Mstari wa Msingi: 2 Wakoritho 4:7 “Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu wala sio kutoka Kwetu”
Utangulizi:-
Ni muhimu kwa kila mmoja wetu
kujitambua na kujifahamu kuwa tumeumbwa kwa njia ya jabu sana, na hivyo ni vema
katika maisha yetu tukampa Mungu utukufu siku zote na kumshukuru yeye
anayetuwezesha na kuyashikilia maisha yetu, Maandiko yanatufananisha sisi kwa
Mungu kama viumbe dhaifu sana yaani tumeumbwa kwa udongo, sisis ni kama chombo
cha udongo katika mikono ya Mungu na Mungu baba yetu ndiye mfinyanzi kwa maana
hiyo imetupasa kuishi na kuendena kwa unyenyekevu mkubwa, vipawa na akili na
karama Mungu alizowekeza ndani ya Mwanadamu ni hazina sio ya kujivunia bali ni
kwaajili ya utukufu wa Mungu.
Vyombo vya Dongo:
2 Wakoritho 4:7 “Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama
kuu ya uwezo iwe ya Mungu wala sio kutoka Kwetu” tunaweza
kuutafasiri mstari huu katika lugha nyepesi ya mkuu wa wajenzi hivi “Lakini
kuna vitu vya thamani kubwa sana vimewekwa katika vyombo vya dhaifu vya udongo,
ili utukufu na sifa kuu iwe ya Mungu wala sio kutoka kwetu”
Kwa nini Paulo mtume anazungumza
maneno mazito namna hii na je yana maana gani kwetu? Ni muhimukwanza tukawa na
ufahamu wa kutosha kuhusu vyombo vya dongo, Vyombo vya udongo anavyozungumza
Paulo Mtume ni vyombo vilivyotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi na kuumbwa na
mfinyanzi kwa ustadi kulingana na makusudi na matakwa ya mfinyanzi husika, Mara
baada ya kufinywangwa vyombo hivyo vilichomwa kwa moto ili kuweza kuvifanya
imara, baada ya hatua hiyo vingeweza kupakwa rangi na kuchorwa maua ya aina
mbalimbali ya kupendeza na kuwa na muonekano mzuri sana
Nyakati za Biblia zamani sana
vyombo vya udongo vilitumika kwa kusudi pia la kuhifadhi au kuficha hazina au
vitu vyenye thamani sana, mfano halisi ni kuwa watu wa kale waliwahi kuhifadhi
katika vyungu magombo ya chuo cha nabii isaya na vitabu vingine vya ngozi
vilivyotumika zamani, Mfano halisi ni katika bonde la Qumran yaliwahi kuokotwa
magombo ya ngozi yaliyokuwamo katika vyombo vya dongo vya kale, vijana wa
kiislamu waliokuwa wakichunga Kondoo walikuwa wakirusha mawe huenda ni katika
lengo la kutafuta kondoo, walisikia mlio Fulani wa chungu katika pango,
walipofika kumbe ni chungu au mitungi iliyoundwa kwa dongo na ndani yake
kulikuwa na ngozi zilizokuwa na maandishi, wao wakiwa hawajui maandishi hayo
walitaka kuzitumia ngozi hizo kutengenezewa viatu, Mafundi waligundua kuwa
yalikuwa ni maandiko matakatifu waliyapeleka kwa Kanisa na yakahifadhiwa chuo
cha nabii Isaya kwa mfano kilipatikana kamili kama ilivyo Biblia katika magombo
hayo.
Kutokana na mtazamo huo Paulo
mtume anatukumbusha katika 2 Wakoritho
4:7 kuwa wanadamu tunafanana sana na vyombo hivyo vya udongo, karama, akili
na vipawa alivyotupa Mungu ni hazina tu iliyohifadhiwa katika vyombo dhaifu
sana vya dongo, vyombo ambavyo ni dhaifu na vinaweza kuvunjika wakati wowote na
kwa njia rahisi “very delicate” ukweli huu haupingiki kwa sababu biblia iko
wazi kuwa wewe na mimi tuliumbwa kwa Udongo Mwanzo 2:7 Biblia inasema “. BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia
puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Unaona? Mpendwa wewe na mimi ni mavumbi yaani ni udongo
tu! Mungu analijua vema sana umbo letu na kukumbuka kuwa sisi ni mavumbi Zaburi 103:14 Biblia inasema “Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka
ya kuwa sisi tu mavumbi.” Je unajua kuwa Mungu anakumbuka kuwa sisi
tu mavumbi? Ndio ni muhimu kukumbuka lakini pamoja na kuwa Mungu ametuumba kwa
udongo ameweka vitu vya thamani kubwa ndani yetu ambavyo hata Malaika hawana!
Kutokana na jinsi Mungu
alivyotuumba kwa thamani kubwa kiasi hicho ingawa ni dhaifu sana lakini ameweka
vitu vya thamani na ujuzi wa hali ya juu na karama na vipawa ndani yetu, Hata
hivyo Mungu anatuonya katika neno lake kuendelea kumuheshimu yeye na
kujihadhari na majivuno ya aina yoyote na kuenda mbele zake kwa unyenyekevu
mkubwa na kumrudishia yeye utukufu, heshima na adhama kwa sababu yeye ni
mfinyanzi na sisi ni kama vyombo hivyo dhaifu mikononi mwake Isaya 45:9 “Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae
kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya
nini? Au kazi yako, Hana mikono?” Unaona ni maonyo makali kutoka kwa
Mungu kupitia Nabii Isaya hatuwezi kuwa Jeuri kwa Mungu mimi na wewe ni kama
Kigae Biblia inasema ole wetu kama tutashindana na Muumba! Isaya 64:8 “Lakini sasa, Ee
Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu
kazi ya mikono yako.” Hatuwezi kushindana na Mungu Baba yetu
inatupasa kuwa wanyenyekevu mno kwani sisi ni udongo na Mungu baba yetu ni
mfinyanzi tu sisi ni dhaifu Mungu na atusaidie tusijivune kwa jambo lolote.
"Paulo Mtume alikuwa dhaifu katika mwili lakini alijaa Neema na Kweli alikuwa kama Malaika"
Hazina katika vyombo vya udongo!
Paulo mtume anapozungumzia Hazina
katika vyombo vya udongo alikuwa na maana pana zaidi ingawa msingi wake mkubwa
ni jinsi Mungu alivyowekeza siri zake katika mioyo yetu, siri ya injili, Paulo
anazungumzia nguvu na uwezo wa Mungu, vipawa na karama ambazo zimewekezwa ndani
ya mtu kiasi ambacho mtu akisikia habari zako anaweza kudhani kuwa wewe ni jitu
kubwa sana
Paulo alikuwa na ujuzi wa nguvu
za Mungu na udhaifu wa mwili wa binadamu ambao ni kama udongo Mungu alimtumia Paulo
mtume kwa miujiza ya viwango vya kupita kawaida Biblia inatoa majumuisho tu ya
huduma ya Paulo na jinsi Mungu alivyomtumia kwa kusema
·
Matendo
19:11 “Mungu
akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida;”
·
Licha ya Mungu kumtumia Paulo kwa mijuiza
mikubwa ya kupita kawaida lakini ni wazi kuwa Mtume Paulo ndiye mtume
aliyefanya kazi kuliko mitume wote kama maandiko yanenavy 1Wakoritho 15:10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema
yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao
wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.”
·
Licha ya Paulo kutumiwa na Mungu na kufanya kazi
kuliko mitume wote yeye alipewa mafunuo makubwa sana kuliko mtume yala mtumishi
yeyote Paulo alipelekwa mpaka Mbingu ya tatu akaonyeshwa mambo mazito na meneno
mazito ambayo mengine ni magumu kuyaeleza angalia 2Wakoritho 12:2-4 “Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na
minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui;
Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu. Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika
mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua); ya kuwa
alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu
mwanadamu ayanene”.
·
Paulo Mtume alikuwa Mwombaji, alikuwa akinena
kwa lugha kuliko mtu yeyote, alikuwa na karama zote alikuwa na uwezo wa kuimba
mpaka malango ya gereza yanafunguka, aliombea watu wa kila aina na kuponya
wenye magonjwa, Paulo alikuwa Msomi ni Daktari wa Sheria aliyebobea na
kadhalika
Lakini pamoja na vipawa alivyokuwa
navyo hakusahau kuwa yeye ni mavumbi alitambua kuwa Mungu ameweka hazina katika
vyombo vya udongo tu na Historia ya kanisa inaeleza kuwa Paulo mtume ndiye
aliyepatwa na majaribu mengi zaidi na mateso mengi zaidi kwaajili ya Kristo na
injili, inasemakana kuwa Paulo mtume hakuwa jitu kubwa alikuwa ni mwembamba
sana mwenye matege na nyele zake zilikuwa zimejinyonganyonga kama mmanga, aidha
alikuwa na udhaifu katika mwili wake alikuwa anaumwa na pia alikuwa na macho
dhaifu sana 2Wakoritho 12:7-9 Biblia
inasema hivi “.Na
makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa
mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita
kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye
akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu.
Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu
yangu”.
Unaweza kuona! Paulom mtume
alikuwa na mwili dhaifu na pia macho dhaifu aliomba kuondolewa tatizo hilo
lakini Mungu alimwambia ni neema yangu tu inakutosha ili asiwe na Majivuno, Wagalatia 4:13-15 “Lakini mwajua ya kuwa naliwahubiri Injili mara
ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili; na jaribu lililowapata katika mwili
wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama
Kristo Yesu. Ku wapi, basi, kule kujiita
heri? Maana nawashuhudu kwamba, kama ingaliwezekana, mngaling'oa macho yenu,
mkanipa mimi”. Paulo mtume
alikuwa na udhaifu katika mwili wake pamoja na kuombea wengi Mungu aliyaachia
kwaajili ya utukufu wake ni kwaajili ya haya Paulo anaona kuwa Mungu ameweka
hazina katika vyombo vya udongo.
Ndugu msomaji wangu hatuna cha
kujivunia? Tunapaswa kuwa wanyenyekevu, tunapaswa kumpa Mungu utukufu, lakini
hata kama ni wadhaifu hatuna hiki ama kile hiyo haipunguzi thamani ya kuumbwa
kwako mfinyanzi ameliweka kusudi lake ndani yako usikate tamaa lakini kumbuka
kuwa sisi ni binadamu ni daifu na Mungu ni mwenye nguvu ni mfinyanzi na tuishi
mbali na majivuno ya aina yoyote tuwapo ulimwenguni
Mungu alimtuma Musa licha ya kuwa
na kigugumizi, alimtumia Elisha licha ya kuwa na Upara, alimtumia Daudi licha
ya kuwa na umri mdogo na kudharaulika hata kwa baba yake, acha kujidharau kwa
sababu zozote zile
Kumbuka kuwa asili ya nguvu zetu,
uzuri wetu, ujuzi wetu, heshima yetu na mali zetu zimetokana na Mungu muumba
wetu. Ukiyajua nhayo heri wewe ukiyatenda
Na mkuu wa wjenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni