Andiko la Msingi: Daniel 3: 1-6
Uwapo katika Mateso makubwa mno Mungu huwa Karibu mno mwamini tu hata kama sio rahisi !
“Nebukadreza, mfalme, alifanya sanamu ya dhahabu, ambayo urefu
wake ulikuwa ni dhiraa sitini, na upana wake dhiraa sita; akaisimamisha katika
uwanda wa Dura, katika wilaya ya Babeli. Ndipo Nebukadreza akatuma watu
kuwakusanya maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na
mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, ili wahudhurie wakati wa
kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadneza aliyoisimamisha. Ndipo maamiri, na
manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili,
na wakuu wa wilaya zote, wakakusanyika ili kuizindua ile sanamu, mfalme
Nebukadreza aliyoisimamisha; wakasimama mbele ya ile sanamu, mfalme Nebukadreza
aliyoisimamisha. Ndipo mpiga mbiu akapiga kelele akisema, Enyi watu wa kabila
zote, na taifa, na lugha, mmeamriwa hivi, wakati mtakapoisikia sauti ya panda,
na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma,
lazima kuanguka na kuiabudu sanamu ya dhahabu, mfalme Nebukadreza
aliyoisimamisha.Na kila mtu
asiyeanguka na kuabudu atatupwa saa iyo hiyo katika tanuru ya moto uwakao”.
Utangulizi:
Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke
siku zake za kuishi si nyingi nazo zimejaa taabu alisema Mtumishi wa Mungu
Ayubu katika Ayubu 14:1,
maneno haya yanabakia kuwa kweli katika maisha ya wanadamu wote bila kujali
anatokea katika tabaka gani, Lakini pamoja na dhiki na magumu tunayokutana nayo
Neno la Mungu linaendelea kututia moyo kumuamini Mungu bila kukata tamaa,
kuendelea kumuamini tu hata kama sio rahisi.
Kisa cha Shadrak,Meshak na
Abednego katika Biblia kinaweza kutufundisha kitu kikubwa na cha ziada katika
maisha yetu,hususani katika nyakati za leo,Vijana hawa watatuwaliweza kupingana
na amri kali ya mfalme Nebukadneza na hatimaye kutupwa katika tanuru la
moto,kisa chao kimekuwa kina mvuto mkubwa sana kwa vijana na wazee kwakarne
nyingi sana, ukweli tendo lao laujasiri linatufundisha sote yunaomwamini Mungu
kuwa na imani kali sana yenye kushangaza hata katika nyakati za Leo. tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
- Kukataa ibada ya sanamu
- Mambo ya kujifunza
- Matokeo ya Imani yao.
Kukataa ibada ya sanamu.
Kisa cha vijana hawa ambao
walijitunza sana imani yao katika Mungu kinaanza kwa kukataa kuabudu sanamu,Bibliai
meagiza kwamba IKIMBIENI IBADA YA SANAMU 1Wakoritho 10:14 “Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.”
Kwa ujuzi usiokuwa wa kawaida wa neno la Mungu na utii wa hali ya juu kwa
Mungu vijana hawa walikataa amri ya mfalme huyu mwenye nguvu, na walikataa
kuitumikia au kuiabudu miungu yakeya dhahabu na lisanamu ambalo alikuwa
amelisimamisha,huku akitangaza kuwa adhabu ya mtu atakayepingana naye ni kifo
tu.
Maneno yao ni yenye kutia moyo
sana angalia na ulikuwani ukweli wenye
kuumiza Daniel 3:15-18 “Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya
panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za
ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali
msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani
Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu? Ndipo Shadraka, na Meshaki, na
Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu
katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na
tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si
hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala
kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
Mambo
ya kujifunza kutoka kwao.
Imani ya Shedrack, Meshack na
Abednego ni yenye kushangaza sana inafunua maswalamuhimu sana ya kujifunza
kutoka kwao.
1. Tegemeo lao lilikuwa kwa Mungu mmoja wa
kweli mwenye nguvu ya kuwaokoa na hasira za Mfalme, walimuamini Mungu kuwa
anaweza kuwaokoa na kila hila iliyokuwa mbele yao. Waliamini kuwa Mungu huwa
anaokoa watu katika mapito mbali mbali, lakini pia walijua sio mara zote
anaweza kufanya hivyo, hata hivyo katika namna ya kushangaza sana na isiyo
rahisi waliamini kuwa hata kama sivyo,hawako tayari kuabudu miungu Jambo hili
lilileta Baraka kubwa sana Biblia inasema amelaaniwa amtegemeaye mwanadamu
amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Yeremia
17:5-7 “Bwana
asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa
kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani,
Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya
chumvi isiyokaliwa na watu.Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye
Bwana ni tumaini lake” Vijana hawa walijifungulia Baraka kubwa sana
kwa sababu walimtegemea Bwana walijikinga kwa Bwana Mungu wao. Tunaweza wakati
mwingine tusijue sababu ya majaribu yanayotupata lakini Mungu anataka tumwamini
yeye hata kama sio rahisi.
2. Shadrack
Meshack na Abednego walikuwa na imani
isiyotikisika,Biblia inatufundisha kuwa mwenye haki ataishi kwa imani
akisitasita roho yangu haina furaha naye, pia biblia inasema tendololote
lisilotokana na imani ni dhambi,kwa sababu hiyo ni lazima tumuamini Mungu hata
kama jaribu lililoko mbele yetu limeruhusiwa na Mungu Ayubu 13: 15-16. “Tazama, ataniua; sina tumaini; ila hata hivyonitaithibitisha
njia yangu mbele yake.Hili nalo litakuwa ni wokovu wangu; Kwani asiyemcha Mungu
hatakaribia mbele yake” tunajifunza kuwa njia njema na bora ni
kumkaribia Mungu hata kama tutahisi ni Mungu ametruhusu jaribu hilo, Ayubu
anasema hata kama atanichinja au ataniua bado nitamthibitishia kuwa ninamwamini
yeye
3. Usimsujudie
wala kumuogopa mwanadamu Nebukadreza alikuwa ni mfalme mwenye nguvu
kubwa duniani mataifa yote na watu wote na kabila zote walimuogopa kwa sababu
ya mafanikio makubwa na uchumi mkubwa aliokuwa nao aliweza kutumia nguvu yake
kuwatisha vijana hao ili waiache imani yao kwa Mungu, lakini wao hawakukubali
kutii waneitii sauti yake wanekuwa wamemtii shetani lakini pia wameabudu
Mwanadamu,kwa Sababu hiyo Shadrack Meshack na Abednego walikuwa tayari kwamba
hata kama wangepitia Magumu na mateso ya kutisha na maumivu mabaya sana ya
kuingizwa katika tanuru lamoto, walikataa kumuacha Mungu na kuabudu miungu,
Yesu anatilia mkazo wazo hili katika Mathayo
10:28 “Biblia
inasema Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni
yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.” Kwa
kawaida wanadamu wakiisha kufanikiwa kwa sababu mbalimbali za kielimu,
kiuchumi, na hekima wengi hujisahau na kuwa na kiburi, wanasahau kuwa ni Mungu
ndiye aliyewabariki, wamamuacha Mungu na kuwataka watu waabudu mali zao,
waabudu akili zao na mafanikio yao, wakati mwingine ni vigumu kupata somo
lakujifunza kutoka kwa waliofanikiwa na ni rahisi kupata somo kutoka kwa
walioshindwa, watu, taifa au kiongozi akiwa na nguvu tayari huacha kumtegemea
Mungu na kutaka watu wamuabudu yeye na uwezo wake na akili yake, ni rahisi
kuona watu wenye uwezo wakinyanyasa wengine, na kuweka madaraja Biblia inatia
moyo kumtii Mungu na kutokuabudu wanadamu.
Matokeo ya Imani yao.
1. Moto haukuwaunguza kabisa Mungu aligeuza
tanuru la moto kuwa bichi kwa Shedrack Meshack na Abednego kila
anayemtumaini Bwana ni lazima aelewe kuwa Mungu anaweza kutumia majaribu kama mlango
wa kukupeleka kwenye hatua nyingine, adui anaweza kufurahi kuingia kwako
majaribuni na matatani lakini Mungu aweza kutumia majaribu kama njia ya
kukuletea faraja ya kweli.
2. Waliowatupa katika moto ndio waliokufa Daniel 3:19-23
“Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake
ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri watie
moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru
baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na
Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Basi watu hao
wakafungwa, hali wamevaa suruali zao, na kanzu zao, na joho zao, na mavazi yao
mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Basi kwa
sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na ile tanuru ilikuwa ina moto sana,
mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na
Abednego. Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka,
hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru iliyokuwa inawaka moto”
Wako watu ambao
ukiwatupa ni kama unajiangusha mwenyewe,Mungu akupe neema kwamba adui zako
wanaokuchukia wawe wamejichukia wenyewe, waliokuchoka wawe wamejichoka
wenyewe,ni ajabu kuwa wana wa Israel walimkataa ndugu yao Yusufu, kumbe
walikuwa wakimfukuza waziri wa chakula na ingewalazimu kumsujudia ili wale,
Mungu akupake mafuta ili kwamba wanaokutaaa wafilisike, wapaytwe na njaa
wakukumbuke wakulilie wakujutie, Mungu na autume moto kuunguza adui zako.
Badala yako.
3.
Walitupwa
wakiwa wamefungwa lakini walikuwa wakitembea wakiwa wamefunguliwa, shetani
na maadui wa Mungu wanaweza kudhani kuwa, wamekufunga lakini katika namna ya
kushangaza wamekufungua, wako watu wanaodhani ukiwa katika himaya yao ndio
umefikia kiwango cha juu cha furaha na kuwa wakikuondoa wanakuhuzunisha jicho la Mungu linaona tofauti kuwa ulikuwa
kifungoniwala hukuwa na furaha lakini na sasa anakuweka huru, Matokeo ya imani
ya vijana hawa ni kuwa kamba walizofungwa ziliwaachia,na sio hivyo tu moto
mkali uliochochewa kuwaunguza haukuwadhuru
Isaya 43:2 “Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee
Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa;
nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa
pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto,
hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza”
4.
Walitupwa peke yao lakini Mungu alijiunga nao,
Daniel 3:23-25 “Na watu hao watatu, Shadraka, na
Meshaki, na Abednego, wakaanguka, hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru
iliyokuwa inawaka moto. Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka;
akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa,
katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu,
akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati
ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu”.
Watu wanaweza kudhani ya kuwa
wanakutupa wewe kumbe wanamtupa Mungu, Ni jambo la kushangaza sana kuwa Mwana
wa Mungu alijiunga na vijana hao nilikuwa najiuliza maswali mengi sana kama
mkuu wa wajenzi najua kabisa Mungu angeweza kufanya muujiza huu akiwa mbinguni
hata bila ya kuonekana kwa umbile na bado ingeashiria kuwa Mungu amewaokoa
lakini swali langu kubwa ilikuwa kwanini ajionyeshe? Mungu alikuwa
anajidhihirisha kuwa yeye ni Mungu aliye hai, na kuwa uhai wa binadamu uko
mikononi mwake na kuwa yuko pamoja na watu wakehata pale wanapoona kuwa hali ni
tete na kuwa mambo hayawezekani yeye anaonyesha wazi kwamba tuamini tu hata
kama sio rahisi, yeye ataingilia kati,ndoa yako hata kama inaonekana kuwa sio
rahisi,Yeye ataingilia kati, hata kama mtihani uliopita unaonekana kuwa
ulifelikwa kiwango kikubwa na kuwa kwa muda uliobaki ni kama haiwezekani, kupata
matokeao mazuri biblia inataka uamini tu
hata kama sio rahisi, watu wamekukatia tamaa kuwa kwa ugonjwa ulionao
utakufa na hutapona nasema leo amini tu hata kama sio rahisi, umekata tamaa juu
ya mabadiliko ya tabia mbaya za watoto wako na inaonekana kama haiwezekani
wakapona nataka nikuambia amini tu hata kama sio rahisi, vijana wameharibika na
madawa ya kulevya na inaonekana kama ni vigumu kuacha kuwa teja mwamini Mungu
tu hata kama sio rahisi, wamesema mirija yako imeziba na kuwa huwezi kuzaa tena
mimi nasema amini tu hata kama sio rahisi, wamesema ukoo wenu nyinyi ndio basi
hamuwezi kufanikiwa hamwezi kutoka nakuambia leo katika jina la Yesu amini tu
hata kama sio rahisi, unasumbuliwa na ukimwi, kisukari, kansa,magonjwa ya
zinaa, matatizo sugu ya kifamilia na watu wanadhani kuwa wewe ndio baaasi
nakuhakikishia amini tu hata kama sio rahisi, ni majini na mapepo
yanakusumbua,umepitia kila aina ya maombezi na inaonekana hujapata ufumbuzi
nakuhakikishia amini tu hata kama sio rahisi, Haikuwa jambo rahisi kukataa
amri ya mfalme laki vijana hawa waliamini tu hata kama ahaikuwa rahisi Yesu
aliahidi kuwa anatakuwa pamoja nasi hata ukamilifu wa dahari Mathayo 28:20,
aliahidi kuwa atatutia nguvu Zaburi 55:22, Psalm 147:6 na aliahidi kuwa
atatuokoa kabisa hata milele Mathayo 25:41,46
5.
Shadrack
Meshack na Abednego walimbadilisha mbadilishaji ( they changed the Changer)
Kutokana na
kiburi chake Nebukadneza alitaka sana kuwabadilisha vijana hawa mwanzoni kabisa
alipowateka vijana hawa wa Kiebrania aliwafundisha Lugha yake, ya kikaldayo,
alibadilisha kuvaa kwao na alibadilisha majina yao Kiibrania Daniel maana yake
Yehova ni mwamuzi wangu alimbadilisha na
kumuita Belteshaza yaani anayependwa na Beli, yaani mungu wa wababiloni, Hannaniah
anayependwa na Yehova, akamuita Shadrak maana yake aliye kama Venus na Azaria
maana yake Yehova ni msaada wangu alimuita Abed nego yaani mtumishi wa Nego,
Nebukadreza alifanya hivi kwa makusudi ya kisaikolojia na kidini, Nebukadreza
alifikiri kwa akili zake anaweza kuwabadilisha watu, kupitia imani ya vijana
hawa tunajifunza kuwa mwenye uwezo wa kubadilisha watu ni Mungu tu na kuwa watu
wa Mungu wakiishi kwa imani wanaweza kuwabadilisha wale wanaofikri
kuwabadilisham, kamwe Hatuwezi kuubadili ulimwengu kwa kuwa kama walimwengu
bali tunaweza kuubadili ulimwengu kwa kuwa kinyume na ulimwengu imani ya vijana hawa ilimfanya aliyekuwa na bidii ya
kuwabadilisha abadilike yeye, Daniel 3:
26-30. “Kisha Nebukadreza akaukaribia mdomo wa ile
tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na
Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na
Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto. Na maamiri, na manaibu, na
maliwali, na mawaziri, waliokuwa wamekusanyika pamoja, wakawaona watu hao, ya
kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala nywele za vichwa vyao
hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala harufu ya moto haikuwapata
hata kidogo. Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na
Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake
waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili
wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe. Basi mimi naweka amri ya kuwa kila
kabila ya watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lo lote
lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa
vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine
awezaye kuokoa namna hii. Kisha mfalme akawakuza Shadraka, na Meshaki, na
Abednego, katika wilaya ya Babeli” Ni Mungu pekee ndiye mwenye uwezo wa
kuwabadilisha watu, hata kama watu hao wamesema hawawezi kuokoka hawawezi
kubadilika wameshindikana kwa Mungu yote yanawezekana dakika chache tu mfalme
alikuwa amekasirikia watu wanaomuabudu Mungu aliye hai na ni dakika chache tu
anamhimidi Mungu wa kweli.
Amini tu hata
kama sio rahisi
Rev. Innocent
Kamote
Mkuu wa Wajenzi
mwenye hekima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni