Jumatatu, 3 Julai 2017

Huyu ndiye Niliyekuambia habari zake!



1 Samuel 9:15-17. “Biblia inasema “Basi Bwana alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema,  Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikilia. Hata Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, HUYU NDIYE NILIYEKUAMBIA HABARI ZAKE; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu.”

 Sauli alikuwa Mfalme wa Kwanza wa Israel na Yuda, alitawala mnamo karne ya 11 hivi kabla ya Kristo akitokea kabila la Benjamin ingawa Baadaye Ufalme wake ulisitishwa na kurejea katika kabila la Yuda, kutokana na uchaguzi wa Mungu kumleta Masihi kupitia kabila hilo.

Utangulizi:

Kitabu cha Samuel ni kitabu cha mpito, ni kitabu kinachoonyesha jinsi wana wa Israel walivyodai kuwa na uongozi wa kifalme, kutoka kuwa na viongozi waamuzi ambao walikuwa ni wawakilishi wa Mungu katika kuongoza Israel, Mungu alikuwa akiwatumia viongozi hao kwa kuwajaza Roho wake Mtakatifu na wakamwakilisha Mungu kama mfalme mkuu hata wakati wa Nabii Samuel, Hata hivyo wana wa Israel waligomea aina hii ya uongozi na walimuomba Samuel awapatie Mfalme,

1Samuel 9:4-8Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama; wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote. Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba Bwana.  Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao. Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe.  swala hili lilikuwa baya machoni pa samuel na machoni kwa Mungu, Hata hivyo Mungu alimwambia Samuel awakubalie na kisha Mungu aliwamwambia Samuel habari za huyo mfalme waliemuhitaji.”

Maandalizi ya Heshima Kubwa.

Baada ya Ushauri huu wa Mungu ni wazi kuwa Samuel aliomba kwaajili ya Mfalme na Mungu alikuwa amemfunulia majira na muda ambao Mfalme huyu angekuja, kwa sababu hiyo Samuel akiwa na mtazamo kuhusu Mfalme aliandaa karamu kubwa sana naya Muhimu sana pia alialika watu wapatao 30 ambao walikuwa wastahiki, bila shaka walikuwa ni wazee muhimu sana katika Israel,aidha Samuel aliandaa Ngombe aliyenona 1Samuel 9: 22-24 “Naye Samweli akamtwaa Sauli na mtumishi wake, akawaleta ndani sebuleni, akawaketisha mahali pa heshima kati ya watu walioalikwa, nao jumla yao walikuwa kama watu thelathini. Samweli akamwambia mpishi, Lete ile sehemu niliyokupa, hiyo niliyokuambia, Iweke akiba. Basi mpishi akatwaa paja, na nyama iliyokuwa juu yake, akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, Iliyowekwa akiba ndiyo hiyo! Iweke mbele yako ule, kwa sababu umewekewa hiyo wewe hata wakati uliokusudiwa, maana nalisema, Nimewaalika watu. Basi Sauli akala pamoja na Samweli siku hiyo”. Hebu jaribu kuwaza Pale Mungu anapokuwa amekujulisha kuwa kiongozi wa Nchi atakuja kwako kwa muda Fulani, ukweli utajiandaa na kumuandalia kwa heshima kubwa sana ndivyo ilivyokuwa kwa Samuel ingawa alikuwa Nabii na mwamuzi lakini alimuandalia kiongozi mpya ajaye maandalizi ya Heshima kubwa sana.

Mungu anamleta Mfalme.

Katika namna ya Kushangaza sana Mungu anamleta Mfalme, lakini ili mfalme afike kwa Nabii Samuel Mungu anasababisha tukio la kupotea kwa Punda ambalo linawapelekea Mzee kishi kumtuma kijana wake Sauli na mtumishi wake na hivyo kuwa na mwendo wa siku tatu kwaajili ya kuwatafuta Punda na hatimaye anakutana na Nabii Samuel 1Samuel 9:1-10, Basi, kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu. Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote. Na punda za Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kishi akamwambia Sauli mwanawe, Haya basi, twaa mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, uende ukawatafute punda hao. Naye akapita kati ya nchi ya milima milima ya Efraimu, akapita na kati ya nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona; kisha wakapita kati ya nchi ya Shaalimu, wala huko hawakuwako; wakapita kati ya nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwapata. Hata walipofika nchi ya Sufu, Sauli akamwambia yule mtumishi aliyefuatana naye, Haya, na turudi, baba yangu asije akaacha kufikiri habari za punda akatufikiri sisi. Naye akamwambia, Tazama, katika mji huu mna mtu wa Mungu, naye ni mtu mwenye kuheshimiwa; yote asemayo hutukia kweli kweli; basi, twende huko; labda yeye aweza kutuambia habari ya safari yetu tunayoiendea. Ndipo Sauli akamwambia mtumishi wake, Lakini angalia, kama tukienda, tumpelekee mtu huyo kitu gani? Maana chakula kimekwisha vyomboni mwetu, wala hapana zawadi ya kumpelekea mtu wa Mungu; tuna nini sisi? Yule mtumishi akamjibu Sauli, akasema, Tazama, mkononi mwangu nina robo ya shekeli ya fedha; nitampa huyo mtu wa Mungu fedha hiyo, atuambie njia yetu. (Hapo zamani katika Israeli, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa Mwonaji.) Basi Sauli akamwambia mtumishi wake, Umesema vema; haya! Twende. Wakaenda mpaka mji ule aliokuwamo mtu wa Mungu.”

Huyu ndiye Niliyekuambia habari zake!

Katika kisa hiki tunajifunza wazi jinsi Mungu anavyotenda kazi kwa viwango tofauti na mitazamo ya kibinadamu, hii ni wazi kuwa Mungu ndiye anayechagua viongozi, Mungu anapochagua kiongozi na anapochagua kumrehemu mtu sio lazima mtu huyo awe ana fiti katika mitazamo yetu ya kibinadamu, Wakati mwingine Mungu hufanya kazi kinyume na mitazamo tuliyo nayo, angalia kwamba Sauli na mtumishi wake wanapita katika mapori wakitafuta punda siku tatunzinapita huenda walikuwa hawajachana nyele zao, au kuoga, wala kupaka mafuta na chakula kilikuwa kimewaishia lakini Mungu kupitia Nabii Samuel alikuwa amemuandalia Heshjima kubwa na Mambo yaliyotamanika katika Israel . Sauli alipoambiwa alisema mimi ni nani na kabila yangu na familia yangu vyote vilikuwa vidogo,

Mungu huwatumia watu wanyenyekevu na waliodharaulika katika jamii, watu ambao katika mitazamo yetu wanweza kuwa hawafai

Mungu anayo mamlaka ya kuchagua na hakuna mwanadamu anaweza kumuuliza Kwanini, wala jitihada za kibinadamu hazina nyongeza katika kusababisha akuchague, awaye yote ambaye anajibidiisha kibinadamu kwa kusudi la kutafuta sifa kwa Mungu amekataliwa, Mungu huwapinga wajikwezao bali huwapa Neema wanyenyekevu ni ukweli ulio wazi kuwa Sauli alipoambiwa habari hizi alijiona hastahili 1Samuel 9: 21Basi Sauli akajibu, akasema, Je! Mimi si Mbenyamini, mtu wa kabila iliyo ndogo kuliko kabila zote za Israeli? Na jamaa yangu nayo si ndogo kuliko jamaa zote za kabila ya Benyamini? Kwa nini basi, kuniambia hivyo?” Sauli alijiona Duni moyoni mwake alijiona hafai lakini Mungu alikuwa amemkusudia Mema ili awatawale watu wake Israel, namna tunavyojitazama na hata namna watu wanavyotutazama sio Mungu alivyotutazama Mungu anatuangalia kwa jicho la tofauti anataka atukuzwe kupitia udhaifu wetu, sio lazima udhaifu huu umaanisha dhambi, lakini hata kama udhaifu huo ni dhambi yeye ndiye atutakasaye hivyo mtu awaye yote asijisifu kwa Matendo yake bali tuheshimu uamuzi wa Mungu wa kuchagua

Warumi 9 :11-18 11. “(kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye),    aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo. Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia. Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha! Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote. Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu.” 

Kila ambaye Mungu memchagua na atembee kwa ujasiri akimtemgemea Mungu na kufahamu kuwa yeye tunayemtumikia sio Mnyonge hata kidogo atakamilisha kile anachokikusudia katika mioyo yetu, kamwe hatupaswi kukata tamaa.
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni: