au embarrassing au abuse ni tendo au neno la kumfanya mtu ajione kuwa duni, ajione amedhalilishwa, amenyanyaswa, amefanywa duni na mnyonge,amefungwa au ametekwa au asiye huru, Daudi anaonekana kukataa kudhalilishhwa yeye na jamii yake 

Kuwanyoa watu nusu ndevu nyakati za Biblia lilikuwa ni tendo la unyanyasaji wa hali ya juu sana katika mashariki ya kati, kunyoa ndevu katika hali ya kawaida kulimaanisha una huzuni au msiba mkubwa Isaya 15:2,  Wanapanda juu hata Bayithi na Diboni, mpaka mahali palipo juu ili walie; juu ya Nebo na juu ya Medeba Wamoabi wanalia; Wana upaa juu ya vichwa vyao vyote; kila ndevu zimenyolewa.” Yeremia 41:5, “wakafika watu kadha wa kadha toka Shekemu, na toka Shilo, na toka Samaria, watu themanini, nao wamenyoa ndevu zao, na kurarua nguo zao, nao wamejikata-kata, wakichukua sadaka na ubani mikononi mwao, ili wazilete nyumbani kwa Bwana. aidha katika Biblia na nyakati za Biblia kuwachania wat nguo zao makalioni lilikuwa ni jambo la kuaibisha lililomaanisha ninyi ni wafungwa au mateka wa vita na zawadi yenu ni kuaibishwa tu Isaya 20:4. “vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawachukua uchi, wafungwa wa Misri, na watu wa Kushi waliohamishwa, watoto kwa wazee, hawana viatu, matako yao wazi, Misri iaibishwe.”

Yesu Hatakubali uaibishwe!

Daudi angekubali jambo hilo maana yake anagekuwa amekubali aibu na huzuni, amekubali salamu za kuaibishwa kwake na jamii yake, Daudi alikataa kudhalilishwa alimtuma Yoabu kupanga vita na kupambana kwa gharama yoyote.

Moyo wa Daudi ni kama wa Yesu Kristo, shetani amekusudia kumuweka kila mmoja wetu katika aibu kubwa ya maisha haya lakini na wengine si ajabu kuwa ameshatuaibisha lakini Kristo Yesu ka Ilivyo kwa Daudi hawezi kuvumilia wewe na mimi tudhalilishwe au tuingie katika aibu, na tumkimbilie yeye atatihufadhi na kutuondolea aibu yetu yote.

Daudi alikuwa anatambua siri ya kuikimbia aibu yetu ni kumkimbilia Mungu tu, kusudi kubwa la shetani ni kutuaibisha katika maisha yetu ni kutufanya tutahayari, ni kutufanya tujione duni wanyonge hatufai masikini na mateka katika ufalme wake.

Lakini leo tunaye wa kumkimbilia yeye ni Mwana wa Daudi na tumkimbilie yeye tusiaibike milele Zaburi 31:1, “Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye,” Zaburi 71:1-71. Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele.  Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe. Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu.  Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi, Katika mkono wake mwovu, mdhalimu, Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU, Tumaini langu tokea ujana wangu.  Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa, Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, Ninakusifu Wewe daima. Nimekuwa kitu cha ajabu kwa watu wengi, Na Wewe ndiwe kimbilio langu la nguvu.”

Wayahudi leo hawako Tayari kupoteza Taifa lao

 "Wayahudi waliokimbilia Masada walikuwa tayari kufa kuliko kwenda utumwani"

Mwaka wa 70 askari wa Rumi walikusudia kuwauwa wayahudi wote kutokana na uasi wao, warumi waliamua kupita mji kwa mjia kuhakikisha kuwa wanawaua wayahudi mpaka mwaka 73 kijiji cha mwisho kuvamiwa na kuzingirwa kilikuwa ni kijiji cha Masada wayahudi waliokimbilia huko inakisiwa walikuwa 960 hivi kwa pamoja waliamua “KULIKO KWENDA UTUMWANI NI AFADHALI KUFIA KATIKA INCHI YETU”

Hitimisho!

·         Shetani siku zote anaandaa mpango wa kutuaibisha
·         Mungu siku zote anamawazo mema juu yetu
·         Watumishi wa Daudi walipoaibishwa walikimbia kurudi kwa Daudi mfalme wao
·         Sisi hatuna budi kukimbia na kurejea kwa Bwana wetu Yesu ili atutetee
·         Daudi alikuwa na tabia ya kumkimbilia Mungu ili asiaibishwe
·         Sisi nasi wakati wote tumkimbilie Bwana wetu Yesu hii ndio namna pekee ya kukataa aibu katika maisha yetu. 

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.
0784394550
0718990796

Hakuna maoni: