Jumamosi, 13 Julai 2019

Kwa mfano wetu na kwa sura yetu!


Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.




Utangulizi:


Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya siri ya mafanikio makubwa sana ya mwanadamu, ni pamoja na kuwa katika mfano  na sura ya Mungu, (Image and likeness). Mwanadamu wa kwanza kabisa katika bustani ya Edeni hakuwa mtu wa kawaida alikuwa mkamilifu na mtakatifu, alikuwa ameumbwa tayari kwa kuutawala ulimwengu na kila kilichomo ndani yake, hakuwa amekusudiwa afe, augue au akose kitu au apoteze uhusiano wake na Mungu hakukusudiwa akose amani na furaha au akose utoshelevu, Chini ya uwepo wa Mungu mwanadamu aliumbwa afanikiwe katika kila jambo, Afanikiwe katika mambo yote, aweke mambo yote chini ya miguu yake, atawale atiishe,awe na mamlaka na uweza chini ya uwepo wa Mungu, Hata hivyo Biblia inaonyesha Katika mwanzo 3 kuwa kila kitu kiliharibika mara baada ya anguko, mwanadamu alipoteza sura na mfano wa Mungu, alipungukiwa na utukufu wa Mungu,


Warumi 3:10-12,23 “10. kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. 11. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. 12. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. 23. kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;


Matokeo yake ni kuwa mwanadamu alitawaliwa na Mazingira yake, alipoteza hekima ya kuyatawala mazingira yake, alipoteza ukamilifu, uwezo wa kuutawala ulimwengu ulipungua, na mwanadamu amepoteza tumaini na Mfano na sura ya Mungu iliharibiwa, Ili mwanadamu aweze kuwa na mafanikio makubwa na kuwa na nguvu kama ile iliyokusudiwa kwa Adamu, ni muhimu sana akarejea katika Mfano na sura ya Mungu.


Kwa mfano wetu na kwa sura yetu.


Katika moja ya mistari ya Msingi na ya Muhimu sana katika kitabu cha mwanzo Mstari wa Mwanzo 1: 26, Mstari huu una nguvu kubwa sana, Uelewa wa kutosha katika mstari huu utatufanya tuweze kuona ubora wa mwanadamu na kumtukuza Mungu hata kwa jinsi alivyotuumba na kisha kuendelea kumtegemea Mungu kwa asilimia 100 na kuacha kujivuna.


Kwa mfano wetu na kwa sura yetu. (in our image, in our Likeness)
Kwa sura wetuin our image – A representation of the external form of a person- Muonekano wa nje
Kwa mfano wetuin our likeness – The fact or quality of being alike, similarity -  mfanano wa kitabia na uadilifu.


Kwa msingi huo ni wazi kuwa mwanadamu aliumbwa akiwa anafanana na Mungu kimaumbile, kitabiana kimaadili. Hivyo basi mafundisho yoyote au theory yoyote inayoshusha thamani ya mwanadamu, au tabia au mwenendo wowote unaoshusha thamani ya mwanadamu kimaandiko unamkosea sana Mungu na kumdhalilisha Mungu na ubora wa uumbaji wake, katika mstari huu tunajifunza sasa kwamba;-


1.       Unaonyesha wazi kabisa kuwa Mwanadamu aliumbwa na Mungu na kuwa hakutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, “Evolution theory” Mwanzo 1;27, Mathayo 19:4, Marko 10:6 Mwanzo 1:27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.”  Mathayo 19:4 “Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke,” Marko 10:6 “Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke.” 


     Mistari hii ya Musa na maneno ya Yesu inatuthibitishia wazi kuwa mwanadamu anatokana na kuweko kwa kusudi la Mungu, Mwanadamu sio kiumbe cha kawaida, Mungu amemtukuza mwanadamu na kumtawaza juu ya kazi zake zote, na kamwe mwanadamu sio matokeo ya bahati mbaya wala mabadiliko ya tabia ya nchi, mwanadamu ni kiumbe cha juu zaidi katika kazi na utendaji wa Mungu, sio kiumbe cha kudharauliwa wala kuvunjiwa heshima, sio kiumbe kilichoumbwa kuwa mtumwa wa mtu au mazingira, sio bidhaa inayoweza kuuzwa kama ng’ombe kila mtu anapaswa kuelewa kuwa anaposhughulika na mwanadamu anashughulika na kiumbe ambacho Mungu amekitukuza mno, uhai wake haupaswi kutolewa kijinga na kirahisi, maisha ya kiumbe hiki hayapaswi kupuuziwa na kuachwa yapotee kirahisi, Mwanadamu ni wa thamani, ametoka katika wazo na mpango kamili wa Mungu.


2.       Mwanadamu ndio kiumbe pekee kilichoumbwa kuwa na ushirika wa karibu zaidi sana na Mungu, hata kama viumbe vyote vimeumbwa kwaajili ya utukufu wa Mungu ili vipate kumuabudu Mungu, Mwanadamu ndie kiumbe bora zaidi ambaye Mungu anapendezwa naye, anafurahia kuabudiwa naye, Mungu alikusudia kuwa na ushirika wa karibu na mshikamanifu sana na Mwanadamu kuliko kiumbe kingine chochote Waebrania 2:6Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie?” linapokuja swala kuhusu Mwanadamu Mungu huwezi kumwambia kitu, yuko tayari kumkumbuka yuko tayari kumwangalia, Historia ya mwanadamu inaonekana hapa kwamba alikuwa na ushirika “mgumu” “Athletic fellowship na Mungu, walikuwa na uadilifu wa hali ya juu, walikuwa wakamilifu, hawakuwa na dhambi, walikuwa watakatifu, wenye hekima, moyo wa ujasiri, waliokuwa na upendo kamili, ukarimu na wasiokuwa na ubinafsi wala choyo, na uamuzi uliweza kutumika kufanya maamuzi yaliyo sahihi, Mungu alikusudia nawe na ushirika wa karibu zaidi na mwanadamu unaozidi undugu na kwamba mwanadamu amtegemee yeye.


3.       Walipewa neema ya kuwa mfano na sura ya Mungu, Hili nalo ni moja ya jambo muhimu sana ambalo wasomi wengi wa kimaandiko hawaelewi uzito wa andiko hili, Swali kubwa la kujiuliza linalozaliwa na Mwanzo 1:26 ni kuwa sisi tuliumbwa kwa mfano na sura yake Mungu, hii ina maana gani? Andiko hili lina maana kubwa sana kinabii kwamba Mungu mwenyewe aliwapa wanadamu Mwili (Sura, Umbile Muonekano) ambao yeye mwenyewe angeweza kuja kujitokeza na kuonekana kwao, na kuwa wenzake 


     Mwanzo 18:1-141.BWANA akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari. 2. Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, 3. akasema, BWANA wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. 4. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. 5. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. 6. Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. 7. Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng'ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. 8. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. 9. Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. 10. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. 11. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. 12. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? 13. BWANA akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? 14. Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume” Unaweza kuona Mungu aliweza kujitokeza kwa Abrahhamu na kufanya mazungumzo naye katika namna ya kawaida kabisa kwa mwili ule ambao Mungu alikuwa nao; Zaidi ya yote Mungu alikuwa anamaanisha kuwa kinabii angekuja na kujitokeza kwa wanadamu akiwa na mwili sawa na ule wanaoutumia wanadamu ili awaonyeshe njia mwili ambao Yesu alikuwa nao Luka 1:35 “Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.” Kimsingi Mungu alipokuwa akimuumba mwanadamu alikuwa na wazo la Yesu, au wazo lake yeye mwenyewe, kwa hiyo basi mwanadamu kuwa na mfano na sura ya Mungu maana yake ni kuwa kama Yesu, ambaye ni Mungu na alikuja duniani kwa nia ya kuutwaa mwili Yohana 1;1,14Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa MunguNaye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Mungu amekusudia wote tuwe kama Yesu tangu mwanzo, tofauti yetu ni kuwa sisi na baba yetu Adamu alipoteza hali ya kuwa na mfano na sura ya Mungu (Likeness) tunapokuwa tumeokolewa na kumuamini Yesu Mungu anaturatajia turejee na kuwa wakamilifu kama yeye mwenyewe kwa kuufuata mfano wa Yesu Kristo “Kwa mfano wetu na kwa sura yetu” tunapomuamini Yesu kwa imani tunakuwa kama Yesu Mungu anatukubali kwa neema na kututazama kama yeye mwenyewe na kuwa na ushirika nasi kama atakavyo yeye, inahitajikia neema ya Mungu kulielewa hili. Na Mungu akupe neema hiyo katika jina la Yesu.


4.       Mstari huu Mwanzo 1;26 unatukumhbusha sisi asili yetu Kimaadili, kwamba tulikuwa wakamilifu kama Mungu, lakini tumepoteza ile hali yabuadilifu ya kuwa kama Mungu, sio hilo tu tumepoteza hali ya kuwa na ushirika na Mungu, kuja kwa Yesu Duniani kulikuwa na kusudi la kutujenga tena katika ule uadilifu, na hivyo Yesu ametuachia kielelezo tukifuate Yohana 13:15 Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.”


Madhara ya kupoteza sura na mfano wa Mungu.


Ni muhimu kufahamu kuwa ili tuweze kuwa na ushirika wa karibu na Mungu ni lazima tushughulikie sana swala la kufanana na Mungu “likeness” ambalo mwanadamu amelipoteza, hili ndio jambo la msingi, tunapokuwa na watumishi wa Mungu walioitwa kwa makusudi mbalimbali ya kuujenga mwili wa Kristo lazima ikumbukwe kuwa kusudi letu kuu ni kuwa kama Kristo, Adamu wa kwanza alikuwa kama Kristo lakini alipoteza, na kuathiri jamii nzima ya iana binadamu, sasa basi ni lazima tulenge kuwa kama Kristo Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa KristoHili ndio Jambo la msingi na la muhimu mno Yesu amekuwa kielelezo chetu tunapaswa kumfuata tunapaswa kumuigiza tunapaswa kuwa kama yeye, kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza kama anafanana na Yesu, Ushirika wa karibu na wenye nguvu na Mungu utategemea namna na jinsi tunavyomtegemea yeye, kwa nguvu zetu hatuwezi lakini chini ya neema yake tunaweza kujitegemeza kwake na sura na mfano wa Mungu ukawepo ndani yetu. Hili ni jambo la Muhimu


Mwaka 1972 wakati wa uchaguzi wa Rais Huko Marekani, wagombea wawili maarufu sana waipambana kuwania kiti cha urais, 1 aliitwa Richard Nixon, aliyetokea California akiwakilisha chama cha the republican na Mpinzani wake aliitwa George McGovern, aliyetokea jimbo la South Dakota akiwakilisha chama cha Democratic Katika uchjaguzi huo George McGovern alishindwa vibaya, Kura za turufu za Marekani Electoral vote Nixon alipata 520 na George alipata 17, Inaelezwa moja ya sababu kubwa ya kushindwa kwa George ni kuwa wakati walipofanya kampeni zao kwa njia ya Radio kila mtu alivutiwa sana na George Sauti yake ilikuwa yenye mvuto mkubwa sana na yenye ushawishi ukilinganisha na Nixon hata hivyo mara walipokuja kuonekana kwa njia ya Television Muonekano wao ulikuwa tofauti sana George alikuwa ametoka kuugua, na hivyo alikuja studia akiwa amejifunika koti na sweta, alionekana kuchoka sana na muonekanao wa afya yake pia haukuwa mzuri, alikataa kufanyiwa make –up na kupakwa poda na kufanyiwa maandalizi ya kurushwa katika televisheni huku Nixon alionekana mwenye afya njema na aliyekuwa amefanyiwa make up ili muonekano wake uwe Mzuri, kumhbuka hii ilikuwa debate ya mwisho, watu walikata tamaa sana walipoona muonekano wa George na hivyo Nixon ambaye hakuwa mnenaji Mzuri alichaguliwa kura rais wa marekani.


 

 








 
George McGovern  Kushoto – Democratic  na Richard Nixon Kulia- Republican


Nini kilimpa Nixon ushindi mkubwa ilikuwa ni Sura yake, muonekano wake, nini kitatupa ushindi katika maisha yetu, ni kitu gani kitatufanya tukubaliwe na Mungu na wanadamu, nini kitatufanya tuwe na mvuto na ushirika wa karibu sana na Mungu ni Sura na mfano wa Mungu, Mwanadamu atakuwa kiumbe chenye utukufu mkubwa anapokuwa anazishika njia za Mungu, atakuwa na ukaribu naMungu akijitahidi kuwa kama Yesu, Ni lazima kila mmoja wetu akubali kumwamini Yesu na kujifunza kuwa kama Yeye ili tuweze kupata kibali kwa Mungu, Shetani atakosa la kutushitaki ikiwa tutamfanania Mungu, Bwana na ampe neema kila mmoja wetu kuwa na sura na mfano wa Mungu ili tuweze kupata kibali mbele za Mungu. Lazima tujitahidi kujionyesha kuwa tumekubaliwa na Mungu 2Timotheo 2;15

Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!

Endapo umebarikiwa na Masomo yangu tafadhali usisite kunijulisha namna na jinsi ulivyobarikiwa kama wafanyavyo wengine sms au whatsapp me kwa +255 718 990 796

Hakuna maoni: