Jumatano, 12 Julai 2017

Amri iliyo kuu:



Mathayo 22:34-40Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu;  Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.  Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.”

 Kutokana na upendo mkubwa usio na mipaka aliokuwa nao Abrahamu asingeliweza kuzuia kumrudisha Isaka kwa Mungu endapo tu kama malaika wa Bwana Hangelimzuia kufanya hivyo

Utangulizi:

Kifungu hiki cha maandiko ni moja ya kifungu muhimu sana kwa wanafunzi wa Biblia kuweza kukipa muda na kujifunza, Kuna jambo au mambo muhimu ya msingi ya kujifunza hasa kutokana na Majibu ya Yesu Kristo kwa  swali la Mwanasheria wa kiyahudi aliyetaka kujua amri iliyo kuu ni ipi ili kupima uelewa na msimamo wa Yesu Kuhusu Torati, Pamoja na kuwa swali liliulizwa kwa hila lakini ukweli unabaki kuwa jibu la Bwana Yesu lilikuwa la muhimu kwa mafarisayo na kwa kila mwanadamu mmoja mmoja kuhusu umuhimu wa Kumpenda Mungu na wanadamu wenzetu, Jibu la Yesu safari hii lililkuwa ni andiko lililonukuliwa moja kwa moja kutoka Kumbukumbu la torati 6:4-5 ambao unasema hivi “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.”Lakini pamoja na hayo Yesu aliongeza amri ya pili inayofanana na hiyo Mpende Jirani yako kama nafsi yako. Unapoangalia kwa makini katima vifungu hivi na majibu ya Yesu Kristo utaweza kuona kuwa Yesu alijibu swali hili kwa Upeo mpana na wa hali ya juu ambao tutachukua Muda kuuchambua leo kwa kuzingatia mambo ya msingi nay a muhimu yafuatayo:-

·         Amri iliyo kuu ni Upendo
·         Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote
·         Mpende jirani yako kama nafsi yako.

Amri iliyo kuu ni Upendo:-

Ni muhimu kwanza kufahamu kuwa katika majibu ya Yesu kwa mwanasheria Yesu amekazia neno Upendo likitumika kote kwa Mungu kwanza na kwa binadamu pia Kwa msingi huo ni muhimu kwetu kuchukua Muda kutafakari kwanza maana ya Neno Upendo linalotajwa katika biblia linamaanisha nini kabla ya kujifunza mambo mengine kwa undani:-

Kwa kawaida unapotaja neno la kibiblia upendo, huna budi kukumbuka kuwa Biblia hususani agano jipya lililetwa kwetu kwa lugha ya kiyunani, na kutokana na mantiki ya Kiswahili kuhusu neno upendo na ya kiingereza kutokutosheleza aina ya upendo tunaotaka kuzungumza ni muhimu kwetu kwanza kuzama katika lugha ya kiyunani na kuangalia maneno yanayotumika kutofautisha upendo na maana zake, katika kiyunani unapotaja neno Upendo kuna maneno manne yanayoelezea upendo kwa maana tofauti Kuna neno PHILEO,STORGE,EROS na AGAPE au AGAPAO.

·         PHILEO aina hii ya upedno kwa kiingereza tunaiita “Companionable love”yaani ni upendo wa Kirafiki, Ni upendo unaojengeka kutokana na kushirikiana kuzungumza kukubaliana kupeana zawadi,kuendana na kadhalika huu ni upendo wa kirafiki.

·         STORGE aina hii ya upendo kwa kiingereza tunaiita “Natural affection love” yaani ni upendo unaotokana na kuweko kwa undugu wa damu, unampenda mtu kwa sababu ni baba, mama, mwana, mjomba shangazi, dadam kaka na kadhalika katika mahusiano ya kindugu na damu.

·         EROS aina hii ya upendo kwa kiingereza tunaiita “Erotic love” yaani ni upendo unaotokana na mvuto wa kimapenzi, ni upendo unaohusu jinsia tofauti na yako, unampenda mtu kwa sababu ya muonekano wake , umbile lake na uzuri wake hii husababishwa na mvuto wa kimapenzi, body morphology is concern Muonekana wa mwili au mvuto unahusika na upendo huu ni wa kihisia.

·         AGAPE aina hii ya Upendo kwa kiingereza tunaiitaunconditional love Yaani ni upendo wenye kupitiliza mipaka ya kibinadamu, ni upendo ambao asili yake ni Mungu ni upendo unaomtakia mema kila mmoja awe adui au ndugu upendo huuunapita mipaka ya kawaida ya kibinadamu, hauangalii hali ya hewa, unampenda Mungu au mtu bila kutarajia kitu kutoka kwake, bila kujali mtu huyo ni mwema au mbaya, bila kujali ni wakati mzuri au mbaya, bila kujali ni wakati wa matatizo au raha upendo huu unabaki vilevile na haubadilishwi na matukio, Mungu anapoamuru kupendana au kumpenda Yeye katika maandiko anamaanisha upendo huu wa Agape.

Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote
Katika Mathayo 22:34-40 Mwanasheria wa kifarisayo alimuuliza Yesu swali la muhimu sana ingawa ni kwa kusudi la kumjaribu, kusudi lao kuu sio kujua Yesu anajua nini lakini wapate kuhukumu kuwa atasema nini kuhusu swala la kumpenda Mungu, Mafarisayo walijifikiri kuwa wao wanampenda Mungu na kuwa wanashika amri za Mungu huenda kuliko hata adui zao Masadukayo ambao Yesu alikuwa ametoka kuzungumza nao punde na kuwashinda kwa hoja jambo ambalo mafarisayo walilifurahia upeo na wakajifikiri kuwa wao ni wenye haki kwakuwa imani yao inafanana na ile ya Kristo, Hata hivyo katika jibu hili la Kristo ujuzi wake na ufahamu wake ulikuwa tofauti na mafarisayo wanavyo fikiri ukitafakari kwa kina kuhusu Majibu ya Yesu kila mmoja atajiona kuwa bado kuna upungufu katika ukiri wake kuwa anampenda Mungu
Unapoangalia maana ya upendo wa Agape kwa Mungu na mkazo wa Yesu, kuhusu kumpenda Mungu kwa Moyo na kwa roho na kwa akili au kwa nguvu hii ina maana wazi kabisa ya kuwa upendo wetu kwa Mungu unapaswa kuwa upendo wa kweli na wa dhati, haupaswi kuwa upendo wa mdomoni tu bali unapaswa kuwa wa kivitendo
1.       Kumpenda kwa moyo wetu wote kunamaanisha kuwa tuwe tayari kumfanya yeye kuwa namba moja, kumjali na kumuwaza yeye kuliko jambo lingine kuwa tayari yamkini hata kupoteza kila kitu cha thamani tulichonacho kwaajili yake, mafarisayo ukweli ni kuwa walikuwa wakijifikiri kuwa wana haki na wanampenda sana Mungu lakini Yesu alikuwa anawaona kama watu waliojaa ubinafsi na ambao hawakuwa tayari kuachia kila walichonacho kwaajili ya wengine ili kumfuata Mungu, Ibrahimu alikuwa tayari kumtoa mwanae wa Pekee Isaka kwaajili ya kumtii Mungu, lakini nani katika binadamu anaweza kufanya tukio hilo labda washirikina peke yao wanaotafuta utajiri kwa shetani, Kumpenda Mungu kwa moyo ni kuwa tayari kuendelea kuambatana na Mungu hata kama kwa kufanya hivyo tunaweza kupata hasara kubwa sana, unaendelea kushikamamana na Mungu tu awe amaekujibu maombi au hajakujibu moyo wako uambatane naye
2.       Kumpenda Mungu kwa roho yako, hii biblia inazungumzia upendo ambao uko tayari kufa kutoa roho yako kwaajili ya Mungu wako, hili sio swala Jespesi kwa Mafarisayo, wayahudi na hata wakristo, ni baadhi tu ya waislamu wachache ambao wanauwezo wa kujitoa muhanga na kupoteza roho zao kwaajili ya Mungu, wako pia mashujaa wachache wa imani ambao wameweza kufanya ahivyo, Kumpenda Mungu kwa roho yako yote maana yake ni kuwa tayari kuachilia kila kitu hata kama itagharimu uhai wetu kwaajili yake.
3.       Kumpenda Mungu kwa akili zako zote, kwa kiingereza tunaweza kusema to submit the intellect to his will, ni kuwa tayari kumpenda yeye na sheria zake zote, na kuamua lolote katika mapezni yake bila kutumia akili zetu, kukubali kufuata muongozo wake na kutokutenda lolote bila kumuuliza Yeye, daudi hakufanya lolote bila kuuliza kutoka kwa Bwana, huku ni kujitoa kwa hiyari kiasi cha kukosa maamuzi yako na kufuata maamuzi ya Mungu hii ni sadaka ya hali ya juu
4.       Kwa nguvu zako zote kama inavyoainishwa katika Marko hii humaanisha kwa roho yako na kwa mwili wako kuwa tayari kumtumikia na hata kuvumilia kwaajili ya utukufu wake kwa gharama yoyote.

Yesu anapozungumzia swala la Kumpenda Mungu anazungumzia hali ya kuendelea kumtegemea na kumtumikia Mungu bila kujali anatufanyia nini au hajatufanyia nini, Mungu anabaki kuwa Mungu, awe amejibu maombi yetu awe ajajibu, awe ametupa mume au hajatupa, awe ametupamnyumba awe hajatupa, awe ametupa gari ,awe hajatupa, awe ametuponya magonjwa yetu awe ahajatuponya, awe ametupandiah cheo au hajatupandisha, awe ametupa utajiri , au umasikini, awe ametupa chakula au njaa, awe ametuokoa na mateso au hajatuokoa, awe amenipa watoto au ameninyima, awe ameniulia kipenzi change, au amemponnya, awe ametupa maadui au hajatupa, awe ametupa ushindi au tumeshindwa, awe ametuokoka au hajatuokoa, awe ametupa au maketupokonya lazima Mungu abaki kuwa Mungu na ni lazima upendo wetu uendelee kuwepo kwake huu ndio upendo wa agape, Upendo wetu kwa Mungu unapaswa kuendelea kuwepo kwa vile ametupa zawadi ya wokovu, Mungu anatarajia tutampenda tu na hakuna sababu ya kutokumpenda.Upendo wetu kwake lazima uendane na ukweli kuwa yeye mwenyewe alitupenda upeo kiasi ambacho  alimtoa mwana wake wa pekee Yesu kufa kwaajili yetu Yohana 3:16, upendo wetu lazima ubebe imani kwake na kuonyesha kuwa tunamtegemea katika hali zote ziwe njema ama mbaya, upendo wetu kwake haupaswi kuwa na masharti, kama yeye mwenyewe alivyotupenda upeo bila sababu, uhusiano wetu na Mungu ni wa Muhimu kiasi kwamba hauwezi kutenganishwa na jambo lolote, lazima tukubali kuikataa dunia kwa gharama yoyote, ukweli wa upendo wetu kwa Mungu utadhihirika kwa matukio ya kuwa tayari hata kufa kwaajili yake inakuwaje kama yesu alikuwa tayari kufa kwaajili yetu? Sisi je hatuwezi kuwa tayari kufa kwaajili yake? Huku ndio iujitoa kwa ngazi ya juu zaidi kwa Mungu Warumi 12:1-2, 1Wakoritho 6:20, 10:31 2Wakoritho 9:15, Efeso 4:30, 5:1-2 Wakolosai 3:12-17.

Mpende jirani yako kama nafsi yako.

Yesu katika kujibu swali la farisayo tunajua wazi kuwa alinukuu Torati 6:4-5 na katika andiko hilo hakuna agizo la Mpende jirani yako kama nafsi yako, Yesu alikuwa ameliongeza jambo hilo kwa makusudi maalumu, kuhusu Mafarisayo kumpenda Mungu swala hilo halikuwa na na mjadala wengi walijitahidi kushika sheria ya Mungu tangu utoto wao, lakini ukweli ni kuwa kumpenda Mungu hakungeweza kukamilika kama hakuna kumpenda Mwanadamu mwenzako kama nafsi yako, watu wengi leo wanakiri kuwa wanampenda Mungu, lakini hawako tayari kuona maisha yaw engine yakiwa kama yao, ubinafsi na uchoyo vimewajaa kiasi ambacho wao hujiweka daraja la juuu kabisa na hawafurahii wengine kuwa kama wao, au kuwafanania, yesu aliwakumbusha Mafarisayo na sisi kuwapenda wenzetu kama nafsi zetu,

Warumi 13: 8-10Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani; na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria”.

Mafundisho ya mitume yanaungana na majibu ya Yesu kuhusu kuwapenda wenzetu kama nafsi zetu,watoto wote wa Mungu wanapaswa kuwapenda watu kwa upendo wa agape, hali hiii ya kupenda ni lazima ipite mipaka na kufikia kiwango cha kuwapenda hata wasiopendeka Biblia inatutaka kuwapenda maadui Mathayo 5:43-15. “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki

Biblia inatufunulia wazi kuwa ni Daudi, Yesu na Stefano amabo waliweza kufikia kiwango hiki cha kuwapenda na hata kuwaombea adui zao, Mafarisayo waliwachukia adui zao, lakini pia walijawa na ubinafsi kiasi ambacho wasingeliweza kwa vyovyote vile kusema wanampenda mungu katika hali ya kuwa ni wabinafsi na wenye choyo.

Na mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote

Hakuna maoni: