Ijumaa, 2 Machi 2018

Mariam mama yake Bwana Yesu!




Mstari wa Msingi: Luka 1:26-33Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu.  Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho
 

 


Maana ya jina Mariam.

Jina Mariam au Maria limetokana na jina la Kiyunani Maria na kwa kiaram Maria, kwa kiibrania Miriam kwa kiarabu Maryam ni Jina maarufu sana katika maandiko ya Kikristo na Kiislamu, Mariam ni mwanamke anayesadikiwa kuwa alibarikiwa sana kutokana na kupata neema ya Kumzaa mwokozi wa Ulimwengu yaani Bwana Yesu Kristo (Masihi). Jina hili Mariam maana yake ni mtumishi wa Mungu!

Mariam anatajwa kama mwanamke aliyekuwa mwanamwali yaani Bikira aliyekuwa anakaribia kuolewa au aliyekuwa amechumbiwa anasifiwa kwa sifa kubwa ya kuwa mwanamke mwaminifu aliyejitunza na mnyenyekevu aliyekuwa na uelewa wa juu sana kuhusu Neno la Mungu na Mapenzi ya Mungu. Mwanamke huyu alikuwa na asili ya ukoo wa Daudi ingawa aliishi Galilaya katika mji mdogo wa Nazareth kama yanenavyo maandiko yaani Agano jipya na Quran

Mwanamke huyu shujaa anatwaja na maandiko yote agano jipya na Quran kwamba alikuwa Bikira na alikuwa amebakiza muda tu wa kufungishwa ndoa kwa Yusufu ambaye naye pia alikuwa wa ukoo wa Mfalme Daudi, Bikira wa aina hii aliitwa PARTHENOS kwa kiyuinani yaani mwana mwali, aliyekuwa tayari kwa kutimiza tu ibada ya ndoa, alionekana kuwa ana mimba ni mimba ambayo vitabu vitakatifu vinaeleza wazi kuwa haikutokana na uashetari wala mbegu za kiume za mwanamume awaye yote, bali zilitokana na muujiza wa kiungu sawasawa na jinsi alivyotabiri nabii Isaya “TAZAMA BIKIRA ATACHUKUA MIMBA NAYE ATAZAA MWANA WA KIUME NAYE WATAMUITA JINA LAKE IMANUEL YAANI MUNGU PAMOJA NASI” 

Isaya 7:14Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.”

Tukio hili halikuweza kumuumiza Yusufu kwa vile alikuwa na uelewa mpana wa Mapenzi ya Mungu aidha malaika wa bwana mjumbe wa Mungu Gabriel alimtokea na kumpa ufafanuzi kuhusu ujauzito huo, ni kutokana na hali hii Mariam aliambatana na Yusufu mpaka Bethelehemu kwaajili ya kuhesabiwa kutokana na amri ya Kaisari Augusto kwamba wahesabiwe watu wa utawala wake kila mmoja kwao na kwa vile Yusufu na Mariamu kwa asili ni watu wa Bethelehemu huko Uyahudi walikwenda huko ili wahesabiwe na kwa bahati nzuri Masihi alizaliwa huko, ili kutimiza Unabii wa Mika katika Mika 5:2 kwamba “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.

Mwanamke huyu maarufu anatajwa kama mara 50 hivi katika injili, Quran imempa Sura maalumu iitwayo Surat al  Maryam  na inasemekana Quran inamtaja mara nyingi zaidi kama mwanamke mtakatifu katika Quran Maryam ametajwa mara 70

Mariam alitokewa Malaika Gabriel na kuelezwa rasmi kuwa amechaguliwa na Mungu kuwa mama wa Masihi, ni mwanamke mwenye uwezo mkubwa sana wa kuvumilia kwani licha ya kuwa na mtoto mwema mno kama Yesu injili imethibitisha kuwa alikuwepo wakati mwanae anasulubiwa na kuuawa kwaajili ya dhambi za ulimwengu hili lilikuwa ni tukio chungu sana na lilihitaji kuyajua mapenzi ya Mungu hasa na kwa uwazi Mariamu huenda katika kipindi hiki alikumbuka maneno ya nabii mzee aliyeitwa simeon ambaye aliahidiwa na Mungu kuwa hatakufa mpaka atakapomuona Masihi mzee huyu alimweleza maneno mazito Mariamu kumuandaa tayari kwa machungu ya kusulubiwa kwa mwanae miaka michache ijayo. 

Luka 2:21-35Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba. Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema;  Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, TAZAMA, HUYU AMEWEKWA KWA KUANGUKA NA KUINUKA WENGI WALIO KATIKA ISRAELI, NA KUWA ISHARA ITAKAYONENEWA. NAWE MWENYEWE, UPANGA UTAINGIA MOYONI MWAKO, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.”

Mariamu hata baada ya kufufuka kwa Yesu alijiunga na wanafunzi wa kanisa la kwanza pale Yerusalem na maandiko yanamtaja kuwa aliungana katika maombi na wanafunzi na alikuwa miongozi mwa watu 120 waliojazwa Roho Mtakatifu japo kwa Mariamu huenda tukio hilo lilikuwa likijirudia kwa mara nyingine kwani Raoho wa Mungu alikuwa juu yake mapema zaidi ili aweze kukabidiwa jukumu la Kumbeba Bwana Yesu.

Kwa mujibu ya masimulizi ya kihistoria hasa ya wakatoliki na makanisa ya Othodox wanaamini kuwa mwili wake ulinyakuliwa Mbinguni moja kwa moja lakini swala hili linaitwa “Assumption” yaani inasadikiwa tu lakini hakuna uthibitisho wa moja kwa moja, Masimulizi mengine yanaeleza kuwa huenda alikuweko mpaka mwaka wa 70 AD wayahudi walipotawanywa na kupoteana na kutokuweko kwa uhakika kuwa ni wapi alifia, Mtume Yohana alipewa jukumu la kumlea Mariam lakini hata hivyo hajawahi kueleza lolote kuhusu Mwisho wake aidha baadhi ya wanawe kama Yuda aliyeandika waraka na Yakobo pia  ndugu zake bwana hawajawahi kueleza lolote kuhusu mama yao.
Mariamu anaheshimika na watu wengi sana na mamilioni ya watu wanaamini kuwa ni moja ya watakatifu muhimu sana katika dini, wengine wanaamini kuwa amewahi kuwatokea kimuujiza katika karne kadhaa, makanisa ya Othodox na Catholic na Anglican na Lutheran yanaamini kuwa kwa kuwa yesu ni Mungu na alizaliwa na Mariam basi Mariamu ni mama wa Mungu, baadhi ya mashirika ya kikatoliki kama Marian wao wanaamini na kumuita kuwa ni mama wa Mungu na wanaamini kuwa hata yeye kama ilivyo kwa yesu Kristo hakuwa na dhambi na kuwa alizaliwa pasipokuwa na dhambi, siwezi kusema lolote katika hili lakini ukweli ni kuwa Quran pia imemkubali sana Maryam na kuonyesha heshima kubwa sana juu yake akitetewa kuwa hakuwa na dhambi tofauti na mama wa Muhamad ambaye hatajwi kabisa katika kitabu hichi ukicha khadithi.

Pamoja na ubora wote huu kuhusu Mariamu na utakatifu wake kwetu sisi na kwangu mimi Mariamu ni mtakatifu kama walivyo watakatifu wote katika biblia, nakubali kuwa Yesu alimuheshimu sana mama yake lakini vilevile sisi nasi tunamuheshimu sana na kama mbingu zilivyomuheshimu sana kuwa ni Mtakatifu hilo hatuna mashaka nalo, kila mtu anaweza kuwa kama Mariamu tu kama tukiyashika maneno ya Mungu Yesu alisema “MAMA NA NDUGU ZANGU NI AKINA NANI? NI WALE WANAOLISIKIA NENO LA MUNGU NA KULISHIKA”  ni imani yangu pia kuwa furaha atakayokuwa nayo Mariamu inaweza kuwa furaha ya kila mmoja anayelisikia neno la Mungu na kulishika Yesu akasema  alipoulizwa ni furaha gani aliyonayo mwanamke aliyekuzaa na kukulea alijibu AMA NI FURAHA GANI WALIYONAYO WANAOLISIKIA NENO LA MUNGU NA KULITII” 

Katika kitabu cha matendo Mariamu anaonekana akiwa muombaji sawa na waombaji wengine kama Petro na wengineo, mariamu amebarikiwa hatuna shaka na hilo, Mariamu ytuko mbinguni kama watakatifu wengine hatuna shaka na hilo, Lakini Mariamu sio njia na kweli na uzima, yeye sio njia ya kumfikia Mungu aliye hai, yeye sio njia ya kutumika kutuombea kwa baba mbinguni, yeye sio mama wa Mungu, wala sio mke wa Mungu, yeye aliendelea kuwa mke wa Yusufu na alizaa watoto sita zaidi ukiacha Yesu mwanawe wa kwanza aliyemzaa kwa muujiza soma Mathayo 13:54-56Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si YAKOBO, NA YUSUFU, NA SIMONI, NA YUDA? Na MAUMBU  (Dada zake) yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote?”

Kama u mwanafunzi wa Biblia utaona wazi kuwa ndugu zake Yesu wametajwa katika Biblia Yakobo. Yusufu, Simoni na Yuda yaaninkaka wane na neno maumbu maana yeke dada zake ambao inakisiwa walikuwa wawili hivyo jumla ya wana wa Mariamu ni Saba na aliozaa na Yusufu ni sita, so kama Mariamu ni mama wa Mungu basi pia ni mama wa wanadamu! Kumbuka ni Yesu pekee ndie alikuwa mwana wa miujiza na yusufu aliendelea kuzaa na kufurahia maisha yake na Mariam inasadikiwa tu kuwa Yusufu alifariki mapema zaidi.

Wakati watu wanakazania kumuomba Mariamu ni muhimu kujikumbusha kuwa Mariamu alikuwa akimuomba Yesu pamoja na wanafunzi wake aliungana nao katika maombi Matendo ya Mitume 1:12-14Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato.Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo. Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.” Unaona Mariamu mama yake Yesu na ndugu zake walikuwa miongoni mwa watu waombaji waliokuwa wakimuomba Mungu kwa jina la Yesu, dhana inayojengwa na baadhi ya watu wanaotaka kupotoshja maandiko wakisema kuwa Mariamu ni muombezi wanajenga hoja kupitia muujiza wa kana ya Galilaya wakati Yesu alipohudhuria harusini na kisha watu wakatindikiwa na Divai, Mariamu alikuja kumuomba Yesu na kumpa taarifa ya kutoikuweko kwa Divai Yesu hakukubali kwa urahisi kwani mariamu alitaka Yesu atumie uwezo wake wa kimuuijiza kabla ya wakati wa Mungu, hata hivyo alimuomba kwa imani na kuwagiza wanafunzi wake kuwa atakalowaagiza walifanye dhana hii haitufundishi kumuomba mariamu aku kumfanya mariamu kuwa ni muombezi bali inatufundisha kuwa tukiwa na uhitaji wowote ni lazima tumweleze Bwana yesu kwa imani naye ataenda Yohana  2:1-9Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai. Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia. Mamaye akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambia, fanyeni. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji),” 

Ni muhimu kufahamu kuwa Yesu Kristo ni Mkuu kuliko Mariam, neema aliyopewa Mariamu ilikuwa ni kushiriki Baraka kubwa ya kumleta masihi Duniani, Lakini Mungu hajamfanya Mariamu kuwa mwombezi kwa sababu zozote zile Makuhani waombezi wote katika uyahudi walikuwa wanaume, Mariamu hakuwa nabii kama ilivyokuwa kwa Miriam wa agano la kale aliyekuwa Dada wa Musa na Haruni,  alikuwa ni mwanamke shujaa jasiri na mwenye imani katika kutunza neno na ahadi za Mungu, Mungu hajawahi kumfanya Mariamu kuwa malkia wa Mbinguni wala hajawahi kumfanya mariamu kuwa sehemu ya ibada, Mariam atasikitika sana kama atarudi duniani na kukuta akuombwa na kuabudiwa kama Mungu kwa unyenyekevu aliokuwa nao angeshangaa kukuta kufuru hii.

Njia pekee ya kumfikia Mungu ni Yesu naye ndiye kipatanisho pekee kati ya Mungu na wanadamu, 1Yohana 2:1-2Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.” 

Unapotumia Muda wako kumuomba Mungu kupitia Mariamu unapoteza lengo la maombi yako huku ukiwa na nia nzuri lakini sio ya kimaandiko ni vema dua zetu na maombi yetu tukamuombababa wa Mbinguni kwa njia ya mwanae Yesu Kristo pekee

Yohana 16:23-24Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa KWA JINA LANGU.  Hata sasa hamkuomba neno KWA JINA LANGU; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.”
 
Wengi hawana furaha hawajawahi nkufurahia uwepo wa Mungu na utendaji wa Mungu kwa sababu hawajawahi kuomba kwa jina la Yesu wamedanganywa na kudanganyika wakiomba kupitia majina mengine Yesu Mwenye yu ashauri hivi Yohana 14:13-14Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya”: ni jambo la kusikitisha sana katika Karne hii ya uwazi na ukweli yautafiti na ujuzi ya hekima na maarifa neno la mungu liko wazi kila mahali bado kuna watu wanatumia jina la Mariamu katika maombezi, ni malizie kwa kusema kuwa Roho Mtakatifu ndiye anayetuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.

Kama hujui kuomba ruhusu Roho Mtakatifu akufundisha kuomba maana yeye ndio muombezi mkuu na sio Mariamu Warumi 8:26-27 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.” 

Ni imani yangu kuwa utaifahamu kweli nayo itakuweka Huru katika jina la Yesu Kristo aliye hai amen!

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima       

Hakuna maoni: