Yohana 19:28-30 “Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha
kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu. Kulikuwako huko chombo
kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo,
wakampelekea kinywani. Basi Yesu
alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, IMEKWISHA. Akainama kichwa, akaisalimu
roho yake.”
Utangulizi:
Mojawapo kati ya usemi wenye maana sana
kati ya semi saba za Yesu alizozisema akiwa msalabani na ambazo zinatajwa
katika sehemu mbalimbali za injili, moja ya usemi huo wa muhimu ni usemi wa
sita wenye Neno IMEKWISHA ambalo leo katika siku ya pasaka tutachukua
muda kulijadili kwa undani na kupata maana iliyokusudiwa, maneno mengine kati
ya maneno saba aliyoyasema Yesu msalabani ni pamoja na:-
·
Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo Luka 23:34
·
Amin nakuambia leo hii utakuwa pamoja nani
peponi Luka 23:43
·
Mama tazama mwanao, mwana tazama mama yako Yohana 19:26-27
·
Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha Mathayo 27:46
·
Nina kiu Yohana
19:28
·
Imekwisha Yohana
19:30
·
Baba mikononi mwako naiweka roho yangu Luka 23:46
Maana
ya neno IMEKWISHA
Ni muhimu kufahamu kuwa Neno IMEKWISHA ambalo katika kiingereza kiingereza
linasomeka “IT IS FINISHED” katika Biblia ya kiyunani yaani Kigiriki
linasomeka kama “TETELESTAI” Neno hili ndio neno la Mwisho kabisa katika
maneno aliyoyatamka Yesu pale msalabani kabla ya kutamka neno “Baba mikononi
mwako naiweka roho yangu” na kufariki dunia pale msalabani, Neno hili Imekwisha
TETELESTAI limetokana na neno TELEO la kiyunani ambalo maana yake ni Kukamilisha
kazi, kumaliza kazi, kutimiza kazi, to complete or to accomplish, neno hili
lina umuhimu mkubwa kwa sababu linazungumzia kumaliza kazi kwa furaha, au kwa
mafanikio, utamu wa neno hili ni kama vile mtu anapokuwa amemaliza mtihani wa
mwisho katika kozi ya mwisho, au mtihani wa mwisho kabisa wa kumaliza shule au
chuo au kama vile mtu aliyekamilisha malipo ya mwisho ya ununuzi wa nyumba au
gari, (Paid in Full) au kukamilisha kwa usahihi kile ulichowaza au kufikiri kuwa utakifanya na
ukakifanya kwa usahihi kabisa, Kama vile Mungu alivyosema tazama kila kitu
kimekuwa chema, well done, kazi imefanyika kwa ufasaha.
Lakini ni muhimu kufahamu kuwa neno hili
IMEKWISHA liko katika wakati
uliopita kwa namna linavyoonekana hapa
lakini katika kiyunani ni sentensi kamili Perfect tense na kwa sababu hiyo neno hili linapata umuhimu mkubwa
kwa sababu lina maanisha imekwisha katika wakati uliopita, uliopo na ujao kwa
msingi huo neno hili linaendelea kufanya kazi kila siku na kila wakati, Neno
hili pia lilimaanisha kuwa kama kulikuwa na deni, basi deni hilo limelipwa
milele, wale wamuaminio Yesu hawana wanachodaiwa, kama ilikuwa ni kesi imefutwa
na hati za mashitaka zimeharibiwa kabisa Wakolosai
2:14-15 “akiisha
kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na
uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua
enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika
msalaba huo”.Neno hili ni kama kupewa ruhusa kutoka hospitalini baada
ya kuugua kwa muda na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kila mtu
akijua umekwisha kisha ukainuka tena ukiwa mzima wa afya. Ni neno muhimu sana
katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu na wokovu wetu.
Umuhimu
wa neno IMEKWISHA.
Yesu alipolia kwa sauti
kuu IMEKWISHA alimaanisha katika
wakati uliopita, sasa na itaendelea kuwa imekwisha hata baadaye. Kumbuka kuwa
hakusema nimekwisha hii ingemaanisha kuwa ameshindwa na kifo, lakini alilia
akisema IMEKWISHA! maana yake nimeikamilisha
kwa ufasaha kazi niliyokuja kuifanya. Kwa msingi huo neno imekwisha lina maana
ya hakuna kilichosazwa katika kazi ya ukombozi aliyokuja kuifanya na hivyo
alikuwa akizungumza ukweli kuwa kila kitu kimekamilishwa sasa ni mambo gani
Yesu aliyakamilisha yako mengi mno lakini baadhi ni pamoja na:-
1. Alikamilisha
kazi yote aliyokuwa ametumwa na baba yake kuja kuifanya duniani Yohana 17:4 “Mimi
nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.”
2. Alikamilisha
kazi ya kuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea Luka 19:10 “Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja
kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”
3. Alikamilisha
kazi ya kutukomboa sisi na adui zetu Luka
1:68-74 “Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Kwa kuwa
amewajia watu wake, na kuwakomboa. Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika
mlango wa Daudi, mtumishi wake. Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha
manabii wake watakatifu; Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote
wanaotuchukia; Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake
takatifu; Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu, Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu,”
4. Alikamilisha
unabii katika torati na manabii uliozungumza kumuhusu yeye kwa unabii, ishara,
alama na vivuli kuhusu ujio wake na kazi zake kutoka kitabu cha Mwanzo mpaka
kitabu cha Malaki ambako kuna nabii zaidi ya 300 kuhusu Masihi Mwanzo 3:15 na Isaya 53
Kwa msingi huo
hatupaswi tena kuteseka, kuwa watumwa, kukandamizwa, kuonewa, kuugua na kuteswa
na magonjwa, kuwa watumwa wa dhambi na shetani, hatupaswi kumuogopa awaye yote,
Nguvu za giza, na wachawi na washirikina na waganga, na mapepo na majini na
mashetani na shetani hazina uwezo juu yetu kwa imani katika kazi aliyoifanya
Bwana Yesu pale msalabani, laana ya torati, na sheria, hatuna deni, hatuna deni
la jana wala la leo wala la kesho kazi imekamilika yakikutokea majanga angalia
msalaba kumbuka kazi iliyofanyika msalabani, kumbuka kuwa mwanaume huyu
amemaliza amakamilisha kazi ya ukombozi huna hatia hata kidogo hakuna wa
kukuhukumu, wewe hata kama ulikuwa na historia mbaya sana yeye anawweza kuifuta
na kuiandika upya endapo utamwamini Bwan Yesu, Neno imekwisha ni neno lenye
nguvu kama vile siku unapotangazwa uhuru wa taifa lililotawaliwa na wakoloni,
tunapoadhimisha siku ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo yaani katika siku hii
ya pasaka ni lazima tujikumbushe kuwa Yesu amekamilisha kazi ya kutuweka huru
na kuvitangazia vifungo vinavyotuzunguka kwa kuvitangazia kuwa imekwisha,
Mateso yamekwisha, kazi za shetani zimekwisha, majini na mapepo kazi zao
zimekwisha kila aina ya vifungo na utumwa wa ibilisi ni lazima zisikie na
kukumbuka kuwa imekwisha
Rev.
Innocent Kamote
Mkuu
wa wajenzi mwenye Hekima!